Leo nataka tutafakari kwa Pamoja mojawapo
ya somo muhimu sana katika maisha ya Ukristo kwa kuwa somo hili ni msingi wa
Imani yetu. Moja ya Misingi ya Imani yetu Wakristo ni tunaamini kuwa Yesu
Kristo alisulubiwa, akafa na kuzikwa na hatimaye akafufuka siku ya tatu, Endapo
imani hii itakuwa ni uongo na tukio hilo kama litakuwa halijawahi kutokea ni
wazi kuwa imani ya Ukristo ni batili. “IKoritho
15:13-19” Ni wazi kuwa unapozungumzia kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo ni
lazima uamini kuwa Yesu alisulubiwa yaani alipata Mateso yaliyosababisha Kifo
chake na hatimaye akafufuka na kama hivyo sivyo basi Ukristo ni imani mbaya na
mbovu kuliko zote.
Upinzani dhidi ya
Kusulubiwa, Kufa na Kufufuka kwa Yesu Kristo.
Kwa kuwa shetani anafahamu kuwa
kusulubiwa kwa yesu Kristo na kufa na kufufuka ndio nguzo muhimu katika imani
ya Ukristo ametumia jitihada kubwa sana katika kuhakikisha kuwa watu
hawataamini hata kidogo kuwa Yesu alisulubiwa, akafa na kufufuka. Aidha ziko
Imani nyingine ambazo kwa makusudi au kwa Bahati mbaya zinapinga vikali kuhusu kusulubiwa
na kufa na kufufuka kwa Yesu na kutumia ujanja mwingi hata wa kupotosha
maandiko ili tusiamini kuwa kweli Yesu alisulubiwa na kufa na kuzikwa na
kufufuka siku ya Tatu.
Kwa
mfano: Waislamu wanaamini kuwa Yesu Hakusulubiwa.
Waislamu wanaamini kuwa Yesu hakusulubiwa na
kufia Msalabani ndivyo wanavyoamini na kufundishwa na ndivyo Quran
inavyofundisha (Surat al Imran 3:54-55, an
Nisaa 4:157-158) aya hizi ndizo zinawathibitishia kuwa Yesu Masihi
hakusulubiwa na kufia msalabani na huunganisha madai haya kwa kutumia aya
zifuatazo katika Biblia.
Ø
Wanafundisha
kuwa Yesu hakufa msalabani sawa na
maneno yake mwenyewe kuhusiana na Ishara ya nabii Yona (Yunusi) sawa na (Mathayo
12:38-40) hivyo kama ilivyokuwa kwa Yona katika tumbo la nyangumi alikuwa
hai na Yesu alikuwa hai katika uso wa nchi.
Ø
Wanahoji
kama ilikuwa ni mapenzi ya Mungu Yesu afe msalabani kwanini aliomba kule
bustanini Baba ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke?(Mathayo 26:39, Marko14;35, Luka22:42)
Ø
Waislamu
wanaamini kuwa Mungu aliyasikia maombi ya Yesu Masihi na kumuokoa katika mauti
sawa na (Yohana 9;31,11:41-42,Waebrania
5:7)
Ø
Wanaamini
kuwa kuna uthibitisho wa kibiblia kuwa Mungu aliyasikia maombi yake na ndio
maana alianza kumshughulikia mkewe Pilato katika ndoto na Pilato mwenyewe (Mathayo 27:19)
Ø
Wanaamini
kuwa Pilato alifanya jitihada binafsi ili kumuokoa Yesu na mauti na kwa kufanya
yafuatayo;-
o
Kunawa
mikono kuonyesha kuwa Yesu hana hatia na kuwa yeye hahusiki na damu yake mtu
huyo
o
Kumfungulia
Baraba ili kupata mbadala wa Yesu
o
Kuchelewesha
hukumu kwa kuipeleka kesi kwa Herode kwani alijua kuwa sabato inakaribia, Pia
kwa asili kifo cha msalabani ni kifo cha polepole hivyo kwa mtu mwenye afya
kama Yesu aliyekuwa na uwezo wa kufunga siku arobaini (40) hangeweza kufa
msalabani kiurahisi na ushahidi unaonekana kwa wenziwe waliosulubiwa pamoja nae
kuwa walilikatwa miguu (Yohana
19:31-32).
Ø
Waislamu
wanahoji kama Yesu alikufa kweli kwanini maiti yake ilitoka maji na damu?
Ø
Wanahoji
zaidi lugha ya kibiblia inayoonyesha Pilato akishangazwa na taarifa kuwa Yesu
amekwisha kufa mara! (Marko 15:42-44).
Wanahoji kuwa jambo lingine la kushangaza ni muonekano wa Yesu mwenyewe baada
ya kufufuka kuonekana na Mariam
Magdalena akiwa na mavazi kama mtunza Bustani jambo linaloashiria kuwa
aliyapata hapo (Yohana 20;13-15)
Ø
Waislamu
wanahoji kuwa kama Yesu alikufa kweli kwa nini hatuna ushahidi toka kwa Yusufu
wa Armathaya na Nikodemo waliomzika na sio Mathayo na Marko au Luka ambao
hawakuwepo na walikimbia? Na wanahitimisha kwa kudai kuwa maisha ya Yesu yaliyosalia aliishi nchini India katika jimbo
la Kashimir na alikuwa na Tomaso aitwe Pacha (yaani alifanana na Yesu) na
aliishi miaka 120 huko na alizaa mtoto wa kike na Mariam Magdalene na alifia
huko na kaburi lake liko hata leo
Ø
Waislamu
wanadai hata wayahudi walitilia shaka kifo cha masihi (Mathayo 27:63).
Ø
Waislamu
pia huamini kuwa Biblia ilitiwa chumvi katika maeneo yanayohusiana na kifo na
kufufuka kwa Masihi kwa madai yafuatayo;-
Unapofungua Biblia yako
katika ukurasa unaokaribia injili ya Mathayo utaona kuna maelezo ya vifungu vya
Mabano na Parandesi za aina mbili 1. Ya mviringo mfano ( ) hii inahusu ufafanuzi. 2 ya mraba mfano
huu [ ] hii inahusu maneno
yanayoonekana katika nakala kadhaa za zamani za kale ila hayaonekani katika nakala
nyingine yaani za sasa
Hoja:-Kama hivyo ndivyo
waislamu wanashangaa kwa nini hizi nakala nyingine yaani za sasa zisionyeshe
tukio la muhimu la kufa na kufufuka kwa Yesu hasa ukizingatia kuwa
·
Mathayo
anashindwa kuelezea tukio la kupaa kwa Yesu.
·
(Marko 16;9-19) ziko kwenye kifungo cha
mraba kuonyesha nakala nyingine za kale je nakala za sasa zimeshindwaje
kuonyesha tukio hili la kufufuka na kupaa kwa Yesu?
·
Yohana
pia anashindwa kuonyesha tukio hili la kupaa kwa Yesu?
·
Je
tunawezaje kumuamini Luka ambaye alikuja baadae na hakuwa miongoni mwa wale 12.
Hoja kama hizi za waislamu
je unafikiri hazipaswi kujibiwa? Na kushughulikiwa je mkristo wa kawaida tu je
hawezi kusilimishwa? Ni muhimu tukajibu hoja hizi ili kuondoa utata utakao zuia
yamkini hata waislamu wenyewe kuokoka na kuifahamu kweli.
KWA NINI TUNAAMINI KUWA YESU ALISULUBIWA ?
Wakristo tunaamini kuwa Yesu amesulibiwa
na alikufa na hatimaye alifufuka toka kwa wafu na sasa yuko mkono wa kuume wa
Mungu baba mbinguni,Hapa ndipo mahali
penye moyo wa Imani yetu wakristo wote na kwa ufupi huu ndio ukristo
wenyewe na ndio maana shetani kwa makusudi kabisa anapingana sana na swala zima
linalohusiana na kusulibiwa, kufa na hata kufufuka kwa Yesu ( 1Koritho 15;12-19).Kwa bahati mbaya
mstari huu nilioutumia hapa ni moja ya mistari inayotumiwa sana na makafiri
katikakudanganyia watu kuwa kristo hakufufuka nitashughulukia mstari huu wakati
wa kujibu hoja hii kuwa Kristo amefufuka Lakini kabla ya jambo hilo nilikuwa nataka
kwanza nikurudishe Nyuma katika historia iliyokuwako wakati wa Muhamadi ambayo
iliathiri uelewa wake na wa watu wa nyakati zake kuhusu ukristo na Kufa kwa
Yesu na kufufuka kwake jambo ambalo linaathiri waislamu wa nyakati hizi
tulizonazo kushindwa kulielewa swala hili ni Muhimu kufahamu kuwa wakati wa
Muhamadi kulikuwepo na Imani potofu zenye mafundisho ya Uzushi kuhusu
ukristo,ambazo zilichangia uelewa potofu kumhusu kristo na kifo chake cha
msalabani,uelewa ambao ulimkumba Muhamadi na unaathiri waislamu wa nyakati
hizi.
Kwa mfano Kama u msomaji mzuri wa quran utakuta kuna
kundi la watu wanaitwa “Manasara”
Kundi hili hufikiriwa kuwa ni wakristo lakini wakristo wengi wa leo wakiulizwa
kama wanajifahamu kuwa wanaitwa hivyo watakushangaa! Manasara Ni mojawapo ya
makundi ya imani potofu yaliyokuwa yameenea sehemu za Arabia Na huko Makka,
jamii ya kundi hili walikuwa ni wakristo wa kiyahudi ambao imani yao ilikua
ikiamini kati ya ukristo na dini ya kiyahudi hawa ndio Muhamadi aliwafahamu kwa
hivyo utaona lile wazo la kuwafikiri wakristo katika quran limejengeka kwa
misingi ya imani ya Kinasara.
Imani
nyinginezo zilizokuwepo ambazo zilichangia mawazo potofu kuhusu kifo cha Yesu
ni pamoja na kundi la imani potofu lijulikanalo kama Gnosticism hawa waligawanyika
katika makundi makuu kama matano hivi nitayataja makundi hayo kwa lugha ngeni
kwa kukosa tafasiri ya Kiswahili ya maneno hayo ingawa wakati wa kuyafafanua
utaelewa kile walichokuwa wakikiamini na ndilo jambo la muhimu kwako.
1. Basilides. Hili
Ni kundi lililofundisha kuwa Yesu asingeweza kuteseka hata kidogo Kwa sababu
wakati woote mateso Ni Kwa mtu muovu tu Na mwenye dhambi, Hivyo mtu aliyetumwa
na Mungu kama Yesu na aliyekuwa mwenye haki kama yeye hangeweza
kuteseka.Waliamini kuwa Yesu alichukua sura ya Simon wa Kirene, na Simon wa
kirene alichukua sura ya Yesu, Hivyo kwa asili wayahudi walimsulibisha Simon
badala ya Yesu, na hivyo Yesu alisimama pembeni akiwasanifu.
2.
Docetism. Hili ni kundi lililofuyndisha kuwa Yesu
alikuwa ni Roho tu.Hivyo matukio yoote yanayohusu kuzaliwa, kukua, kula,
kunywa, kulala nk.hayakuwa mambo halisi “ it
was an illusion, some thing that does not really exist” Kumbuka wazo hili
kuwa Yesu ni roho limo katika quran
3. Cerenthus. Hili Ni kundi lililofundisha kuwa wakati
Yesu alipobatizwa Yesu halisi alishuka kutoka mbinguni kuja Kwa Yesu mtu Kwa
umbo Kama njiwa, akafanya miujiza, na kuhubiri ufalme na kumtambulisha baba.
Wakati wa kusulibiwa Kristo wa kiroho aliondoka zake na Kristo mwanadamu
alikufa na akafufuka baadae.
4. Manichaeism. Kundi hili lilifundisha kuwa sio Yesu
aliyekufa msalabani isipokuwa ni mwana
wa mwanamke mjane huenda ni yule aliyefufuliwa katika (Luka. 7; 11-17)
5. Carpocrates.
Kundi hili lilifundisha kuwa
sio Yesu aliyesulibiwa lakini ni mojawapo ya wafuasi wake, Yesu alikuwa pembeni
akiwasanifu wayahudi kwa kukwepa mateso waliyotaka kumtendea kisha baadae
akapaa mbinguni.
Unafikiri
kwa mtindo huu wa imani potofu zilizokuwepo Muhamad na waislam wengine je wanao
mtazamo sahihi kuhusu ukristo? Jibu ni la
Tukirudi
nyuma kwenye andiko la Wakoritho
15;12-19 ambalo waislamu hulitumia katika kupotosha kuwa Yesu hakusulibiwa
ni muhimu kufahamu kuwa hapa Paulo mtume alikuwa anacheza na falsafa ya maneno
hasa kwa sababu wakoritho wenyewe walikuwa wanafalsafa Paulo aliwataka
wakoritho kufikiri vema (Logicaly)
na kwa kuanzia na haya hii ni muhimu msomaji akafahamu mazingira na historia ya
andiko kabla ya kujisomea hovyo na kufasiri hovyo kama makafiri wafanyavyo;-
Kihistoria,
kuhusiana na andiko hili kulikuwa na tatizo miongoni mwa wakoritho kuhusu
ufufuo wa wakristo waliokufa katika Bwana huko koritho ya kuwa hawatafufuka kwa
sababu wafu hawafufuliwi, shida ya wakoritho haikuwa katika ufufuo wa Kristo
mwenyewe hili waliliamini na kwa kweli lilikua ni kiini cha injili ya mitume na
waliyoiamini wakati ule
Paulo anajibu
hoja hii akitumia uzoefu au tabia ya watu ya wakati ule iliyokuwa inaendelea
pale Koritho ili kuwasilisha kweli kitaalamu mtindo huu unaitwa “Ad-Homeinem” Wakoritho walikuwa
wamekata tamaa kuwa hakuna kiama (Ufufuo wa wafu) hasa kwa waamini wenzao
waliokuwa wamekwisha kufa (I koritho
15;12-34.)Huku wakati huohuo wakiamini kuwa Yesu yuko hai na kuwa
alisulibiwa,alikufa na alifufuka ! jambo hili lilikuwa wazi kwao.
Paulo anajibu
kwa kujenga hoja zifuatazo;-
a). Wakoritho
15;16-
Kama wafu hawafufuliwi Kristo naye hakufufukaa!(Maana yake ninini?) jibu Kama
mnaweza kuamini kuwa Yesu amefufuka katika wafu mnashindwaje basi kuamini kuwa
Ndugu zenu waliokufa katika bwana watafufuka? Kwa vipi kwa maana Kristo ndio
limbuko lao yaani wa kwanza wao ona mst 20.
b). Wakoritho
15;29- (“
au je wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu watafanyaje kama wafu hawafufuliwi
kamwe ;kwanini kubatizwa kwa ajili ya wafu?) maana yake kulikuwa na desturi
zinazozunguka jamii ya wakoritho ambapo watu walibatizwa kwa niaba ya wafu wao
waliokufa kabla ya kubatizwa (ingawa zoezi hilo lilifanywa na wapagani na sio
wakristo) Paulo anahoji je watafanyaje kama wafu hawafufuliwi? Maana yake hata
hao waliofanya hayo walifanya wakiamini kuwa kuna ufufuo.
c). Wakoritho 15;32 - Kama hakuna ufufuo na tule na tunywe; maana
yake kama kifo ndio mwisho wa yoote na hakuna ufufuo yanini kujinyima starehe
za dunia kwa ajili ya Mungu? watu na wastarehe wale wanywe maana tutakufa!.
Kwa maana
nyingine Paulo alimaanisha kuwa ufufuo wa Yesu Kristo ni ishara iliyokuwa wazi
kuwa siku moja Mungu atafufua wafu kama alivyo fufuka kristo ndio maana quran
inasema yeye ndie Ishara ya kiama.
Ushauri
mwingine kwa wasomaji wa biblia ni kuwa tofauti na quran ambayo kila aya
inajitegemea, Kanuni za usomaji wa biblia zinamuongoza msomaji kusoma fungu
zima la juu na chini ili kupata maana kamili inayokusudiwa na mwandishi huyo
kumbuka vitabu vingine ni nyaraka yaani barua unawezaje kuisoma barua nusunusu
kisha ukapata maana aliyoikusudia mwandishi? Kwa mfano Wakoritho 15;12-19 inakamilishwa kwa kusoma Wakoritho 15;1-11 na Wakoritho
15;20-28 nk. Kwa mfano swasa ukisoma fungu lile la kwanza Paulo anasisitiza
kuwa Yesu alisulibiwa, alikufa na alifufuka na aliwatokea watu wengi baada ya
kufufuka kwake unaona? Jambo la kushangaza ni kuwa waislamu hawajui namna ya
kuisoma biblia bali hudandia treni katikati ya safari na unajua matokeo, kwa
kuwasaidia tu Hebu niwahoji wanaharakati wa kiislamu kwamba ninyi mnamkataa
Paulo mtume na mnamuona kua ni muongo na aliharibu dini sasa iweje leo myaamini
maandiko haya kipande ambacho kimeandikwa na Paulo?
Baada ya
kufafanua aya hizo hapo juu sasa tuchambue aya katika quran yaani (Imran 3;54-55, An Nisaa 4;157-158).
Linganisha na injili inayoitwa ya Barnaba uk 14. Sura ya 215; Aya hizi zinadai
Mungu alibadili hila za wayahudi maana yeye ni mbora wa kupindisha hila na
hivyo alisulubiwa mtu mwingine Yesu akanyakuliwa mbinguni? Ukiachia imani
potofu ambazo zilichangia uelewa huu mimi ninashangazwa na quran kuwa ni kitabu
cha Mungu au cha majahili? Maana aya hizi zinamtukanisha Mungu kwa kuonyesha
wazi kuwa Allah ni mjuzi wa kufanya utapeli na kuwa hana nguvu ya kufufua ila
ana nguvu ya kudanganya watu eti waone sura ya Yesu anasulibiwa na kumbe ni mtu
mwingine! Wanaharakati wa kiislamu ni lazima watubainishie hili;-
Kama Yuda ndiye
aliyesulibiwa badala ya Yesu je Yesu ndiye aliyejinyonga?.
Je Mungu
mtakatifu asiyeweza kusema uongo aliamua kuwadanganya Askari, Pilato, Herode,
Yusufu wa arimathaya, Nikodemo, wanafunzi waliokuwa karibu kama Yohana, Mariam
mama yake na Mariam Magdalene hawa wote walidanganywa na Mungu alipokuwa
anapindua hila za wayahudi?(Yohana
19;25,26-27). Je Mungu angeweza kuwaumiza na kuwadanganya watu watakatifu
waliokuwepo? Hata Mariam (Quran 3;36,19;16). Waliguswa na mateso haya
na kulia huku wakiangalia mpaka mtu anakufa wakidhani ni Mwanae kumbe eti Mungu
alikuwa anacheza kamchezo ka utapeli, Nani atakuwa mwenye makosa pale wanafunzi
akiwemo Paulo walipohubiri kuwa yesu amesulibiwa?na kuwa aliukufa na akafufuka
na zaidi ya yoote walikubali kufa kwa ajili ya injili hii,Je malaika pia ni
waongo pale waliposema na wanawake kuwa Yesu amefufuka? Ona (Mathayo 28;5-7,Mdo 2;23-24). Injili
inamtukuza Mungu kwa kuonyesha uwezo wake kuwa yeye anao uwezo wa kufufua
tofauti na allah ambae kwake kufanya hila ni jambo jepesi kuliko kufufua?
Mungu ambae
sisi tunajifunza habari zake katika Biblia hawezi kusema uongo (Hesabu 23;19,1Samuel 15;29, Malaki 3;6,
Tito 1;2;Yakobo 1;17),Aya zote
hizi zinabainisha jinsi Mungu alivyo mkweli,Kristo mwenyewe alisema kuwa
atakufa na atafufuka pia ni mkweli.Inasikitisha kuona Mungu wa Muhamad na wa
waislamu akifanya hila? Sisi tunaamini kuwa Mungu wa kweli aliyefunuliwa kwetu
kupitia Yesu Kristo ni wa kutumainiwa lakini kumuamini Mungu wa kwenye Quran
inatutia mashaka na kutupotezea tumaini “ Hawezi
kufufua ila anaweza kufanya utapeli?”
Hoja kuhusu Ishara ya nabii Yona (Yunusi).
Waislamu wanadai kuwa Ishara hii inathibitisha kuwa Yesu hakufa bali
alikuwa hai, na pia Hakukaa siku tatu kamili kaburini,mara nyingi humnukuu Yesu
katika matamshi yake katika (Mathayo
12;33-40).
Hili
nalo ni jambo la kushangaza sana nah ii inatusaidia kujua kuwa unapozungumza na
mwislamu aneyeamini hivyo kuwaq unazungumza na jahili au maaamumah wasiojua
kabisa maandiko wala hawana utaalamu nayo ila hudandia tu na kwa bahati mbaya
ni kama watu wanaodandia gari kwa mbele jambo ambalo unajua nini kinaweza
kutokea kwa kuwa mimi ni mwalimu hebu fuatana nami tena tupate kulichambua
andiko hilo.
Ø
.
Ni wazi kuwa waislamu hawajui kanuni ya uchambuzi wa agano la kale (Torati) na
uhusiano wake na agano jipya (Injili).Kitaalam mambo mengi katika agano la kale
yalikuwa ni ya kinabii (kivuli) cha mambo halisia katika agano jipya.
“Mfano mimi
ninampenda mke wangu na mwanangu,ninaposafiri husafiri na picha zao,na
inapotokea nimerudi nyumbani sihitaji picha zao tena kwa sababu sasa ninae mke
wangu na mwanangu halisi”
Hivi
ndivyo Mungu alivyowatumia manabii wengi katika agano la kale kutoa unabii
kuelekea kwa kristo (Kolosai 2;16-23)Hivyo
ishara ni picha tu ya tukio halisi lililotokea au litakalotokea,mfano rahisi ni
jinsi ambavyo zamani wayahudi walikuwa wanandama mwezi kama wafanyavyo waislamu
wengi leo,Mwezi ukiingia gizani na unapotoka huitia nuru dunia hii ilikuwa ni
ishara ya kuja kwa Masihi Yesu kristo
ambaye yeye ni nuru ya ulimwengu (Yohana
1;6-14). Hivyo kwa kua masihi alikwisha kuja duniani naye ndiye nuru halisi
na tumekwisha kumjua na amekwisha tia nuru mioyoni mwetu, Wakristo hatuitaji
tena kuandama mwezi maana mwezi ulikuwa ni kivuli tu (copy)Bali kristo ni
halisi (Original).
Kwa msingi
huu basi tukio la nabii Yona ingawa lilikuwa la kweli kwake kama tukio halisi
hata hivyo lilikua ni Ishara au unabii wa tukio halisi litakalompata Kristo.
Hakuna shaka kuwa kuna uwezekano Yona alikuwa hai ndani ya tumbo la Nyangumi,
wala hatuambiwi kua alikufa kasha akafufuka toka kwa wafu na labda kwa ajili ya
hili waislam hufikiri kuwa ndivyo ilivyokuwa kwa Yesu kuwa alikuwa hai pale
kaburini. Kwanini Yesu alitumia mfano wa Yona? Yesu alikuwa na maana gani.
Mstari wa 40 wa Mathayo 12 unasema.
“Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo
la nyangumi, Hivyo ndivyo mwana wa Adamu atakavyikuwa siku tatu mchana na usiku
katika moyo wanchi ”
Ni wazi
kuwa mtu anapotafasiri unabii vivuli (Types) na uhalisia wa jambo huwezi
kuchukua kila kitu kama kilivyo ila unachukua wzo la jumla au ile dhana mfano (Yohana 3;14).
“Na
kama vile Musa alivyomuinua yule nyoka kule jangwani vivyo hivyo mwana wa Adamu
hana budi kuinuliwa juu”
Hivyo
unaweza kuona wazi Yesu anasisitiza na kamavile. Hapa anazungumzia ile
dhana ya kuinuliwa juu (Kusulubiwa). Nyoka aliinuliwa kuleta uponyaji kwa
wayahudi waliokuwa wakiumwa na nyoka, Kristo aliinuliwa kuleta uponyaji kwa
ulimwengu kutoka katika dhambi na madhara yake.
Sasa
tukitafasiri biblia au mfano ule wa yona kama waislamu wanavyotaka je mfano huu
tutaufafanua vipi? Nyoka alikuwa wa shaba na alikuwa hana uhai je Kristo naye
alikuwa na mwili wa shaba na aliinuliwa akiwa amekwishakufa? Maana hivi ndivyo
waislamu wanavyo itafasiri biblia!. Hivyo ni wazi Yesu alikuwa anazungumzia
lile wazo la Yona kufichika katika Tumbo lanyangumi kwa siku tatu.
Ufahamu kuhusu siku tatu Mchana na usiku.
Wote
tunakubali kuwa Yesu alikufa na akafufuka siku ya tatu bila shaka. Lakini kwa
waislam hii ni hoja! Wao wanadai kuwa Yona alikaa tumboni mwa nyangumi suku
tatu usiku na mchana na hivyo kutimiza masaa 72 lakini kwa.Lakini yesu hakukaa
masaa zaidi ya 33 tu. Ijumaa saa 9 alikufa na alizikwa na jumapili saa 12
aliffufuka ,hivyo alikaa usiku wa ijumaa na jumamosi tu na mchana mmoja tu wa
jumamosi,hivyo waislamu huona hakuna uwiano wa unabii wa yona na uhalisia wa
Tukio la Kristo.kuhusiana na siku tatu. Shida waliyonayo waislamu hapa ni
kukimbilia kutafasiri kitabu kisichokua chakwao huku wakiwa hawana utaalamu wa
kutosha na kanuni za kuitafasiri biblia,Ni muhimu kufahamu kuwa kuna tofauti
kubwa kati ya kizazi cha leo na lugha,tamaduni,historia na nyakati yaani Muda,hivyo unapotaka kuifasiri
biblia unakumbana na mambo hayo manne kufikia wakati tulionao.Hivyo kuna mengi
yakufahamu kati ya nyakati za muandishi na nyakati tuliopo na matumizi ya mambo
yale manne katikati ya hayo.
Kitu ambacho
wanaharakati wa kiislamu wanashindwa kukielewa ni kuwa kuna tofauti kati ya
waebrania wa karne zile na tamaduni za kiingereza na Kiswahili cha nyakati za
leo. Kwa mujibu wa tamaduni za wayahudi wa nyakati hizo wao walihesabu hata
sehemu ndogo tu ya siku kamasiku nzima,hivyo Yesu kuzikwa Ijumaa,akashinda
jumamosi, akafufuka jumapili mapema alfajiri, kwa mujibu wa tamaduni na kalenda
na lugha za kiyahudi Yesu alikuwemo kaburini siku tatu (Mathayo 27;64)na ndio maana walilinda kaburi.kumbuka mitume pia walihubiri
juu ya siku hizo tatu (Matendo 10;40).Swala
hili halikuwa na shaka katika injili ya mitume. (1Koritho 15;3-4).Hivyo ishara ya Yona inawathibitishia waislamu na
maadui wa ukristo uhakika ya kuwa Yesu alisulibiwa,alikufa na alifufuka siku ya
tatu na si vinginevyo.
Ufahamu kuhusu maombi ya Yesu kwa Baba
aokolewe na mauti.
Baadhi ya
waislamu na hasa wa madhebu ya ahmadia huwa wanatumia baadhi ya mistari kama
vile (Mathayo 26;39.Marko 14;35;Luka
22;42) kuhoji kuwa kama yalikuwa ni mapenzi ya Mungu afe msalabani kwanini
aliomba “ikiwezekana kikombe hiki
kiniepuke” na wanatumia aya zifuatazo kujithibitishia kuwa Mungu alimsikia (Yohana 26;39 11;11-42 na Ebrania 5;7). Kabla ya kushughulikia mengineyo hebu tushughulikie hoja hii
ya kusikiwa kwa maombi ya Yesu.
Waislamu wengi hawamjui Yesu kama jinsi ambavyo hawamjui Mungu, wale
wakristo wanaomfahamu Kristo vizuri wanafahamu lile fundisho maarufu la
unyenyekevu wa Yesu (The Doctrine of
Kenosis),Fundisho hili lafundisha
jinsi ambavyo kitu Fulani cha ulimwengu wa kiroho kinavyoweza kuvaa mwili wa
kibinadamu (Incarnation) na kufanya
shughuli za kibinadamu; (Kwa waislamu majini hufanya hivyo).Kristo kwa asili
maisha yake hayakuanzia katika tumbo la mariam yeye alikuwako tangu mwanzo. (Yohana 1;1-5,14). Quran inasema “Yesu
ni Roho” Hivyo alipotungwa mamba tumboni mwa mariam alikuwa anachukua mwili wa
kibinadamu (Filipi 2;5-8) na kwa
tendo hili tunapata Mungu mwanadamu yaani Immanuel Mungu pamoja nasi (Mathayo 1;23) hata hivyo kwa
unyenyekevu wake Yesu hakutumia uwezo
wake wa kiungu,bali aliishi kama mtu wa kawaida, angeweza kubadili mawe kuwa
mkate lakini hakufanya hivyo na angeweza kuagiza majeshi kumi na mawili ya
malaika lakini hakufanyahayo.Yesu mwenye asili ya kiungu wakati huohuo akiwa
mwanadamuanayeishi bila kuutumia uwezo wa kiungu kama mwanadamu alihisi
njaa,alichoka,alikula na zaidi ya yoote aliogopa kifo na mauti kama binadamu
yoyote.Yesu aliomba ikiwezekana kikombe hiki kimuepuke
Lakini si kwa mapenzi yake bali ya Baba yake hivyo kwa
kuwa ilikuwa ni mpango wa Mungu Yesu kufa kwa ajili ya ulimwengu alitumwa
malaika kumtia nguvu kukabiliana na kifo cha msalaba hivyo hatimaye
alisulubiwa,alikufa na kufufuka kama majibu ya kuokolewa na mauti unaona!,Hii
ni tofauti na mauti iliyomkuta Muhamadi ambaye alihaha na kuogopa kufa sana
badala ya kumtumainia mungu,Muhamad alisema “Enyi watu! Hakika kukata roho kuna
machungu makubwa” (Maisha ya nabii Muhamad uk 80 kifungu cha tatu)Hivyo Yesu
asife bali kuokolewa na mauti baada ya
kifo.
·
Kwa
mujibu wa IVP Bible background commentary (New Testament) inasema “Wayahudi
wanaamini kuwa Mungu alisikia maombi ya Yesu na Mungu aliyajibu kwa kumfufua na
sio kwa kuikwepa mauti yenyewe bali kwa kufufuka kutoka mautini”
·
The
applied New testament commentary by Thomas Hale inasema hivi “Yesu aliomba
aokolewe na mauti ya msalaba (Marko
14;35-36) lakini Mungu hakuchukuliana na Maombi hayo,Mungu angeweza
kumuokoa kutoka mautini lakini hakuchagua hivyo,ingawaje siku ya tatu alimfufua
toka kwa wafu”Matendo 2;22-28.
Kwa kufundisha
kinyume na ukweli huu waislamu wanataka kutuambia kuwa Yesu ni Muongo,huku
quran inathibitisha kuwa hakuwa na dhambi.Yesu mwenyewe alisema anautoa uhai
wake (Yohana 10;14-18)Yesu mwenyewe
anawachanganya wislamu kwa kuwa yeye mwenyewe ni njia kweli na uzima hivyo aliutoa uhai wake yeye mwenyewe na
kuutwaa tena.
Yesu Kristo
hakuwa na Hatia ya aina yoyote.
Yako madai ya Baadhi ya waislamu kuwa biblia
inathibitisha kua Mungu aliyasikia maombi maombi ya Yesu na kuanza
kuwashughulikia mke wa Pilato ambae alimtahadharisha Pilato kujihadhari na
hukumu dhidi ya Kristo andiko hili hutumika (Mathayo 27;19),Pia wanaorodhesha kile kinachodaiwa kuwa ni jitihada
za Pilato kumnusuru Masihi na mauti kwa kunawa mikono,Kumfungulia Baraba ili
kupata mbadala wa Yesu (Luka 22;36) na kile kinachodhaniwa kuwa ni
kuchelewesha hukumu kwa kumpeleka Masihi kwa Herode.
Nikianza
kuwajibu waislamu hoja hizi nataka kukazia kwanza kichwa cha Habari hapo juu
cha kifungu hiki Yesu Kristo hakuwa na hatia ya aina yoyote.Hakuna mtu Yeyote
aliyemshuhudia Masihi kuwa na Dhambi(Yohana
8;46).Yeye hakutenda dhambi wala
hakuwa na hila ya aina yoyote soma mistari hii (2Koritho 5;21,Ebrania 4;15,1Petro 2;22).Masihi alitafutiwa
kubambikizwa hatia katika Mazingira makuu matatu ambayo ni Kumtafutia makosa ya
1) Kidini, 2) Uhaini dhidi ya Serikali ya Kikoloni ya Rumi na 3) Uhaini dhidi
ya ufalme wa kiyahudi Jimbo la Galilaya kwa Herode, katika mazingira hayo yote
hakuna aliyepata kosa wala hatia inayostahili auwawe.
Mashitaka Ya
Kidini.
Yesu alipokamatwa kwanza alipelekwa kwa
Anasi mkewe Kayafa.na aliyekua kuhani mkuu kabla ya Kayafa.Hapa kwa anasi
ilionekana wazi kuwa Hakuwa na hatia Soma (Yohana
18;12-14,19-23).Baadaye ndipo walimpeleka kwa Kayafa aliyekuwa kuhani mkuu
mwaka ule ambapo hapo walitafuta ushahidi hata wa uongo ili wamuue wasiuone (Mathayo 26;57-68).
Mashitaka
mbele ya Serikali ya Rumi.
Biblia iko
wazi kuwa walipoona kuwa hakuna hatia walimpeleka kwa Pilato ambae Kihistoria
alikuwa liwali katili na aliyeamuru wengi kusulubiwa,Pilato pia hakuona hatia
ya aina yoyote na alijua kuwa alitolewa kwa Husuda;Ni wazi kuwa kuteseka kwa
mkewe Pilato dhidi ya hukumu ya Masihi kulikuwa kunaweka bayana kuwa masihi
hakuwa na hatia ya kidini,kisiasa na kihaini;Kufunguliwa kwa Baraba ilikuwa ni
desturi ya Pilati kila inapokaribia sikukuu, jambo ambalo hufanywa na viongozi
wengi wa Kisiasa hata leo,Baraba alijulikana
wazi kuwa ni muuaji na muhaini hata hivyo mioyo ya watu wenye dhambi
iliona vema kuchagua uovu kuliko wema na hivyo “Walipenda giza kuliko Nuru”(Mathayo 27;11-23).Pilato aliona ni Vema Masihi apelekwe kwa Herode labda hatia
ingeonekana,Hivyo hapa hakukuwa na Jitihada za Pilato au mkewe kumuokoa Masihi
na mauti ya Msalaba bali ni kuweka wazi kwa ulimwengu kuwa Masihi Hakuwa na
Hatia iliyostahili Yeye kuuawa isipokuwa ni kwa ajili ya Dhambi zetu mimi na
wewe (Isaya 53;1-9).
Mashitaka
Mbele ya Mfalme Herode.
Biblia
inathibitisha wazi kuwa Pilato alipoona kuwa Masihi hana hatia na kupata
uhakika kuwa ni mgalilaya aliamuru apelekwe huko nako ambapo hawakuona hatia
dhidi yake (Luka 23;3-15). Hatua
zote hizi zilikuwa na lengo lilelile la kutudhihirishia sisi walimwengu kuwa
Kristo hakuwa na Dhambi nay a kuwa alikuwa ni Mwana kondoo wa mungu aichukuaye
dhambi ya ulimwengu.
Yesu
anahukumiwa Kifo.
Baada ya kuthibisha wazi kuwa Yesu hakuwa na hatia ni
wazi kuwa hakimu yeyote ambaye ameapa kusimamia haki anawezaje kukubali
kumhukumu kifo mtu asiye na hatia?Akitaka kujihadhari na damu isiyo na hatia
pilato alinawa mikono (Mathayo 27;24-25)
ni wazi kabisa kuwa Hukumu ya Kristo ilichangiwa na mpango kamili wa
Mungu,uchaguzi wa watu waovu,shinikizo la wayahudi dhidi ya Pilato,Hofu binafsi
ya Pilato ambaye aliogopa ghasia,kupoteza cheo,Hadhi na manufaa yake mwenyewe
Ingawa alijua wazi kuwa Masihi hakuwa na hatia na alithibitisha hivyo mara
Kadhaa (Math 27;18,Yohana 19;4,6)
lakini kumbuka kuwa ni yeye ndiye aliyeidhinisha hatimaye kutoa hukumu ya kifo
dhidi ya Kristo.hii ndio ilikuwa Hatima,Ni lazima tujiulize kama ni kweli Pilato
alikuwa na nia ya dhati ya kumuokoa Kristo na mauti?kulikuwa na ulazima gani
basi kutoa hati ya hukumu ya kifo mbona waovu wengine walifungwa magerezani kwa
muda? Hata Yohana mbatizaji si aliwekwa Gerezani Tangu lini kesi ya hukumu ya
kifo ikasikilizwa siku moja na siku hiyohiyo kutolewa hukumu yake? Ni lazima
Tujue kuwa pilato anawajibika katika hatia ya kuhukumu isivyo halali hivyo
anayo dhambi (Yohana 19;11-19).
Yesu alifia Msalabani.
Kwa sababu
ya athari za imani potofu zilizokuweko Nyakati za Muhamad na upinzani wa
makusudi dhidi ya Injili Wanaharakati wa kiislamu wanatilia mashaka kama kweli
Yesu alifia Msalabani kwa madai kadhaa yafuatayo;-
- Kukatwa miguu kwa wanaume waliosulubiwa pamoja naye (Yohana 19;42-44)
- Kushangaa kwa Pilato kama Yesu amekwisha kufa (Marko 15;44-45).
- Kutoka kwa damu na maji kwa Yesu baada ya kufa
- Kwa kuzingatia historia kuwa kifo cha Msalabani ni cha Polepole;
Ukweli kuwa
Yesu alifia Msalabani unathibitishwa na matukio hayo hapo juu,Tendo la askari
wa kirumi kuvunja miguu ya wanaume wale wengine wawili linathibitisha kuwa Yesu
alifia msalabani;(Yohana 19;32-33).Kuacha
kumvunja Yesu miguu ni uthibitisho kuwa Yesu amefia msalabani,Haingekuwa rahisi
kabisa kwa askari wa kirumi kuliachia swala hili kama Isingekuwa Yesu
amekufa!Kwa mujibu wa taratibu za wakati ule askari wa kirumi kushindwa
kutekeleza wajibu aliopewa ni kujitakia hukumu ya kifo,wao walikuwa na wajibu
wa kuhakikisha kuwa watu hao wanafia msalabani kama hukumu yenyewe ilivyoamuru
na kwa kuwa wanaume wale wengine walikawia kufa ilikuwa ni lazima wakatwe miguu
ili wafe,
Kushangaa kwa
Pilato kuwa Yesu amekwisha kufa Mara hakutokani na jitihada zake za kutaka
kumuokoa Yesu,bali mshangao wake ulifuatiwa na Kupata uhakika kuwa Yesu amekufa
toka kwa Akida wa kikosi kilichomsulubisha Kristo Jambo lililomfurahisha
alipothibitisha hilo (Marko 15;44-45)
wahubiri wa kiislamu husoma mstari wa 44
tu na kusimamia uongo.
Kwa mujibu wa
historia na tabia za jeshi la askari wa
kirumi, ilikuwa ni kosa linalostahili kufa kwa kushindwa kusimamia wajibu
waliopewa mfano pale ,Petro alipofunguliwa kimuujiza na malaika na kutoka
gerezani, askari wote waliokuwa zamu na usimamizi wa siku ile waliuawa soma (Matendo 12;18-19). Jambo lingine
lifananalo na hilo ni pale gereza lilipojifungua kimuujiza baada ya maombi ya
Paulo na Silla ambapo vifungo vyao na vya wafungwa wengine viliachia mkuu wa
gereza alichagua kujiuwa kwani ni hukumu bmayo angeipata tu kama Wafungwa
wangekuwa wamekimbia (Matendo 16;27).Hivyo
kama askari wa kirumi alipewa jukumu na akashindwa kutekeleza jukumu
alihukumiwa kifo, ni wazi kuwa akida wa kikosi kilicho tumwa kumhukumu Masihi
kifo angeshindwa kusimamia jukumu lake angeuawa nafikiri ndio maana
alithibitisha kwa kumchoma mkuki ubavuni yaani kwenye moyo (Yohana 19;34). Tendo la kuchoma mkuki
katika moyo halikufanywa kwa wale waliokatwa miguu kwani walikuwa hai na kama
Yesu angalikuwa hai lile tendo la kusokomeza mkuki ubavuni ilikuwa ni Ishara ya
kummalizia kabisa!Ni lazima Waislamu wajue pia kuwa Tendo la Kristo
kutokuvunjwa miguu ni la kinabii na lilitabiriwa katika torati na zaburi soma (Zaburi 34;20),Jambo hili lilikuwa
linadhihirisha kuwa Kristo ndiye Pasaka ya kweli,Moja ya amri waliopewa wana wa
Israel kabla ya ukombozi kule Misri ni kumla mwana kondoo wa pasaka bila
Kumvunja mifupa yake soma (Kutoka 12;46).
Swala la Maiti ya Yesu kutoa maji na Damu;
Tendo hili nalo hutumiwa na waislamu kushutumu kuwa Yesu alikuwa amezimia
tu kwani maiti haiwezi kutoa damu na maji,Hii nayo inashangaza sana hebu soma
kwanza (Yohana 19;31-36).Tendo la
kutoka maji na damu liko miongoni mwa matukio yaliyo wazi yanayothibitisha kuwa
Yesu alifia msalabani, Yohana mwanafunzi wa Yesu aliyependwa sana anathibitisha
kuwa ushuhuda huu ni kweli kwanini? Kwa sababu yeye alikuwa karibu kabisa na
Msalaba wa mateso wa Kristo (Yohana
19;25-27),pia mama yake Yesu ambaye wakati huu alikuwa mtu mzima anayejua
maiti ninini naye alikuwa karibu kama shuhuda ya kuwa Yesu alikufa.
Sitaki kuchukua Muda kujadili
swala hili,wala sihitaji utafiti wa kisayansi kujua kuwa mtu aliyekufa anatoa
damu ya namna gani na aliye hai anatoa damu ya aina gani,lakini kwa ufahamu
wangu mdogo wa sayansi Damu ni muundo wa chembechembe hai za aina kuu mbili
yaani chembechembe hai nyekundu na nyeupe,hizi ndizo zinaunda damu,mtu aliye
hai anapoumia kwa kujikata hutoka damu yaani mchanganyiko wa chembechembe
hizo,Mtu anapokufa chembechembe hizi huganda,na endapo mtu anatoa damu na maji
maana yake,chenbechembe hizo zinazounda damu zimeachana hivyo huu ni uthibitisho
wa wazi kuwa mtu huyo amefariki,kwa habari ya maiti kutoa damu tumeshuhudia
watuwengi wakiwa wamekufa na siku mbili au tatu zikapita na wanaweza kutoa
damu,ni zaidi sana mtu aliyeuawa muda si mrefu ni rahisi kutoa damu, hivyo maji
na damu ni uthibitisho kuwa Yesu alikufa Msalabani.
Kama
hilo aliaminiki maandalizi na taratibu za mazishi ya kiyahudi ilikuwa ni pamoja
na maiti hiyo kuzongwazongwa kwenye sanda ya kitani namna walivyokuwa
wanafungasha ilikuwa hatakama uko hai kuna uwezekano ukafa(Yohana 11;43-44 19;40).Nafikiri kama Yesu alikuwa hai wasingeweza
kigiza mchezo huu wa kufungasha maiti kama ilivyokuwa desturi yao hivyo aina
hii ya ufungashaji wa maiti inathibitisha kuwa Yesu alikufa hakika pale
msalabani na alizikwa! Na siku ya tatu alifufuka.
Kwanini Yesu
alikufa mapema zaidi ya wahalifu wale wawili wengine?
Mazingira
ya kifo cha Msalabani kwa Yesu.
Yako madai
kutoka kwa wanaharakati wa kiislamu kuwa Yesu alikuwa na afya nzuri na ndio
maana aliweza kufunga siku arobaini na kutembea kwa miguu sehemu mbalimbali, na
kutokana na mazingira ya hukumu ya kifo cha msalabani kilikuwa ni kifo cha
polepole isingekuwa rahisi Yesu kufa msalabani mapema na ushahidi ni kwa wale
wahalifu wengine waliolazimika kukatwa miguu ili wafe mapema.
Nataka kuwajibu
waislamu hoja hii kwa ufupi kuwa waalifu wale wengine wawili walibeba misalaba
yao na kwenda kusulubiwa moja kwa moja bila mateso ya aina yoyote mbadala.
Lakini kwa Bwana Yesu yeye alikamatwa Mapema alfajiri katika siku hii
hatuambiwi kama alihudumiwa kwa chakula au la? lakini bila shaka wafungwa wale
wengine walihudumiwa gerezani kama kawaida, akiwa hajala kitu alianza kuteswa (Mathayo 26;67),Tunaambiwa kuwa alipigwa
makonde na makofi,hatuambiwi ni kwa kiasi gani,Pia tunaambiwa kuwa alipigwa
mijeledi ambayo kwa mujibu wa Historia Enzi za Warumi, Mtuhumiwa alivuliwa nguo
zote na kuwambwa kwenye nguzo au kuinamishwa kwenye nguzo fupi na kufungwa
mikono yake na kuchapwa na kifaa maalumu,Kifaa hiki cha kuchapia yaani mjeledi
kilikuwa ni kifaa chenye Mpini mfupi wa mbao ambapomikanda kumi na mbili ya
ngozi iliambatanishwa ikiwa na vipande vya chuma au mifupa iliyofungwa kama
shanga kwenye kila mkanda,vipigo vilifanywa na wanaume wawili mmoja upande huu
na mwingine upande huu, Kipigo hicho kilipelekea nyama ya mwili kupurwa au ku
katwa katwa kiasi cha kuweza kuathiri mishipa ya fahamu, vena na ateri na hata
kuumiza viungo vya ndani vya vya tumbo na wakati mwingine vilitoka nje jambo
hili pekee lilifanya watuhumiwa wengi kufa
wakati wa kupigwa mijeledi,Mijeledi ilikuwa inaharibu kabisa sura ya Mtu
ukweli ilikuwa ni adhabu yenye kutisha sana,Inawezekana kabisa kushindwa kwa
Yesu kuubeba msalaba wake na kuanguka mara tatu na hatimaye kusaidiwa na Simon
mkirene kulitokana na kuchoshwa na kipigo cha mijeledi alichopata (Math 27;32, ), Achilia mbali kule
kusimikwa kwa taji la miiba kama mfano wa taji kichwani ambapo kulitoboa maeneo
ya kichwa na mishipa,kubeba ule msalaba,Na baadae kugongomelewa masumari mazito
ya chuma yenye umbo la mraba miguuni na kusimamishwa na kuchuruzika madamu kwa
masaa masaa tkribani sita hivi,misuli inavutwa Ngozi inaharibika,huku kukiwa na
dhihaka na matusi na shutuma ili kuteswa kiakili katika hali kama hii hata kama
ulikuwa unalia huwezi kulia tena ni
rahisi kuhisi kuwa Mungu amekuacha! Acha kiu ya maji ambayo kwa mateso kama
haya mtu alalamika kua ana kiu maana yake kutokana na kumwagika kwa damu nyingi
akiomba maji akinywa anakufa(Yohana
19;28).hivyo kuomba maji kwa Yesu
kunaashiria alikuwa amefikia hatua ya kukata roho na kwakweli ALIKUFA!. Mateso haya kwa kweli
yalichangia Yesu kufa mapema kuliko wale wengine.
Pamoja na
mateso hayo yoote aliyoyapata Masihi ambayo yalichangia kufa kwake mapema kabla
ya wale wawili,Inashngaza eti kuona wahubiri wa kiislamu wanakosa shukurani na
kugundua Upendo mkuu aliokuwa nao Yesu kwa ajili ya ulimwengu na wao pia badala yake wandhihaki kazi hii ya huruma kwa
wanadamu na wanafanya jitihada za kuipinga kazi hii kwa makusudi hii ndio
shukurani wanayomlipa Mungu kuupinga msalaba jaribu kuwaza ni hukumu gani
itawapata watu wa jinsi kama hii kwa kushindwa kumuamini Yesu na kushikamana na
marehemu Muhamad na kusahau kuwa mateso ya Kristo yalikuwa ni kwa ajili yao.
(Isaya 53;2b-5). “…Yeye hana umbo wala
uzuri, Na tumuonapo hana uzuri hata tumtamani, Alidharauliwa na kukataliwa na
watu; Mtu wa huzuni nyingi ajuaye sikitiko; Nakama mtu ambaye watu humficha
nyuso zao,Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu,Hakika ameyachukua
masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu, Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, amepigwa
na Mungu na Kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu. Alichubuliwa kwa Maovu
yetu, Adhabu ya amani Yetu ilikuwa juu yake na kwa kupigwa kwake sisi
tumepona….”
Pichani Hivyo ndivyo jinsi mjeledi ulivyo.
Isaya nabii
alitabiri vema na kuonyesha wazi kuwa ni kifo cha namna gani Masihi angekufa
soma aya hizo hapo juu za unabii wa Isaya kumhusu masihi, Hivi karibuni
wataalamu wa biblia walifanya utafiti wa kutosha kuhusu Mateso yaliyompata
Masihi na kujaribu kuyaigiza katika filamu iitwayo “The passion of Christ”Tunaweza kusema kuwa lile kilichoigizwa
katika filamu ile ni sahihi kabisa na kuna uwezekano kuwa mateso hayo yalikuwa
zaidi ya kile kilichoigizwa,Lakini lile wazo la nabii Isaya limeweza kufikiwa
kwa aslimia zaidi ya themanini!
Pichani juu ni muigizaji maarufu wa filamu “The passion of the Christ” akiigiza kwa
karibu sana aina ya Mateso aliyoyapata kristo ndugu huyu amejipatia sifa kubwa
kwa uigizaji unaokaribiana na kile Biblia inachosema.(Picha na Maelezo Na Rev.
Innocent Samuel kamote Mwandishi na
Mtunzi wa somo hili. @ 2007.)
Pichani juu
ni kaburi alilozikwa Bwana Yesu kisha akafufuka,liko wazi hata leo,Watu wengi
huenda mahali hapo kwa shughuli za kutalii tu .Eneo hili huitwa Garden
Tomb,Yaani Bustani ya Kaburi,Mungu amepatunza mahali hapa hata leo hii ili watu
wapate kusadiki kuwa Yesu yu hai.Maelezo
na Innocent Samuel Kamote,Picha kwa hisani ya The Zondervan Pictoria Encyclopedia of the Bible 2002.
Hoja Kuhusu
Wasiwasi wa Wayahudi kuhusu kifo cha Yesu.
Hii ni
mojawapo ya hoja ambayo waislamu huitumia kuwa tendo la viongozi wa kiyahudi
kuomba kaburi la Yesu lilindwe lilikuwa linamaanisha kuwa Yesu aliteremshwa
Msalabani akiwa amejeruhiwa tu yaani aklwa hai Hivyo waliomba kwa Pilato kaburi
lilindwe sawia asije akakimbia (Mathayo
27;63). Soma Mstari huu kwa makini,
Hapo utagundua tatizo,la waislamu,jinsi wasivyojua kusoma Biblia!,sawa na
kanuni zake,Hapa kanuni iliyokiukwa Inaitwa kanuni ya kifungu kizima “The principle of Context”Wakati wanaharakati wa kiislamu wakifikiri kuhusu Yesu kupona
na kutoroka,Hofu ya wayahudi hapa ilikuwa ni kuibiwa kwa Maiti kisha watu
kuambiwa kuwa amefufuka!. (Mathayo
27;63-66).Hapa kuna mambo mawili hasa ambayo wayahudi walikuwa wakiyahofu
ndani yake kuna kweli kuu ambazo zinafunuliwa kwetu, angalia sentensi ifuatayo
kwa makini
“…Tumekumbuka kwamba yule Mjanja alisema
alipokuwa akali hai…”
Sentensi hii inatuthibitishia kuwa wayahudi, na
viongozi wao walikuwa na uhakika bayana kuwa Yesu alifia msalabani,na kua
alizikwa,angalia maneno yale “….alisema
alipokuwa akali hai” maana yake sasa amekufa! Hapa walikuwa wakifanyia kazi
maneno ya unabii wa Yesu mwenyewe kuwa hata baada ya kuuawa kwake siku ya Tatu
atafufuka (Luka 9;22). Hofu yao kuu
ilikuwa kwamba kufufuka kwa Yesu Masihi kungeathiri,Mipango na umaarufu wao
kumbuka kuwa ulimwengu ulikuwa unamwendea yeye hususani pale alipomfufua lazaro
Yohana 12;9-19, ikiwa umati mkuu
ulikuwa unamwamini Yesu na hivyo kusababisha wao kupanga kumuuaYohana 12;47-53, unafikiri wangefurahi
kuona yeye mwenyewe akifufuka?Kwao Yesu aliitwa muongo na kuwa kwa uongo wake
watu walimwamini na kama akifufuka uongo wa mwisho utapita ule wa kwanza, Hata
hivyo yeye ndiye kweli halisi (Yohana
1;16-17).Hofu yao ilikuwa kufufuka kwa Yesu kungeleta kuaminiwa zaidi na
heshima zaidi kuliko mwanzoni hii ndio ilikuwa hofu ya maadui wa Kristo, hata
leo wale wanaotaka kupunguza heshima ya kristo huushambulia msalaba na ujumbe
wake (1Koritho 1;18). Ningependa
kutoa ushauri wa bure kwa waislamu kuwa
wanapoisoma biblia wawe na mioyo yenye utii,mioyo safi na si kwa lengo la kuikosoa, Mtu yeyote
aliyeharibika moyo hawezi kulifasiri neno la Mungu kwa halali.Moja ya kanuni za
mwanzo kabisa za kulitumia neno la mungu kwa halali ni pamoja na utii “The principle of Obidient”
Na Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima
Rev. Innocent Mkombozi Kamote
kwa maoni na ushauri ikamote@yahoo.com
Na Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima
Rev. Innocent Mkombozi Kamote
kwa maoni na ushauri ikamote@yahoo.com
Asante sana Mtumishi kwa mada hii tamu sana.
JibuFuta