2Timotheo 1:3-6 “Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani
za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku
na mchana. Nami natamani sana kukuona,
nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha; nikiikumbuka imani uliyo nayo
isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama
yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo. Kwa sababu hiyo nakukumbusha,
uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa kila
mwanadamu amezaliwa kwa kukiwa na kusudi fulani au wajibu fulani wa kuutimiza
ulioko ndani yake, na katika wajibu huo ili aweze kuutimiza ipaswavyo, Mungu
huweka karama au kipawa kwaajili ya kumuwezesha mtu huyo kutimiza kusudi la
Mungu lililowekwa ndani yake
Hata hivyo karama au kipawa
kinapokuwa ndani ya mtu kuna maswala kadhaa yanayopaswa kufanyika ili kiweze
kukua au kukomaa au kujitokeza katika ubora wake swala hilo sio lingine ni
kuchochea kipawa hicho kilichomo ndani ya mtu aliyekusudiwa na Mungu kutumiwa
katika shughuli husika. Tutajifunza somo hili muhimu kwa kuzingatia vipengele
vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya kuchochea Karama
·
Jinsi karama zinavyochochewa!
·
Namna karama zinavyochochewa!
Maana
ya kuchochea Karama
Paulo mtume anamwandikia Muhubiri
na kiongozi kijana na mchanga katika Imani na maongozi ili kumtia moyo wakati
yeye akiwa anaelekea ukingoni wakati huu Paulo mtume alikuwa gerezani kwa
sababu ya injili, akisubiri kuuawa kwake muda si mrefu kwa hiyo anaandikwa
waraka huu akiwa na hisia kali sana akijua ya kuwa anatengwa na wapendwa wake
lakini vilevile akijua kuwa Timothy atakabiliwa namaswala mengi
ya kuhubiri injili, uongozi, nausimamizi wa kanisa na shughuli nyingunezo
katika jamii, na sasa anataka kumtia moyo ili asimame kiume awe imara
ahakikisha anafanya kazi kwa bidii na uaminifu na ndipoi anaposema manenoi haya
“Kwa sababu hiyo
nakukumbusha uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani kwa kuwekewa mikono yangu”Neno
hili katika biblia ya kiingereza NKJV (New King James Version) linasomeka hivi “Therefore I remind
you to stir up the gift of God which is in you trough the laying of my hands”
Biblia nyingine zimetumia neno “Keep a blaze the gift” na neno “rekindle the gift” Maneno ya kiyunani
yanayotumika katika lugha hii ni “xesikono”
yaani kuchochea mfano wa kusogeza vijinga vya moto ili moto wa kutumia kuni
uweze kuendelea kuwaka, kwa kawaida moto wa kuni kama umewashwa na ukaachwa
bila kuchochewa unaanza kuzimika na ili uendelee kuwaka vema unahitaji
kuchochewa, Moto unapochochewa huwa na tabia ya kuendelea kuwaka na kubaki
katika hali ileile na nguvu ileile au kuwaka zaidi. Paulo anamtaka Timotheo aendelee kuwaka na
kubaki katika hali ile ile na nguvu ileile au kuwaka zaidi, akiwa na imani
ileile kama iliyokuwa kwa bibi yake loisi na mama yake Eunike nay eye mwenyewe
aliwa kamawao na kuzidi. Kwa hiyo wale wanaotumia tafasiri ya kuchochea kwa
maana ya kukoroga mfano wa sukari kwenye chai maana hjii ni ya kipuuzi kwa
mujibu wa asili ya maandiko haya hayazungumzii kukoroga yanazungumzia kuongeza
moto kuchochea kuhakikisha moto unabaki pale plale au unaendelea.
Hii ina maana gani? Matokeo
makubwa katika jambo lolote tunalolifanya yatawezekana kama moto wetu
hautazimika, Chakula kitaiva vizuri na Matunda yataonekana kama hakuna mtu
anazimia moyo, Mungu amempa kila moja wetu karama na vipawa kwaajili ya
shughuli mbali mbali, ili kufanikisha huduma na utumishi aliouweka ndani yetu
na ndani ya kila mmoja wetu, Kama wewe ni mwana michezo mfano Bondia na
umefanikiwa kuchukua mikanda mbalimbali ya kimataifa haupaswi kuishia hapo,
Kama ni shule ya msingi au sekondari na imefanikiwa kiwilaya au kimkoa au
kitafifa kushika nafasi nzuri ya juu kwa kufaulisha zaidi katika mitihani ya
kitaifa haipaswi kuridhika na kubweteka na kukaa hapohapo tu, Kama ni kanisa
limefanikiwa kuwahubiri injili watu maelefu kwa maelfu na kuwaleta kwaq Yesu
hawapaswi kuridhika na kuishia hapohapo, kama Mungu amekupa nafasi ya kuwa
Kiongozi mkubwa wanchi yaani Rais, au makamu wa Rais au waziri waziri mkuu, au jaji mkuu au mkuu wa jeshi la pilisi, au
Magereza, au uhamiaji, au zimamoto au kujenga taifa au mkuu wa majezi ya ulinzi
na usalama, spika wa bunge au mkuu wa
mkoa au mbunge au mkuu wa wilaya na kadhalika na viongozi wengine wote na
katika kanisa vilevile Hatupaswi kuishia hapo lazima tuichochee moto wa
maendeleo na kuhakikisha kuwa kila tulifanyalo haliwi nguvu ya soda lazima
tuchochee moto wa maendeleo na kuhakikisha kuwa tunasonga mbele na kupiga hatua
kubwa sana hiki ndicho Mungu anachokitaka, Mungu anataka moto uwe mkali zaidi, Nimeona pia
katika nchji yetu Makocha wengi wa mpira wa miguu wanatoka katika nji nyingine
kana kwamba hatuna makocha hodari hapa nyumbani Makocha wa nyumbani wanapaswa
kuchochea uwezo wao na kujiapiza kuifunga kila timu yenye kocha mgeni mpaka
wakubali kuwa nyumbani tunaweza hiki ndio kitu Mungu anataka, mpaka ulimwengu
ugundue kuwa wako watu wanaweza, ikiwa wewe ni muhubiri hubiri injili kwa
viwango na ufanisi mkubwa, ikiwa wewe ni mwanamuziki wa injili imba kwa
mafundisho yaliyo sahihi huku wewe mwenyewe ukiwa ni kielelezo cha kila unachokihubiri,
mwimbaji wa nyimbo za kawaida wekeza hisia zako zote kwa bidii, mchezaji wa
mpira, bondia, mwanariadha, mwalimu, mwanafunzi, nakila mtu hata katika ndoa
zetu hatuna budi kuhakikisha kuwa tunachochea upendo, uzalendo na mshikamano na
kuhakikisha kuwa unawake na kuwa moto mkali sana na tutaona maendeleo makubwa
katika taifa letu, Kila mmoja akichochea kipawa na karama aliyopewa na Mungu
matunda yetu hayawezi kuzimika na kila sekta katika taifa letu itaonekana
ikistawi kwa namna ya kipekee na ya tofauti, Na ndio maana Paulo mtume alikuwa
anamtaka Timotheo aichochee karama ya Mungu iliyomo ndani yake, Leo mimi
nawataka wananchi wote kwa pamoja tuchochee kila karama na kipawa kilichomo
ndani yetu kila ambacho Mungu ametupa na kuwa tusizimie moyo wala tusiogope.
Paulo mtume alikuwa akimuomba
Mungu na kutamani kuona Maisha ya Timotheo yanakwenda juu zaidi ya pale
alipokuweko na kuwa imani yake inapaa na kuongezeka, Paulo alikuwa anajua kuwa
Timotheo ana vipawa vingi na anajua kuwa zikichochewa atafanya na kuwa bora
zaidi, Kila mtu na kila mmoja wetu ana kipawa fulani ndani yake na karama
ambazo mungu ameweka ndani yetu kwa makusudi mbalimbali lakini hatuwezi kujigundua
mpaka mtu mwingine aone, atuchochee na kututia moyo, Kila mwanadamu anahitaji
kutiwa moyo, Hakuna mwanadamu anayefurahia kutukanwa kila siku na kukashifiwa
na kuambiwa kuwa hana lolote, Ni lazima tuwe na tabia chanya yenye kuwajenga na
kuwatia moyo wengine badala ya kuwa watu wenye kuonyesha kuwa wengine hawawezi
ilihali kumbe ni sisi ndio hatuwezi, swala la kutia moyo mtu na kumuona mtu
akifanya vema halihitaji kusomea saikolojia ni falsafa ya asili tu “Natural Philosophy” Mara kadhaa mtoto
anapoanza kusimama katika mila na desturi zetu huwa tunawaimbia kamimama peke
yake kwamakusudi la kuwatia moyo wasimame, kweli kweli na hatimaye husimama, Wanamichezo wa soka na
wa aina mbalimbali wanawahitaji sana washabiki wao kufika kwa wingi uwanjani
ili kuwatia moyo na kuwashangilia jambo hili huwapa moyo na kuwafanya wafanye
bidii na kufanikiwa, Mungu anapokuwa ameweka vipawa ndani yetu na karama za
aina mbalimbali zinahitaji watu wenye ujuzi wa kututia moyo na kuhakikisha kuwa
kwa namna chanya wanatujenga na kututia moyo ili kipawa na karama zisipotee na
kufifia.
Jinsi Karama zinavyochochewa!
Ndani ya Timotheo kulikuwa na
Huduma au karama ya Uongozi, yeye aliitwa na Mungu na kufanya kazi na Paulo
mtume akisimamia makanisa alikuwa anapaswa kuyaongoza makanisa alikuwa nafanya
kazi za kichungaji, alikuwa ni mwangalizi wa makanisa ya Mungu ni askofu
kijana, alikuwa Muhubiri wa injili lakini kama binadamu alikuwa muoga kidogo,
na alikuwa mwenye haiba ya aibu hivi na Paulo alifahamu jambo hili na hivyo alitaka kumtia moyo asiogope kwani
Mungu hakutupa roho ya woga ona 2Timotheo1:7
“Maana Mungu
hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.” Hii
maana yake ni kuwa Mungu anaweza kutupa vipawa vikubwa sana ndani yetu lakini
kuna madhaifu ya kibinadamu inaweza kuwa woga, inaweza kuwa tunaona aibu au
tunakosa nidhamu na kadhalika au tunaweza kuwa waoga na kwa kujua hili ndipo
Mungu huwapa watu wake Roho Mtakatifu ili kuwawezesha kuwa wajasiri na
kukabiliana na kila aina ya upinzani na kuweza kujihami dhidi ya upinzani
wowote tutakaokutana nao Luka 12:11-12 “Na watakapowapeleka ninyi mbele ya masinagogi na maliwali na
wenye mamlaka, msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema;
kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema”. Matendo
1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho
Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi
wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” na Warumi 8;26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana
hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua
kusikoweza kutamkwa.” Mungu yupo kututia nguvu na kutuwezesha na
kutupa nidhamu na kiasi kuweza kushinda changamoto mbalimbali tunazokabiliana
nazo katika maisha, Roho Mtakatifu hutuombea na kutusaidia kwa sababu anajua
udhaifu wetu na hivyo hatupaswi kuogopa, kwa hiyo kuchochea kwetu hapa ni
pamoja na kumtanguliza Mungu mbele katika kila tunalolifanya na Roho Mtakatifu
atakuwepo kutusaidia kwa dhamiri njema!
Namna karama zinavyochochewa
Kwa kuwa Karama na vipawa hutoka
kwa Mungu, ni lazima Mungu atangulizwe mbele, katika karama za maongozi ya
kanisa na vipawa vya roho mtakatifu kamwe hatuwezi kutumia akili zetu wenyewe
wala hatupaswi kutumia ngubvu zetu Roho Mtakatifu hufanya kazi na sisi kama
tutakubalia atutumia kwa hiyo lazima kwetu kuwekewa Mikono na watumishi wa
Mungu ili watuombee neema ya Mungu katikalile tunalokwenda kulifanya
1. 2Timotheo 1;6 “Kwa
sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa
kuwekewa mikono yangu.”
Viongozi wa kanisa wanapotuombea neema na kuweka
mikono yao juu yetu kazi zile zilizowekwa mbele yetu zinapata kibali cha kiungu
na karama zilizokuwa zimejificha huibuka, hekima na maarifa hutukalia na ndio
maana mtu akiwekewa mikono na kubarikiwa mwenendo wa maisha yake huwa tofauti Matendo ya mitume 13: 1-3 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na
manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio
Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli.
Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu
akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha
kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.” Mtu
wa Mungu anapowekewa mikono na kuombewa neema kwaajili ya majukumu aliyopewa
roho ya maarifa na hekima ya kutekeleza wajibu wake kwa uzuri hukaa juu yake Kumbukumbu la torati 34:9 “Na Yoshua, mwana wa Nuni, alikuwa amejaa roho ya hekima;
maana Musa alikuwa amemwekea mikono yake juu yake; wana wa Israeli
wakamsikiliza, wakafanya kama Bwana alivyomwamuru Musa.” Yoshua
aliweza kuwa kiongozi shujaa na mwenye imani na akasikilizwa na wana wa Israel
kwa kuwa aliwekewa mikono na Musa hivyo kwa kuwekewa mikono na kuombewa neema
kamama zilizoko ndani yako zinaweza kuchochewa kwa msaada wa Roho Mtakatifu.
2.
Kubali
kufundishwa
1Timotheo 4:13 “Hata
nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha.” Paulo
Mtume pia alimwambia Timotheo afanye bidii sana katika kusoma, Tayari Timotheo
alikuwa ni Muhubiri wa Injili na alikuwa ni mwangalizi wa makanisa lakini
anatakiwa afanye bidii sana katika kusoma, uko ujuzi mwingi umejificha katika
vitabu, lakini kutokana na watu wengi kuwa na uvivu wa kusoma na kuelimika
wamezima moto au wameshindwa kuuchochea moto na kuchochea vipawa vyao, kila
kitu duniani kinahitaji kujiongeza, wako watu wengi sana hawafurahii ndoa zao
kwa sababu wanandoa wameridhika na hali ile ile na ujuzi uleule na hawataki
kujaribu kujifunza na kutafuta mambo mengine kutoka vitabuni, wako wafanya
biashara ambao biashara zao zimedumaa kwa sababu wana mbinu zilezile na mitindo
ileile, wafanyakazi katika taasisi, walimu na kadhalika wanapaswa kujiongeza,
serikali mara kadhaa katika sekta ya elimu wamebadili silabasi, mifumo ya
mitihani, mbinu za ufundishaji bila kutoa semina ya kutosha na kueleweka kwa kwa walimu, ili
waendane na mfumo mpya na kuwapeleka katika ngazi ya juu, wapo wachungaji
wamesoma zamani na mambo yamebadilika wanapaswa kupata semina elekezi katika
Nyanja zao ili kujiongeza na kuchochea uelewa walio nao mpaka kuwapeleka ngazi
nyingine kila ki[pawa karama na nafasi Mungu anayotupa inahitaji maarifa ya
kutosha na bidii katika kujifunza ili
ifanyike kwa usahihi zaidi
Kuna baadhi ya
karama na vipawa ambavyo Mungu ameweka ndani yetu ambavyo ili vifanye kazi na
kunolewa na kutumika katika viwango vya juu lazima kusoma na kujisomea na
kujiongeza kuhusike au mazoezi makali na miiko yake au nidhamu zake zihusike,
siku hizi kumeibuka wimbi kubwa sala la watu wanaomtumikia Mungu huku wakiwa
hawana mafunzo ya utumishi huo, huu ni msiba mkubwa sana nakubali kuwa utumishi
ni huduma na ni karama na ni kipawa lakini kinaweza kufanya kazi vizuri kwa
kupitia mafunzo aidha mafunzo rasmi au mafunzo yasiyo rasmi lakini ni muhimu
kupitia mafunzo hayo kwa muda wa kutosha ili utumishi wetu uwe na ufanisi na
hii ndio njia mojawapo ya kuichochea Karama, Mungu humtumia mtu vuziri zaidi
baada ya kumuandaa kwa muda wa kutosha na mrefu zaidi Matendo ya Mitume 7:22 “Musa akafundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa hodari wa
maneno na matendo” Mungu alimtumia sana nabii Musa lakini Musa
alikuwa msomi alifundishwa hekima yote ya wamisri na akawa Hodari wa maneno na
matendo, ni kwa kusoma tunaweza kuchochea Karama zilizoko ndeani yetu na tukawa
watu Hodari, lazima ufikie wakati tukubali kujifunza tuwasikilize walimu na
kuwatii, tuwasikilize wazazi na kuwatii, tuwasikilize makocha na kuwatii,
tujifunze kwa waliostaafu, tujifunze kwa waliotutangulia, tujifunze hata kwa
walioshindwa kwa kuwauliza walishindwaje ili sisi tusipite katika njia ileile.
Matendo 18:24-26 “Basi
Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika
Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia
ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha
kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena
kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua
kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.”
Maandiko yanaonyesha jinsi
Apollo alivyokuwa mtu mwenye Elimu na alikuwa hodari katika maandiko na alikuwa
Muhubiri hata hivyo alihitaji kujua maswala kadhaa kwa usahihi zaidi na mwalimu
wa neno la Mungu Prisilla na Akila ambao walikuwa ni watumishi wa Mungu Pamoja
na Paulo mtume wao walimfundisha njia ya bwana kwa usahihi zaidi ili kuichochea
huduma yake, Tunapokubali kujifunza tunajiweka katika kutumiwa na Mungu katika
viwango bora zaidi na kusaidia kupunguza makosa ya kibinadamu, hivyo unapobaini
kuwa una kipawa fulani tafuta watu sahihi watakaosaidia kukinoa ili kukiweka
kitaalamu zaidi, ili utumiwe vema na kwa ubora zaidi.
3.
Hakikisha
unaonana na watu sahihi.
Mungu anapokuwa
ameweka Karama au kipawa au aina fulani ya maono, mwanzoni ni rahisi sana watu
kukataa kutambua kipawa au karama uliyo nayo na unaweza kujikuta uko katika
mazingira ya watu ambao wanaweza kuua kile ulicho nacho kwa nia njema au mbaya
lakini pia kwa kutokujua kuwa umebeba nini, Nilipotembelea taifa la Korea ya
kusini mwaka 2016 niliwahi kukutana na wat kadhaa wanaotumia mkono wa kushoto
kwa ubora sana kama mimi na watanzania wenzangu tunaotumia mkono wa kulia,
Mkorea mmoja akaniambia kuwa watu wanaotumia mkono wa kushoto ni wenye akili
sana na hapa Korea wako wengi mno, kwa haraka nilisikia uchungu moyoni kabla ya
kujibu lolote niliwaza kuwa ina maana sisi tunaotumia mkono wa kulia hatuna
akili? Lakini haraka sana jibu llikuja na nikamwamboa mkorea yule kuwa kama ni
hiyo Afrika watu wengi wana akili sana kwa sababu kila mtoto anayezaliwa na
niliowaona mimi wanatumia mkono wa kushoto lakini wazazi wetu hutuchapa na
kutukemea kisha hutufundisha kutumia mkono wa kulia kwa sababu kwetu Afrika
kutumia mkono wa kushoto kwa mila na desturi zetu sio jambo la busara na halna
heshima, na mkorea yule aliacha majivuno yake,
kwa nini nimetumia mfano huu hapa unaweza kuwa na kipawa cha aina fulani
na unaweza kuwa umezaliwa nacho unaweza kuwa unapenda kuchora na wazazi
wanaweza kudhani unajisomea kumbe unachora na wakakukataza kuchora ili kwamba
usome lakini kumbe wanaua kitu cha thamani ulichojaliwa na Mungu, Unaweza kuwa
unapenda sana kucheza mpira lakini wazazi wakakukataza ili kwamba usije ukaumia
au uweze kuweka mkazo katika kusoma lakini kumbe wakawa wanafifisha kipawa
kilichoko ndani yako! Mtu mwenye karama
au kipawa ili aweze kukichochea hana budi kuhakikisha kuwa anaelekea mahali
sahihi ili kupata mafunzo na kutiwa moyo zaidi kuhusu kipawa chake ona katika
Luka 1:39-40 “Basi,
Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji
mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti.”
Unaweza
kujiuliza kuwa ni kwa nini Mariamu alipotaarifiwa na Malaika Gabriel kuwa atakuwa na Mimba na
atamzaa Masihi ambaye ni mrithi wa kiti cha enzi cha Daudi milele? Na tunaona
Mariamu anafanya haraka kwenda kumtembelea Elizabeth na kukaa kwake miezxi
mitatu wakati malaika anamwambia jambo hili Mariamu pia alimueleza jambo
jingine kwa kusudi la kumtia moyo Mariamu maana alijiuliza inawezekanaje jambo
hili kutokea naye hajui mume? Malaika alitaka kumuonyesha Mariamu kuwa Mungu
hashindwi jambo na hata Elizabeth aliyeitwa tasa sasa ana ujauzito wa miezi
sita ona:-
Luka 1:34-37 “Mariamu
akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu
akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu
zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa
kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua
mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye
aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.”
Unaona Jambo
hili lilimfanya Mariamu kwenda haraka sana kwa Elizabeth kwa sababu alikuwa
amechanganyikiwa kwa maono makubwa ambayo malaika alisema naye ni kama malaika
alikuwa amemuonyesha wazi kuwa mtu sahihi anayeweza kukusaidia kwa wakati huu
ni Elizabeth ambaye naye Mungu amemfanyia mambo makubwa na magumu
yaliyoshindikana kibinadamu Mariamu hangeweza kumwambia mama yake. Wala mwalimu
wake au mtu yeyote aliyemjua alijua kuwa mtu aqnayeweza kumuelewa ni Elizabeth
tu mtu mwenye maono na ndoto na muujiza na kipawa na karama kama zake
Luka 1:36-37”
Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume
katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa
hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.” Mariamu alikuwa ametiwa moyo
kupitia maneno haya alihitaji kujifunza kwa mtu sahihi aliyemtangulia alihitaji
muongozo, alihitaji kupokea uzoefu, Elizabeth ndiye aliyekuwa mtu sahihi wakati
huu wa kumtia moyo Mariamu, kumfundisha, kumuelekeza, kumuonyesha upendo na
urafiki, kumpandisha imani na kumtetea ona maneno ya Elizabeth
Luka 1:41-45 “Ikawa
Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani
ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu
akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa.
Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia
masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu.
Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.”
Unadhani Mariamu angeenda kwa mtu asiye
sahihi ingekuwaje angeambiwa Mungu wangu ni nani atakayekuelewa umekwisha
unaanzaje kumwambia mtu una mimba unawezaje kutimiza ndoto hii unawezaje
kuifanya biashara hii, unawezaje kuandkia andiko maoni haya ndugu yangu hii ni
kazi ngumu sana haiwezekani, vifaa vimepanda sana haiwezekani, ujenzi ni
gharama mno hutaweza unapokuwa na karama au ndoto au maono enenda kwa mtu sahihi Elizabeth anamwambia Mariamu
tena akiwa amejaa Roho Mtakatifu “Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na
Bwana.” Elizabeth anamwambia
mariamu ulichoambiwa na Mungu kitatimia tu na ni baraka kubwa kama utaamini,
mwamini Mungu yeye anaweza ndipo Mariamu akamuadhimisha Mungu na kutulia kwa
Elizabeth kwa miezi mitatu, Unapokuwa na njozi au hata mapito na majaribu
enenda kwa watu wanaopitia majaribu kama yako mtazungumza lugha moja, unapokuwa
na karama waone waliokutangulia walio
sahihi wenye kipawa kama chako jifunze kutoka kwao ambao lugha zao zitakuwa
chanya watakuambia UTATOBOA TU, Mwanangu utatoka hii kitu nakuhakikishia
utatoka kirahisi tu, hivyo ndivyo unavyoweza kuichochea karama iliyo ndani
yako.
4.
Kuwa
mkomavu.
Acha ulimbukeni,
watu wengi sana wameua vipawa vyao kwa sababu ya ulimbukeni, vipawa vinapowapa
mafanikio wanakuwa na mbwembwe nyingi, kiburi kinapanda na kujidai,
wakijifikiri kuwa wao ni watu maarufu sana wanapoteza adabu na kujali utu,
wanaongeza mbwembwe nyingi sana, wanakosa umakini, na wanaacha kujilinda Kipawa ni zawadi ni
uwakili ni amana ambayo Mungu amewekeza ndani yako lazima uilinde 2Timotheo 1:14 “Ilinde
ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.” Unawezaje kujilinda kuhakikisha kuwa uko vilevile
au unazidi mno lazima ujilinde na kiburi,
watu wenye mafanikio sana duniani wala hawajidai, Hawana maringo, hawajifanyi wanajua, wanapokea
ushauri, wanajali wengine. Ni vema tukajivika unyenyekevu kwa sababu njia ya
Mungu ya kutupeleka juu ni kujishusha 1Petro
5:6
“Basi nyenyekeeni
chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;” Kumbe kanuni ya Mungu ya kukukweza ni
kujishusha na kuishi maisha ya unyenyekevu. Unyenyekevu ndio unaoonyesha
ukomavu lakini tukiwa na kiburi ni muhimu kufahamu kuwa hatuko mbali na aibu Mitahli 11:2 “Kijapo
kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.” Watu
wengi wenye vipawa na karama wameharibu
sifa zao kwa sababu ya kiburi na hivyo wamefupisha muda wao wa kumtumikia Mungu
au kutimiza kusudi walilokusudiwa na Mungu duniani ni kutokana na
kujinyenyekeza sana Yesu aliinuliwa sana hii ndio kanuni ya mafanikio ya
kutunza kipawa chako mbele za Mungu na wanadamu nia nyenyekevu itakuweka juu
kama ilivyomuweka yesu juu mno Wafilipi
2:5-11” Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo
ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya
Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;
bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa
wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa
mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha
mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti
lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila
ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”
5. Usikubali kupoa
Tunaweza
kuchochea karama vilevile kwa kuhakikisha kuwa hatuuzimi moto wa Mungu ulioko
ndani yetu, usikubali kupoa au kuwa vuguvugu, Maandiko yanaonyesha kuwa Mungu
akikupa amekupa na haondoi kipawa wala karama alizoweka ndani yetu lakini ni
kwa nini watu hufulia na kuisha kabisa sababu kubwa ni kupoa au kuwa vuguvugu
Mungu anachukizwa sana na watu vuguvugu maandiko yanaonyesha uwezo wa kupoa uko
katika mikono yetu na uwezo wa kuwa Moto pia, Mungu ameweka karama ndani yako
wewe ni wajibu wako kuhakikisha unabaki moto Ufunuo 3:15-16 “Nayajua matendo yako, ya kuwa
hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa
sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika
kinywa changu.” Unaona Mungu hapendezwi na watu vuguvugu hii maana
yake anatujua vema anataka tuwe moto, au ukishindwa uwe baridi ijulikana umekwisha
umepoa lakini kamwe Mungu hataki tuwe vuguvugu atakutapika ndio maana utaweza
kuona watu wanaibuka kisha wanatokweka na karama na vipawa vinakwisha.
6.
Usimzimishe
Roho Mtakatifu.
Biblia inaeleza
katika 1Wathesalonike 5:19 “Msimzimishe Roho;” Roho Mtakatifu ni Mungu na
ndiye chanzo cha Karama na vipawa vyote anavyowapa wanadamu, Kumzimisha Roho
Mtakatifu maana yake nini Roho Mtakatifu
kama Mungu Hakuna mtu anaweza kumzimisha
haiwezekani lakini sisi wenyewe tena tunaweza kuanza kumuhuzunisha Roho
wa Mungu kutokana na mtindo wa maisha unaomuhuzunisha Roho Mtakatifu kama Mungu
na kumfanya aondoe neema yake Waefeso
4:30 “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu;
ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.” Tunapofanya dhambi na uasi endelevu dhidi
ya Mungu Roho wa Mungu anaweza kutuacha na ushujaa wetu utakuwa umefikia kikomo
na ndio maana Daudi aliomba asiondolewe Roho Mtakatifu Zaburi 51:11 “Usinitenge na uso wako, Wala
roho yako mtakatifu usiniondolee.” Kwa
Msingi huo tukiishi mtindo wa maisha unaomnyima Mungu Roho Mtakatifu kutuongoza
na kutusaidia huku yeye akiwa chanzo cha vipawa vyetu tutapoteza uwepo wake
Napenda sana tafasiri ya Kiibrania ya neno Msimzimishe Roho wenyewe wanatumia
neno “KABAH” sawa na kusema Msimkabe
Roho Mtakatifu, Msimbanie, kiingereza Do
note Expelled, au do not neglected au Quench not, Kwa maana hiyo sisi wenyewe ndio tunawajibu wa kujiachia katika neema
ya Mungu, kwa kufunga, kuomba, kusoma neno, kuabudu, kujiweka karibu na Mungu
kuutafuta uso wake kwa bidii, kutubu kwa haraka endapo tumekosea na tutaona
Roho wa Mungu alkiendelea kukifungua kipawa kilichopo ndani yetu kidogo kidogo.
Na kututumia kwa viwango vikunbwa na vya hali ya juu.
7.
Uwe
hodari
Watu wenye
vipawa wanapigwa vita sana wanapambana watu wenye wivu, Ibilisi pia hapendi kwa
sababu karama ni silaha za maangamizi zinampa Mungu utukufu na kuharakisha kazi
ya Mungu na kwa sababu hizo upinzani ni lazima, Karama na vipawa pia Mungu
huzitumia kuinua maisha binaksi ya Muhusika kwaajili ya hayo ni lazima uwe
hodari na uwe shujaa Yoshua 1:9 “Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa;
usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila
uendako.” Mungu anataka tuwe hodari na tuwe na moyo wa ushujaa kwa
sababu anajua kuna changamoto mbele yetu, Kila mtu anayetaka kuzichochea karama
akumbuke kuwa mbali na hofu na awe na ujasiri, kwa sababu kila utakapoitumia
Karama uliyonayo kutainuka wasiopendezwa na watajaribu kwa kila jinsi na kila
namna kupingana nawe kama nduguze Yusufu walivyochukizwa naye hata kutaka
kumuua kwaajili ya ndoto alizokuwa nazo
Mwanzo 37:5-11 “Yusufu
akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii
niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda
wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya
mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe
utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno
yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni,
nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja
zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea
akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako
tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu
zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.” Unaweza
kuona Mungu anampa ndoto Yusufu kuwa mtawala, ana maono mazito kwaajili ya kuja
kuisaidia familia yake ana karama ya maongozi, ana karana ya unabii na kipawa
cha kutafasiri ndoto kipawa hiki kingembeba na kumpeleka kwenye kiwango kingine
kingeisaidia jamii na ndugu nzake pia lakini wao ndio walikuwa wa kwanza kuona
wivu na hata kutaka kumuua kabisa ona
Mwanzo 37:18-20 “Wakamwona toka mbali, na kabla
hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao,
Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika
birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje
ndoto zake.”
Unaweza kuona ndugu zake Yusufu walikusudia kumuua kwa
sababun ya ndoto zake yaani ileile karama aliyopewa iliwavutia maadui,
ningeweza kukupa mifano Mingi kama Daudi alivyotaka kuuawa na Sauli kwa sababu
ya karama, ningeweza kukupa mfano wa Samsoni alivyowindwa na Wafilisti kutokana
na ngvu zake na uwezo wake wa ajabu aliokuwa nao, ningekueleza jinsi Yesu
alivyokuwa tishio kwa viongozi wa dini sio kwa sababu alikuwa mwovu bali kwa
wema uliovutia watu kwa maelfu yao na miujiza mikubwa aliyoifanya, ningekuopa
habari za Petro na Yohana walivyokutana na uopinzani kwa sababu ya muujiza
mashuhuri walioufanya, sikwambii habari za Paulo aliyetumiwa kufanya miujiza na
kuwavuta wengi kwa Yesu alivyotaka kuuawa,
sikwambii habari za Daniel ambaye alifanyiwa njama za kila namna
kutokana na vipawa alivyokuwa navyo, sikwambii Michael Jakcson alivyochukiwa na
wazungu na kufanyiwa kila aina ya hila kutokana na vipawa, haya na mengineyo ni mifano ni mifano tu
inayokutaka uwe makinina uhakikishe unakuwa na ushujaa na moyo mkuu ili
kutokuizima ile karama iliyoko ndani yako! Kipawa na karana zina tabia ya
kuvutia watu wema na wabaya
Luka 11:
53-54 “Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza
kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi, wakimvizia, ili wapate neno
litokalo kinywani mwake.” Unaweza kuona namna na jinsi waandishi yaani
walimu nwa sheria na Mafarisayo walivyokuwa wakimzongazonga Yesu na kumchokoza
ili waweze kumsonga kwa maswali mengi kusudi lao kuu ni kupata neno la
Kumshitaki, ili kumuharibia Mungu akupe hekima na Busara kama alivyompa Yesu ili kujilinda na kujihami
na maadui.
Kwa sababu hiyo
nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono
yangu”
Na Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
0718990796
0718990796
If you're looking to burn fat then you need to start using this totally brand new custom keto plan.
JibuFutaTo produce this service, licensed nutritionists, personal trainers, and chefs united to develop keto meal plans that are efficient, convenient, price-efficient, and delicious.
Since their first launch in January 2019, thousands of people have already transformed their figure and health with the benefits a proper keto plan can provide.
Speaking of benefits; in this link, you'll discover eight scientifically-tested ones given by the keto plan.
nimebarikiwa saaaaana na nasaha zako katika mada hii. Ubarikiwe sana
JibuFutaNeno zuri...barikiwa
JibuFutaNeno zurii sana barikiwa
JibuFutaHakika nimejifunza vyema mtumishi wa Mungu
JibuFutaHakika nimefurahi na somo lako
JibuFutaNimejifunza barikiwa sana
JibuFuta