Alhamisi, 28 Januari 2016

UJUMBE: AGANO LA RANGI SABA!



Mstari wa Msingi Mwanzo 9: 12-17.
Utangulizi:
Rangi saba Kisayansi ni matokeo ya kuakisiwa kwa Mwanga wa jua katika matone ya maji ya mvua au mabaki ya matone ya maji ya mvua yaliyoko angani ambayo husababisha kuonekana kwa umbile la Duara lenye rangi saba maarufu kama Upinde wa Mvua, umbile hili hutoea wakati jua likiwa upande wa mashariki zaidi linapoelekea kutoka kuchomoza au upande wa magharibi zaidi linapoelekea kuzama “rainbow”


Kibiblia upinde wa mvua ni agano la Mungu alilolifanya Nuhu pamoja na wanadamu wote waliosalia juu ya uso wa nchi tangu baada ya gharika ya hasira za Mungu zilizoanguka juu ya uso wa nchi kwa sababu ya dhambi za wanadamu.
13-15 “Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni Ishara ya agano kati yangu na nchi, Hata itakuwa nikitanda mawinguni juu ya nchi, upinde utaonekana winguni nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili”
Angalia maneno hayo kwa makini! Angalia kwa makini sana! Tukiacha sababu za kisayansi Upinde wa mvua ni Ishara, ni ishara ya agano kati ya Mungu na wanadamu, Upinde ni wa Mungu, Pamoja na maelezo mazuri ya wanasayanzi Mungu ni zaidi ya wanasayansui Yeye ndiye anayeuweka upinde huo na autazamapo hukumbuka agano lake, ni Ishara ya uwepo wa Mungu mwenyewe angalia maneno yale Itakuwa NIKITANDA MAWINGUNI ni yeye ndiye anayeusababisha utokee na kutukumbusha na kujikumbusha “REHEMA ZAKE KWA WANADAMU MILELE” Hataruhusu tugharikishwe tena na maji! Hataruhusu Hasira yake iwahukumu wanadamu kila autazamapo upinde, Upinde huu ni agano la Milele sio kwa Nuhu na wanawe tu, bali na wanadamu wote tulioko leo ambao ni uzao wa Nuhu. Hivyo upinde wa Mvua ni alama muhimu ya milele iliyobaki inayoweza kuonekana kwa macho, ukiacha Nguzo ya wingu, iliyowaongoza Israel Jangwani.
Ni muhimu kufahamu je katika upinde huu wa mvua Mungu anatufundisha nini, ni muhimu kufahamu kuwa katika agano hili la upinde wa mvua ndani yake kuna rangi saba na rangi hizi ndio zinazoleta ujumbe muhimu kwa wanadamu
1.       Rangi nyekundu (Red)– Katika upinde wa mvua rangi hii huonekana kwa ukali zaidi kama rangi muhimu na iliyo juu ya nyingine, ni alama ya Damu, hakuna mtu anaweza kumfikia Mungu au kupokea rehema za Mungu, damu ndio njia pekee ya kumfikia Mungu,Israel walikombolewa kutoka Misri na kulindwa dhidi ya hukumu kwa tendo la Pasaka yaani walichinja kondoo kwa maelekezo ya Mungu na Damu yake ilitumika kupaka miimo ya malango, hivyo hasira ya Mungu haikuipiga nyumba zao badala yake walipata rehema (Kutoka 12:12-13) Kumbuka pia jinsi Rahabu kule Yeriko alivyookolewa na nyumba yake kwa kuweka alama ya kamba nyekundu Yoshua 2:18-21,  watu waliomwamini Kristo wamekombolewa kwa Damu ya thamani ya Mwana wa Mungu(1 Petro. 1:18-19)
    Tuionapo rangi nyekundu katika upinde wa mvua inatukumbusha kuwa hakuna pigo lolote la hukumu ya Mungu linaloweza kutupiga, na linamkumbusha Mungu ahadi hii na kuwa katika kuhukumu kwake atakumbuka Rehema, hili ni agano linalotuthibitishia kuwa sasa basi hakuna hukumu ya adhabu juu ya hao walio katika Kristo Yesu! Rangi nyekundu ikiwa juu yako, haijalishi historia yako ilikuwa ni ya namna gani Mungu anayo njia na ametupa njia ya kumkaribia yeye na kufaidi rehema zake hii ni damu ya Yesu inatukumbusha Rehema ni damu inayolia ili kwamba tusilipizwe kisasi bali tusamehewe, Rehema za Mungu zipo na zinapatikana kwa kazi aliyoifanya Yesu msalabani , tunaweza kumuendea yeye na kupata neema,
2.       Rangi ya Zambarau (Purple) -  Rangi hii Kihistoria na kibiblia ni rangi ya utawala au ufalme licha ya kuelezea Kuwa Yesu ni mfalme wa wafalme pia inaelezea kuwa sisi ni watawala au wafalme  (I Petro 2:9 ) Biblia inasema hivi “ Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema. Biblia inaonyesha Jinsi ambavyo Mungu amaetufanya ukuhani wa kifalme watu wa milki yake waliopata rehema ujumbe huo uko katika rangi ya zambarau kila tuionapo katika upinde wa Mvua unatukumbusha mamlaka na utawala tuliopewa wanadamu dhidi ya ulimwengu na mazingira yake, Mungu anataka tuutawale ulimwengu na kumiliki kila kitu.
3.       Rangi ya Chungwa (Orange) – Rangi hii inazungumzia Maisha mapya, Mungu mwenye uwezo wa kufanya yote kuwa mapya kwa rehema zake, anasahau yote yaliyofanywa na wanadamu huko nyuma na sasa anaanza Historia mpya, sahahu uharibifu na maangamizi yote yaliyokupata huko nyuma, kamwe sio mpango wa Mungu kuhusu future yako MUngu anakusudia kuandika historia mpya wakati wote katika maisha yako, sahau historia ya kushindwa, ya kuharibikiwa, ya kuonewa, ya misiba, ya kutokufanikiwa liangalie agano lake hili jipya muamini Mungu kuwa ni wa mambo mapya na yakuwa anakwenda kuyafanya yoote kuwa mapya 2Wakoritho 5:16-19 Mungu kwa nafsi yake ametupatanisha naye.hata kama umekuwa na historia mbaya ya uovu Isaya 1:18 Mungu anakukaribisha useme naye apate kukusafisha, 1Yohana 1:9
4.       Rangi ya Kijani (Green) – Rangi hii inazungumzia Ustawi na faraja na amani Zaburi 23 inatuthibitishia kuwa Mungu ni Mchungaji mwena nayakuwa fadhili zake ni za Milele, Yeye ametupa namna tunavyoweza kustawi sana Yoshua 1:5-8 endapo tutaliangalia neno lake na kulitii tutastawi na kufanikiwa sana na Mungu mwenyewe atakuchunga, na penye majani mabichi atakulaza na kukufariji.
5.       Rangi ya Blue (Sky) – Rangi hii inazungumzia kuhusu ufamle wa Mbinguni au ufalme wa Mungu, inatushuhudia jinsi ambayo ufalme huu uko karibu na kuwa mwanadamu pasipo mbingu yaani Mungu hawezi kwa namna yoyote kustahimili Yohana 3:13 Yesu pekee aliyeshuka na kupaa tena mbinguni ndiye mwenye uwezo wa kuleta majibu yenye matumaini kwa wanadamu, zaidi ya yote Mungu kwa rehema zake anamkaribisha kila mtu katika ufalme wake na hatima yetu ni kuingia mbinguni
6.       Rangi ya Manjano (Yellow) – Ni rangi inayozungumzia Uhai, inawakilisha mwanga wa jua, inawakilisha nafaka na inawakilisha kiini cha yai, inazungumzia uhai wetu, licha ya kumtaja Yesu kama Nuru ya ulimwengu Yohana 8:12 jambo linalotuthibitishia kuwa hatutaingizwa gizani tena na kuwa uhai wetu umefichwa katika Mungu, hakuna mtu awezaye kuondoa ustawi wa uhai wetu bali Mungu mwenyewe nay a kuwa tukimuamini uhai wetu utaungwa naye milele na milele
7.       Rangi ya kioo au Maji (white) – Ni rangi ambayo ni ngumu zaidi kuiona katika upinde wa mvua, inazungumzia usafi wa Mungu na utakatifu wake na haki, Haki yetu mbele za Mungu hakuna mtu anaweza kuiona ni Mungu ndiye anayeweza kutuhesabia haki hiyo hakuna mwanadamu mwenye kuweza kuisimamia wala kujitia katika kiti cha hukumu ya Mungu na kutuhukumu isipokuwa Mungu mwenyewe, ni vizuri kila mwanadamu akajifunza kukaa kimya kuhusu maisha ya wengine, unapotaka kujihusisha na kufuatilia maisha yaw engine bila kujua wamesimamamje na Mungu unajiweka katika hatari Warumi 8:33-34 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye  mwenye kuwahesabia haki, Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo ndiye aliyekufa, naam na zaidi ya hayo amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu, tena ndiye anayetuombea” haya ni majibu mazuri kwa wale wenye tabia ya kutaka kujivika madaraka  ya kuhukumu wengine na kutoa adhabu, wakati aliyeteseka ni Yesu na mwenyewe Yuko mkono wa Kuume wa Mungu anatuombea.
Sifa za Upinde wa Mvua
1.       Hakuna mtu anaweza kuona mwanzo wala mwisho wa Upinde wa Mvua – Fadhili za Mungu hazina kikomo kamwe
2.       Hakuna mtu anayeweza kuuweka - Baraka za Mungu na neema yake ikiwekwa juu ya mtu imewekwa huwezi kubadilisha , Karama za Mungu hazina majuto wala mwisho wake
3.       Hakuna mtu anaweza kuumiliki – Hakuna dini inaweza kukiri kuwa alama ile ni ya kwao, Iliwekwa kabla ya dini, iko kwaaajili ya wanadamu wote imewekwa na Mungu, Yesu sio wa dini Fulani wala wa Mtu Fulani yeye yuko kwaaajili ya watu wote, hakuna mtu mwenye hati miliki ya kummiliki Yesu.
4.       Hakuna mtu anaweza kuuomba Upinde utokee ni wazo la Mungu, - Huwezi kushindana na kusudi la Mungu, Mungu anayo haki ya kubariki yeyote amtakaye, kumuhesabia haki, kumuokoa na hatuwezi kumpangia
5.       Kila mtu huuona hivyohivyo – na huwezi kuuondoa, Mungu ndiye anayeuweka na ni Mungu ndiye anayeuondoa, Kama chanzo cha Baraka za Mtu ni Mungu mwenyewe basi hakuna mtu anaweza kukuondolea, kila mmoja anaweza kumuona Mungu kubwa ni Baba yake kwa namna ileile,
6.       Upinde ni agano linalomweleza wazi Ibilisi kamwe asitegemeee kusikia tena hata milele hasira za Mungu zigimgharikisha mwanadamu, endapo yuko mtu anategemea kusikia habari zako mbaya tena, mwambie nina agano la rangi saba usitegemee kusikia mabaya toka kwangu.
Ujumbe na : Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni