Jumapili, 15 Julai 2018

Enyi kizazi kisichoamini!

Mathayo 17:14-20Nao walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia magoti, akisema, Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. Yesu akajibu, akasema, ENYI KIZAZI KISICHOAMINI, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu.  Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.” 



Imani binafsi ambayo haionekani kufanya kitu wakati wa matatizo hiyo sio Imani sahihi –W. Willberfoce

Utangulizi:

Mungu anamtarajia kila mwanadamu, aliyeitwa naye kuwa mwenye uwezo wa kuleta suluhu kwa matatizo yanayoizunguka jamii yake, Kusudi kubwa la Mungu kulichagua kanisa ilikuwa ili kanisa liweze kuwa na majibu ya changamoto zote katika jamii, Mungu anataka watu wenye uhodari, wanaoweza kutatua matatizo yanayoikabili jamii, alipokaa na wanafunzi wake alikuwa na matarajio ya jinsi hii hii, Lakini kama ilivyo kwa jamii ya leo na kanisa la leo, Wanafunzi wake pia walishindwa kutatua na kumaliza changamoto zilizowasilishwa kwao na mtu mmoja katika jamii. 
       
Katika Mistari ya msingi tunaona Wanafunzi wa Yesu wanaletewa kijana wa Pekee na Mzee mmoja, kijana huyu anateswa na Mapepo na kumtupa kila wakati, na ni lazima alimjeruhi, Baba wa mtoto ameingiwa na mashaka makubwa kwani anakosa tumaini anaona atapoteza kijana wake wa pekee ambaye shetani anamsumbua, Swala hili linatokea kuwa kitu cha kusikitisha kwa wanafunzi wa Yesu na inakuwa ni aibu kuwa wanashindwa kutatua tatizo hili, Yesu hakuweko karibu wakati huu alikuwa pamoja na wanafunzi watatu Petro, Yakobo na Yohana,  Hivyo wanafunzi tisa wanajaribu kutoa pepo wanashindwa hii ilikuwa mbele ya umati mkubwa wa watu, Tatizo halikuwa jipya kwa vile Walikutana na changamoto kama hii na Yesu aliitatua  

Marko 1:23-27Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii!”  na pia Marko 5:1-9Wakafika ng'ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi. Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu;  makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo;kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe. Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia;  akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese. Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu.  Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi” 

Lakini vilevile Yesu alishawapa Mamlaka ya kufanya kazi hii Mathayo 10:1, Lakini hapa wanashindwa, Yesu anatokea na kila mmoja ana furaha kwani Yesu aliweza kutatua tatizo, lakini wanafunzi wa Yesu hawakuweza kutatua tatizo lililokuweko, Swali kuu linazaliwa nao, Yesu anajibu kwa kukemea Enyi kizazi kisichoamiana. 

Kwanini sisi hatukuweza kumtoa? 

Yesu hakuwaambia kuwa tatizo liko kwenye mioyo yenu, Tatizo haikuwa kwamba kuna kanuni fulani haijatumika, Maana wengine mpaka wayaimbie Pambio mapepo kwanza, Tatizo sio kuwa hawakuwa na bidii, au kuwa hawana uzoefu, au hawakujaribu sana, wala sio kwa sababu hawakuwa na nguvu za uuongu ndani yao hapana, Yesu anawaambia ni” kwa sababu ya Upungufu wa Imani yenu” 

Math 17:20 “Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.”

Kanisa linapaswa kuelewa kanuni za utendaji wa Mungu

1.       Mungu hufanya miitikio yeke kwa Mtu anayemwamini, watu wanaomwamini Mungu wanaitwa “Risk takers” watu wenye uwezo wa kufanya maamuzi magumu, ni wenye ujasiri wa kutatua matatizo pasipo hofu ni watu ambao hawana shaka ni watu ambao wanamuamini Mungu na uwezo wake na hivyo kuchukua hatua za hatarishi, Ibrahimu, Musa, Joshua, Daniel na wengine wote walimuamini Mungu Waebrania 11:6 Pasipo imani haiwezekani kumpendeza Neno la Mungu linasema Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”

2.       Mungu anataka tumuamini na kumtegemea Kama tunataka kuona kazi zake zikitendeka 

kwetu haijalishi tatizo ni baya kiasi gani au kubwa kiasi gani lakini nini kinaendelea moyoni mwako? Kinachoendelea ndani yako ni cha muhimu kuliko kinachotokea nje yako, Moyo wako unakuawaje unapokutana na changamoto, je unaogopa? Au una ujasiri ukijua kuwa Mungu yuko pamoja nawe hupaswi kuogopa, Yesu hajali ukuu wa tatizo, kuwa limeanza tangu utoto, au ni la ukoo mzima au limelishinda taifa zima Yesu haogopi hilo wala haangalii hilo, haijalishi Madaktari wanasemaje, Mzee alipomuona Yesu alimwambia ukiweza unaweza kutusaidia, Yesu alishangazwa na mashaka makubwa aliyokuwa nayo baba yule, kweli ilikuwa ni kizazi kisichoamini, Ukiweza? Yesu alimjibu Yote yawezekana kwake aaminiye Marko 9:22-23 “Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize; lakini ukiweza neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia. Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye”.

3.       Mzee aliomba Naamini nisaidie kutokuamini kwangu, zinapotokea changamoto, hatupaswi kuangalia ukubwa wa changamoto,  uweza wa changamoto au muda wa changamoto bali tunapaswa kumsihi Mungu atuongezee imani aondoe mashaka ndani yetu, wakati tunapokabiliana na changamoto zozote acha kuwaangalia wanadamu, acha kuangalia ukubwa wa tatizo, acha kuangalia umati wa watu, acha kufadhaika Muamini Mungu muamini na Bwana Yesu kila kitu kitakuwa shwari.

4.       Ni imani kiasi gani inahitajika kwetu? Kimsingi kwa vile tatizo lilikuwa kubwa na lina historia ya kutisha basi wanafunzi walifikiri wanahitaji kuwa na imani kubwa sana  na hivyo labda jibu sahihi la Yesu lingekuwa kwamba kwa vile tatizo ni kubwa basi mnahitaji imani kubwa sana au kuongezewa imani, Lakini ni dhahiri wanafunzi wa Yesu na hata mzee yule hawakuwa na imani kabisa, walijifikiri kuwa wao ni watu maalumu, Yesu alisisitiza kuwa na imani na sio kuhusu size au kipimo cha imani, Ni lazima tumuamini Mungu kwa kiwango cha juu sana na kuacha kujiamini sisi, tusiangalie umaarufu wa dhehebu letu, muda wa kutembea na Yesu, umaalumu wa aina ya huduma uliyo nayo, uzoefu katika huduma, uwezo wetu wa kumtii Mungu au sheria za Mungu bali namna na jinsi unavyomtegemea Mungu chini ya neema yake, Lazima tumwangalie yeye kwa kuwa yeye Hashindwi kitu Luka 1:37 “kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.”

Enyi Kizazi kisichoamini.

Mara nyingi tunaweza kuona kuwa kuna tofauti kubwa kati ya kizazi kilichopita na kizazi cha leo kwa sababu ya imani, Inaonekana kama Mungu aliwatumia sana wazee wetu kuliko anavyotumia watu leo, Matamanio ya Mungu ni kuona watu wakimtumaini Mungu kwa uzito zaidi nyakati za leo na kutumiwa na Mungu kwa kiwango kikubwa katika nyakati za leo kuliko zamani, lakini shida Kubwa ni Hiki kizazi kisichoamini, Yesu alikemea Enyi Kizazi kisichoamini, Mungu anajua kuwa matatizo ya dunia hii na shuda zinazoukabili ulimwengu zinaweza kutatuliwa na watu waliamuamini na wanaomtumaini Mungu sio katika kutoa pepo tu bali kutatua matatizo ya wanadamu. 

-          William Wilberforce –  Alizaliwa 24 August 1759 – 29 July 1833 alikuwa mwanasiasa huko Uingereza na alijulikana kama kiongozi mwenye ushawishi aliyeendesha mpango wa kukomesha Biashara ya utumwa, alikuwa ni mbunge wa jimbo la Yorkshire kati ya mwaka 1784 – 1812, mwaka 1785 aliokoka na kumuamini Yesu kuwa Bwana na Mwokozi, jambo ambalo lilimpelekea kubadilika kabisa katika mtazamo wake wa maisha  na kusukumwa katika kupinga na kukomesha biashara ya utumwa, alipata elimu yake katika chuo cha ST Johns College cha Cambridge. 

-          Elisha aliweza kutatua Matatizo ya Mjane mmoja katika jamii yake na kukomesha kabisa tatizo lililokuwepo kwa Neema ya Mungu “ 2Wafalme 4:1-7” 

-          Dunia ina matatizo Mengi yanayohitaji ufumbuzi leo, Utunzaji wa Mazingira, Matumizi  mazuri ya ardhi, uwepo wa kemikali hatarishi, ugaidi, magonjwa, umasikini, shida za kisiasa, uongozi, uchumi, maji, ukame, ubaguzi, mauaji, kutekwa, ujangili, wizi, ujambazi, uchawi, uadui, Mafarakano, talaka, watoto wa mitaani, Elimu duni, picha za ngono, na kadhalika, Yesu anataka watu wote wamuamini Mungu na kutumia uhusiano walio nao nay eye kwa imani katika kutatua matatizo ya watu, Hatuwezi kumtumia yesu Kristo kwa kutafuta umaarufu naye akakubali, Kila msomi anayesoma shule ya seminary anapaswa kuwa mtu atakayekuja kutatua matatizo ulimwenguni na kuleta mabadiliko kwa jina la Yesu.

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima 
Rev. Innocent Kamote 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni