Jumapili, 14 Oktoba 2018

Kurejeshwa kwa chuma cha Shoka!.



2Wafalme 6:5Lakini mmojawapo alipokuwa katika kukata boriti, chuma cha shoka kikaanguka majini; akalia, akasema, Ole wangu! Bwana wangu, kwani kiliazimiwa kile.”

Moja ya jambo baya kabisa kuliko yote Duniani ni pamoja na kukata tamaa, Mtu awaye yote hata awe na uwezo vipi, awe na pesa vipi, awe na akili vipi, awe na imani, vipi, awe na uzoefu vipi, awe na nguvu vipi na awe na karama na vipawa kiasi gani, au awe na elimu kubwa kwa kiwango chochote kile, ikitokea tu mtu huyu amekata tamaa, kwa vyovyote vile hakuna atakachoweza kukifanya, Kwa ufupi naweza kusema miongoni mwa mambo mabaya sana Duniani ni Pamoja na kukata tamaa. 



Unapofikiri kuwa Ndoto zako zimezama kumbuka Mungu ana nguvu za kushinda ngvu ya mvutano

Mtu mmoja alisema hivi “when we have lost everything , including hope life becomes disgrace and death a duty” Yaani “tunapopoteza kila kitu ikiwemo tumaini, maisha yanakuwa mabaya sana na kifo tu ndiocho kinachofuata” 

Ndoto za wana wa manabii.

2Wafalme 6:1-3Kisha, wana wa manabii wakamwambia Elisha, Angalia basi, mahali tukaapo mbele yako ni padogo kwetu. Basi twende mpaka Yordani, twakuomba, tutwae huko kila mtu mti mmoja, ili tujifanyie huko mahali pa kukaa. Akajibu, Haya! Nendeni. Mmoja wao akasema, Uwe radhi, basi nakusihi, uende pamoja na watumishi wako. Akajibu, Nitakwenda.”

Wana wa manabii waligundua kuwa sehemu waliyokuwa wanaishi ilikuwa ni ndogo na kuwa walihitaji kujitanua zaidi, ama nyumba walizokuwa wakiishi zilikuwa zimechakaa na sasa walikuwa na mawazo ya kufanya upya kila kituili kukidhi mahitaji ya wakati ule waliokuwa nao, waweze kujifunza vizuri katika shule za kinabii.

Hili linatufundisha kuwa walikuwa na Ndoto, walikuwa na maono ya kutaka kuingia katika level nyingine, hawakuwa wanataka kubaki palepale kwa hivyo walihitaji kukua zaidi, kwa kawaida kila mwanadamu hafurahii kudumaa, anahitaji kujipanua, anahitaji kwenda katika kiwango kingine kila mtu mwenye akili timamu hawezi kukubali kubaki pale alipo na hivyo atakuwa na mawazo ya kuongeza kiwango cha kule anakotaka kufikia hiki ndicho tunachoweza kujifunza katika maisha ya watu hawa wa Mungu, walihitaji kujiongeza.

Walieleza wazo lao kwa Mtumishi wa Mungu, naye aliwakubalia, lakini kwa kufahamu umuhimu wake walimuomba aende pamoja nao, Elisha hakuwa mwenye kuanzisha wazo hili lakini alikubali kuwasaidia kwa kuwepo kwake wao walitambua kuwa mtu wa Mungu ni wakili wa Mungu na anamwakilisha Mungu na hivyo waliona vema waende pamoja naye naye aliwakubalia.

Chuma cha shoka chazama majini.

2Wafalme 6:4-5Basi, akaenda pamoja nao. Nao walipofika Yordani, wakakata miti. Lakini mmojawapo alipokuwa katika kukata boriti, chuma cha shoka kikaanguka majini; akalia, akasema, Ole wangu! Bwana wangu, kwani kiliazimiwa kile”.

Wakati kazi ya kukata miti kwa matumaini ya kufikia ndoto zao inaendelea mara chuma cha shoka cha mojawapo ya wana wa manabii kilianguka na kuzama katika maji yo mto Yordani, hapa ndipo matumaini yalipoweza kutoweka kwa nabii huyu mwanafunzi, unaweza kuona akilia kwa kukata tamaa, yeye alikuwa ameazima chuma kile ili zweze kujikomboa na kujikwamua lakini mambo yanaharibika, hii ni sawa na mtu aliyechukua mkopo Bank na kuamua kuanzisha biashara ili aweze kupata faida kisha mtaji ule wa kuazima unaharibika na anapata hasara hana namna ya kurejesha mkopo ule, au mzazi alikopa ada ili kijana asome, lakini matokeoa ya kijana hayaridhishi, ama aunampeleka kijana shule ya seminary ukitegemea kuwa atabadilika kisha unashangaa kijana anabadilika tabia zainakuwa mbaya hata walimu wanashangaa, kile ambacho ulikuwa unakitegemea kinazama kwenye maji, ulikuwa unategemea kazi na ukadhani kazi hiyo ndio itakayokutoa kimaisha, baada ya Muda mfupi unaambiwa huna kazi, ulikuwa unamtegemea mtu fulani, kwamba angekuwa msaada mkubwa katika maisha yako anageuka adui yako, waswahili wanasema “Cha kuazima haisitiri makalio” Hiki ndio kilicjowatokea wana wa manabii, Ndoto zao zilianza kufifia sasa walikuwa wakitazamia Deni kubwa na namna ya kulilipa, katika nyakati za Elisha Chuma kilikuwa ninjambo adimu sana haikuwa rahisi kwa mtu wa kawaida kununua chuma au shoka ilikuwa ni bidhaa adimu sana ni wazi kuwa ndugu huyu aliyepoteza chuma alikuwa na uchungu sana alimumia mno kilio chake kilikuwa kilio cha kweli kwamba amepoteza chuma tena kumbe hakikuwa chake kilikuwa kimeazimwa, hii ilikuwa ni tukio baya zaidi pale ambapo mtu alikuamini akakukabidhi mali yake kisha ikapotea je utaeleza nini atakapokidai? Nabii huyu aliamua kulia na Mtu wa Mungu nabii Elisha ili aweze kuleta msaada unaohusika je tunawezaje kurejesha deni la gharama kubwa kiasi hiki? Nabii aliona hakuna njia nyingine zaidi ya umasikini tu unaomkabili alilia kwa uchungu Ole wangu Bwana wangu kiliazimwa kile alilia maandiko yanasema.

Kurejeshwa kwa chuma cha shoka!

2Wafalme 6:6-7 “Mtu wa Mungu akasema, Kilianguka wapi? Akamwonyesha mahali. Akakata kijiti, akakitupa pale pale, chuma kikaelea. Akasema, Kiokote. Basi akanyosha mkono, akakitwaa.”

Baada ya kilio chenye uchungu ni jambo la Kumshukuru Mungu kwamba hawakuenda peke yao, hali ingekuwa mbaya sana walikwenda na nabii Elisha mtu mmoja alimwambia mtu wa Mungu twende pamoja nawe, na sasa kumbe limetokea tatizo wanaye wa kumlilia ni mtu wa Mungu wanamueleza kuwa ile kitu iliazimwa ile kitu ni bei ghali, ile kitu itanifanya niwe mtumwa, Mtu wa Mungu alikata kijiti akakitupa pale shoka ilipozama na chuma cha shoka kikaelea, Nilikuwa najiuliza kuhusu kijiti, kujiti hiki ni cha namna gani na kuna uhusiano gani kati ya kijitoi na muujiza huu mkubwa? Nikakumbuka kuwa Musa alipoona maji ni machungu na wana wa Israel wanalia kuhusu maji, Mungu alimwambia Musa atupe kijiti katika maji na maji yale yakawa matamu, na sasa hapa Elisha anatupa kijiti na shoka linaelea, hakuna uhusiano wowote wa kijiti kufanya Muujiza, Lakini kuna uhusiano wa imani na kile kijiti, Hii ndio ilikuwa nbguvu ya uponyaji wake Msalaba pekee hauwezi kutusaidia kitu lakini imani kwa kile kilichofanyika msalabani inaweza kutubeba, Mungu yupo kutusaidia na kufanya muujiza lakini hata akisababisha chuma kuelea ni muhimu kufahamu kuwa tunapaswa kukiokota wenyewe 

Mungu anaweza kufanya mambo yote kwa imani katika kristo Yesu, hatuna budi kumuamini Yesu na kwenda pamoja naye kila tuendako na kumuita pale tunapohitaji msaada wake na kuonyesha tatizo pale lilipotokea, Kila mmoja anapaswa kufanya wajibu wake na Mungu naye atafanya sehemu yake kama hatutafanya sehemu yetu tunaweza kushindwa kufikia malengo, Mungu nageweza kufanya muujiza shoka likawa mkononi mwa nabii mwanafunzi lakini Nabii alimtaka aokote shoka yeye mwenyewe. 

Hatupaswi kukata tamaa tunaye Mungu mwenye uwezo wa kufanya yasiyowezekana lazima tumuamini Mungu na kufanya yaliyo wajibu wetu nasi tutaziona Baraka zake!  Wakati tunapofikiri kuwa ndoto zetu zimezimika Mungu anayo njia ya kuzuia nguvu ya kumeza ndoto zetu, wakati watu wanapofikri kuwa tumezama yeye atatuinua tena.Tunaye Mungu mwenye uwezo wa kuinua upya ndoa zetu, kujenga upya mahusiano yaliyoharibika, kuhakikisha kuwa kila kiti kinakaa sawa na matumaini yote yaliyozama kuyainua tena 

Mungu mwema mtumishi wako ninakuomba kwa unyenyekevu mkubwa inua upya matumaini ya msomaji wangu, huyu popote ambapo chuma cha shoka kimezama na matumaini yametoweka nakusihi kwa imani ukaliinue tena shoka lake ili aendelee na ndoto zake na kutimiza mahitaji yake na makusudi ya maisha yake asante kwa sababu najua ya  kuwa siku zote unanisikia, na hata sasa kwaajili ya mwanaume huyu, na mwanamke huyu anayesoma habari hii njema muinue kwa upya katika Jinala Yesu Kristo Bwana na Mwokozi wetu amen!

Na. Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.

Maoni 2 :