Alhamisi, 25 Februari 2016

Tabu Akaniambia Labda Mama Yangu!



Ni mwaka juzi tu sio siku nyingi wakati huo nilikuwa nasubiri kwenda kujiunga na chuo cha biashara, baada ya kuapata nafasi pale, nilikuwa kwa kweli sina shughuli maalumu, nakumbuka hapo jirani na nyumbani (Tandika) kulikuwa na jamaa mmoja ambaye alikuwa mnoko sana yaani mkorofi sana , huyu jamaa alikuwa haelewani na mtu, anajifanya mjuaji na anajifanya kasoma sana  na anajifanya kuwa ndsiye mwenye hela kuliko kila mtu.

 Huyu ndiye Tabu aliyeshikisha mtu Adabu!

Alikuwa ni mtu mzima kidogo mwenye umri kama wa miaka 50 kiumri, mkewe alikuwa na umrimdogo mwenye miaka kama 22-23 huyo alikuwa ni mkewe wanne kwani kwa sababu ya ukorofi alikuwa akikimbiwa na wanawake, siku moja nikiwa nimekaa nilisikia kelele hapo kwa huyo jirani , ilibidi nitoke kwenda kushuhudia kulikoni tabia ambayo kwa kweli ni umbeya mtupu, nilipofika pale nilimkuta Yule jirani akiwa amemkunja kijana mmoja kwa kumkosea adabu. Nilipoona anataka kumpiga ilibidi niingilie kati  na kujaribu kumsihi amuache nikimwambia kuwa amekosa, Yule jamaa aliacha kumshughulikia Yule kijana na kunigeukia mimi  na kuanza kunishambulia kwa maneno nilishangaa kwa sababu nilichokuwa nakifanya mimi niliona ni kitendo cha uungwana , alichambua kwamba najifanya nimesoma sana najiona msomi wa mtaa na kwamba ati tunajifanya familia tajiri, kwa kweli sikumjibu kwa sababu nilikuwa namfahamu vizuri kuwa ni mtu wa shari, nilichokifanya ni kuondoka na kurudi nyumbani, umbea ulikuwa umenitokea puani. Lakini nilipofika nyumbani niliona sikuwa nimejitendea haki kumwacha Yule jirani aniadhiri kiasi kile halafu aende akiwa huru, Nilijiuliza maswali na kujipa majibu kwamba nilitakiwa kujibu mashambulizi yale.

Niliamua kurudi tena  nikiwa nimepania kumfundisha adabu, Nilipofika pale kwa jirani niliambiwa na mkewe kwamba alikuwa ameshaondoka, nilianza kumpa mkewe maagizo ya kiamri kwamba mumewe akija amwambie kwamba  kunyamaza kwangu hakukutokana na kumuogopa na kumwambia kuwa ni lazima ningemshikisha adabu, Yule mke wa jirani alibadilikia na kuniambia nimsubiri mwenyewe akija niende nikamwambie  yeye (mke) hakuwa tarishi wangu, nilimwambia kwamba wenzake watatu wameshaoindoka kwenye nyumba ile yeye pia hana nafasi ya kudumu Yule mke wa jirania alisema kuwa hayo hayanihusu kwani hata mama yangu anaweza kuachika pia, alipomwingiza mama yangu kwenye mabishanao hayo niliona kama amenivua nguo hadharani, nilimwambia nitamshikisha adabu asipochunga mdomo wake. Nadhani alikuwa amefundishwa tusi moja tu maishani mwake  linalohusu mama wa wengine  kwani aliniambia nimshikishe adabu mama yangu kwanza, Hapo sikuweza kuvumilia, nilimfuata pale mlangoni  alipokuwa amesimama, nilipomfikia tu nilirusha kibao, lakini kwa ustadi wa ajabu sana alikidaka  kile kibao changu na kunisukuma, niliyumba na kurudi nyuma  hatua kadhaa nilimfuata nikiwa nimepania sana safari hii,

Nilimkata mtama, lakini hakuanguka Badala yake alinishika na kunipinda ghafla  kabla hajanitupa chini, niliinuka nikiwa nimetahayari nilijua ule wakati wa kufedheheka umewadia nilipomfuata safari hii nilijaribu kitu kingine, Nilimrushia ngumi za chapuchapu, lakini zote aliziona na kuzikwepa, halafu nilihisi vitu kama mawe kimoja kikitua kwenye mbavu na kingine chini ya jicho, zilikuwa ni ngumi za mwanamke, kabla sijakaa sawa nilikuwa nimeenda chini yule mwanamke ambaye alikuwa mrefu mwembamba alinifuata pale chini na kunikwida. Alianza kunisulubu kwa ngumi za usoni za haraka haraka. Naomba kwanza niseme kwamba zile sifa za majina ambazo huwa zinaandikwa na wataalamu wa utambuzi wakati mwingine ni kweli Yule mwanamke alikuwa anaitwa Tabu, hivi karibuni nilisoma jina la tabu gazetini wakielezewa kuwa ni wanawake wenye nguvu hasa wakiwa warefu wembamba, 

Nilipojaribu kuinuka sikuweza, ilibidi jirani waingilie kati  waje kuniamulia niliposimama nikiwa na nundu mbili na damu ikinichuruzika mdomoni nilisema tutaona  nimekwachia kwa sababu u mwanamke, Bila shaka jirani zangu walikuwa na kila sababu ya kucheka kwani walicheka  baada ya mimi kusema maneno yale, nilianza kuondoka polepole kinyonge, kwa aibu na kifedheha kuelekea nyumbani, najua unataka kujua kama mume wa Yule mtesi wangu akiambiwa kuhusu ugomvi ule na kama alikuja nyumbani kunitafuta kama nilivyoamuru, Utanisamehe kwani tangu siku ile nilijifunza kuwa jambo baya kuliko kuliko yote duniani ni umbeya,  na kuingilia mambo ya watu wengine, kwa hiyo naomba usiingilie mambo yangu. Au we mwandishi wa habari? Nyau we!

Maoni 2 :

  1. shukran sana yaan ni perfect ni nimejifunza mamb mengi kuhusu udereva

    JibuFuta
  2. shukran sana nimejifunza mamb mengi kuhusu udereva

    JibuFuta