Jumamosi, 29 Julai 2017

Mwamini tu hata kama sio rahisi!


Andiko la Msingi: Daniel 3: 1-6 
 Uwapo katika Mateso makubwa mno Mungu huwa Karibu mno mwamini tu hata kama sio rahisi !


Nebukadreza, mfalme, alifanya sanamu ya dhahabu, ambayo urefu wake ulikuwa ni dhiraa sitini, na upana wake dhiraa sita; akaisimamisha katika uwanda wa Dura, katika wilaya ya Babeli. Ndipo Nebukadreza akatuma watu kuwakusanya maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, ili wahudhurie wakati wa kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadneza aliyoisimamisha. Ndipo maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, wakakusanyika ili kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha; wakasimama mbele ya ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha. Ndipo mpiga mbiu akapiga kelele akisema, Enyi watu wa kabila zote, na taifa, na lugha, mmeamriwa hivi, wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, lazima kuanguka na kuiabudu sanamu ya dhahabu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha.Na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa saa iyo hiyo katika tanuru ya moto uwakao”.

Utangulizi:

Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake za kuishi si nyingi nazo zimejaa taabu alisema Mtumishi wa Mungu Ayubu katika Ayubu 14:1, maneno haya yanabakia kuwa kweli katika maisha ya wanadamu wote bila kujali anatokea katika tabaka gani, Lakini pamoja na dhiki na magumu tunayokutana nayo Neno la Mungu linaendelea kututia moyo kumuamini Mungu bila kukata tamaa, kuendelea kumuamini tu hata kama sio rahisi.

Kisa cha Shadrak,Meshak na Abednego katika Biblia kinaweza kutufundisha kitu kikubwa na cha ziada katika maisha yetu,hususani katika nyakati za leo,Vijana hawa watatuwaliweza kupingana na amri kali ya mfalme Nebukadneza na hatimaye kutupwa katika tanuru la moto,kisa chao kimekuwa kina mvuto mkubwa sana kwa vijana na wazee kwakarne nyingi sana, ukweli tendo lao laujasiri linatufundisha sote yunaomwamini Mungu kuwa na imani kali sana yenye kushangaza hata katika nyakati za Leo. tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

  • Kukataa ibada ya sanamu
  • Mambo ya kujifunza
  • Matokeo ya Imani yao.


Kukataa ibada ya sanamu.

Kisa cha vijana hawa ambao walijitunza sana imani yao katika Mungu kinaanza kwa kukataa kuabudu sanamu,Bibliai meagiza  kwamba IKIMBIENI IBADA YA SANAMU 1Wakoritho 10:14 “Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.” Kwa ujuzi usiokuwa wa kawaida wa neno la Mungu na utii wa hali ya juu kwa Mungu vijana hawa walikataa amri ya mfalme huyu mwenye nguvu, na walikataa kuitumikia au kuiabudu miungu yakeya dhahabu na lisanamu ambalo alikuwa amelisimamisha,huku akitangaza kuwa adhabu ya mtu atakayepingana naye ni kifo tu.
Maneno yao ni yenye kutia moyo sana angalia  na ulikuwani ukweli wenye kuumiza Daniel 3:15-18 “Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu? Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”

Mambo ya kujifunza kutoka kwao.

Imani ya Shedrack, Meshack na Abednego ni yenye kushangaza sana inafunua maswalamuhimu sana ya kujifunza kutoka kwao.

1.       Tegemeo lao lilikuwa kwa Mungu mmoja wa kweli mwenye nguvu ya kuwaokoa na hasira za Mfalme, walimuamini Mungu kuwa anaweza kuwaokoa na kila hila iliyokuwa mbele yao. Waliamini kuwa Mungu huwa anaokoa watu katika mapito mbali mbali, lakini pia walijua sio mara zote anaweza kufanya hivyo, hata hivyo katika namna ya kushangaza sana na isiyo rahisi waliamini kuwa hata kama sivyo,hawako tayari kuabudu miungu Jambo hili lilileta Baraka kubwa sana Biblia inasema amelaaniwa amtegemeaye mwanadamu amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Yeremia 17:5-7Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake” Vijana hawa walijifungulia Baraka kubwa sana kwa sababu walimtegemea Bwana walijikinga kwa Bwana Mungu wao. Tunaweza wakati mwingine tusijue sababu ya majaribu yanayotupata lakini Mungu anataka tumwamini yeye hata kama sio rahisi.
2.       Shadrack Meshack na Abednego walikuwa na imani isiyotikisika,Biblia inatufundisha kuwa mwenye haki ataishi kwa imani akisitasita roho yangu haina furaha naye, pia biblia inasema tendololote lisilotokana na imani ni dhambi,kwa sababu hiyo ni lazima tumuamini Mungu hata kama jaribu lililoko mbele yetu limeruhusiwa na Mungu Ayubu 13: 15-16. “Tazama, ataniua; sina tumaini; ila hata hivyonitaithibitisha njia yangu mbele yake.Hili nalo litakuwa ni wokovu wangu; Kwani asiyemcha Mungu hatakaribia mbele yake” tunajifunza kuwa njia njema na bora ni kumkaribia Mungu hata kama tutahisi ni Mungu ametruhusu jaribu hilo, Ayubu anasema hata kama atanichinja au ataniua bado nitamthibitishia kuwa ninamwamini yeye
3.       Usimsujudie  wala kumuogopa mwanadamu Nebukadreza alikuwa ni mfalme mwenye nguvu kubwa duniani mataifa yote na watu wote na kabila zote walimuogopa kwa sababu ya mafanikio makubwa na uchumi mkubwa aliokuwa nao aliweza kutumia nguvu yake kuwatisha vijana hao ili waiache imani yao kwa Mungu, lakini wao hawakukubali kutii waneitii sauti yake wanekuwa wamemtii shetani lakini pia wameabudu Mwanadamu,kwa Sababu hiyo Shadrack Meshack na Abednego walikuwa tayari kwamba hata kama wangepitia Magumu na mateso ya kutisha na maumivu mabaya sana ya kuingizwa katika tanuru lamoto, walikataa kumuacha Mungu na kuabudu miungu, Yesu anatilia mkazo wazo hili katika Mathayo 10:28Biblia inasema Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.” Kwa kawaida wanadamu wakiisha kufanikiwa kwa sababu mbalimbali za kielimu, kiuchumi, na hekima wengi hujisahau na kuwa na kiburi, wanasahau kuwa ni Mungu ndiye aliyewabariki, wamamuacha Mungu na kuwataka watu waabudu mali zao, waabudu akili zao na mafanikio yao, wakati mwingine ni vigumu kupata somo lakujifunza kutoka kwa waliofanikiwa na ni rahisi kupata somo kutoka kwa walioshindwa, watu, taifa au kiongozi akiwa na nguvu tayari huacha kumtegemea Mungu na kutaka watu wamuabudu yeye na uwezo wake na akili yake, ni rahisi kuona watu wenye uwezo wakinyanyasa wengine, na kuweka madaraja Biblia inatia moyo kumtii Mungu na kutokuabudu wanadamu.
 Matokeo ya Imani yao.

Ni muhimu kufahamu kuwa kutokana na ujasiri wa imani ya Shedrack Meshack na Abednego Mungu alijitukuza sana Nebukadreza alishangazwasana na mambokadhaa yaliyojitokeza kwa vijana wale,

1.    Moto haukuwaunguza kabisa Mungu aligeuza tanuru la moto kuwa bichi kwa Shedrack Meshack na Abednego kila anayemtumaini Bwana ni lazima aelewe kuwa Mungu anaweza kutumia majaribu kama mlango wa kukupeleka kwenye hatua nyingine, adui anaweza kufurahi kuingia kwako majaribuni na matatani lakini Mungu aweza kutumia majaribu kama njia ya kukuletea faraja ya kweli.

2.       Waliowatupa katika moto ndio waliokufa  Daniel 3:19-23
Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto. Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Basi watu hao wakafungwa, hali wamevaa suruali zao, na kanzu zao, na joho zao, na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Basi kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na ile tanuru ilikuwa ina moto sana, mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakaanguka, hali wamefungwa, katikati ya ile tanuru iliyokuwa inawaka moto
Wako watu ambao ukiwatupa ni kama unajiangusha mwenyewe,Mungu akupe neema kwamba adui zako wanaokuchukia wawe wamejichukia wenyewe, waliokuchoka wawe wamejichoka wenyewe,ni ajabu kuwa wana wa Israel walimkataa ndugu yao Yusufu, kumbe walikuwa wakimfukuza waziri wa chakula na ingewalazimu kumsujudia ili wale, Mungu akupake mafuta ili kwamba wanaokutaaa wafilisike, wapaytwe na njaa wakukumbuke wakulilie wakujutie, Mungu na autume moto kuunguza adui zako. Badala yako.

3.       Walitupwa wakiwa wamefungwa lakini walikuwa wakitembea wakiwa wamefunguliwa, shetani na maadui wa Mungu wanaweza kudhani kuwa, wamekufunga lakini katika namna ya kushangaza wamekufungua, wako watu wanaodhani ukiwa katika himaya yao ndio umefikia kiwango cha juu cha furaha na kuwa wakikuondoa wanakuhuzunisha  jicho la Mungu linaona tofauti kuwa ulikuwa kifungoniwala hukuwa na furaha lakini na sasa anakuweka huru, Matokeo ya imani ya vijana hawa ni kuwa kamba walizofungwa ziliwaachia,na sio hivyo tu moto mkali uliochochewa kuwaunguza haukuwadhuru Isaya 43:2 “Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza

4.        Walitupwa peke yao lakini Mungu alijiunga nao, Daniel 3:23-25 “Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakaanguka, hali wamefungwa, katikati ya ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme. Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu”.  Watu wanaweza kudhani ya kuwa wanakutupa wewe kumbe wanamtupa Mungu, Ni jambo la kushangaza sana kuwa Mwana wa Mungu alijiunga na vijana hao nilikuwa najiuliza maswali mengi sana kama mkuu wa wajenzi najua kabisa Mungu angeweza kufanya muujiza huu akiwa mbinguni hata bila ya kuonekana kwa umbile na bado ingeashiria kuwa Mungu amewaokoa lakini swali langu kubwa ilikuwa kwanini ajionyeshe? Mungu alikuwa anajidhihirisha kuwa yeye ni Mungu aliye hai, na kuwa uhai wa binadamu uko mikononi mwake na kuwa yuko pamoja na watu wakehata pale wanapoona kuwa hali ni tete na kuwa mambo hayawezekani yeye anaonyesha wazi kwamba tuamini tu hata kama sio rahisi, yeye ataingilia kati,ndoa yako hata kama inaonekana kuwa sio rahisi,Yeye ataingilia kati, hata kama mtihani uliopita unaonekana kuwa ulifelikwa kiwango kikubwa na kuwa kwa muda uliobaki ni kama haiwezekani, kupata matokeao mazuri biblia inataka uamini tu  hata kama sio rahisi, watu wamekukatia tamaa kuwa kwa ugonjwa ulionao utakufa na hutapona nasema leo amini tu hata kama sio rahisi, umekata tamaa juu ya mabadiliko ya tabia mbaya za watoto wako na inaonekana kama haiwezekani wakapona nataka nikuambia amini tu hata kama sio rahisi, vijana wameharibika na madawa ya kulevya na inaonekana kama ni vigumu kuacha kuwa teja mwamini Mungu tu hata kama sio rahisi, wamesema mirija yako imeziba na kuwa huwezi kuzaa tena mimi nasema amini tu hata kama sio rahisi, wamesema ukoo wenu nyinyi ndio basi hamuwezi kufanikiwa hamwezi kutoka nakuambia leo katika jina la Yesu amini tu hata kama sio rahisi, unasumbuliwa na ukimwi, kisukari, kansa,magonjwa ya zinaa, matatizo sugu ya kifamilia na watu wanadhani kuwa wewe ndio baaasi nakuhakikishia amini tu hata kama sio rahisi, ni majini na mapepo yanakusumbua,umepitia kila aina ya maombezi na inaonekana hujapata ufumbuzi nakuhakikishia amini tu hata kama sio rahisi,    Haikuwa jambo rahisi kukataa amri ya mfalme laki vijana hawa waliamini tu hata kama ahaikuwa rahisi Yesu aliahidi kuwa anatakuwa pamoja nasi hata ukamilifu wa dahari Mathayo 28:20, aliahidi kuwa atatutia nguvu Zaburi 55:22, Psalm 147:6 na aliahidi kuwa atatuokoa kabisa hata milele Mathayo 25:41,46

5.       Shadrack Meshack na Abednego walimbadilisha mbadilishaji ( they changed the Changer)
Kutokana na kiburi chake Nebukadneza alitaka sana kuwabadilisha vijana hawa mwanzoni kabisa alipowateka vijana hawa wa Kiebrania aliwafundisha Lugha yake, ya kikaldayo, alibadilisha kuvaa kwao na alibadilisha majina yao Kiibrania Daniel maana yake Yehova ni mwamuzi  wangu alimbadilisha na kumuita Belteshaza yaani anayependwa na Beli, yaani mungu wa wababiloni, Hannaniah anayependwa na Yehova, akamuita Shadrak maana yake aliye kama Venus na Azaria maana yake Yehova ni msaada wangu alimuita Abed nego yaani mtumishi wa Nego, Nebukadreza alifanya hivi kwa makusudi ya kisaikolojia na kidini, Nebukadreza alifikiri kwa akili zake anaweza kuwabadilisha watu, kupitia imani ya vijana hawa tunajifunza kuwa mwenye uwezo wa kubadilisha watu ni Mungu tu na kuwa watu wa Mungu wakiishi kwa imani wanaweza kuwabadilisha wale wanaofikri kuwabadilisham, kamwe Hatuwezi kuubadili ulimwengu kwa kuwa kama walimwengu bali tunaweza kuubadili ulimwengu kwa kuwa kinyume na ulimwengu imani ya  vijana hawa ilimfanya aliyekuwa na bidii ya kuwabadilisha abadilike yeye, Daniel 3: 26-30. “Kisha Nebukadreza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto. Na maamiri, na manaibu, na maliwali, na mawaziri, waliokuwa wamekusanyika pamoja, wakawaona watu hao, ya kuwa ule moto ulikuwa hauna nguvu juu ya miili yao, wala nywele za vichwa vyao hazikuteketea, wala suruali zao hazikubadilika, wala harufu ya moto haikuwapata hata kidogo. Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe. Basi mimi naweka amri ya kuwa kila kabila ya watu, na kila taifa, na kila lugha, watakaonena neno lo lote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii. Kisha mfalme akawakuza Shadraka, na Meshaki, na Abednego, katika wilaya ya Babeli” Ni Mungu pekee ndiye mwenye uwezo wa kuwabadilisha watu, hata kama watu hao wamesema hawawezi kuokoka hawawezi kubadilika wameshindikana kwa Mungu yote yanawezekana dakika chache tu mfalme alikuwa amekasirikia watu wanaomuabudu Mungu aliye hai na ni dakika chache tu anamhimidi Mungu wa kweli.

Amini tu hata kama sio rahisi
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye hekima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni