Jumanne, 24 Desemba 2019

Fimbo ya kukomesha Manung’uniko!.



Hesabu 17:1-11Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,Nena na wana wa Israeli, kisha upokee kwao fimbo, fimbo moja kwa ajili ya nyumba ya kila baba, katika wakuu wao wote, kama nyumba za baba zao zilivyo, fimbo kumi na mbili; kisha andika jina la kila mtu katika fimbo yake. Na katika fimbo ya Lawi utaliandika jina la Haruni; maana, itakuwa fimbo moja kwa kila kichwa cha nyumba za baba zao. Nawe utaziweka katika hema ya kukutania mbele ya huo ushahidi, hapo nikutanapo pamoja nanyi.  Kisha itakuwa, mtu huyo nitakayemchagua, fimbo yake itachipuka; nami nitayakomesha kwangu manung'uniko ya wana wa Israeli, wanung'unikiayo juu yenu. Basi Musa akawaambia wana wa Israeli, ndipo wakuu wao wote wakampa fimbo, fimbo moja kwa kila mkuu, kama nyumba za baba zao zilivyokuwa, fimbo kumi na mbili; na fimbo ya Haruni ilikuwa kati ya fimbo zao.  Kisha Musa akaziweka hizo fimbo mbele za Bwana katika hema ya kukutania.  Ilikuwa siku ya pili yake, Musa akaingia ndani ya hema ya ushahidi; na tazama, ile fimbo ya Haruni iliyokuwa kwa nyumba ya Lawi ilikuwa imechipuka, imetoa michipukizi, na kuchanua maua; na kuzaa malozi mabivu. Kisha Musa akazileta nje hizo fimbo zote kutoka hapo mbele za Bwana na kuziweka mbele ya wana wa Israeli wote; nao wakaangalia, na kila mtu akaitwaa fimbo yake. Kisha Bwana akamwambia Musa, Irudishe fimbo ya Haruni mbele ya ushahidi, ili itunzwe iwe ishara juu ya hawa wana wa maasi; ili uyakomeshe manung'uniko yao waliyoninung'unikia, ili wasife.  Basi Musa akafanya vivyo; kama Bwana alivyomwagiza, ndivyo alivyofanya.” 
          

Utangulizi:

Ni muhimu kila mmoja wetu kuwa na ufahamu wa kutosha kwamba linapokuja swala la Uongozi, tujue kuwa uongozi unatoka kwa Mungu, na kwa sababu hiyo hatuna budi kufahamu kuwa tunapaswa kuiheshimu mamlaka ambayo Mungu ameiruhusu itawale kwa wakati huo, Biblia inasema katika

Warumi 13:1-2Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu. Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.”

Kumbe basi ni wazi kuwa Mungu anahusika kwa kiwango chote katika kuruhusu aina flani ya mamlaka itawale, hii ni kila mahali na katika kanisa lake bado ni Mungu ndiye anayechagua yeye mwenyewe na kuwaweka watumishi wake ili waliongoze kanisa hakuna mtu anayejiita mwenyewe japo wako walimu wa uongo, manabii wa uongo, wachungaji wa uongo, wainjilisti wa uongo, manabii wa uongo na mitume wa uongo maandiko yanaonyesha kuwa wapo, lakini wale halisi tunaambiwa kuwa Mungu aawachagua yeye mwenyewe ona katika

Waefeso 4:11 Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;” Biblia ya kiingereza ya The Amplified Bible inasomeka katika maneno hayo hivi nanukuu “He Himself Appointed and gave men to us” yaani Yesu mwenyewe, Ndiye anayechagua nani aongoze watu wake bila kujali ni njia gani anaitumia! Swala la kuchagua viongozi hufanywa na Mungu kwa matakwa yake na sio yetu ni muhimu kukumbuka hili ona

Marko 3:13-14Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri,” unaona anaita anaowataka mwenyewe kwa makusudi, kusudi la kwanza wawe pamoja naye yaani wakae katika uwepo wake, wawe na uwepo wa Mungu na pili awatume wawe wajumbe wake wawe wawakilishi wake, watimize makusudi yake wahubiri injili. Jambo hili si kwa sababu ya juhudi za kibinadamu wala si kwa sifa za kibinadamu bali kama Mungu atakavyo  Mungu huchagua viongozi kwa rehema zake tu na sio uwezo wa kibinadamu ona

Warumi 9:15-16Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.

Kwa msingi huu basi ni muhimu kufahamu kuwa tunaponung’unika juu ya kiongozi fulani na au kusimama kinyume naye kumpinga au kumuasi na kuanza kumpiga vita ni wazi kabisa kuwa unapambana na Mungu, na hili ndio tatizo kubwa la wanadamu, Mungu anapochagua mtu wa kuongoza na kutimiza kusudi lake sio lazima mtu huyo awe anafiti katika akili zako, wakatimwingine unaweza kuona kwa nje kuwa ni mtu dhaifu sana na ni kama hatoshi, lakini ndani yake mapenzi ya Mungu yatatimizwa!.

Kunung’unikiwa kwa Mamlaka ya Musa na Haruni.

Katika Mstari wa msingi hapo juu tunagundua kuwa Mamlaka ya Musa na Haruni ilinung’unikiwa na baadhi ya watu, Kama wewe ni kiongozi kumbuka kuwa wewe sio wa kwanza kunumg’unikiwa wala kutukanwa au kuasiwa au kupingwa hadharani au kusengenywa au kusemwa vibaya, Musa na haruni walikuwa viongozi waaminifu, waliojitoa na kuwapenda watu wao, waliohatarisha maisha yao kwa kumkabili Farao wakiwa hawana Jeshi na kudai uhuru wa waisrael, wakiwa na lengo la dhati kutoka moyoni kuwapeleka katika nchi ya mkanaani nchi iliyojawa maziwa na asali lakini mamlaka yao ilinung’unikiwa, baadhi ya waisrael wa kabila ya lawi walianza maneno maneno kwamba Musa na haruni wanajipa madaraka makubwa mno wanajitukuza sana angalia katika

Hesabu 16:1-4Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni; nao, pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa; nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, Bwana naye yu kati yao; n'nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa Bwana? Musa aliposikia maneno haya, akapomoka kifudifudi;

Hesabu 16:8-11Musa akamwambia Kora, Sikizeni basi, enyi Wana wa Lawi; Je! Mwaona kuwa ni jambo dogo kwenu, kuwa Mungu wa Israeli amewatenga ninyi na mkutano wa Israeli, ili apate kuwakaribisha kwake; ili mfanye utumishi wa maskani ya Bwana, na kusimama mbele ya mkutano ili kuwatumikia; tena ya kuwa amekuleta uwe karibu, na ndugu zako wote wana wa Lawi pamoja nawe? Nanyi, je! Mwataka na ukuhani pia? Kwa sababu hii wewe na mkutano wako wote mmekusanyika kinyume cha Bwana; na Haruni, je! Yeye ni nani hata mkamnung'unikia?

Unaona vifungu hivyo? Watu wakuu wenye cheo, watu wazito wenye mamlaka kubwa maarufu na wanaojulikana wanalalamika wananung’unika kinyume na Musa na haruni na maarufu zaidi wanatajwa kuwa Korah, Dathan na Abiramu wanazungumza maneno ya kutisha mno wanasema hivi “Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, Bwana naye yu kati yao; n'nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa Bwana?” Ni maneno ya ajabu sana kutoka kwa watu ambao huwezi kufikiri kuwa wanaweza kusema maneno kama hayo, Musa na haruni waliposikia walijua madhara ya uasi walianguka kwa Mungu kifudifudi na kuanza kuwaombea wao walikuwa wanajua wazi kuwa mtu akinza kushinda na mamlaka zilizoko anapamba na Mungu, walipata madhara makubwa sana kwa sababu ya ujeuri wao na maneno yao mabaya waliyoyasema biblia inatuelezea kuwa walifutiliwa mbali kwa mtindo wa kipekee kwani walimezwa na ardhi ona

Hesabu 16:28-33Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba Bwana amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe.  Kama watu hawa wakifa kifo cha sikuzote, kama watu wote wafavyo, au kama wakipatilizwa kwa mapatilizo ya watu wote; hapo basi Bwana hakunituma mimi. Lakini Bwana akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao washukia shimoni wali hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau Bwana Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka;  nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote. Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wali hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni.”

Hawa walikufa namna hiyo kwa sababu walimuasi Mungu na waliwaasi viongozi, huwezi kuja kuwa kiongozi mzuri kama unamtukana kiongozi aliyepo, watu hawatakuja wakuheshimu kama unashindwa kuwaheshimu wengine au viongozi walioko, ndio maana Daudi aliendelea kuwa mpole kwa Sauli kwa sababu alikuwa ni mpakwa mafuta kwa wakati ule licha ya kuwa na madhaifu ya kibinadamu, kumbuka kuwa aushikaye upanga ataangamia kwa upanga, ni kanuni ileile mbovu unayoitumia kumsakama kiongozi aliyeko madarakani ndio hiyo hiyo itakuangamiza utakapokuja kutawala, kama una ndoto au Mungu amekuotesha kuwa utakuja kuwa kiongozi kumbuka hilo, viongozi waliokuwa na sifa kama Korah Dathan na Abiramu, walipomuasi Musa na Haruni walipoteza kabisa sifa zao na leo tunawasoma kama mfano wa watu wasiofaa, haiwezekani usema unamcha Mungu na wakati huo huo ukawa Humuogopi Mungu, je wadhani tutakuja kukulinda na kukupigia saluti zetu ilihali tunajua wazi kuwa hukuwaheshimu waliotangulia?  Mungu aliwafutilia mbali waasi, walikuwa wamejifunza kuwa “Usimtukane Mungu wala usimlaani mkuu wa watu wako” soma Kutoka 22:28 Lakini hawakujali walifutiliwa mbali

Hata hivyo kama haitoshi baada ya hawa kuuawa na Mungu mwenyewe siku ya pili tu badaya ya watu kumuogopa Mungu, vuiongozi wengine wakuu wa kabila za Israel, walinungu’unika tena angalia Hesabu 16:41Lakini siku ya pili yake mkutano wote wa wana wa Israeli wakamnung'unikia Musa, na Haruni, wakasema, Ninyi mmewaua watu wa Bwana.

Ukweli ninkuwa Mungu alikuwa amekusudia kuwafutilia mbali mkutano wote walioanzisha manung’uniko Lakini Musa na haruni tena wakijua madhara yatokana nayo na roho ya kuasi walipomoka kifudifudi na kuwaombea watu kwa Mungu kwamba hasira zake zisiwaangamize, Ndipo Mungu alipoamua kutuma pigo kali lililoua waisrael wapatao 14,700 unaweza kuona katika

Hesabu 16:45-50Ondokeni kati ya mkutano, ili niwaangamize mara moja. Wao wakapomoka kifudifudi. Musa akamwambia Haruni, Haya, shika chetezo chako, ukatie moto ndani yake, moto wa madhabahuni, kisha utie na uvumba juu ya moto, ukakichukue haraka, wende nacho katika huo mkutano, ukawafanyie upatanisho; kwa kuwa ghadhabu zimetoka kwa Bwana; hiyo tauni imeanza. Basi Haruni akakishika chetezo kama Musa alivyonena, akapiga mbio akaenda katikati ya mkutano; na tazama, tauni ilikuwa imeanza kati ya watu; akatia uvumba juu ya moto na kufanya upatanisho kwa ajili ya hao watu. Akasimama kati ya hao waliokufa na hao waliokuwa wakali hai; tauni ikazuiwa. Basi waliokufa kwa tauni walikuwa kumi na nne elfu na mia saba, zaidi ya hao waliokufa katika jambo la Kora. Haruni akamrudia Musa pale mlangoni pa hema ya kukutania; hiyo tauni ikazuiwa.”

Unaona hapa maandiko yanaeleza kuwa walioangamizwa kwa uasi hapa walikuwa wengi kuliko wale wa kwanza, Tabia ya wanadamu kunung’ung’unikia viongozi haikuanza leo, hata nyakati za biblia tunaona wanungunikaji wakiongezeaka kila wakati na Mungu aliona njia ya kuwaangamiza itasababisha wafutike wengi hivyo Mungu alianzisha mpango mahususi wa kukomesha manung’uniko hayo milele.

Umuhimu wa fimbo ya Haruni!

Fimbo ya Haruni inawakilisha jambo muhimu sana katika mpango wa Mungu, hususani katika swala zima la kuwaongoza wana wa Israel kutoka utumwani Misri kuelekea Kanaani katika nchi ya ahadi, Kwa mujibu watamaduni za Israel na kwa mujibu wa kanuni za kinabii, fimbo huwakilisha Mamlaka na utawala, Wachungaji walitumia fimbo kuongoza na kurekebisha maisha ya Kondoo Zaburi 23:4 “Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.Mungu alipomuita Musa alikuwa Mchungaji wa kundi la mkwewe na alitaka akawaongoze Waisrael kutoka Misri, aliitumia fimbo ya Musa kuonyesha uwezo wake na nguvu zake kwa kufanya miujiza akiitumia fimbo ya Musa ona katika


Kutoka 4:1-5 “Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea. BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo. Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake.BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;) ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba BWANA, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea."

Hesabu 20:11 “Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia.  

    
Mungu aidha alimchagua kaka wa Musa Haruni ambaye naye alitumiwa kufanya miujiza kwa fimbo yake ona
Kutoka 7:19 “BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Shika fimbo yako, kaunyoshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya mito yao, juu ya vijito vyao, na juu ya maziwa ya maji yao, na juu ya visima vyao vyote vya maji, ili yageuke kuwa damu, nako kutakuwa na damu katika nchi yote ya Misri, katika vyombo vya mti, na katika vyombo vya jiwe

Kutoka 8:5 BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha mkono wako na fimbo yako juu ya mito, juu ya vijito, na juu ya maziwa ya maji, ukawalete vyura waje juu ya nchi yote ya Misri.

Kutoka 8:16BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri.

Ni fimbo ya haruni ambayo iligeuka nyoka mbele za Farao, na hata wachawi wa farao walipogeuza fimbo zao kuwa nyoka ni fimbo ya Haruni iliyogeuka kuwa nyoka iliyomeza fimbo za wachawi wote

Kutoka 7:8-10
BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaambia, Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka. Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka.” Fimbo ya Haruni iliyogeuza maji yote ya Misri na mto nile kuwa damu

Kutoka 7:19-21BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Shika fimbo yako, kaunyoshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya mito yao, juu ya vijito vyao, na juu ya maziwa ya maji yao, na juu ya visima vyao vyote vya maji, ili yageuke kuwa damu, nako kutakuwa na damu katika nchi yote ya Misri, katika vyombo vya mti, na katika vyombo vya jiwe. Musa na Haruni wakafanya hivyo, kama BWANA alivyowaambia; naye akaiinua ile fimbo, na kuyapiga maji yaliyokuwa mtoni, mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake; na hayo maji yote yaliyokuwa katika mto yakageuzwa kuwa damu. Hao samaki waliokuwa mtoni nao wakafa; na ule mto ukatoa uvundo, Wamisri wasipate kunywa maji ya mtoni; na ile damu ilikuwa katika nchi yote na Misri.”                  

Na miujizi mingine Mingi ilifanyika kupitia Fimbo hii ya haruni, Baada ya Musa na Haruni kuwaongoza wana wa Israel nje ya utumwa Jangwani Mungu alimchagua Haruni nwanae kuwa makuhani

Kutoka 28:1Nawe umlete Haruni ndugu yako karibu nami, na wanawe pamoja naye, miongoni mwa wana wa Israeli, ili anitumikie katika kazi ya ukuhani. Haruni, na Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari, wana wa Haruni.” na Hesabu 18:1Bwana akamwambia Haruni, Wewe na wanao na nyumba ya baba zako pamoja nawe mtachukua uovu wa patakatifu; wewe na wanao pamoja nawe mtauchukua ukuhani wenu.”  na Walawi wote waliosalia walikuwa wahudumu katika nyumba ya Mungu kwaajili ya kusimamia utoaji wa sadaka za kuteketeza na usimamizi wa ibada kwa taifa zima.  Hivyo ni wazi kuwa Mungu alimtumia Haruni na Musa na ni wazi kuwa walitumika kwa kiwango kikubwa katika ukombozi wa wana wa Israel wakitumiwa na Mungu na ni wazi kuwa Mungu alikuwa amemchagua aweze kuwa kuhani mkuu, Hata hivyo watu hawakuacha kumnung’unikia.

Fimbo ya kukomesha manung’uniko

Kwa vile mara kwa mara watu walikuwa wakinung’unikia na kusahau wapi walikotoka na walikotolewa Mungu alinza kuingilia kati ili aweze kukomesha manug’ung’uniko Mungu alimuamuru Musa kuwaita viongozi wote wa Kabila za Israel na kuwataka wote walete fimbo zao na kuwa fimbo zao ziandikwe majina na fimbo ya Haruni iandikwe jina lake ikiwakilisha kabila la walawi, na Mungu alimwambia Musa kuwa aziweke hizo fimbo katika hema ya kukutania na kuwa fimbo itakayochipuka itaashiria kuwa mtu huyo ndie ambaye Mungu amemchagua  na jambo hili litakuwa mwisho wa Manunguniko

Hesabu 17:5
Kisha itakuwa, mtu huyo nitakayemchagua, fimbo yake itachipuka; nami nitayakomesha kwangu manung'uniko ya wana wa Israeli, wanung'unikiayo juu yenu.”

Waliacha fimbo zao mbele za Bwana na asubuhi kumbe Fimbo ya haruni iliyokuwa ikiwakilisha kabila la walawi ilikuwa imechipuka imetoamajani, na imeota maua na ilizaa tunda liitwalo lozi (almond) Ilidhihirisha wazi kuwa Mwenye nguvu, mwenye kuteua viongozi, mwenye kuweza kufanya kilichokufa kuwa hai, mwenye uwezxo wote  na mwenye kutia uzima alikuwa amemchagua Haruni, adiha Fimbo hiyo Musa aliiagiza iwekwe katika Sanduku la agano ili uwe ukumbusho wa milelena hii ingekomesha manunguniko ambayo yangeweza kusababisha vifo kila wakati

Waebrania 9:4yenye chetezo cha dhahabu, na sanduku la agano lililofunikwa kwa dhahabu pande zote, mlimokuwa na kopo la dhahabu lenye ile mana, na ile fimbo ya Haruni iliyochipuka, na vile vibao vya agano;”

Fimbo ya haruni iliyochipuka ilibaki kuwa ushahidi dhidi ya uchaguzi wa Mungu wa maongozi, Kuchipuka kwa fimbo hii pia kulikuwa na maana kuwa Mungu hatakuwa na Muda  wa kushughulika na waasi tena na mtumishi wake atakuwepo pale uwepo wa Mungu ulipo, Mungu hatawavumilia watu wanaoutesa mwili wa Kristo na kuugawanya, Mungu hatawavumilia watu wanaowashambulia viongozi aliowaweka mwenyewe madarakani, Mungu atasimama upande wa viongozi wake siku zote za maisha yake, atahakikisha kuwa wanastawi hata wakipigwa vita, wanazaa matunda, na kutoa maua yaani wataendelea kuwa watu wa kukumbukwa kutokana na yale watakayoyafanya kwa uweza wa Mungu milele na milele, unaweza kujutahidi kuwachafua watu wa Mungu na kuwashutumu na kuwasengenya, na kuwanena vibaya lakini Mungu si mjinga atasimama na watu wake atawastawisha kumbukumbu zao zitawekwa na hawataondoka kamwe katika moyo wa wala wanaowaongoza na moyo wa Mungu, Uongozi unaotoka kwa Mungu kamwe hauwezi kundolewa kwa fitina za wanadamu, Mungu anataka chaguo lake liheshimike na katika kanisa lazima ieleweke wazi kuwa wote wenye kuleta mafarakano na kutaka kutugawa wanapaswa kukemewa vikali

Yakobo 5:9Ndugu, msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango.”

Mungu yuko tayari kuhukumu na kuwashughulikia watu wenye kunung’unika, Mungu anataka tushirikiaqna na kuchukuliana na kuhakikisha kuwa tunaleta maendeleo kwa pamoja hatupaswi kulalamika na kufikiri kuwa labda wewe unafaa zaidi kuliko mwingine sisi sote ni viongozi lakini kamwe hatuwezi kuongoza kwa wakati mmoja Mungu katika mpango wake anataka mmoja aongoze hivyo mmoja wetu anaposimikwa kuongoza sisi wengine tukae kimya na kumsaidia kufanikisha mambo kwa faida ya wote badala ya kutafuta kuwafutilia mbali huku tukisahau mchango wao katika jamii,  Mungu anapolkuwa amekuweka mahali, au amekupa cheo fulani kumbuka kuwa sio watu wote watafurahia lakini kumbuka Mungu amekuweka katika sabduku lake la agano ili akukumbuke daima amekuweka katika uwepo wake ni malaka yako ndiyo itakayostawi, ni wewe ndiwe utakaewaokoa watu wako, ni wewe ndiye ambaye Mungu ataitumia fimbo yako kukutana na kiu ya watu wako, kuwakimbiza adui zaokuwaweka huru watu wako, kuondoa ujinga wao, kuondoa umasikini wao, kuwapa raha ya kanaani wanayoitizamia kuwapatanisha na Mungu hivyo hupaswi kuogopa kelele za watu kustawi kwako na kuzaa kwako matunda kutanyamazisha kelele za adui zako, kuwa chaguo la Mungu hakumaanishi kuwa tutakosa wapinzani kumbuka hata shetani ni mpinzani wa Mungu, hatupaswi kuogopa kamwe, haruni na Musa waliosnga mbele walikuwa na ujasiri waliwaonea huruma hata wapinzani wao kwa sababu walijua kuwa wanaowapinga wanapingana na Mungu mwenyewe, Ndugu yangu kama wachawi wanakupinga, maadui wanakupinga watru wanakuasi watu wanakuteta wanakusengenya wewe endela kutekeleza agizo la mungu endelea kupiga kazi, kazi zako zitatangaza kuwa wewe ni mtu wa namna gani, Yesu pia watu hawakumuamini lakini alitoa wito kwa wapinzani wake na adui zake waangalie yale aliyoyafanya kuwa yanatokana na uweza wa uungu ndani yake Musa na Haruni unaweza kuwapima katika mzani wako na ukawaona hawafai Lakini kazi walizozifanya kupitia Mamlaka waliyopewa na Mungu zinatangaza wazi kuwa wao ninani, na hayo ndio matundana ustawi wa watumishi wa Mungu unawapiga vita waoa wanaizdi kustawi na kuchanja mbuga piga kazi zaidi kadiri adui zako wanavyojipanga kwa majungu wewe endelea mbele na fimbo yako itakomesha manung’uniko

 Yohana 10:37-38 Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba.

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

0718990796

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni