Jumatatu, 23 Oktoba 2017

Kwa bidii si walegevu!



Mstari wa Msingi: Warumi 12:11kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;”

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa kila tunalolifanya duniani Mungu anataka tulifanye kwa bidii, kufanya kazi ya Mungu kwa bidii, kuabudu, kwa bidii, kuomba kwa bidii, kusoma kwa bidii, kufanya kazi za kawaida, kwa bidii Mungu anataka tuwe na bidii, tuwe na Juhudi, katika kila jambo, Haya ni mapenzi ya Mungu kabisa ni kanuni ya mafanikio. Kama mtu anataka kufanikiwa katika kila jambo basi ni muhimu jambo analolifanya likafanyika kwa bidii, Neno la Mungu linaunga mkono utendaji wa kazi kwa bidii na linaeleza faida za kuwa na bidii katika kila jambo.

Kwa kuanzia na Mstari wa msingi 

Warumi 12:11 SUV, Inasema kwa bidii, si walegevu, mkiwa na juhudi
Romans 12:11 NIV, Never be lacking in Zeal, but keep your spiritual fervor
Romans 12:11 KJV, Not slothful in business; fervent in spirit;

Neno hilo Kwa bidii, kwa juhudi katika Biblia ya kiyunani linasomeka kama AGONIZOMAI ambalo kwa kiingereza kuna maneno kadhaa yanaingiliana kuhusu neno hilo

Kwa ujumla maneno hayo yote yanakazia kufanya kazi kwa bidii, kufanya kazi kwa juhudi,kwa wivu, kwa moto, kwa muwako, kwa shauku, kwa viwango, kwa ufundi na kwa njia nyingine zozote lakini hakuna lugha ya kueleza vema katika Kiswahili zaidi ya kukazia bidii na juhudi, au kwa moyo wako wote.

Mfano Biblia inazungumza kumpenda Mungu kwa Moyo wetu wote

1.      Kumbukumbu 6:5Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.” Kwa maana nyingine Biblia inataka tumpende Mungu kwa moyo, kwa roho na kwa nguvu hii maana yake nini kwa bidii

2.      Yakobo 5:16Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.”Kumbe hata katika kuomba Biblia inatutaka tuombe kwa bidii unaona 

3.      Matendo 12:5Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake.” Maombi yaliyomtoa Petro gerezani yalikuwa ni maombi yaliyofanyika kwa juhudi

4.      Matendo 18:24-25Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu.” Apolo alikuwa hodari yaani alikuwa na juhudi na hata alipoanza kuhubiri alikuwa na “zeal” yaani alikuwa anawakwa anahubiri kuhusu Yesu kwa nguvu.

5.      Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;”Biblia inatutia Moyo vilevile ikitakam bidii katika kuwa na amani na watu wote, kumbe kila kitu kinahitaji bidii

6.      Mithali 8:17Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.” Biblia inatia moyo kwamba tumtafute Mungu kwa bidii, bidii inahitajika katika kila eneo

Kwa msingi huo basi kama kila kitu kitafanyika kwa bidii maana yake mafanikio ni lazima, ni lazima kila mwanafunzi ajifunze kusoma kwa bidii, wanaofanya kazi wafanye kwa bidii, “USITAMANI KUTEMBEA IKIWA UNAUWEZO WA KURUKA” “do not desire to walk when you have wings to fly”

Mfano:

Wakati fulani kulikuwa na Mfalme aliyekuwa mkarimu sana na mwenye moyo Mzuri, lakini pia alikuwa rafiki wa wanyama na ndege, aliwapenda kiasi ambacho hakufurahi hata kuona mnyama akichinjwa

Kutokana na ukarimu wake kwa wanyama na ndege siku moja mfanya biashara mmoja alimpatia  zawadi ya mwewe  wawili “Falcon” Mfalme alifurahi sana na kumuomba kiongozi wa wa mifugo kuwatunza mwewe hao wawili na kuhakikisha kuwa wanaishi kwa fuaha na faraja lakini wakiwa na uwezo na mpaka wawe na uwezo wa kuruka, kwani walikuwa hawawezi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na wakati wa ukamatwaji walipunguzwa baadhi ya manyoya ili wasiruke



Baada ya Muda Mfalme alitamani kuwaona mwewe wale wakiruka, lakini kiongozi wa mifugo alimueleza kuwa ni mwewe mmoja tu ndiye aliyeweza kuruka kwa kasi na huwa anarejea kwa kasi ya ajabu lakini mwingine hajawahi kuruka hata siku moja,

Mfalme alishangaa sana na alitoa zawadi kwa mtunzaji wa mifugo kutokana na kuruka kwa mwewe wa kwanza, hata hivyo alisisitiza kuwa ni lazima ahakikishe kuwa na mwewe wa pili anaruka. Lakini hata hivyo mwewe wa pili hakuweza kuruka bali alikaa tu kwa upole katika tawi la mti na kutulia alijaribu kila mbinu lakini ndege yule hakuweza kuruka.
Mfalme alimwambia usisikitike nitaita mtu mmoja atakayeweza kumfanya mwewe aweze kuruka mfalme alitangaza kama yuko mtu anayeweza kumfanya mwewe yule aweze kuruka ajitokeze na atapewa zawadi


Baada ya kusikia tangazo hilo Mzee mmoja wa miaka alijitokeza na kufika ikulu na kumuhakikishia mfalme kuwa yeye anaweza kumfanya mwewe kuruka, Mfalm,e alimuagiza mkuu wa wanyama kumchukua Mzee yule na kumpeleka kwenye eneo la mifugo na ndege na kuifanya hiyo kazi na kuwa yeye atatembelea siku inayofuata kuona itakavyokua na kama kuna mabadiliko.

Siku ya pili Mfalme alishangaa sana kuona kweli mwewe ameruka kwa mara ya kwanza  na akaenda mbali sana kwa spidi ya ajabu na kurejea, Mfalme alifurahi sana na kumpa zawadi mzee yule, kisha akamuuliza Mzee umewezaje kumfanya ndege huyu kuruka Mzee alicheka na kujibu Nilikata tawi alilokuwa analitegemea kwa kukaa.

Wengi wetu tuna mbawa za kurukia, tunajua kuruka na tunajua wapi kwa kurukia lakini tumekaa bila sababu na hatufanyi lolote na tunabakia duni.

Kila mmoja anaweza kufanya jambo kwa bidii, kila mwanafunzi anaweza kujisomea kwa bidii watu wengi na wanafunzi wengi wanao uwezo, wanauwezo wa kupata hata maxi kubwa zaidi ya hizi wanazozipata lakini kuna mahali wamekaa, 

Mithali 10: 4Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.” Ndugu hakuna muujiza wa mafanikio unaokuja kwa kuambiwa pokea! Pokea! Mafanikio yoyote yanakuja kwa kufanya kazi kwa bidii, Yeye aliye na sikio na asikie neno hili ambalo mkuu wa wajenzi anawaambia wasomaji wake.

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni