Jumanne, 10 Oktoba 2017

“Wala msimpe Ibilisi Nafasi”


Waefeso 4: 27Wala msimpe Ibilisi nafasi”.


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Kila mtu wa Mungu yuko katika vita na shetani, Shetani anatajwa katika maandiko kuwa ndiye adui yetu mkubwa yeye anatajwa kama simba aungurumaye akitafuta mtu apate kummeza  1Petro 5:8Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” Shetani amejaa hila na mbinu za kuwasumbua watu wa Mungu kila wakati na kuhakikisha kuwa hakuna mtu anaishi kwa amani au kukaa kwa amani hivyo ni muhimu tukawa tayari kupambana naye kila wakati Waefeso 6:11Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.” 2Wakoritho 2:11Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake”. Biblia inatufundisha kuwa tuna uwezo wa kumshinda kwa sababu tunazijua sana fikra zake yaani mbinu anazozitumia ili aweze kutushinda
Paulo mtume anakazia kuwa tusimpe nafasi, tusimpe mlango, tusiifanye njia yake kuwa rahisi katika kutujia na kutushambulia, tumnyime njia kwa kuangalia kuwa tunambana kiasi ambacho ni lazima asiwe na nafasi hata ya kuchungulia

Mtu mmoja alikuwa anauza nyumba yake kwa shilingi za kitanzania milioni 30. Na mtu mmoja akajitokeza akasema yeye atainunua nyumba hiyo kwa kuwa amaeipenda sana lakini yeye alikuwa masikini na hakuwa na uwezo wote wa kuinunua nyumba ile, hivyo alibembeleza sana sana ili auziwe nyumba ile, na hivyo mwenye nyumba aliamua kumuuzia kwa nusu ya bei yaani miliioni 15 lakini kwa sharti moja tu kwamba anataka awe anamiliki msumari mmoja uliokuwa sebuleni mwa nyumba ile nyuma ya mlango hivyo walikubaliana.

Baada ya miaka kadhaa yule mwenye nyumba wa zamani alitaka kuinunua nyumba ile tena, lakini mwenye nyumba mpya hakukubali kuiuza, kwa hiyo mwenye nyumba wa zamani aliondoka na baada ya muda alirudi akiwa na mzoga wa mnyama aliyekufa na akaomba autundike katika msumari anaoumiliki, mara nyumba yote ikawa inanuka na imejaa harufu mbaya na nyumba ile ikawa ngumu sana kuishi familia ile ililazimika kuiuza nyumba ile tena kwa mmiliki wa msumari

Hivi ndivyo ilivyo ikiwa tutakubali kumpa ibilisi nafasi hata kama nafasi hiyo ni ndogo sana, ayaitumia nafasi hiyo hiyo kutuharibia maisha yetu na uhusiano wetu, shetani hutumia vitu vidogo vidogo kuharibu uhusiano wetu hatupaswi kumpa nafasi kwa namna yoyote kutushambulia.

Mungu ametupa nguvu ya kumpinga shetani, Biblia inaposema wala msimpe ibilisi nafasi ni wazi kuwa jambo hili liko katika uwezo wetu, Mungu ametupa mamlaka juu yake tunaweza kumkatalia kabisa asituguse wala asimguse awaye yote katika maisha yetu, hii ina maana kuwa shetani anaweza kutukaribia iwapo tu tutamruhusu kutusogelea Yakobo 4:7 Biblia inasema “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.”

Uwe hodari na ushujaa mwingi uwe na imani na ujasiri, unapokuwa vitani hupaswi kumpa kisogo adui ni muhimu kumkabili uso kwa uso tukishindwa adui atafurahi, ssisi ndio tunapaswa kumpa shetani wakati mgumu na sio yeye atupe sisi wakati mgumu Luka 10:19 “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.”

Wakristo wengi sana huwa wanasahau kuwa zile dhambi zinazofikiriwa kuwa ndogo kwamba zinamadhara makubwa sana kwani kuna uwezekano kabisa mtu asiwe mlevi, au mwesharati, au mchawi, au mpiganaji lakini wakawa na mawazo machafu, wakawa na uadui, wakawa na husuda na wivu, wakawa na uchungu, na ulafi na uzushi, na mafarakano, na kufitiniana, na majungu, na kusengenyana na kusemana vibaya na hasira na kiburi na majivuno na kujisifu, hivi vinapuuziwa lakini vina madhara Makubwa kwani ibilisi anaweza kabisa kuvitumia kwa kusudi la kuharibu maisha yetu.

Bwana na ampe neema kila mmoja wetu kutokumpa ibilisi nafasi katika jina la Yesu amen!

Na mkuu wa wajenzi mwenye hekima.

Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni