Jumanne, 26 Julai 2016

Ujumbe: Kikombe Changu Cha Uaguzi!


Mwanzo 44:1-5 Biblia inasema Hivi “1. Akamwamuru yule msimamizi wa nyumba yake akisema, Jaza magunia ya watu hawa chakula kwa kadiri wawezavyo kuchukua, utie na fedha ya kila mtu kinywani mwa gunia lake. 2. Na kikombe changu, kikombe kile cha fedha, ukitie kinywani mwa gunia la yule mdogo pamoja na fedha ya nafaka yake. Akafanya kama vile alivyomwambia Yusufu. 3. Asubuhi kulipopambazuka, hao watu wakapewa ruhusa, wao na punda zao. 4. Na walipotoka mjini, wala hawajaendelea sana, Yusufu akamwambia yule msimamizi wa nyumba yake, Ondoka, uwafuate watu hawa, nawe utakapowapata, waambie, Kwa nini mmelipa mabaya kwa mema? 5. Je! Kikombe hiki, sicho anyweacho bwana wangu? Naye hufanya uaguzi kwa hicho. Mmefanya vibaya kwa kufanya hivi.” 

 kikombe cha uaguzi hakikuhusu maswala ya uchawi bali kilihusu upambanuzi wa Kimungu kuhusu badiliko la Ndugu zake yaani wana wa Israel


Leo tunataka kuchukua Muda kujifunza kwa undani kutoka katika kifungu hicho hapo juu cha maandiko, Ni muhimu kufahamu kuwa watu wengi sana wanapenda sana Mungu awabariki na kuwafanyia mambo mazuri, huku wanasahau kuwa Mungu naye anahitaji mambo Fulani ya muhimu kutoka kwetu ili atubariki na kutimiza ahadi zake na makusudi yake kwetu. “Kama tukimpa Mungu yale anayoyahitaji kwetu, Mungu atatupa lolote tulitakalo kwake” alisema Muhubiri Mkubwa mwenye asili ya Afrika TD Jakes.

Katika kifungu hiki cha maandiko wote tunakumbuka Vizuri Habari ya Yusufu, tunakumbuka wazi jinsi Yakobo alivyompenda sana Yusufu, tunakumbuka jinsi ndugu zake walivyomchukia na kumtendea mabaya, tunakumbuka uchungu aliokuwa nao Yakobo kwa kumpoteza Yusufu, aliomboleza maombolezo makubwa sana kumpoteza Yusufu, na sasa upendo wake mkubwa umeelekezwa kwa Benjamin, ambaye Yakobo alimtoa kwa shida sana akihofia kuumia moyo kama alivyompoteza Yusufu aliogopa sasa asimpoteze Benjamin.Wakati umefika sasa Yusufu aliyetunzwa na Mungu huko Misri kwa muujiza mkubwa sasa anataka kujifunua kwa ndugu zake amekwisha kuwahoji mengi na kuwajaribu kwa namna nyingi sasa anataka kujifunua kwao, lakini anataka kujua Je Ndugu zake wamebadilika? Atajuaje sasa anatumia Kikombe cha Fedha kupambanua mabadiliko yao huu ndio mpango wake kupitia kikombe hiki je kikombe hiki kilihusu nini?

1.      Mpango wa siri wa kutafuta uhakika  
·        Yusufu na Ndugu zake walikuwa na wakati mzuri wa kufurahi pamoja Mwanzo 43:31-34 Ndugu zake bado hawajamfahamu kuwa ni Yusufu, lakini yeye amekwisha kuwajua na kupata uhakika, anawajua vilivyo kuliko wao wanavyo mjua, Mfano walipokuwa wakila aliwapanga kwa kufuata umri wao kuanzia mkubwa hata mdogo, Mwanzo 43:33, Benjamini alikuwa amependelewa kwa chakula kingi mara tano zaidi ya nduguze Mwanzo 43:34.

·        Siku ya pili baada ya karamu kila mmoja akiwa na furaha na uhakika kuwa wamemthibitishia waziri mkuu wa Misri kuwa wao sio wapelelezi, na kuwa wamefanikiwa kumuokoa Ndugu yao Simeon ambaye alikuwa amefungwa kwa muda na kuwa wanarudi nyumbani wakiwa na Benjamin ambaye Yuda alimuapia baba yake kuwa atahakikisha anamrudisha mtoto Mwanzo 43:3-10.

·        Sasa wanarejea nyumbani asubuhi mizigo ikiwa juu ya punda zao na mbegu na chakula, hawana mashaka wamejawa na furaha  wanafikiri kufika nyumbani na kuungana na familia zao na watoto wao, wanafurahia mafanikio yao nay a safari yao, Lakini hawakuwa wanajua kuwa Mungu yuko nyumba ya mambo anataka kuwakutanisha na dhambi yao waliyoifanya miaka 22 takribani iliyopita

·        Wakati wanajiandaa kuondoka Yusufu anamtuma mtumishi wake kuwaandalia nafaka na kuwapatia kadiri wawezavyo kubeba, alimwambia pia awarudishie na fedha zao walizolipa kwa nafaka, lakini Yusufu alimwambia Mtumishi wake afanye jambo geni zaidi, kuweka kikombe chake cha fedha katika mzigo wa Benjamin mdogo wake wa kunyonya hayo yalifanyika wakiwa bado hawajaondoka

·        Baada ya kuwa wamefika mbali Yusufu anamtuma mtumishi wake kuwakabili na kuwahoji kwa nini wamelipa Mabaya kwa mema? Wao walikuwa na uhakika kuhusu haki yao, walikuwa na uhakika kuwa hawakuwa wezi kwa vile walirejesha fedha zote ambazo waliwekewa mwanzoni na hivyo hawakuwa na sababu ya kuiba kikombe cha Yusufu cha fedha na hatimaye kwa kujiamini waliapa kuwa  swa atakayekutwa na kikombe chako cha fedha na afe! Na sisi tutakuwa watumwa wa wamisiri

·        Hili lilikuwa jambo geni sana kufanywa na Yusufu Mungu alikuwa anamtumia Yusufu kuwarejesha ndugu zake katika toba ya kweli, wao walikuwa wamemtenda mabaya Yusufu lakini Yusufu alikuwa anawalipa Mema, Ni lazima tukumbuke kuwa katika maisha haya hakuna jambo linalotokea kwa bahati mbaya kila jambo linalotokea katika maisha yetu ni mpango kamili wa Mungu nyuma yake Warumi 8:28Nasi twajua yakuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema wale walioitwa kwa kusudi lake” Mungu hufanya kazi kwa kusudi la kutuleta katika mapenzi yake njia zake ziko juu sana Isaya 55:8-9Maana mawazo yangu si mawazo yenu wala njia zenu si njia zangu asema Bwana kwa maana kama vile mbigu zilivyo juu sana kuliko nchi kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu na mawazo yangu kuliko mawazo yenu” Jambo hili Mungu hulifanya pia anapojihusisha na tabia zetu mbaya anapotaka kutubadilisha na kutuleta katika toba

·        Uko wakati ambapo tunaweza kujisahau katika maisha yetu na tukaendelea kuishi maisha ya dhambi na tukaona Mungu yuko kimya kama hashughuliki namaisha yetu wala hajatughadhabikia wala kutuonya tukaendeleza tabia Fulani kama kawaida na tukaona Baraka zake huku akitufanikisha na kukutana na mahitaji yetu, akitutumia na watu wakibarikiwa na kila huduma tuifanyayo, Ukweli unabaki kuwa Mungu anajua ni namna gani atatuagua atatutibu tatizo letu anajua namna anavyoweza kukutana na kuzungumza na mioyo yetu, na hapo ndipo hufikia wakati nanabana kifungi Fulani maalumu kutunyenyekesha na kutuleta katika toba

·        Kikombe cha uaguzi cha Yusufu kilikuwa ni kibano cha dakika za mwisho cha kuwapima wana wa Israel kama wametubu, wamebadilika, wanampenda baba yao ambaye walikuwa wamemdanganya kuhusu Yusufu, walikuwa wanampenda Benjamin ambaye sasa anapendwa na baba yao zaidi baada ya Yusufu, wanampenda Benjamini ambaye ni mtoto wa raheli kama Yusufu, wanawajibika kiasi gani kwa familia zao, ndugu na baba yao.

·        Mungu anajua namna ya kutuleta katika ukamilifu, anajua namna ya kupima mioyo yetu kujua tumekuwa kiasi gani na kubadilika kiasi gani, na ili atupate anajua ni wapi akuweke katika kibano ambacho kitakuleta katika toba na badiliko la kweli, ni Mungu anayejua namna ya kuweka kikombe chake cha uaguzi katika gunia lako.

·        Hatuwezi kumficha Mungu maisha yetu kwa muamini au mkristo anayejua wajibu wake na mwenye kufikiri sawa sawa ni lazima akubali kutubu haraka Mithali 28:13 afichaye dhambi zake hatafanikiwa, bali aziungamayena kuziacha atapata rehema, Tukiziungama dhambi zetu yeye ni mwaminifu na wa haki anatusamehe 1Yohana 1:9, tukikataa toba na kubadilika gharama itakuwa kubwa kuliko tunavyoweza kufikiri, Waebrania 12:6-11 Mithali 13:15

·        Mungu alikuwa anatafuta uhakika wa mabadiliko katika maisha ya wana wa Israel, alitaka waonyeshe kuwa wamebadilika toba sio maneno ni vitendo ni mabadiliko makubwa katika maisha yetu, kama hatubadiliki kila wakati tutajikuta katika marudio ya mitihani ileile katika nmaisha yetu.

2.      Mpango wa Mungu wa kuwakabili
·        Magunia yalifunguliwa wana wa Israel walikuwa na uhakika hawana hatia wanasimama wakijiamini na wakiwa na nyuso za furaha kila mmoja anasaidia kufungua gunia lake  kwa ujasiri na sasa wanafika gunia la Benjamin hali inabadilika wanakuta kikombe cha fedha cha Yusufu katika namna isiyoweza kuaminika walipigwa na Butwaa!!!

·        Huu ni wakati wa majuto na ukweli sasa ni kipimo cha mwisho cha Yusufu kwa ndugu zake wakati woote Yusufu alikuwa anawajaribu ili kuona je kuna mabadiliko?
-         Walimleta Benjamin kama alivyowaagiza Mwanzo 43:15-16
-         Walirejea kwaajili ya kaka yao Simeon Mwanzo 43:23
-    Walirejesha Fedha yoote waliyokuwa wamezidishiwa na kurejeshewa katika magunia yao Mwazno 43:20-22

·        Haya yote yalikuwa ni majaribio, ni mkiaka karibu 22 imepita walimchukia Yusufu sana walimshambulia walimtupa katika shimo, walimuuza utumwani, walimuhuzunisha baba yao walimvinja moyo, walimuambia uongo kuhusu kilichomtokea Yusufu, walifanya msiba pamoja naye kama kwamba amekufa walipatana kwa nia moja kunyamaza kimya siku zote, walikaa na uongo huo kwa muda wote huo, sasa wangekuwa na nafasi nyingine ya kufurahia kifo cha mwana mwingine wa Raheli, Kwa vile sasa ni wazi kuwa Benjamin anapendwa sana na baba yao kama alivyopendwa Yusufu Mwanzo 42:36, 43:13-14, labda wakati huu wangeruhusu Benjamin kupatwa na mabaya kama ilivyokuwa kwa Yusufu, wangejirudia tu nyumbani, wangeuumiza tena moyo wa baba yao ambaye amevumilia maumivu ya kupotelewa na mwanae kwa miaka yote hiyo bila kujielewa Yusufu alikuwa anapata picha kuwa Ndugu zake wamebadilika sana wamekuwa watu wengine sasa wako tayari hata kufa hata kuwa watumwa ndugu zao na baba yao awe na furaha 

·        Hawakutaka hata kumuuliza Benjamin kikombe kimefikaje kwako, hawakutaka hayt kumkemea kwanini umechukua kikombe cha watu, walikuwa tayari kubeba mzigo wa Benjamin hata ikiwezekana kufa ili kuokoa maisha yake na baba yao, wako tayari kubeba hukumu bila kujali Benjamin alifanya nini, wameacha ubinafsi, wameacha uongo, wameacha kupenda fedha, wanalia kwa huzuni, hawamlaumu yoyote wakati huu

·        Huu ndio wakati ambao Mungu anausubiri kwa kila mmoja wetu, kuwa tayari kufanya mambo sahihi na kwa njia sahii, wana wa Israel wamekomaa sasa hawahukumu wengine, hawahukumiani tena, hawachekani, wako tayari kubeba tatizo lao kama la mtu mmoja, wako tayari kuwa wakeli hata kama ukweli utawagharimu

·        Ndugu yangu mpendwa Mungu anakusubiri ufikie wakati ambapo huwezi kumtupia mwingine lawama, wala kumsingizia mwingine tatizo kwa kushindwa kwetu kuwajibika, anataka tufikie wakati ambapo tutakuwa tayari kukabiliana na dhambi zetu wenyewe na kuzikiri na kuzitubu na kuziacha na kubadilika.

·        Mungu anatutaka tufikie wakati ambapo hatutanyoosha vidole kwa wengine, dhambi zetu sio za wazazi wetu, wala wake zetu, wala waume zetu, hakuna wa kulaumiwa Mungu anatusubiri tufikie ngazi hii ya kujitambua ndipo anapoweza kujifunua kwetu, Mungu anataka tufikie ngazi ya kuweza kuwa wakweli hata kama kweli hiyo itatugharimu

·        Mungu haogopi kuifunua dhambi yetu wazi kwetu ili kwamba tuweze kufikia toba, Mungu anapotutaka tumgeukie atatumia kila analoliweza kuhakikisha kuwa anarudisha uhusiano wetu nayeye, Ndugu zanhgu Dhambi si ya kucheza nayo, sio ya kuirudiarudia ni lazima itubiwe mara moja, kwa ukamilifu na uaminifu, hapo ndipo Mungu anapoweza kutusamehe, kutubariki, kujifunua kwetu na kuonyesha nguvu zake

3.      Mpango wa Mungu kuwarejesha katika toba
·        Sasa wana wa Israel wanarejea ikulu kwa Yusufu hapo hajajifunua kwao bado, Yusufu alikuwa anasubiri sasa kujifunua kwao, anataka kuona mabadiliko, je atamuona Benjamin peke yake? Maana ndiye aliyewekewa kikombe cha uaguzi, njia hii ilikuwa ni ya kumlinda Benjamin kutoka kwa ndugu zake kama wanekuwa hawana mabadiliko.

·        Walipotokea wote walimsujudia hata chini wakiitimiza ile ndoto ya Yusufu alipokuwa kijana Mwanzo 37:5-11, Yusufu anawauliza kuhusu kikombe chake cha fedha, na anawaambie hamkujua ya kuwa naweza kufanya Uaguzi?

·        Ni muhimu kufahamu kuwa Yusufu hakuwa muaguzi wala hakufanya uaguzi kabisa, lakini uaguzi na ramli lilikuwa ni jambo la kawaida la wamisri na waaguzi walitumia kikombe cha Fedha na kukiweka divai na shanga za thamani na walitumia kusoma maisha ya watu, Yusufu hakufanya uaguzi huo lakini hapa alikuwa anawajua ndugu zake vilivyo, alifahamu sana matendo yao mabaya na tabia zao zilizokuwa za kutomkumjali Mungu, alitaka kujua kuwa Baba yake sasa amewafunza neno la Mungu na kuwa huenda je sasa wamebadilika au bado baba hana watu hapo ? Kitendo cha Yusufu kutambua kila kilichokuwa kinaendelea na wao kutokutambua, kitendo cha wao kuonyesha badiliko kubwa hata wakiwa mbali ambako watu hawawaoni kilionyesha uaminifu ulio wazi kuwa ni kweli wamebadilika je ni wangapi wanaweza kufanya uovu hata wakiwa katika miji au nchi ngeni ambako huko hakuna anayewajua? Yusufu alikuwa akifanya kile ambacho Mungu alikuwa anamuongoza kuwaleta nduguze katika ukamilifu wake

·        Yuda alikuwa wakwanza kujitokeza mbele na kuzungumza maneno ya muhimu sana katika neno la Mungu ni maneno yanayoonyesha kuwa ni moja ya watu waliobadilika sana
·        Alikiri wazi kuwa wamefanya dhambi alisema Mungu ameona uovu wao, alisema sisi sote nay eye aliyekutwa na kikombe chako ni watumwa wako, alitambua kuwa Mungu alikuwa akiwahukumu kwaajili ya dhambi, kitendo cha kuwa Mwenye kikombe anataka aliyekutwa na kikombe awe mtumwa wake, kilimkumbusha wazi kuwa ni ile dhambi ya kumuuza ndugu yao utumwani Misri sasa kimewageukia, alikubali kuwa yeye na ndugu zake wote ni watumwa tu Mwanzo 45:16
·        Yusufu alikataa wao kuwa watumwa wake aliwataka wote kuendelea na safari isipokuwa yeye aliyekutwa na kikombe chake cha uaguzi tu Mwanzo 45:17
·        Mwanzo 45”18-34 Ni maandiko yenye maneno mazito ya Yuda, alimkubusha Yusufu kuwa sababu ya kuja na Benjamin ilikuwa ni kwa vile yeye alikuwa amewaagiza 19-23 Yuda alimueleza Yusufu kuwa Baba yao Yakobo angekufa tu kama Benjamin atapatwa na mabaya ndiye mwanaye mdogo naye anampenda 24-31, kisha Yuda alisema yeye yuko tayari kuchukua nafasi ya Benjamin, alikuwa tayari kubaki Misri kama Mtumwa ili kwamba Benjamin aweze kurudi kanaani na ndugu zake 32-34, Moyo wa Yuda unakuwa kama wa yesu Kristo yuko tayari sasa kubeba adhabu ili ndugu zake na baba yake wawe na amani na furaha
·        Huu ulikuwa ni kama wakati muafaka ambao Yusufu alikuwa akiutazamia alithibitisha wazi kuwa wamebadilika sana
·        Wako na umoja kama mtu mmoja, wako tayari wameiva Yuda yuko tayari kuchukua nafasi ya Benjamin na kumpendezesha baba yake, hapa ndipo mambo yalipobadilika Ukiri wa Yuda ulionyesha wazi kuwa amebeba majukumu makubwa ya kuwajibika kwaajili ya familia yake hakuna ubinafsi ndani yake yuko tayari kupoteza kila kitu, kumbuka alikuwa na watoto na mke na mali zake lakini alikubali kubaki Misri kama mtumwa ndugu yake awe huru, aidha amefanya dhambi au hakufanya, na aliweza kuwaza moyo wa baba yake, kutokana na hali hii Yusufu alishindwa kujizuia na alijifunua kwa Ndugu zake Mwanzo 45:1-4

·        Kwa ujumla kuna jambo la kujifunza kutoka kwa Yuda ni wazi kuwa dhambi yoyote ile ni matokeo ya ubinafsi na choyo na umimi, kadiri mtu anavyokuwa mbinafsi ndivyo na dhambi yake ilivyo, dhambi yoyote inayotendwa na wanadamu ni matokeo ya ubinafsi na kujihurumia, toba halisi inaonekana pale tunapoanza kujali wengine na kuweza kukubali kuwa tayari hata kujidhabihu kwaajili yaw engine kumbuka siku zote asili ya dhambi zote ni ubinafsi Isaya 14:12-15, 1Yohana 2:16

·        Tunapofanya dhambi huwa hatuko tayari kujali madhara yake tunajitoa kikamilifu kuasi kwa sababu ya ubinafsi, tunaweza wakati mwingine kutubu au kuogopa dhambi au kunyenyekea kwa sababu ya kuogopa aibu au kushikwa tu, Mkristo aliyekomaa anaiangalia dhambi kwa mtazamo zaidi ya huo, kuwa ina madhara kwa jamii, kanisa na familia nay eye mwenyewe na kazi ya mungu pia njia pekee ya kuikabili dhambi na kukubali kulipa gharama na kuwa wakweli kwa Mungu na nafsi zetu hata kama itatugharimu hivi ndivyo Yuda alivyofanya

·        Watu wengi wanataka Baraka za Mungu na Mungu amekuwa mvumilivu kwetu kwa miaka mingi, inawezekana unawacheka hata wale waliotengwa makanisani kwa kubainika kuwa ni wenye dhambi lakini wewe una za kwako haijawahi kuonekana lakini kiko kikombe cha uuguzi cha bwana kiko katika gunia lako atakubana tu ni vema sasa ukabadilika na kuacha dhambi na kuwa tayari kwa gharama yoyoye kuwa mbali na Ubinafsi na Yesu atajifunua kwako na kukupa memma ya nchi na kukuhifahdi na kukualika katika furaha yake, Yuda alitambua kuwa hawakuwa wamemfanyi Yusufu mabaya walijua kuwa wamemkosea Mungu, ni muhimu kwako kujitathimini yale unayowafanyia wengine kuwa unamkosea Mungu.
·        Je unakua kiriho?
·        Je una dhambi unapaswa kuitubu?
·     Je unaogopa hukumu ya Mungu (kikombe cha Fedha cha uaguzi) Badilika leo na Bwana takaubariki sana na kukustawisha sana.

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni