Zaburi 137: 1-4 “Kando ya mito ya Babeli
ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati
yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka
tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za
Sayuni. Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni?”
Utangulizi:
Kila mwanadamu katika maisha yake
ana historia ambayo imejaa milima na mabonde katika mapito mbalimbali ya
maisha, Ukimuuliza mtu swali akuelezee au akuandikie siku ambayo hatakuja
kuisahau katika maisha yake kwamba siku ambayo ilimpa furaha kubwa sana (Golden Age) au siku ambayo aliwahi
kuuzunika sana (Ashes Age) utaweza
kugundua kwamba wengi wataandika siku zao ambazo hawatazisahahu katika maisha
yao kutokana na huzuni na mapito mazito waliyoyapitia.
Wengine wataeleza siku yao
wasioweza kuisahahu kama siku ya harusi yake, au siku ya msiba wa mtu wake
aliye karibu, au siku timu yake ilipofungwa, au siku timu yake ilipopata
ushindi, au siku alipopata kazi, au siku alipofukuzwa kazi, kila mmoja anaweza
kuelezea siku yake ya huzuni za wakati wake wa furaha hii ni hali ya kawaida
katika maisha ya mwanadamu, na ndio maana waswahili wanasema maisha ya
mwanadamu yana milima na mambonde. Halii hii pia inaweza kugusa hata taifa
fulani au bara fulani na kadhalika.
Zaburi hii ya 137:1-9
imegawanyika katika sehemu kuu tatu.
·
Mstari wa 1-4 inaelezea hali halisi ya huzuni
waliyokuwa nayo wayahudi huko utumwani, walilia na walivitundika vinubi vyao
juu ya miti kwa sababu wasingeliweza kuimba wimbo wa kumuabudu Mungu ugenini
·
Mstari 5-6 inaelezea jinsi walivyojipa moyo na
kujiapiza juwa haitakuja itokee waisahau Sayuni yaani Yerusalem yaani uwepo wa
Mungu, na ni afadhali kusahahu mkono wa kulia au kuwa bubu kuliko kuisahai
Sayuni
·
Mstari 7-9 jamaa anaomba kwamba Mungu
ashughulike na Babeli pamoja na Edomu ambao walishangilia kuangamia kwa
Wayahudi na kuboibmolewa kwa Yerusalem
Katika kifungu za Zaburi hii leo
tunaweza kupata picha ya wana wa Israel waliorejea kutoka utumwani, ambao
walishuhudia uzuri wa Taifa lao lilipokuwa chini ya uongozi wa Mungu na baadaye
lilipoadhibiwa na kuruhusiwa kwenda utumwani
Zaburi 137:1-4 “Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia
tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi
vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea
walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni. Tuuimbeje wimbo wa Bwana
Katika nchi ya ugeni?”
Mwandishi wa zaburi hii japokuwa
wengine wanadhani ni Yeremia lakini mimi bila shaka naamini atakuwa Ezra au
mojawapo ya watu waliorejea kutoka uhamishoni kwa sababu anajaribu kuelezea hali halisi waliyoipitia
walipokuwa nje ya Israel yaani utumwani huko Babeli, na historia haionyeshi
kuwa yeremia alikwenda uhamishoni Babeli kama ilivyo kwa Ezekiel na Daniel,
kwani inasemekana huenda yeye Yeremia alikwenda Misri. Ingawa nchi ya Babeli yaani Iraq na Iran ya
leo zilikuwa na mito mkubwa na mizuri na yenye matawi mengi sana yaliyochangia
taifa hilo kuwa na uwezo mkubwa wa kujitosheleza kwa chakula na umwagiliaji na
ujenzi ulioruhusu maji kupita katikati ya majiji yao mito kama Mto Kebari, Mto Frati na mto Tigris na
ustaarabu mkubwa na wa hali ya juu, Babeli ulikuwa mji wa kifahari sana ndio
ulikuwa mji wenye bustani zinazoelea angani na kuingizwa katika moja ya maajabu
saba ya kale ya dunia (The Seven wonders
of the ancient world ) ukiacha pyramid
la Chiops lililoko Gezer nchini Misri hata leo, Bustani na uzuri wa jiji la
Babeli lilikuwa linashika nafsi ya pili kwa ajabu zake duniani, Mfalme
Nebuchadnezar aliwahi kujisifia kuhusu ujenzi wa mji huu na akaadhibiwa na
Mungu kwa kiburi chake akidhani kuwa alifanya kwa nguvu zake na utukufu wake
Daniel 4:29-33 “Baada
ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika
Babeli. Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi,
uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi
yangu? Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka
mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme
huu umeondoka kwako. Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa
pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng'ombe, na nyakati saba
zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika
ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote. Saa iyo hiyo jambo hilo
likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani
kama ng'ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele
zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.”
Unaweza kuona Babeli kulikuwa ni kuzuri sana kuliko hata Sayuni, lakini wana wa
Israel walilia walipoikumbuka Sayuni kwanini? Unaweza kuwa na ndoa ya kifahari
sana lakini huo sio uthibitisho wa furaha ya kweli, unaweza kuwa na kila kitu
lakini kama Mungu hamo haiwezi hiyo kitu kukupa furaha ya kweli unaweza kuwa
katika nchi iliyoendela sana lakini hili sio suluhisho la furaha ya kweli ya
mwanadamu, unaweza kuwa na mume mzuri na mke mzuri lakini bila uwepo wa Mungu
ni sawa na shamba la miwa karibu na shule ya msingi, wako watu wengi wanalia
japokuwa wanaishi katika mageti, na nyumba nzuri, na magari mazuri si dhambi
kuwa navyo lakini the best ni kuwa na uwepo wa Mungu, Mungu ndiye furaha yetu
ya kweli, Elimu na ujuzi na maendeleo hayatupi guarantee ya uhakika wa furaha
yetu.
Kwa nini walilia walipoikumbuka sayuni?
Wayahudi waliketi na kutafakari,
kwamba wao ingawa walikuwa katika nchi nzuri sana yenye mito mingi, Machozi
yaliwatoka kwa sababu sasa walikuwa wametengwa mbali na uwepo wa Mungu,
walipotafakari juu ya Nyumba ya Mungu iliyokuwako Sayuni yaani Yerusalem,
walipokumbuka makaburi ya baba zao, walipokumbuka sikukuu zao namna na jinsi
walivyokuwa wakipanda kwenda kumuabudu Mungu wa baba zai Ibrahim na Isaka na Yakobo, Jinsi walivyokuwa na fahari kuu wakati
wa utawala wa Daudi na Solomon, walikumbuka walivyokuwa
wakikwea kwenda kuabudu na makuhani wakiwaongoza, walivyokuwa wakitoa sadaka za
kuteketeza na kumuabudu Mungu wa kweli kwa furaha na uhuru wao waliokuwa nao,
jinsi walivyotumia vinubi na vinanda kumsifu na kumuheshimu Mungu huu ulikuwa
ni wakati ambao ni kama golden age kwao, ulikuwa ni wakati wa furaha
Sasa Israel wako utumwani hawana
uhuru wao wenyewe, hawawezi kuabudu kama walivyozoea, wanapangiwa kila kitu,
waliowachukua mateka wanawasanifu wanasema wawaimbie kama walivyokuwa wakiimba
huko sayuni, wakati wao wakiwa na huzuni waliowateka kama mateka wanataka waimbiwe
wanataka wafurahie, wao kwao ilikuwa ni swala gumu, uzuri wa Babeli haukuwa na
maana kwao, walikumbuka misiba mikubwa, walikumbuka walivyoamuriwa wawaue ndugu
zao kwa upanga, wamepoteza mali zao, hawana mashamba yao, hawana nyumba zao, hawana serikali yao, hawana wafalme wao
matumaini waliyokuwa nayo yametokweka, walikumbuka mateso waliyoyapata,
walikumbuka walivyochomwa moto, walikumbuka manabii waliokuwa nao, walikumbuka
jinsi Mungu alivyowadekeza na kuwapa kila walichokihitaji, sasa ni kama mbingu
zimefungwa, ni kama wameondolewa kwenye uwepo wa Bwana, hakuna tena hekalu
kubwa kama lile la Sulemani,Unawezaje kuimba wimbo wa Bwana katika nchi ya
Ugenini
Waliikumbuka Sayuni waliikumbuka
Yerusalem, waliweka nadhiri na kujiapisha kuwa hawatakuja waisahau Yerusalem na
kama ikitokea ni sawa na kusahahu mkono wa kulia au mdomo ugande kwa kushikana
na ulimi kuliko kuisahau Israel, lakini pia walikumbuka jinsi wakati wanaondoka
watu wa Edomu walikuwa wakishangilia kuharibiwa kwa mji huo Bomoeni bomoeni
bomoeni walisema na pia waliomba kisasi dhidi ya Babeli kwamba isiachewe salama
Zaburi 137:5-9 “Ee
Yerusalemu, nikikusahau wewe, Mkono wangu wa kuume na usahau. Ulimi wangu na
ugandamane Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka. Nisipoikuza Yerusalemu
Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu. Ee Bwana, uwakumbuke wana wa Edomu, Siku ya
Yerusalemu. Waliosema, Bomoeni! Bomoeni hata misingini! Ee binti Babeli, uliye
karibu na kuangamia, Heri atakayekupatiliza, ulivyotupatiliza sisi. Heri yeye
atakayewakamata wadogo wako, Na kuwaseta wao juu ya mwamba.”
Hivi ndivyo inavyotokea katika
maisha yetu na maisha ya kanisa la Mungu, hakuna jambo ba ya sana kama kutengwa
mbali na uwepo wa Mungu, hatuwezi kufurahia fahari za dunia na dhambi, hatuwezi
kuabudu kwa uhuru ikiwa tumechukuliwa mateka, aidha inatia uchungu sana wakati
unapopitia mambo magumu kisha wakawepo kando watu wa kufurahia unayoyapitia au
kuunga mkono kile unachokipitia, Maandiko yanaonyesha kuwa mwandishi aliomba
Mungu akutane na watesi na mashabiki wao pia awalipize kisasi, hatuwezi kuwa na
furaha kamili kama maadui zetu wanaisshi na wanashangilia kuangamia kwetu, ni
lazima Mungu afanye kitu ili yamkini hata kama wanaishi waweze kuona na kujua
kuwa Mungu hawatupilii mbali watu wake, ni lazima wasikie na wajue, Mungu
awapatilize, Natangaza habari njema
kwako ya kuwa uko wakati wako wa golden age unakuja ikiwa utakubali Yesu Kristo
akutawale, jitegemeze kwake yeye atakutetea anatayafuta machozi yako yote nawe
utapata raha nafsini mwako, jitie katika utawala wake nawe utaonja ya kuwa Yesu
hatakuacha yeye ni mwema katika maisha yako, hatakusahau kamwe. Kumbuka kurudi
katika uwepo wa Mungu, usikubali kutengwa mbali na uwepo wake, uwepo wa Mungu
ndio furaha ya kweli, ndio ushindi wa maisha yetu, kila kitu kitakuwa na maana
kwetu iwapo tutajikinga katika uwepo wake Zaburi
27:1-4, wale wote wanaotazamia kuwangamia kwetu lazima wajue na wasikie
kuwa Mungu wetu yu hai nay a kuwa anafanya kazi kubwa ya kutukomboa pale
tunapojitegemeza kwake.
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!.
Asante mtumishi
JibuFuta