Jumamosi, 5 Machi 2016

Toba hupokelewa wakati gani?



Toba hupokelewa wakati gani?
     Ndugu msomaji wangu nataka kuzungumzia kwa masikitiko kuhusu kongwa lingine ambalo wahubiri wengi sana wanawafungia watu mizigo na kuwatishwa kupitia kutokuelewa au kiburi cha uzima au kuchukua nafasi ya Mungu hii itafahamika zaidi kwa kujiuliza swali kuwa Toba hupokelewa na Mungu wakati gani? Bila shaka umepata kusikia au kuona au kushuhudia watu waliookoka wakitangazwa na wachungaji mimbarini kuwa wametengwa kwa miezi sita au mitatu au mwaka au penginepo yamekukuta wewe mwenyewe hata kama moyo wako umepondeka na umemaliza na Mungu lakini unalazimika kutengwa kwa muda anaotaka mchungaji au askofu je swala hili ni sawa na injili au ni mapokeo? Na kwa makanisa yenye misimamo mikali zaidi watu hufukuzwa au kuondolewa ushirika pia unaweza kuwa umesikia hili je ni sawa na injili je kama watu hawa wametubu kwa Mungu toba yao imepokelewa anayewafunga ni nani Munu au Mwanadamu? Nataka kabla sijajibu maswali haya nikurudishe nyuma kidogo katika somo la wokovu nilipokuwa nikizungumzia kuhusu toba ni nini Bila shaka nilieleweka vema lakini nataka kufafanua tena kidogo kisha kujibu swali hili muhimu.


 Ni muhimu kufahamu kuwa Toba ya kweli haipaswi kupitia kwa wanadamu!

Neno Toba repent ni kuhuzunika moyo kwa mujibu wa Biblia ya Kiebrania neno Sigh hutumika ambalo maana yake ni kuhuzunika moyo, kujuta, kughairi, kuomboleza au kuwa na mpango mpya Tunaweza kuona asili ya neno hili katika Mwanzo 6;6-7 Biblia inasema hivi “Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani akahuzunika moyo Bwana akasema nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemuumba usoni pa nchi mwanadamu na mnyama na kitambaacho na ndege wa angani kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya” kwa msingi huo basi neno kutubu kwa kiibrania ni kuhuzunika na kughairi mpango fulani uliokuwa nao. kwa hiyo kimsingi toba ni lazima iwe na mfuatano wa kuhuzunika moyo na kuchukua hatua mdhubuti. Kuhuzunika bila kuchukua hatua sio toba kamili. Kama ulikuwa unafanya jambo fulani lazima ughairi Kutoka 32; 14, 1Samuel 15;11

Neno toba Katika Biblia ya kiyunani linatumika neno Metanoeo au metanoia au metamelomai ambalo maana yake ni kuwa na hisia nyingine, au kuhuzunika na kuchukua hatua ni kubadilika hivyo toba ni kuhuzunika na kubadilika au kuhuzunika na kuchukua hatua mfano Mathayo 21: 28-31 Biblia inasema hivi “Lakini mwaonaje mtu mmoja alikuwa na wana wawili, akamwendea yule wa kwanza  akasema mwanangu nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu, Akajibu akasema naenda Bwana  asiende, Akamwendea Yule wa pili akasema vilevile, Naye akajibu akasema Sitaki baadaye akatubu akaenda , Je katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia ni Yule wa pili…”Bila shaka ni wazi kabisa kuwa katika mfano huu wa Bwana Yesu alikuwa akionyesha ni nani ametubu toba ya kweli, kuhuzunika bila kuchukua hatua sio toba kamili Yuda alihuzunika alipokuwa amemsaliti bwana Yesu alifanya vema kuhuzunika  lakini hakufanya mapinduzi dhidi ya huzuni yake bali aliamua kwenda kujiua hii haikuwa toba kamili, Toba ya kweli hujumuisha kuhuzunika na kubadilika kimtazamo na toba hii ya kweli itapelekea maisha yako kuwa yenye furaha hutakuwa mtumwa wa huzuni tena utawekwa huru kutoka kongwa la huzuni.

Mafundisho kuhusu toba leo yamefanywa kuwa magumu na wahubiri na wamewafunga watu katika makongwa yasiyokuwa na Dawa kwa nini kwa sababu kama umefahamu vema maana ya toba utaweza kuona kuwa toba hutokea wakati mkosaji amedhamiria kwa dhati kutambua na kurekebisha makosa yake kwa wakati uleule na anapokea msamaha wakati uleule anapokuwa amelazimika au ameamua kutubu, kumbuka kuwa hata kuokolewa kwetu kulitegemeana na toba tuliyotubu kwa kumuamini Kristo na ingawa tulikuwa wabaya na tusiofaa kwa Mungu saa ileile tulipotubu tuliweza kupokea wokovu na Mungu akatukubali kana kwamba tumezaliwa tena na ndivyo ilivyo, hebu tuangalie kibiblia kwa maneno ya Mungu zaidi kuona kuwa toba hutokea wakati gani? Nitatoa mifano michache ya kibiblia ili tuweze kujifunza kimsingi toba hutokea wakati gani?

*      Mfano wa kwanza ni mfano wa Daudi wote tunafahamu jinsi ambavyo Daudi alifanya dhambi alifanya uzinzi, mauaji na uongo na kwa hivyo alikuwa na hatia alikuwa amelidharau neno la Mungu na Mungu mwenyewe pia tena alijikausha kwani alijua wazi kuwa mpango wake hakuna mtu anaujua 1Samuel 11;2-27 hili lilikuwa ni swala ambalo lilimchukiza sana Mungu kuna uwezekana kabisa kuwa wengi wetu hatujawahi kufikia kiwango hiki cha dhambi ambacho Daudi alikuwa amekifikia na kwa mujibu wa sheria alistahili kulipa mara nne na kufa pia sawa na hukumu aliyojitamkia na sawa na sheria ya Musa  hata hivyo Mungu alimtuma Nabii Nathani kama mchungaji kwa kusudi la kumrejeza mtumishi wake Daudi ambaye wakati huu alikuwa anaona kama amefaulu katika swala alilolifanya na pamoja na kuwa na dhamiri laini daudi alikuwa amejikausha tu wakati huu na sifikiri kama alikuwa na mpango wa toba, hata hivyo baada ya nabii Nathani kumueleza kile alichokifanya na kubaini kuwa Mungu amejua dhambi yake ndipo sasa Daudi anaingiakatika toba 1Samuel 12;1-14. Mstari wa 13 toba ya Daudi inaonekana na msamaha wa Mungu wakati huohuo angalia Biblia inasema hivi “Daudi akamwambia Nathani nimemfanyia Bwana dhambi.Nathan akamwambia Daudi Bwana naye ameiondoa dhambi yako hutakufa.” Hapa Biblia inaonyesha kuwa Daudi alisamehewa wakati uleule mara alipomaliza kutubu na hatuoni Nabii Nathani akimtenga Daudi miezi mine au sita n.k

*      Ahabu ni moja ya wafalme wa Israel aliyekuwa muovu sana aliabudu miungu migeni lakini zaidi sana alidhulumu shamba la Nabothi 1Wafalme 21;1-26 Mungu alimtuma nabii Eliya kumkemea na kumueleza namna Mungu alivyochukizwa na uovu wake Msatari wa 27 Biblia inasema hivi “Ikawa Ahabu aliposikia maneno hayo akayararua mavazi yake akavaa magunia mwilini mwake akafunga akajilaza juu ya magunia akaenda kwa upole” ni wazi kuwa Mfalme huyu muovu aliona anapaswa kunynyekea kwa Mungu kwa ajili ya uovu wake Mungu anayeheshimu toba alipoliona tendo hilo Mungu alitangaza msamaha 1Wafalme 21;28-29 Neno la Bwana likamjia Eliya “Mtishibi kusema Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili (Alivyojishusha) sitayaleta mabaya….” Ni wazi kuwa mfalme huyu alisamehewa mara baada ya kuonyesha toba ya kweli na ingawa ni wakati wa agano la Kale hatuoni akitengwa akipokonywa ufalme, Mungu anaheshimu sana toba na mtu akitubu husamehewa mara moja hakuna maandko popote yanapoagiza kumtenga mtu miezi mitatu au mwaka au miezi minne haya ni makongwa ambayo watu wengi wamefanyiwa makanisani wamenyanyasika na kudhalilishwa na wanadamu wenzao wenye mwili na damu kama wao wakiwatangaza madhabahuni na kueleza aina za uovu waliofanya na kuwatangaza kuwatenga je unafikiri huo ni mpango wa Mungu? Je toba hupokelewa wakati gani? Tunaona mara tu mtu anapotubu anastahil kusamehewa awe amemkosea Mungu au mwanadamu mwenzake hapa duniani hakuna jambo la Muhimu kama msamaha kwani sisi sote twakosea Yakobo ndugu yake Bwana mtume aliyeheshimika sana anasema wote tunakosea katika mambo mengi  Yakobo 3;2 “Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi, mtu asiyejikwaa katika kunena huyo ni mtu mkamilifu awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu” maandiko yanaonyesha wazi kuwa kila mtu anaweza kukosea hata kama yuko katika ngazi ya kuwafikia mitume au kuwazidi maadamu ni mtu lazima tujifunze kusamehe.

*      Mfano mwingine ni wa mfalme aliyeitwa Manase huyu ni moja ya wafalme waliowahi kufanya uovu kwa kiwango cha kupindukia Tunasoma katika 2Wafalme21;1-10 “Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala, akatawala katika Yerusalemu kwa miaka hamsini na mitano. Jina la mama yake aliitwa Hefsiba. Akafanya maovu machoni pa BWANA, akafuata desturi za machukizo za mataifa ambayo BWANA aliyafukuza mbele ya Waisraeli. Akajenga tena mahali pa juu pa kuabudia miungu ambapo baba yake Hezekia alikuwa amepabomoa, pia akasimamisha madhabahu za Baali na kutengeneza nguzo ya Ashera, kama Ahabu mfalme wa Israeli alivyofanya. Akasujudia na kuabudu jeshi lote la angani. Akajenga madhabahu ndani ya hekalu la BWANA, ambalo BWANA alikuwa amesema, “Katika Yerusalemu nitaliweka Jina langu.’’ Katika nyua zote mbili za hekalu la BWANA, akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la angani. Akamtoa kafara mwanawe mwenyewe katika moto, akafanya uchawi na uaguzi, akataka shauri kwa wapiga ramli na kwa mizimu. Akafanya maovu mengi sana machoni mwa BWANA na kumghadhibisha.”Unaweza kuona aina ya uovu alioufanya Manase kwa kweli alifikia hatua ya kumtoa mtoto wake kuwa sadaka kwa miungu huu ni uovu mkubwa sana kuwahi kufanywa na mtu wa Mungu duniani na hivyo Munu aliruhusu waashuru kumchukua utumwani na kumpa shida sana ndipo manase aliamua kutubu baada ya toba ilikuwaje? Soma 2Nyakati 33 10-14 Biblia inasema “BWANA akasema na Manase pamoja na watu wake, lakini hawakumjali. Hivyo BWANA akaleta juu yao majemadari wa jeshi la mfalme wa Ashuru, ambao walimchukua Manase kwenda kifungoni, wakaweka ndoana katika pua yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli. Katika dhiki yake akamsihi BWANA Mungu wake na kujinyenyekeza sana mbele za Mungu wa baba zake. Naye alipomwomba BWANA akaguswa na kule kusihi kwake na akasikiliza kilio chake, kwa hiyo akamrudisha Yerusalem na kwenye ufalme wake. Ndipo Manase akatambua kwamba BWANA ndiye Mungu. Baadaye akajenga ukuta wa nje wa mji wa Daudi, magharibi mwa chemchemi ya Gihoni katika bonde, hadi kufikia ingilio la Lango la Samaki na akakizunguka kilima cha Ofeli, pia akaufanya kuwa mrefu zaidi akaweka majemadari katika miji yote ya Yuda iliyokuwa imejengewa ngome. Akaondolea mbali miungu ya kigeni na kuondoa sanamu kutoka katika hekalu la BWANA pamoja na madhabahu zote alizozijenga katika kile kilima kilichojengwa hekalu na katika Yerusalemu, akazitupa nje ya mji. Kisha akarudisha madhabahu ya BWANA na kutolea juu yake dhabihu za sadaka za amani pamoja na sadaka za shukrani, naye akawaamuru Yuda wamtumikie BWANA, Mungu wa Israeli.” Je msomaji wangu unajifunza nini rehema za Mungu zinapatikana mara moja mtu anapoangukia katika toba kwa kumaanisha Biblia inasema katika Mithali 28;13 “afichaye dhambi zake hatafanikiwa bali aziungamaye na kuziacha atapata rehema” ni wazi kwa namna iwayo yote kuzificha haimaanishi kuzificha kwa wanadamu lakini kunamaanisha kuzificha kwa Mungu si lazima umweleze mwanadamu dhambi zako lakini ni Mungu pekee tunayeweza kuweka wazi kila aina ya uovu tulioutenda na mara tunapotubu kwa dhati anatusamehe mara moja! , msamaha kwa watu wengi waliookoka leo ni shida kubwa sana kuupata mpaka unaweza kujiuliza kuwa wanasoma biblia gani ni mpaka wamekusulubisha na kukudhalilisha na kukutangaza duniani na kuharibu jina lako wakati mwingine wakiwa hawataki hata kukuona katika utumishi milele na ikiwezekana hata maisha yako yawe yamefilisika na umepoteza haki za nafasi zako zote ndipo bila msaada wa kutaka kujua kuwa umetubu au la sivyo alivyo Mungu na sivyo ulivyo wokovu!

*      Katika Mathayo 18;21-35 Yesu alifundisha kuhusu kusamehe Mungu anapoagiza kuhusu kusamehe anasema hivi sikuambii hata mara saba bali hata saba mara sabini. Msamaa wa kibinadamu unatakiwa kuwa hata zaidi ya mara saba mara sabini kwa siku unaonaje kuhusu msamaha wa Mungu bila shaka unatiririka kama maji, Mwana mpotevu alipozingatia moyoni na kuamua kurudi kwa babaye Babaye alimpokea baada ya kumuona kwa mbali Mungu hutusamehe tangu anapoiona nia yetu ikiwa imegeuka kumuelekea Yeye kutokuwasamehe watu kwa muda mrefu watu ambao wametubu wamehuzunika kunaweza kutupelekea kuingia katika mbinu za ibilisi za kutunyima Baraka za Mungu Biblia inasema hivi katika 2Wakoritho2;5-11 “Lakini iwapo mtu amehuzunisha, hakunihuzunisha mimi tu bali kwa sehemu nisje nikalemea mmno amewahuzunisha ninyi nyote, Yamtosha mtu wa namna hii adhabu ile aliyopewa na walio wengi hata kinyume cha hayo ni afadhali mmsamehe na kumfariji mtu kama huyo asije akamezwa katika huzuni yake ipitayo kiasi kwa hiyo nawasihi kumthibitishia upendo wenu maana naliandika kwa sababu hii pia ili nipate bayana kwenu kwamba mmekuwa wenye kutii katika mambo yote Lakini kama mkimsamehe mt kwa neno lolote name nimemsamehe kwaajili yenu mbele za Kristo Shetani asije akapata kutushinda kwa maana hatukosi kuzijua fikra zake.” Kama kanisa linashindwa kujua umuhimu wa kutoa msamaha kwa haraka kwa wakosaji ambao wamehuzunishwa na yale waliyoyafanya na wametubu kanisa hilo au wahubiri wa jinsi hiyo wameingia katika mtego wa shetani, baadhi ya wanatheolojia wanaamini kuwa maandiko haya yanamuhusu mtu Yule aliyekuwa anaishi katika maisha ya zinaa katika 1Wakoritho 5;1-10 na mtu huyo mwanzoni alikuwa anaona kitendo hicho kama kitendo halali na hivyo alikosa toba lakini ilipoeleweka kupitia maagizo ya mtume Paulo kuwa linalofanyika kuwa sio sahii mtu huyo alitubu na kanisa lilitakiwa kumsamehe unaona toba hupokelewa wakati gani?ni pale tu mtu anapokuwa ametubu kwa dhati Mungu humsamehe mtu huyo kanisa linapaswa kusamehe mara tu mtu anapoonekana kuwa ni mwenye toba na adhabu itolewe kwa wale wasiotaka kutubu.
*      Mfano wa mwana mpotevu pia ni moja ya mifano iliyo wazi kuwa toba hupokelewa wakati gani Biblia inasema hivi katika Luka 15;24 “Yesu akaendelea kusema: “Kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili. Yule mdogo akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe urithi wangu.’ Hivyo akawagawia wanawe mali yake.‘‘Baada ya muda mfupi, yule mdogo akakusanya vitu vyote alivyokwa navyo, akaenda nchi ya mbali na huko akaitapanya mali yake kwa maisha ya anasa. Baada ya kutumia kila kitu alichokuwa nacho, kukawa na njaa kali katika nchi ile yote, naye akawa hana cho chote.Kwa hiyo akaenda akaajiriwa na mwenyeji mmoja wa nchi ile ambaye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akatamani kujishibisha kwa maganda waliyokula wale nguruwe, wala hakuna mtu aliyempa cho chote.‘‘Lakini alipozingatia moyoni mwake, akasema, ‘Ni watumishi wangapi walioajiriwa na baba yangu ambao wana chakula cha kuwatosha na kusaza, bali mimi hapa nakufa kwa njaa! Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu na kumwambia, ‘Baba, nimetenda dhambi mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili tena kuitwa mwanao, nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’Basi akaondoka, akaenda kwa baba yake. “Lakini alipokuwa bado yuko mbali, baba yake akamwona, moyo wake ukajawa na huruma. Akamkimbilia mwanawe, akamkumbatia na kumbusu. “Yule mtoto akamwambia baba yake, ‘Baba, nimekosa mbele za Mungu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwanao tena.’“Lakini baba yake akawaambia watumishi, ‘Leteni upesi joho lililo bora sana, mkamvike pete kidoleni mwake na viatu miguuni mwake.Leteni ndama aliyenona, mkamchinje ili tuwe na karamu, tule na kufurahi. Kwa maana huyu mwanangu alikuwa amekufa na sasa yu hai tena, alikuwa amepotea na sasa amepatikana!’ Nao wakaanza kufanya tafrija. Ndugu mpendwa bila shaka umeyaona maneno haya “Lakini alipokuwa akali mbali Baba yake akamuona moyo wake ukajawa na huruma” Hili ni jambo la ajabu sana Baba huyu anatufundisha jinsi moyo wa Mungu ulivyo mwema na jinsi ulivyojawa na huruma kwa wenye dhambi na jinsi ulivyo tayari kusamehe kumbuka kuwa wakati huu hata mwana wake alikuwa bado hajawakilisha toba lakini tendo lile la kugeuka tu na kuonekana machoni pa baba yake tayari msamaha ulipatikana, je msamaha si ni jambo la muhimu sana katika ulimwengu huu tulio nao? Nani ni mkamilifu katika ulimwengu huu kila mmoja anahitaji msamaha wa Mungu na wa wenzetu na kanisani ndiko mahali pekee ambako tunaweza kuyafanyia kazi mambo haya kivitendo!.
*      Kisa kifuatacho kitakufundisha jinsi Msamaha ulivyo wa Muhimu sana kwa watu wa ungu ikiwa wapagani na watu wasiomjua Mungu wanaweza kuona umuhimu wa msamaha sisi ni zaidi sana soma kisa hiki cha kweli cha ndugu Sulemani Mdeni.

 “Naitwa Sulemani  Mdeni , sipendi kuzungumza mengi sana kwa sababu habari yenyewe imejaa vitu vingi vidogovidogo, nitasema yale ya muhimu tu ambayo ndiyo hasa  yamenifanya niandike habari hii, Nilizaliwa Tanga mjini mwaka 1954, nilikulia na kusomea Tanga ambapo nilipofika darasa la nne pale Chumbageni , nilianguka mtihani ambapo nilichukuliwa na mjomba kwenda Hedaru huko upareni, mjomba wangu alikuwa ni fundi cherehani, nilipofika Hedaru mwaka 1966 nilianza kujifunza kushona  wakati huo Hedaru kalikuwa ni kamji kadogo sana, nilijifunza uufundi hapo na kuwa fundi mzuri sana, Mwaka 1975 nilikwenda Korogwe ambapo nilipata kazi dukani kwa mzee mmoja pale Manundu. Siku moja mwaka 1977 niliamua kwenda Tanga kumsalimu mzazi wangu mama.

Nikiwa hapo nyumbani siku moja mama aliniambia kwamba kuna mtoto anateswa sana nyumba ya jirani, Nilimuuliza sababu ya kuteswa, mama akaniambia ni mtoto wa kaka wa huyo jirani ambapo mtoto wa huyo alikuweko, Niliambiawa alifika hapo  baada ya wazazi wake kufa na huyo ndugu ndiyo akamchukua, niliuliza mateso yake nikaambiwa kwamba alikuwa anafanyishwa kazi kama punda, anapigwa sana na kusimangwa  na kuna wakati watoto wa huyo jirani yetu wanataka kumlawiti, mama aliniambia kuwa kwa wakati ule Yule mtoto alikuwa anaumwa sana , niliambiwa kwamaba alikuwa na kidonda kikubwa sana ambacho alikipata kwa kujikata na ndoo iliyomwangukia wakati akichota maji, nilisimuliwa mengi sana kuhusu maswala ya mtoto Yule na roho ikaniuma sana , hasa baada ya kuambiwa pamoja na hali aliyonayo bado anafanyishwa kazi sana , hata watoto wa kike wa ile nyumba ya jirani walikuwa hawafanyi kazi isipokuwa mtoto tule ambaye niliambiwa alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili tu. Nilipiga akili hatimaye niliipata, (nilikuwa na rafiki yangu polisi naomba nisitaje kituo) pale Tanga niliamua nikamwambie aje awatishe wale majirani zetu na kumchukua mtoto kwa lengo la kumpeleka Hospitali, haja yangu ilikuwa ni kumchukua mtoto Yule na kwenda naye Korogwe.

Ni kweli mpango wangu ulifanikiwa bila wale majirani kujua kuwa kwamba nilikuwa nimeusuka mimi, mtoto Yule alichukuliwa na polisi na kupelekwa kweli Bombo Hospitali kuu mkoani hapa , baada ya siku nne ambapo muda wangu wa kuondoka ulikuwa umefika  niliondoka na Yule mtoto, alikuwa ni mtoto mwenye mwili mkubwa licha ya kuonewa na alionyesha pia kuwa na akili, nilimuuliza kama mangependa kusoma  na alikubali, nilimtafutia shule ambapo alianza darasa la nne  kama nilivyokuwa nimefikiria mtoto alikuwa na akili  sana kwani alianza kuongoza , alimaliza la saba mwaka 1980 na kufaulu kwenda shule ya sekondari Magamba Lushotoalisoma hapo hadi mwaka 1985 ambapo alimaliza kidato cha nne, hakufaulu vizuri sana , lakini ilikuwa inaeleweka , alipokuwa kidato cha pili alianza uhuni wa mambo ya kutafuta wasichana na kuvuta sigara. Niliitwa mara mbili shuleni na alisimamishwa shule mara moja ,hata mimi alianza kunidharau sasa, lakini jinsi maisha yake yalivyokuwa  niliona sina budi kuendelea kumsaidia , alipomaliza shule alikuwa ni mtu wa vijiwe tu na ukimsemesha anasema hawezi kuzungumza na watu wasiosoma , yaani alibadilika sana.  

Niliamua kumsaidia apate kazi , nilipata bahati siku moja ya kukutana na mzee mmoja amabaye nilimshonea suti ya sherehe ya miaka 20 ya ndoa yake, pamoja na familia yake , amabaye aliafurahishwa sana na kazi yangu, mzee huyu zamania alikuwa serikalini, nilimuombea kazi huyu kijana , ambaye kwangu alikuwa kama mdogo wangu hasa kwa kuzingatia kuwa sikuwa na mdogo wa kiume , huyu mzee alinisaidia  nikapata kazi kwaajili ya huyu ndugu yangu kwenye kampuni moja pale (Tanga naomba nisiitaje)ilikuwa kama bahati kwani alipata kazi mahali pazuri sana , nikisema pazuri kwa mazingira ya kijinga  ni mahali ambapo aliweza kuiba  hii ilikuwa ni mwaka 1990. Baada ya kuanza kazi sikumuona tena hadi mwaka 1993 nilipoenda Tanga  nilimpitia kazini kwake kumjulia hali, ambapo hakuchangamka kabisa, ilikuwa kama vile hakuwa akinifahamu, Sikujali kwani hata mama aliniambia kwamba kuna siku alipatwa na dharula akaenda kumuomba msaada, akamwambia mama kwamba hana kitu, ikiwa ni uongo mkubwa, wakati huu huyu bwana mdogo alishajenga nyumba Muheza na alishanunua kiwanja pale Korogwe na alikuwa na teksi Dar hiyo ni kwa miaka mitatu tu, sikujali niliumia lakini nilijiambia lengo langu la kumsaidia lilikuwa limetimia Nilisema hayo kutoka moyoni kabisa.

Mwaka 1996 nilikuwa ndio kwanza nimeoa mke wa pili baada ya Yule wa kwanza kunishinda, siku moja jioni wakati mimi na mke wangu tunatembea pale Tanga nilikutana na Yule bwana mdogo , Nilishangaa kwamba alinichangamkia sana, Aliniomba radhi kuwa hanitembelei kule Korogwe  kwa sababau yuko bize, sana amepandishwa cheo kazini , Nilimtambulisha kwa mke wangu mpya  na aliuliza kwa mshangao kama nimemuacha Yule shemeji yake (mke wangu wa kwanza)niliomwambia ndio  hakusema neno  lakini nadhaniu alifurahi, kwani walikuwa hawaelewani kabisa, alinipa hela nakumbuka kwa mara ya kwanza kabisa  tangu kuanza kazi, nilitaka kuzikataa lakini niliona haitakuwa vizuri zilikuwa ni 12,000 kwa wakati ule zilikuwa nyingi kidogo, halafu alihaidi kwamba angenitembelea Korogwe.

Alinitembelea kweli siku nne tu baadaye, alifika nyumbani kwanza mimi nikiwa kazini, Kuanzia hapo akawa anakuja nyumbani kwangu haipiti wiki amekuja kusalimu, Akawa analeta vyakula, samaki na hata nguo anatununulia, hatimaye akanisaidia nikapata zabuni ya kushona nguo za kazini kwao. Niliweza kumalizia nyumba yangu pale Pongwe kwa fedha hizo, lakini siku moja  mwaka 1997 jirani yangu mmoja tena mtu mzima  aliniomba tuzungumze nikamkubalia, aliniambia jioni nikifunga kazi tukae mahali tuzungumze. Huyu mzee alianza kwanza kwa maneno ya hekima na busara, halafu alisema alichoniitia, Sikuwa nategemea alichiniambia kwamba mke wangu alikuwa ananiendea kinyume, alisema wazi kwamba alikuwa akitembea na Yule kijana ambaye huyu mzee alikuwa anamjua tangu namleta pale akiwa ananuka kidonda, sikuamini kwani kwa jinsi nilivyokuwa namjua Yule mzee niliamini kuwa kuna ukweli. Niliporudi nyumbani sikumuuliza mke wangu ingawa nilikuwa na maumivu ambayo nina sitakuja kuyahisi tena maishani mwangu, Yule mzee alinishauri nisiseme chochote nyumbani kwani kumfumania mke wangu kwenye tendo ingekuwa rahisi sana.

Siku mbili tu baada ya taarifa ile Yule mzee alinifuata kazini kwangu na kuniambia kwamba mke wangu yuko na Yule bwana mdogo nyumba ya wageni, Alinitajia nyumba yenyewe na tuliondoka naye kwenda huko, Ni kweli alikuwa hapo na Yule kijana, sikuumia palepale sijui kwanini, nilipohakikisha nilifunga mlango na kuondoka. Yule mzee alinisaidia kufanya utaratibu wa talaka, nilitoa talaka siku ileile na baada ya kutoa talaka ndipo hasa nilipohisi maumivu ya kweli, niliumia kiasi kwamba niliona ni lazima ningekufa, hguwa sinywi pombe lakini nilitaka kwenda kunywa, ilipofika saa nne usiku niliingia chumbani kwangu na kuzima taa halafu nilichukua mswala  na kukaa chini nilianza kumshitakia Mungu nilianza kunuia mabaya  kwayule kijana  nilipotea kabisa kwenye sala ile  ya kunuia ubaya hadi majogoo yanawika. Nilisali hadi nikaona mwanga nisioujua, nililenga ubaya tu.

Najua hutaamini, siku ya nne tangu tukio lile nikiwa nyumbani kwa mama yangu ambapo nilienda kupumzika nililetewa taarifa kwamba Yule kijana alikuwa ameshakamatawa na yuko Polisi, niliambia alikuwa amekamatwa kwa tuhuma za wizi,wiki moja baadaye kilakitu alichokuwa anakimiliki kilikamatwa  na alikuwa rumande, lakini wiki mbili baadaye aliachiwa  huru baada ya mwenye kampuni  kumuomba polisi wamwachie maana amepata mali zake, aliachiwa akiwa hana hata senti tano, alihamia mji wa Tanga . Mwaka huohuo nilihama kutoka Korogwe kuja Tanga na kuanzisha shughuli pale Pongwe, Lakini nilipofikiria kuwa nyumba ile nimeijenga kwa zabuni ya dhambi niliiuza, mwaka 2002 nikiwa nyumbani pamoja na mama na ndugu zangu wawili wa kike tuliona mtu akija. alikuwa ni  mwanaume ambaye wazi alikuwa anaumwa , alikuwa mchafu, kupindukia na alikuwa na kidonda mguuni, baada ya kutusalimia ndipo polepole  tulipobaini kwamba alikuwa ni Yule kijana, Mahali alipokuwa na kidonda mguuni ni palepale ambapo alikuwa na kile kidonda  wakati namchukua, alipokwisha kusalimu alipiga magoti  na kusema kaka najua ni vigumu kunisamehe, lakini naomba uendelee kufikiria kunisamehe  siku moja hata nikiwa nimeshakufa, nilikuwa mjinga, kichaa, mnyama asiyefaa hata kuliwa…” alianza kulia , mimi nilinyamaza kimya  nikimtazama sikuwa na hasira naye kabisa, dada zangu na mama ndio walikuwa wakimzonga huku wakimcheka kwa kebehi, Naomba kaka uniombee heri niwe binadamu tena , ni wewe ulinifanya nikawa binadamu nikakosa shukuraninaomba uniombee niwe mwenye hekima  tu nipate hekima tu si utajiri..’

Akina dada na mama walimcheka  na kuanza kumtukana Mimi sikufanya hivyo nilimsjhika mkono Yule kijana na kumuinua Ni kweli umekosa  na umejua kosa lako, mimi na wewe tutaomba pamoja  kwa Mungu urejewe Ufahamu, Dada zangu walipiga kelele  za mshangao na kupinga jambo lile  nilimsaidia Yule kijana kuoga  na alipewa chakula ingawa kwa masimango, usiku nilimwomba aingie chumbani kwake aombe anachokitaka kimtokee, nami nliingia chumbani mwangu na kuanza kusali  nikimwombea mabadiliko, Najua wakati mwingine ni vigumu kuamini mambo haya lakini nasema hivi yapo, huyu kijana alikaa pele nyumbani na kidonda chake kilikauka  baada ya wiki tatu tu, wakati alikuwa amehangaika nacho kwa mwaka mzima, unajua huyu kijana siku hizi yuko wapi? Ukiona watu wanaokuja Dar wakitokea Mombasa kama wafanya biashara ulizia Bwana Abuubakar au jitu kubwa, Amerudi kwenye hali yake ya kawaida ya zamani bwana mafedha lakini hivi sasa anajua kuheshimu nwatu hata watoto wadogo, na mimi nimepata ndugu hivi sasa. Je nguvu ya maombi iko wapi? Je kumtendea mtu uovu ni swala unalolichukuaje na unalielezea vipi? Je huoni kwamba Kusamehe ni jambo la muhimu sana? Najua kuwa unakodoma mimacho kwa mshangao lakini Kristo alisema waombeeni wanaowaudhi watendeeni mema adui zenu.

Bila shaka utakuwa umejifunza maswala muhimu sana kutoka katika kisa hiki cha Sulemani mdeni ingawa yeye sio mkristo lakini anaona umuhimu wa kusamehe sisi nasi inatupasa kuwa watu wa kusamehe, tusifurahi watu wanapofanya makosa na kukimbilia kuhukumu huku tunafahamu wazi kuwa na sisi ni binadamu wala tusifanye msamaha kuwa kitu kinachopatikana kwa shida sana hali wokovu unapatikana kwa urahisi sana Bwana alipe neema kanisa na kuliponya kutoka katika kongwa la kuwatenga watu kwa muda ssio wa kibiblia bali kama tu mchungaji anavyojisikia hayo sio mafundisho ya injili wala wokovu tulionao

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni