Jumatatu, 18 Septemba 2017

Mfano wa kuku avikusanyae vifaranga vyake!


Luka 13:34.

Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka.”
 
Mathayo 23:37

Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka!

Utangulizi:

Leo tutachukua muda kujifunza na kutafakari kwa kina kuhusu maneno haya ya Yesu, ambayo kitaalamu inaaminika yalizungumzwa wakati Yesu anaulilia mji wa Yerusalem siku chache kabla ya kusulubiwa kwake 

Luka 19:41- 44 “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako 

wataalamu wengi wa kimaandiko tunaamini kuwa huenda Yesu alizungumza maneno yale pale juu katika wakati huu, ingawa waandishi waliyaweka katika vifungu vingine kwaajili ya kusisitiza umuhimu wa kile walichotaka kukiwakilisha chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu,  kwa vyovyote vile Yesu alikuwa akifanya maombolezo kwaajili ya jiji la Yerusalem ambalo lingeshuhudia hukumu kubwa miaka michache kama 37  ijayo,  Yesu alikuwa akiulilia mji wa Yerusalem kutokana na tabia yake ya kuwaua Manabii, wenye hekima na walimu,(waandishi). Lakini sio hivyo tu bali pia kulikuwa na mpango wa kumuua Yesu mwenyewe na Yesu alitambua mpango huo, sio tu Yesu angeuawa bali hata wale atakaowatuma wangeuawa 

Mathayo 23:34 “Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji

 Yesu alikuwa akitabiri kuwa tabia ya watu wa Israel kuwatendea vibaya manabii, siku moja ingefikia mwisho na kuwa hukumu kwaajili ya mji wa Yerusalem ingefika na kila kitu kingesambaratishwa, Yesu anatangaza hukumu mbaya sana katika Yerusalem na Israel kutokana na tabia na mwenendo wake mbaya wa kile inachokifanya dhidi ya watu wa Mungu. Lakini katika maonyo hayo  Mazito hakukuwa na nafasi ya rehema tena kwani neno la Yesu lilitimizwa sawa sawa na unabii wake Katika mwaka wa 70 AD Yerusalem uliteketezwa kwa moto na wayahudi waliuawa kila mahali na waliikimbia inchi yao mpaka waliporejea tena miaka ya 1940 na kupata uhuru 1948. Israel ilikuwa imekataa mpango wa Mungu. Miaka 27 tu ilipita tangu YESU alipopaa mwaka wa 33

Yesu katika maonyo yake alibainisha wazi sababu za Israel kuangukia katika hukumu ya Mungu ni kwa sababu ilikataa mpango wa Mungu wa upendo. Mungu alikuwa na Mapenzi mema na Israel kila ambacho Mungu alikuwa amekikusudia kimefichwa katika Mfano wa kuku akusanyaye vifaranga vyake 

Kwanini wakati huu Mungu anatumia mfano wa kuku avikusanyee vifaranga vyake? Ukweli ni kuwa kuku ana mambo kadhaa muhimu ya kujifunza na Yesu aliutumia mfano huu kwa sababu katika mazingira ya kawaida ya wakati huo Israel walifuga kuku sawa na mazingira ya kawaida ya kitanzania na Afrika kwa siku za zamani, kuku wa kienyeji walifugwa kwa njia ya asili na ya kawaida tofauti na nyakati za leo.

Mfano wa kuku avikusanyae vifaranga vyake 

Kuku anapotaka kuwa na vifaranga jambo la kwanza anataka mayai ya kutosha  Jambo hili linatufundisha MPANGO MWEMA – Mungu ana mpango mwema na kila mmoja kama alivyokuwa na mpango mwena na Israel Yeremia 29:11-13. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote”.


Kuku anapoanza kulalia ili aweze kutotoa anapunzuza mizunguko yaani hazuruli hovyo jambo hili linatufundisha kujitia NIDHAMU

Wakati kuku anapolalia mayai yake huwa anapungua uzito anakonda KUJIKANA 

Kuku anapolalia huwa hajali analalia mayai ya kuku mwingine au hata ya kanga yeye hulalia tu bila ubaguzi hii inatufundisha UKARIMU hana UBAGUZI wala UPENDELEO

Kuku ili aweze kutotoa anapaswa kulalia kwa siku 21 kwa kuvumilia hii inatufundisha UVUMILIVU

Kuku anapolalia anaweza kujua yai lenye kifaranga na yai lililoviza hii inatufundisha kuwa anauwezo wa KUPAMBANUA na KUTABIRI

Kuku baada ya kutotoa  anaacha mayai viza na anatunza vifaranga vyake hii inatufundisha kuwa kuku ana HEKIMA huwezi kumbeba asiyebebeka.

Hakuna anayeweza kukigusa kifaranga chake hii inatufundisha kuwa uko ULINZI WA MUNGU Na upendo wake na kujali

Anakusanya vifaranga vyake chini ya Mbawa zake ni hali ya kuhakikisha wanakuwa na UMOJA na kuwatunza hawagawanyi ili awatawale 

Hawezi kuwaacha mpaka wakue yaani inatufundisha kuwa kuku anafundisha UALIMU

Mungu alikuwa ana makusudi mema na Israel, alikuwa nawqwawazia mema na amani, Mungu alitoa muda wake kwa israel zaidi kuliko mataifa mengine, Mungu alimleta masihi kwa Israel na ulimwengu mzima ili, Mungu alitoa neema yake bila upendeleo, Mungu alikuwa akiwavumilia ili wazae matunda, Mungu aliamini kuwa siku moja watu wake watakomaa, Mungu alikusudia kuwa mwalimu kwa kila mmoja lakini kutokana na Israel kuendelea kukataa mapenzi ya Mungu, Yesu alitangaza hukumu,  na maangamizi kutokana na jeuri ya kuendelea kukataa maonyo na kuwakataa manabii.

Je ni mara ngapi tumekataa maonyo kutoka kwa watumishi wa Mungu  ambao Mungu aliwatuma kwetu kwa makusudi mema ni mara ngapi tumewaua na kuwapiga kwa mawe wale wanaotumwa kwetu, hali ya kutokukubali maonyo itatuletea hukumu ya Mungu

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni