Jumanne, 26 Septemba 2017

Heri wenye moyo safi!



Mathayo 5:8 “Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu
 
Injili maalumu kwa watoto: “Waacheni watoto wadogo waje kwangu msiwazuie maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao”




Siku moja katikati ya umati mkubwa sana wa watu kijana mmoja alisimama na akapiga kelele akisema Jamani niangalieni mimi kwakweli nina moyo Mzuri kuliko watu wote Duniani
Watu wote walishituka na kumwangalia na kweli walishangaa kuona kwamba ana moyo mzuri sana na ulikuwa mkamilifu katika umbile lake na haukuwa na mikwaruzo ya aina yoyote, wote walishangazwa na uzuri wa moyo wake na walimsifu sana. 
 
Hata hivyo baada ya muda kidogo mzee mmoja alisimama na kumwambia kijana Hapana mwanangu mimi nina moyo safi na mzuri zaidi kuliko wa kwako na nina moyo mzuri zaidi kuliko wote duniani
Kijana akamwambia nionyeshe moyo wako! Tuuone

Mzee yule alionyesha Moyo wake, kwa kweli ulikuwa mbaya hauna sura nzuri una majeraha na makovu makubwa ulikuwa umeharibika kiasi ambacho hata ile sura ya moyo haikueleweka vizuri, ulikuwa kama vipande vipande vilivyoungwa.

Kijana alimcheka sana na kumwambia Babu yangu umechanganyikiwa angalia moyo wangu jinsi ulivyo mzuri kweli unaweza kufananisha na wako? Moyo wangu hauna hata mkwaruzo ni mkamilifu katika kila eneo, unaweza kulinganisha na wa kwako kweli? Una majeraha mengi umeungwaungwa umepoteza sura yake kabisa unawezaje kusema kuwa una moyo mzuri kuliko wote Duniani?

Mwanangu moyo wangu ni mzuri kuliko wa kwako alisema mzee yule, umeona majeraha? Umeona makovu, umeona ulivyoungwaungwa?umeona ulivyopoteza sura? Nilinyofoa nyofoa moyo wangu kwa kuwasaidia wengine, nilionyesha matendo ya huruma na upendo kwa watu mbalimbali, lakini wengine hawakunirudishia, niliwatendea watu mema lakini wengine walinirudishia mabaya, kwa hiyo nilitafuta vipande vya nyama nyingine na kuziba sehemu za moyo wangu nilizowapa wengine,

Kijana alishangaa!

Nisikilize kijana wangu moyo wangu ni mzuri kama wa kwako tu unaona makovu haya? Kila kovu linawakilisha sehemu ya moyo wangu nilioutoa kwa wengine, wakati mwingine nilitoa kipande cha moyo kilichokuwa kikubwa zaidi, lakini sikurudishiwa! Kwa sababu niliowapenda wengine walinilipa mabaya, wengine hawakunirudishia, wengine waliuumiza moyo wangu zaidi wengine waliuchoma kwa mkuki na kuufanyia moyo wangu kila walichokitaka,Sehemu nyingine nilitoa moyo wangu wote na wakanirudishia kidogo au wasirudishe kabisa, sehemu nyingine niliwakopesha sehemu ya moyo wangu hawakurudisha aidha wengine niliwapa wakauchezea, nililazimika kuachilia kusamehe na kusahau na kuushona moyo wangu na kuuungauunga na kuutibu ndio maana moyo wangu una majeraha na makovu makubwa, na hauna sura nzuri ya kupendeza kama wako, Moyo wako wewe unaonekana kuwa mzuri kwa sababu hujawahi kutoa hata kipande ukawapa wengine je hili sio kweli?

Kijana alitulia kimyaa na akaishiwa maneno, alianza kutokwa na machozi, alimkumbatia mzee yule na kuuchana moyo wake na kumpa mzee yule kipande.

ISamuel 16:7Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.”

Watu wengi sana huangalia watu kwa umbile la nje na kuwasifu watu kwa umbile la nje lakini Mungu huangalia moyo, umeutumiaje moyo wako kwa wengine moyo wako umejaa nini utu wa mtu utapimwa kulingana na kile anachokitoa kutoka moyoni mwake je wewe unatoa nini kwa watu Mungu huitazama mioyo Marko 7: 15-23Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu.Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie.] Hata alipoingia nyumbani, ameuacha mkutano, wanafunzi wake wakamwuliza habari za ule mfano. Akawaambia, Hivi hata ninyi hamna akili? Hamfahamu ya kwamba kila kitu kilicho nje ya mtu, kikimwingia, hakiwezi kumtia unajisi; kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote. Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu.Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.”

Na mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima

Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni