Alhamisi, 28 Januari 2016

NIMEKUKIMBILIA WEWE BWANA NISIAIBIKE MILELE


ZABURI 71:1-24.
 
Utangulizi:
Zaburi ya 71 ni zaburi inayofikiriwa kuwa ni zaburi yatima kwa vile mwandishi wake hajulikani, hata hivyo naweza kuifikiri zaburi hii kuwa ni ya Daudi kwa vile ina muungano na Zaburi ya 70 ambayo tuna uhakika kuwa imeandikwa na Daudi, Zaburi hii ni zaburi ya Maombi na inaonekana kuwa ni maombi yanayofanywa na mtu mzima au mzee, akililia msaada wa Mungu kwa Haraka.

Zaburi 71:1-4.
Mwandishi amekuwa mtu mzima lakini maisha yake ya uzee yanasumbuliwa na adui, adui mwenyewe ni mwovu, katili na mdhalimu hana huruma, anachokitaka ni kusambaratisha na kuangamiza maisha ya mtu huyu, Mzee anaona ni kama ataaibishwa hapa, Uzee hapa pia unaweza kutumika kama uzoefu. Kutokana na mazingira haya magumu ya kuzungukwa na adui, mwovu na mdhalimu, Mwandishi anaonyesha kuwa ana uzoefu kuhusu Mungu na jinsi alivyoweza kumshindia vita za aina mbalimbali katika maisha. 

Mstari 4 “Ee Mungu wangu uniopoe mkononi mwa mkorofi, Katika mkono wake mwovu Mdhalimu”
Mwandishi wa Zaburi anajua kuwa hakuna njia nyingine, namna iliyoko mbele ni kumuomba Mungu na hivyo anajitegemeza katika kuomba na kumkumbusha Mungu namna alivyomshindia vita za aina mbalimbali, tangu ujana wake na jinsi Mungu alivyokusudia mema tangu kuzaliwa na tangu tumboni mwa mama yake Zaburi 71:5-9.

Mwandishi anaangalia mpango wa adui wa sasa “Mstari wa 10-11”  “kwa maana adui zangu wananiamba nao wanaoniotea roho yangu hushauriana , wakisema , Mungu amemwacha, Mfuateni mkamateni, hakuna wa kumponya”

Adui ana mpango mbaya juu ya maisha ya kila mmoja wetu, anataka kuivizia roho yetu anataka kutuua, anafikiri Mungu ametuacha, anafikiri ni kipindi cha kutukandamiza,kutukamata na hakuna namna tunavyoweza kuponyoka. Haya ndio yalikuwa mazingira ya mwandishi wa zaburi hii na wakati mwingine huwa ndio mazingira yanayokuzunguka. 

Mst 12-24 mwandishi kupitia uzoefu alionao anatabiri kuwa Mungu hatamuacha aaibike milele na kuwa  Mungu atakuwa upande wake na kuwa Mungu atampigania na kuwa atasimulia na kushuhudia Matendo makuu ya Mungu na na sifa zake na haki yake kwakuwa wameaibishwa wametahayarika walionitakia mabaya, waliokusudia kumuaibisha wameaibishwa wao.

Msomaji wangu Ukimtumaini Bwana hutatahayarika!, Mungu ndio kila kitu katika maisha yetu ni lazima tumkimbilie na kumtegemea yeye kwake kunalipa tukimtegemea Mungu, hatatuacha tuaibike, Bwana atakushindia kutoka vita moja kwenda nyingine aina yoyote ya udhalimu wa kishetani, kiafya, kiuchumi, kikazi, na mengineyo Mungu atatutetea yeye alisema nitawapigania nanyi mtanyamaza kimya Neno la Mungu ni dhahiri na tujikinge kwake

Mkuu wa Wajenzi Mwenye Hekima.
Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni