Jumapili, 25 Novemba 2018

Watapigana nawe lakini Hawatakushinda!


Mstari wa Msingi: Yeremia 1:19Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe.”



Pichani ndege za Jeshi la Anga la Israel (IAF) Israel Air Force  tayari kwa mashambulizi dhidi ya adui wa Israel

Utangulizi:

Nabii Yeremia alikuwa moja ya manabii aliyepata ahadi nyingi sana za Mungu za kutia moyo, na sababu kubwa ni kuwa pia alikuwa ni nabii aliyepitia changamoto nyingi sana katika maisha, hususani upinzani mkubwa sana kwa ujumbe aliokuwa akiutoa, ambao kimsingi haukuwa wake bali ulikuwa ni ujumbe kamili wa Mungu dhidi ya watu wake kwa kinya cha nabii Yeremia.

Mungu mwenye upendo mwingi na rehema alikuwa anajua wazi kuwa mtumishi wake atapitia changamoto, kubwa na nyingi dhidi ya ujumbe wake wa kinabii aliokuwa anautoa ambao kimsingi haungeweza kuwafurahisha watu wayahudi kwa vile huenda walidhani kuwa Yeremia anatabiri kinyume na watu wa Mungu, mji wa Mungu na Hekalu la Mungu, aidha alionekana kama anawatukuza wakaldayo ambao kimsingi walikuwa ni adui wa Israelk na mataifa mengine.

Kutokana na ugumu wa kazi hii mapema sana Mungu alimuahidi Yeremia kuwa atakuwa pamoja naye, Mungu kuwa pamoja na Yeremia ulikuwa ni ujumbe wazi kuwa Mungu mwokozi wa wanadamu angekuwa pamoja naye, hii ilieleweka wazi kwa Yeremia kuwa ushindi uko pamoja naye, uwepo wa Mungu unapokuwa na mtu awaye yote ni vigumu sana kumshinda mtu wa namna hiyo, Kama Mungu amesema mtu huyu niko naye tayari mtu huyo ni mshindi, uwepo wa Mungu ni ushindi, uwepo wa Mungu ni ulinzi, uwepo wa Mungu bwana wa majeshi ni ishara iliyowazi kuwa hata kuwe na jeshi kubwa namna gani litasambaratika kabisa na hii ndio maana ya “ Immanuel” Isaya 7:14Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.” Unaweza kuona Katika mstari wa Msingi Mungu alimuahidi Nabii Yeremia  mambo ya msingi makuu matatu ambayo anamuahidi kila mtu wake leo kama yeremia wa sasa au kama mtu unayepitia mambi magumu au uko kwenye vita ngumu kama ile aliyokuwa akiipitia Yeremia.

1.       Watapigana naye (au watashindana naye) Lakini hawatakushinda, watapigana nawe hii ina maana ya Muungano mkubwa wa maadui, ya kwamba adui sio mmoja tu, wanaweza kuwa wengi wanaweza kuwa ni timu kubwa ya watu walioungana kwa nia moja kuweza kukufutilia mbali, na wewe unaweza kusalia peke yako, Hili lisikupe shida lisikutese angalia Waamuzi 20:11Basi waume wote wa Israeli walikutana pamoja juu ya mji huo, walikuwa wanashikamana pamoja kama mtu mmoja.” Kuna wakati adui wataungana na kuwa kama mtu moja wakiwa na lengo au kusudi la kupigana nawe hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Yeremia, Israel na hata wewe pia lakini Mungu ameahidi kuwa HAWATAKUSHINDA. 2Mambo ya nyakati 20:1- 15 “Ikawa baadaye, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, na pamoja nao baadhi ya Wameuni, wakaja juu ya Yehoshafati vitani. Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema, Wanakuja jamii kubwa juu yako watokao Shamu toka ng'ambo ya bahari; na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio En-gedi).Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute Bwana; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote. Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute Bwana; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta Bwana. Yehoshafati akasimama kati ya kusanyiko la Yuda na Yerusalemu, nyumbani mwa Bwana, mbele ya ua mpya; akasema, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu, si wewe uliye Mungu mbinguni? Tena si wewe utawalaye falme zote za mataifa? Na mkononi mwako mna uweza na nguvu, asiweze mtu ye yote kusimama kinyume chako. Si wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, ukawapa wazao wa Ibrahimu rafiki yako hata milele? Nao walikaa humo, wamekujengea patakatifu pa jina lako humo, wakisema, Yakitujia mabaya, upanga, hukumu, au tauni, au njaa, tutasimama mbele ya nyumba hii, na mbele zako, (maana jina lako limo katika nyumba hii), na kukulilia katika shida yetu, nawe utasikia na kuokoa. Na sasa, tazama, wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, ambao hukuwaacha Israeli waingie katika nchi yao, walipotoka nchi ya Misri; lakini wakawageukia mbali, wasiwaharibu; tazama, jinsi wanavyotulipa, wakija kututupa toka milki yako, uliyoturithisha. Ee Mungu wetu, je! Hutawahukumu? Maana sisi hatuna uwezo juu ya jamii kubwa hii, wanaotujia juu yetu; wala hatujui tufanyeje; lakini macho yetu yatazama kwako. Wakasimama Yuda wote mbele za Bwana, pamoja na wadogo wao, na wake zao, na watoto wao. Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya Bwana, katikati ya kusanyiko; akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; Bwana awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu.”

2.       Hawatakushinda; Maana yake ni kuwa hawataweza, hawatakuweza, yaani hata kama watatumia silaha kubwa na za kisasa namna gani, yaani hata kama watatumia uchawi, yaani hata kama watajikita na  kuleketa watu waliobobea kiasi gani Mungu ameahidi kuwa hawatakushinda Yeremia 15:20-21Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema Bwana. Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha.” Unaweza kuona kumbe hata adui awe mwenye kutisha kiasi gani Mungu ameahidi kutokoa na mikono ya watu wabaya na kutukomboa kwa mkono wenye kutisha, licha ya ushindi mkubwa sana Mungu atakaotupa dhidi ya adui zetu Pia mungu ameahidi kuwa watapata aibu ambayo haitasahaulika  hii ni kwa sababu Mungu atakuwa pamoja nasi  Yeremia 20:10-11.Maana nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote, wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki, huenda akahadaika, nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake. Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe.” 

3.       Kwa kuwa mimi nipo pamoja nawe: Siri kubwa ya ushindi ambayo kila muumini anaweza kuwa nayo ni kwakuwa Bwana Mungu yuko pamoja naye Yeremia 1:8 “Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana.” Wakati wote Mungu anapokuwa pamoja nasi uwepo wake unaleta ushindi katika maisha yetu, Mungu anapokuwa pamoja nasi yeye anakuwa ndio ushindi wetu, na mlinzi wetu hatuna budi kutembea kifua mbela tukijua kuwa Bwana yu pamoja nasi 2Timotheo 4:17-18Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba. Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina.”  
            
Hitimisho!

Ahadi hii kimsingi haikuwa tu kwaajili ya Yeremia pekee, Ahadi hii ni agano kwa watu wote wanaomtumaini Bwana, ni ahadi kwa Taifa la Israel na ni ahadi kwa kanisa na ni ahadi kwa kila Mtu wa Mungu, Katika Israel wote tunakumbuka kuwa mara kadhaa mataifa pinzani yanayoizunguka Israel wakiwahi kutaka kuifuta na kuikusudia mabaya, Misri, Jordan, Lebanon, Syria na Iraq waliwahi kukusudia mabaya dhidi ya Israel lakini walibamizwa vibaya na kusambaratishiwa mbali, watapigana nawe lakini hawatakushinda, Ndugu mpendwa kama tunamtumaini Mungu na kutembea katika uwepo wake hatupaswi kuogopa kitu, Hakuna atakayeweza kutushinda, hata kama maadui wataungana na kuwa kundi kubwa la watu au jeshi kubwa litasambaratishwa hatupaswi kuogopa kwa sababu tumemtumaini Mungu naye ametuahidi kuwa yuko pamoja nasi ili atuokoe na wale waliotukusudia mabaya watotaoka wakiwa wanatahayari, wamesambaratika, wamerudhishwa nyuma, Mpendwa liamini neno lake uone kama Mungu ninayekuhubiri habari zake atakuaibisha, Muaminini Mungu waaminini manabii wake ndipo mtakapothibitika.

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Rev. Innocent Kamote
0718990796/0781394550

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni