Jumanne, 27 Novemba 2018

“Kama wakitenda Mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”

Mstari wa Msingi: Luka 23:27-31

Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea.Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”

 “Kama wakitenda Mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”

Utangulizi:

Leo nataka tuchukue Muda kutafakari kwa kina kuhusu usemi huu wa Yesu Kristo, Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”  Usemi huu ambao ni usemi mzito sana na unaweza kuwa mgumu katika kuutafasiri kwa namna nyepesi nyepesi, Usemi huu ni usemi wa kitaaluma katika maswala ya semi za “Marabbi” na “Manabii” Ni usemi mzito uliojaa unabii, maana na maonyo na ndani yake kuna maana nzito sana ukilinganisha na mfumo wa maisha ya sasa tuliyonayo katika ulimwengu, lakini vilevile katika maisha ya kila mmoja wetu, Bwana na atupe neema kuuangalia usemi huu kwa undani, hata tuweze kupata, maana inayokusudiwa! Na kujifunza kutoka kwa Mwalimu mkuu Roho Mtakatifu!Katika jina la Yesu Kristo Amen.

Maana ya mti mbichi.
Mstari wa 31 Kwa kuwa wakitenda mambo haya katika mti mbichi, -  Kimsingi mti mbichi unaotajwa hapa na Yesu ni mti mwema mti wenye kuzaa matunda “Productive tree” mti ambao unaonekana kuwa una faida kubwa sana kibiblia mti huu unaitwa mti wa uzima angalia Ufunuo 2:7Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu”. Ufunuo 22:2Katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.” 14, “Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake”. 19 “Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.” 

Mti mbichi hapa unawakilisha Yesu Kristo, ambaye ndio mti wa uzima, wenye kuzaa matunda, kupitia kazi ya ukombozi na huruma zake amekuwa akiwaponya watu na kuwatendea mema, amekuwa mzuri na mwenye moyo mzuri, aliwafundisha watu neno la Mungu kwa huruma zake, aliwalisha watu wenye njaa, aliwaponya wenye ukoma, vipofu, walemavu na watu wenye shida na maatatizo ya aina mbalimbali, lakini pasipo huruma wakuu wa makuhani walimkabidhi kwa askari wa Kirumi watu wa mataifa wasiotahiriwa, ili wamsulubishe japokuwa Pilato hakuona dhambi yoyote ndani yake, hakuwa na hatia yoyote Yesu hakutenda dhambi yoyote lakini alifanyiwa tukio baya sana, alipigwa mijeledi, alitemewa mate, alivunjiwa heshima, alifedheheshwa, alinyanyashwa, alivishwa taji ya miiba japo kuwa alikuwa mwema Pilato alitoa hukumu ya kifo dhidi ya mtu ambaye mwenyewe alihakikisha kuwa hana hatia, lakini alitendewa mambo yasiyofaa, Yesu alikuwa akiwawazia mema, alikuwa akiwapenda, alikuwa akiwahurumia lakini aliteswa na kudhulumiwa uhai wake vibaya pasipo hatia yoyote, Yesu kristo alimtii Mungu kwa viwango vya juu zaidi hakuwa na dhambi Yohana 8;46 Je, kuna ye yote miongoni mwenu awezaye kunithibitisha kuwa nina dhambi? Kama nawaambia yaliyo kweli, mbona hamniamini?” Kama Yesu Kristo mti wenye faida wenye kuzaa matunda wenye kutii na kutenda mema wenye kweli yote amepita katika wakati mgumu namna hii siku ya mtu mbaya au mti mbaya kupita katika hukumu utakuwa ni wakati mbaya sana, ikiwa watu wa Mungu wanaokoka kwa shida, asiye wa Mungu atapata taabu sana 1Petro 4:18 “Na mwenye haki akiokoka kwa shida, Yule asiyemcha Mungu na mwenye dhambi ataonekana wapi? ”
 
Maana ya Mti mkavu.

31.b Itakuwaje kwa mti mkavu – Kwa upande mwingine mti mkavu inazungumzia kibiblia mti usio na matunda na mti usiozaa matunda “un Productive tree” unawakilisha watu wasiomcha Mungu, mti usio na faida mti usiozaa matunda au mti usiozaa matunda mazuri Mathayo 3:10Na shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.” 

Luka 13:7-9 “Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?  Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate”.

Mti mkavu unawakilisha watu waiozaa matunda, watu wabaya wasiomcha Mungu, wenye dhuluma waliojaa wivu kama mafarisayo na wakuu wa makuhani waliomsulubisha Yesu Kristo, pamoja na wote waliokataa neema ya Mungu lakini pia kwa lugha ya kinabii mti mkavu ni nabii wa uongo na mpinga Kristo.

Onyo kwa wanaomkataa Yesu!

Luka 23:27-31 “27.Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea. 28. Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. 29. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. 30. Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni.

Lakini vilevile katika jamii tunao watu wenye nia mbovu wasio wema ingawa wakati mwingine unaweza kushangaa watu wema wakafanyiwa vitu vibaya sana vya kusikitisha na ukajiuliza je itakuwaje kwa watu wabaya, Muda unakuja kwa wabaya pia kuhukumiwa na hukumu yao itakuwa mbaya sana, kama Mungu anaweza kumuadhibu mwana wake mpendwa Yesu, na kumuacha achinjwe kama kondoo wa kafara na watu wema wakawa wanamlilia na kumuhurumia Yesu aliwaonya kuwa afadhali waache kumlilia yeye na waanze kulia na kuomboleza kwaajili ya watoto wao, Yeye kristo anauawa kwaajili ya faida ya watakaomwamini, kifo chake ni ushindi dhidi ya adui zake, kifo chake kinaleta uzima wa milele  na wokovu kwa wote watakaomwamini, kwa sababu hiyo hakuna sababu ya kulia na kuomboleza kwaajili ya Kristo, lakini iko sababu ya kulia na kuomboleza kwaajili ya nafsi zetu na watoto wetu hususani kama tutaikataa neema ya Mungu.

Hata hivyo kinabii vilevile Yesu alikuwa akizungumza na wayahudi ambao wangeuawa na kuteswa vibaya na Warumi hao hao miaka michache kwa sababu ya kumkataa Yesu wayahudi walijuta sana kile ambacho Yesu alikuwa amewaonya kilitimizwa mwaka wa 70 BK. Ilikuwa ni kilio na kusaga meno. Ni muhimu kukumbuka kuwa kama mti mbichi na mti mkavu itatiwa moto ukweli ni kuwa mti mkavu utawaka na kuteketea na kusahaulika ukilinganisha na mti mbichi.

Ni ukweli ulio wazi kuwa baada ya Yesu kutabiri hili kwenye mwaka wa 33BK tunaelezwa katika historia kuwa mwaka wa 70 BK yaani (70-33=37) yaani miaka 37 baada ya maneno ya Yesu Askari wa kirumi waliizingira Yerusalem na kuwanza kuwaua wayahudi chini ya utawala wa Kaisari TITUS baada ya uasi wa mwaka 66 Israel walipotaka kuwa na serikali huru, Yerusalem uliharibiwa vibaya, Hekalu lilichomwa kwa moto na halikujengwa tena mpaka naandaa ujumbe huu, wayahudi waliuawa kila upande chini ya Jemadari aliyeitwa Tiberius Julius Alexander , Wayahudi waliuawa kijiji kwa kijiji na kumalizikia katika kijiji kilichoitwa Masada ambako wayahudi walijiua wenyewe wakikataa kwenda utumwani, hali ilikuwa mbaya sana na wayahudi walitawanyika dunia nzima mpaka mwaka wa 1949 may walipopata uhuru na kujitangaza tena kama taifa pekee la kiyahudi lililoko hadi leo, hii ilikuwa ni hukumu mbaya na yenye kutisha kama alivyoonya Bwana Yesu.

Wito wa Kimungu unamtaka kila mtu duniani atubu, ajirekebishe aache dhambi, ikiwa Mungu aliruhusu mwana wake Mpendwa Yesu Kristo achubuliwe na kudhihakiwa na kufa kifo kibaya na cha aibu Msalabani, huku kwa hakika hakuwa mwenye dhambi, alikuwa mti mbichi sembuse mimi na wewe leo, tusiofaa kitu, tulio mti mkavu, Bila unyenyekevu na toba ya kweli ni wazi kuwa hatutaweza kustahimili siku ya kuadhibiwa kwetu, ni lazima kama taifa tutubu, tuache uovu, tuzae matunda unabii huuwa Yesu Kristo bado unafanya kazi hata sasa kwa kila mtu na kwa kila Taifa, Kama humuamini Yesu wewe hutaweza kustahimili Hasira  ya Mungu, angalia dhuluma, uonevu, wizi, uasherati,zinaa, mmommonyoko mkubwa wa uadilifu ulioko kwa dunia ya sasa, uovu unapoonekana akama sifa ya kujivunia.

Mataifa yaliyoendelea yaliyokuwa yanajulikana kama mataifa ya Kikristo mabunge na viongozi na hata wa kidini angalia walivyopigwa upofu kuruhusu ndoa za jinsia moja, kutokukemea matendo ya usagaji na ushoga, angalia mataifa ya Kiislam yasiyotenda haki na kuruhusu injili ya Kristo kuhubiriwa kwao, au kuruhusu uhuru wa kuabudu, utapeli uliokithiri na ufisadi hizi zote zinatufanya kuwa mti mkavu ambao hautaweza kustahimili, Hukumu ya moto wa Mungu itakapofika, kukandamiza wanyonge, dhuluma kwa wajane na yatima, dhuluma za mipaka ya mashamba na viwanja, dhuluma za hati za nyumba na viwanja, vilio kila mahali, mauaji yenye utata haya yote utafika wakati ambapo Mungu mwenye haki hatoweza kuyafumbia macho, siasa makanisani, uchawi, na ushirikina kampenzi za kimwili nyakati za chaguzi hata za kidini, kuonewa na kudhulumiwa kwa watu wema haya yote yanaandaa mti mkavu kuwashwa moto.

“Kama wakitenda Mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?” Yesu aliwaonya kina mama wa Yerusalem kuwa wasilie kwaajili yake bali walilie nafsi zao na watoto wao, Dunia nakutangazia ni wakati wa kujililia na kuililia nafsi za watoto wetu, leo ni taabu ukizaa mtoto wa kiume tabu ukizaa wa kike taabu  Mungu na aingilia kati na kuwaponya watu wake, usijifikiri kuwa wewe utapenya, hakuna upenyo dhiki ya Yerusalem iliwapata wema na waovu, lakini zaidi sana wale waliomkataa Kristo, Kama humuamini Yesu ndugu wewe ni mti mkavu, kama ungali unaishi katika dhambi ndugu wewe ni mti mkavu na kama wametenda yale kwa mti mbichi itakuwaje kwa mti mkavu? Kristo anasema siku ile watu watasema heri matumbo yasiyozaa,  na maziwa yasiyonyonyesha,watu wataiambia milima na vilima tuangukieni na kutufunika bila toba hali hii inaweza kumkuta mtu awaye yote.

“Kama wakitenda Mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?”
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni