Jumanne, 3 Oktoba 2017

Maombi yenye Nguvu!


Wafilipi 2:3-4Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.”

 Musa Mtumishi wa Mungu mara kwa mara aliwaombea israel na kuwatanguliza wao kuliko yeye
 
Yakobo na Yohana walikuwa marafiki wa karibu sana, walikuwa majirani, walisoma pamoja kisha walikwenda chuoni pamoja na pia walipata kazi sehemu moja.

Siku moja waliamua kusafiri kwa meli kwenda katika visiwa vigeni, walianza safari yao na kuzunguka na meli na wakatokomea mbali sana, kwa bahati mbaya safari yao ilikumbwa na dhoruba kubwa sana kiasi ambacho meli waliyokuwa wakiitumia ilivunjika vunjika na baadhi ya abiria walikuwa, lakini hata hivyo Yakobo na Yohana walifanikiwa kuogelea kwa muda mrefu na kufikia moja wapo ya kisiwa kilichokuwa karibu.

Kisiwa hiki kilikuwa kama nyika tu hakukuwa na miti ya maana na Yakobo na Yohana waligundua kuwa hakuna uwezekano wa kuishi pale bila msaada wa Mungu, Hivyo waliamua kuomba Mungu aingilie kati, lakini waliambiana tuone ni maombi ya nani yatakuwa yenye nguvu? Yakobo aliamua kwena upane wa mashariki ya kisiwa na Yohana aliamua kwenda upande wa Magharibi wa kisiwa kila mmoja alidhamiaria kwenda kumuomba Mungu huko ili msaada utokee

Yakobo aliomba kwanza Mungu ampe chakula ili aweze kuishi, na mara akaona sahani ya chakula na matunda na mboga za majani na samaki, akaanza kula, 

Baada ya siku mbili aliomba apate mwanamke mzuri sana ili awe mke wake kwa vile alihisi upweke wa hali nya juu kule kisiwani, baada ya masaa machache kulikuwa na Meli iliyopata ajali karibu na kisiwa kile kwa mbali na ni mwanamke mmoja tu aliyeweza kupona katika ajali ile kwa kuogolea mpaka kisiwani na Yakobo alimpokea kama mke wake, sasa ikawa kila anachokiomba Yakobo anakipata.

Hatimaye kama mwezi mmoja ulipita tangu ajali ile ya meli itokee, Yakobo aliomba kutokee meli itakayomrudisha nyumbani yeye na mkewe, na kwa hakika ikatokea meli na kumchukua yeye na mkewe kurudi nyumbani.

Lakini walipokuwa wanakaribia kuingia katika lango  la meli, Yakobo alisikia sauti ikimwambia “Je unaondoka mwenyewe? Bila mtu muhimu katika maisha yako?” Yakobo alishangaa na kujibu hebu niambie unamaanisha nini ? mtu muhimu katika maisha yangu ni mke wangu na niko naye hapa!

Sauti ikamwambie mimi ndiye uliyekuwa ukiniomba na ndiye niliyekuwa nikijibu Maombi yako, ndiye niliyekupa chakula na kuyatunza maisha yako na hata huyo mke wako mimi ndiye niliyekupa, Yakobo alipiga magoti na kumwambia Mungu asante kwa fadhili zako zote.

Kisha Yakobo akamkumbuka Yohana ambaye alikuwa amekwisha sahau habari zake, na akajisikia vibaya 

Mungu akamwambia sikuwa najibu maombi yako kwa sababu ya wema wako, nilikuwa wakati wote nasikiliza maombi ya Yohana na kuyatimiza, Yohana wakati wote alikuwa akiomba ombi moja tu Mungu wangu tafadhali mkumbuke rafiki yangu Yakobo mtimizie kila anachokihitaji hayo ndio yalikuwa maombi ya Yohana wakati wote.

Yakobo alilia sana na alikimbia magharibi ya kisiwa kwaajili ya kumtafuta rafiki yake, alitambua kuwa alikuwa mbinafsi hakufikiri kuhusu wengine alijifikiria mwenyewe tu na kufurahia baraka zile, hata hivyo alipofika magharibi ya kisiwa hakumuona Yohana na Yakobo alimuuliza Mungu sasa yuko wapi Yohana Mungu akamwambia Nilimchukua na yuko name, Mtu mwenye moyo wa dhahabu kama Yohana anapaswa kukaa na mimi, lakini nitayatimiza maombi yake kama nilivyomuahidi.

Yakobo alijisikia vibaya sana na ndipo alipogundua kuwa rafiki yake ndiye aliyekuwa na maombi yenye nguvu kuliko yake, kwa sababu maombi yake, hayakuwa na hata chembe ya ubinafsi kama yak wake.

Maombi yenye nguvu ni maombi ambayo ndani yake hakuna chembe ya ubinafsi. Watu wakubwa katika maandiko hawajiombei wenyewe wanaombea wengine, Manabii waliokuwa rafiki wakubwa wa Mungu ni wale walioombea watu na sio kujiombea wenyewe, Mungu ampe neema kila mmoja wetu kuacha ubinafsi.

Kumbukumbu 9:18-20Nikaanguka nchi mbele za Bwana siku arobaini usiku na mchana, kama pale kwanza; sikula chakula wala kunywa maji; kwa sababu ya makosa yenu yote mliyokosa, kwa kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, kwa kumkasirisha. Kwa kuwa niliogopa hasira na makamio aliyowakasirikia Bwana kutaka kuwaangamiza. Lakini Bwana alinisikiza wakati huo nao. Bwana akamkasirikia sana Haruni akataka kumwangamiza; nikamwombea Haruni naye wakati huo.”

1Samuel 7: 5-9Samweli akasema, Wakusanyeni Israeli wote Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa Bwana. Wakakusanyika huko Mispa, wakateka maji na kuyamimina mbele za Bwana; wakafunga siku ile, wakasema huko, Tumemfanyia Bwana dhambi. Samweli akawaamua wana wa Israeli huko Mispa. Hata Wafilisti waliposikia ya kuwa wana wa Israeli wamekusanyika huko Mispa, mashehe wa Wafilisti walipanda juu ili kupigana na Israeli. Nao wana wa Israeli waliposikia, wakawaogopa Wafilisti. Wana wa Israeli wakamwambia Samweli, Usiache kumlilia Bwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, kwamba atuokoe na mikono ya Wafilisti. Ndipo Samweli akatwaa mwana-kondoo mchanga, akamtolea Bwana sadaka ya kuteketezwa nzima; Samweli akamlilia Bwana kwa ajili ya Israeli; Bwana akamwitikia.” 

Mafanikio yako wakati wote kumbuka kuwa kuna watu wanaoomba kwaajili yako na wala sio kwa sababu ya wema wako na Tunapoomba kwaajilin yaw engine Mungu hujishughulisha na mahitaji yetu pia.

Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni