Jumapili, 3 Machi 2019

Maana Mungu hakutupa roho ya woga.


2Timotheo 1:3-7.

Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana. Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha; nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo. Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.”

Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, usilie ;tazama,Simba aliye wa kabila ya Yuda,Shina la Daudi,Yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu,na zile muhuri zake saba.” Ufunuo 5:5

Ni muhimu kufahamu kuwa Maandiko Matakatifu yanatufundisha kuwa kuna aina mbili za hofu, hofu ya kwanza ni hofu yenye manufaa, hofu yenye faida, aina hii ya hofu ndio inayotufanya tuogope kujiumiza, au tuogope kufanya mambo mabaya, na tuweze kumcha Mungu na kuogopa kutenda maovu hii ni hofu njema na yenye ufanisi, Lakini hofu ya pili ni hofu mbaya,  aina hii ya hofu ni hofu yenye hasara ni hofu mbaya na ni roho hii ndio hofu ambayo maandiko yanatufundisha kuwa haitokani na Mungu ni hofu mbaya sana na ni hofu inayowafanya wengi waogope kuthubutu au kufanya jambo.

Hofu ya Mungu.

Hofu ya Mungu huambatana  pamoja na baraka nyingi na faida. Ni mwanzo wa hekima na inaongoza kwa uelewa mzuri Zaburi 111: 10. “Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima, Wote wafanyao hayo wana akili njema, Sifa zake zakaa milele.” Pia unaweza kuona katika Mithali 1: 7Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu”. Zaidi ya hayo, hofu ya Bwana inaongoza kwa maisha, pumziko, amani, na ridhaa Mithali 19:23.Kumcha Bwana huelekea uhai; Atakaa ameshiba; hatajiliwa na ubaya” kumcha bwana kunaongeza Maisha ni chemichemi ya uzima inayoepusha na mauti Mithali 14:27 “Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti” Kwa msingi huo hofu ya Mungu yaani lkumcha Mungu ni jambo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu na ndani yake  Nguvu, upendo na moyo wa kiasi hofu hii inafaida kubwa sana na biblia imewekea mkazo umuhimu wa aina hii ya hofu.

Roho ya woga (Hofu isiyotokana na Mungu)

Katika mstari wa msingi tuliousoma sasa Paulo mtume anaorodhesha aina nyingine ya Hofu na anamuieleza Timotheo kuwa hofu hii haitokani na Mungu wala Mungu hatupi hofu ya aina hii na zaidi sana anaiita hofu hii “ROHO YA WOGA” maana yake ni kuwa ainha hii ya hofu ni dhahiri kuwa inatokana na shetani ni hofu mbaya  2 Timotheo 1: 7: "Kwa maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi."

Katika Biblia ya kiyunani neno hili roho ya woga linaweza kutafasiriwa kama Hali ya kujiona Duni, “inferiority complex”  hili ni tatizo kubwa la kisaikolojia linaloweza kuwapata hata watu wa Mungu, hata watu ambao wamekua vizuri katika imani, lakini kwa vile ndani wanajiona duni basi wanafikiri kuwa wao hawafai, wanaogopa, wanaogopa wanadamu, wanamuogopa shetani, wanaogopa ni namna gani watazungumza mbele za watu, wanaogopa kukosea, wanaogopa kwa sababu hawajui kiingereza vizuri, wanaogopa kwa sababu ya udhaifu fulani wa mwilini ambao wanao, wanaogopa kwa sababu ya udhaifu katika roho zao, na kwa sababu hiyo wanadhani kuwa hawataweza kufaa kwa namna yoyote kuwa watumishi wa Mungu, wana jiona duni, wanajiona hawafai na hivyo wanajumlisha na kutoa na kupata jawabu kuwa hawasytahili kuwa wachungaji, waisnjilisti au walimu, mitume na manabii kwa sababu eti hawatoshi katika vipimo vya Mungu.

Hali ya aina hii ndio aliyokuwa anaipitia Timotheo, aliwekwa kuwa mwangalizi wa Kanisa la Efeso, hili lilikuwa moja ya Makanisa makubwa sana nyakati za kanisa la Kwanza, Na Timotheo alikuwa tayari amekwisha chunga kanisa la Thesalonike, lakini Timotheo alikuwa ni kijana mdogo, na alikuwa akiugua mara kwa mara lakini alitiwa moyo kwa uwepo wa Paulo mtume, hofu ya aina hii bila shaka halikuwa tatizo kwa Timotheo lakini Paulo alijua kuwa kwa vile Paulo alikuweko Duniani, aliweza kumtia moyo Timotheo lakini sasa Paulo yuko gerezani na siku zake za kuondoka Duniani zilikuwa zinakaribia na alijua kuwa kwa vyovyote vile Timotheo angeogopa au angepoteza ujasiri na sasa anataka kumtia moyo kuwa asiogipe hofu ya aina hii sio sehemu ya maisha ya mtu aliyeokoka.
Mungu hajatuita, tuwaogope wanadamu, Mungu hajatuita, tuogope kusimama mbele ya umati mkubwa wa watu, Mungu hajatuita tuwe waoga, Mungu hajatuita tuwe duni miongoni mwa wanadamu, waluimu wa uongo na kazi za shetani na nguvu za giza kinyjme chake sisi tuna Roho Mtakatifu, Roho wa Bwana, tuna roho ya nguvu, tuna roho ya hekima, tuna roho ya uchaji wa Mungu, tuna roho ya Ushauri, tuna roho ya maarifa na ujuzi Isaya 11:1-2 “Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana;

Roho ya ya woga haitoki kwa Mungu. 

Hata hivyo, wakati mwingine sisi uhofu, wakati mwingine hii "roho ya woga"inatulemea, na kuishinda tunapaswa kumwamini na kumpenda Mungu kabisa . "Hakuna hofu katika upendo. Lakini upendo kamili unatoa nje hofu, kwa maana hofu inatumika na adhabu. Mtu mwenye woga hajafanywa mkamilifu katika upendo "1 Yohana 4:18. Hakuna mtu mkamilifu, na Mungu anajua hilo.  Mungu wakati mwingine hataondoa kabisa madhaifu tuliyo nayo lakini badala yake atataka tumtegemee yeye hivyo hivyo hivyo pamoja na udhaifu wetu naye ataleta utoshelevu wa neema na upendo wetu kwetu kwaajili ya utukufu wake, kamwe usingije eti uwe mkamilifu kisha ndio umtumikie Mungu, Biblia inatuhimiza wakati wote tusiogope, Roho ya Hofu ina nguvu sana ya kuharibu vipawa na uwezo wa watu, na ndio maana Mungu anataka tumuamini, bila kujali kuwa tuna umri mdogo, au hatuna elimu ya kutosha, au hatujui kiingereza, au hatuna ujuzi na jambo fulani.
Isaya 41:10 inatuhimiza, "Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifahdaike, kwa maana mimi ni Mungu wako, nitakutia nguvu, maana nitakusaidia, naam nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Zaburi 56:11 "Nimemtumaini Mungu sitaogopa, mwanadamu atanitenda nini?" 

Yeremia 1:5-8Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana.”

Joshua 1:5-8 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.  Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”

Mungu wakati wote atatoa neema kwa kila aina ya ulemavu tulio nao anajazilizia, nimekutana na watu ambao hawakusoma kabisa lakini wana akili za ajabu sana, Bibi yangu alikuwa ni moja ya watu waliokosa elimu kabisa wakati wa Mkoloni, alitokea familia duni, lakini yeye ndiye aliyekuwa analima na kulisha watu nyumbani, wenye fedha walikuwa wakinunua mboga tu, lakini ugali na mahindi na mihogo bibi alileta kutoka shambani, alisimamia watoto wake wote wakaenda shule na kuelimika na kuwa watu wakubwa, leo tuna wanasiasa, wakubwa, tuna askari, tuna mainjinia, tuna pilisi, tuna usalama wa taifa, tuna walimu, tuna madereva, tuna mafundi, mchundo, waashi, lakini walilelewa na Bibi ambaye hakusoma Mungu atakupa neema katika mapungufu uliyonayo, Usiogope simama na mtumikie Mungu kwa kile Mungu alichoweka ndani yako Usiogope Mungu hakutupa Roho ya woga. Uwe na ushujaa Yesu ni Simba wa kabila la Yuda tukiwa naye msituni hatupaswi kuhofia lolote.

Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda,Shina la Daudi,Yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu,na zile muhuri zake saba.” Ufunuo 5:5

Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima.
0718990796.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni