Jumapili, 31 Januari 2016

NIKA BWABWANYA MWANAUME!



Nilikuwa nina miezi kama mitatu tangu kuoa kwangu, Ilikuwa ni juni mwaka 2003, mke wangu alikuwa akiniamini sana na hata wazazi wake hasa mama yake kwani alinifundisha shule ya msingi wakati akiwa mwalimu mwaka huo 2003 alistaafu.

 
Mdomo ulikipoza Kichwa !

Siku moja nilikuwa nyumbani na mke wangu alikuwa ameenda kwao, ilikuwa ni mapema bado kama saa nane  kwa hiyo sikuwa nategemea kumuona  kwa wakati ule  tulikubaliana kuwa angerudi jioni, nilikuwa nimekaa sebuleni nikiangalia televisheni, mara simu yangu ikaita, nilipunguza sauti tv yangu hadi mwisho na kupokea simu, ilikuwa inatoka kwa msichana ambaye nilikuwa nimeanza uhusiano naye kama mwezi mmoja nyuma , ukweli hadi leo najiuliza niliweza kufanya vipi jambo kama lile kwani sikuwa kabisa mpenda wanawake  na nilikuwa pia naheshimu ndoa yangu.

Nilipokea simu na kuanza kuzungumza naye usijali mpenzi kesho nitakuona …Nani first Lady? Hana neno huyu wala hawezi kunishtukia, kwani ananizimia sana, nimemshika kwelikweli, unajua nini ulichelewa kidogo tu kujitokeza kwangu lakini pale madhabahuni kabla ya miezi mitatu tu ulitakiwa uwe wewe na sio yeye niliendelea kubwata na kubwabwanya lakini hata hivyo hakujaharibika neno huku nimefungwa pingu za kanisani lakini moyo wangu uko kwako mpenzi, nakuhakikishia kwamba  nikiwa nawe kila kitu kinabadilika  kinakuwa super, Naanza kumchoka jamaa kwani hata nikiwa naye naiona sura yako kwake …”  ilinibidi ninyamaze kwani nilistuka kwa namna ambayo hata ingeweza kuniua kwa shinikizo unajua nini ? Nilimuona mke wangu akiwa na mama yake  wakiwa wamesimama, kwa kweli nilijifaragua sana kutaka kuwakaribisha  lakini walivyokuwa wakinitazama  nilinywea na sauti ikakauka  ‘Ulikuwa unaongea nini  na nani mke wangu aliuliza nilibabaika na kabla sijasema  ni..ni.. Jamaa mmoja …’ niliwashwa kibao cha maana sana  shavuni na mke wangu . Halafu alinivaa na kunitupa chini nilikuwa sina nguvu kabisa bwege hasa , kweli kufumaniwa ni kubaya sana, mama mkwe aliingilia kati na kuamua kumuondoa mwanae wapangaji upande wa pili wa nyumba nao walifika na kutuamulia. 

Mama mkwe alimshika mkono binti yake na kumwambia twende acha kila kitu humu ndani usichukue chochote inatosha kwa haya tuliyoyaona waliondoka na binti yake, nilibaki nikiwa nimefedheheka vibaya sana, wapangaji wa upande wa pili wa nyumba walionekana kufurtahia sana dhahama ile, kwani tulikuwa tukiwasema sana kuwa ndoa yao ni ya kuunga na gundi, Najua unataka kujua ilikuwaje baada ya pele huo ndio unaitwa umbeya!

Lakini kwa kukukata kiu yako ya umbea ni kwamba baada ya pale tulikuja kurudiana, Alikuja kunisamehe na baada ya kumueleza ukweli wote kwa kweli siku hizi nikiona mwanamke nisiyemjua ananichekea nafunga viatu vizuri ili kuanza mbio za marathoni zisizo na malipo maana nilikwisha kuyapata.
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni