Jumatano, 27 Septemba 2017

Hekima hupita Upumbavu!



Mstari wa Msingi: Muhubiri 2:3 “Ndipo nilipoona ya kuwa kweli hekima hupita upumbavu, kwa kadiri nuru ipitavyo giza



Utangulizi:

Wengi wetu tumewahi kusikia habari za Sulemani kwamba alikuwa mfalme mwenye hekima, lakini wengi wetu tunaweza tusiwe na uelewa wa kutosha kuhusu faida ya hekima, tunapojifunza somo hili fupi sana Pende tu utaiona faida ya Hekima na utagundua umuhimu wa kuomba Hekima.
Zamani sana katika inchi fulani watu waliishi kwa furaha chini ya mfalme mmoja, watu wa ufalme ule walikuwa na maisha ya furaha na amani na walibarikiwa kwa utajiri mwingi sana na hakukuwa na majuto.

Siku moja mfalme aliamua kufanya ziara katika maeneo ya kihistoria ya taifa lile na katika sehemu mbalimbali za makumbusho, aliamua kwamba atatembea kwa miguu ili kwamba apate nafasi ya kusalimiana na watu wake na kuwafahamu kwa ukaribu, watu wa maeneo mbalimbali walifurahia sana kupata nafasi ya kuongea na hata kumuona mafalme kwa ukaribu, walifurahi na kujivunia moyo mwema wa mfalme wao.

Baada ya majuma kadhaa ya ziara ya mfalme, hatimaye alirejea ikulu katika makazi yake, Alikuwa na furaha sana kwa ziara aliyoifanya na kwa kutembelea maeneno muhimu ya taifa lile. Alifurahi kushuhudia watu wake wakiishi maisha ya amani na furaha huku wakiwa wametajirika sana lakini jambo moja tu lilikuwa likimsikitisha sana.

Hakuweza kuvumilia maumivu katika miguu yake, na hasa kwa sababu ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufanya ziara ya miguu, alilalamika na kuwaelezea mawaziri wake na kuwaambia kwamba Barabara zetu sio nzuri na nyingi ni za mawe na hivyo yanaumiza sana, alisema nawahurumia sana wananchi wangu ambao wanatumia barabara hizo kwa sababu nao watapata au huwa wanapata maumivu kama niliyoyapata mimi.

Walipofikiri kuhusu hilo, Mfalme aliamuru watumishi wake kupitia wizara ya ujenzi watandaze ngozi katika barabara za nchi yake yote ili watu wa ufalme wake watembee kwa raha!

Mawaziri wote wa mfalme walishitushwa na jambo hili na wakawaza kwa agizo hili ili liweze kutekelezeka hatuna budi kuwa tutachinja ngombe wote inchi nzima ili kupata ngozi ya kutosha kutandaza katika barabara zote, waitafakari kuwa jambo hili litagharimu fedha nyingi sana.

Mwisho waziri mmoja mwenye hekima alikuja na wazo kwa mfalme na kumwambia mfalme nina wazo, Mfalme alimwambia sawa elezea wazo lako, Waziri yule alisema badala ya kufunika barabara zote kwa ngozi, kwa nini tusitumie kipande cha ngozi na kukikata vizuri kwa umbile la kupendeza kisha wewe uvae na kufunika miguu yako?

Mfalme alishangaa sana kwa wazo hilo na hekima aliyokuwa nayo waziri wake akaagiza atengenezewe viatu kwaaajili yake na kisha wakaamuru kila mtu katika ufalme ule avae viatu, watu wote wakaanza kuvaa viatu tangu wakati huo. 

Unaona huwezi kuubadili ulimwengu kabla ya wewe mwenyewe kubadilika!, kama tutakuwa na hekima tutaweza kutatua matatizo mengi sana katika kila eneo la maisha yetu kwa njia ya usahii zaidi, tunaweza kuwa na mawazo mazuri, lakini bila hekima mawazo hayo yakawa yanatumika vibaya na kutugharimu, nd ndio maana Mfalme Sulemani aliona kuwa ni Muhimu kwanza amuombe Mungu hekima 

1Wafalme 3:6-10Sulemani akasema, Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo. Na sasa, Ee Bwana, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia. Na mtumwa wako yu katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi. Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi? Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili.”

Tunawezaje kuwa na Hekima Biblia inasema tunaweza kumuomba Mungu Hekima lakini pia tunaweza kujifunza hekima

Yakobo 1:5Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa”.Unaona tunaweza kuwa na hekima kwa kumuomba Mungu, Mungu ndiye chanzo cha hekima na maarifa yote,  

Mithali 1:7Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.”

Na. Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni