Jumanne, 16 Februari 2016

Shemeji we piga kazi tu!



Shemeji piga kazi tuu!

Nilikutana na binti huyu mwaka 1990 wakati huo nikikaa na kaka yangu maeneo ya Mwenge. Siku hiyo nilikuwa nimetumwa maeneo ya Ubungo na nilikuwa naendesha gari la kaka yangu aina ya Toyota Mark II ambayo ilikuwa bado ina hali nzuri na mziki mnene. Nilikuwa nimepiga T-shirti na Jinzi na miwani ya jua. Niliamua kupitia barabara ya Chuo Kikuu lengo langu likiwa ni kujaribu bahati yangu kama nitakutana na binti yeyote anayesubiri usafiri nimpe lifti na kujaribu kutupia nyavu.


                                                          Walikuwa wawili na Mzungu mmoja.............!


Ilikuwa ni kawaida yangu kila nikitumwa na kaka na kupewa gari napitia barabara ya Chuo Kikuu lengo langu likiwa ni hilo la kuopoa vimwana na mara nyingi nilikuwa sikosi kimwana wa kumpa lifti na kumtongoza. Wapo niliokuwa nikiwapata na wale niliokuwa nikiwaona washamba nilikuwa nawapotezea.

Siku hiyo nilibahatika kumpata binti mmoja. Alikuwa ni mzuri hasa kwa sura na umbo na weupe unaoashiria kuwa mambo yake ni mazuri. Nilisimama na kumtupia salaam, na yeye bila kusita aliniitikia na ndipo nikamwambia kama anaelekea Ubungo nimsogeze. Awali alisita lakini baada ya kumsisitiza alikubali kupanda nikaondoka naye. Njiani nilianza kumsomesha, hakuonekana kuwa mgumu, ingawa nilijishtukia kutokana na binti huyo kuonekana ni wa matawi.

Aliponiuliza ninaishi wapi na ninachofanya, nilimwambia ninaishi kwa kaka yangu ambaye ni mwanajeshi na nikamdanganya kwamba, ndio nimemaliza chuo kikuu mwaka uliopita na kwa sasa ninafanya kazi kama mwanadiplomasia pale wizara ya mambo ya nchi za nje. Nilimwambia kuwa, huwa nasafiri mara kwa mara nje ya nchi kwa shughuli za kikazi na kuonekana kwangu nchini ni mara chache sana. Aliponiliza kama huwa nasafiri nchi gani, nilimwambia, huwa natembelea zaidi nchi za Maziwa makuu. Hata hivyo nilimwambia kwamba, ndio ninajipanga nitafute nyumba ili nihame kwa kaka yangu kwa kuwa ndio nimeanza kazi nilikuwa bado najipanga ingawa kaka yangu hataki nihame hapo kwake.

Kwa upande wake alinijulisha kwamba na yeye amesoma nchini Uingereza na anafanya kazi katika ubalozi fulani wa mojawapo ya nchi za Scandinavia (naomba nisiutaje huo ubalozi) na anaishi na wazazi wake ambapo baba yake ni mhadhiri hapo Chuo kikuu. Alianza kunipigisha mastori yanayohusiana na mambo ya kidiplomasia ikabidi nimpotezee na kubadilisha stori ili asije akanishtukia.

Baada ya kumpa soma alikubali na kuniahidi nimtembelee hapo nyumbani kwao wiki ijayo mwishoni mwa juma ili tutoke out kwa ajili ya kufahamiana zaidi. Kwa kuwa simu za mkononi zilikuwa bado hazijaingia nchini alinipa namba ya simu ya nyumbani kwao. Tulipofika Ubungo aliteremka na kushika hamsini zake akiniacha na mimi nikifanya shughuli iliyonipeleka hapo Ubungo. Kwa muda mfupi nilioongea na yule binti alionekana kunipenda sana kwani hata wakati anashuka kwenye gari alinisisitiza sana tuonane hiyo wiki ijayo.

Ukweli ni kwamba nilikuwa sina kazi, na nilikuwa ndio nimemaliza kidato cha nne na kuangukia pua, yaani kwa kupata divisheni ya ziro. Wiki iliyofuata tangu nikutane na yule binti nilipata kazi ya kutembeza vitu na kuuza, maarufu kama promosheni. Siku hiyo nikiwa na furushi langu la vyombo na mwenzangu mmoja, yule binti aliniona. Alinikuta maeneo ya Kijitonyama akiwa kwenye gari. Mimi sikumwona, na alinipigia honi na alipoona sisikii alishuka. Alinikimbilia huku akiniita jina. Niligeuka na kugundua kuwa ni yule mpenzi wangu wa Chuo Kikuu niliyempa lifti na kumpiga fix.

Nilibabaika sana kwa kweli. Ilibidi hata kabla hajanisemesha, nimwambie Yule mwenzangu, ;au labda ni nyumba hii hapa, maana nimechoka sana.Yule binti akiwa ameshikwa na butwaa aliniuliza mbona niko kule na furushi kubwa. Nilimwambia,;ninamsindikiza huyu boy shamba wetu kwao. Ameacha kazi nyumbani nataka nimkabidhi kwa kaka yake. Ndio anajaribu kunionyesha nyumba, lakini naona kama naye kapasahau. Nilimjibu nikiwa nimebabaika sana.

Nilishangaa kukuona na hilo furushi. Je nikupeni lifti ili tutafute hiyo nyumba yenyewe? aliniuliza. Nilimwambia asisumbuke, tutatafuta hiyo nyumba na tutaipata tu. Aliniaga akionyesha kutoridhishwa na maelezo yangu.

Baada ya tukio lile niliona kazi ile haifai na nikaamua kuiacha. Nilipata kazi kwenye mghahawa mmoja uliopo mjini karibu na posta. Nilianza kazi pale kama mhudumu yaani waiter. Siku moja nikiwa nachukua order ya chakula waliingia wateja, sikuwatazama vizuri kwa sababu ya kashkash ya kazi mchana huo. Nilikwenda katika meza yao ili kuchukua order yao. Nilipofika pale walipokaa hao wateja nilikutana uso kwa uso na yule mpenzi wangu wa Chuo Kikuu. Niliishiwa pozi. Niligeuka haraka na kutaka kuondoka. Nilikuwa nataka kukimbilia jikoni. Lakini nilikuwa nimechelewa. Kwani aliniita kwa jina na kusema,;usijali, najua kinachoendelea. Ndio maana nimeamua kuja kula hapa. Chukua order yetu ya chakula na kuwa tu huru, kwani tangu wakati wa promosheni ya vyombo, nilikuwa najua

Aliposema hivyo aliwatazama wale wenzake. Mmoja wao aliniambia,;shem usijali piga mzigo, mapenzi kitu kingine na kazi zetu kitu kingine.; Nilienda jikoni, lakini sikurudi tena. Yaani ilikuwa ni kashfa kubwa ambayo sitakuja kuisahau mpaka leo hii niko na mama Ngina. Hadi leo sijui yule binti yuko wapi. Maana niliacha kazi na kwenda kusoma mkoani Arusha. Nashukuru hakujua ninaishi wapi pale Mwenge. Hata hivyo nilijifunza mengi, lakini kubwa zaidi nilijifunza kujiamini na ndio maana hadi leo mtu akiniliza nakaa wapi na ninafanya kazi gani ninamwambia ukweli kwamba ninaishi Mwanayamala kwa Kopa na ninafanyakazi ya Kuuza kahawa mjini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni