Jumatatu, 23 Julai 2018

Pesa Katika Mdomo wa samaki

Andiko: Mathayo 17:24-27

Hata walipofika Kapernaumu, wale watozao nusu-shekeli walimwendea Petro, wakasema, Je! Mwalimu wenu hatoi nusu-shekeli? Akasema, Hutoa. Naye alipoingia nyumbani, Yesu alitangulia kumwuliza, akisema, Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? Kwa wana wao au kwa wageni? Naye aliposema, Kwa wageni, Yesu alimwambia, Basi, kama ni hivyo, wana ni mahuru. Lakini tusije tukawakwaza, enenda baharini ukatupe ndoana, ukatwae samaki yule azukaye kwanza; na ukifumbua mdomo wake utaona shekeli ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kwamba hapa duniani, kila mtu anahitaji fedha kwaajili ya kutimiza mahitaji yake, Bila fedha wakati mwingine ni vigumu kukidhi mahitaji yetu yote,kwa kadiri siku zinavyokwenda na hali ya uchumi inabadilika na kwa sababu hiyo fedha inazidi kuwa ngumu sana, na maisha yanabadilika mno na kwa sababu hiyo fedha zinahitajika ili wana wa Mungu wasiweze kukudhalilisha, kutokana na kukosekana kwa fedha,

Yesu anatoa suluhu namna ya kupata fedha katika muujiza huu
Muujiza wa Yesu, kumtuma Petro kuvua samaki na kupata fedha unaonekana kutajwa katika Injili ya Mathayo pekee, penginepo kwa vile yeye alikuwa mtoza ushuru, ingawa watoza ushuru hawa hawakuwa mawakili ya serikali ya Rumi bali walikuwa watoza ushuru kwaajili ya ujenzi wa Hekalu.
Watoza ushuru wa Hekalu walimuuliza Petro kama Mwalimu nwao analipa kodi ya hekalu nae aliwajibu kuwa analipa,Petro aliporejea Yesu alizungumza naye kuhusu swala aliloulizwa kuhusu kodi

Naye alipoingia nyumbani, Yesu alitangulia kumwuliza, akisema, Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? Kwa wana wao au kwa wageni? Naye aliposema, Kwa wageni, Yesu alimwambia, Basi, kama ni hivyo, wana ni mahuru.” Yesu alikuwa akimaanisha wao kama wana wa Mungu wako huru wasingelipaswa kulipa kodi ile, lakini ili aiwakwaze watoza ushuru, Yesu alitoa maagizo kwa Petro nini anapaswa kufanya ili kukidhi hitaji hilo la kulipa kodi, tunaona Yesu akimuelekeza Petro kwenda kutupa Ndoana na kuvua samaki na samaki yule wa Kwanza angekuwa na fedha ambayo ingetosha kulipa Kodi yake na Petro. Watu wengi na walimu wengi wa neno la Mungu hawasemi mengi kuhusu muujiza huu,

Lakini mimi naona yako mambo ya kujifunza katika muujiza huu
1. Wote tunahitaji fedha kwaajili ya kukidhi mahitaji mbalimbali tuliyonayo katika Maisha
2. Wote tunahitaji fedha kwaajili ya kumuabudu Mungu na kumtumikia
3. Wote tunahitaji fedha kwaajili ya kulipia ada za shule za vijana wetu
4. Wote tunahitaji fedha kwaajili ya hatima ya wale wanaotuzunguka na wanaotutegemea
5. Wote tunahitaji fedha kwaaji ya kujiwekea hadhina mbinguni, tunapomtolea yeye na kuwapa wajane na masikini, na kutunza wazee wetu, na kuukuza ufalme wa Mungu.

Kama Petro na Mwalimu wake hawangelipa Kodi hii wangedhalilika, watu wangemsema Yesu, kuwa anajifanya mtu wa Mungu lakini halipi kodi ya Hekalu, hivyo Yesu anatambua kuwa watoto wake wanapokosa fedha wanadhalilika, wanaingia katika fadhaa, na hivyo alimuelekeza Petro nini cha kufanya.

Yesu alifanya Muujiza huu kuonyesha kuwa ana nguvu dhidi ya Fedha, “Jesus Has power over money” Yeye anauwezo juu ya fedha, Tatizo kubwa la watu wengi wa Mungu leo hawajawahi kumuambia Yesu kuwa wanashida ya fedha, linapokuja tatizo la fedha haraka sana hapo ndipo watu wengi sana hutumia akili na kuanza kusugua vichwa vyao, sio tu kusugua vichwa pia huanza kuumia moyo, na kuingia hofu na hata kulalamika, Tumesahau kabisa kuwa Mungu wetu anauwezo wa kutusaidia kama alivyomfanyia Petro .

Ni muhimu kufahamu kuwa Yesu ana uwezo juu ya fedha, Biblia inaeleza wazi kuwa yeye ingawa alikuwa tajiri alifanyika Masikini ili sisi tuwe matajiri 2Wakoritho 8:9 “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.”

Biblia inatufundisha kuwa ni yeye anayetupa nguvu ya kupata utajiri Kumbukumbu 8:18 “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.”

Biblia inaonyesha kuwa Petro alikuwa na uhitaji na hivyo huenda alimtaarifu Yesu kilichotokea, kwa ufupi alimuomba, kuhusu uhitaji wa kulipa kodi kwamba wanadaiwa kodi, na Yesu alijibu maombi hayo, kwa msingi huo kama tunavyoomba kwaajili ya mahitaji mengine tunahitaji pia kumuomba Mungu atupe fedha ili tusidhalilike.

Biblia inasema Hamna kitu kwa sababu hamwombi ni lazima tumuombe Mungu kwaajili ya hali ya uchumi wa familia zetu na mahitaji yetu, Sala ya Bwana inasema utupe leo riziki yatu ya kila siku, riziki yetu ya kila siku haiwezi kupatikana bila kuhusisha fedha je tumewahi kuomba fedha?

labda wengi tumefungwa na ile dhana ya fundisho la shina la mabaya yote ni kupenda fedha, lakini biblia inamaanisha kupenda fedha kuliko Mungu, na haimaanishi kuwa watu wake hawahitaji fedha, hapa mimi nazungumzia ule uhitaji fedha wa kawaida, kama ilivyokuwa kwa Petro anadaiwa kodi, labda huenda na wewe unadaiwa kodi ya nyumba, ama una madeni, ama unadaiwa ada ya watoto wako na kadhalika haja za namna hii ni vema pia Mungu akazijua, wengi hunijia wakitaka maombezi ya namna mbalimbali, lakini sijawahi ona mtu akinijia kuomba maombi apate fedha, wengi linapokuja swala la uhitaji wa kifedha, wanatumia akili zao wenyewe na wanaishia kupata msongo wa mawazo, huku haja hiyo ikiwa haijawasilishwa kwa Mungu, kutokumwambia Mungu uhitaji wetu wa kifedha ni daharau, ni sawa na kufikiri kuwa labda swala la kupata fedha Mungu haliwezi, lakini maandiko yanasemaje yote yawezekana kwa Mungu. kwa nini unasumbuka hali neno la Mungu linasema

Wafilipi 4: 6 maandiko yanasema “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.”

Je umewahi kumuomba Mungu waziwazi kwamba akupatie fedha ? umewahi kumuombea Mumeo, mkeo, wazazi, ndugu zako wawe na upenyo wa kifedha? Lazima tumuombe Mungu katika hitaji hili.

Mathayo 7: 7-11 Biblia inatukumbusha kuwa, Mungu ni Baba mwenye upendo ambaye huwapa watoto wake Mahitaji kwa kadri walivyoomba.

Anauliza je ni nani kati yenu mwanaye akiomba mkate atampa Jiwe? Au akiomba samaki atampa nyoka? Nauliza umewahi kumuomba Mungu akupe fedha ? au umetamani tu kuwa na fedha kwa kutumia akili zako mwenyewe bila kumwambia Mungu

Anamalizia kwa kusema " kama ninyi mlio waovu mwaweza kuwapa watoto wenu vipawa vyema je si zaidi sana Baba yenu Wa Mbinguni .........'' Hivyo kile tunachokiomba ndicho tutakachopokea.

1 Petro 5: 7 maandio yanasema wazi kuwa, Mungu hujishughulisha Zaidi na Mambo Yetu na hivyo tumpe yeye Fadhaa/haja zetu.

Anasema.
7 huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.
Kama utasema hujui namna ya kuomba hususani kuomba fedha kwa Mungu basi fuata muongozo wa mambo ya kuombea:-

Mambo ya kuombea:
• Omba Mungu akuweke mbali na Madeni, Yesu na Petro hapa walikuwa wanadaiwa kodi ya hekalu. na petro alipatwa na fadhaa
• Omba Mungu akusaidie usiwe mzigo kwa wazazi wako
• Omba Mungu kwamba akupe fedha nyingi kuliko matumizi
• Omba Mungu kwamba uwe na uwezo wa kukopesha na sio kukopa
• Vunja roho ya umasikini, kataa mikosi inayoendana na kipato chako
• Kataa roho ya umasikini na magonjwa na masumbufu
• Kemea Roho za wizi, hasara, mikosi, chuma ulete, kukopera na jicho baya, Mwambie Mungu akupatie ulinzi wa kutoshja katika mali zako.

Mwambie Mungu atumie ujuzi aliokupa au atakaokupa kukupa fedha

Yesu alitumia ujuzi aliokuwa nao Petro, kumpatia fedha, Petro alikuwa Mvuvi kabla ya kumtumikia Mungu, kwa kuwa mwanafunzi wa Yesu. Hivyo Yesu alitumia ujuzi na kipawa alichokuwa nacho ili kupata fedha ya kulipa kodi. alimuagiza aende akavue samaki na muujiza ulikuwa ndani ya samaki wa kwanza atakayevuliwa, kumbe fedha zetu ziko katika midomo ya samaki, ni lazima twende kwenye ujuzi ule tulionao tuweze kuzitoa fedha zetu huko na kukidhi mahitaji yetu tuliyo nayo
Fanya kazi kwa bidii, ile kazi aliyokupa Mungu fanya kwa uaminifu, fanya kama unamtumikia Mungu yeye anasema atazibariki kazi za mikono yako.

Yesu hakumwambia Petro akacheze Biko wala tatu mzuka hii ni michezo ya watu waliokata tamaa, wanaishi kwa kubahatisha, ni michezo ya watu masikini, wanaoishi kwa ndoto za mchana, wakitarajia kitu kutoka kwa miungu ya bahati nasibu, Mungu hajatuleta duniani ili tuishi maisha ya kubahatisha kanuni kuu za mafanikio ziko katika kazi naujuzi au kipawa ulichopewa na Mungu huko ndioko pesa yako iliko,

Biblia inatutaka tufanye kazi kwa bidii, Pesa iko katika mdomo wa samaki. Lakini ni lazima ukavue, ukienda kuvua samaki yule utakayemvua ana pesa mdomoni mwake, za kukidhi mahitaji yako ya ya jamaa zako, Nikutakie uwajibikaji mwema na Mungu aibariki kazi ya mikono yako Amen. Nakukumbusha kuwa fedha yako iko katika midomo ya samaki endenda ukatupe ndoana.

Na.Rev. Innocent Kamote
 
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni