Alhamisi, 5 Oktoba 2017

Hekima imejulikana kuwa na haki !


Luka 7:33 - 35Kwa kuwa Yohana Mbatizaji alikuja, hali mkate wala hanywi divai, nanyi mwasema, Ana pepo. Mwana wa Adamu amekuja, anakula na kunywa; nanyi mwasema, Tazama, mlafi huyu, na mnywaji wa divai, rafiki wao watoza ushuru na wenye dhambi. Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa watoto wake wote."
 


Utangulizi:-

Bill alikuwa ni mtu mwenye umri wa miaka ipatayo 40 na alikuwa akifanya biashara ya kuuza nguo, aliuza nguo za aina tofauti tofauti, kwatika miji na vijiji mbalimbali, siku zote alitumia punda kubeba mizigo ya nguo alizokuwa akiziuza.

Siku moja aliamua kumchukua kijana wake mwenye umri wa miaka 15 aliyeitwa Ron na kwenda naye katika miji na vijiji vilivyokuwa karibu,Punda alibeba behi mbili za nguo walizokuwa wakiuza, wote walikuwa na furaha kubwa sana Bill na Ron, baada ya kuuza na kufanya biashara kubwa sana na kupata faida , Bill alikuwa na furaha yeye na mwanaye ron na punda wao waliamua kurudi nyumbani.

Walitembea umbali mrefu sana mwishowe walichoka, wote watatu walitembea pole. Pole wakirejea nyumbani.

Watu wawili waliwaona wakiwa wamechoka sana, wakaanza kusema “angalia hawa wajinga wamechoka mbaya inavyoonekana, wana punda lakini kwanini mmojawao asipande juu ya punda wanapata shida ya bure hali wanaye punda si wangemtumia!”

Bill na Ron walisikia lililokuwa likizungumzwa na watu walke wawili kuhusu wao na Ron alimwambia baba yake apande juu ya Punda.

Alikubali na akakaa juu ya punda, lakini baada ya dakika chache Mzee mmoja alimuona Bill juu ya punda na akamwambia “we mzee huna hata huruma mwangalie kijana wako alivyochoka bado mdogo mno, wewe unapanda ju ya punda na unamuacha mtoto atembee ?”

Bill aliamua kumpandisha mwanae juu ya punda na wakaendelea na safari lakini baada ya muda kidogo Mgeni mmoja akapiga kelele akimkemea Ron “ weee bado ni kijana sana huwezi kutembea? Unaachaje mzee anatembea wewe kijana uko juu ya punda uvivu tu shuka haraka” 

Bill na mwanaye Ron walichanganyikiwa na wasijue nini cha kufanya, wakaamua wote wakae juu ya Punda na kuendelea ingawa punda alitembea kwa shida sana kwa vile uzito wao ulikuwa ukimuelemea.

Mtu mwingine akawaona kwa mbali akawakimbilia na kuwaambia kwa kupiga kelele akiwaambia Bill na mwanaye, hivi ninyi mna kichaa?inawezekanaje wote wawili mumpande punda mmoja je hamuwezi kutembea? Kwanini mnamtesa huyu mnyama?
Bill na Ron walishangaa sana wakanyamaza kimya kwa Muda.

Sio rahisi kumpendeza kila mtu, kila mmoja ana mawazo tofauti na maoni tofauti, ni vigumu kumpendeza kila mtu au kufuata wazo la kila mtu, wakati mwingine ni lazima kuamua kile tulichokiamua na kwa kweli fuata moyo wako na Mapenzi ya Mungu.

Mungu katika hekima yake amejaribu kwa kilanjia kuwapata wanadamu, alituma manabii kwa njia nyingi na kwa namna mbalimbali

Yohana mbatizaji alitumwa kwa Israel akihubiri mahubiri makali sana akiishi maisha ya kujikana, aliishi porini, akila nzige na asali ya mwituni, alivaa ngozi na singa za ngamia, hakuhudhuria sherehe za aina zozote, alionya kuhusu hukumu ya Mungu na kukemea dhambi akiwataka watu watubu na kugeuka kwa Mungu lengo kuu ikiwa ni kuwaleta watu kwa Yesu hata hivyo walisema ni kichaa ana pepo na hatimaye walimuua.

Yesu alikuja kwa kusudi la kuokoa alijichanganya na wenye dhambi alifanyika rafiki, alikula na kunywa naovyakula vyao vya kawaida na vinywaji vyao vya kawaida lakini hata hivyo walimuita mlafi.

Kristo anatufundisha kuwa Hekima ya Mungu imejulikana kuwa na haki kwa watoto wake, ni wazi tu kuwa kwa njia yoyote wanadamu hawapendi kuitikia wito wa Mungu aidha kwa kuwachezea au kwa kuwahuzunikia, ukiwaita kwa sherehe hawaji au ukiwaita kwa huzuni hawaombolezi,

Luka 7:31- 32. “Bwana akasema, Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Nao wamefanana na nini? Wamefanana na watoto walioketi sokoni na kuitana, wakisema, Tuliwapigia filimbi wala hamkucheza; tuliomboleza, wala hamkulia.”

Wanadamu hawana jema ukiwa mpole watasema huyu naye kazidi sana upole, ukiwa mkali watasema mmh huyu naye mkali mno, ni vema kila mmoja akatimiza kusudi la Mungu kama alivyokusudiwa na hii ndio hekima hatuwezi kuwa vile wanadamu wanavyotaka tuwe lakini tunaweza kuwa vile Mungu anavyotaka tuwe, Mungu alimuita Yohana kwa Kusudi lake na alimtuma Yesu vilevile kwa kusudi lake, hii ndio hekima ya Mungu, hatupaswi kujali watu wanasema nini timiza kusudi la Mungu uliloitiwa, Faida ya wito wako itaonekana baadaye.

Kikwete hawezi kuwa Magufuli na Magufuli hawezi kuwa Kikwete, Tulimuomba Mungu atupe Rais tumuachie atomize kusudi lile ambalo Mungu amempa kwaajili ya watanzania, iwapo Mungu angekuwa anataka mfumo uleule na aina ileile ya uongozi, angeachia mtu anayefanana na Kiwete atawale, hakuna anayeweza kusema yeye alikuwa Rais Mzuri zaidi ya mwingine kwa vile kila mmoja ameitwa kwa kusudi lake, Hali kadhalika katika Huduma, Mtume, Nabii, Mwinjilisti Mchungaji na Mwalimu, hakuna aliye mkubwa kuliko mwingine, kila mmoja anatimiza kusudi lake, Mtume hawezi kusema kuwa yeye ni mkuu kuliko Mwalimu kwa vile amefundishwa na mwalimu, Nabii, Mtume mwinjilisti wanalelewa na wachungaji Kanisani, ipi ni huduma iliyokuu ni ile inayohitajika kwa wakti huo. Na hii ndio hekima ya Mungu.

Sio rahisi kumpendeza kila mtu, kila mmoja ana mawazo tofauti na maoni tofauti, ni vigumu kumpendeza kila mtu au kufuata wazo la kila mtu, wakati mwingine ni lazima kuamua kile tulichokiamua na kwa kweli fuata moyo wako na Mapenzi ya Mungu.

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekim.

Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni