Jumapili, 1 Julai 2018

“Imeandikwa Mtu hataishi kwa Mkate tu”


Andiko la Msingi: Mathayo 4:3-4Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate. Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu”.



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Katika majaribu ambayo Yesu amewahi kupitia, Jaribu la kugeuza mawe kuwa mkate lilikuwa limekaa vizuri sana katika kumtega Bwana Yesu ili atende dhambi, Jaribu hili ndilo ambalo lilikuwa na uwezo mkubwa sana wa kufanikiwa, kwa sababu Yesu alikuwa amethibitishwa wazi  na hadharani tena na Mungu mwenyewe kuwa yeye ni Mwana wa Mungu Mathayo 3:17na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Na Hapa ni kama anapewa wakati muafaka na mzuri wa kuonyesha kwamba yeye kweli ni mwana wa Mungu ulikuwa ni wakati sahihi kabisa kwanza kumuonyesha shetani kuwa yeye ni nani, pili alikuwa na njaa tena amechoka,tena ana uhitaji, tena yuko peke yake, tena masikini, na ana uwezo wa kufanya muujiza na zaidi ya yoteni Mwana wa Mungu na uhitaji ulikuweko ilikuwa ni kama ujinga kwamba hutumii mamlaka kubwa uliyonayo hivi ndivyo shetani alivyokuwa akimjaribu Yesu, Yesu kama mwana wa Mungu ilikuwa ana wajibu wa kutoa amri tu au kutamka neno tu na kuonyesha nguvu zake na angefanya kusingelikuwa na tatizo.

Yesu alikuwa na uelewa Mkubwa sana alitambua kabisa kuwa anajaribiwa kama Adamu wa Kwanza, Ili apoteze kibali kwa Mungu, Yesu alijua kuwa anapaswa kulitii Neno la Mungu, na kufuata maelekezo ya Roho Mtakatifu Mpaka dakika ya mwisho, kwa vile ndiye aliyemuongoza ili ajaribiwe, Kama Yesu angeshindwa wokovu ungekuwa wa taabu sana, Utii wake ulikuwa unapimwa kama ulivyopimwa wa Adamu, Adamu alishindwa kulitii neno la Mungu, na hivyo akaleta mauti, Yesu aliweza kulitii neno la Mungu na hivyo akaletauzima

Jibu la Yesu kwa kweli lilikuwa tamu sanaNaye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Munguwote tunafahamu umuhimu wa Chakula kwamba hakuna uhai bila kula, tunajua kuwa hatuwezi kustahimili maisha na shughuli zetu za kila siku bila chakula, au maswala yanayotupatia Chakula, Lakini Yesu alionyesha kuwa Mwanadamu hataishi kwa chakula tu, kuna jambo lingine muhimu zaidi ambalo ni neno la Mungu, ni muhimu tu kujiuliza kwa nini neno la Mungu ni Muhimu? Kuliko chakula?

1.       Neno la Mungu lina Nguvu, lina uwezo mkubwa sana kama Moto na uwezo mkubwa sana kama nyundo ya kuvunjia mawe Yeremia 23:28-29 “Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana.  Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?Mungu anaonyesha ya kuwa Neno lake lina nguvu, ili maisha yetu yaweze kufanikiwa ni muhimu kuzungumza neno katika kila aina ya jaribu na mapito tunayoyapitia, tafuta neno la Mungu na lizungumze katika hali yoyote inayokukabili, tunaweza kuikabili haliyoyote ile katika kwa kulitamkia neno.

2.       Neno la Mungu ni Upanga wa kiroho Waebrania 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.”Neno la Mungu linasifiwa hapa kuwa lina UHAI, LINA MGUVU, KALI KULIKO UPANGA UKATAO KUWILI,LINACHOMA, LINAWEZA KUGAWANYA NAFSI, ROHO, VIUNGO, NA MOYO  Hivyo linaweza kutumika kuzima mishale yote ya adui na kila elimu inayojiinua na Elimu ya Utukufu wa Mungu

3.       Neno la Mungu ni kweli, Ukweli ni silaha yenye nguvu kuliko silaha zozote, Shetani hutumia uongo kutushambulia lakini kweli ina nguvu, kweli ni silaha kuu kwa mujibu wa Maandiko,Waefeso 6:10-14 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuaniKama tunataka kuwa washindi wakati wote na kupata matokeo yaliyo thabiti hatuna budi kuhakikisha kuwa tunasimama katika kweli ya Neno la Mungu, Neno la Mungu lina uwezo wa kutakasa na kumfanya mtu wa Mungu akamilike Yohana 15:3,  17:17

4.       Neno la Mungu ni Roho tena ni uzima Yohana 6:63 “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.”Yesu alikuwa akimaanisha kuwa Neno analotupa yeye lina uzweza linanufaisha roho na sio mwili, Torati ya Musa ilikuwa na manufaa ya kimwili lakini Maneno na mafundisho ya Kristo yana nufaisha roho yana uzima ndani yake, Biblia inaonyesha ya kuwa kila kitu kitapia lakini neno la Mungu litasimama milele, ni neno la Milele, Kila mtu anayetaka kufanikiwa katika jambo lolote anapaswa kuliishi neno, kuliangalia neno, kulitazama neno, katika mazingira yoyote ishi kwa neno, Acha kuangalia nafasi uliyonayo, uanafunzi ulionao, cheo ulicho nacho akili ulizo nazo, Uzima wetu umewekwa katika neno, likitumika kwa halali shetani anajua kuwa lina nguvu na analiogopa neno.

Hitimisho:
Kama Yesu angetii maneno ya shetani na kugeuza mawe kuwa mkate maana yake angekuwa amelikataa neno la Mungu sawa na adamu na angekuwa ameyakubali maneno ya shetani kama Eva
Kila mmoja wetu anapaswa kuishi sawasawa na neno la Mungu, kila siku hatuna budi kuishi na sawa na neno la Mungu, Chakula cha siku moja tu kinatosheleza mahitaji ya mwili usio wa Milele lakini neno la Mungu linautoshelevu wa milele, Liseme neno. Liishi neno. Lihubiri neno litumikie neno, litendee kazi neno, liamini neno, litumie neno la MUngu na utaona faida kubwa sana katika maisha yetu, Mtu hataishi kwa Mkate tu Bali kwa kila neno litokalo katika Kinywa cha Mungu.

Ushindi wa Yesu Kristo ulitokana na ufahamu wa neno, maisha yetu na mafanikio yetu yamefungwa katika neno Yoshua 1:5-8 Biblia inasema “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.”  
          
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Rev. Innocent Kamote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni