Jumanne, 16 Februari 2016

Eti mla ndizi husahau ila mtupa maganda hasahau?




Mwaka 1988 nilipata kibarua katika kampuni iliyokuwa eneo la Vingunguti. Kampuni ilikuwa ikishughulika na vifaa na utengenezaji wa vyakula vya kuku wa kisasa.

Kazi yangu ilikuwa kusimamia upakiaji na upakuaji wa vifaa mbalimbali vya kampuni na kwa kiasi fulani nilikuwa napata fedha za hapa na pale. Nilianza kutanua kwa kunywa na wanawake.

Miazi minne tu baada ya ajira,nilishawajaza mimba mabinti wawili,tena mmojawapo alikuwa mwanafunzi! Lakini niliwatolea nje mabinti wale,kwamba hazikuwa zangu..

Kwa kuogopa mkono wa sheria hasa juu ya yule mwanafunzi,ilibidi niache kazi mwaka 1989.

Mwaka 1990,nilijiunga na kozi ya Uhasibu,na kuhitimu 1993. Nilipata kazi safari hii katikati ya mji.
Mwaka 1995 nilichukua maamuzi ya kuachana na mambo ya ujana na kuoa. Nilipata dada mmoja,na tukaanza mahusiano,hatimaye tukaamua tuoane. Zikaanza hatua za barua,nayo ikajibiwa na mahari ikatajwa.

Kisha ikatangazwa siku ya bwana harusi mtarajiwa kwenda kutambulishwa kwa wazazi wa mwanamke. Nakumbuka ilikuwa Jumamosi. Wazazi wa binti walikuwa wakiishi Mabibo External.
Tulipata mapokezi mazuri na kukaribishwa ndani.

Msichana niliyempa Mimba akatokea!

Tukiwa sebuleni,nilimwona msichana mmoja akichungulia.Akachungulia tena,na kisha akajitokeza kabisa. Unajua kuna wakati jambo linaweza kutokea na ukahisi kabisa unaota tu!

Msichana aliyejitokeza, ni yule msichana mwanafunzi niliyempa ujauzito, na kisha kutoroka! Alisimama pale sebuleni bila kusalimia,na aliondoka kuelekea uani ambako tulisikia kilio. Halafu tulisikia kimya cha muda fulani.

Baadaye, baba wa bi harusi mtarajiwa akaja sebuleni na kutangaza kwamba ameshwasiliana na Polisi,kwani bwana harusi mtarajiwa alishatenda jinai kwenye nyumba ile. Nilielewa maana ya kauli ile,ingawa baba,mshenga,na rafiki yangu aliyenisindikiza,hakuelewa chochote.

Nilijua mambo yameshakuwa magumu,Polisi tena?! (miaka 30) Na kwa nguvu ambazo siwezi kuzielezea hadi leo,nilijikuta niko mlangoni,na nilitimua mbio nadhani kwa Tanzania hii,hakuna mwanariadha ambaye angenipita kwa kasi ile. Nikajikuta niko ndani ya Taxi.

Lakini ulikuwa ni ubwege tu,kwani baba,mshenga na rafiki yangu walikuwa wamebaki pale.

Sina haja ya kukupa maelezo mengi..ila kwa kifupi,yule binti aliyeangua kilio baada ya kuniona,ndiye mke wangu,na tuna watoto watatu sasa! Nikitaka kumchekesha mke wangu,huwa namkumbushia sakata lile..

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni