Jumatano, 2 Agosti 2017

Iwapo watakuchukia !


Mstari wa Msingi: Yohana 15:18Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.” 

 "Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu"



Utangulizi.
Chuki ni hisia za kutokupendezwa na kitu au mtu Fulani kwa sababu mbalimbali, ni hisia za kutokumpenda mtu, Biblia imeonyesha mikasa mingi ambapo watu kadhaa waliwachukia wengine kwa sababu mbalimbali, au wakati mwingine bila sababu, ingawa ukweli unabaki kuwa ziko sababu Fulani, Je wewe umewahi kuchukiwa na mtu? Je ni Bila sababu? Nadhani unaweza kudhani kuwa hakuna sababu lakini neno la Mungu linafunua sababu mbalimbali za wewe kuchukiwa, na linakutaka ujue kwa nini watu wanakuchukia na nini cha kufanya iwapo watakuchukia, ni kwa msingi huo leo tutachukua muda kutafakari kwa kina somo hili muhimu IWAPO WATAKUCHUKIA kwa kuzingatia vipengele vifuatavyo.

·         Amri ya kutokumchukia awaye yote.
·         Iwapo watakuchukia!

Amri ya kutokumchukia awaye yote.
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu katika neno lake tangu nyakati za agano la kale alikemea chuki, alikataza mtu kuwa na chuki moyoni dhidi ya ndugu yako yaani aina binadamu wa aina zote, Mambo ya walawi 19:17-18 Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi BWANA”. Kwa kiwango cha maandiko chuki inahesabika sawa na uuaji na kwamba hakuna ufalme wa Mungu kwa mtu mwenye chuki dhidi ya mwingine1Yohana 3:15Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake.” Aidha biblia imeonyesha wazi kuwa awaye yote amabaye anamchukia mwingine kwa sababu yoyote ni muongo uongo wake unadhihirishwa na chuki yake na hivyo haweze kuwa na madai ya kuwa anampenda Mungu iwapo ana mchukia binadamu mwenzake anayemuona kwa macho 1Yohana 4:20-21Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.” Maandiko yanakemea na kukataza chuki, lakini wewe ni shahidi wa wazi kwamba ulimwengu wa sasa umejawa na chuki, katika taarifa nyingi za habari tunazozisikia kila leo, matendo ya kikatili na mauaji vita na kadhalika kwa asilimia kubwa yanaongozwa na chuki, chuki zimeenea kama sumu katikajamii, chuki iko miongoni mwa wakristo kwa wakristo  hata wale wanaosali katika kanisa moja, kama haitoshi chuki ikokwa kiwango kikubwa hata kwa watumishi wa Mungu yaani wale walioko katika mstari wa mbele kutuhudumia kwa neno la Mungu na kuishi kama kielelezo cha injili unaweza kushangaa kwamba kuna chuki, vijembe, uadui na hata ugomvi, visa na visasi, Chuki chuki chuki kila mahali ulimwenguni, ziko chuki za watu kwa sababu ya ukabila, ziko chuki za watu kwa sababu ya rangi, ziko chuki za watu kwa sababu ya kuishi maisha ya mashindano, ziko chuki kwa sababu ya mafanikio ya mtu mwingine, ziko chuki kwa sababu ya kuchukuliana waume, wake,tofauti za kiimani au kihistoria na kadhhalika, Chuki ni ushahidi ulio wazi kuwa bado watu wako gizani  1Yohana 2:9 “Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani hata sasa.” Mwanafunzi wa Yesu ni yule anaweza kudhihirisha upendo wake hata kwa wale wanaomuudhi na kumtendea vibaya.

Iwapo watakuchukia.

Iwapo watakuchukia! Ni ishara kwamba ziko sababu ambazo kwazo zinaweza kupelekea ulimwengu ukakuchukia kama umeokoka lakini vilevile hata kama hujaokoka bado unaweza ukachukiwa na watu wengine kwa sababu kadhaa, Biblia ina majibu ya kutia moyo kwa niniwatu wanakuchukia ziko sababu nyingi lakini zifuatazo ni baadhi na zinaweza kukutia moyo ukiona watu wanakuchukia fahamu!

1.       Wewe si wa ulimwengu huu,
    Yohana 15:18-25Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka. Kama nisingalikuja na kusema nao, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa hawana udhuru kwa dhambi yao. Yeye anichukiaye mimi humchukia na Baba yangu. Kama nisingalitenda kwao kazi asizozitenda mtu mwingine, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa wametuona mimi na Baba yangu, na kutuchukia. Lakini litimie lile neno lililoandikwa katika torati yao, Walinichukia bure.”  Yesu anazungumza maneno ya kutia moyo sana kama mkuu wa wajenzi sitamani kuongeza lolote ni kama Yesu amemaliza kila kitu kwamba ukiona watu wanakuchukia wewe ujue si wa ulimwengu huu viwango vyako zi vya kawaida wewe uko juuu, wewe sio kama bata au kuku ndege wa chini wewe ni wa viwango vya juu, Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Yesu alikiri kuwa yeye mwenyewe sio wa ulimwengu huu, Yohana 17:16Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.” Yesu hakuwa wa ulimwengu huu na ndio maana walimchukia kila mtu aliyeokolewa anapaswa kufahamu kuwa yeye sio wa ulimwengu huu na kamwe ulimwengu hauwezi kukufurahia wakufurahiaje wewe ni wa tofauti wakuungeje mkono umewazidi wewe ni wa juu wao ni wa chini wakupendee nini? Wewe ni mtu ambaye ulimwengu haukustahili kuwa nawe Waebrania 11: 32-38Nami niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii; ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni. Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.”

2.       Ndoto zako kubwa sana!

     Mwanzo 37:3-19Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili. Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu.  Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Akamwambia, Mimi hapa. Akamwambia, Enenda, basi, ukaone kama ndugu zako hawajambo, na kundi nalo li salama, ukaniletee habari. Basi akampeleka kutoka bonde la Hebroni, akafika Shekemu. Mtu mmoja akamkuta, naye alikuwa anazunguka-zunguka katika nyika; yule mtu akamwuliza, akisema, Unatafuta nini? Akasema, Nawatafuta ndugu zangu; tafadhali uniambie mahali wanakochunga. Yule mtu akasema, Wametoka hapa, maana niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja”.  Unapokuwa na ndoto kubwa kamwe usitarajie dunia itakukubali dunia haiwezi kuvumilia ndoto zako ndugu zake Yusufu walimchukia kwa sababu alipendwa sana na baba yake na alikuwa mtu mwenye maono ya mbali, watu wanaweza kukuonea wivu na kukuchukia kwa sababu umewazidi viwango vya kufikiri, haushikiki, wewe sio wa kawaida una kitu cha ziada wakupendee nini ndugu ukiona watu wanakuchukia usiwasimulie ndoto zako haiyamkini hawawezi kustahimili ndoto na maono na akili na uweza ulio nao.

3.       Sifa zako ni kubwa kuliko zao.

     1Samuel 18:6-9Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda.  Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile”. Ndugu yangu ukiona watu wanakuchukia, wanakuhusudu, wanataka kukuua, wanataka uangamie kabisa, wanataka uanguke, wanataka mabaya yakupate wanapanga mabaya na  magumu dhidi yako jua ya kuwa sifa zako ni kubwa sana, nikubwa mno adui zako hawawezi kustahimili kuzibeba watafanya nini sasa watatafuta kukuua watakuchukia watakuogopa wewe umekuwa tishio kwao, unawazidi una kitu cha ziada una akili una kibali kwa Mungu, kama hungelikuwa na kitu wangekuhurumia tu, Kumbuka kila mara unapopata sifa kubwa kuliko wengine wanadamu wenye wivu watatafuta kuchafua sifa zako, watashangilia utakapojikwaa, watakuza udhaifu wako ili wakumalize kabisa Daniel 6:1-5Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote; na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake”.

4.       Umejaa neema na uwezo.
 
     Matendo 6:8-15 Mungu anapokuwa amekupa neema na uwezo jambo hili pia linaweza kualika maadui angalia Matendo 6:8-15 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano;lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu. Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi, wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza. Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati; maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa. Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika”. Unaona Stefano alikuwa amejaa neema na uwezo wa Mungu.Mungu alikuwa akimtumia kwa miujiza na ishara kubwa sana , Mungu alimpa hekima ya kupita kawaida, alikuwa mmnenaji Hodari, alijaa Roho mtakatifu, watu walioshindana naye hawakumuweza, walimchukia na kumzushia maneno ya uongo na kutafuta kumuua,mtu huyu alikuwa mwema alijaa upako na uzuri uso wake ulikuwa kama wa malaika, watu walitafuta kumuangamiza na  wakamuua,hii ilikuwa chuki dhahiri kwani Stefano hakutenda neno ovu lolote, Lakini kwa vile alikuwa amewazidi watu katika neema na uwezo aliuawa, kumbuka kila talent utakayopewa na Mungu wenzako wakigundua kuwa inawafunika wakaacha kumtazama Mungu anayewapa watu bila upendeleo wakakuangalia wewe watakuchukia na matokeo yake watakuua.

5.       Wewe ni wa Roho.

   Wagalatia 4:29Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa.” Biblia inaonyesha kati ya chuki zilizokuweko kati ya Ishmael kwa Isaka na inaonyesha kuwa sababu kubwa ya chuki ya Ishmael kwa Isaka ni kwa sababu mmoja alikuwa wa mwilini na mwingine alikuwa wa Roho, chuki na uonevu unaoletwa juu yako unatokana na wewe kuwa rohoni wewe umezaliwa kwa roho wewe ni mwana wa Mungu weweni mrithi wa ahadi zilezile za Ibarahimu na Isaka na Yakobo.Mi lazima utachukiwa,wewe umezaliwakwa Mapenzi ya roho na sio ya mwili Yohana 1:12-13Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu

6.   Bwana yuko Pamoja nawe na umebarikiwa

     Ni muhimu kufahamu hata kama wakati mwingine huwezi kujua kuwa una kitu gani cha ziada lakini pale unapoona watu wanakuchukia ni muhimu ukafahamu kuwa sio wakati wote unachukiwa kwa sababu wewe haufai, hapana, watu wanaweza kukuchukia na hata kukufukuza kwa sababu wanaona katika ulimwengu war oho Bwana yuko pamoja nawe na kuwa umebarikiwa angalia Mwanzo 26:12-31Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi.  Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko.  Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna.  Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.  Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba. BWANA akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu. Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko. Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake.  Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu? Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba BWANA alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa BWANA.  Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa. Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaapiana wao kwa wao, kisha Isaka akawapa ruhusa, nao wakaenda zao kwa amani.”

7.       Maisha yako yanapoathiri yao kuliko yao kuathiri yako.

     Tabia na mwenendo utendaji na maisha ya Yesu Kristo ulikuwa na athari kubwa sana kwa Mafarisayo na masadukayo ni ukweli uliokuwa wazi kuwa Yesu alikuwa anaendelea kupata umaarufu mkubwa  na mafarisayo walijiona kuwa wanapoteza umaarufu, ulimwengu ulikuwa unakwenda nyuma ya Yesu hii ilijumuisha Yesu kukubalika sio na wayahudi tu bali hata wagiriki yaani wayunani dunia ilikuwa imamuendea Yesu, Yesu alikuwa ni kama chumvi inayofanya mboga inoge na bila yeye isinoge unapoona wakati mwingine watu wakikuchukia fahamu wazi kuwa Maisha yako yaanaathiri uwepo wao, unapoteza Heshima yao,kupitia wewe Mungu yu afanikisha mambo na wao wanajiona kuwa sio kitu nakwa sbabu hiyo watakuchukia Yohana 12:9-22 “Basi watu wengi katika Wayahudi walipata kujua ya kuwa yeye yuko huko, nao wakaja, si kwa ajili yake Yesu tu, ila wamwone na Lazaro, ambaye Yesu alimfufua katika wafu. Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri la kumwua Lazaro naye;maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walijitenga, wakamwamini Yesu. Nayo siku ya pili yake watu wengi walioijia sikukuu walisikia ya kwamba Yesu anakuja Yerusalemu; wakatwaa matawi ya mitende, wakatoka nje kwenda kumlaki, wakapiga makelele, Hosana! Ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli! Naye Yesu alikuwa amepata mwana-punda, akampanda, kama vile iliyoandikwa, Usiogope, binti Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda. Mambo hayo wanafunzi wake hawakuyafahamu hapo kwanza; lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka ya kwamba ameandikiwa hayo, na ya kwamba walimtendea hayo. Basi wakamshuhudia wale mkutano waliokuwapo pamoja naye alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua. Na kwa sababu hiyo mkutano walikwenda kumlaki, kwa kuwa wamesikia ya kwamba ameifanya ishara hiyo.Basi Mafarisayo wakasemezana wao kwa wao, Mwaona kwamba hamfai neno lo lote; tazameni, ulimwengu umekwenda nyuma yake.Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu.  Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu.Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu.
Yohana mbatizaji alikuwa kiongozi mwenye nguvu sana hakuwa na wivu wala hakuathiriwa na hali ya Yesu kuwa maarufu, wako watu wengine kwa sababu tu pale wengine wanapokuwa maarufu kiasi cha kuathiri maisha yao,wanakuwa hawatambui mchango wa wengine na wanaukataa, Yesu alikuwa anafanya kazi na kuwa na wanafunzi wengi kuliko Yohana mbatizaji, hata wanafunzi wengine wa Bwana Yesu walikuwa wanahama kwa Yesu na watu walimletea habari, lakini yohana hakuogopa wala kufadhaika bali alisema yeye hana budi kuzidi bali mimi kupungua, huu ni moyo wa kipakee sana na ndipo ukristo wetu unapopimwa unajisikiaje mwengine anapofanikiwa, anaposifiwa anapokuwa maarufu kuliko wewe? Kama unajisikia vibaya unahitaji toba! Ni muhimu kutambua mchango wa wengine kwani hakuna mtu asiyefanya kitu,  viongozi dhaifu huponda kabisa kazi za waliowatangulia kana kwamba hawana mchango wowote hili sio jambo jema, je tunajisiakiaje pale washirika wa kanisa letu wanapoondoka kwenda kwa mchungaji wakanisa lingine? Kama tunajisikia vibaya badala ya kusubiri neema ya Mungu kutuinua na sisi kwa wakati wetu Yohana 3:22-30Baada ya hayo Yesu na wanafunzi wake walikwenda mpaka nchi ya Uyahudi; akashinda huko pamoja nao, akabatiza. Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele; na watu wakamwendea, wakabatizwa. Maana Yohana alikuwa hajatiwa gerezani. Basi palitokea mashindano ya wanafunzi wa Yohana na Myahudi mmoja juu ya utakaso. Wakamwendea Yohana, wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani, yeye uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea. Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua.”

8.   Wanataka uwaabudu na kuwasujudia

    Ni muhimu kufahamu kuwa wanadamu wanapokuwa na mafanikio makubwa sana na kadiri wanavyobarikiwa na kupelekwa juu sana wanapaswa kukumbuka kuwa wanyenyekevu sana vinginevyo ni rahisi kwao kuwa na kiburi na kutaka kuabudiwa na kusujudiwa Biblia inasema imeandikwa utamuabudu na kumsujudia bwana Mungu wako peke yake Luka 4:5-8 5. “Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako. Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” Unaona sio rahisi kwa mwanadamu aliyetukuka kujijua kuwa anataka ibada lakini kiburi kinapoinuka ndani ya mwanadamu na shetani akapata nafasi wanadamu hupenda kuchukua nafasi ya Mungu na kutaka waabudiwe wao, je umewahi kusoma kisa cha Mordekai na Haman umewahi kuona ni kwa kiasi Gani hamani alimchukia Mordekai na sio yeye tu na kabila zima la wayahudi kwa sababu gani kwa sababu Mordekai hakuinama wala kumsujudia, tunaposimama kidete katika imani yetu kwa Mungu tunapaswa kutambua kuwa ni dhambi kumpa mwanadamu nafasi ya Mungu, wako watu wengine wakishaona wamepewa kumiliki watu,au wameajiri watu, au ni wasimamizi wa watu basi wanataka kila mtu awaogope na kuwa tetemekea na kama wanaona una msimamo thabiti wala hutetemeshwi na mafanikio yake wala kile alicho nacho anatafuta namna ya kukufanya umnyenyekee kwa kiwango cha kumuabudu na kumsujudia Esta 3:1-6 biblia inasema hivi “Baada ya hayo mfalme Ahasuero alimwongezea cheo Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, akampandisha, akamwekea kiti chake juu ya maakida wote waliokuwapo pamoja naye. Nao watumishi wote wa mfalme, walioketi mlangoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana ndivyo alivyoamuru mfalme kwa habari zake. Bali Mordekai hakuinama, wala kumsujudia.Basi watumishi wa mfalme walioketi mlangoni pa mfalme wakamwambia Mordekai, Mbona wewe waihalifu amri ya mfalme? Ikawa, waliposema naye kila siku asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama mambo yake Mordekai yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni Myahudi. Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hainami wala kumsujudia, alighadhibika sana. Akaona si shani kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila yake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai.” Katika injili pia tunao mfano wa Yesu Kristo alipokuwa mbele ya Pilato Yesu hakujibu neno katika mashitaka yake, kwa namna ya kustaajabisha Pilato alitumia mamlaka yake kumlazimisha Yesu amjibu na hapa ndipo Yesu alipomjua kuwa ulicho nacho umepewa kutoka juu Yohana 19:10-12Basi Pilato akamwambia, Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulibisha? Yesu akamjibu, Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu; kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.” Majibu ya Yesu yalimfanya pilato kuogopa na kuwa mpole, watu wengi waliopewa kitu na Mungu au mamlaka na Mungu huyatumia vibaya huyatumia kunyanyasa wanyonge na pale wanapoona wanyonge hawako tayari kusujudia wanawachukia je wewe unapendwa kuogopwa? Unachukia watu wanapoonyesha kutokukutetemekea jifunze kukubali kushughulishwa na mambo manyonge na tumuachie anayestahili kupokea utukufu apokee yeye tu.

9.       Mungu amelikuza Jina lako.
     
     Mungu anapokusudia kumbariki mtu pia hulibariki jina la mtu huyo na kulikuza sana angalia Mwanzo 12:1-3 Biblia inasema “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa” Katika ahadi za Mungu kwa Ibarahimu mojawapo ilikuwa ni kulikuza jina lake, ni wazi kama umepata kibali kwa Bwana na wewe umrithi sawa wa ahadi zilezile za Ibrahimu Baba yetu wa Imani, Jina lako litakuzwa sana kutokana na aina ya utumishi na Baraka ambazo Bwana amezikusudia kwako, katika namna ya kushangaza sana Yesu alisema watu wanaotuchukia au wanaokuchukia pia watafanya kila liwezekanalo  kulitupa nje jina lako ili uonekane kuwa hufai au uonekane kama kitu cha hovyo au kiovu angalia Luka 6:22-23 Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu.Furahiwani siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni, maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo” Je umewahi kukutana na hali za namna hiyo maadui zako wanataka kukuchafua ili kwamba usiinuke tena, ili kwamba uonekane kuwa hufai kwa lolote? Nini kinatafutwa hapo wanataka kulifuta jina lako! Wanataka kulishusha wanataka kuliharibu wanataka kulichafua kwa sababu gani Mungu amelikuza jina lako. Yesu anatutia moyo kuwa hata hivyo thawabu yetu ni kubwa mbinguni.

10.   Iwapo utainuka tena!

Endapo itatokea kuwa maadui zako watagundua kuwa ulianguka aidha kimaisha, kiroho, kibiashara kikazi na kwa njia nyingine zozote, wakati wote adui au dunia au ulimwengu haauwezi kufurahi kugundua kuwa unainuka tena, watatamani ubaki vilevile, watatamani usiinuke tena, swala hili lilikuwa dhahiri pale wakuu wa makuhani walipogundua kuwa Yesu atafufuka angalia kwamba kwa ujinga mkubwa kabisa waliomba wawekewe askari walilinde kaburi barabara ili kwamba Yesu asifufuke Mathayo 27:62-66. “Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi”. Unaona ni tabia iliyo wazi kwa watu wenye chuki kutofurahjia maendeleo yako watataka uendelee kuharibikiwa na pale unapofanya matengenezo na kujipanga tena na wakagundua kuwa unainuka tena ndipo maneno ya kejeli huanza kwanini kwa sababu hawawezi kufurahia mafanikio yako na hata kuinuka kwako tena, watatoa maneno ya kejeli, watatukana na wataweza hata kupigana nawe au kuipinga vikali kazi unayoifanya Nehemia 4:1-9Lakini ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi. Akanena mbele ya nduguze na mbele ya jeshi la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je! Watajifanyizia boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je! Watayafufua mawe katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto? Basi Tobia, Mwamoni, alikuwa karibu naye, akasema, Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe. Sikia, Ee Mungu wetu; maana tunadharauliwa; ukawarudishie mashutumu yao juu ya vichwa vyao, ukawatoe watekwe katika nchi ya uhamisho; wala usiusitiri uovu wao, wala isifutwe dhambi yao, mbele zako; kwa maana wamekukasirisha mbele ya hao wanaojenga. Basi tukaujenga ukuta; nao ukuta wote ukaungamanishwa kiasi cha nusu ya kimo chake; maana watu walikuwa na moyo wa kufanya kazi. Lakini ikawa, Sanbalati, na Tobia, na Waarabu, na Waamoni, na Waashdodi, waliposikia ya kuwa kazi ya kuzitengeneza kuta za Yerusalemu inaendelea, na ya kuwa mahali palipobomoka panaanza kuzibwa, basi wakaghadhibika mno; wakafanya shauri wote pamoja kuja kupigana na Yerusalemu, na kufanya machafuko humo. Bali sisi tulimwomba dua Mungu wetu, tena tukaweka walinzi, mchana na usiku, kwa sababu yao, ili kuwapinga.” Unaona hakuna mwanadamu anayefurahia mafanikio yaw engine, wako wachache tu wanaofurahia wengine kuwa kama wao au hata kuwazidi, lakini kumbuka adui zako watafurahi kuona umeangamia, umeanguka na hauinuki tena, iwapo wataona unainuka hawatafurahia.

11.   Bila sababu.
Yohana 15;25 biblia inasema “Lakini litimie lile neno lililoandikwa katika torati yao, Walinichukia bure” Biblia inaonyesha wazi kuwa wakati mwingine sababu hizo za chuki hazijulikani torati ilitabiri kuwa kuna kuchukiwa bure tu, pasipo sababu, hata hivyo wanasaikolojia wanasema kuwa mtu mwenye chuki mara kadhaa huwa ni kama mtu anayejidhuru mwenyewe, ni mgonjwa kiakili,kwa sababu mwisho wa siku hakuna faida atakayoipata, tu mwenye chuki anaweza kumchukia mwingine kwa sababu hawezi kuwa kama wewe,unaweza kuchukiwa kwa sababu ya vipawa na uwezo uliokuwa nao, au kwa sababu ya changamoto unazotoa, au kwa sababu unafanya sana kuliko wengine, unaimba sana kuliko wengine, nk lakini biblia imesema wakati mwingine bila sababu. Yaani walinichukia bure!

Yatupasayo kufanya ulimwengu ukituchukia.
 
1.       Samehe wote wanaokuchukia.
Katika ulimwengu uliojaa chuki kamwe hatuwezi kuiondoa chuki kwa kutumia chuki,ulimwengu utaharibika kwaninsisi ni chumvi ya ulimwengu, ni muhimu kwetu kuwalipa mema wale wanaotutendea mabaya na kuwahakikishia kuwa tumewasamehe kabisa, sisi sio badala ya Mungu,Mungu mwenyewe atalipa kisasi,wala wanaotuchukia ni wadhaifu, ni wagonjwa wanaumwa hivyo wahurumie kwa kuwasamehe kabisa, kiumbe mwenye nguvu kabisa duniani ni yule anayesamehe na sio yule anayelipa kisasi. Mwanzo 50: 15-21Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye. Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako. Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema.
Watu wa daraja la juu kabisa la kiroho husamehe, wenye chuki wanahitaji msamaha kwa sababu wana matatizo ya kisaikolojia wanahitaji kuhurumiwa waombee kwa Mungu kwa sababu “Luka 23:33-35Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura. Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake

2.       Chuki itakupeleka Mahali pa Heshima.

Hakuna mtu aliyechukiwa na wengine na huku anamtegemea Mungu ambaye mambo yake yaliharibika au Bwana asimtokee tena, Ni muhimu kukumbuka kuwa chuki dhidi ya Yusufu ilileta mafanikio katika maisha yake na hata ya wale waliomchukia,

3.       Kuna thawabu kubwa sana Mbinguni.

Luka 6:22-23 Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu.Furahiwani siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni, maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni