Jumamosi, 10 Desemba 2016

Mungu wa Faraja yote. (God of all Comfort).



Andiko: 2Wakoritho 1: 3-7

3. Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote

Utangulizi:

Neno Mungu wa faraja yote linalojitokeza hapa na sehemu nyingine katika agano jipya limetokana na neno la asili la kiyunani “Paraklesis” ambalo maana yake ni wakili au mtetezi au mtu anayesimama karibu na mtuhumiwa ili kumtetea na kumsaidia,Neno hili limetumiwa mara nyingi sana na Paulo mtume katika nyaraka zake, na Mwandishi Luka na baadhi ya waandishi n wengine wa nyaraka na katika waraka wa Waebrania, ambapo neno hilo hujitokeza Mara 12 au kwa maneno yanayofanana na hilo mara 28

Neno hili ni la muhimu sana kwa wakristo wanaopitia magumu na mapito ya aina mbalimbali lakini zaidi sana mapito a taabu zinazotokana na kazi ya injili, ni muhimu sana kufahamu kuwa maisha ya ukristo yanajumuisha pamoja na kuteseka kwaajili ya Kristo biblia inasema tumeitwa si kumwamini tu bali kuteseka pamoja na Kristo, lakini hata pamoja na mateso hayo wakati huu Mungu hujihusisha kwa namna ya kipekee katika kufariji na hiki ndicho Paulo anakikazia katika kifungu hiki tunachojifunza leo.



Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia maswala ya msingi yafuatayo:-

·         Ahimidiwe Mungu. Mstari 3
·         Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo Mstari 3
·         Baba wa Rehema Mstari wa 3
·         Mungu wa Faraja yote Mstari wa 3

Ahimidiwe Mungu.

Neno Ahimidiwe Mungu katika Biblia ya kiingereza ya NIV linasomeka “Praise be to the God” na Biblia ya kiingereza ya KJV ambaoyo ndiyo iliyotumika kutafasiri Biblia ya Kiswahili ya Union Version linasomeka katika lugha hiyohiyo ambayo Kiswahili chake kingesomeka “Abarikiwe Mungu” Hata hivyo Biblia ya kilatili Vulgate inatumia neno “Benedictus” ambalo kiingereza chake lingesomeka “Heartfelt thanks be to the God” ambalo lingesomeka kwa Kiswahili rahisi  Atukukuzwe au Ashukuriwe sana Mungu, unaweza kuona vema katika Waefeso 1:3 “Atukuzwe Mungu

Salamu hizi kwa ujumla zinafunua moyo wa Paulo mtume ambaye alikuwa amejawa na wingi wa shukurani, na hivyo anaonyesha kufurahi na kushukuru kwa kiwango cha juu sana kwa Mungu, kwa nini Paulo anajawa na wingi wa shukurani kiasi hiki kwa Mungu? Paulo alikuwa ni mtu mwenye mzigo na kazi ya Mungu, alikuwa ni mtume mwenye moyo wa kichungaji, alikuwa na mambo mengi sana ya kuwaonya na kuwafundisha wakoritho hasa baada ya kanisa kumuandikia na kumsimulia yale waliokuwa wakiyapitia wakati akiwa hayupo, na aliwajibu kwa kuandika waraka wa Wakoritho ule wa kwanza sasa anapata taarifa kuwa Kanisa la Koritho sasa linaendelea vizuri, Paulo mtume alikuwa amekemea mambo mengi katika waraka wake wa kwanza ambao ulileta huzuni na toba kwa kanisa la Koritho na waliweza kufanya marekebisho mengi, sasa Paulo amesikia taarifa kuwa Kanisa linaendelea vema na sasa anafarijika na kufurahi sana kutokana na maendeleo mazuri ya Kanisa la Koritho, habari za maendeleo mazuri Paulo alizipata kutoka kwa Tito aliyekuwa akisimamia makanisa ya Akaya au Macedonia 2Wakoritho 7:8-10,12-16, Ni kwasababu hii Paulo mtume anamtukuza Mungu, anafurahi anamhimidi Mungu, ni kama mtu uliyekuwa na mgonjwa kisha ukapewa taarifa kuwa mgojwa huyo sasa anaendelea vema, au ameruhusiwa, kila mchungaji mwenye mapenzi ya kweli na kanisa hawezi kufurahi kanisa linapoharibika, hafurahii watu wakienenda katika njia isiyopasa, lakini watu wanapoendelea vizuri kunakuwa na furaha kubwa sana hali kadhalika walimu watafurahi kusikia wanafunzi wao wanaendelea vizuri wanafanya vizuri, madaktari na manesi hawafurahii kuona wagonjwa wakipoteza maisha wanapenda kuona wagonjwa wanapona

Huu ndio ulikuwa moyo wa Paulo Mtume anafurahi, anamtukuza Mungu anamhimidi bwana Mungu anamsifu anaonyesha moyo wa kufurahi, mambo yanapokwenda vema, kila mmoja anapaswa kufurahia mabadiliko mema ya kila mmoja wetu katika kumpenda Mungu, hatutarajii watu watasababisha huzuni, kila mmoja ataonyesha ukomavu, maendeleo katika kila Nyanja ni jambo hilo linaleta faraja kubwa sana, hakuna mama anayefurahia kuwa na mtoto asiyekua, lakini kila mtoto anapopiga hatua kina mama hushangilia sana anakaa, anatambaa, anaota meno, anasimama, anatembea anazungumza na hatua nyinginezo zote huleta faraja kubwa sana kwa kina mama wanaofanya malezi ya watoto.

Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo Mstari 3

Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo – Mahali hapa Paulo anamtaja Mungu lakini anaunganisha Mungu Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, kwa nini ? sababu kubwa ni kuwa hakuna mtu anaweza kuunganishwa na rehema za Mungu baba pasipokuweko kwa Yesu Kristo, Ni muhimu kufahamu kuwa watu wengi sana duniani hata wapagani wanafahamu sana Mungu kama Baba wa rehema lakini tatizo kubwa ni kuwa hawa wanataka kwa vinywa vyao tu hawajui kuwa rehema hizi za Mungu zimepitia kwa Yesu Kristo, ni kwa mateso ya yesu Kristo tu, ni kwa kusulubiwa kwake tu ni kwa kuiamini kazi aliyoifanya Yesu Kristo tu ndipo watu wanaweza kufaidika na rehema za Mungu baba  na upendo wake hakuna njia nyingine, Upendo wa Mungu umeunganishwa kwa mwana wake wa pekee Yesu Kristo na hakuna namna nyingine, kama tunapitia mateso katka imani yetu ni kupitiamateso ya Kristo 2Wakoritho 1:5 kama tunafarijika faraja hiyo ni kwaajili ya Yesu Kristo tu, Pasipo Kristo hatuwezi kufanya neno lolote. Shukurani anazozitoa Mtume Paulo kwa Mungu baba pia zinaunganishwa na Yesu Kristo yeye pekee ndio kipatanisho cha kweli kati ya Mungu na wanadamu

Baba wa Rehema Mstari wa 3

Baba wa Rehema – Ni muhimu kufahamu kuwa Paulo mtume alikuwa Mwebrania na ingawa aliandika waraka huu kiyunani, ni wazi kuwa alikuwa anawaza kiebrania, katika tamaduni za Kiibrania neno Baba lilitumika pia kumaanisha MWANZILISHI au chanzo kwa msingi huo linapotumika hapa linamaanisha Rehema zinatoka kwa Mungu, asili yake ni kutoa Rehema  na ndiye mwenye kuitunza rehema, 

Rehema ni sifa kuu ya Mungu, Ndani ya rehema kuna huruma, neema uvumilivu usioelezeka tunaita Mungu wa Rehema na neema , mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli Zaburi 86: 15 na ni kupitia sifa hizo ndio Mungu husaidia na kufariji, Vitabu vya tamaduni za kiyahudi Talmud vinaeleza kuwa ndiye yeye huanza kwa rehema na kumaliza kwa rehema, kila sura ya Quran isipokuwa moja tu zinaanza kwa kusema Mungu ni mwingi wa Rehema, hii ilikuwa ni salamu ya kawaida kwa waru wa mashariki ya kati kuhusu tabia ya Mungu kwa kiibrania “RACHAMIM” likimaanisha huruma au rehema Warumi 12:1 ni kutokana na tamaduni hizi na sifa hii ya kweli ya Mungu ilikuwa ni utaratibu wa kawaida kwa nyakati za kanisa la kwanza kumtaja Mungu kama Baba wa rehema

Mungu wa Faraja yote Mstari wa 3

Neno hili Mungu wa faraja yote ndio nenola Muhumu sana key word dhidi ya maneno yote katika kifungu hiki ni wazi kuwa kutoka mstari wa 3-7 neno faraja limetajwa mara kumi likiunganishwa na neno Mateso mara nne hivi au dhiki 

Mahali hapa panatupa matumaini yalkiyo wazi kuwa katika dhiki ya aina yoyote na mateso ya aina yoyote kamwe Mungu hawezi kutuacha wala kujitenga na upendo wake, Paulo ameona katika uzoefu wake kuwa wakati wote walipopita katika magumu Mungu alikuwa ni faraja , kwa msingi huo Mungu anafaraja yote, Mungu anaweza kuruhusu sisi kupita katika mateso na dhiki ili tuweze kuwafunza wenzetu jinsi Mungu alivyo mwema tuwe na ujasiri wa kuwashuhudia wengine upendo na neema ya Mungu, 

Mungu singeliweka faraja zake tungelikata tamaa, Dunia ni ngumu lakini kwaajili ya faraja zake tumejifunza kuvumilia kwa kuwa na tumaini Mungu anatufariji kwa Roho wake Mtakatifu, Paulo anaiona faraja nyingine kuwa ni kuendelea mbele na kukua wa kanisa la Koritho ambalo alilitaabikia, likaingiliwa na waalimu wa uongo, likaonyesha dalili mbaya akakemea ingawa alitumia waraka wake wa kwanza sasa wanaendelea vizuri, wanakua kiroho kwa kasi, kwa Paulo mtume hii ni aina ya faraja, Mungu anatufariji kwa viwango vikubwa anajua kutufariji katika kila aina ya dhiki na mateso, kila aina ya pito lisilo jema unalolipitia kumbuka kuwa Yuko Mungu wa faraka yote

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi.

Maoni 1 :