Jumatatu, 30 Desemba 2019

Kustawi kama Mwerezi wa Lebanon!


 Zaburi 92:12-15 “Mwenye haki atasitawi kama mtende, Atakua kama mwerezi wa Lebanoni.  Waliopandwa katika nyumba ya Bwana Watasitawi katika nyua za Mungu wetu. Watazaa matunda hadi wakati wa uzee, Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.  Watangaze ya kuwa Bwana ni mwenye adili, Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu.


 

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu katika Hekima yake, huwa anatumia vitu vyenye uhai na visivyo na uhai wakati mwingine kwa kusudi la kutufundisha maswala kadhaa sisi wanadamu, Miti kadhaa katika Biblia imeweza kutumiwa na Mungu kwa kusudi la kutufundisha mambo ya kiroho sisi wanadamu, Moja ya Mti ambao umetajwa sana katika Biblia ni pamoja na mti ujulikanao kama Mwerezi wa Lebanon, Mti huu unaheshimika sana na ni hazina kubwa sana ya dunia, Taifa la Lebanon limeweka mti huu katikati ya Bendera yake kama alama kuu ya uchumi wa taifa la Lebanon, Leo tutachukua Muda kuutafakari mti huu kwa kina na kisha kujifunza Maswala kadhaa katika vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Ufahamu kuhusu mti wa Mwerezi
·         Mambo ya kujifunza kutokana na Mwerezi
·         Kustawi kama Mwerezi wa Lebanon

Ufahamu kuhusu mti wa Mwerezi.


Ni muhimu kufahamu kuwa miti katika biblia mara kadhaa imetumika kuwakilisha watu au taifa katika lugha ya kinabii, na mara kadhaa imetumiwa katika biblia kumaanisha watu, mtu au taifa au mataifa, Kwa msingi huo miti inapotumiwa katika biblia hutumika kuwakilisha jamii ya watu au aina ya watu na sifa zao, Sifa za mti fulani kulingana na jinsi ulivyo unaweza kutumika katika kufundisha sifa ya mtu au watu kutokana na tabia na mwenendo wao mfano, Sifa za Mwerezi zinaweza kufanana kwa kiwango fulani na sifa za Mpingo kwa hapa Tanzania kutokana na ugumu wa mti huo unaotumika kuchongea vinyago, miaka kadhaa Nyuma kulikuwa na Band inaitwa Mchinga Sound wakiwa na kiongozi wao Muumini Mwinjuma waliwahi kuimba na kusema maneno haya “Mimi Kisiki cha mpingo wamekuja wenye shoka unakuja na panga unajisumbua” akionyesha ugumu wa mti huo na uimara wake ndivyo ambavyo Mwerezi nao ulikuwa na sifa zake katika maandiko na Mungu ameutumia kutufunza maswala kadhaa muhimu katika maisha yetu ya kawaida nay a kiroho.


Waamuzi 9:7-15 “Kisha walipomwambia huyo Yothamu, yeye akaenda, akasimama juu ya kilele cha kilima cha Gerizimu, akapaza sauti yake, akapiga kelele, na kuwaambia, Nisikieni mimi, enyi watu wa Shekemu, ili kwamba Mungu naye apate kuwasikia ninyi. Siku moja miti ilitoka ili kuutia mmoja mafuta uwe mfalme juu yao; ikauambia mti mzeituni, Tawala wewe juu yetu. Lakini huo mzeituni ukaiambia, Je! Niache mafuta yangu, ambayo kwangu mimi watu wamheshimu Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti? Kisha miti ikauambia mtini, Njoo wewe, utawale juu yetu. Lakini huo mtini ukaiambia, Je! Niuache utamu wangu, na matunda yangu mazuri, niende nikayonge-yonge juu ya miti? Kisha miti ikauambia mzabibu, Njoo wewe, utawale juu yetu. Huo mzabibu nao ukaiambia, Je! Niiache divai yangu, ambayo humfurahisha Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti? Ndipo hiyo miti yote ikauambia mti wa miiba, Njoo wewe, utawale juu yetu. Huo mti wa miiba ukaiambia miti, Kwamba ninyi mwanitia mafuta niwe mfalme juu yenu kwelikweli, basi njoni mtumaini kivuli changu; na kwamba sivyo, na utoke moto katika mti wa miiba na kuiteketeza mierezi ya Lebanoni”. 


 Unaona katika kisa hiki Yothamu anajaribu kuwaelezea watu kwa kutumia miti, kwa msingi huo miti kibiblia inaweza kutumika kuwakilisha taifa au watu, au jamii au maana ya tabia na mwnendo wa mtu mmoja mmoja utaweza pia kuona katika vikiwakilishwa na miti;-



Luka 21:29-31”
Akawaambia mfano; Utazameni mtini na miti mingine yote. Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu. Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu.” 

 Hapa Yesu alikuwa analizungumzia Taifa la Israel na mataifa mengine kuwa yatakapoanza kupata uhuru basi tuelewe kuwa Ufalme wa Mungu unakaribia, hii ina maana gani mtini unawakilisha Taifa la Israel na miti mingine inawakilisha mataifa mengine, Kwa msingi huo leo tutachukua Muda kuuchambua mti wa mwerezi wa Lebanon kisha tutaanza kuona namna mti huo unavyotufundisha kitu katika maisha ya kiroho.


Mwerezi ni mti wenye historia katika nchi ya Lebanon. Hujulikana sana kama (Mti wa Furaha na Neema n- the joy and Grace  tree) hukua mpaka kufikia futi 130 hivi na matawi yake hunyooka vizuri, ni wa kijani siku zote kwa muda wa mwaka mzima. Mizizi yake huenda chini sana Hosea 14:5-6 “Nitakuwa kama umande kwa Israeli; naye atachanua maua kama nyinyoro, na kuieneza mizizi yake kama Lebanoni. Matawi yake yatatandaa, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake kama LebanoniInasemekana kuwa matawi ya muerezi hunyooka kwa mfano wa pyramid na kukua mpaka kufikia futi 30-50 hivi.



Historia ya mwerezi wa Lebanon inaanzia miaka mingi nyuma kabla Yesu hajazaliwa, kwa mfano katika Isaya 2:13 Unatajwa kama moja ya miti mirefu duniani Isaya 2:13Na juu ya mierezi yote ya Lebanoni iliyo mirefu na kuinuka, na juu ya mialoni yote ya Bashani” Ni mti unaostahimili hali zote za hewa yaani za baridi kali na joto pia.  Inadumu duniani kwa zaidi ya miaka 1000-2000 maisha yake.


Mwerezi hukua taratibu sana na hivyo kuufanya kuwa mti wenye mbao imara. Kwa sababu hiyo mierezi ya Lebanon imekuwa ikikatwa kwa wingi tangu enzi za mfalme Suleiman (na wafalme wengine pia) Wakati wa Mfalme Sulemani aliitumia mierezi ya Lebanon katika ujenzi wa hekalu la Yerusalemu hivyo ni Mti utumikao au uliotumika Kujenga Nyumba ya Mungu. 


Mierezi ya Lebanon imekuwa pia ikitumiwa na wenyeji wake kutengenezea mashua ambazo ziliwawezesha kuwa wafanyabiashara wa kwanza wa kimataifa. Mti huu Mzuri wenye kukua kwa mfano wa Pyramid kwa umbile lake, pia mafuta yake hutumika kutengenezea manukato na pia picha yake wengi wameitumia kutengeneza Cheni za namna mbalimbali na kuzivaa shingoni kama ishara ya furaha, nguvu na kilele cha mafanikio.

Hata hivyo kutokana na ukataji uliokithiri, mierezi imekuwa michache sana katika nyakati hizi. Kwa mfano kusini mwa Lebanon ni ngumu hata kuamini kwamba kuliwahi kuwa na misitu yenye miti mikubwa na kuiletea sifa nchi ya Lebanon. Imebaki miti michache katika maeneo ya kaskazini karibu na mpaka wa Syria


Kutokana na historia iliyotukuka ya mwerezi, mti huo umewekwa katikati ya bendera ya nchi ya Lebanon na kuwa miongoni mwa alama muhimu za taifa la Lebanon. 


Nyakati za Biblia mbao ya mwerezi wa Lebanon ilikuwa ndio mbao imara na yenye ubora ambayo ilikuwa haiwezi kuharibika kwa haraka, wala kushambuliwa na wadudu, Nchi ya Lebanon ndio ilikuwa maarufu kwa aina hii ya miti na misitu ya mti huo mashuhuri wa kifahari na imara, mti huu ni mti mzuri sana, ni mti unaosifiwa kwa uzuri katika biblia unatajwa kama mti mzuri kuliko miti yote kiasi ambacho miti mingine inauonea wivu na inatamani kuwa kama mwerezi   


Ezekiel 31:3-9 “Tazama, Mwashuri alikuwa mwerezi katika Lebanoni, wenye matawi mazuri, na kifuniko chenye uvuli, na kimo kirefu; na kilele chake kilikuwa kati ya matawi mapana. Maji yalimlisha, vilindi vilimsitawisha; mito yake ilipita pande zote za miche yake; naye akapeleka mifereji yake kwa miti yote ya kondeni. Basi kimo chake kilitukuzwa kuliko miti yote ya kondeni, na vitanzu vyake viliongezeka; matawi yake yakawa marefu, kwa sababu ya maji mengi, alipoyachipuza. Ndege wote wa angani walifanya vioto vyao katika vitanzu vyake, na chini ya matawi yake wanyama wote wa kondeni walizaa watoto wao, na chini ya uvuli wake mataifa makuu yote walikaa. Basi hivyo alikuwa mzuri katika ukuu wake, katika urefu wa matawi yake; maana mizizi yake ilikuwa karibu na maji mengi. Mierezi ya bustani ya Mungu haikuweza kumficha; misunobari haikuwa kama vitanzu vyake, na miamori haikuwa kama matawi yake, wala bustanini mwa Mungu hamkuwa na mti wo wote uliofanana naye kwa uzuri. Nalimfanya kuwa mzuri kwa wingi wa matawi yake; hata miti yote ya Adeni, iliyokuwa ndani ya bustani ya Mungu, ilimwonea wivu.”


Mwerezi wa Lebanon umetajwa katika Agano la kale mara kadhaa sehemu nyingi mara 103, unawakilisha Utajiri na ufahari, Mfalme yeyote maarufu wa nyakati za Biblia alijenga nyumba yake kwa kutumia Mwerezi, Daudi alitumia mierezi kujenga Ikulu yake 

2Samuel 5:11, 7:2 ona 5:11. “Kisha Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na maseremala, na waashi; nao wakamjengea Daudi nyumba”. 7:2 “mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. 

Mfalme Daudi aliona kuwa anakaa katika nyumba ya kifahari iliyojengwa kwa kutumia mierezi na aliona kwanini Sanduku la Bwana Mungu wake lisijemgewe nyumba, Mierezi hali kadhalika ilitumika katika ujenzi wa HEKALU maana yake ya kiroho tutaiona baadaye 


1Wafalme 5:6 “Basi uamuru wanikatie mierezi ya Lebanoni; na watumishi wangu watafuatana na watumishi wako; na ujira wa watumishi wako nitakupa kama utakavyosema; kwa kuwa wajua ya kwamba hakuna kwetu mtu ajuaye kukata miti kama Wasidoni. Ikawa, Hiramu aliposikia maneno yake Sulemani, alifurahi sana, akasema, Na ahimidiwe Bwana leo, aliyempa Daudi mwana mwenye akili juu ya watu hawa walio wengi. Hiramu akatuma watu kwa Sulemani, akasema, Nimeyasikia yale uliyoniletea; nami nitafanya kila ulitakalo katika habari ya miti ya mierezi, na miti ya miberoshi

 
Mierezi ilitumika kujengea mahali pote ambapo Sanduku la agano la bwana lilipaswa kukaa 1Wafalme 6:15-19 “Akazijenga kuta za nyumba ndani kwa mbao za mwerezi; toka sakafu ya nyumba hata boriti za juu, akazifunika ndani kwa mti; akafunika sakafu ya nyumba kwa mbao za mberoshi. Akajenga mikono ishirini pande za nyuma za nyumba toka chini hata juu kwa mbao za mwerezi; naam, ndani akaijengea chumba cha ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu. Nayo nyumba, ndiyo hekalu la mbele, ilikuwa mikono arobaini. Na ndani ya nyumba, mlikuwa na mwerezi ulionakishiwa maboga na maua yaliyofunuka wazi; mlikuwa na mwerezi mahali pote; wala mawe hayakuonekana. Akaweka tayari chumba cha ndani katikati ya nyumba ndani, ili atie humo sanduku la agano la Bwana.


Wakati wa ujenzi wa Hekalu la pili pia baada ya hekalu la Sulemani kubomolewa bado tena Mwerezi ulitumika kulijenga tena upya hekalu Ezra 3:7 “Tena waliwapa waashi na maseremala fedha; wakawapa watu wa Sidoni, na watu wa Tiro, chakula, na vinywaji, na mafuta, ili walete mierezi kutoka Lebanoni mpaka Yafa kwa njia ya bahari, kwa kadiri walivyopewa ruhusa na Koreshi, mfalme wa Uajemi. Kama mtu alikuwa na mierezi mingi sana ilikuwa ni ishara ya mafanikio makubwa sana, Daudi na Sulemani mwanae walitumia mierezi katika ujenzi na hasa mierezi ya Lebanon kwa sababu huko ndiko ilikokuwa inapatikana mierezi iliyo bora zaidi.


Ukweli ni kwamba Mierezi ni zawadi kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu, ni sihara ya uzuri, nguvu na wema, Mierezi ya Lebanon iliitwa miti ya Bwana aliyoipanda mwenyewe Zaburi 104:16 “Miti ya Bwana nayo imeshiba, Mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.”


Kwa hiyo ni muhimu vilevile kukumbuka kuwa hatupaswi kuwa na majivuo na kiburi kwa jambo lolote ambalo ni zawadi au karama kutoka kwa Mungu, kwa msingi huo kama watu watajivuna kama mierezi Mungu ameahidi kuwa atawakatilia mbali, Mungu ana nguvu kubwa sana na sauti yake inaweza kuivunjilia mbali Mierezi hakuna mwenye nguvu kumshinda Mungu hivyo mierezi haipaswi kujivuna Zaburi 29:5 “Sauti ya Bwana yaivunja mierezi; Naam, Bwana aivunja-vunja mierezi ya Lebanoni;”  

     
Ni kutokana na ubora na ufahari na uzuri wa mti huu Nchi ya Lebanon inayoongozwa na Rais Mkristo, na waziri mkuu muislamu, wa madhehebu ya Suni na spika wa bunge muislamu wa madhehebu ya shia kwa mujibu wa sheria na mikataba yao, utaweza kuona bendera ya taifa hili na nembo ya rais wa nchi hii ina alama ya mti wa mwerezi.




Mwerezi


Kuna mierezi ya aina nyingi sana Duniani Lakini Mwerezi wa Lebanon ndio pekee unaoweza kukua na kufikia futi zipatazo 130 aidha mataiw yake hukuwa kwa umbile la mfano wa pyramid kwa ukubwa wa kati ya futi 30-50 na hivyo kufanya msitu mkubwa na mzito unaotegemewa na ndege na wanyama mbalimbali ,ni mti mkubwa na mnene na imara sana Isaya 37:24, “Umemshutumu Bwana kwa watumishi wako, kwa kuwa umesema, Kwa wingi wa magari yangu nimepanda juu ya vilele vya milima, mpaka mahali pa ndani ya Lebanoni; nami nitaikata mierezi yake mirefu, na misunobari yake mizuri, nami nitaingia ndani ya mahali pake palipoinuka, palipo mbali sana, msitu wa shamba lake lizaalo sana.” Kibiblia mtu mwenye haki anafananishwa na Mwerezi wa Lebanon, Mizizi ya Mwerezi huenda chini sana na hivyo kuufanya mti huu pia kuwa na uwezo wa kwenda juu mno, Ukuwaji wake unafananishwa na ukuaji wa mtu imara kiroho kama jinsi mtu anavyokua na kufika katika cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo, ukuaji wake unafananishwa na ukuaji katika Nyanja zote za mtu wa Mungu, kukua katika imani, kuikulia neema ya Mungu, kukua katika unyenyekevu, kukua kwa kujikana na utii kwa Mungu na katika kumjua Yesu Kristo,  na kujitoa katika kumuelekea Mungu na kuutafuta uso wake, aidha Mwerezi ni mti ambao haufi na una uwezo mkubwa sana wa kuvumilia joto na baridi hii ni sawa na hali ya mtu wa Mungu aliyemuaminifu ambaye hawezi kuondoshwa katika imani linapokuja swala la kumtegemea na kumuamini Mungu.


Mambo ya kujifunza kutoka kwa Mwerezi.


1.     Unawakilisha watu wanaostahili kuwa Nguzo katika nyumba ya Mungu.
Mwerezi ndio mti pekee imara uliotumika wakati wa Sulemani katika ujenzi wa Hekalu la Mungu 2Nyakati 2:1-9,16,Basi Sulemani alikusudia kujenga nyumba kwa jina la Bwana, na kuujengea ufalme wake nyumba. Sulemani akahesabu watu sabini elfu wawe wachukuzi wa mizigo, na watu themanini elfu wawe wachongaji milimani, na elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi wao. Sulemani akatuma watu kwa Hiramu mfalme wa Tiro,akisema, kama ulivyomtendea baba yangu Daudi, na kumletea mierezi, ajijengee nyumba ya kukaa, unitendee na mimi.Angalia, najenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wangu, ili kumfanyia wakfu, ya kufukizia mbele zake fukizo la manukato, na ya mkate wa wonyesho wa daima, na ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na za siku za sabato, na za mwezi mpya, na za sikukuu zilizoagizwa za Bwana, Mungu wetu. Hili ni agizo la milele kwa Israeli. Nayo nyumba nitakayoijenga ni kubwa; kwa sababu Mungu wetu ndiye mkuu juu ya miungu yote. Lakini ni nani awezaye kumjengea nyumba, ikiwa mbingu hazimtoshi, wala mbingu za mbingu? Nami ni nani basi, hata nimjengee nyumba, isipokuwa kwa ajili ya kufukizia fukizo mbele zake? Unipelekee basi mtu mstadi wa kazi ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya urujuani, na nyekundu, na samawi, mwenye kujua kuchora machoro, pamoja na wastadi walioko Yuda na Yerusalemu pamoja nami, aliowaweka baba yangu Daudi. Niletee tena mierezi, na miberoshi, na miti ya msandali kutoka Lebanoni; maana najua ya kwamba watumishi wako hujua sana kuchonga miti Lebanoni; na tazama, watumishi wangu watakuwa pamoja na watumishi wako, ili wanitengenezee miti kwa wingi; kwani nyumba nitakayoijenga itakuwa kubwa ajabu.” 


 Bila Mierezi Hekalu la suleimani lisingeliweza kusimama na kudumu kwa muda mrefu


Mierezi inawakilisha watu wenye sifa watu walio karibu na Yesu wanaojua ufunuo tofauti na wengine kuhusu Yesu, wenye siri za kipekee kutoka kwa baba kuhusu Yesu, waliojengeka walio imara ambao wanaweza kuliimarisha kanisa hawa wanafananishwa na mwerezi  


Ufunuo 3:7-12 7. “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye. Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu. Tazama, nakupa walio wa sinagogi la Shetani, wasemao kwamba ni Wayahudi, nao sio, bali wasema uongo. Tazama, nitawafanya waje kusujudu mbele ya miguu yako, na kujua ya kuwa nimekupenda. Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi. Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako. Yeye ashindaye, nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo tena kabisa, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, na jina la mji wa Mungu wangu, huo Yerusalemu mpya, ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, na jina langu mwenyewe, lile jipya.” Petro, Yakobo na Yohana walikuwa ni wanafunzi wa Yesu walioimarika kwa viwango vya juu zaidi na hivyo walihesabika kuwa Nguzo katika kanisa la Kwanza 


Wagalatia 2:1-9Kisha, baada ya miaka kumi na minne, nalipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua na Tito pamoja nami. Nami nalikwenda kwa kuwa nalifunuliwa, nikawaeleza injili ile niihubiriyo katika Mataifa, lakini kwa faragha kwa hao walio wenye sifa, isiwe labda napiga mbio bure, au nalipiga mbio bure. Lakini Tito aliyekuwa pamoja nami, naye ni Myunani, hakulazimishwa kutahiriwa. Bali kwa ajili ya ndugu za uongo walioingizwa kwa siri; ambao waliingia kwa siri ili kuupeleleza uhuru wetu tulio nao katika Kristo Yesu, ili watutie utumwani; ambao hata saa moja hatukujitia chini yao, ili kwamba kweli ya Injili ikae pamoja nanyi. Lakini wale wenye sifa ya kuwa wana cheo; (walivyokuwa vyo vyote ni mamoja kwangu; Mungu hapokei uso wa mwanadamu); nasema, hao wenye sifa hawakuniongezea kitu; bali, kinyume cha hayo, walipoona ya kuwa nimekabidhiwa injili ya wasiotahiriwa, kama vile Petro ya waliotahiriwa;(maana yeye aliyemwezesha Petro kuwa mtume wa waliotahiriwa ndiye aliyeniwezesha mimi kwenda kwa Mataifa); tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;” 

Wanafunzi wenye sifa kuwa ni nguzo, walikuwa na ufahamu wa Tofauti na wanafunzi wa kawaida, walimfahamu Yesu kwa viwango vya juu zaidi na Sauti ya Mungu baba waliwahi kuisikia kwa ukaribu na uwazi, waliweza kujua ufunuo wa Torati na manabii, walimjua Musa na Eliya 

Mathayo 17:1-5Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye. Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye. Na wale wanafunzi waliposikia, walianguka kifulifuli, wakaogopa sana.  Yesu akaja, akawagusa, akasema, Inukeni, wala msiogope. Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu ye yote habari ya maono hayo, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu.

 Yesu Katika Utukufu wake akitokewa na Musa na Eliya, Petro, Yakobo na Yohana wenye sifa kuwa ni Nguzo pekee walilishuhudia tukio hili.


Kwa sababu hiyo ili mtu awe nguzo katika kanisa la Mungu, mitume hawakuruhusu awe mtu alkiyeokoka hivi karibuni, viongozi katika kanisa la Mungu ni nguzo wanapaswa kuwa watu wenye uzoefu wa kutosha katika wokovu, kisha baadaye ndipo wateuliwe kuwa viongozi 1Timotheo 3:6 “Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.Mwerezi hauwezi kuwa na manufaa unapokuwa mchanga, ni Muhimu kufahamu kuwa Mungu anataka watu waluioshiba neno lake waliojengeka kwenye neno lake ambao sio watu wa kuyumbishwa yumbishwa na kila aina fulani ya upepo, watu wenye msimamo watu wagumu katika imani, walimmeza Yesu watu ambao Yesu kristo ameumbika ndani yao kwa wingi, wasio na uchanga, waliokomaa hawa ndio waaweza kufananishwa na mwerezi wa Lebanon.

 
2.     Unawakilisha watu wanaoweza kustahimili katika mazingira yote. 


Tunaendelea kuuchimba na kujifunza kuhusu mti huu wa Mwerezi wa Lebanon ambao kitaalamu unaitwa “Cedrus Libani” mti huu una sifa nyingi na za kipekee ni alama ya Utakatifu, Amani, uvumilivu na umilele, ni mti ambao pia kwa mujibu wa mwanamashairi maarufu wa Ufaransa Alphonse de Lamartine aliuita mti huu Mnara mashuhuri wa asili Duniani, hapa sasa nataka kuzungumzia sifa ya mwerezi katika eneo la uvumilivu au kustahimili.

Tumeelezwa wazi kuwa mti wa Mwerezi katika sifa zake unauwezo mkubwa sana wa kustahimili hali zote yaani wakati wa Baridi na wakati wa joto, majani yake huwa ya kijani wakati wote, kiroho unawakilisha watu wanaoweza kustahimili katika hali zote, ni mfano wa watu wanaoweza kusimama na Mungu aidha hali ikiwa njema ama ikiwa mbaya wana uwezo mkubwa wa kustahimili mabaya na uvumilivu na kumkubali Mungu katika hali zote, manabii wengi wa bwana walikuwa watu wa namna hii Yakobo 5:10-1 “Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma”. Ayubu alikuwa ni mfano wa watu waliostawi kwa Mungu katika hali zote.


Alikuwa Tajiri mno lakini utajiri wake haukuweza kumfanya amuache Mungu, aliendeleza ibada na kumtanguliza Mungu, Utafiti unaonyesha kuwa wako watu ambao maisha yakifanikiwa huwa Mungu anakuwa hana maana tena, mafanikio yanawapelekesha kiasi ambacho Mungu anakuwa hana maana Ayubu alikuwa tajiri lakini hakumuacha Mungu aliendelea kushikamana naye wakati wa Raha ona Ayubu 1:1-5 “Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. Kisha walizaliwa kwake wana saba, na binti watatu. Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watu wa nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki. Nao wanawe huenda na kufanya karamu katika nyumba ya kila mmoja wao kwa siku yake; nao wakatuma na kuwaita maumbu yao watatu ili waje kula na kunywa pamoja nao. Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote.” Lakini sio hivyo tu hata wakati wa misukosuko bado Ayubu aliendelea kushikamana na Mungu, hakuweza kusema kuwa nataachana na Mungu kwa sababu eti anapitia magumu, tena wakati wa Ayubu hakukuwa na ufunuo kama tulio nao kuhusu shetani kwani Ayubu alijua kuwa kila baya lililompata lilikuwa limetoka kwa Mungu, Mateso yote yalitoka kwa ibilisi japo Mungu alimruhusu ili kuonyesha kwake kuwa Ayubu ni mtu mwenye msimamo na anayeweza kustahimili mazingira yote.


·         Alipatwa na majaribu mfululizo Ayubu 1:13-19Ilitukia siku moja hao wanawe na binti zake walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, mjumbe akamfikilia Ayubu na kumwambia, Hao ng'ombe walikuwa wakilima, na punda walikuwa wakilisha karibu nao; mara Waseba wakawashambulia, wakawachukua wakaenda nao; naam, wamewaua hao watumishi kwa makali ya upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wakaldayo walifanya vikosi vitatu, wakawaangukia ngamia, wakaenda nao, naam, wamewaua wale watumishi kwa makali ya upanga; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wanao na binti zako walikuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa; mara, tazama, upepo wenye nguvu ukatoka pande za jangwani, ukaipiga hiyo nyumba pembe zake nne, nayo ikawaangukia hao vijana, nao wamekufa; na mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.


·         Ayubu ni mtu aliyeteseka mno kuliko mtu awaye yote “Ayubu 3:24- 26, Kwani kuugua kwangu kwaja kana kwamba ni chakula, Na kunguruma kwangu kumemiminika kama maji. Maana jambo hilo nichalo hunipata, Nalo linitialo hofu hunijilia. Mimi sioni raha, wala situlii, wala kupumzika; Lakini huja taabu.”


·         Alipata maumivu makali kiasi cha kuchagua kufa kuliko aina ya maumivu aliyoyapata Ayubu 7: 15, “Hata nafsi yangu huchagua kunyongwa, Na kuchagua kifo kuliko maumivu yangu haya.”


·         Ayubu aliugua na kuoza na kutoa harufu kwa majipu mabaya Ayubu 13: 28,Nijapokuwa ni kama kitu kilichooza, kinachosinyaa, Mfano wa nguo iliyoliwa na nondo.”


·         Kila mtu aliyemjua Ayubu hakumuheshimu tena na kila mtu alimkimbia hata mke wake Ayubu 19:13-21, “Amewaweka ndugu zangu mbali nami, Na wanijuao wametengwa nami kabisa. Watu wa mbari yangu wamekoma, Na rafiki zangu niwapendao wamenisahau. Wakaao nyumbani mwangu, na vijakazi vyangu, wanihesabu kuwa mgeni; Mimi ni mgeni machoni pao.  Namwita mtumishi wangu, wala haniitikii, Ingawa namsihi kwa kinywa changu. Pumzi zangu ni kama za mgeni kwa mke wangu, Nami ni machukizo kwa ndugu zangu. Hata watoto wadogo hunidharau; Nikiondoka, huninena. Wasiri wangu wote wanichukia; Na hao niliowapenda wamenigeukia. Mfupa wangu unagandamana na ngozi yangu na nyama yangu, Nami nimeokoka na ngozi ya meno yangu tu. Nihurumieni, nihurumieni, enyi rafiki zangu, Kwa maana mkono wa Mungu umenigusa


·         Ngozi ya Ayubu iliharibiwa vibaya alikata tamaa Ayubu30: 16-18,27-30 “Sasa nafsi yangu inamwagika ndani yangu; Siku za mateso zimenishika.Wakati wa usiku mifupa yangu huchomeka ndani yangu, Na maumivu yanayonitafuna hayapumziki. Kwa ugonjwa wangu kuwa na nguvu nyingi Mavazi yangu yameharibika; Hunikaza kama shingo ya kanzu yangu, 

Matumbo yangu yatokota, wala hayaachi; Siku za taabu zimenijilia.Ngozi yangu ni nyeusi, nayo yanitoka, Na mifupa yangu imeteketea kwa hari

·         Hata pamoja na majanga haya yote jamaa alisimama na kuendelea kumuamini Mungu aliamini kuwa Mungu yu hai nay a kuwa atamtetea siku moja na kuwa hata bila mwili wake atamuona Mungu Ayubu 19:25-27 “Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine. Mtima wangu unazimia ndani yanguunaona Ayubu hakuwa mtu wa kuyumbishwa na hali zinazomzunguka alikuwa imara alisimama kama mwerezi aliweza kustahinili hali zote hiki ndio Mungu anachokitafuta kwa watu wake watu wa namna hii atawafanya kuwa nguzo katika nyumba ya Mungu.




Bendera ya Jeshi la Ulinzi la Lebanon kukiwa na alama ya mti wa Mwerezi!


Mungu anajivunia watu ambao wanaweza kustahimili hali zote, Mapema Bwana Yesu alipokuwa akiwafundisha wanafunzi wake katika hutuba ya mlimani alihitimisha mafundisho yake kwa kuonyesha kuwa anataka watu imara ambao wataimarika kwa Mafundisho yake kiasi ambacho hawataogopa Dhuruba za aina yoyote Mathayo 7:24-27 “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga;mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa”.            


Unaweza kuona Mungu anapendezwa na watu imara watu wenye msimamo wasioyumbishwa katika imani kwa sababu zozote zile, Ayubu anatajwa kuwa mfano wa watu hao kwa sababu alipokuwa na kitu alionyesha imani kwa Mungu na hata kila kitu kilipoondolewa kwake bado alisimama na Mungu, hakuweza kuyumbishwa kwa sababu zozote zile Yeye alistawi katika Mungu katika mazingira yote watu wa namna hii katika imani ni Mwerezi wa Lebanon,  watu wenye uwezo wa kumzalia Mungu matunda wakati wote bila kujali ni mazingira gani yanawazunguka Yesu alitoa mfano wa watu hao kama mbegu iliyomea kwenye mnchanga ilihali wale wasiona uwezo wa kustahimili haraka sana majaribu yakija wanashndwa kusimama na kunyauka 


Mathayo 13:3-8,20-21 “Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda.Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila;  nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina; na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka. Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga; nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. “Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa.  

   
Kustahimili misukosuko na majaribu lilikuwa mojawaponya somo muhimu nyakati za kanisa la kwanza, mitume waliwaeleza wazi wakristo kuwa imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi mno Matendo 14:21-22 “Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.” 

 Nyakati za kanisa la kwanza somo kuhusu nustahimilivu ndio lilikuwa somo kuu, somo kuhusu kustahimili majaribu lilikuwa somo muhimu sana ilikuwa ndio injili, lakini nyakati za leo watu wanataka kusikia utapata upenyo, mambo yako yatakunyookea, pokea na kadhalika, Mwerezi ni watu wanaoweza kushahimili mazingira yoyote, Leo hii watu wanaweza kumuacha Mungu kirahisi tu, wanashindwa kuwa wavumilivu, wanaweza kuacha wokovu kwa sababu zilizo nyepesi sana zisizo na uzito, Mungu anataka watu imara watakaosimama katika hali zote, na kulitukuza jina lake  hata katika saa ya kujaribiwa, lazima imani yetu iwe thabiti katika kiwango cha kuwa imara, iwe unaumwa au la! Hali yoyote ile, uwe umeolewa au la lazima ufikie wakati tukubaliane kuwa Mungu anabaki kuwa Mungu tu na tuendelee kumuadhimisha tukisubiri kwa uaminifu.


3.     Unawakilisha watu wenye subira au uwezo wa kuvumilia kwa muda mrefu.


Moja ya tatizo kubwa ambalo limewasumbua watu wengi, hususani kanisa ni tabia ya kukosa Subira, mwerezi wa Lebanon ni mti unaosubiri na unaelewa kuwa utakuwa mti mrefu sana kuliko miti yote, lakini haukui kwa haraka, unachukua muda mrefu kukua na kufikia katika kilele kinachompa Mungu utukufu mkubwa huku ukiwa ni mti imara sana, Mwerezi huwa haunung’uniki kupitwa na miti mingine kwa haraka kwa sababu hatima yake huwa mrefu kuliko miti mingine kwa hiyo hauogopi kupitwa, kitaalamu mti wa mwerezi unakawia sana kukua unakua polepole na mpaka uweze kufaidika nao inachukua miaka mingi inasemekana kuwa kitaalamu mti wa mwerezi hukua kwa kiwango cha sentimita 6-12 kwa mwaka hiki ni kiwango kidogo sana cha ukuaji na ni cha polepole mno,  kumbuka kuwa mti wa mwerezi unafananishwa na mtu mwenye haki katika zaburi ile ya 92 na mtu mwenye haki maana yake ni wale wanaomuamini Mungu, wakimtegemea yeye na kufuata ahadi zake na mausia yake hawa ni watu wanaosimama imara katika imani kwa maizingira yote, wakiwezeshwa kwa neema ya Mungu kustahimili magumu yote na mpaka wakifikia ngazi ya kuzaa matunda na kuonyesha uzuri katika maisha na kuonyeshwa lile kusudi la Mungu lililokusudiwa kwao utakuja kugundua kuwa wanachukua Muda mrefu mno, hii ina maanisha kuna maswala mengine katika ufalme wa Mungu na katika maisha ya ukristo yanachukua muda mrefu mno na inaweza kuwa safari ya taratibu sana kwa kweli kama mtu hana subira huwezi kusubiria matunda na kufaidika na mwerezi hata kidogo katika eneo hili tunajifunza nini yako maswala kadhaa ya kujifunza:-


Ni muhimu kuwa na ufahamu kwamba kama ungepanda miti ya mierezi mpaka uje unufaike na matunda yake inachukua muda mrefu sana, wako watu Mungu anapowaita katiia neema ya wokovu na hata katika neema ya kumtumikia Mungu wanahitajinsana kuvumiliwa mpaka wafikie hatua ya kumtumiakia Mungu katika viwango bora zaidi, Hakuna mtumishi mzuri wa Mungu katika biblia ambaye aliibuka tu kama mchicha wengi iliwachukua Muda mrefu mpaka kuwa watumishi wenye kufaa, Mungu alichukuliana nao sana katika maswala ya udhaifu, na taratibu, aliendelea kuwavumilia kisha baadaye wakawa wenye kufaa


John Mark ambaye ndiye Mwandishi wa injili ya Marko aliambatana na Barnaba na Paulo Mtume katika safari ya kwanza ya umisheni na kutokana na ugumu wa kazi za kimisheni alikata tamaa na kurejea nyumbani  

Matendo 13:13 “Kisha Paulo na wenziwe wakang'oa nanga wakasafiri kutoka Pafo, wakafika Perge katika Pamfilia. Yohana akawaacha akarejea Yerusalemu.” Yohana anayetajwa hapa alijulikana pia kama Yohana Marko na baadaye ndiye aliyekuja kuwa mwandishi wa injili ya Marko, kutokana na kuwaacha wamisionari na kurejea nyumbani Paulo hakufurahi na hivyo katika safari ya pili ya umisheni Paulo hakutaka kuambatana naye lakini Barnaba alitaka kuambatana naye hivyo ilibidi safari ya kimisheni igawanyike 

Matendo 15:36-40 “Baada ya siku kadha wa kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Mrejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani. Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao. Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini. Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda Kipro. Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na wale ndugu apewe neema ya Bwana.” Unadhani nini kilitokea hapa? ilivyo ni kwamba Barnaba alikuwa Mchungaji alikuwa nimlezi na Marko alikuwa ni kijana mdogo ambaye Mungu alikuwa amekusudia kuja kuandika injili, Marko alikuwa na kama mwerezi unaokuwa polepole alikuwa na madhaifu mengi, alikuwa bado mchanga alipaswa kulelewa na kukuzwa kwa huduma ya Kichungaji, Paulo alikuwa Mwinjilisti alitaka watu walioandaliwa na waliokuwa tayari kwa kazi hivyo Barnaba alikuwa anajua kuwa Bado Marko alihitaji muda, Barnaba alikuwa na Roho ya uvumilivu na subira alifahamu kuwa akimpa Muda Marko atakuja kuwa na faida kubwa katika ufalme wa Mungu, kumbuka kuwa ni barnaba huyuhuyu ndiye aliyemlea Paulo Mtume na ndie aliyemleta Antiokia na ndiye aliyemtambulisha kwa Mitume, Barnabas alikuwa mtu maarufu nyakati za kanisa la kwanza kwa sababu ya kuwajali wengine na kuwalea katika huduma anaonekana kwa mara ya kwanza katika 

Matendo 4:36-37 “Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro,  alikuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume”. Hapo Barnaba ambaye aliitwa Yusufu alianza kujulikana kuwa alikuwa ni mtu wa namna gani, na mitume ndio waliompa jina hilo la Baranaba kwa maana alaikuwa mwana wa faraja, alikuwa ni faraja kuwa katika kanisa, alijitoa kwaajili ya wengine, na sio hivyo tu aliweza kuwavumilia watu na hasa wale waliokataliwa au ambao watu walikuwa hawawaelewi ona  


Matendo 9:26-29Na Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina la Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka. Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao wakajaribu kumwua” 

Unaweza kuona kazi ya Barnaba namna na jinsi alivyokuwa mwenye uwezo wa kuvumiliana na kuchukuliana na kupitia yeye moja ya mitume waliofanya kazi mno kuliko mitume wote alilelewa vema kiimani na Barnaba hata watu walipoona shaka naye yeye alisimama kumtetea, lakini kama haitoshi alipoenda kuchunga kanisa kule Antiokia, alienda mpaka Tarso kumtafuta Sauli/Paulo  na kumleta Antiokia kwa hiyo ni wazi aliweza kuwa mvumilivu na mwenye subira dhdi yaw engine kwa muda mrefu yeye ndio sababu kuu ya kuonekana kwa Paulo mtume ona  


Matendo 11:19-26 “Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao. Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kiyunani, wakihubiri habari njema za Bwana Yesu. Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana. Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia. Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana. Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo” 


Ni Barnaba huyuhuyu aliyemvumilia Paulo ndiye aliyekuwa sasa anataka kulea Marko ili aweze kuja kuwa mwenye kufaa baadaye angalia sasa baada ya miaka kadhaa mbele 2Timotheo 4:11 “Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi.” Unaona Paulo mtume baadaye akiwa mtu mzima anasema Umtwae Marko umlete pamoja nawe maana ananifaa kwa utumishi, ni yeye aliyeona kuwa Marko hafai lakini sasa anamkubali kwa sababu ya kazi ya Barnaba ya kuwavumilia watu.Marko huyu huyu ndiye ambaye alikuja kuandika injiliya Marko tunayoitumia leo kama injili ya kazi 


Kaka zangu dada zangu maranyingi sana tumewahukumu watu kwa haraka kutokana na udhaifu wa kibinadamu, tumewahukumu kutokana na uchanga wao, tukawadhani kuwa hawafai, tumewahukumu kwa sababu wanaanguka kana kwamba sisi ni wakamilifu, tumewahukumu, tumewakomesha watu kana kwamba sisi tunamiliki funguo za Mbinguni, mara kadhaa tumewehesabu watu kadhaa kuwa watu waioweza kufiti tena hatukujua kuwa watu hao ni Mwerezi unakua kidogo-kidogo na kuwa baadaye unakuja kuwa mti mkubwa, lazima ifikie ngazi ya kuyafumbia macho maswala kadhaa kwa kuwasamehe watu makosa yaoa na kuendelea kuwaamini katika nafasi zilezile badala ya kuwaondoa na kuwatupilia mbali kama kiytu najsisi na kisichofaa ni lazima tuwe na uvumilivu kwa watu wengine na kutoa muda wa Malezi, kama mama anavyolea mtoto kwa uvumilivu katika hatua zote za kichanga, kukaa, kutambaa, kusimama, kutembea, lugha na kusoma na kuandika mpaka mtu anakuwa mtu mzima na kutambua uwezo wao na kuwasapoti katika maisha yao mpaka wanakuja kuwa watu wenye kufaa.


Barnaba alikuwa na uwezo wa kuona uweza alionao mtu na kugundua umuhimu wao na hivyo alitaka kuwapa nafasi kubwa mno, ili waweze kukua na kuja kuwa wenye kufaa baadaye,  

1Petro 5:13 Mwenzenu mteule hapa Babeli awasalimu, na Marko mwanangu.” Marko alifanya kazi na mitume wakubwa na alipata habazi za Yesu kwa usahihi na kuja kuwa miongoni mwa waandishi wanne maarufu wa injili, huku injili yake ikimtaja Yesu kama mtendakazi, au mtumishi wa Mungu mkuum, Yule aliyedharauliwa na kukataliwa sasa anakubalika na kutajwa katika nyaraka 

Wakolosai 4:10 “Aristarko, aliyefungwa pamoja nami, awasalimu; na Marko, mjomba wake Barnaba, ambaye mmepokea maagizo kwa habari yake; akifika kwenu mkaribisheni.” 


Nini tunaweza kujifunza kutokana na Marko na uvumilivu uluofanyika kupitia Barnaba, Mpaka baadaye Marko anaonekana kuwa mtu muhimu katika kanisa na mitume wanataka kufanya naye Kazi?

1.      Makosa tuliyoyafanya nyuma hayamaanishi kuwa sisi tutakuwa wakosaji milele!, Ni mungu ndiye anayefanya kazi ndani yetu, yeye anayeukuza mwerezi taratibu anamkuza kila mmoja wetu taratibu ili tumkaribie yeye, kazi ya kubadili mwenendo wa Mtu haifanyi na sisi inafanya na Mungu, ni lazima tuwaache watu na Mungu wao ili kumruhusu Mungu kufanya kazi ndani yao yeye ataendelea na kazi ya utakaso taratibu mpaka yule aliyemuita aona kuwa amefaa

2.      Kama mtu akikosea asifikiri kuwa hawezi kuendelea na huduma, Marko alikuwa kama sisi wengine miongoni mwetu lakini lazima ikumbukwe kuwa wakati mwingine Mungu huchukua miaka kadhaa kutengeneza mtu wake wanaweza kuanguka mara nyingi sana kabla hawajafaa kwa huduma na baadaye wanakuwa watumishi wazuri.

3.      Bado tunaweza kuwarejesha tena wale ambao tuliwaondoa katika mioyo yetu au waliokosea katika maisha yao kwani huwezi kujua watakuwa muhimu kiasi gani baadaye.

4.      Hatujachelewa kuwasamehe wale waliotukosea, sisi sote tunatenda dhambi, sisi sote tunakosea na Mungu ametuvumilia mara kadhaa je si jambo jema tukiwavumilia na sisi wale waliotuudhi, wakati mwingine mtu anaweza akakosea na sisi tukafikiri kuwa hafai tena? Je wewe ndio unaebadilisha watu? Wewe ndio Mungu? Wewe ndio seremala wa Nazarethi? Je wewe ndiye mfinyanzi?, wakati mwingine watu wanaweza kwenda miaka na miaka wakimuhukumu mtu kwa kudhani kuwa yuko vilevile na wanadhani hawezi kubadilika, lakini hebu tuwakumbuke na kuwarejeza uone kama hawatakushangaza !

Achilia wacha kuukata huo mti, uache ukue kama unakuwa taratibu nani ajuaye baada ya miaka kadhaa utakuwa mti mkubwa na Mrefu kama mwerezi na kutumika kama Nguzo katika nyumba ya Mungu, Mierezi inachukua muda kukua kiroho, haina haraka inakuwa taratibu huwezi kula matunda yake kama utakavyo, Viongozi wengi wa kanisa wamejiweka katika kiti cha hukumu cha Mungu na kudhani ya kuwa Mungu amemaliza na mtu fulani, au fulani ndio basi tena nataka nikukumbushe usihukumu mtu wa Mungu, wengina wanaweza kufikiri kuwa mtu fulani hana maana kwao kabisa kwa sababu tu amehama dhehebu lao, huu ni uchanga wa kiroho, mtu kuhama dhehebu lako haimaanishi kuwa ameahama mwili wa Kristo, wala haimaanishi kuwa huwezi kumita na kumtumia, watu wamekuwa wajinga kiroho kwa sababu ya mitazamo duni isiyo ya kimungu wala kiimaandiko, watu ambao ni mwerezi wanao uwezo wa kuwavumilia wengine!


Uvumilivu ni moja ya tabia ya uungu inayoashiria kuwa sisi tumekomaa na kukua ni pamoja na kuwa na tabia kama zile tabia za Mungu, na kumzalia Mungu matunda, matunda ambayo sisi tunapaswa kuyazaa yanatajwa katika Wagalatia 5:22-23 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. 

Neno uvumilivu hapo au subira kwa kiingereza linatumika neno longsuffering yaani uwezo wa kuvumilia 


Katika maisha haya lazima tukue na kuwa na uwezo wa kuvumilia, hatuwezi kusema kuwa tumekomaa katika upendo kama hatuna uwezo wa kuvumilia 1Wakoritho 13:1-7Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.  Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.”


Unaona maandiko yanasema upendo huvumilia, tena yanakazia huvumilia yote, kisha anamalizia hustahimili yote, Katika safari ya kwenda mbinguni ni lazima tuwe wavumilivu, huwezi kuwa Mchungaji, au mwinjilisti au mwalimu wa neno la Mungu kama hauna uvumilivu, vongozi wengi wa kanisa na hata washirika wameumiza wengi makanisani kwa sababu ya kushindwa kuwavumilia, Kama kuna jambo kanisa tunapaswa kuliomba kuwa tuweze kuwa nalo ni uvumilivu long suffering  hii haiji hivi hivi ni lazima uwezeshwe na Mungu hivyo hatuna budi kumuomba Mungu atusaidie  

Wakolosai 1:11 “mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha;” 

 unaona Paulo analiombea kanisa pamoja na mimi na wewe kwamba tutiwe nguvu kwa kadiri ya utukufu wa Mungu tuwe na uwezo wa kusubiri na kuvumilia tukiwa na furaha anapozungumzia kuvumilia maana yake kuwa na uwezo wa kuwavumilia wengine, tuwe na uwezo wa kujidhibiti sisi wenyewe ili tusimkosee Mungu lakini vilevile tusimkosee Mungu kwa kushindwa kuwavumilia wengine, Maandiko yanaonyesha wazi kabisa kuwa hatupaswi kukasirika kwa haraka Mithali 14:29  Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi; Bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu” ukomavu wa kiroho katika Kristo unapimwa kwa uvumilivu


4.     Unawakilisha watu wasioweza kutikiswa, Kuyumbishwa na kuchukuliwa  na kila aina ya upepo.

Biblia inaelezea namna na jinsi ukuaji wa Mwerezi ulivyo, mwerezi ni mti unaokuwa polepole na hivyo mizizi yeke huweza kwenda chini sana na hivyo kuufanya mti huu kurefuka na kwenda juu sana, Mungu anamtarajia kila mtu aliyeokolewa kukua na kufikia hatua ya juu sana ya kilele cha ukuaji wake kumfikia yeye aliye juu ambaye ni Yesu Kristo, Biblia imekazia sana juu ya ukuaji wa kiroho 1Petro2:2 “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;Mungu anataka tuukulie wokovu, tusiwe watoto wachanga wa kiroho wanaochukuliwa na upepo wa kila nammna wa Elimu 

Waefeso 4:11-15 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo 

Unaona Neno la Mungu linakazia kukua Kiroho, ziko “levels” viko viwango ambavyo mtu anatakiwa kukua kiroho, anapaswa kukua kiasi ambacho hataweza kuwa kama unyasi unaotikiswa na upepo, watu wasioyumba kama Yohana mbatizaji, ambaye alikuwa tayari kuingia Gerezani kwaajili ya kusimamia ukweli, ambaye alikuwa tayari kukatwa kichwa kwaajili ya kusimama katika kweli ambaye alisema ukweli., hakumumunya maneno linapokuja swala la kusimamia kweli ya Mungu, ni ukweli usiokanushika kuwa Yohana mbatizazi hakuwa unyasi unaotikiswa na upepo


 Mathayo 11:7-9 “Na hao walipokwenda zao, Yesu alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Tazama, watu wavaao mavazi mororo wamo katika nyumba za wafalme. Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona nabii? Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya nabii” 

 Nyakati tulizo nazo ni nyakati ambazo watu huchukuliwa chukuliwa tu na kila aina ya upepo wa Elimu hawaifahamu kweli halisi ya neno la Mungu, watu wamekuwa wenye kutikishwa huku na kule sababu kubwa ni kuwa watu hawatulii darasani na kujifunza kuhusu Yesu, tumekuwa na watu ambao hawakimbilii mahali kwa sababu kuna mwalimu mzuri anaifundisha kweli ya Mungu bali wanakimbilia mahali kwa sababu kuna miujiza, wanakimbilia mahali kwa sababu watatabiriwa mambo kadhaa katika maisha yao wamesahau kuwa Yesu aliagiza kuwafanya watu kuwa wanafunzi na sio watu wa mikate yaani watu wanaofuata miujiza huku na kule, si unakumbuka Yesu alisema enendeni makwafanye watu kuwa wanafunzi, na sio wakimbilia maombezi, leo hii watu wamekuwa wakihamia kila kanisa badala ya kutulia na kujifunza kweli ya neno la Mungu ili wakue kama mwerezi na wafikie hatua ya kuwa walimu wa wengine, mwerezi hukua taratibu huzamisha mzizi yake chini na hivyo huenda juu sana na hauwi kama unyasi unaotikishwa na upepo unaona? 


Waebrania 5:11-14 “Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia.  Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya. 


Ni lazima tukue na kukomaa kiroho katika ngazi ambayo hatutaweza kutikiswa na mtu awaye yote, hatutaogopa kufa, hatutaogopa mabaya, tutakuwa na kiwango kikubwa cha imani kiasi ambacho, tutakuwa tayari hata kufa kwaajili ya Kristo, na hatutaweza kudanganywa kutokana na kuimarika katika ujuzi wa neno la Mungu. Tutakuwa kama Nehemia aliyeweza kusimama imara katika kazi ya Ujenzi wa ukuta wa Yerusalem ambaye alikuwa na uwezo wa juu sana wa kupambanua maandiko na kuwashinda kina Tobia na Sanbalati watu waliosimama kama mwerezi hawawezi kutikiswa na uzushi, wala uongo wala imani potofu haziwezi kuwaondoa katika kweli ya Kristo., Watu wenye sifa hizi katika maandiko ndio wanaitwa mwerezi wa Lebanon., Kanisa leo limekuwa likishabikia wahudumu wa injili kuliko kumshabikia yeye aliyetufia msalabani, unapoona watu wanashambikia madhehebu, wanayatukuza madhehebu yao kuliko Yesu, wanashabikia wahudumu wa injili kuliko Yesu mwenyewe, ujue wao bado hawajakomaa, bado ni wachanga bado wanatabia za mwilini, hawajakua kama mwerezi. 1Wakoritho 3:1-7 “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu? Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye”. Watu waliokomaa kama mwerezi hawana muda wa kushabikia wahudumu wa injli, haraka sana wanakuwa wanajua nini wanachotakiwa kukifanya wana ukomavu wa hali ya juu, hawajali elimu ya mtu au mahubiri ya mtu bali wao wenyewe kwa uungwana wao nao huchukua muda kuyachunguza maandiko ili waijue kweli bila kujali yanahubiriwa na nani Matendo 17:10-11 “Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi.  Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.” Watu wa Beroya wanatajwa kuwa walikuwa waungwana maana yake wenye hekima, waliyapokea mahubiri ya Paulo mtume kwa uelekevu wa moyo, lakinoi vilevile walichukua muda kuyachunguza maandiko ili wajue au waone kama mambo hayo ndivyo yalivyo, wakristo wazuri wanaofanananishwa na mwerezi, wanapaswa kuwa wanafunzi wa maandiko, wanayachunguza wanajifunza wanachimba, haijalishi cheti alichokuwa nacho Muhubiri., Paulo mtume alikuwa Muhubiri wa viwango vya juu sana lakini hata hivyo bado watu wa Beroya walikuwa na muda wao wa kuyachunguza aliyoyahubiri walikuwa wakiyapima maneno yake kama yako sawa na kile wanachokijua na kukiamini, kizazi cha leo hakina muda huo, waoa wanakimbizana na maombezi, kila siku wanaombewa hawakui kiroho, hawafikii ngazi ya kujua au kujifunza kuomba hata wakaomba wao wenyewe na hata wao wakatumiwa na Mungu kuwaombea wengine, na kutatua matatizo yaw engine kwa sababu ya uchanga miaka inaenda miaka inarudi unaombewa tu wewe utaombea lini, Nyakati zaKanisa la Kwanza sio mitume tu waliofanya ishara na maajabu, na nkuombea wagonjwa hata watu wa kawaida walifungua makanisa, walihubiri injili, walifanya kazi sawa na zile mitume walizifanya kwa sababu walikuwa wakidumu katika fundisho na kuwa na uwezo uleule au hata zaidi ya ule na kazi ya Mungu ikakua kwa kasi sana angalia 

Matendo 6:8 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.” Matendo 8:4-8 “Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule” Matendo 11:19-21 “Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao. Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kiyunani, wakihubiri habari njema za Bwana Yesu. Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana”. 


 Unaona nyakati za kanisa la kwanza watu wa kawaida walitumiwa na Mungu, walitumiwa kufanya miujiza, walitumiwa kugfungua makanisa walitumiwa katika kuhubiri injili hawa walikua walikomaa na kuwa kama mwerezi, mimi sipingani na huduma zozote za maombezi, lakini swali kubwa la msingi ni kuwa nini kinafuata baada ya maombezi na unabii je watu wanakomaa? Watu wanakua kiroho? Watu wanafanyika kuwa wanafunzi wa Yesu? Wanaomaa kiroho ama wanakuwa watu wa kuombewaaaa na kutolewa unabiii mpaka kuibuka nabii mwingine? Je watu wanapata nafasi ya kupambanua na kuyapima mafundisho, je wala tunaowaendea ili kutupa msaada wana malengo ya kutuombea siku zote au kutupeleke akatika ngazi za juu za kiroho na kuwa na ukomavu unataotu pelekea sisi tuwe kama wao?


5.     Unawakilisha kilele cha ujuzi, ufahamu na hekima ya juu!


Ile tabia ya ukuaji wa mierezi na kufikia hatua ya juu kabisa kuliko miti mingine iliufanya mti huu kuitwa Mfalme wa miti yote, ukuaji wake na uwezo wake wa kuipita miti mingine unawakilisha ujuzi, ufahamu, hekima na maarifa ya juu zaidi kwa binadamu, hivyo mtu mwenye hekima pia huitwa mwerezi wa Lebanon 

1Wafalme 4:30-33Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya wana wote wa mashariki, na hekima zote za Misri. Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka. Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano. Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki” 

Ujuzi wa hali ya juu, ufahamu na hekima na maarifa katika kumjua Mungu hukufanya kuwa kama mwerezi, Mungu anataka kila mtu aliyeokolewa ajae hekima awe na Hekima  

Yakobo 1:5 “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.”  Wote tunajua kuwa katika agano la kale na agano jipya na katika maisha haya hekima ni ya muhimu sana kila mahali walipo wenye hekima watatatua matatizo na kuleta suluhu ya mahitaji ya watu na  kwa jamii, Kigezo kikubwa cha kupata viongozi ambao wangetatua tatizo katika jamii na kanisa ni watu waliojaa Roho Mtakatifu na Hekima Matendo 6:3Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili;” ni wazi kuwa Petro alishakuwa na ujuzi uliowazi kuwa wenye hekima hutatua matatizo ya jamii, wenye hekima wana mawazo ya juu kabisa yenye kuweza kuisaidia jamii, wenye hekima ni kama mwerezi  Sulemani alikuwa ni mfano wa mti wa mwerezi kwa hekima aliweza kutatua matatizo magumu yaliyomkumba mtu yeyote na hata kutoa suluhu ya kilicho nyuma ya maswali yake tunaelezwa kuwa Malkia wa Sheba alikwenda na maswali magumu aliposikia Hekima ya Suleiman na kila alichokiuliza kilijibiwa na kuzidi 1Wafalme 10:1-8 “Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la Bwana, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo.Akaingia Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno alilofichiwa mfalme asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga,  na chakula cha mezani pake, na watumishi wake walivyokaa, na kusimamia kwao wangoje wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana, roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako.” Unaweza kuona namna na jinsi ambavyo hakukuwa na neno lililofichika katika maisha ya Suleimani aliweza kufumbua mafumbo yote na magumu yote malkia aliyokuja nayo Biblia ya kiingereza The Amplified Bible inasema katika mstari wa kwanza b  SHE CAME TO TEST HIM WITH HARD QUESTIONS  Yaani alikuja kumjaribu kwa Maswali magumu, Lakini unaweza kuona Sulemani akiyatatua, Ndio maana kwa uwezo alionao Yesu aliweka wazi kuwa yeye ni mkuu kuliko Sulemani Mathayo 12:42Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.” Yesu ni mkuu kuliko Suleiman yeye ndiye aliyemuumba na ni yeye ndiye aliyempa Hekima Suleimani, Kanisa na watu wa nyakati za leo lazima tumuombe Mungu atupe hekima, watu wengi leo hujiita wachungaji, hujiita mitume, hujiita manabii, hujiita wainjilisti na hujiita Wachungaji na walimu maaskofu na kadhalika lakini nataka kuwakumbusha kuwa Yesu alisema anatuma manabii na wenye hekima Mathayo 23:34 “Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji;” Nashangaa kusikia Yesu ametuma manabii na waandishi yaani walimu na wengine lakini sisikii wenye hekima? Wako wapi? Kanisa la Mungu lazima liwe na “wise men” lazima liwe na wenye hekima, Bila shaka Yesu anawatuma wenye hekima anataka watu wenye hekima na wakiwemo watatatua matatizo ya jamii hawa wanaitwa Mierezi ya Lebanoni., Muda usingeliweza kutosha kueleza habari za Stephano ambaye Hekima yake iliwaazidi wapinzani wa injili mpaka wakaona hakuna njia nyingine zaidi ya kumuua tu, waligundua ni mtu hatari kwa dini ya kiyahudi, aliwazidi kwa hekima mpaka wakamsagia meno Matendo 6:8-10 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.” Wako watu wanadai kuwa Stefano aliuawa kwa kukosa Hekima hii sio kweli, maandiko yanaonyesha alikuwa amejaa Hekima aliuawa na watu wajinga ambao hawakutaka kuiamini kweli aliyoiweka mbele zao, watu wa masinagozi ya kisomi kutoka SIGAGOGI LA MAHURU, SINAGOGI LA WAKIRENE (LIBYA), SINAGOGI LA ISKANDERIA (MISRI), SINAGOGI LA KILIKIA na ASIA, Hawa wote walishindana kwa hoja wakakutana na mtu mwenye hekima mwerezi akawashinda wakaamua kumuua, Biblia hijasema alikuwa nabii, au alikuwa mchungaji lakini alikuwa mwenye hekima kama alivyosema Yesu kuwa atatuma wenye hekima na watawaua! Je leo wako wapi Mungu anataka mierezi ya Lebanon ili aifanye kuwa nguzo katika nyumba ya Mungu, anataka watu wenye uwezo wa kutatua matatizo ya wakristo,watu wenye majibu watu wenye ufumbuzi watru watakaosimama kama waamuzi wa maswala mbali mbali ya wakristo, Watu wengi wa Mungu wameumizwa makanisani kwa sababu tu ya viongozi wabovu waliokosa hekima, walioshindwa kutatua matatizo yao kwa usahihi, wakiitwa watu wengi waliachana katika ndoa zao, wakiitwa wengi waliohama makanisa yao, wakiitwa wengi hata watumishi waliohama madhehebu yao, wakiitwa na kuulizwa wengi waliokutana na changamoto hii au ile utagundua nkuwa sababu zake nyingi ni kukosekana kwa watu wenye hekima, Mungu anataka kanisa liwe nao hao ni muerezi wataweza kuwaweka wakristo pamoja na kuzima migogoro mikubwa ya kikanisa, na kesi nyingi za kijinga na za hovyo hovyo, Hivi majuzi hapa Tanzania kulitokea vipande vya video vilivyokuwa vikidaiwa kuwa ni vya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na uzima ukweli jambo hili liliwagusa watu wengi na liliumiza wengi na lingeweza kuleta madhara makubwa sana kwa mwili wa Kristo lakini aluipotokea Askofu wa Kanisa la full Gospel na kufundisha kwa muda mfupi tu “USIKUBALI MASHITAKA DHIDI YA MZEE” mgogoro ule ulipotelea mbali na kuyeyuka kabisa hii ni kwa sababu mwenye hekima alisimama aliamua kesi na kuzima fukuto kubwa na bila shaka Hata askofu wa ufufuo na Uzima alipata mani na kibali, sababu kubwa ni nini hali ilikuwa mbaya kwa sababu kanisa limejaa wajinga limejaa watu wasio na hekima wengi walikuwa waliunga mkono, wengi labda wangetamani afadhali Gwahima aharibikiwe na sijui ingekuwa ni kwa faida ya nani lakini kile kilichofanywa na Kakobe kama ni kuamua Kesi ilikuwa ni sawa na ile kesi Suleimani aliiamua kwa wanawake waawili waliokuwa wanagombania mtoto hii ndio faida ya kuwa na wenye hekima katika kanisa, Paulo mtume alihopji je kanisa kule Koritho halina watu kama hao? Kwanini watu wa Mungu wapeleke kesi zao mahakamani je kanisa linakosaje wenye Hekina mahalia ambapo Roho Mtakatifu yupo wanakosekaje waru wenye hekima? Tunahitaji watu wa aina hii watakaofikia kilele cha hekima na kuwa kama mwerezi, mwerezi unawakilisha watu wenye hekima!  

1Wakoritho 6:1-6 “Je! Mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala si mbele ya watakatifu?Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya? Basi, mkiwa na mahali panapohukumiwa mambo ya maisha haya, mwawaweka kuwa waamuzi hao waliohesabiwa kuwa si kitu; katika kanisa? Nasema hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima, awezaye kukata maneno ya ndugu zake? Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao wasioamini”.


6.      Unawakilisha watu wanaoishi maisha matakatifu!


Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu ametuita kuishi maisha matakatifu lazima tuseme ukweli huu ndio wito muhimu tulioitiwa UTAKATIFU, kama kuna jambo ambalo kanisa la Mungu linakosa leo ni watu wanaoishi maisha matakatifu na sio tu wanaoishi maisha matakatifu bali pia watu wanaohubiri utakatifu hawa wanaitwa mwerezi wa Lebanon Ushahidi wa kimaandiko unaonyesha wazi kuwa katika Isaya 1:18 “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.” 

 Ni muhimu kufahamu kuwa asili ya neno hili la Isaya “Zitakuwa Nyeupe kama Theluji” neno hilo Theluji analolitumia Isaya katika biblia ya kiibrania ni “LAWBAN” ambalo ni sawa na neno LEBANON ambayo yote kwa pamoja maana yake ni NYEUPE au THELUJI,  Neno hili limetumika hasa kutokana na Milima katika nchi ya Lebanon ambayo imejaa theluji na katika milima hii ndiko ambako Mierezi ilistawi, kutokana na jambo hili mti wa Mwerezi wa Lebanon pia unatumika kuelezea weupe au utakatifu.


Utakubaliana nami kuwa mti wa mwerezi pia ulitumika katika kufanya kazi za utakaso hekaluni au katika hema ya kukutania angalia Mambo ya walawi 14:4-6 Biblia inasemandipo huyo kuhani ataagiza kwamba watwae kwa ajili yake atakayetakaswa ndege wawili walio hai, ambao ni safi, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo; kisha kuhani ataagiza ndege mmoja achinjwe katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni; kisha huyo ndege aliye hai atamshika, na huo mti wa mwerezi, na hiyo sufu nyekundu, na hisopo, naye atavichovya hivyo, pamoja na yule ndege aliye hai, katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa juu ya maji ya mtoni; Unaona kile alichokisema Isaya kuhusu weupe kama theluji na sufu kinakubaliana na ukweli kuwa anazungumzia mwerezi ambao ulitumika kwa kazi za utakaso Hekaluni tuongeze maandiko 

Mambo ya Walawi 14: 49-52 “Naye atatwaa ndege wawili, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo, kwa kuitakasa hiyo nyumba; naye atamchinja mmojawapo wa ndege hao katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni; kisha atatwaa huo mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, pamoja na huyo ndege aliye hai, na kuvichovya vyote katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa, na katika hayo maji ya mtoni, na kuinyunyiza nyumba mara saba; naye ataitakasa hiyo nyumba kwa damu ya ndege, na kwa maji ya mtoni, na kwa huyo ndege aliye hai, na kwa mti wa mwerezi, na kwa hisopo, na kwa sufu nyekundu;” Pia tunaweza kuona katika Hesabu 19:6 “kisha kuhani atatwaa mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, na kuvitupa katika huo moto unaomchoma ng'ombe.


Unaona kwa msingi huo kilele cha juu kabisa cha wito wa maisha yenye kumpendeza Mungu ni kuishi maisha matakatifu, wakristo lazima tukumbuke kuwa tumeitiwa maisha matakatifu 1Petro 1:15-16 “bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu”. Ni muhimu kufahamu kuwa utakatifu ndio tulioitiwa, kila mtu aliyeokoka anapaswa kuhakikisha ya kuwa anautafuta utakatifu kwa bidii na kuwa na amani na watu wote kwani pasipo huo haiwezekani kumuona Mungu Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; 


Watu wa Mungu lazima tuukubalia utakatifu, tusikubali kuchukuliana na dhambi, tusikubali kuwa sisi ni ndhaifu, Mungu hangetuagiza kuishi kile ambacho hatungekiweza najua kuwa mwanadamu ni dhaifu lakini Yesu ana nguvu ya kubadilisha na kubadili mwenendo wetu wote wito unatolewa wa kuacha dhambi, za kila aina tuzifanyazo, wito unatolewa kutubu, tutubu na kuziungama dhambi zetu ili tusamehewe na kuishi maisha matakatifu yanayompendeza Mungu, na tukiishi maisha ya usafi namna hii sisi mbele za Mungu tutakuwa sawa na mwerezi wa Lebanon Mungu atatufanya kuwa nguzo katika nyumba yake, Nyumba ya Mungu kanisa la Mungu haliwezi kushikwa na nguzo mbovu au za waovu, Mungu anataka watu watakatifu wasimame katika imani na kulisimamia neno la Mungu na kuwa tayari kusema mnifuate mimi kama ninavyomfuata Kristo, wakati wa kuishi maisha ya kisanii umepita, wakati wa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu umepita lazima tuishi maisha matakatifu, lazima tuuuhubiri utakatifu lazima tuhakikishe kuwa tunawaambukiza watu utakatifu na sio dhambi, Lazima ufikie wakati tuutetee utakatifu badala ya kuitetea dhambi, Mungu ni mtakatifu watu wake wanaomfuata yeye na kumtaja wanapaswa kuwa watakatifu watu waliojitenga na maovu 2Wakoritho 6:14-18 “.Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike”, 

Mwerezi wa Lebanon unatumika kuelezea Mtu anayeishi maisha matakatifu ambaye yeye pia ni sababu ya watu kuishi maisha matakatifu. Anauhubiri utakatifu analitaja jina la bwana huku yeye aliwa ameuacha uovu 2Timotheo 2:19 “Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu”. Ni vema kufahamu kuwa baada ya kuokolewa Mungu anatutaka tuishi maisha matakatifu, watu ambao ni mwerezi wanapaswa kuishi maisha matakatifu, hakuna namna nyingine tunaweza kumuona Mungu pasipo utakatifu.    

   
7.     Unawakilisha watu wanayoyatoa maisha yao kwaajili ya wengine!


Ni muhimu kufahamu kuwa mierezi pia ilitumika kutengenezea Meli, na kutokana na teknolojia ya wakati huo na hivyo kuifanya nchi ya Lebanon au Phoinecia wakati huo kuwa nchi yenye mafanikio makubwa sana ya kibiashara,


1Yohana 4:10Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu


Kuja kwa Yesu Kristo Duniani ni matokeo ya upendo mkuu wa Mungu kwa mwanadamu, ni matokeo ya juu kabisa ya upendo usioweza kupimika


Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”


Yohana 15:13:-Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake”.


Ni Muhimu kufahamu kuwa upendo unaotajwa hapa sio upendo wa kawaida ni upendo wa kimungu ni upendo wenye huruma za kiungu sio upendo wa kibinadamu kwa kawaida katika lugha ya kiyunani neno upendo lime gawanyika katika tafasiri kuu nne za upendo ambazo ni Phileo, Storge, Eros, na Agape au agapan:- aina hizi za upendo tunaweza kuzichambua kama ifuatavyo:-


·         PHILEO aina hii ya upedno kwa kiingereza tunaiita “Companionable love”yaani ni upendo wa Kirafiki, Ni upendo unaojengeka kutokana na kushirikiana kuzungumza kukubaliana kupeana zawadi,kuendana na kadhalika huu ni upendo wa kirafiki

·         STORGE aina hii ya upendo kwa kiingereza tunaiita “Natural affection love” yaani ni upendo unaotokana na kuweko kwa undugu wa damu, unampenda mtu kwa sababu ni baba, mama, mwana, mjomba shangazi, dadam kaka na kadhalika katika mahusiano ya kindugu na damu

·         EROS aina hii ya upendo kwa kiingereza tunaiita “Erotic love” yaani ni upendo unaotokana na mvuto wa kimapenzi, ni upendo unaohusu jinsia tofauti na yako, unampenda mtu kwa sababu ya muonekano wake , umbile lake na uzuri wake hii husababishwa na mvuto wa kimapenzi, body morphology is concern Muonekana wa mwili au mvuto unahusika na upendo huu ni wa kihisia.

·         AGAPE aina hii ya Upendo kwa kiingereza tunaiitaunconditional love” Yaani ni upendo wenye kupitiliza mipaka ya kibinadamu, ni upendo ambao asili yake ni Mungu ni upendo unaomtakia mema kila mmoja awe adui au ndugu upendo huunapita mipaka ya kawaida ya kibinadamu, hauangalii hali ya hewa, unampenda Mungu au mtu bila kutarajia kitu kutoka kwake, bila kujali mtu huyo ni mwema au mbaya, bila kujali ni wakati mzuri au mbaya, bila kujali ni wakati wa matatizo au raha upendo huu unabaki vilevile na haubadilishwi na matukio, Mungu anapoamuru kupendana au kumpenda Yeye katika maandiko anamaanisha upendo huu wa Agape. Upendo huu pia hujulikana kama Sacrificial love , upendo wenye kujitoa sadaka kwaajili ya wengine, ni upendo unaojali kuwahudumia wengine zaidi ya sisi wenyewe, Huu ndio upendo ulioamriwa katika 1Wakoritho 13 upendo wa kiungu.

1.      Daktari  mmoja wa Uingereza aitwaye Will Pooley alikuwa ni moja ya madaktari waliokuwa mstari wa mbele Nchini “Sierra Leone” huko walikuwa na wenzake wengi wakipambana na wagonjwa wa EBOLA na virusi vyake  katika  harakati hizo Madaktari wengi sana na Manesi wengi sana wakiwemo wa Afrika Magharibi waliambukizwa virusi vya ebola wakati walipokuwa wakiwauguza wagonjwa na wengi wao walikufa


Ugonjwa utokanao na kirusi cha Ebola ni ugonjwa hatari wenye uwezo wa kusababisha kifo kwa asilimia 90.  Shirika la afya duniani, WHO katikatovuti yake inasema kwa mara ya kwanza ulibainika mwaka 1976 huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Sudan. Chanzo cha kirusi hiki hadi sasa hakijulikani lakini popo aina ya (Pteropodidae) wanaonekana kuwa wabebaji wa kirusi hicho, kwa mujibu wa ushahidi uliopo sasa.


Maambukizi hupatikana kwa kila aina ya majimaji yanayotoka katika mwili wa binadamu ni ugonjwa hatari na unaoua kwa haraka na hauna tiba
Will Pooley alipoupata ugonjwa huu alirejeshwa katika ndege maalumu na kuanza kutibiwa chini ya uangalizi maalumu huko uingereza

  
Pichani Doctor Will Pooley  Mwingereza aliyenusurika na Ebola!


Jambo la kushangaza ni kuwa baada ya kupona kwa bahati tu Will Pooley alitangaza nia yake ya kurudi tena Sierra Leone kusaidiana na wenzake kupambana na ugonjwa huo.

Mtu huyu aliwashangaza wengi sana na kuwaogopedha wengi sana akiwa amepona kwa asilimia 100%alisema atarudi Africa kusaidia zaidi maana alizaliwa kwaajili ya hayo, jambo hili lilimfanya aandikwe kama shujaa na mwanadamu mwenye uwezo wa kujitoa kwa kiwango cha juu.

2.      Maximilian Kolbe alikuwa ni Padre aliyetokea Poland aliuawa kama mfungwa tarehe 14 August 14,1941, Jeshi la wa NAZI waligundua kuwa baadhi ya wafungwa wamejaribu kutoroka na hivyo waliamua kuwaua wafungwa kadhaa, walijaribu kuwaua kwa njia mbalimbali, na hivyo walichagua wafungwa 10 ili wauawe na kifo chao kiliamuriwa kuwa kifo cha njaa, wafungwa waliamuriwa kujitoa mmoja mmoja yeye mwenyewe na mfungwa wa kwanza kuchaguliwa alijulikana kama Franciszek Gajowinczek mfungwa huyu alipochaguliwa alilia kwa huzuni kubwa akimtaja mkewe, watoto wake na familia yake na kusikitika kuwa hatowaona tena kutokana na swala hili Maximillian alisimama na kusogea mbele na kuomba afe yeye kwa niaba ya Franciszek ombi lake lilikubaliwa, wafungwa waliwekwa kizuizini kwa muda wa siku kadhaa bila kula wengine walikunywa mikojo yao ili waweze kuishi, Maximillian alikaa kwa wiki mbili bila kufa huku wengine wote wakiwa wamekufa, walimchoma sindano ya kufa hakufa na hivyo waliamua kukata kichwa Pope John Paul II alimtangaza kuwa Mtakatifu kutokana na moyo wake


Pichani Padre Maximilian Kolbe


3.      Mifano hii inatusaidia kujua kile ambacho Bwana wetu Yesu amekifanya Pale alipojibu kuwa kwaajili ya haya Nalizaliwa alikuwa akimkumbusha Pilato kuwa yeye amekuja kuwafia wanadamu, amekuja kuwaonyesha upendo wa Mungu jinsi ulivyo Isaya 53:1-5Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”


Huu ni upendo mkubwa sana Yesu alikufa kwaajili yetu, Hatuna budi kuhakikisha kuwa tunasimama upande wake siku zote za maisha yetu, tusihesabu damu yake ya thamani kuwa kitu cha hovyo tudumu katika wokovu na kuwa wavumilivu kwaajili ya Mungu wetu.


8.     Unawakilisha watu wenye msimamo usiotikisika.


Kutokana na ukuaji wa mierezi na urefu wake kwenda juu na nuimara wake umeufanya mti huu kuwa mti wenye msimamo ambao hautikisiki, au hauyumbishwi na upepo, hivyo kiroho unawakilisha watu wenye msimamo

Wote tunafahamu kuwa katika maisha haya kila mmoja anapitia au amewahi kupitia maswala kadhaa ambayo yamewahi kutikisha maisha yake tunatikiswa katika kila eneo la maisha yetu, misingi ya imani yetu, mashaka, kukata tamaa, kusalitiwa, na kuvunjika moyo, huku tukiwa katika mchakato wa kujijenga kiimani ili kwamba hata kutokee jambo la namna gani lisitufikishe katika hatua ya kuyumba 

Maandiko yanatufunza kupitia mwerezi kwamba tunapaswa kuwa imara na hatupaswi kuyumba lazima tuwe tayari kukabiliana na majaribu ya aina mbalimbali yanayotujia ni lazima tuwe na imani isiyotikisika

1.      Hakuna ajuaye namna tunavyoweza kuitikia Majaribu ya aina mbalimbali, tunaweza kukosa amani wakati wa majaribu lakini kila tunapopitia aina yoyote ya hatupaswi kukata tamaa ni lazima mitikisiko ya kila aina itukute kuwa tuko tayari na tuko zaidi ya kinachotarajiwa  

       Matendo 21:10-14 “Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi. Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa. Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu. Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu. Alipokataa shauri letu, tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke.” 

      Paulo mtume alikuwa ni kama mwerezi alikuwa amekwisha kujengeka katika mfumo wa uwezo wa kukabiliana na lolote lile kwa hiyo hata nabii agabo na wakristo wa nyakati za kanisa la kwaza walipofunuliwa ju ya kile knachomkabili yeye alikuwa tayari zaidi ya kile kinachomkabili.

Majaribu humtikisha kila mwanadamu na wakati mwingine yanaweza kututupa nje kama wanafunzi wa Yesu, Shetani ni mjaribu kama anavyotajwa katika maandiko Mathayo 4:3 “Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.”  Mjaribu ambaye pia alimjaribu Masihi, yeye ni adui yetu pia na atatujaribu atataka kujua mismamo wa imani yetu kwa Mungu, amekuwa akiwajaribu wanadamu wengi kwa miaka mingi hivyo anazo njia nyingi na uzoefu mkubwa wa ujuzi wa ni namna gani anaweza kutuingiza katika majaribu 2Wakoritho 2:11 “Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.”          

Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
0718990796.

Maoni 10 :

  1. barikiwa, nashauri iweke katika pdf format iwe rahisi wanaohitaji kutumia matini hii kama inaruhusiwa wafanye hivyo.

    JibuFuta
    Majibu
    1. Mashauri kuipata PDF yake itafaa sana

      Futa
  2. Ninaomba kama nitapata kibali nitumiwe hii makala katika mfumo wa pdf www.johridaharoon147@gmail.com

    JibuFuta
  3. Kiswahili ambacho nikisafi.

    Mwandishi amezingatia maadili ya lugha na pia ya neno la Mungu.

    Ningependa sana kujua Biblia unayo itumia kwani lugha yake ni safi sana.

    Asante

    JibuFuta
  4. Kazi hii ipo vizuri lakin weka mfumo wa PDF ili ipatikane kwa urahisi kingine endelea na kazi hiii ni nzuri

    JibuFuta
  5. Renatus Nyaluhela

    JibuFuta
  6. Bwana Yesu kristo asifiwe,nashukru kwa Historia hii ya mti Mtakatifu Mwerezi wa lebanoni.Mungu atasaidie tufanyike mierezi ya Tanzania.

    JibuFuta
  7. Ubarikiwe sana mwandishi na MUNGU akutunze sana kwa damu yake

    JibuFuta
  8. mwinjilist kisusi20 Agosti 2023, 07:36

    Naomba unitumie kwa e-mail jerekisusi384 @gmail.com au whatsap 0753458269 amina na barikiwa sana

    JibuFuta
  9. Kazi nzuri sana, nimejifunza mnoo, Mungu atusaidie tuwe kama mti mwerezi sehemu tulizopo

    JibuFuta