Ijumaa, 14 Februari 2020

Mtendeeni Yule Kijana Absalom kwa Upole kwaajili yangu!



2 SAMUEL 18:1-5Kisha Daudi akawahesabu watu waliokuwa pamoja naye, akaweka maakida wa elfu elfu, na maakida wa mia mia juu yao. Daudi akawapeleka hao watu vitani, theluthi moja chini ya mkono wa Yoabu, na theluthi ya pili chini ya mkono wa Abishai, mwana wa Seruya nduguye Yoabu, na theluthi ya tatu chini ya mkono wa Itai, Mgiti. Mfalme akawaambia watu, Bila shaka mimi mwenyewe nami nitatoka pamoja nanyi. Lakini watu wakasema, Wewe usitoke nje; kwa maana tukikimbia, hawatatuona sisi kuwa kitu; au tukifa nusu yetu, hawatatuona kuwa kitu; lakini wewe u wa thamani kuliko watu elfu kumi katika sisi; kwa hivyo sasa ni afadhali ukae tayari kutusaidia toka mjini. Mfalme akawaambia, Yaliyo mema machoni penu ndiyo nitakayofanya. Basi mfalme akasimama kando ya lango, na hao watu wakatoka kwa elfu zao na mia zao. Mfalme akawaamuru Yoabu na Abishai na Itai, akasema, Mtendeeni yule kijana, Absalomu, kwa upole kwa ajili yangu. Nao watu wote wakasikia, mfalme alipowaagiza maakida wote katika habari za Absalomu.”   

    

Utangulizi:-
Moja ya maswala magumu sana katika maisha ni pamoja na kufanya maamuzi hususani wakati mtu unayempenda na kumthamini anapokufanyia jambo baya sana na jambo hilo ukawa umelithibitisha, kuwa ni la kweli katika nyakati kama hizo.
·         Watu wengi huweza kutoa adhabu kali sana za kukomesha na kuangamiza pale wanapokuwa wamefanyiwa mambo mabaya.
·         Tumeshuhudia watu wakiwachoma moto watoto wadogo kwa sababu tu wamechukua fedha ua wameiba
·         Wengine wamewaadhibu kwa kuwachapa vibaya kwa mikanda na kuwajeruhi wakosaji
·         Wengine wamemwagiwa tindi kali, au kuwapeleka polisi
·         Wengine wamepeleka taarifa katika vyombo vya habari na magazeti
Makanisani pia tunashuhudia watu wakitengwa na kufukuzwa utumishi bila malipo yoyote, wakinyimwa posho, kutengwa miezi kadhaa, kufungiwa huduma kuchafuliwa na kuwazuia kihuduma ili yamkini ikiwezekana wasiinuke tena. Na kila wakati kunukuu taarifa zao kana kwamba wao ndio watu waovu zaidi wa kutolewa mifano
Je unafanya nini wakati uwapendao, watoto, ndugu, jamaa, rafiki, na kadhalika wanapokuasi na kusimama kinyume nasi na kuanza kutubomoa, wale tuliowagharimia wanapotukosea tunafanya nini?

2 Samuel 18:1-5
Katika kifungu hiki Daudi analazimika kupigana vita, vita hii ni mbaya kuliko zote alizowahi kupigana katika maisha yake ni vita ngumu safari hii mfalme hapigani na wafilisti wala Goliath wala maadui za Bwana anapigana na ndugu zake mwenyewe Israel wakiongozwa na mwanaye mwenyewe kijana wake mzuri aliyeitwa Absalom!
Hakuna vita mbaya duniani kama vita vya wenyewe kwa wenyewe, ni vita ngumu, ukisema ummalize adui ni kama unajimaliza mwenyewe

Mathayo 12:25-26 “Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama.  Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje?”            
 

Yesu anaonyesha ubaya wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vita hii ndio iliyokuwa ikimkabili Daudi wakati huu, hapa ilikuwa vita inayoweza kuleta ukiwa mkubwa sana na huzuni kubwa mno.
Vita yoyote ya Taifa kwa taifa yaani taifa lililogawanyika
Vita yoyote ya Familia iliyogawanyika
Vita yoyote ya mtu na mkewe au mtu na mumewe
Vita vya mtu na rafiki yake
Vita ya mtu na mchumba wake
Vita ya watoto na wazazi
Vita vya mtu uliyengharimia
Vita vya mchungaji na wachungaji wenzake au na wazee wa kanisa ama na washirika, vita vya taasisi moja inayofanana, vita vya wakristo kwa wakristo,
Au wanakwaya kwa wanakwaya

Vita za namna hii zinakuwa mbaya sana na zinasababisha ukiwa mkubwa hasa inapotokea kuwa upande mmoja unakusudia kuumlaliza upande mwingine kabisa huku hakuna anayefaidika na vita hiyo.
Haya ndiyo yaliyomkuta Daudi mara hii anapigana vita na mwanaye mpendwa mzuri aliyeitwa Absalom.
Absalom alikuwa kijana wa mfalme aliyesifiwa sana, alikuwa mzuri na msafi, alipendeza na kuvutia  na alikuwa na ushawishi kwa watu, alikuwa na nywele nzuri na ndefu ambazo zlilikatwa mara tatu tu kwa mwaka, hakuwa na ila ya aina yoyote kwa habari ya uzuri, pia alikuwa na akili hata hivyo mambo kadhaa yalichangia kuharibu maisha ya kijana huyu.
Alikuwa na Uchungu
 Alikuwa ni kisasi
Alikuwa na Hila
Alikuwa na kiburi na mwenye kukosa Subira pia hakuwa na msamaha

Mambo haya yalipelekea kijana huyu kumuasi baba yake na kujitangaza kuwa Mfalme 2Samuel 14:25-26”Basi katika Israeli wote hapakuwa na mtu hata mmoja mwenye kusifiwa kwa uzuri wake kama huyo Absalomu; tangu nyayo za miguu yake hata utosi wa kichwa chake hapakuwa na ila kwake. Naye aliponyoa kichwa, (basi mwisho wa kila mwaka hunyoa; na kwa sababu nywele zilikuwa nzito kwake, kwa hiyo akanyoa;) hupima nywele za kichwa chake shekeli mia mbili kwa uzani wa mfalme.”  

        
Kijana huyu alikuwa na uwezo wa kutumia hila na akili aliyonayo aliweza kuhadaa mioyo ya watu kwa muda wa miaka kama minne hivi 2Samuel 15:1-12, “Ikawa baada ya hayo, Absalomu akajiwekea tayari gari na farasi, na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake. Tena Absalomu huondoka asubuhi na mapema, na kusimama kando ya njia ya lango; kisha ikawa, mtu ye yote aliyekuwa na neno, lililokuwa halina budi kufika kwa mfalme ili kuhukumiwa, Absalomu humwita mtu huyo kwake, na kumwuliza, Wewe u mtu wa mji gani? Naye akasema, Mtumwa wako ni mtu wa kabila fulani ya Israeli.  Naye Absalomu humwambia, Tazama, maneno yako ni mema yenye haki; lakini hapana mtu aliyeagizwa na mfalme kukusikiliza. Tena Absalomu husema, Laiti mimi ningewekwa kuwa mwamuzi katika nchi hii, ili kila mtu mwenye neno au daawa aje kwangu, nimpatie haki yake! Tena ikawa hapo alipokaribia mtu ye yote kumsujudia, hunyosha mkono wake, na kumshika, na kumbusu. Hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Israeli wote, waliomwendea mfalme ili wapate hukumu; na hivyo Absalomu akawadanganya watu wa Israeli. Hata ikawa mwisho wa miaka minne, Absalomu akamwambia mfalme Tafadhali uniache niende nikaondoe nadhiri yangu, niliyomwekea Bwana huko Hebroni. Maana mimi mtumishi wako naliweka nadhiri hapo nilipokuwa nikikaa Geshuri katika Shamu, nikasema, Kama Bwana akinirudisha Yerusalemu kweli, ndipo nitamtumikia Bwana. Naye mfalme akamwambia, Enenda na amani. Basi akaondoka, akaenda Hebroni. Lakini Absalomu akapeleka wapelelezi katika kabila zote za Israeli kusema, Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta, ndipo mtakaposema Absalomu anamilikl huko Hebroni. Na watu mia mbili walioalikwa wakatoka Yerusalemu pamoja na Absalomu, wakaenda katika ujinga wao wasijue neno lo lote. Absalomu naye akatuma kumwita Ahithofeli Mgiloni, mshauri wake Daudi, kutoka katika mji wake, yaani, Gilo, alipokuwa akitoa dhabihu. Fitina yao ikawa na nguvu; maana watu waliokuwa pamoja na Absalomu wakazidi kuwa wengi. 

Safari hii uasi wake ulikuwa na nguvu ya kupita kawaida na alitaka kuithibitishia Isarael ya kuwa kweli amaemuasi baba yake

2Samuel 16:21-23Naye Ahithofeli akamwambia Absalomu, Ingia wewe kwa masuria ya baba yako, hao aliowaacha ili kutunza nyumba; na Israeli wote watasikia ya kuwa umechukizwa kabisa na baba yako; ndipo itatiwa nguvu mikono yao wote walio pamoja nawe. Basi wakamtandikia Absalomu hema juu ya nyumba darini; naye Absalomu akaingia kwa masuria ya babaye machoni pa Israeli wote. Na shauri lake Ahithofeli, alilokuwa akilitoa siku zile, lilikuwa kama mtu aulizapo kwa neno la Mungu; ndivyo yalivyokuwa mashauri yote ya Ahithofeli, kwa Daudi, na kwa Absalomu.” 

   
Mshauri wa Absalom alishauri kuwa anayepaswa kuuawa hapa ni Daudi peke yake na sio vinginevyo ili watu wakae katika amani 2Samuel 17:1-4 “Zaidi ya hayo Ahithofeli akamwambia Absalomu, Niache nichague watu kumi na mbili elfu, nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu; nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake; na hao watu wote nitawarejeza kwako; mtu yule umtafutaye ni kana kwamba wamerudi wote; na hivyo watu wote watakuwa katika amani. Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni pa wazee wote wa Israeli.” 

  
Unaweza kuona kuwa kijana wako uliyemzaa mwenyewe na ni Mashuhuri anakuasi waziwazi na anakusudia kukumaliza kabisa, amekuvunjia heshima yako hadharani amekudhalilisha anakuweka katika wakati mgumu je? katika hali kama hii unafanya nini hivi ndivyo Daudi alivyofanya nasi ni muhimu tukafanya au kujifunza kutoka kwake!

1.       Kubali kushuka

Watu wengi sana hususani vijana  na viongozi mbalimbali watu wao wanapowaasi, hawakubali kujishusha hata siku moja, wanataka kushughulikia matatizo wakiwa katika mamlaka yao ileile au katika mfumo wa cheo chao hujui mi mumeo, hujui mi askofu wako, Daudi alijua kuwa nia hii sio rahisi kufanikiwa kumpata mpendwa wake yeye aliamua kujishusha, aliachia ikulu na kukimbia pekupeku alijua kuwa hawezi kujiokoa wala kuwaokoa watu wake na mwanaye kama atabakia ikulu aliondoka

2samuel 15:14,30  Basi Daudi akawaambia watumishi wake wote waliokuwa pamoja naye Yerusalemu, Ondokeni, tukakimbie kwa kuwa tusipokimbia hapana mtu miongoni mwetu atakayeokoka mikononi mwa Absalomu; haya! Fanyeni haraka, tuondoke, asitupate Kwa upesi, Na kutuletea maovu, na kuupiga mji huu kwa makali ya upanga. , Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda."            

Ili kumpata mwanadamu aliyeasi Yesu alikubali kuacha Enzi na utukufu, akanyenyekea kama mwanadamu mtumwa, watu wanavutiwa na mtu aliyejishusha, na sio Yule anayebaki ikulu, anayebaki katika haki yake na mamlaka yake, Absalom aliweza kuihadaa mioyo ya watu kwa sababu alijinyenyekeza kwao watu wakampenda

2Samuel 15:5-6,
Tena ikawa hapo alipokaribia mtu ye yote kumsujudia, hunyosha mkono wake, na kumshika, na kumbusu. Hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Israeli wote, waliomwendea mfalme ili wapate hukumu; na hivyo Absalomu akawadanganya watu wa Israeli.         

Absalom alifahamu kuwa ili aipate mioyo ya watu  hana budi kujishusha katika kiwango chao, ili kuipata mioyo ya watu jishushe katika kiwango chao, Kamwe usitumie mamlaka yako katika kutatua matatizo, hujui mimi ni mzazi wako?, hujui mimi ni mumeo? Hajui mimi ndiye Rais?, hujui mimi ndiye Askofu? Atanitambua atajua kuwa mimi ndiye mwenyeji, mimi ndiye mwangalizi, mimi ndiye alwatani, mimi ndiye nimeshika mpini. Daudi aliacha viatu, alichukua namna ya mtumwa, aliondoka ikulu, Kujishusha kunasaidia kutatua matatizo,


1Samuel 25:5-8, Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana, Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mnisalimie; na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani mwako, na amani kwao wote ulio nao. Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu wanaokata manyoya kondoo zako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli. Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, cho chote kitakachokujia mkononi, uwape watumwa wako na mwanao Daudi.”
Unaona katikamkfungu hiki jinsi daudi anavyojishusha kwa Nabal wakati anaomba chakula?  Mungu humwangalia mtu mnyonge, mwenye roho iliyopondeka na kumuinua Isaya 66:2 “Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema Bwana; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.
Hatuwezi kutatua matatizo yetu bila kuamua kujishusha, kujishusha na roho ya unyenyekevu kumesaidia kujenga maisha ya watu wengi sana, kiongozi anayekaa ofisini tu bila kujali wala kujua matatizo ya watu na mahitaji yao, hawezi kukubaliaka na kufaa kwa Mungu na watu, Unyenyekevu ni njia ya kutupeleka juu sana katika kukubalika kwa Mungu na wanadamu tunapojishusha tunampa Mungu nafasi ya kuonyesha nguvu zake dhidi ya wale wanaotuandama kitendo cha Daudi kukimbia ikulu miguu peku na kulia na kurusha mavumbi juu kilikuwa ni kitendo cha kujishusha na kuhitaji neema ya Mungu kwamba Mungu aingilie kati katika mgopgoro huu mzito kati yake na mwanae mwenyewe, Yesu alikuwa ni Mungu na aliaxcha enzi na utukufu ili kuja duniani kutupatanisha tena isis tulioasi na kuturejesha mioyo yetu, Ndoa nyingi na migogoro mingi  duniani inawezankusuluhishwa kwa unyenyekevu endapo upande mmoja utajishusha!

2.       Rudisha sanduku la Mungu mahali pake 2Samuel 15:24-29

Na tazama, Sadoki naye akaja, na Walawi wote pamoja naye, huku wakilichukua sanduku la agano la Mungu; kisha wakalitua hilo sanduku la Mungu; Abiathari naye akapanda juu, hata watu wote walipokwisha kuutoka mji.  Naye mfalme akamwambia Sadoki, Rudisha sanduku la Mungu mjini; nikipata kibali machoni pa Bwana atanirudisha, na kunionyesha tena sanduku hili, na maskani yake;  lakini akisema kama hivi, Mimi si radhi nawe kabisa; basi, mimi hapa, na anitendee kama aonavyo kuwa vyema. Kisha mfalme akamwambia Sadoki, kuhani, Angalia, rudini mjini kwa amani, na wana wenu wawili pamoja nanyi, Ahimaasi,mwana wako, na Yonathani,mwana wa Abiathari. Angalia, mimi nitangoja penye vivuko vya jangwani, hata litakaponifikilia neno la kunipasha habari kutoka kwenu. Basi Sadoki na Abiathari wakalichukua sanduku la Mungu, wakalirudisha Yerusalemu; wakakaa huko. 

 
Sanduku la Agano la Mungu lilikuwa chombo muhimu sana chenye kuwakilisha uwepo wa Mungu, Ni chombo kinachoonekana kinachowakilisha uwepo wa Mungu asiyeonekana, Chombo hiki kilimwakilisha Yesu Kristo, aliye chapa ya mng’ao wa utukufu wa Mungu, Israel waliamini kuwa hata ukiingia vitani na chombo hiki lazima utashinda, Viongozi wengi sana wanapokuwa madarakani, huwa wanasahau kuwa unaweza kuwepo madarakani lakini Mungu au uwepo wa Mungu ukawa hauko pamoja nawe, unaweza kuwa mpakwa mafuta lakini Mungu akawa amekuacha, kama ilivyokuwa kwa Sauli mfalme, Ni lazima kwanza ufahamu Mungu yuko upande wa nani unapokuwa na migogoro, Absalom au wewe? Mungu yuko upande gani Hakuna mtu mwenye hati miliki ya uwepo wa Mungu, Mungu yuko kwaajili ya watu wote, si vema kuwahesabu wengine na kuwahukumu kama waasi tu, Daudi alitaka apate muda wa kupata na kusikia neno la Bwana ili kujua kuwa Bwana amempa kibali nani kati yake na Absalom, kama Bwana yuko na Absalom basi Absalom awe na uhuru wa kuabudu kupitia sanduku la agano, na kama Bwana yuko naye basi atampa neema ya kuliona sanduku hilo tena lakini sio kuondoka nalo, halikuwa la kwake lilikuwa kwaajili ya watu wote wa Mungu,

·         Viongozi wengi sana wa kiroho nimeona wakiwatenga watu wanaodhani kuwa ni wenye dhambi na zaidi ya yote huwafukuza na kuwanyima hata kuabudu, au kufanya huduma fulanifulani kabisa wakiwahesabia dhambi na kuwapimia muda wa miezi na hata miaka lakini huwa wanasahau kuwa kipimo cha utii katika moyo wa Mwanadamu anacho Mungu tu, Mtu hapimwi kwa kumzuia asihubiri, asiombe au asitoe sadaka huko ni kuhukumu na kujichukulia madaraka makubwa, wewe sio Mungu wala mimi sio Mungu huwezi kupima kati ya wewe na yule unayemdhania ni adui Mungu yuko na nani, huwezi kuwa na hati miliki ya uwepo wa Mungu, Mungu anaweza kuwa na yeyote tu Absalom au wewe, Daudi alifahamu hilo aliliacha sanduku la agano ili yeyeote anayetaka uwepo wa Mungu aukaribie.

·         Au wanaweza kumzuia mtu asifanyie wengine maombezi, swala la Ibada kwa binadamu liko wazi kwa kila mtu, swala la ibada halina hakimiliki, kuabudu ni swala huru kwa kila mtu hata kama sio wa dhehebu lako, Mungu si wa dehebu Fulani au dini Fulani kila mtu anahaki ya kuabudu na anapaswa kuabudu, kila mtu anapewa nafasi na maandiko na anapewa haki ya kuufikia uwepo wa Bwana Luka 9:49-50, Yohana akajibu akamwambia; Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kwa jina lako; tukamkataza, kwa sababu hafuatani na sisi. Yesu akamwambia, Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu.” Matendo 4:18-20 “Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu. Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe; maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.” Ni kwa kujua haya Daudi aliwaambia makuhani walirudishe sanduku la agano mahali pake, Mungu atusaidie kuwa na moyo kama wa Daudi wa kutambua kuwa uwepo wa Mungu sio hatimiliki ya mtu fulani, au kanisa Fulani au mchungaji Fulani au askofu Fulani kila mtu ana haki ya kuabudu.

3.       Fanya maombi ya kujidhili (Kujishusha).

2samuel 15:30-32 “Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda.  Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee Bwana, nakusihi, uligeuze shauri la Ahithofeli liwe ubatili. Ikawa, Daudi alipofika juu, hapo Mungu alipoabudiwa, tazama, Hushai, Mwarki, akaja kumlaki na joho lake limeraruliwa, tena ana udongo kichwani mwake.”
               
Daudi alifanya maombi ya kujidhili yaani alijishuhsa, alilia, hakwenda mbele za Mungu kama mwanamume na mfalme bali alikwenda kama mjakazi wa kike, alijifunika kichwa alipokuwa akimuomba Mungu

Kutoka 34:29-35, Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling'aa kwa sababu amesema naye. Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling'aa; nao wakaogopa kumkaribia. Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao. Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo BWANA amemwambia katika mlima Sinai. Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya uso wake. Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za BWANA kusema naye, kuuvua huo utaji mpaka atoke; akatoka akawaambia wana wa Israeli maneno yote aliyoambiwa.  Wana wa Israeli wakauona uso wa Musa ya kuwa ngozi ya uso wake Musa iling'aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia kusema naye.

 
Mwanamume hapaswi kufunika kichwa anapoingia katika uwepo wa Mungu, kuomba, hivyo maombi na dua za Daudi zilihusisha kujishusha kwa kiwango kikubwa na cha hali ya juu, Musa alipoingia katika uwepo wa Mungu kwa kusudi la kusema naye hakujifunika kichwa, alijifunika kichwa alipotoka, Mwanaume hapaswi kufunika kichwa chake anapokuwa katika uwepo wa Mungu ndiomaana wakristo huwa tunaondoa kofia wakati wa kusali  kwa desturi za kikristo ni aibu mwanaume kuingia katika uwepo wa Mungu akiwa amefunika kichwa chake angalia katika

 1Wakoritho 11:3-7, Lakini nataka mjue ya kuwa kichwa cha kila mwanamume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanamume, na kichwa cha Kristo ni Mungu. Kila mwanamume, asalipo, au anapohutubu, naye amefunikwa kichwa, yuaaibisha kichwa chake. Bali kila mwanamke asalipo, au anapohutubu, bila kufunika kichwa, yuaaibisha kichwa chake; kwa maana ni sawasawa na yule aliyenyolewa.  Maana mwanamke asipofunikwa na akatwe nywele. Au ikiwa ni aibu mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa, na afunikwe.  Kwa maana kweli haimpasi mwanamume kufunikwa kichwa, kwa sababu yeye ni mfano na utukufu wa Mungu. Lakini mwanamke ni utukufu wa mwanamume.”        
Tendo la Daudi kumuomba Mungu huku amefunika kichwa kilikuwa ni kitendo cha kujishusha sana alijihesabu kama mjakazi wa kike mbele za Mungu aliweka mbali ufalme wake na uanaume wake na ujemedari wake alijidhili mnombele za Mungu na dua zake zilisikiwa

Luka 18:9-14
Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.  Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.  Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.  Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.Mungu hakubalia maombi ya watu wenye kujihesabia haki, Daudi alifahamu kuwa anahitaji maombi ya kujinyenyekesha wakati huu kupita kawaida ili hatimaye Mungu aweze kumuinua tena, alirusha michanga juu alitembea pekupeku alijifunika kichwa na kulia Mungu alisikiliza dua zake kutokana na unyenyekevu mkubwa alioonyesha mbele zake.

4.       Panga vita (Mikakati) ya ukombozi.

Ni muhimu kukumbuka kuwa hakuna vita ngumu duniani kama vita ya ndugu kwa ndugu, vita ya aina hii haina mshindi, ni ngumu na ni lazima  itaacha majeraha yanayoweza kudumu kwa muda mrefu, huwezi kupanga vita ya ndugu ikawa vita ya kumalizana, mwisho wa yote utalia mwenyewe, Ni lazima vita ya aina hii iwe vita ya ukombozi 2Samuel 18:1-5Kisha Daudi akawahesabu watu waliokuwa pamoja naye, akaweka maakida wa elfu elfu, na maakida wa mia mia juu yao. Daudi akawapeleka hao watu vitani, theluthi moja chini ya mkono wa Yoabu, na theluthi ya pili chini ya mkono wa Abishai, mwana wa Seruya nduguye Yoabu, na theluthi ya tatu chini ya mkono wa Itai, Mgiti. Mfalme akawaambia watu, Bila shaka mimi mwenyewe nami nitatoka pamoja nanyi. Lakini watu wakasema, Wewe usitoke nje; kwa maana tukikimbia, hawatatuona sisi kuwa kitu; au tukifa nusu yetu, hawatatuona kuwa kitu; lakini wewe u wa thamani kuliko watu elfu kumi katika sisi; kwa hivyo sasa ni afadhali ukae tayari kutusaidia toka mjini. Mfalme akawaambia, Yaliyo mema machoni penu ndiyo nitakayofanya. Basi mfalme akasimama kando ya lango, na hao watu wakatoka kwa elfu zao na mia zao. Mfalme akawaamuru Yoabu na Abishai na Itai, akasema, Mtendeeni yule kijana, Absalomu, kwa upole kwa ajili yangu. Nao watu wote wakasikia, mfalme alipowaagiza maakida wote katika habari za Absalomu. Daudi aliona uzito wa vita hii kwani sasa hapigani na Mfilisti wala Goliath anapigana na mwanaye aliyetoka katika viuno vyake.

Vita unayopigana na nduguyo ni lazima iwe vita ya ukombozi, Mara nyingi viongozi wengi wa kiroho na Kikristo, kunapotokea shida za kimahusiano mioyo yao hubadilika na kusahahu hili, mapambano yao na makusudi yao yanakuwa ni kumaliza kabisa au kumuumiza nduguyo, kumpoteza, kufuta jina lake kumfanya akome, asione suluhu tena Daudi hakutaka kabisa kumpoteza Absalom aliagiza wazi mbele ya makamanda wote “MTENDEENI YULE KIJANA ABSALOM KWA UPOLE KWAAJILI YANGU” haya ni maneno mazito Daudi aliyasema haya hadharani, na watu wote walisikia, alikuwa na moyo, Daudi alikuwa na moyo wa kiungu, siku zote Mungu anapotuadhibu kwaajili ya makosa yetu na dhambi hutuadhibu kwa kusudi la kuturekebisha na kuturejesha, na sio kutuangamiza, Daudi alitambua udhaifu wa mwanawe Absalom kuwa ni ujana ndio unaomsumbua ni mchanga ni kuwa hajakomaa hajajua maisha, ni dasari ndogondogo zinamsumbua na aliona ni afadhali angelikufa yeye badala ya mwanawe Asalom  hakuona ufahari kupoteza hata pamoja na kuwa amemwasi alitamani kuuona tena uso wa mwanae kipenzi


2Samuel 18:33-19:4  Naye mfalme akataabika sana, akapanda juu, akaingia kile chumba kilichokuwa juu ya lango, akalia; na katika kwenda kwake alisema hivi, Mwanangu Absalomu! Ee mwanangu! Mwanangu Absalomu! Laiti ningalikufa badala yako, Absalomu, mwanangu, mwanangu! - Mfalme akajifunika uso; na mfalme akalia kwa sauti kuu, Mwanangu Absalomu, Absalomu, mwanangu, mwanangu!” Biblia inasemaje ndugu yako anapokukosea ni lazima arejeshwe kwa upole Wagalatia 6:1Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.”               

Daudi alikuwa na moyo wa urejeshi huu ndio moyo wa Mungu ndio moyo wa mtu aliyekomaa kiroho, awaye yote anayefurahia kuangamia na kupotea kwa ndugu yake na kumpoteza kabisa na akaona sawa sawa huyu atakuwa ana matatizo makubwa mno, Yuko tafauti na Moyo wa Mungu na wa Daudi.

Mungu kamwe hafurahii kufa kwake mtu mwenye dhambi Ezekiel 33:11 Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?       
Daudi hakufurahia kifo cha Absalom mwanawe, ambaye kwa vyovyote alikuwa hajaifikilia toba, Upendo wa kweli haufurahii udhalimu, Moyo wa Daudi ulikuwa tayari, kufanya kitu kwaajili ya mtu muovu, kuliko watu wema waliokuwa upande wake 2Samuel 19:5-6Basi Yoabu akaingia nyumbani kwa mfalme, akasema, Wewe leo umefedhehesha nyuso za watumishi wako wote, waliokuokoa leo roho yako, na roho za wanao, na za binti zako, na roho za wakezo, na roho za masuria wako; KWA KUWA UNAWAPENDA WAKUCHUKIAO, NA UNAWACHUKIA WAKUPENDAO. Maana umetangaza leo ya kuwa wakuu na watumishi wako si kitu kwako; maana leo nimetambua hivi; kama Absalomu angaliishi, na sisi sote tungalikufa leo, ingalikuwa vyema machoni pako”.            

Ulikuwa ni moyo wa ajabu sana na upendo mwingi usioweza kupimika najua angekuwa mtu mwingine angesema ndio afadhali kafa, Mungu kamlipizia kisasi, Mungu ameshughulikia adui zangu lakini huu haukuwa moyo wa Daudi na sio moyo wa Mungu. Ni mara ngapi tumeweza kujishughulisha na watu wanaofikiriwa kuwa wamerudi nyuma, au mara ngapi tumewajali watumishi nwanaofikiriwa kuwa wameanguka na je tumejishughulisha vipi kuirejesha mioyo yao au je umehakikisha kuwa nduguyo amerejea katika toba? Wengi wetu mtu akianguka tunamuita muasi akihama dhehebu tunavunja urafiki naye tunadhani kuwa hastahili tena hafai huo sio moyo wa mtu anayeupendeza Moyo wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Daudi tuna kitu cha kujifunza kwake

5.       Mtendeeni kwa Upole

Ingawa Absalom alikuwa amekusudia kumuua baba yake na kuwaacha watu hai, Daudi alikusudia wazi kwamba Absalom aachwe hai, Daudi alitoa nafasi ya pili kwa mkosaji, alitoa nafasi ya tatu na nne na tano na kuendelea, ni vema kuwapa wakosaji nafasi nyingine tena nani ajuae kuwa mioyo yao itabadilika nani ajuaye kuwa watakuwa wamejifunza maswala kadhaa? Naniajuaye kuwa makosa yao ilikuwa njia ya roho wa Mungu kuwafundisha kitu kama ilivyokuwa kwa mwana mpotevu? Je Mungu amemaliza kazi nao? Lazima tujihoji?

Daudi hakutaka kushindana na Absalom ni muhimu kufahamu kuwa hatupaswi kushindana na mtu aliye chini yako, Daudi hakuhesabu kuwa yuko vitani huwezi kupigana na mwanao hata kama yeye ni shetani, Mungu hapigani na shetani, hata siku moja ingawa yuko chini yake ni ujinga, Daudi hakufurahia kufa kwa mwanaye, hakufurahia kifo cha kudhalilika cha mwanaye ingawa yeye alikuwa amedhalilishwa na mwanaye, Daudi anaumia sana asiposamehe, alipenda kama angelipata nafasi ya kumtangazia mwanaye msamaha, alijuta kuikosa  nafasi hiyo alitamnani kama laiti angelipata nafasi ya kumwambia mwanangu nimekusamehe, Dhambi ya Absalom ni maumivu kwa Daudi Isaya 43:25 “Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.”  Mungu anapotusamehe dhambi hutusamehe kwaajili yake mwenyewe upendo wake unamsukuma kusamehe na anaumia anapokosa nafasi ya kutusamehe anatamani tuhojiane naye anatamani tumjie tena ili azisafishe dhambi zetu anatamani kututendea kwa upole hataki mtu aangamie hafurahii mtu awaye yote apotee anataka watu wote wafikie toba 2Petro 3:9 “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.” , unaweza kuona Daudi anamtaka kijana Absalom aachiwe uhai wake asife na dhambi ni mwanae anampenda na aliagiza wazi  “Mtendeeni Yule kijana Absalom kwa upole kwaajili yangu” Tabia ya Daudi ni tabia ya uungu inayoonyesha ukomavu wa hali ya juu, wenye kujitoa usio na ubinafsi wenye kujali maisha ya wengine.

Daudi hakumuhukumu Absalom kwa vyovyote vile alimuachia Mungu ahukumu adui zake na wote waliomkataa na kumkana.

Mungu ndiye hakimu wa kweli atakayehukumu kwa haki dhidi nya maisha yetu
Mtazamo wako si ukweli kuhusu Mungu wakati wote.

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

Maoni 1 :

  1. Okay then...

    This may sound a little creepy, and maybe even a little "supernatural"

    HOW would you like it if you could just hit "Play" and LISTEN to a short, "miracle tone"...

    And miraculously attract MORE MONEY into your life?

    I'm talking about BIG MONEY, even MILLIONS of DOLLARS!!

    Think it's too EASY? Think it's IMPOSSIBLE?!?

    Well, I've got news for you..

    Many times the largest miracles life has to offer are the EASIEST!!

    In fact, I will provide you with PROOF by letting you listen to a real-life "miracle money tone" I've synthesized...

    You just press "Play" and watch how money starts piling up around you.. starting so fast, you will be surprised..

    CLICK here now to play this magical "Miracle Wealth Building Tone" - it's my gift to you!!

    JibuFuta