Alhamisi, 28 Januari 2016

UJUMBE: NINA NINI NAWE, YESU, MWANA WA MUNGU ALIYE JUU?


ANDIKO LA MSINGI MARKO 5:1-20.
   Jacob Koshy alikulia katika mji mkuu wa Singapore akiwa na maono ya kuwa Dereva na kuwa na mafanikio makubwa sana katika maisha, alikuwa na ndoto za kupata fedha na kumiliki mali, Hata hivyo mpango wake huo ulimpelekea kujiunga na mtandao wa kimataifa wa kusambaza madawa ya kulevya Duniani, mwaka 1980 alikamatwa na seriakali na kuwekwa Gerezani.
    Alikata tamaa sana, alichoka kabisa, kwa vile ndoto zake, makusudi na mipango ya maisha aliyokuwa nayo iliharibika kabisa hakukuwa na tumaini tena na alivunjika moyo, alijiingiza katika uvutaji mkubwa wa sigara na tumbaku, hata ingawa havikuwa vinaruhusiwa huko Gerezani, alipopata tumbaku ili aweze kuivuta alitumia karatasi za Biblia ya GIDEON ili kusokotea tumbaku na kuvuta, siku moja alipitiwa na usingizi huku akiwa anavuta, aliposhituka aliona karatasi yote ya sigara imeungua na kimebaki kipande kidogo cha karatasi, alipoamua kukikunjua alikuta kimeandikwa “Saul Saul Mbona waniudhi?”  Jacob aliomba Biblia nyingine na kuisoma habari ya Saul kwa undani zaidi, kisha akajisemea Kama Yesu anaweza kubadili mwelekeo wa mtu katili namna hii, bila shaka anaweza kubadili mwelekeo wangu, aliamua kupiga magoti na kumkubali Yesu akiwa Gerezani, Maisha yake yalibadilika alikuwa ushuhuda kwa wafungwa wengine, alitolewa gerezani kutokana na badiliko kubwa, alijiunga na kanisa na kufanya kazi za kanisa alioa mke wa Kikristo, kwa sasa Jacob amekuwa Mmishionari anayehubiri njili huko Mashariki ya mbali akiwaeleza watu, Yesu ni Mwana wa Mungu aliye Juu.
    Marko 5:1-9 Biblia inasema “ Wakafika ng'ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi.  Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu;     makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo;  kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda.  Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe.  Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese.  Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu.  Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni,”
     Ndugu Msomaji wangu nafahamu kuwa husomi ujumbe huu kwa bahati mbaya Nguvu zake Mjenzi mkuu wa Mbinguni zimekuvuta ili apate kukuganga na kukuponya moyo wako, inawezekana umepigika, huna amani, umepoteza kiu na shauku ya maisha, ndoto zako na mitazamo yako imepotea, unaona giza kila inapoitwa leo, hujui hata kesho itakuwaje, hupendi kufa lakini unaona heri hata ya kifo, unashindwa uchague nini unaona heri kusikuche, ni giza linakuzunguka kila kona unajuta laiti ningefanya hivi au vile na unaweza kumchukia Mungu na kuona ni kama anakuleta katika hatima ngumu na ya aibu kila kitu kinakataa!
   Hali hii ndio inayomkuta Kichaa tunayesoma Habari zake katika Marko 5:1-7 mtu huyu aliishi makaburini, ni kama alikua anawaza kufa au alizungukwa na mauti na akawa anatamani kufa ama alikuwa akiwajutia ndugu zake waliokufa zamani, au mapepo yalimuongoza kushinda makaburini, alijitenga na ulimwengu wa walio hai, alijiona hastahili kuwa miongoni mwao, alijawa na huzuni, maisha yake yalisikitisha, aliishi maisha ya upweke, hakuwa na mtu wa kumtia moyo, alikuwa amekwazwa na jamii na jamii imechoka naye, amaumizwa ni muhitaji, hakuwa na mtu wa kumuonyesha upendo, hakuna aliyesema dally wala honey hakuna mtu aliyetamani kuwa naye wala kupiga naye story hali yake ilikuwa mbaya, alikuwa ni picha ya mtu aliyetengwa mbali na huruma za Mungu, amekatiliwa mbali na Mungu na watu wake pia hali ya mtu huyu ilikuwa ya kusikitisha hakuwa na nguo mwili wake haukujua jua wala baridi aliishi maisha ya kusikitisha mnomno.
Mstari 3-5 hakuwa na msaada biblia inasema hakuna mtu aliyekuwa na uwezo wa kumfunga tena kwa minyororo, ilikuwa ngumu kumdhibiti tena mtu huyu, alikuwa anauwezo wa kukata kila aina ya minyororo, alijichukia alitamani kufa alijikatakata na kupiga makelele ukichaakichaa ulimvamia hii ilikuwa ni picha ya mtu aliye katika vifungo vya Ibilisi, hata watu waliojaribu kumsaidia walichoka naye, alibaki na huzuni na kukosa msaada ni kama alikuwa katika gereza la Mateso na uonevu na katika mikono isiyo na huruma ya mashetani.
Mstari wa 5 Mateso yake yalikuwa endelevu ilikuwa usiku na mchana, alijikatakata na kujijeruhi kwa mawe, hakuwa na uzuzi wala ngozi nzuri, angeoga saa ngapi, aligeuka kuwa kama mnyama, huenda alirushiwa chakula kwa mbali na alikula kama mbwa, hii inaonyesha hali zinazowazunguka walimwengu wengi, huwezi kujua kwa nini wengine wanajiingiza katika ukahaba wa hali ya juu, uvutaji wa bangi na madawa ya kulevya, ulevi na ujambazi uliokithiri na hawawezi kujitoa kamwe huko kwani ziko nguvu za manyanyaso zinawakandamiza huko na wakati mwingine hawafanyi kusudi, hawawezi kujiweka huru na wanamezwa na huzuni za historia ya maisha yao yasiyo na msaada
Akiwa katika hali ya kusikitisha na amekosa msaada mji mzima siku moja Yesu alifunga safari kwenda katika nchi ile, iko wazi kabisa kuwa Yesu hakuwa na jambo lingine lolote la kufanya katika mji ule alikwenda akiwa na jambo moja tu, kutoa msaada kwa mtu huyu, hatujui kama akili zake ziliweza kutambua chochote maana alikuwa amepagawa na mapepo yaliyojiambulisha kwa jina la Legion la kirumi ambalo maana yake ni kikosi cha jeshi la askari 6000, askari hao au mapepo hayo ndiyo yaliyoweza kumtambua Yesu, walipiga mbio wakiwa katika mwili wa mtu huyu na kusujudu na kupiga kelele NINA NINI NAWE, YESU, MWANA WA MUNGU ALIYE JUU? Kumbuka jinsi ambavyo hata safari ya Yesu ya kufika nchi ile ilikuwa ngumu kulikuwa na upepo mkali ambao Yesu aliukemea ni wazi kuwa mazingira ya mji ule na nchi ile ya wagerasi yalikuwa na nguvu za giza tupu, yalikuwa ni ngome ya shetani yalikuwa hayapenyeki kirahisi, ilikuwa ngumu hata mapepo yale kuhama nchi ile kwani yaliomba yasihamishwe katika nchi ile yalikuwa na madai maalumu, yalikuwa na miliki maalumu, yalikuwa yameufanya mji ule kuwa kiti chao cha enzi, Lakini hata hivyo mapepo yale yalikuwa na uelewa maalumu kuwa Yesu ni nani Yalimuapisha Yesu kwa Mungu kuwa asiwatese Biblia inasema mashetani huwa yanatetemeka Yakobo 2:19 Yalitetemeka na kusujudu yalipomuona Yesu ambaye ni kiboko yao.
Leo ni siku yako ya kuwekwa huru ninakutangazia ukomo wa misiba na majanga na mikosi na balaa na nuksi na laana na mitazamo na manuizo na matamshi mabaya uliyotamkiwa kwa mamlaka niliyopewa kama myumishi wa Mungu aliye hai namuomba Mungu abadilisha maisha yako, iwe ghafla au kidogokidogo Mungu akubadilishe kabisa imetosha mateso yako, vifundo vya kichawi na nguvu za kiza ziharibiwe na uwe huru kwa Damu ya Yesu Kristo matatizo yako yapige kelele nina nini nawe Yesu mwana wa Mungu aliye juu!
Ashukuriwe Yesu mwana wa Mungu aliye hai kijana huyu aliyefungwa kwa miaka alijikuta akiwa katika mikono salama ya Bwana na mwokozi mwenye wingi wa huruma na neema Yesu alitoa msaada Yesu hakufanya jingine katika nchi ile zaidi ya kumponya mtu huyu na kumuweka huru!
Hali ya mtu huyu mwenye kuteswa na mapepo na Jacob Koshy zinafanana na hali za wengi wetu kwa mazingira tofauti, kumbe Bwana anatujali anajishughulishja na maisha yetu, hajabadilika Yesu Kristo ni Yeye Yule jana leo na hata milelel amaegharimika kwaajili yetu, yuko tayari kubadili maisha yetu, kutoka katika hali ya kutokuheshimika kutupeleka katika hali ya kuheshimika, kutoka katika kupoteza tumaini kutupeleka katika tumaini, kutoka katika hali ya ukichaa kuwa wapeleka habari njema, kutoka katika kufanyika kuwa nyumba ya shetani kutufanya kuwa nyumba ya Roho Mtakatifu, maisha ya mtu huyu yalibadilishwa na kujaa neema ya Mungu angalia kuwa
Mtu huyu aliponywa, akili zake zilirejea
1.   aliketi akiwa salama
2.  alivaa mavazi
3.  alirudiwa na akili zake
4.  alikuwa tayari kumfuata Yesu
5.  alifanyika Muhubiri wa Injili
6.  na Mungu alitukuzwa kwaajili yake.
Yesu alimkomboa kwa gharama kubwa Machoni pa Yesu mtu huyu alikuwa wa thamani kuliko wanyama wa kufugwa waliokuweko katika mji ule, ni muhimu kufahamu kuwa watu waliofuga nguruwe hawakuwa Wayahudi  wayahudi waliamini kuwa nguruwe ndiye moja ya wanyama wachafu zaidi walio najisi hivyo ni wazi wafugaji walikuwa ni mataifa hivyo ni wazi kuwa walishiriki maswala ya kichawi na Yesu aliwatia hasara, kwani ni wazi pia ya kuwa mtu huyu alirogwa! Wachawi hao waliogopa kupata hasara kwani walimsihi Yesu aondoke katika nchi yao
Gharama ya ukombozi wake Mapepo yaliyotoka yaliomba yawaingie Nguruwe, mapepo yaliwaingia Nguruwe 2000, kilo moja ya nguruwe leo ni 6000-7000 kama kila nguruwe alikuwa na kilo 200 chukua 7000 x 200 x 2000 = 2,800,000,000/- Bilion 2 na milioni mia nane ilikuwa ni thamani ya kichaa Yule aliyeokolewa na Yesu
Ndugu yangu thamani yako katika macho ya Mungu Baba na Mikono ya Yesu kristo ni kubwa sana, haijalishi wewe ni kahaba, kichaa, mvuta bangi, shoga, mla madawa ya kulevya, uliyekataliwa, chokoraa, usiyesoma, mwenye ukoma, mwenye ukimwi, unaishi na hiv, una sukari, huna thamani kwa mumeo, mkeo, ndugu zako, unaonekana mzigo na kadhalika wewe kwa Yesu sio mzigo kwa mjenzi mkuu mwenye huruma wewe ni wa thamani, unamuhitaji Yesu tu abadilishe maisha yako yeye Yuko tayari kubadili historia yako na kukupa msaada ikiwa uko tayari fuatilia maombi haya ninayokuombea kwa kumaanisha kabisa kutoka Moyoni
Mungu mwema! Na Baba yangu! mtumwa wako ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa nikibubujikwa na machozi, ninajishusha chini ya magoti yangu najiinamisha katika miguu yako kwaajili ya msomaji na msikilizaji wa ujumbe huu Eeeee Bwana Mungu wangu hakuna mwanadamu aliye mbaya sana duniani kiasi ambacho asihitaji au asisitahili kupata rehema zako nakuomba leo eeeeee bwana Mungu wangu katika Jina la Yesu Mwana wa Mungu aliye Juu umponye na kumuhurumia msomaji wangu ili ajue ya kuwa nguvu zako zipo hata katika maadnishi haya badili kabisa maisha yake nakulilia ee mwokozi usiitazame dhambi yake wala ya jamaa zake wala ukoo wake, wala makosa yake, kumbuka rehema zako hata katika hasira zakoooo  oooooh ohhhhho Bwana mtumwa wako ninakusihi badili kabisa maisha ya mtu huyu leo aliyekosa msaada ufanyike msaada kwake katika Jina la Yesu Kristo ameeen!
Baada ya sala hiyo nilikuwa nalia machozi nilipokuwa nakuombea naamini umetembelewa na Mungu huyu tumwabuduye niandikie ili nimshukuru mungu pamoja nawe au acha ujumbe wako chini ya ujumbe huu katika face book
Rev. Innocent Kamote
0718990796
MKUU WA WAJENZI MWENYE HEKIMA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni