Jumatano, 24 Januari 2018

Mambo Muhimu saba unayopaswa Kujaa.


Mstari wa Msingi: Matendo 6:3-5


Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia;”  

 
Mungu kamwe hamtumii mtu ambaye yuko tupu, awaye yote ambaye yuko tupu ni rahisi kutumiwa na shetani na mapepo Mathayo 12: 43-45 “Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate. Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa.Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya.”

Yesu Kristo mwana wa Daudi kutoka katika ukoo wa Yese alitumiwa sana na Mungu kwa viwango kwa sababu Hakuwa tupu alijaa Roho Mtakatifu katika ukamilifu wake Isaya 11:1-2 “Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana;”

Mungu anataka kumtumia mtu aliyejaa mambo muhimu saba yafuatayo:-

1.        “Kujaa utimilifu wa Mungu”Be filled with the fullness of God.
Waefeso 3:14-19 “Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa, awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani.       Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu.

Kwa lugha nyepesi kusudi kubwa la Mungu ni kutupeleka katika hatua ya kuwa watu wazima, kukomaa kutokuwa wachanga kiufahamu na kiroho, kuwa wakamilifu kama Kristo Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.

Kujaa utimilifu wa Mungu ni kujaa ujuzi kuhusu Mungu na kuigiza kila kitu na kila tabia aliyokuwa nayo Yesu Kristo kwa sababu katika yeye na katika tabia zake na mtindo wake wa maisha tunajifunza utimilifu wa Mungu Wakolosai 2:9 “Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.

Kama utimilifu wa Mungu utajaa ndani yetu kuna faida kubwa sana nyingi tutakazoweza kufaidika nazo
a.       Tutajaaa upendo wenye kujitoa kwaajili ya wengine Yohana 15:13 “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu wa mtu kuutoa uhai wake kwaajili ya rafiki zake” Upedno wenye kujidhabihu kwaajili yaw engine PHILEO, STORGE, EROS,  AGAPE., Mother Teresa, Will Pooley and Maximilian Kolbe. Ni mifano ya kuigwa duniani katika upendo wenye kujitoa kwaajili ya watu wengine upendo wa aina hii hatuwezi kuwa nao kama hatujajaa utimilifu wa uungu ndani yetu tuone mifano ya watu hao:-

Mama Teresa wa Culcuta India (1910-1997) anaheshimika sana duniani kwa kuwahurumia wengine,alipewa nishani ya Nobel 1979,alianza akiwa masikini lakini alianzisha vituo vya ukarimu kwa ajili ya kuwasaidia yatima na wajane,wasiojiweza na wenye njaa, leo hii kuna matajiri wengi sana wasio na huruma kwa wengine wanaongoza kwa dhuluma na ufisadi wewe utalifanyia nini taifa upendo wenye kujitoa tu ndio  unaweza kukusaidia kuhisi maumivu ya wengine.

Daktari  mmoja wa Uingereza aitwaye Will Pooley alikuwa ni moja ya madaktari waliokuwa mstari wa mbele Nchini “Sierra Leone” huko walikuwa na wenzake wengi wakipambana na wagonjwa wa EBOLA na virusi vyake  katika  harakati hizo Madaktari wengi sana na Manesi wengi sana wakiwemo wa Afrika Magharibi waliambukizwa virusi vya ebola wakati walipokuwa wakiwauguza wagonjwa na wengi wao walikufa

Ugonjwa utokanao na kirusi cha Ebola ni ugonjwa hatari wenye uwezo wa kusababisha kifo kwa asilimia 90.  Shirika la afya duniani, WHO katikatovuti yake inasema kwa mara ya kwanza ulibainika mwaka 1976 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Sudan. Chanzo cha kirusi hiki hadi sasa hakijulikani lakini popo aina ya (Pteropodidae) wanaonekana kuwa wabebaji wa kirusi hicho, kwa mujibu wa ushahidi uliopo sasa.
Maambukizi hupatikana kwa kila aina ya majimaji yanayotoka katika mwili wa binadamu ni ugonjwa hatari na unaoua kwa haraka na hauna tiba
Will Pooley alipoupata ugonjwa huu alirejeshwa katika ndege maalumu na kuanza kutibiwa chini ya uangalizi maalumu huko uingereza

Jambo la kushangaza ni kuwa baada ya kupona kwa bahati tu Will Pooley alitangaza nia yake ya kurudi tena Sierra Leone kusaidiana na wenzake kupambana na ugonjwa huo.
Mtu huyu aliwashangaza wengi sana na kuwaogopedha wengi sana akiwa amepona kwa asilimia 100%alisema atarudi Africa kusaidia zaidi maana alizaliwa kwaajili ya hayo, jambo hili lilimfanya aandikwe kama shujaa na mwanadamu mwenye uwezo wa kujitoa kwa kiwango cha juu.

Maximilian Kolbe alikuwa ni Padre aliyetokea Poland aliuawa kama mfungwa tarehe 14 August 14,1941, Jeshi la wa NAZI waligundua kuwa baadhi ya wafungwa wamejaribu kutoroka na hivyo waliamua kuwaua wafungwa kadhaa, walijaribu kuwaua kwa njia mbalimbali, na hivyo walichagua wafungwa 10 ili wauawe na kifo chao kiliamuriwa kuwa kifo cha njaa, wafungwa waliamuriwa kujitoa mmoja mmoja yeye mwenyewe na mfungwa wa kwanza kuchaguliwa alijulikana kama Franciszek Gajowinczek mfungwa huyu alipochaguliwa alilia kwa huzuni kubwa akimtaja mkewe, watoto wake na familia yake na kusikitika kuwa hatowaona tena kutokana na swala hili Maximillian alisimama na kusogea mbele na kuomba afe yeye kwa niaba ya Franciszek ombi lake lilikubaliwa, wafungwa waliwekwa kizuizini kwa muda wa siku kadhaa bila kula wengine walikunywa mikojo yao ili waweze kuishi, Maximillian alikaa kwa wiki mbili bila kufa huku wengine wote wakiwa wamekufa, walimchoma sindano ya kufa hakufa na hivyo waliamua kukata kichwa Pope John Paul II alimtangaza kuwa Mtakatifu kutokana na moyo wake.
Hawa walijitoa maisha yao kwaajili ya wengine kutokana na upendo wenye kujitoa na kujidhabihu, Yesu Kristo aliyatoa maisha yake kwaajili yetu sisi nasi hatuna budi kujitoa kwaajili yaw engine katika upendo. 

b.      Tutajaa Unyenyekevu!
Yesu Kristo alikuwa mnyenyekevu lakini vilevile alikuwa mtii, aliyatii mapenzi ya Mungu hata katika namna yenye kuumiza, hakujihesabu kuwa ni Bora wala hakujikweza na hivyo Mungu alimheshimu sana Wafilipi 2:3-5 “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.  Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.  Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;”

Njia ya kuinuliwa na kupelekwa juu na Mungu ni unyenyekevu, kama tutajifikiri wenyewe kuwa ni bora kuliko wengine tutapoteza neema ya Mungu kwetu Mungu huwapinga wenye kiburi bali huwapa wanyenyekevu neema, Injili ilikuja kwaajili ya watu wanyenyekevu Luka 4:17-19 Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

Watafasiri wa Biblia za kiingereza na kiswahili walionukuu Yesu walikuwa na mawazo ya kufikiri kuwa Yesu alikuja kwa ajili ya masikini hivyo walitumia neno “Poor” hii haikuwa tafasiri sahii ya andiko hili kwa vile andiko hili lilinukuliwa kutoka katika kitabu cha Isaya mwenyewe anazungumzia wanyenyekevu na sio masikini, Isaya 61:1-3Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri WANYENYEKEVU habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao;”
 
Ukweli wa kibiblia unaonyesha wazi kuwa Mungu anafanya kazi na wanyenyekevu na anapendezwa nao na kuwapa neema na kuwaangalia Isaya 66:1-2Bwana asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani? Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.” 

Kama hatutakuwa wanyenyekevu ni vigumu kuhudumiana, ni vigumu kutambua uweza alionao mtu mwingine endapo kila mtu atajifikiri kuwa ni bora katika nafsi yake , lakini biblia pia inataka watu wenye umri mdogo kuwaheshimu wenye umri mkubwa  1Petro 5:5 “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;” 

Unyenyekevu ni nini hasa ?-  unyenyekevu ni hali ya kutokujifikiri kuwa wewe ni wa muhimu kuliko wengine, Humble or Humility ni hali ya kutokufikiri kuwa wewe ni bora kuliko wengine, hali ya kutokutumia mamlaka uliyo nayo kufanya lolote kwa mtu unayeweza hata kumdhuru.

Kwa Mungu hali hii inakubalika kama namna ya kujifunza kutoka kwa Yesu Kristo.    

c.       Hakutakuwa na Mafarakano!
Kama hatutakuwa katika utimilifu wa Mungu, kutakuwa na mafarakano kwetu, migawanyiko na hii ni dalili ya uchanga, nyakati za kanisa la kwanza huko Koritho kulikuwa na migawanyiko, watu walisahau kuwa wao ni kitu kimoja na wakaanza kushabikia wanadamu Paulo mtume aliwakemea 1Koritho 1:10-13a “Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo.  Je! Kristo amegawanyika?

Paulo mtume aliyakemea mafarakano haya na kuwaeleza wazi kuwa kama watu kanisa, familia, shirika lina mafarakano basi ni wazi kuwa hawajakomaa 1Wakoritho 3:1-9 “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye. Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe. Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu. kila mmoja katika mwili wa Kristo ana nafasi yake na hivyo hatupaswi kuwa na mafarakano na kufikiri kuwa fulani ni bora kuliko mwingine

2.       Kujaa Roho Mtakatifu. “Be filled with the Spirit.”

Hakuna jambo muhimu katika maisha ya mwanadamu na maisha ya Ukristo kama kujaa Roho Mtakatifu, katika maswala yaliyokaziwa sana na maandiko ni pamoja na kujaa Roho Mtakatifu biblia inasema katika Waefeso 5:18 Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;” Kwa nini ni Muhimu kujaa Roho Mtakatifu?  Mungu anatumia watu waliojaa Roho, ni muhimu sana kukubali kwamba maisha yetu yaongozwe na Roho Mtakatifu, Roho Mtakatifu akiyaongoza maisha yetu au akiachiwa aongoze maisha yetu tunakuwa na amani, tutakuwa na furaha, tutakuwa na ujasiri, hatutapoteza tumaini, tutakuwa wavumilivu, tutakuwa watu wema, tutakuwa wanyenyekevu au wapole. Na hakutakuwa na bahati mbaya katika maisha yetu Luka 4:1-2Na Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa.” Roho wa Mungu atatupa maisha ya furaha na ushindi hata kama utakutana na changamoto za aina yoyote, nyakati tulizonazo watu wengi sana wamekuwa wakilalamika na kushindwa kusimama katika nafasi zao kwa sababu ya kumuacha Roho pembeni, hii haimaanishi kuwa hawana Roho wa Mungu hapana, wanaye lakini hawataki kijizoeza maisha ya kuongozwa na Roho mtakatifu na wanataka kujiongoza wenyewe na hivyo wanashindwa na hivyo wanaishi maisha yasiyo na furaha,  Mtu aliyejaa Roho wa Mungu
·         Atakupa ujasiri wa kuwa shahidi wa Yesu Kristo hata kifo Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”

·         Anawezeshwa kufanya mambo ya kupita kawaida Matendo 6:8Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.”

·         Anapewa ujasiri wa kupita kawaida na kukuwezesha kushinda majaribu Matendo 4:8-13Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu.” 

·         Atakuongoza katika kweli ya neno la Mungu ili kwamba mjaribu asikushinde Yohana 16:13 Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

·         Atakufariji na kukushauri wakati wa maswala magumu Yohana 14:16Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;
3.       Kujazwa maarifa ya Mapenzi yakeBe filled with the knowledge of His will

Wakolosai 1:9Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni; Kuyajua mapenzi ya Mungu ni jambo la Muhimu, watu wengi sana wanashindwa kujua kuwa wanachokifanya au walipo ni mapenzi ya Mungu au hapana kwa kujaa neno lake na kulielewa na kulifahamu itatusaidia kuyajua mapenzi ya Mungu,  kila mmoja anahitaji kujua maarifa ya mapenzi yake
Angalia kwamba Paulo mtume anawaombea kanisa la kolosai ili wajazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa Rohoni, kumbe kwamba pamoja na kuwa tumeokolewa bado kuna maswala ya msingi tunapaswa kuyafahamu, mojawapo ni kujazwa maarifa ya mapenzi yake, ni nini maana ya maarifa ya mapenzi yake?
Nyakati za kanisa la kwanza katika Asia ndogo na ulaya kulikuwa na kiu kubwa sana kuhusu kujaa maarifa na falsafa za aina mbalimbali, watu walijaa maarifa ya maswala mbalimbali “Gnosticism” waliamini kuwa ukiwa na maarifa tayari umeokoka na kukosa maarifa ni dhambi, kwa vile walikuwa wameiamini injili Paulo sasa alitaka wajae maarifa ya mapenzi ya Mungu na waweze kuyaishi ni kama Paulo anawaambia kuwa maarifa pekee hayatoshi, lakini mtu akiyajua mapenzi ya Mungu atajua namna na jinsi ya kuenenda kwa hekima katika ulimwengu huu “Hekima ni matumizi sahii ya maarifa” “wisdom is the application of Knowledge” kwamba kama watajaa maarifa ya mapenzi ya Mungu na kuyatumia watakuwa na ufahamu wa maswala ya Rohoni pia kama Paulo anavyowaombea wakolosai ni wazi kuwa moja ya maombi muhimu ambayo tunaweza kuwaombea wenzetu ni pamoja na kujaa maarifa ya ujuzi wa mapenzi ya Mungu.

4.       Be filled with joy “Ujawe na Furaha”

2Timotheo 1:3-4Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana. Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha;”Ni ukweli ulio wazi kuwa waraka huu Paulo aliandika akiwa kifungoni akiwa anakaribia kunyongwa au kuuawa na huku ndugu wengi wakiwa wamemuacha huenda jambo hili lilikuwa limemliza sana Timotheo ambaye aliishi vema na Paulo mtume kama mtu na baba yakewakati huu Paulo anatamani sana kumuona Timotheo ili kwamba aweze kujawa na furaha, Kujawa na futaha ni mapenzi ya Mungu hususani tunapokuwa katika mapito ya aina mbali mbali Shetani anapenda kuona kwamba tunahuzunika na kukata tamaa ni furaha ya maadui pia kuona machozi yako lakini hupaswi kuhuzunika Biblia inasema kama tunafanya kwaajili ya Bwana basi furaha ya Bwana ndio nguvu zetu Nehemia 8:10Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu. Biblia inaamuru tuwe na furaha siku zote  1Wathesalonike 5:16Furahini siku zote;” Shetani na maajenti wake siku zote watataka uwe na huzuni usikubali hakikisha kuwa unapigania furaha yako kwa gharama yoyote.

5.       “Jaa imaniBe filled with Faith 

Mtualiyejaa imani hi mtu wa kiwango kingine na kamwe hapotezi mwelekeo hata siku moja mtu aliyejaa imani anaona kwa mlango wa sita wa fahamu ambao wengine hawaoni, mtu wa imani anaona kuwa aliyekufa amelala tu, uwezo wa mtu wa imani ni tofauti na uoni wa mtu wa mwilini, mtu wa imani anakuwa imara zaidi wakati wa maswala magumu kwa vile anaona upenyo mahali ambapo wengine hawaoni, Stefano alikuwa moja ya watu mashujaa waliokuwa tayari kufa kwaajili ya kristo kwa vile alikuwa anaona kwa uhakika kuwa kifo ni hatua ya kumpeleka sehemu nyingine yeye anasifiwa katika maandiko kuwa mtu aliyejaa imani  Matendo 6:5 “Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia;” Biblia inasema pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, Mungu anataka mwenye haki wake aishi kwa imani na akisistasita roho yake haina furaha naye Habakuki 2:4Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake.”
Imani ni nini hasa? Waebrania 11:1 “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.Mungu anataka tujawe na imani imani inaleta kujitegemeza kwa Mungu na kuonyesha nguvu ya mtu anayemtegemea Mungu na huleta utukufu kwa Mungu.

6.       “ mjazwe  Neema”Be filled with Grace 

Nyakati za kanisa la kwanza walikuwa na ufahamu sana kuhusu umuhimu wa neema na hivyo mara kwa mara moja ya Baraka kubwa sana iliyotolewa na mitume ilikuwa ni pamoja na kuwatakiwa watu neema angalia  1Koritho 1:3 Neema na iwe kwenu, 2wakoritho 1:2 Neema na iwe kwenu,Wagalatia 1:3 Neema na iwe kwenu, Waefeso 1:2 Neema na iwe kwenu, Wafilipi 1:2 Neema na iwe kwenu, Wakolosai 1:2 Neema na iwe kwenu,2Thesalonike 1:2 Neema na iwe kwenu, Tito 1:4 Neema na iwe kwako, Filemoni 1:3 Neema na iwe kwenu, Je unadhani ni kwa nini Neema inaonekana kuwa ni kitu cha Muhimu na Baraka kubwa sana ? neema ikiwa juu yako wewe sio mtu wa kawaida, wewe utatenda maajabu na mambo ya kushangaza, watu wote na mashujaa wote wa biblia walikuwa ni watu waliojaa neema, ukiwa na neema wewe una ngekewa, wewe una bahati, wewe ni wa tofauti, utapata kibali kwa Mungu na wanadamu, Mungu mwenyewe atakutumia kwa viwango vya kupita kawaida ni muhimu kwetu kumuomba Mungu atujaze neema, neema itatuwezesha kutenda mambo makubwa chini ya uvuli na msaada wa Mungu Yesu alijaa neema, Stefano alijaa Neema , Paulo mtume alijaa neema, Musa alipata neema na wote walifanyamambo makubwa duniani na katika mwili wa kristo

Matendo 6:8 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. “ Luka 2;40 “Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.” Yohana 1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”  Ni watu waliojaa neema tu ndio walioweza kutumiwa na Mungu kwa namna ya kutisha na kushangaza, kama mtu anataka mafanikio ni muhimu kujitafutia neema ya Mungu, ukijazwa neema wewe ni tajiri wa ajabu wewe utatenda mambo makuu na hakuna mtu anaweza kushindana na mtu aliyepewa neema Paulo mtume alipewa neema kubwa sana na Mungu na akafanya kazi kubwa sana ya kulijenga kanisa kwa mafundisho yake 1Wakoritho 3:10 “Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake.” mwenyewe alitambua wazi kuwa alikuwa amepewa neema kusimamia ujenzi wa kazi ya Mungu na kuweka msingi ambao ni yesu Kristo. Musa alijaa neema Kutoka 33:12 “Musa akamwambia BWANA, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu.” Bwana na ampe kila mmoja wetu kujaa neema katika jina la Yesu Kristo amen

7.       “Ujazwe wema” Be filled with goodness. 

Warumi 15:14. “Ndugu zangu, nimehakikishwa mimi mwenyewe kwa habari zenu ya kuwa ninyi nanyi MMEJAA WEMA, mmejazwa elimu yote, tena mwaweza kuonyana.” Paulo mtume alikuwa badohajaonana na wakristo waliokuwa Rumi lakini alikuwa amesikia sifa zao kuwa wamejaa wema , ni muhimu kwa kila mmoja kujiuliza katika maisha yake kuwa amejaa nini? Watu wanasema nini kukuhusu, je wewe ni mwema? Mtumishi wa Mungu Tito  na mwenzake walikuwa watu wema na sifa zao zilienea  makanisani na sehemu mbalimbali Munhgu anataka tujae wema wako watu wengine kila unakokwenda unasikia habari zao aidha njema au mbaya , wengina hata kabla hujawaona unasikia habari zao, je wewe umejaa wema una sifa za aina gani kila mahali, wengine wana sifa mbaya,  nimewahi kufika mahali nikasikia watu waliomba yule hata akifa sitalia,yule afadhali afe hiki ni kiwango kibaya sana cha sifa haiwezekani watu watatu au wane waseme tunatamani afe Wakristo wanapaswa kuwa na sifa nzuri kila mahali 2Wakoritho 8:16-21 “Lakini ahimidiwe Mungu atiaye bidii ile ile kwa ajili yenu katika moyo wa Tito. Maana aliyapokea kweli yale maonyo; tena, huku akizidi kuwa na bidii, alisafiri kwenda kwenu kwa hiari yake mwenyewe. Na pamoja naye tukamtuma ndugu yule ambaye sifa zake katika Injili zimeenea makanisani mwote. Wala si hivyo tu, bali alichaguliwa na makanisa asafiri pamoja nasi katika jambo la neema hii, tunayoitumikia, ili Bwana atukuzwe, ukadhihirike utayari wetu. Tukijiepusha na neno hili, mtu asije akatulaumu kwa habari ya karama hii tunayoitumikia; tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za Bwana tu, ila na mbele ya wanadamu.

Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuweza kujawa na mambo haya ya msinhgi saba katika jina la Yesu Kristo

Na Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni