Jumapili, 4 Desemba 2016

Mungu wa Kisasi Uangaze!



Andiko : Zaburi 94:1-3

“1. Ee Bwana, Mungu wa kisasi, Mungu wa kisasi, uangaze, 2. Mwenye kuihukumu nchi, ujitukuze, Uwape wenye kiburi stahili zao. 3. Bwana, hata lini wasio haki, Hata lini wasio haki watashangilia?



Utangulizi:

Je wewe umewahi kuona watu wakidhulumiwa? Umewahi kuona mahali haki haitendeki? Je hujawahi hata kusikia mahali watu wakionewa, wakiteswa, wajane na yatima na hata wageni au wakimbizi na wanyonge wakikandamizwa na kuonelewa huku wale wanaofanya dhuluma wakishangilia na kufurahi? Na hata wakidharau kuweko kwa Mungu na utetezi wake?

Jambo hili ndio hali halisi katika zaburi hii iliyoandikwa na Daudi, Hatuwezi kujua kuwa Daudi wakati huu alikuwa ameshuhudia nini katika mazingira yake, lakini kile anachokizungumza na kukililia katika zaburi hii kinafunua wazi aidha jambo ambalo amelishuhudia katika uzoefu wake wa maisha ama limewahi kumkuta, vyovyote vile iwavyo maswala haya yanaikumba hata jamii inayotuzunguka leo na Biblia hapa kupitia kinywa cha Mfalme Daudi ambaye pia Roho wa Kinabii alikaa ndani yake kuna mswala kadhaa muhimu ya kujifunza ambayo tutajifunza katika vipengele vifuatavyo:-

·         Kumuita Bwana kwaajili ya Haki (Zaburi ya 94:1-4)
·         Kushitaki kile wanachikifanya wadhalimu (Zaburi 94:5-7)
·         Kushangazwa na ujinga wa wadhalimu (Zaburi 94:8-11)
·         Baraka za kupitia katika magumu (Zaburi 94:12-13, 14-15)
·         Hatima ya kucheza na mwenye haki (Zaburi 94:16-23)

Kumuita Bwana kwaajili ya Haki (Zaburi ya 94:1-4)

Daudi anaiimba Zaburi hii katika mtazamo wa watu wanaoonewa, wanoteswa na kudhulumiwa na kutokutendewa haki watu hao wakimuangalia Mungu kama Jaji mkuu mwenye uwezo wa kutoa hukumu ya mwisho, wakati wengine wote wameshindwa kutoa msaada, Daudi anamuonyesha Mungu kuwa ndio mahakama ya juu zaidi tunayoweza kukata rufaa na tena mahakama hii ya juu zaidi inauwezo wa kutulipia Kisasi, Daudi anamtaka Mungu huyu mwenye uwezo wa kulipiza kisasi dhidi ya maadui zetu  aangaze, yaani aangalie kila kinachofanyika na kutoa haki

Wewe na mimi tumewahi kushuhudia kile ambacho Daudi alikishuhudia na kukililia katika Zaburi hii, inawezekana umewahi kushuhudia mume akifariki na kuacha mjane na yatima na Ndugu wa Mume wakiingilia kati na kudhulumu mali za yatima na kumuacha mjane huyo akiwa mikono mitupu wakiishi maisha ya dhiki, tumewahi kushuhudia wanawake wakorofi wakipora mali za waume zao na kujimilikisha, ndugu jamaa na hata watoto wakigombea hati za viwanja, kadi za magari, watu wakichongeana makazini na kusababisha wenngine wafukuzwe kazi, na kushangilia mafanikio ya anguko la mwingine, watu wakichafuana kwa faida na maslahi yao wenyewe na hila za aina nyingi zikifanyika duniani zinazofanana na hayo

Biblia inatufundisha kuwa endapo tumezulumiwa kila tunachokistahili na hakuna wa kututetea pako mahali ambapo tunaweza kudai haki zetu, Yesu alifundisha kwa msisitizo kuhusu madai ya haki zetu kwa Jaji mkuu wa majaji wote duniani, Mfalme wa wafalme mwenye uwezo sio tu wa kutoa haki bali pia kulipiza kisasi kwa watakaotudhulumu 

Luka 18: 1-81. Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. 2. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. 3. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. 4. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, 5. lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. 6. Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. 7. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? 8. Nawaambia, atawapatia haki upesi;”

Daudi anamuomba Mungu haki iweze kupatikana, Yesu anatufundisha kuendelea Kumuomba Mungu mpaka haki yetu iweze kupatikana Yeye ni Jaji mkuu, ni Hakimu wa Dunia nzima, tunaweza kuimuendea yeye kwa ujasiri atupatie haki yetu, hatuhitaji kulalamika Yuko Mungu wa kisasi mwenye kuihukumu inchi na kuwapa stahili zao wenye kiburi, Yeye atawahukumu watu wote na pia ndiye mwenye kulipiza kisasi kwa wadhalimu na ndiye anayeteua majaji Warumi 13:4

Biblia inatufundisha kuwa tunapodhulumiwa tumuombe Mungu na kumsihi aangazie kile kinachoendelea, Hatupaswi kutumia njia yoyote ile yenye kutaka kujilipia kisasi wenyewe ni muhimu kumuachia Mungu yeye ndiye atakayetulipia kisasi.

 Warumi 12:19Wapenzi, Msijilipizie kisasi, Bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa Kisasi ni juu yangu mimi nitalipa anena Bwana

Kushitaki kile wanachikifanya wadhalimu (Zaburi 94:5-7)

Daudi mwandishi wa Zaburi anaendelea kumwambia Mungu kilie wanachokifanya wadhalimu, wote tunajua kuwa Mungu anafahamu kila kinachoendelea lakini Daudi anataka kufafanua, kuchamganua kile ambacho ameona kinaendelea na anataka Mungu akiangazie 

5. Ee Bwana, wanawaseta watu wako; Wanautesa urithi wako; 6. Wanamwua mjane na mgeni; Wanawafisha yatima. 7. Nao husema, Bwana haoni; Mungu wa Yakobo hafikiri.”

Daudi anaelezea jinsi sifa ya wadhalimu hao walivyo, hawana huruma, wana kiburi na wanazungumza kwa kejeli na kiburi cha hali ya juu, hawajali hata kile wanachokizungumza, wanazungumza vibaya na wengine, sio watu wa dini wala hawamjali Mungu, wanajiamini wanajitegemea, wanavunja watu mioyo, wanagawa watu, wanawaua watu,hawajali huyu mjana wala yatima, wanajisemesha kuwa nani atatwatetea nani atawaokoa na uwezo walio nao ni makatili, hawajali wageni wala wakimbizi, Daudi aliwasoma vema maadui hawa na kuwaona jinsi walivyo wabaya na wakatili na alieleza Moyo wake kwa Mungu kuwahusu, wako watu Duniani ni wabaya na hawana haya unaweza kujiuliza ni roho ya namna gani waliyonayo na usipate majibu kwamba wanaongozwa na ibilisi au vipi wakati mwingine unaweza kuona ukatiliwao unazidi hata ule wa ibilisi mwenyewe Mungu atulinde na watu wa aina hii 

Kushangazwa na ujinga wa wadhalimu (Zaburi 94:8-11)

8. Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? 9. Aliyelitia sikio mahali pake asisikie? Aliyelifanya jicho asione?         10. Awaadibuye mataifa asikemee? Amfundishaye mwanadamu asijue? 11.  Bwana anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili.”

Daudi anashangwazwa na jinsi wadhalumu hao walivyojawa na roho ya udanganyifu wanafanya uovu mkubwa kwa kujiamini kiasi cha kupofuka macho na kuwa wajinga na wasiofikiri wala kuwa na akili Daudi anauzoefu kuwa Mungu Jaji mkuu atafanya kitu haiwezekani Yeye aliyemuumba mwanadamu awe na sikio kisha yeye mwenyewe asisikie, Yeye aliyemuumba mwanadamu kuwa na jicho kisha asiione yanayotendeka, yeye anayeshikisha watu adabu asikemee udhalimu unaoendelea, yeye anayewafundisha wanadamu sheria na jinsi iwapaswavyo kuenenda asijue uharibifu unaoendelea, anahitimisha kuwa Mungu anayajua mawazo ya wanadamu na anatambua kuwa ni ya ubatili

Wako watu wameharibika mioyo kiasi cha kutokutambua kuwa yuko Mungu anayeona na kusikia, wako watu wanafanya uovu kana kwamba wao ndio Miungu na hakuna awaye yote aliye juu yao, Daudi anasema huu ni ujinga wa watu na unaweza kufanywa na watu wasiofikiri, tena anawaita wapumbavu na anajiuliza ni lini watakapopata akili

Baraka za kupitia katika magumu (Zaburi 94:12-13, 14-15)

12. Ee Bwana, heri mtu yule umwadibuye, Na kumfundisha kwa sheria yako; 13. Upate kumstarehesha siku za mabaya, Hata asiye haki atakapochimbiwa shimo.14. Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake, Wala hutauacha urithi wake, 15. Maana hukumu itairejea haki, Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata.

Daudi anatumia mistari hii kumuita heri mtu anayepitia katika majaribu kwake yeye kupitia katika hali ngumu ni kuadibishwa na Mungu ni kufundishwa sheria na kanuni za Mungu na kuwa hatima ya Mungu ni kuja kutupa starehe wakati wa mabaya na kuwa mwisho wa adui upon a tutawaona adui zetu wakizikwa wakichimbiwa shimo, Daudi aonyesha ya kuwa Mungu hatawatupa watu wake hawezi kutuacha maana kila anayemcha yeye ni urithi wake, ana uhakika kuwa Mungu atafanya hukumu atarejea  na haki itapatikana na waliowanyofu wa moyo watanufaika nayo

Dhuluma zinazoendelea Duniani hazitadumu, uko wakati Mungu atakomesha , atahukumu kwa haki na kuwasterehesha wote walioonewa na mwisho wa wabaya tutauona Ndugu yangu kama asemavyo Daudi na kama lisemavyo neno la Mungu Bwana hatawatupa watu wake hawezi kuuachia Urithi wake 

Hatima ya kucheza na mwenye haki (Zaburi 94:16-23)

16. Ni nani atakayesimama Kwa ajili yangu juu ya wabaya? Ni nani atakayenisaidia Juu yao wafanyao maovu? 17. Kama Bwana asingalikuwa msaada wangu, Nafsi yangu kwa upesi ingalikaa penye kimya. 18. Niliposema, Mguu wangu unateleza; Ee Bwana, fadhili zako zilinitegemeza. 19. Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu, Faraja zako zaifurahisha roho yangu. 20. Je! Kiti cha udhalimu kishirikiane nawe, Kitungacho madhara kwa njia ya sheria? 21. Huishambulia nafsi yake mwenye haki, Na kuihukumu damu isiyo na hatia. 22. Lakini Bwana amekuwa ngome kwangu, Na Mungu wangu mwamba wangu wa kukimbilia. 23. Naye atawarudishia uovu wao, Atawaangamiza katika ubaya wao, Naam, Bwana, Mungu wetu, atawaangamiza

Mwandishi wa zaburi anahitimisha kwa kuuliza swali nani atasimama kunitetea dhidi ya adui zangu? Na ni atanisaidia dhidi ya waovu au wadhalimu? Kisha anaonyesha kuwa Bwana ni Msaada na kama asingelikuwa msaada waovu waneipoteza nafsi yake, Lakini fadhili za Bwana ni njema na zilimtegemeza Mungu alifanyika faraja kubwa  pamoja na udhalimu wanaoufanya Mungu akikimbiliwa anakuwa mwamba na atawarudisha waovu hawezi kukaa nao kiti kimoja atawaangamiza katika ubaya wao na hakika atawaangamiza 

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu anaona kila aina ya uonevu unaoendelea katika ulimwengu, inatupasa kukata rufaa na kudai haki zetu kwa dua sala na maombi, Mungu atatutetea, ataingilia kati jambo kubwa la msingi ni kumwambia mlipiza kisasi aangaze Tumuombe Mungu wa kisasi aangaze amulike aangalkie aone atazame na kukemea kila aina ya ubaya , uovu  na udhalimu wa watu walioota sugu walioharibika mioyo wasiojali wanaodhulumu, wanaoibia watu wakidhani kuwa hakuna utetezi dhidi ya wanyonge Bwana ana aliangalie jambo hilo na kulikemea Katika Jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!

+255718990796

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni