Jumanne, 14 Machi 2017

Hazina katika vyombo vya Udongo.


Mstari wa Msingi: 2 Wakoritho 4:7Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu wala sio kutoka Kwetu


Utangulizi:-

Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kujitambua na kujifahamu kuwa tumeumbwa kwa njia ya jabu sana, na hivyo ni vema katika maisha yetu tukampa Mungu utukufu siku zote na kumshukuru yeye anayetuwezesha na kuyashikilia maisha yetu, Maandiko yanatufananisha sisi kwa Mungu kama viumbe dhaifu sana yaani tumeumbwa kwa udongo, sisis ni kama chombo cha udongo katika mikono ya Mungu na Mungu baba yetu ndiye mfinyanzi kwa maana hiyo imetupasa kuishi na kuendena kwa unyenyekevu mkubwa, vipawa na akili na karama Mungu alizowekeza ndani ya Mwanadamu ni hazina sio ya kujivunia bali ni kwaajili ya utukufu wa Mungu.



Vyombo vya Dongo:

2 Wakoritho 4:7Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu wala sio kutoka Kwetu” tunaweza kuutafasiri mstari huu katika lugha nyepesi ya mkuu wa wajenzi hivi “Lakini kuna vitu vya thamani kubwa sana vimewekwa katika vyombo vya dhaifu vya udongo, ili utukufu na sifa kuu iwe ya Mungu wala sio kutoka kwetu”

Kwa nini Paulo mtume anazungumza maneno mazito namna hii na je yana maana gani kwetu? Ni muhimukwanza tukawa na ufahamu wa kutosha kuhusu vyombo vya dongo, Vyombo vya udongo anavyozungumza Paulo Mtume ni vyombo vilivyotengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi na kuumbwa na mfinyanzi kwa ustadi kulingana na makusudi na matakwa ya mfinyanzi husika, Mara baada ya kufinywangwa vyombo hivyo vilichomwa kwa moto ili kuweza kuvifanya imara, baada ya hatua hiyo vingeweza kupakwa rangi na kuchorwa maua ya aina mbalimbali ya kupendeza na kuwa na muonekano mzuri sana

Nyakati za Biblia zamani sana vyombo vya udongo vilitumika kwa kusudi pia la kuhifadhi au kuficha hazina au vitu vyenye thamani sana, mfano halisi ni kuwa watu wa kale waliwahi kuhifadhi katika vyungu magombo ya chuo cha nabii isaya na vitabu vingine vya ngozi vilivyotumika zamani, Mfano halisi ni katika bonde la Qumran yaliwahi kuokotwa magombo ya ngozi yaliyokuwamo katika vyombo vya dongo vya kale, vijana wa kiislamu waliokuwa wakichunga Kondoo walikuwa wakirusha mawe huenda ni katika lengo la kutafuta kondoo, walisikia mlio Fulani wa chungu katika pango, walipofika kumbe ni chungu au mitungi iliyoundwa kwa dongo na ndani yake kulikuwa na ngozi zilizokuwa na maandishi, wao wakiwa hawajui maandishi hayo walitaka kuzitumia ngozi hizo kutengenezewa viatu, Mafundi waligundua kuwa yalikuwa ni maandiko matakatifu waliyapeleka kwa Kanisa na yakahifadhiwa chuo cha nabii Isaya kwa mfano kilipatikana kamili kama ilivyo Biblia katika magombo hayo.

Kutokana na mtazamo huo Paulo mtume anatukumbusha katika 2 Wakoritho 4:7 kuwa wanadamu tunafanana sana na vyombo hivyo vya udongo, karama, akili na vipawa alivyotupa Mungu ni hazina tu iliyohifadhiwa katika vyombo dhaifu sana vya dongo, vyombo ambavyo ni dhaifu na vinaweza kuvunjika wakati wowote na kwa njia rahisi “very delicate” ukweli huu haupingiki kwa sababu biblia iko wazi kuwa wewe na mimi tuliumbwa kwa Udongo Mwanzo 2:7 Biblia inasema “. BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Unaona? Mpendwa wewe na mimi ni mavumbi yaani ni udongo tu! Mungu analijua vema sana umbo letu na kukumbuka kuwa sisi ni mavumbi Zaburi 103:14 Biblia inasema Kwa maana Yeye anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi.” Je unajua kuwa Mungu anakumbuka kuwa sisi tu mavumbi? Ndio ni muhimu kukumbuka lakini pamoja na kuwa Mungu ametuumba kwa udongo ameweka vitu vya thamani kubwa ndani yetu ambavyo hata Malaika hawana!

Kutokana na jinsi Mungu alivyotuumba kwa thamani kubwa kiasi hicho ingawa ni dhaifu sana lakini ameweka vitu vya thamani na ujuzi wa hali ya juu na karama na vipawa ndani yetu, Hata hivyo Mungu anatuonya katika neno lake kuendelea kumuheshimu yeye na kujihadhari na majivuno ya aina yoyote na kuenda mbele zake kwa unyenyekevu mkubwa na kumrudishia yeye utukufu, heshima na adhama kwa sababu yeye ni mfinyanzi na sisi ni kama vyombo hivyo dhaifu mikononi mwake Isaya 45:9Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono?” Unaona ni maonyo makali kutoka kwa Mungu kupitia Nabii Isaya hatuwezi kuwa Jeuri kwa Mungu mimi na wewe ni kama Kigae Biblia inasema ole wetu kama tutashindana na Muumba! Isaya 64:8 “Lakini sasa, Ee Bwana, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako.” Hatuwezi kushindana na Mungu Baba yetu inatupasa kuwa wanyenyekevu mno kwani sisi ni udongo na Mungu baba yetu ni mfinyanzi tu sisi ni dhaifu Mungu na atusaidie tusijivune kwa jambo lolote.

 "Paulo Mtume alikuwa dhaifu katika mwili lakini alijaa Neema na Kweli alikuwa kama Malaika"

Hazina katika vyombo vya udongo!

Paulo mtume anapozungumzia Hazina katika vyombo vya udongo alikuwa na maana pana zaidi ingawa msingi wake mkubwa ni jinsi Mungu alivyowekeza siri zake katika mioyo yetu, siri ya injili, Paulo anazungumzia nguvu na uwezo wa Mungu, vipawa na karama ambazo zimewekezwa ndani ya mtu kiasi ambacho mtu akisikia habari zako anaweza kudhani kuwa wewe ni jitu kubwa sana
Paulo alikuwa na ujuzi wa nguvu za Mungu na udhaifu wa mwili wa binadamu ambao ni kama udongo Mungu alimtumia Paulo mtume kwa miujiza ya viwango vya kupita kawaida Biblia inatoa majumuisho tu ya huduma ya Paulo na jinsi Mungu alivyomtumia kwa kusema 

·         Matendo 19:11Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida;”
·         Licha ya Mungu kumtumia Paulo kwa mijuiza mikubwa ya kupita kawaida lakini ni wazi kuwa Mtume Paulo ndiye mtume aliyefanya kazi kuliko mitume wote kama maandiko yanenavy 1Wakoritho 15:10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.
·         Licha ya Paulo kutumiwa na Mungu na kufanya kazi kuliko mitume wote yeye alipewa mafunuo makubwa sana kuliko mtume yala mtumishi yeyote Paulo alipelekwa mpaka Mbingu ya tatu akaonyeshwa mambo mazito na meneno mazito ambayo mengine ni magumu kuyaeleza angalia 2Wakoritho 12:2-4 “Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu.  Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua); ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene”.
·         Paulo Mtume alikuwa Mwombaji, alikuwa akinena kwa lugha kuliko mtu yeyote, alikuwa na karama zote alikuwa na uwezo wa kuimba mpaka malango ya gereza yanafunguka, aliombea watu wa kila aina na kuponya wenye magonjwa, Paulo alikuwa Msomi ni Daktari wa Sheria aliyebobea na kadhalika 

Lakini pamoja na vipawa alivyokuwa navyo hakusahau kuwa yeye ni mavumbi alitambua kuwa Mungu ameweka hazina katika vyombo vya udongo tu na Historia ya kanisa inaeleza kuwa Paulo mtume ndiye aliyepatwa na majaribu mengi zaidi na mateso mengi zaidi kwaajili ya Kristo na injili, inasemakana kuwa Paulo mtume hakuwa jitu kubwa alikuwa ni mwembamba sana mwenye matege na nyele zake zilikuwa zimejinyonganyonga kama mmanga, aidha alikuwa na udhaifu katika mwili wake alikuwa anaumwa na pia alikuwa na macho dhaifu sana 2Wakoritho 12:7-9 Biblia inasema hivi “.Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu”. 

Unaweza kuona! Paulom mtume alikuwa na mwili dhaifu na pia macho dhaifu aliomba kuondolewa tatizo hilo lakini Mungu alimwambia ni neema yangu tu inakutosha ili asiwe na Majivuno, Wagalatia 4:13-15 Lakini mwajua ya kuwa naliwahubiri Injili mara ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa mwili; na jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu.  Ku wapi, basi, kule kujiita heri? Maana nawashuhudu kwamba, kama ingaliwezekana, mngaling'oa macho yenu, mkanipa mimi”.  Paulo mtume alikuwa na udhaifu katika mwili wake pamoja na kuombea wengi Mungu aliyaachia kwaajili ya utukufu wake ni kwaajili ya haya Paulo anaona kuwa Mungu ameweka hazina katika vyombo vya udongo.

Ndugu msomaji wangu hatuna cha kujivunia? Tunapaswa kuwa wanyenyekevu, tunapaswa kumpa Mungu utukufu, lakini hata kama ni wadhaifu hatuna hiki ama kile hiyo haipunguzi thamani ya kuumbwa kwako mfinyanzi ameliweka kusudi lake ndani yako usikate tamaa lakini kumbuka kuwa sisi ni binadamu ni daifu na Mungu ni mwenye nguvu ni mfinyanzi na tuishi mbali na majivuno ya aina yoyote tuwapo ulimwenguni

Mungu alimtuma Musa licha ya kuwa na kigugumizi, alimtumia Elisha licha ya kuwa na Upara, alimtumia Daudi licha ya kuwa na umri mdogo na kudharaulika hata kwa baba yake, acha kujidharau kwa sababu zozote zile 

Kumbuka kuwa asili ya nguvu zetu, uzuri wetu, ujuzi wetu, heshima yetu na mali zetu zimetokana na Mungu muumba wetu. Ukiyajua nhayo heri wewe ukiyatenda

Na mkuu wa wjenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni