Jumatatu, 15 Oktoba 2018

Maisha ya Nabii Yusufu:


1.Timotheo 4:12 “Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.”


Yakobo alikuwa makini wakati wa Kuweka Mikono Mkono wa kuume ni Yule unayekusudia kumfanya kuwa kicha na Mkono wa Kushoto ni Yule unayekusudia awe mdogo Je wachungaji nwa leo wanaweka vipi Mikono? Wakati wa kubariki Ndoa ua viongozi wa kanisa, usiweke mikono hovyo hovyo kuna kanuni Yusufu na Yakobo walizijuaMwanzo 48:1-22

Utangulizi:

Maisha ya Yusufu ni moja ya Maisha ya mfano, na ya kuigwakatika Biblia, Tunaona Biblia ikizungumza kwa upana kuhusu uumbaji kwatika Mwanzo 1-2, wakati Mwanzo 3 pekee ikizungumzia Anguko la Mwanadamu, Mwanzo 4-5 habari ya kaini na Habili pamoja na kuongezeka kwa maasi, Mwanzo 6-9 Ni habari za Gharika na Nuhu mtu wa Mungu, Mwanzo 10-11 ni habari za Mnara wa Babeli na kutawanyika kwa mataifa, Mwanzo 12-24 ni Habari za Ibrahimu baba wa Imani,  Mwanzo 25-36 Kidogo Isaka, Esau lakini zaidi sana Yakobo, Mwanzo37:1-50:26 Ni habari za Yusufu, Kwa hiyo utaweza kuona Kuwa Neno la Mungu linamzungumzia Yusufu kwa upana na urafu zaidi, huku Biblia ikiwa haijawahi kuonyesha uzaifu wowote aliokuwa nao Yusufu, Kuna kitu cha ziada cha kujifunza katika maisha yake.

Yusufu anapewa Madaraka makubwa sana Katika Biblia, Miongoni mwa mababa wa Isarel Yusufu ni Mmojawao “The Patriarchs” hii ilikuwa nafasi ambayo labda Ruben angepewa Lakini kutokana na uaminifu wa Yusufu baba yake alimpa mbaraka huu kwa hiyo wakitajwa Mababa wa taifa la Israel basi Yusufu Ni mmojawao

a.      Abraham baba wa imani
b.      Isaka Mwana wa Ahadi
c.       Yakobo (Israel) Baba wa taifa la kiyahudi baba wa Kabila 12 za Israel
d.      Yusufu Mwokozi wa Israel na Misri Baba wa Kabila mbili za Israel Manaseh na Efraimu

Pamoja na umuhimu wao wote utaweza kuona habariza Yusufu zinaandikwa kwa kina zaidi kuliko wengine na hakuna dhambi yoyote inaonyeshwa kuhusu Maisha ya Yusufu, Maisha yake yenye uadilifu wa hali ya juu, Usafi wa Moyo, na maisha, kutokulipiza Kisasi, kuelewa vema makusudi na mipango ya Mungu, kuna mfanya kuwa mtu wa kuigwa miongoni mwa watu wa agano la kale na kufananishwa na Yesu Kristo kwa kile alichokifanya kwa ulimwengu.

Tutajifunza somo hili Muhimu kuhusu Maisha ya yusufu kwa Kuzingatia vipengele vine vifuatavyo:-

1.      Maisha ya Yusufu Katika nchi ya kanaani
2.      Maisha ya Yusufu Katika Nchi ya Ugeni kama Mtumwa
3.      Maisha ya Yusufu Katika Nchi ya Ugeni kama Mtawala.

Maisha ya Yusufu Katika Inchi ya Kanaani.

A.     Alichukiwa na Kaka zake
a.      Alifanya kazi za baba yake kwa bidii na uaminifu Mwanzo 37:2
b.      Alitoa ripoti ya kazi zilizofanyanyika kwa baba yake Mwanzo 37:2
Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya”.
c.       Yakobo alikuwa na wana kumi na mbili na binti mmoja, Dina (Mwanzo 29:31;30:24; 35:16-18). Wanawe walikuwa:-
·         Wana wa Lea: Reubeni, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zabuloni
·         Wana wa mjakazi wa Lea (Zilpa): Gadi na Asheri
·         Wana wa Mjakazi wa Raheli (Bilha): Dani na Naftali
·         Wana wa Raheli: Yusufu na Benyamini
d.      Kutokana na uaminifu wake pia mzaliwa wa kwanza wa Raheli mke aliyependwa sana na Yakobo, Baba yake alimpenda sana na kumtengenezea vazi maalumu Mwanzo 37:3-4, Maisha ya Yusufu sio yalimpendeza babaye tu Bali hata Mungu na hivyo Mungu alisema naye kuhusu Maisha yake ya baadaye Mwanzo 37:5-11, Mungu alisema naye kwa Njia ya Ndoto kuhusu kusujudiwa na ndugu zake, yaani kuwa mfalme dhidi yao lakini wao walimchukia upeo.
e.      Yusufu aliuza Misri baada ya kunusurika jaribio la kuuawa Mwanzo 37:12-36
f.        Ruben alitaka kumuokoa lakini Mpango wake ulishindikana Mwanzo 37:21-22
g.   Yuda alitaka kumuokoa nduguye na kifo kwa kutoa wazo auzwe utumwani Mwanzo 37:26-27 na mpango wake ulifanikiwa
Yusufu alimtii baba yake na hakutaka kuwapendeza ndugu zake kwa kufunika maovu yao, Pamoja na Yusufu kufanyiwa mabaya na ndugu zake aliendelea kuwa mwaminifu hata mbali na mzazi wake huko Utumwani Misri.

Maisha ya Yusufu Katika Nchi ya Ugeni kama Mtumwa

A.     Mungu alikuwa pamoja naye
a.      Alinunuliwa kama mtumwa katika nyumba ya Potifa, Mungu alimpa kibali Mwanzo 39:1-6, aliweza kuwa mwenye kuleta faida na Baraka na kuaminiwa
b.      Yusufu alikuwa Mzuri sana “Handsome” kwa sababu hiyo alivutia watu akiwemo mke wa Potifa Mwanzo39:b-20
c.       Mara kwa mara au mara kadhaa mke wa Potifa alimjaribu Yusufu ili alale naye
d.      Lakini Yusufu alikataa kwa sababu alimuheshimu Potifa lakini alimuheshimu Mungu pia Mwanzo 39:8-9
Je wewe kama kijana wa leo unaliweza hili? Leo hii ulimwengu umebadilika wanawake wenye uwezo wa kifedha kama ilivyo kwa potifa wanafuata vijana wadogo wanawashawishi na kutembea nao wanaviita “VIBENTEN” zamani Serengeti Boys, sio rahisi kwa vijana kushinda katika hili, maswala ya mapenzi ni yenye kvutia sana hususani kama mwanamke ndiye anayekutongoza, inawezekana pia haikuwa rahisi kwa Yusufu na ndio maana alikimbia na kuacha vazi lake huko Biblia inasema “Ikimbieni Zinaa” 1Wakoritho 6:18 “Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.”
1.      Kutokana na singizio hilo Yusufu aliwekwa Gerezani
2.      Hasira za Potifa ziliwaka juu ya Yusufu.

B.      Maisha ya Yusufu Gerezani.
a.      Mungu aliendelea kuwa Pamoja na Yusufu Mwanzo 39:21-23
b.      Alipata kibali mbele ya mkuu wa Gereza na kuamini wa sana
c.       Alifanikiwa katika kila alilolifanya
d.      Alijihusisha na maisha ya ndani kabisa ya wafungwa wenzake aliwaonea huruma na alijua kusoma nyuso zao ili kujua kuwa wana huzuni, wana furaha na amani au la?, Mungu alimpa karama ya neno la Maarifa na aliitumia kuweza Kufasiri Ndoto
Wakati wote Alimpa Mungu utukufu na hakuchukua utukufu wa Mungu, Tumeumbwa ili tumtukuze Mungu, Mungu na awe kipaumbele chetu cha kwanza katika maisha yetu Mwanzo 40:1-41:36
e.      Yusufu alitafasiri Ndoto za Muokaji na Mnyweshaji gerezani na ndoto zilikuwa za kweli na zilitimia
f.        Mungu ndiye mwenye kutafasiri Ndoto alisema Yusufu Mwanzo 40:8
g.      Alitafasiri Ndoto ya mnyweshaji na kumuomnba amkumbuke Mwanzo 40:20-23
Wanadamu wana uwwezo mkubwa sana wa kuwasahau wenzao, tenda mema bila kutarajia kitu ni Mungu pekee ambaye hataweza kukusahau Isaya 49:15 “Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.” Ni Mungu pekee anayeweza kutufadhili na kutulipia kwa wema wetu wote tunaoufanya yeye fadhili zake zinadumu milele, Mungu hawezi muacha mtu mwenye haki Zaburi 37:25Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula.

C.      Mungu anamkumbuka Yusufu.
a.      Mungu alimpa Ndoto Farao Mwanzo 41:1-7
b.      Wenye hekima, waganga, na wachawi  wote wanashindwa kuitafasiri Mwanzo 41:8
c.       Mungu anaweka mazingira ya lazima kwa mnyweshaji kumkumbuka Yusufu Mwanzo 41:9-13,.Wanadamu wasipokuwa waaminifu kwetu Mungu ni Mwaminifu
d.      Yusufu aliitwa kutafasiri Ndoto, alimpa Mungu utukufu Mwanzo 41: 16, 25, 32 Wakati wote Yusufu alitambua kuwa Mungu ndiye mwenye kutenda kila jambo
e.      Yusufu alibadilishwa mavazi yake, huwezi kumkaribia mfalme ukiwa katika hali ya mfungwa Mwanzo 41:14.
f.        Licha ya Kufasiri Ndoto alikuwa na majibu ya tatizo kwa farao Mwanzo 41:33-36
g.      Maisha yalikuwa magumu na yenye uchungu, alikataliwa na nduguze, aliuzwa kama mtumwa, alihukumiwa kifungo kwa uonevu, alisahaulika hata na wale aliowatendea wema, kuna haja gani tena ya kuendelea kuwa mwaminifu katika mazingira kama haya? Lakini Yusufu aliendelea kutenda haki, alijua kuwa Mungu hawezi kumsahau, Wagalatia 6:9 “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.” Mungu alimpa kibali Farao na hatimaye farao hakuona mtu mwingine sahihi wa kusaidia jamii yake isipokuwa Yusufu. Ndugu usipozimia roho utavuna mema yote unayowatendea watu.

Maisha ya Yusufu Katika Nchi ya Ugeni kama Mtawala.

Mungu si Athumani akiwa na miaka 30 Yusufu anakuwa mtawala wa Misri chini ya farao anainuliwa sana Mwanzo 41:38-46 
a.      Alitawazwa kuwa kuwa mkuu katika nchi yote ya Misri Mwanzo 41:38-40
b.      Aliwekwa juu ya Ncho yote, akavishwa Pete ya Mamlaka Mwanzo 41:41-45
c.       Aliozwa mke Mzuri sana aliyeitwa Asenath
d.      Watu wote walimpigia Magoti, akiwemo Potifa, Mnyeshwaji, Askari wa Magereza na  raia wote
e.      Aliongoza kwa Hekima kubwa sana, alianza kufanya wajibu wake hakulipiza kisasi kwa Mtu
f.        Mungu alimbariki kwa watoto wawili wa Kiume Mwanzo 41:50-52
g.      Yusufu anafanyika Mwokozi sio wa Misri tu na ulimwengu mzima Mwanzo 41:55-57, Kuwa Baraka kwa wengine kunaanzia katika maisha ya uaminifu tangu nyumbani, shuleni, kazini, na hata ugenini Mungu alimbariki kweli kweli.

Kutimia kwa Ndoto ya Yusufu.

Baada ya miaka ipatayo 13 sasa Yusufu alkiwa na miaka 30 anakuwa ameinuliwa sana na Mungu na kuwa mtawala mwenye heshima ya kifalme Misri Mwanzo 41:38-46, Hekima aliyopewa na Mungu inaonekana katika Utendaji wa uongozi wake
a.      Alijua nini cha kufanya wakati wa Miaka ya mavuno Mwanzo 41:47-49
b.      Alijua nini cha kufanya wakati wa Miaka ya njaa Mwanzo 41:53-57, 47:13-26
c.       Aliunganisha maisha yake na Mambo aliyotendewa na Mungu Mwanzo 41:50-52
·         Manase Mungu amenisahaulisha taabu za nyumba ya Baba yangu
·         Efraimu Mungu amenineemesha Katika Nchi ya Ugeni
d.      Ndugu zake wanakuja Misri kwaajili ya kununua Chakula
·         Mwanzo 42:1-13 Yusufu aliwagundua Ndugu zake walipokuja na Kumuinamia na aliikumbuka Ndoto yake yaani ile ahadi ya Mungu aliyoahidiwa kwa Ndoto
·         Yusufu alitaka kuwakumbusha Ndugu zake Tatizo lao na kujua kama wamebadilika Mwanzo 42:14-24
·         Reben alikuwa Tayari kupoteza watoto wake wawili ili waende na Benjamin ambaye Yusufu alimdai waende naye wakati Simeon aliwekwa kizuizini, Mwanzo 42:36-38
·         Yuda naye anaonyesha kuwajibika kwa Maisha ya Ndugu zake Mwanzo 43:1-14
·         Mungu anataka tuwe mbali kabisa na maisha ya ubinafsi, ukomavu wa kweli unakuja pale tunapoonyesha kujali wengine na hata kuwa tayari kuyapoteza maisha yetu kwaajili ya wengine
·         Yuda anaonekana kuwa Tayari kuwajibika pia kwaajili ya Benjamin na kwaajili ya baba yake Mwanzo 44:18-34
·         Yusufu alishindwa kujizuia Mwanzo 45:1-4
·         Alihesabu kuwa kila kilichotokea ilikuwa ni mpango wa Mungu Mwanzo 45:5-15
·         Anawaahidi kuwatunza katika Nchi ya Gosheni Mwanzo 46:16-20,28-34;47:1-12
·         Yusufu alionyesha Moyo wa Msamaha Mwanzo 45:4-8, 50:15-21

Mungu huweza kutumia njia Mbaya kuleta jambo zuri Mwanzo 50:20
Mungu ni mwaminifu katika kutunza ahadi zake Mwanzo 50:24-25

Hitimisho:
Katika maisha ya Yusufu kuna mambo ya msingi ya Kujifunza
a.      Alimwamini Mungu na Kumtegemea
b.      Alijitoa kumtumikia Mungu na Mwanadamu kwa Heshima naUaminifu
c.       Hakukubali kumezwa na Chuki,Usaliti,Kusahaulika alionyesha upendo na hakulipiza kisasi
d.      Alikuwa tayari kuwasamehe wengine
e.      Alikuwa na akili na uwezo wa kujua Mapenzi ya Mungu katika kila alichokuwa anakipitia
f.        Alikuwa mwaminifu tangu ujana wake, na hata alipokuwa mbali na Nyumbani
g.      Alitambua kuwa Israel waterejea katika inchi ya ahadi na kuomba mifupa yake izikwe Israel
h.      Kupitia yeye tunaweza kujifunza namna ya kuwa Kielelezo katika. usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.

Limeandaliwa na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni