Jumanne, 10 Oktoba 2017

Kufanya kazi kwa Bidii



Mithali 12:24Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipishwa kodi.”



Moja ya kusudi kubwa la kuumbwa kwetu sisi kama wanadamu ni ili tuweze kufanya kazi, hii ndio ulikuwa mpango mkuu wa Mungu kabla ya anguko la mwanadamu Mwanzo 2:15BWANA Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.” Agano jipya linakazia zaidi kuwa yeye asiyetaka kufanya kazi kula na asile 2Wathesalonike 3:10Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula.” Unaona biblia inatia moyo kufanya kazi kwa bidii, kufanya kazi kwa bidii ni ibada ya kwanza kabisa ambayo Mungu alikuwa amewakusudia wanadamu waifanye, Biblia iko kinyume sana na uvivu.Zaburi 128:2 “Taabu ya mikono yako hakika utaila; Utakuwa heri, na kwako kwema” unaonyesha kuwa Baraka za Mungu zinakaa katika kazi za mikono yetu.

Ujumbe.

Kulikuwa na mzee mmoja ambaye alikuwa na watoto wane wa kiume, hata hivyo kwa bahati mbaya watoto hao walikuwa wavivu.

Siku moja mzee huyu alianza kuugua sana na siku zake za kufa zikakaribia, alikuwa na hofu sana kuhusu maendeleo ya baadaye ya watoto wake kwani walikuwa wavivu na waliamini kuwa wana bahati kwa sababu ya mali ya baba yao.

Hali ya afya ya baba yao iliendelea kuwa mbaya siku hadi siku, na mwishoe mzee huyu aliamua kuwaita watoto wake na kuzungumza nao kuhusu maendeleo yao, lakini watoto wake hawakumsikiliza, Hatimaye mzee yule alipata wazo na akataka watoto wake watambue umuhimu wa kufanya kazi, aliwaita na kuwaambia kuwa alikuwa na box moja lenya mali za thamani kubwa sana la dhahabu na fedha na madini mengineyo ambalo alikuwa amewahifadhia na alikuwa anataka wagawame sawasaw.

Vijana walifurahi sana waliposikia kuwa baba yao ana mali nyingi kiasi kile kwaajili yao, Mzee aliendelea kueleza kuwa Tatizo kubwa sikumbuki ni wapi nilipoweka box hilo la thamani kwani alilizika kwenye ardhi yao shambani lakini amesahau kabisa aliliweka upande gani.

Hata hivyo vijana wavivu waliendelea kufurahia habari hiyo, ingawa walihuzunika tu kuwa mzee wao amesahau ni wapi alikoliweka, baada ya siku chache Mzee wao alifariki dunia, baada ya maziko vijana waliamua kulitafuta boxi la thamani, walifanya kazi kwa bidii wakichimba kila sehemu ya shamba lao, walichimba na kulima na kukata misitu na kujaribu kuchimbua kila mahali wakitafuta mali, hawakutaka kukodisha mtu kwani walijua wanaweza kuliona boxi na kuondoka nalo, hivyo walifanya wenyewe  lakini hawakufanikiwa kuona kitu.

Hatimaye waliamu kuchimba shimo kila pembe ya shamba lao na kwa bahati shimo moja walilolichimba lilitoa maji na chemichemi ikawa inabubujisha maji, Mtu mmoja alipita karibu na shamba lao na kuwapongeza kwa kugundua maji aliwashauri kulimba mboga mboga na kutumia maji hayo kumwagilia, vijana waliamua kulima mboga mboga na kumwagilia  na kuuza kwa watu mablimbali na walianza kupata fedha nyingi sana na wakawa matajiri wakubwa.

Hawakuweza kuliona boxi alilowaambia baba yao lakini hatimaye waligundua kuwa baba yao alikuwa amemaanisha wafanye kazi kwa bidii na kwamba kufanya kazi kwa bidii kunalipa. Walitambua kuwa kufanya kazi kwa bidii kuliwapa utajiri mkubwa.

Ndgu yangu Mungu anatutaka tufanye kazi kwa bidii, Mungu anataka kila tunalotia mkono wetu kufanya tulifenye kwa bidii, kusoma kwa bidii, kuomba kwa bidii, kazi, kwa bidii, kusali kwa bidii, kuabudu kwa bidii.

Kama tutafanya kila kitu kwa bidii Biblia inasema tutasimama mbele ya wafalme Mithali 22:29 “Je! Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme; Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo.”

Na. Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni