Jumamosi, 5 Machi 2016

Mafundisho sahii kuhusu zaka katika Agano Jipya !



je zaka ni halali katika agano jipya?
Moja ya maswala yanayosumbua sana wakristo katika nyakati hizi za leo ni pamoja na swala la zaka! Zaka ni moja ya kongwa kubwa sana la sheria ambalo limewatesa Wakristo wengi na watumishi wengi wa Mungu na hii inatokana na aidha kukaziwa sana kwa kupita kawaida na wakristo wengi wamekuwa wakikataa kutii swala zima la utoaji wa zaka. Kwa ujumla swala la utoaji lilitakiwa kuwa la furaha na Baraka lakini kinyume chake huzuni imekuwa ikitawala na uchungu  katika swala zima la utoaji na hasa zaka!

 Zaka kikaangoni tafadhali wewe mwenyewe uhukumu!

Zaka ni sehemu ya sheria
Biblia inasema katika Walawi 27;30 “Tena zaka yote ya nchi kama ni ya mbegu ya nchi au kama ni matunda ya nchi ni ya Bwana ni takatifu kwa Bwana”
Malaki 3;9 inasema “Ninyi mmelaaniwa kwa laana maana mnaniibia mimi naam taifa hili lote” Kumbe kutokutoa zaka kwa mujibu wa sheria ni laana lakini Agano jipya linatuambia Wagalatia 3;13 “ Kristo alitukomboa katika laana ya torati kwa kuwa alifanywa laana kwaajili yetu maana imeandikwa amelaaniwa kila aangikwaye juu ya mti”

Je sisi tuko chini ya sheria ya agano la kale leo?
Jibu la swala hilo ni ndio na sio. Agano la kale linahusiana na mitazamo miwili ya maisha ya kiyahudi wao binafsi na taifa lao katika uhusiano wao na Mungu.Agano hilo la kale lina kanuni za kiraia na za kidini na kimaadili zile za kiraia bado zinatumika hata leo katika mifumo ya serikali mbalimbali. Lakini sheria zenye uhusiano na maswala ya uhusiano wetu na Mungu katika agano la kale zimekomeshwa na kubadilishwa Waebrania 7; 12Kwa kuwa yanapotokea mabadiliko ya ukuhani, pia lazima yawepo mabadiliko ya sheria”. Kwa sasa basi tuko chini ya sheria ya Kristo Galatia 6;2 ambayo ina chachu ya sheria za kimaadili ambazo mzizi wake uko katika agano la kale.
Lakini sheria za kidini za agano la kale yakiwemo maswala ya zaka, Tohara na maswala ya kiibada ya kutawadha na sabato na kadhalika vimebatilishwa hata ingawa tunazo baadhi ya sheria za maswala ya kiibada kama Ushirika wa meza ya Bwana na ubatizo wa maji, lakini haya si ya lazima katika kutufanya tusiwe na mahusiano maalumu na Mungu, Hayo ni ya muhimu katika kutimiza kila ambacho kristo alikiagiza na kukitenda. Wakati katika agano la kale zaka na tohara na mengineyo yalikuwa ni ya lazima ili uwe na uhusiano mzuri na Mungu, lakini kwa habari ya wokovu ushirika na ubatizo haviwezi kutuzuia kuwa na Ushirika na Mungu.

Ukweli kwamba tuko huru kutoka katika sheria ya agano la kale ndio ufunuo ambao Paulo mtume aliupokea na ndio alioupigania vikali, wazo hili lilikuwa gumu kukubalika hata na kwa mitume wengine na ilikuwa ngumu kuelewana nalo Lakini ndio ufunuo aliopewa na Bwana Yesu Kristo. Yesu alizungumza kuwa sheria imekamilishwa na kuwa imekwisha kupita lakini hawakuwa na masikio ya kusikia.Kama tunajaribu kuishika sheria leo tunauweka wokovu wetu katika hali yenye utata Wagalatia 5;4 Biblia inasema hivi “Mmetengwa na Kristo ninyi Mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; Mmeanguka kutoka katika hali ya Neema.” Kwa nini

1.      kwa sababu hakuna mtu aliyeweza kuitimiza Sheria yote isipokuwa Yesu Kristo peke yake
2.      Pili kwa sababu ukivunja moja tu katika sheria utakuwa na hatia ya kuwa umeivunja yote na unastahili kifo.

Kujaribu kuishika sheria ni kujaribu kuendeleza haki yako mwenyewe. Kumpokea Yesu ni kupokea haki yake na kutambua kuwa hatuwezi kuwa na wema wa kutosha sisi wenyewe na kwa hiyo Mungu anataka tuache kujaribu, Mungu anataka kujaribu kutuzuia kulitii agano la kale, Tunapokuwa tumempokea Yesu  sheria yake inaandikwa katika mioyo yetu. Wokovu wetu ni mara moja na endelevu, na kutembea kwetu kunajumuisha maendeleo ya wokovu wetu na nafsi zetu kwa kuruhusu maisha katika roho kupiga hatua kila wakati kutoka utukufu hata utukufu. Roho zetu zinakuwa mpya mara tu unapokuwa umeokoka roho zetu zinakuwa kiumbe kipya mara moja na nafsi zetu zinahuishwa siku hadi siku Neno la Mungu linakata pazia la nafsi na roho na kuruhusu mabadiliko ya maisha kwa nguvu ya neno la Mungu ndani yetu na Roho wa Mungu anatujulisha mara tunapokuwa tumeivunja sheria ya ndani. Sasa basi zaka, kutahiriwa, kutawadha kwa namana ya kidini, kushika miandamo ya mwezi na sabato, siku takatifu, na aina za vyakula, msishike msiguse msionje, ibada za hekaluni, kuua kwa mawe, haya yote ni sehemu ya sheria za agano la kale unaweza kuamua kuyashika YOTE au Kutokuyashika yote.Tafadhali ndugu msmaji wangu hebu tafakari kwa kutumia Biblia yako na soma pamoja name maandiko kadhaa yafuatayo katika hali ya kuomba kasha utaanza kuhisi uhuru mkubwa na utajiri mkubwa uliomo katika Kristo na wokovu wetu.

Sheria imetimizwa, kwa uwazi kabisa Biblia inasema mpaka wakati wa Yohana mbatizaji Yesu alizaliwa chini ya sheria na ndio maana aliwaambia wayahudi kuifuata sheria nah ii ilikuwa sahii mpaka baada ya kifo chake, Kuzikwa na kufufuka, ninaamini kuwa Yesu alishika kila kitu kilichoamriwa na Torati na nina hakika inamuuma sana kuona sisi nasi tukijaribu kuishika vilevile, Yeye alifanya hivyo ili sisi tusiwe na haja. Aligongomelea utaratibu huo msalabani Wakolosai 2; 14 sasa tuko huru tuko huru tuko huru!.

Kama tukidanganya leo tunaivunja sheria ya agano la kifalme na sio agano la kale “Usishuhudie uongo” hii sio propaganda bali ni uwazi wa kibiblia kabisa
·         Wagalatians 5:4.- Mmetengwa na Kristo ninyi Mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; Mmeanguka kutoka katika hali ya Neema.
·         Mathayo 11:13 Kwa maana manabiiwote na torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana
·         Luka 16:16 Torati na manabii vilikuwako mpaka wakati wa Yohana Tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa na kila mtu hujiingiza kwa nguvu.
·         Mathayo 22:37. Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote, mpende jirani yako kama nafsi yako, hizi mbili ndio sheria yote na manabii.
·         Yohana 1:17 Sheria ilikuja kwa mkono wa Musa neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.
·         Yohana 7:23 Tohara ni ya lazima kwaajili ya sheria ya Musa
·         Matendo 13:39 na kwa Yeye kila amwaminiye huhesabiwa haki katika mambo yale yote asiyoweza kuhesabiwa haki kwa torati ya Musa
·         Matendo 15:5-20 Je waishike sheria si wanaokolewa kwa imani.
·         Matendo 18:13 Wakisema mtu huyu huwavuta watu ili wamuabudu Mungu kinyume cha Sheria
·         Matendo 21:21Unawafundisha Wayahudi wote  wakaao katika mataifa kumwacha Musa
·         Warumi  3:19 Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa walio chini ya Torati
·         Romans 3:21 Lakini sasa haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheia inashuhudiwa na torati na manabii, ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya Imani katika Kristo Yesu kwa wote waaminio.
·         Warumi 3:27 Kwa sheria ya imani na sio ya Matendo.
·         Warumi 3:28 Mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria
·         Warumi 4:1-16 kuhesabiwa haki ka njia ya imani.
·         Warumi 6:14 Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi kwa sababu Hatuko chini ya sheria bali chini ya neema
·         Warumi 7:4 tumeifia Torati
·         Warumi 7:6 Tumefunguliwa katika sheria.
·         Warumi 8:3-4 Sheria imekwisha kutimizwa
·         Warumi 10:4 Kristo ndiye mwisho wa Sheria
·         Warumi 13:8, 10 Upendo huitimiza Sheria.
·         1Wakorintho 9:20 Mimi mwenyewe siko chini ya sheria.
·         Wagalatia 2:16 hatuhesabiwi haki kwa Matendo ya Sheria.
·         Wagalatia 2:21 ikiwa haki Hupatikana kwa sheria Basi kristo alikufa bure
·         Wagalatia 3:2 Roho hapokelewi kwa Sheria
·         Wagalatia 3:5 Je miujiza inapatikana kwa sheria?
·         Wagalatia 3:10 Kwa maana wale walio wa matendo ya sheria wako chini ya laana maana imeandikwwa amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati ayafanye.
·         Wagalatia 3:11 Hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu atika sheria.
·         Wagalatia 3:13 Kristo alitukomboa katika laana ya torati
·         Wagalatia 3:17-29 si Kwa sheria bali kwa imani twapokea mbaraka wa Ibrahim.
·         Wagalatia 5:3-4 mmetengwa na Kristo ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria.
·         Galatians 5:14 sheria inatimizwa katika upendo
·         Galatians 5:18 lakini mkiongozwa na Roho hamko chini ya sheria
·         Galatians 6:2 sheria ya Kristo.
·         Wafilipi 3:9 haki ipatikanayo kwa imani
·         1Timotheo 1;9  Sheria haimuhusu mtu wa haki bali waasi
·         Waebrania 7;12 Ukuhani ukibadilika ni lazima na sheria ibadilike.
Waebrania 7:28 baada ya sheria Mwana
·         Waebrania 8:6 Tuko chini ya Agano lililobora zaidi.
·         Waebrania 8:7 baada ya lile la kwanza la pili.
·         Waebrania  8:13 Kwa kule kusema agano jipya amelifanya lile la kwanza kuwa kuu kuu
·         Waebrania 9-10 Ukuhani mpya na dhabihu moja inayodumu milele.

Kimsingi kanisa lingefaidika sana kama kila mkristo angepeleka fedha na kwa makusudi ya kutimiza agizo kuu.  na angalau kibinadamu fungu la kumi au zaka ingelikuwa jibu la swala hilo na hususani kama ingekuwa inaishia katika hilo tu basi hali ya kanisa kifedha ingekuwa duni zaidi. Fungu la kumi linazuia utoaji wa fedha zaidi kuliko tunavyofikiri kwa sababu kama unaongozwa na sheria na sio Roho ungetoa au utatoa kiasi hicho tu na hakuna hata mtu mmoja angetoa 20%, 30%, 40%. Ya mapato yake na nini kinafanya hilo lisiwezekane ni dini na sheria na sio kusikia kunakotokana na imani Wagalatia 3;2b. Jijaribuni wenyewe kwamba mmekuwa katika imani.

Je Zaka (Fungu la Kumi) ni sehemu ya Agano Jipya?
Kama ndio basi Mungu aliamua kulificha hilo kwa Paulo Mtume na kwa waandishi wengine wa agano jipya, kwani ukitaka kufundisha kuhusu zaka hata ukijaribu vipi hutaweza kuhalalisha mpaka utumie agano la kale ili ufundishe kuhusu zaka, wengine watajitetea kuwa zaka ilikuweko kabla ya sheria na ikawa sehemu ya sheria kwa msingi huo hata sasa inapaswa kuweko? Ni sawa na jiulize kuhusu kutahiri je? Hakukuweko kabla ya sheria? Mwanzo 17;24 na ikawa sehemu ya sheria je inapaswa leo kutahiriwa?baadhi ya mitume katika agano jipya walijaribu kufanya hayo Matedno 15;5-11 wagalatia 2;11 Lakini Paulo hakufanya hayo hata moja
Kitabu cha waebrania kinaonyesha kuwa Abraham alimpa zaka Melkizedeki lakini ni katika kifungu hichohicho inapozungumzwa kuwa sheria ilibadilishwa Waebrania 7;12, waebrania 8;13 na 9;1.inazungumza kuwa agano la kwanza lilikuwa na kawaida zake za ibada (regulations) na zaka ni sehemu ya taratibu hizo likaondolewa waebrania 10;9 yaani na zaka pia iliondolewa ili kustawisha agano la pili ambalo zaka si sehemu ya agano hiliambalo huandikwa moyoni katika nia  Waebrania 10;16 je Mungu ameandika zaka katika moyo wako na nia yako au ni kongwa? Zaka haikuandikwa katika moyo wangu wala nia yangu.

Hoja ya Melkizedeki
Baadhi wanasema kuwa melkizedeki alikuwa ni Yesu Kristo, na kwa sababu hiyo kama Ibrahimu alitoa zaka basi Kristo anapaswa kupokea zaka leo. Hii ni dhana tu isiyo na msingi wa kimaandiko. Na tatizo kubwa ni kuwa Yesu sio Mtu na wala sio Melkizedeki Huduma ya Kikuhani ya kwa mfano wa Melkizedeki Yesu Kristo si ya kidunia.
Melkizedeki alikuwa Kuhani aliyembariki Ibrahimu katika mifumo mikuu miwili Kwa sheria alichukua Zaka na kwa Neema walishiriki mkate na divai Mwanzo 14; 18 Yesu naye ni Kuhani wa mifumo miwili Kanisa (Mataifa sasa) na mfumo wa Hekalu (mfumo wa ibada za kiyahudi baada ya unyakuo) katika Yerusalem mpya Ufunuo 21;9-27.

Je Yesu alikuwa Melkizedeki?
Katika Mwanzo 14;17-23 tunaona Melkizedeki akijitokeza kwa mara ya kwanza na mfalme wa Sodoma walikwenda kumlakikatika bonde la shawe Abrahamu alipokuwa ametoka kumpiga mfalme Kedorlaoma na Melkizedeki mfalme wa salem akaleta mkate na divai naye alikuwa kuhani wa Mungu aliye juu sana  akambariki  na kusema  Abrahamu na abarikiwe na Mungu aliye juu sana, muumba wa mbingu na nchi na ahimidiwe Mungu aliye juu sana aliyewatia adui zako mikononi mwako .Abrahamu akampa fungu la kumi la vitu vyote. Na Mfalme wa Sodoma alimwambia Ibarahim nipe mimi hao watu na hizo mali uchukue wewe, Abrahamu akamwambia nimeinua mkono wangu kwa Bwana Mungu aliye juu sana Muumba wa mbing na nchi  ya kuwa sitatwaa uzi wala gidamu usije ukasema nimemtajirisha Abraham

Biblia inamtaja Melkizedek kama Mfalme na kuhani na inaelezwa kuwa abrahamu alimpa zaka 10 ya yote hii ilikua ni kivuli cha utoaji wa zaka na alipokea mkate na divai kivuli cha ushirika wa meza ya Bwana . kwa ufupi Melkizedeki alifahamu kuwa anabariki vyote Sheria na Neema kwa Ibrahimu.
Zaburi 110 ni Eneo lingine linalomzungumzia Melkizedeki.

BWANA amwambia Bwana
wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
mpaka niwafanye adui zako kuwa mahali pa
Kuweka miguu yako.’’
BWANA ataeneza fimbo yako ya utawala
kutoka Sayuni,
Utatawala katikati ya adui zako.
Askari wako watajitolea kwa moyo
Katika siku yako ya vita.
Ukiwa umevikwa fahari takatifu,
kutoka kwenye tumbo la mapambazuko
Utapokea umande wa ujana wako.
BWANA ameapa,
naye hatabadilisha mawazo yake:
“Wewe ni kuhani milele,
kwa mfano wa Melekizedeki.’’
Bwana yuko mkono wako wa kuume,
atawaseta wafalme siku
ya ghadhabu yake.
Atawahukumu mataifa, akilundika mizoga
na kuwaseta watawala wa dunia nzima.
Atakunywa maji katika kijito kando ya njia, kwa hiyo atainua kichwa chake juu.

Unabii huu unatambulika kama Mungu baba anamwambia Yesu kuwa atakuwa kuhani milele kwa mfano wa Melkizedek kwa ujumla zaburi hii inatabiri matukio yatakayotukia baada ya Msalaba nah ii inamaanisha kuwa ukuhani huo ungeanza baada ya kifo cha Msalaba na inaonekana kama Waebrania 5;1 inasema Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwaajili ya wanadamu katika mambo yamuhusuyo Mungu ili atoe matoleo na dhabihu kwaajili ya dhambi, Inaonekana  maaandiko haya yanayozungumzia ukuhani wa Kristo yanazungumza kuhusu kuhani aliyetwaliwa katika wanadamu je ni wakati gani Mungu alifanyika mwanadamu? Mungu hakufanyika mwanadamu wakati wa Ibrahimu, na mstari wa pili kuhani alitakiwa kuwa anayeujua udhaifu wa wanadamu ili kuchukuliana nao sasa ni wakati gani Mungu alikuwa katika hali hiyo bila shaka ni wakati Kristo alipozaliwa na Mariam

Waebrania 5;7 inasema “siku hizo za mwili wake”  na mstari wa 10 unasema sasa anatajwa kama kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki kwa msingi huo ni wazi kabisa kuwa Melkizedeki wa wakati wa siku za Ibrahimu hakuwa Kristo na waebrania 7;1-28 inaangalia ulinganifu wa Melkizedeki na Yesu Kristo kweli wote walikuwa makuhani lakini katika mitindo tofauti Waebrania 7;3 Je Melkizedeki hakuwa na baba wala mwana? Hapana alikuwa na baba na mwana lakini Roho wa Mungu aliruhusu kutokunukuliwa kwa uzao wake ili kuweka unabii unaohusiana na Kristo ambaye ni Mungu Waebrania 7;3, Waebrania 7;4, Maandiko yanaonyesha kuwa Melikizedeki alikuwa ni mwanadamu,waebrania 7;6.inazungumza kuwa uzao wa Melkizedeki hautoki katika Ibrahimu, lakini wa Yesu unatoka katika Ibrahimu Mathayo 1;1-17,waebrania 7;15 inazungumzia kuhani kwa mfano wa Melkizedeki kwa mfano haimaanishi ni kufanana au ni sawa inamaanisha kama.Waebrania 7;22 inasema Yesu amekuwa maana yake siku zote yuko au amekuwa kuhani kwa mfano wa Melkizedeki. Na ingawa kuna maswala yenye kufanana kati ya Yesu na Melkizedeki biblia inaweka wazi kuwa ni watu wawili tofauti waebrania 8;4 Jambo linalokubaliana na zaburi 110 uketi mkono wangu wa kuume linalomaanisha ni huduma ya kikuhani ya Yesu Kristo Mbinguni.baada ya kuliweka hilo sawa sasa turejee katika smo letu kuhusu zaka

Je Yesu amesema nini kuhusu zaka?

Luka 11; 42 “Ole wenu Mafarisayo kwa kuwa mnatoa zaka za mnnaa na mchicha na kila mboga na huku mwaacha mambo ya adili na upendo wa Mungu iliwapasa kufanya hayo ya kwanza bila kuyaacha hayo ya pili”.
Mathayo 23; 23-24 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo wanafiki kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na Bizari na jira lakini mmeacha mambo makuu ya sheria yaani adili na rehema na imani hayo imewapa kuyafanya wala yale mengine msiyaache Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia.”

Mathayo 5; 17-20 “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii la sikuja kutangua bali kutimiliza kwa maana nawaambia, mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka hata yote yatimie, basi mtu yeyote atakayevunja amri moja kati ya hizi zilizo ndogo na kuwafundisha watu hivyo ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni, maana nawaambia ya kwamba haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
Mstari wa 17 unanifurahisha zaidi kwani unatumia neno Torati na Manabii na Mstari wa 18 anatumia Torati, kuuelewa mstari huu ni moja ya jambo la muhimu sana  na kuelewa muktadha wake katika mazingira aliyoyasemea sasa kwa kuiangalia historia ya mwanadamu tunaona kuwa kutoka Adamu mpaka Abrahamu na Musa ni miaka 2000  na kutoka Musa mpaka Yohana Mbatizaji na Yesu iko miaka 2000, na kutoka kifo cha Yesu kuzikwa na kufufuka mpaka sasa ni miaka 2000 vipindi hivi vikuu vitatu ni vya muhimu sana, katika kushughulikia maswala ya Mungu anavyojishughulisha na mwanadamu kutoka Abrahamu mpaka wakati wa Musa ni kipindi cha Mpito (miaka 430) kufikia wakati wa sheria na manabii, Ibrahimu alikuwa mtu wa Muhimu sana kwani maisha yake yanazungumza kuhusu maswala makuu mawili maisha yake yanazungumza kuhusu Wayahudi chini ya sheria na Wakristo chini ya Neema kwa kuwa maisha ya Ibarahimu yana wazo la [kuhesabiwa haki kwa imani] na wazo la sheria [Zaka na Tohara] 

Sheria ilitolewa kwa wayahudi ni mfumo wa kiyahudi Luka 16;16 ( torati na manabii vilikuwa ni mpaka wakati wa Yohana mbatizaji) Biblia inasema ni mfumo uliotumika mpaka wakati wa Yohana sasa nini kinafuata baada ya Yohana mbatizaji ni kipindi kingine cha mpito kutoka Yohana mbatizaji mpaka wakati wa Mateso, kifo kuzikwa na kufufuka kwa Bwana Yesu Wagalatia 4;4-5 inasema Yesu alizaliwa chini ya sheria Yesu ndiye alikuwa funguo ya kipindi cha mpito alifundisha agano la kale Mathayo 5;17-20, Luka 11;42, Mathayo 23;23-24 na alifundisha sheria ya kifalme yaani Agano jipyaMathayo 22;37 na Warumi 13;9 kwa hiyo anaposema usizini,usiue, usiibe, usishuhudie uongo usitamani n.k anasema mpende jirani yako kama nafsi yako.

Baada ya ufufuo alipokuwa ameyatimiza matakwa ya sheria  kwa damu yake tumeingia katika mfumo mpya na agano jipya na ukuhani mpya na (zaka ilikuwa ni ya ukuhani wa walawi) sawa na maagizo ya sheria, sheria Torati ilikuja kwa mkono wa Musa Lakini neema na kweli zimekuja kwa mkono wa Yesu Kristo Yohana 1;17, mfumo wa Musa ulikuwa ni torati yaani zaka, siguse, msishike, msionje, kula aina Fulani ya wanyama wengine msile, n.k lakini mfumo mpya katika Kristo unahitimishwa na warumi 6;14 Hatuko chini ya sheria yaani mfumo wa Musa bali tuko chini ya neema, kwa msingi huo sisi tulio wa mfumo wa neema hatupaswi tena kufuata mfumo wa agano la kale kama kutoa dhabihu za kuchinja wanyama,kuchoma ubani, kukusanyika hekaluni kwa ibada za hekaluni na halikadhalika kujishughulisha na zaka au kutahiriwa au kushika sabato “Kumbukumbu la torati 32;21”.

Sasa tunaporejea katika mstari wetu wa 18 wakati Yesu anaendelea kuzungumza alikazia kuitimiza sheria yaani ya (Musa) na baadhi ya Unabii (Eliya) na hii nduio maana mstari wa 18 unajumuisha na manabii ikiwa na maana baadhi ya unabii hautatimia mpaka wakati wa kuja kwake mara ya pili, kwa wayahudi walifikiri kuwa wakati ule Kristo angeweza kusimamisha ufalme na angetanguliwa na Eliya lakini wayahudi hawakujua kuwa kuna nafasi iliyo wazi kutoka Kristo aliyeteseka Isaya 53 na Kristo Mtawala Ufunuo 21;15-16 na kwa msingi huo kuna nafasi kati ya kuitimiza sheria (Musa) na kuitimiza Manabii (Eliya)  na naamini kuwa utakuwa umeona wazi kabisa kuwa sheria imetimizwa.

       Ni wazi kabisa wayahudi walielewa kuwa Mitume wanafundisha mafundisho tofauti mapya na ambayo yanapingana na sheria Matendo 18; 13 Biblia inasema hivi “wakisema mtu huyu huwavuta watu ili wamuabudu Mungu kinyume cha sheria” Matendo 21; 21. “Nao wameambiwa habari zako ya kwamba unawafundisha Wayahudi wote wakaao Katika Mataifa kumwacha Musa ukiwaambia wasiwatahiri watoto wao wala wasizifuate desturi.” Yesu alizaliwa chini ya sheria lakini pia ndiye mwisho wa sheria Warumi 10;4. Je sheria ni nini? Inapatikana wapi je ni kwenye agano la kale? Baadhi hudhani ni vitabu vitano vya Musa, lakini huu ni mgawanyo tu, Yesu ananukuu na kusema imeandikwa katika sheria katika Yohana 15;25 ananukuu Zaburi 35;19,69;4 na katika 1Wakoritho 14;21 walinukuu kutoka katika sheria lakini ni Isaya 28;11 kwa msingi huo nafikiri kwamba Mungu anaiita migawanyo yote hiyo kuwa ni sheria na kutoka Musa mpaka wakati wa Yohana mbatizaji ilikuwa ni sheria (Musa) sheria na Manabii (Elia) inawakilisha maswala ambayo yamekwisha kupita na sasa tuko chini ya agano jipya.

Ni ukweli kuwa ziko nabii ambazo bado hazijatimizwa kazi ya Eliya haijakamilika, Lakini ya Musa tayari, kwa sababu kuna mvunjiko mkubwa wa Mungu kujishughulisha na wayahudi kwa sasa unabii unaonyesha atakapokuja tena atafanya kazi kimsingi na wayahudi tena Zekaria 2;12,8;23 Yesu aliposema Livunjeni Hekalu hili name katika siku tatu nitalijenga(Siku moja ni sawa na miaka 100). hakuwa anamaanisha tu mwili wake ambao ungefufuka siku ya tatu lakini pia alikuwa anazungumzia Hekalu halisi yaani Mfumo wa tamaduni za Kiyahudi ambao angeujenga upya katika siku tatu Mathayo 27;51”Na tazama pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata nchi ikatetemeka miamba ikapasuka” hii ina maana Yesu na Hekalu walikufa siku moja wote walitoa roho, Hekalu litakapofufuka Mungu ataanza kufanya kazi na wayahudi chini ya sheria na sheria ilitolewa kwa wayahudi na sio kwa Mataifa.

Ukweli kuwa Ibrahim hakuwa anatoa zaka kama sheria alitoa zaka kama kivuli tu kama ilivyo kwa Yohana mbatizaji ni kivuli cha Eliya. Kwa msingi huo hakuna ushahidi wa maandiko mengine yanayoonyesha kuwa Melkizedeki alikuwa anakuja tena na tena kuchukua zaka kwani hakukuwa na sheria wakati huo (Musa na Makuhani wa Lawi)

Je tuko sawa kwa Mungu tukiifuata sheria Leo?

Je ni haki kuisimamia sheria na je tumeamriwa kutoa zaka leo? Na je tusipoitoa hatuko sawa na Mungu Biblia inasema katika Wagalatia 2;21 “Siibatili neema ya Mungu maana ikiwa haki hupatikana kwa sheria basi Kristo alikufa Bure” haki yetu inapatikana kwa kusikia kunakotokana na imani Wagalatia 3;2 “.....au kwa kusikia kunakotokana na imani?”

Sheria ilikuwa ni Mwalimu ilitufundisha kutoa zaka wagalatia 3;25 kwa kuwa sasa imani imekuja hatuhitaji tena Mwalimu, wale walio chini wa sheria ni watumwa wa sheria Wagalatia 4;7 sisi sio watumwa tena Warumi 9;31-32 kwa njia ya imani na sio matendo, Sheria ya zaka inaweka pia deni kubwa sana la fedha Amosi 5;11 Kama hatulipi zaka tuko katika shida sheria ina madai kadhaa ili uwe sahii kwa Yule unayempa nah ii itaharibi kabisa asili yetu ya haki katika agano jipya  Amosi 5;7  na ndio maana aliye chini ya sheria amelaaniwa Wagalatia 3;10

Kuiacha sheria ni jambo Gumu kwa wapendwa wengi!

Maisha ya Abrahamu yana kitu cha kutufundisha kuhusu sheria, Abrahamu alikuwa na watoto wawili Ishmael (Sheria) na Isaka (Ahadi) Wagalatia 4;21-31,5;1-10, Mwana wa Ibrahimu aliyezaliwa kupitia Hajiri ambaye alipatikana kwa mujibu wa sheria ya kimwili yaani sheria na tamaduni za wakati huo, mwana wa Abrahamu ambaye alimpata kupitia Sara ni Isaka mwana wa Ahadi. Siku moja Roho Mtakatifu alimwambia Abrahamu Kupitia Sara Mfukuze mjakazi na mwanawe yaani (Agano la kale) na (zaka) Kisha Mungu Baba alimwambia Abrahamu kukubali kumuondoa Ishamel milele au nje ya kambi yake nafikiri unaweza kuhisi maumivu gani aliyoyapata Abrahamu unaweza kuona huenda alijiuliza maswala kadhaa kwa Mungu je sitaweza kumtembelea hata mara moja kwa wiki?(Sabato)Lakini Mungu akamwambia hapana, akauliza tena je siweszi kupeleka hata kiasi Fulani cha fedha (Zaka) Bwana akamwambia hapana je naweza kumpelekea baadhi ya vyakula au mlo maalumu (Sheria za vyakula) jibu ni hapana atakuwa mwenyewe huko jangwani je siwezi kumlinda (Hukumu Ya kupiga mawe) hapana , je siwezi kumtembelea katika siku kadhaa za sikukuu? (Kushika siku, miezi na sikukuu za kiyahudi) Bado Mungu alisema hapana, je Mungu siwezi ku.... lakin Mungu aliendelea kusema Hapana, hapana, hapana.

Sheria yaani (Ishmael yaani zaka) lazima awekwe nje ya kambi Neema (Kanisa). Wakristo (Neema) wanaweza kujaribu kuishika sheria (Ishmael/Waarabu) Lakini sheria (Ishael/Waarabu) wataiharibu Neema (Isaka) Isaka (Neema) pekee anaruhusiwa kuishi ndani ya kambi, ishimael haruhusiwi kwani anamdhihaki atamuua motto wa ahadi (Ahadi, Isaka, Neema). Ukweli huu unabaki kuwa kweli jana leo na hata mlele. 

Haijalishi inatuuma vipi kuhusu kuiacha sheria lakini ni lazima itupwe nje ya kanisa hili ni kongwa lazima litupwe jangwani, kama wachungaji najua tunajua umuhimu wa zaka katika kanisa na mazingira yake na ni yenye faida kubwa sana kanisani, ni kweli kama daktari anaweza kuona umuhimu wa Tohara kwa wanaume ina faida nyingi sana, kama mtaalamu wa tiba mbadala anaweza kuona umuhimu wa kujihadhari na baadhi ya vyakula katika kuimarisha afya zetu lakini inatupasa kuweka mbali haya yote Tohara, Zaka,agano la kale na taratibu zake na kutii matakwa ya Mungu Hajiri na Mwanaye ni lazima wawe nje ya kambi hakuna manungu’uniko hakuna kujiuliza maswali.

Kanuni za utoaji katika gano jipya

Ni muhimu kufahamu kuwa baada ya kulivunja kongwa la sheria la zaka ni muhimu sasa kufahamu kanuni za utoaji katika agano jipya inaonekana katika Wagalatia 6;6, inasema “mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote” andiko hili linafanana na ile kazi ya zaka zaka ilikuwa kwaajili ya ukuhani wa kilawi, lakini hapa tuafundishwa  kuwashirikisha mema wale wanaotufundisha neno la Mungu kwa maana ningine ni jukumu la wte wanaofundishwa neno la Mungu kuwasaidia wale wanaowafundisha neno la Mungu kwa kuwapa vitu vya kimwili 1Koritho 9;14, 1Timotheo 5;18 “Usimfunge ng’ombe kinywa apurapo nafaka”  na kila mtenda kazi anastahili ujira wake naamini hili ndilo jibu la wale wanaojiuliza itakuaje? Tukiamini kuwa agano la kale lilikuwa linatoa kivuli tu cha agano jipya swali linaweza kuwa inakuwaje endapo tutaachana na zaka? Naamini unaondoka katika kongwa la sheria sasa na kuifurahia neema ya Mungu na uhuru tulionao katika Kristo jambo la msingi sasa ni kumsikiliza Roho wa Mungu anakusukuma nini moyoni unapaswa kusaidia pale unapolishwa neno la Mungu kwa kanuni hii ya upendo na msukumo wa moyo na kumpenda kwako Mungu.

Tunafundishwa pia kanuni ya kupanda na kuvuna Wagalatia 6;7,2Wakoritho 9;6 upandaji huu unaendana na kuvuna lakini sio deni kuwa ni lazima uvune, tunafundishwa kutoa kwa kadiri ya neema na moyo 2wakoritho 8;2-3 kwa msingi huo katika Agano jipya kutoa ni mpango au msukumo wa moyoni na sio sheria, kutoa huko kwa moyo sio kule kwa manunguniko na maumivu bali kwa ukarimu 2Koritho 9;7 ni kwa msukumo wa huruma waefeso 4;28 kuwagawia wahitaji, kuacha ubinafsi, 2Wakoritho 11;9, kwa nini Paulo asifundishe kuhusu zaka?Paulo anazungumza kuhusu ujira 1Timotheo 5;18 anazungumza pia kuhusu zawadi na sio kupokea zaka na msaada na sio zaka au mafungu wafilipi 4;15-19, ni kwa moyo 2Wakoritho 8;16, Mungu ameiandika sheriaya agano jipya katika mioyo yetu kwa msingi huo viongozi wa kanisa wanapaswa kumuamini Mungu kuwa wasshirika wao watamsikiliza Mungu katika mioyo yao na siku zote njia ya mwanadamu ni pamoja na kutokuamini tunaweza kuhubiri injili hata bila ujira 2wakoritho 11;7. Kama nitalipa zaka nitakuwa na la kujisifia lakini katika Kristo ni kwa neema na Imani na sio kwa matendo si kwa matedno mtu awaye yote asijisifu Efeso 2;8-9.

Zaka kwa kweli ni kodi ndani ya uhuru wetu katika Kristo ni muhimu kwetu kuasi kodi hii na kudai uhuru wetu katika Kristo, Mungu anataka kuweko na uhuru ambao utaruhusu utoaji wa imani na wakimiujiza ambapo watu watatoa kwa ukarimu hata zaidi ya zaka imebainika hata katika inchi ambazo wanalegeza kodi uchumi huimarika na wanapata sana kuliko katika inchi zinazokazia, je unadhani kama kanisa litaachana na kutegemea zaka kama mabaki ya sheria na wakaundishwa kutoa kwa moyo uchumi wa kanisa utaongezeka? Jibu ni ndiyo 2Wakoritho 8;2 Biblia inasema “Maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umasikini wao ulikuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimuwao maana nawashuhudia kwamba kwa uwezo wao na zaidi ya uwezo wao kwa hiyari yao wenyewe walitoa vitu vyao”unaona watu masikini sana lakini walitoa zaidi ya kawaida huu ni utoaji wa kiimani na kimuujiza ni wazi kuwa hata ufanye nini huwezi kupata ushahidi wa kimaandiko katika agano jipya ili kupata mashahidi wawili au watatu na kufanya fundisho 2Wakoritho 13;1, Warumi 8;2 na tuifuate sheria ya Roho wa uzima.

Hebu jaribu kuwaza mpezni msomaji kuhusu sheria za agano lake zilivyokuwa ngumu Hekalu la agano la kel na sheria zake yaani pamoja na zaka zimekufa hekalu limekufa miaka 2000 iliyopita Mathayo 27;51 Warumi 7;2 hatuwezi tena kuendesha farasi aliyekufa sasa ni zaidi ya miaka 2000 tangu hekalu na taratibu zake zilipozikwa kwa nii tuendelee kuabudu kwa namna za kihekalu?Je inatupasa kutoa sadaka za kuteketezwa sasa? Je inatupasa kutahiriwa sasa? Je ni sheria ngapi za agano la kale tunazifuata katika mtindo huu mpya wa kuabudu? Ni nini makusudi ya kifo cha Kristo? Je sadaka yake haitoshelezi? Efeso 2;15, Wakolosai 2;14-23
Fedha zinazolipwa zaka leo zinaweza kulaaniwa
Waangalie wanandoa ambao wamekuwa wakilipa zaka kwa miaka mingi leo makanisani je wamewahi kutoa asilimia Ishirini ya mapato yao? Jibu ni la Binafsi naamini tunapaswa kutenda vema zaidi ya wakati wa agano la kale, Zaka wanazotoa wengi ni katika mfumo ule wa agano la kale katika mfumo huo 10% walawi 27;30 na ingine ni ile itolewayo kwa upendo Warumi 13;8, wengi wameacha sheria iliyoko katika mioyo yaom wanafuata ile iliyoandikwa katika mbaombili za mawe Warumi 14;23 na wanaacha kuitii sheria ya kifalme yaani imani na upendo ambao ndio udongo mzuri. Kuna maandiko zaidi ya 39 katika agano la kale na agano jipya yanayozungumzia au kugusia zaka lakini ni 7 tu kati ya hayo ni ya agano jipya esu alioyatimiza hayo yote 39 na hatuko chini ya deni katika agano la kale usipolipa zaka ya shs 3;76 utadaiwa kulipa shs 9 na tukiifuata hii kwa asilimia 99.9999 tutakuwa chini ya laana asilimia 100 je Mungu angetupenda tena? Si vema kuwatishia waamini katika agano jipya kuwa watalaaniwa kwa kutokutoa zaka laana? Ndani ya agano jipya? Yesu alikufa kwaajili gani sasa? Wale washikao sheria wamelaaniwa Wagalatia 1;6-8 na wale wanaowahubiri watu injili nyingine ya kuambatana na sheria ndani ya Kristo wamelaaniwa Warumi 4;15 “sheria ndiyo ifanyayo hasira Pasipokuwa na sheria hapana kosa”

Utoaji halisia
Kwa bahati mbaya unaweza kusoma kitabu hiki na ukaamua kutokutoa au kupunguza swala la utoaji nitakuomba usome tena na tena mada hii ili uweze kuielewa vema kwa moyo wako na sio kwa kichwa chako, utahitaji kichwa chaki kiasi kwaajili ya kujifunza maarifa, unahitaji kutumia akili kiasi kupiga hesabu wakati unataka kutoa zaka lakii pia utahitaji kupiga hesabu pia wakati unataka kujaribu kuacha kutoa vyote vinahitaji kichwa na sio moyo Yakobo 2;26 inasema hivi na mwili pasipo roho imekufa kwa hiyo imani pasipo matendo pia imekufa kama akili zako zitakuwa sawa utaendelea kutoa zaka kwa sababu uko chini ya sheria na utumwa na utavuna haba Hagai 1;6 mtu ambaye sio mtoaji amejitenga na tabia ya uungu kabisa.

Wengi wa wachungaji wanaosoma habari hii watakubaliana name kuwa ni asilimia chache sana ya washirika wanaotoa Fungu la Kumi kwa ujumla inaweza kuwa chini ya asilimia tano ya washirika ndio wanaotoa zaka aibu kwa kanisa hii ni kwa nini kwa sababu hawalijui neno la Mungu Mungu aliupenda ulimwengu na akamtoa.......Yohana 3;16 lazima tuwe na tabia ya uungu moja ya tabia ya uungu ni pamoja na kutoa Waefeso 5;1-2,Kwa hiyo, mfuateni Mungu kama watoto wapendwao, Mkiishi maisha ya upendo, kama vile Kristo alivyotupenda sisi akajitoa kwa ajili yetu kuwa sadaka yenye harufu nzuri na dhabihu kwa Mungu”.Luka 6;38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”Matendo 20;35 “Ni heri kutoa kuliko Kupokea” Biblia inaahadi nyingi sana kuhusu utoaji kadiri unavyojitoa ndivyo unavyofungua mlango wa kupokea zaidi huu ni wakati wa mwisho Mungu anakusudia kuleta uamsho mkubwa sana ambao unahitaji fedha kufanikisha kazi yake ma inahitaji wakristo wakarimu nimalizie kwa kusema hivi katika agano jipya zaka ni 100% kila kitu ni cha Mungu na hivyo tumkumbuke Mungu ka kuisapoti kazi yake, usijifunge katika kifungo cha laana ya zaka ya agano la kale bali ruhusu Mungu akuongoze ukitoa zaidi ni vema na ukiwa na kichache usijihukumu.

Maoni 7 :

  1. kazi ya Mungu haiwezi kwenda bila Sadaka na Fungu la kumi.ili kanisa liweze kufunguwa milango linahitaji pesa na bila pesa kanisa lolote lile ulimwenguni halita funguliwa na watumishi wake wachungaji ambao hawana kazi wanategemea kuhubili Injili tu hawataweza kulihubili neno la Mungu.
    Yatupasa kufahamu pia kuwa nyumba za Mungu ''Makanisa' hayawezi kujengwa bila ya hizi sadaka..Yesu alisema nendeni mkaieneze Injiri kote ulimwengunilakini aliposema haya zamani hakukuwa na usafiri vyombo vya kuhubilia ambavyo ka sasa vipo na vinahtaji pesa na pesa hii inatoka kwenye Fungu la kumi au Sadaka.
    Kwa hiyo basi Injiri ya zamani na ya sasa ni tofauti ya sasa inamahitaji mengi ili iweze kuwafikia wengikwa hiyo sadaka na fungu la kumi ni lazima ili kumpendeza bwana.Na Yesu alisema sikuja kutengua Toulati nimekuja kutimiliza na mbingu na nchi vitapita lakini hakuna hata neno moja litakalo undoka... Asanteni sana

    JibuFuta
  2. Bwana Yesu asifiwe.
    Ahsante kwa mafundisho mazuri ya utoaji wa zaka na sadaka uliyotoa.
    Nadhani ni vyema kufahamu ya kwamba utoaji wa zaka ni tendo la imani. Ukiamini kuwa kutoa zaka ni kujiingiza kwenye kongwa la sheria, ni heri uache kutoa. Lakini ukiaminikwamba hatuwezi kutengua hata neno moja katika torati, bado hutakuwa chini ya sheria kwa sababu ni moyo wako unaoamua bila hofu kuitimiliza torati. Bado naamini zaka inafungua madirisha ya mbinguni kwa ajili ya baraka zangu kwa kadri nitakavyotoa sadaka. Naona hiyo siyo sheria bali mapenzi ya mtu binafsi. Haijasema kuwa usipotoa zaka utapata madhara lakini inakuhimiza utoe kwa ajili ya kazi hasa siku za mwisho kwa kuwa tunahitaji mali kwa ajili ya kuwaleta watu kwa Yesu. Mimi nahimiza tutoe zaka si kwa sababu ya sheria ya torati bali kwa ajili ya kazi iliyoko mbele yetu ya kuipeleka ijnili kwa watu wote. Tutaipelekaje tusipopelekwa? Zaka inatupeleka pamoja na sadaka. Ijaribu zaka na sadaka na utaona bila hofu ya sheria na utaona kweli mambo ya ajabu yakitokea kwa ajili ya kuisukuma injili. Nadhani sio sahihi kuogopa kwamba kutoa zaka ni dhambi. Sijayaona mafanikio ya kanisa lililoacha kutoa zaka likafanya maendeleo makubwa kwenye Injili. Washirika wako duni na kazi inasimama. Adui anaweza kutumia nafasi hii kudumaza huduma zetu za uinjilisti na umisheni.Jambo la msingi ni KUANGALIA KUSUDI. Kwa nini natoa? Ni kwa saababu naiogopa sheria au natimiza kusudi la Malaki ya kwamba tutoe zaka kamili kwa kusudi maalumu. Nashauri kila mtu ATOE ZAKA KAMILI ili tuweze kwenda shambani tukiwa tumeshiba. Kinyume na haya ni kutoa nafasi kwa adui azuie mifuko ya wenye imani haba wasitoe.
    Rev. SIMBA MSUYA
    28TH SEPTEMBER 2020

    JibuFuta
  3. Ni muhimu kumtolea Mungu vyote vilivyo vizuri KWA moyo wa kupenda na Huku ukijua vyote ni vya kwake.Amina

    JibuFuta
  4. Nikupitia matoleo ya zaka na sadaka ndipo tunaonesha utii wetu kwa Mungu

    JibuFuta
  5. Asante kwa ufafanuzi mzuri wa zaka, mtu hapati huduma za kiroho eti kwa sababu hajatoka zaka, tumefika kubaya, kama unapenda kutoa, toa sadaka Yako iliyonona ili injili isonge mbele ila isifikie hatua ya mtu kutopewa huduma za kiroho eti kwa sababu hajatoka zaka.

    JibuFuta
  6. Ukosawa wachungaji wengi hushikilia sana kipengele hiki nakutishia

    JibuFuta