Alhamisi, 23 Aprili 2020

Yesu Kristo na Mitandao ya kijamii!


Luka 13:1-5Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao.  Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.”




Utangulizi:


Ni muhimu kufahamu kuwa taarifa (Habari) ni moja ya nyenzo yenye kubwa sana yenye kubeba maana zinazoweza kujenga au kubomoa jamii, taarifa zina nguvu, zina nguvu zote mbili za kujenga au kubomoa, Mungu ndiye mwanzilishi wa taarifa, Alipomuumba mwanadamu alimpa taarifa ya namna na jinsi ya kuutawala ulimwengu alimweleza kama mtu huru namna anavyoweza kuutumia ulimwengu na alimuelekeza namna nzuri ya kuutumia ulimwengu lakini pia alimuonya kuwa kama atautumia ulimwengu vibaya angeweza kuleta madhara makubwa kwa maisha yake na jamii yake yaani kifo. Taarifa inaweza kuwa ndogo lakini kama ikitumika vibaya inaweza kuleta madhara makubwa sana kwa jamii kama njiti ya kiberiti inavyoweza kuchoma msitu mzima!


Ni muhimu kufahamu kuwa nyakati za Biblia pia kulikuwa na namna ambavyo watu waliweza kupokea na kutoa taarifa kama unavyoweza kuona katika kifungu hiki Luka 13:1-5Na wakati uo huo walikuwapo watu waliompasha habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao.  Akawajibu akawaambia, Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.” 


Yesu alikuwa amepokea taarifa au habari kuhusu Wagalilaya waliouawa vibaya na Pilato, na baada ya kupokea taarifa hizi tunaona namna Yesu alivyozitumia taarifa hizo sasa kuwafundisha watu wake somo kuhusu toba na pia akiunganisha na taarifa nyingine ya watu kumi walioangukiwa na mnara huko siloamu, Kutoa na kupokea taarifa ni haki ya kila jamii, Yesu aliitumia taarifa hii kwa sababu huenda aliamini au kulikuwa na namna ya uthibitisho kuwa chanzo cha taarifa alichokipokea kilikuwa ni chanzo cha kuaminika na kwa sababu hiyo taarifa alizozipokea zilikuwa na ukweli, na hivyo alizitumia kufundisha kama mfano kwa jamii iliyomzunguka, Unapochunguza kwa kina mafundisho ya Yesu Kristo utaweza kuona alikuwa na mifano mingi sana na alikuwa na stori nyingi sana na khadithi nyingi sana na nyingi alizitumia katika kuielimisha jamii na kuijenga kama jinsi Mungu anavyotaka.


Kutokana na kupanuka kwa technolojia leo hii kumekuweko na vyanzo vingi sana vya kupokea na kutoa habari, lakini ni jambo la kusikitisha sana kuwa jamii ya leo haizingatii uadilifu katika swala zima la kupokea na kutoa habari, Mfano mzuri ni tukio la hivi karibuni ambapo watangazaji/ waandishi wa habari wa TBC walifariki, lakini wakati huo huo kulikuwa na taarifa za kufariki kwa Mtangazaji wa shirika hilo wa habari za biashatra aliyeitwa “Gloria Maiko” aidha kabla ya kuenea kwa taarifa hii kuhusu kufa kwake iliebnea taarifa kuwa Gloria anaumwa sana tena ana ugonjwa wa Corona, Mimi napenda habari, mimi ni mwana habari, mimi nimesoma Introduction to jounalism, napenda kupata taarifa kwa sababu huwa pia natoa taarifa yaani nazitumia kuijenga jamii, sio hivyo tu unaposoma chuo cha Biblia kwaajili ya kazi ya uchungaji hausomei Biblia pekee unaandaliwa pia kuwa mwana habari kwa sababu kanisa linaweza kuwa na gazeti, Kanisa linaweza kuandika vitabu, kanisa linaweza kuwa na televisheni, kanisa linaweza kuwa na radio, kanisa linaweza kuwa na ukurasa wa faceboo, instagram, blog na nyenzo nyingine za utoaji wa taarifa kwa hiyo lazima watu wa Mungu wawe na angalau ufahamu mdogo tu kuhusu upokeaji na utoaji wa habari, wakati huu nilisoma chanzo kingine kuhusu Gloria kinasema hivi ngoja nikinukuu

 “TBC1 tuliwaonya kukusanyika siku ya msiba wa Marini Hassan hamkusikia! Haya leo Joseph Kambangwa mfanyakazi wenu kafa kwa corona na maziko ni kesho saa 4 huko huko Mloganzila! **Gloria Maiko (anatangazaga habari za biashara) yuko hoi ana dalili zote za corona! RIP Kambangwa 

mwisho wa kunukuu, angalia huyu ni mtu mwenye akili timamu, ni mtu ambaye jamii inamtegemea, jamii inaamini labda katika hiki alichokisema lakini je habari hii ilikuwa na malengo gani kwa jamii, ilikusudia nini kwa Gloria? Na kwa familia yake, je ilikuwa inajenga au inabomoa? Kwa sababu baada ya kuenea kwa Taarifa hii Gloria Maiko alijitokeza kwenye mitandao ya kijamii akithibitisha kuwa yeye yuko hai na wala haumwi! Lakini mwandishi anajisikiaje? Baada ya Gloria mwenyewe kutokea je wale walioeneza katika mitandao ya kijamii na kutoa salamu za astarehe kwa amani wanajisikiaje katika mioyo yao baada ya mtu mliyemzushia kifo kujitokeza na kuonyesha yuko hai, nimetoa tu mfano huu lakini Jambo hili limewahi kuwatokea wengi, hapa nchini hata Mheshimiwa Augustin Lyatonga Mrema alizushiwa mara kadhaa mpaka alipojitokeza na kuionya jamii kuwa yeye ni mzima na kuwa kuanzia sasa atawafungulia mashtaka watu wanaoanzisha uzushi huu, Huko ulaya mambo ya aina hii yako sana lakini kwa mujibu wa tamaduni zao, Lakini sisi ni Watanzania na wana Afrika Mashariki je mambo haya ni sawasawa? Je wale waliosomea uandishi wa habari jambo hili ni sawa katika utoaji wa taarifa na upokeaji, Je wale wanaozushia wenzao hujitokeza kuomba radhi? Je wanachukuliwa hatua gani je ni aina gani ya jamii tunaijenga ya watu wanaosema ukweli au jamii ya waongo? Mungu ametupa hekima na akili na maendeleo makubwa ya nyenzo za utoaji wa taarifa lakini ni muhimu zikatumika kwaajili ya utukufu wa Mungu, kwa wakristo tunaambiwa katika maandiko kwamba lolote tulifanyalo kwa neno au kwa tendo tulifanye kwa utukufu wa Mungu ona 

Wakolosai 3:17 “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.” 

Swali kubwa ambalo kila mwana jamii anapaswa kujiuliza na kuhoji ni kuwa kama Yesu angekuwepo Duniani leo ni habari gani angeikubali na habari gani angeikataa na je angetumiaje mitandai ya kijamii, na sisi vilevile tujiulize je tunapopata habari ambazo hazina uhakika haziko sahihi, hazina utu, zina mitazamo hasi, zinaupendeleo, na kama ni za uongo wanaozitoa hawawajibishwi, habari hazina kiasi, na ziko kinyume na uadilifu je tungejisikiaje? Nafikiri wote tuna namna ambavyo tunatarajia jinsi habari au taarifa inavyopaswa kuwa! Mkurugenzi wa Maadili ya uandishi wa habari aitwaye Aidan White anasema ziko kanuni 400 ambazo wanahabari wanapaswa kuzizingatia lakini ziko kanuni 5 Muhimu zaidi ambazo kila mwandishi na mtoa habari anapaswa kuzifuata bila kushindwa.


1.       Ukweli na Uhakika (Accuracy) – “the quality or state of being correct or precise” Maana yake kila mtoa habari na mpokea habari na mtawanya habari au taarifa anapaswa kuhakikisha kuwa taarifa anayoitoa ina UKWELI na pia IMEHAKIKISHWA.  Lakini pia kuzinagatia kuwa habari inaweza kuwa ya ukweli na imehakikishwa lakini swali je ni wakati muafaka kuitoa? Kwa sababu inaweza kuwa kweli na ya uhakika lakini wakati ukawa hauruhusu kuisema au mazingira yakawa hayaruhusu kusema !, tunapohubiri injili watu wa Mungu huwa hatuleti maneno ya kushawishi, wale yenye ufundi wa kibinadamu tunapopeleka habari njema tunapeleka habari ambazo ni za kweli na zinathibitishwa na Roho Mtakatifu, ile Nguvu ya ukweli pekee inauwezo wa kuwaweka watu huru na kuiponya jamii. Waandishi wa habari ni kama manabii wanapaswa kutia habari za ukweli na uhakika ona  Kumbukumbu la Torati 18:22 “Atakaponena nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena Bwana; kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogopeBiblia liagiza kuwa kama nabii atatia taarifa na akadai taarifa hiyo imetoka kwa Mungu na kumbe sivyo yaani haikutimia yaani haina ukweli asiogopwe maana yake achukuliwe hatua, kwa hiyo kama watu wanaotoa habari na habari zao zikawa sio za uhakika torati inashauri wachukuliwe hatua katika agano la kale waliuawa, katika agano jipya  wanapaswa kuchukuliwa hatua, Yesu angelikuwepo leo hangeweza kukubalia habari ambayo haijathibitishwa haina ukweli na haijahakikishwa!


2.       Huru – Independence – yaani taarifa inapaswa kuwa ya haki isiyopendelea upande wowote, Kila mtoa habari na mpokea habari anapaswa kuwa na mtizamo wa haki, hapaswi kuwa mwenye kupendelea upande fulani, mfano kama ni kwa habari ya vyama vya siasa ni vema mtoa habari na mpokea habari wakawa hawana mtazamo wa kisiasa au mtazamo wa siasa zinazofungamana na upande fulani, taarifa itolewe kwa uwazi na kwa haki na ihaririwe kwa uwazi na kwa haki, Maandiko yanatufundisha wale wanaomuamini Yesu kuwa imani yetu katika Kristo isiwe kwaajili ya kupendelea watu Yakobo 2:1 “Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu unaona Yesu angelikuwepo leo hangeweza kupokea au kutoa habari inayomkandamiza mtu fulani haki ingesimama


3.       Usiyo na Masalahi nayo – Impartiality kwa kiingereza neno hili maana yake “Impartiality is a principle of justice holding that decisions should be based on objective criteria, rather than on the basis of bias, prejudice, or preferring the benefit to one person over another for improper reasons“ yaani kanuni ya haki inayotaka maamuzi yafanyike kwa mujibu wa vigezo na sio kwa sababu mtu una masalahi fulani, au ukungu fulani unaotaka mtu mmoja anufaike dhidi ya mwingine kwa sababu zisizo sahihi, unapopokea au kutoa habari kwa makusudi maovu au kwa uependeleo kwa Mungu hufai kuwa mtu wa haki, Yesu angekuwepo leo kwa habari ya kupokea na kutoa habari angehukumu kwa haki  Isaya 11:1-5Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia” Mtoa habari au mpokea habari anapaswa kuwa mwaminifu na kuwa mtu wa haki, wakati mwingine kwa sababu ya mitazamo fulani na hata kwaajili ya kupokea rushwa tumepokea au kutoa habari kwa maslahi ya upande fulani kwa sababu tunaletu jambo, Mungu hapendezwi na utaratibu huo na ndio maana hatua kali sana zinapaswa kuchukuliwa endapo itabainika mwandishi kuwa ana dalili za kupokea rushwa.


4.       Taarifa yenye kujali utu – Humanity Ni muhimu kufahamu kuwa biblia inasema usiue kuua kuko kwa namna nyingi sana unaweza kuua kwa kutumia maneno, unamuua mtu kisiasa, umamuharibia mtu au unamchafua mtu huku ni kuua mpokea habari au mtoa habari anapaswa kuhakikisha kuwa anajali utu, ni dhambi kuandika, kupokea au kutoa habari yenye kudhuru, yenye kuharibu ubinadamu wa mtu, au yenye kumvunjia mtu heshima hatupaswi kutoa habari wala kusambaza habari au habari picha yenye kuharibu maisha ya wengine au kudhalilisha, watu wasiojua kutumia mitandao ya kijamii wanapiga picha hata za watu waliopata ajali mbaya na kuzisambaza katika mitandao ya kijamii, katika nchi nyingi zilizoendelea hata mwili wa Marehemu anapoagwa haupigwi picha, Picha ya marehemu inayoruhusiwa kuonekana ni ile ambayo wanafamilia wataiweka juu ya jeneza kwaajili ya kumbukumbu yake, nchi nyingi zawatu wasiostaraabika utaona mtu aliyepasuka kichwa kwa ajali, waliovunjika miguu, mtu mwenye ulemavu wa jabu na picha za kutisha sana zinarushwa kwenye mitandao ya kijamii, je umewahi kujiuliza kwanini mtu akipata ajali watu hutoa nguo zao na kuufunika mwili wa marehemu?  Ni kwaajili ya kujali utu, Mungu hawezi kukubali na kufurahia utu wa mtu udhalilishwe, kwa msingi huo kila mtoa habari na mpokea habari namsambazaji anapaswa mno sana kuzingatia utu, Yesu alikubali kifo cha aibu pale msalabani ili kutunza heshima ya mwanadamu, natarajia kuona jamii iliyostaarabika ambayo haitarusha picha ya marehemu yoyote akiwa na pamba puani, wala hata jeneza ikiwezekana na kama umefiwa weka picha ya aliyefariki ikiwa katika hali ya ubora na usiiwekee “X” muonyehse mtu enzi za ubora wake, sikitika kwa kumpoteza mtu huyo lakini usimdhalilishe nduguyo, aidha usisambaze wala usizikubali picha za watu walio katika hali mbaya za ajali, mwanadamu ameumbwa kwa sura na utukufu wa Mungu na lazima utu wa kila mtu uheshimiwe, hali kadhalika picha za ngono na zenye kuonyesha uchi ni mwiko kwa watu waadilifu, Mtu wa haki huwa hadhalilishi mtu mwingine. Mathayo 1:18-19Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.Mtu wa haki huwa hafanyi mambo kwa kusudi la kumuaibisha mtu mwingine hata kama mtu huyo ni kweli amefanya jambo hilo Yesu angekuwepo leo hangekubali kupokea au kutoa taarifa zinazodhalilisha utu wa mwanadamu ambao ni uumbaji wake.


5.       Kuwajibika – accountability - In ethics and governance, accountability is answerability, Maana yake kila mtoa habari na mpokea habari na msambaza habari wanapaswa kujua na kukubali kuwa wanawajibika kwa habari wanazotoa au kusambaza, kwa msingi huo kama utatoa habari na ikasababisha madhara au hata isiposababisha madhara ufahamu kuwa unatakiwa kuwa na utayari wa kuijibia kuitolea maelezo na kuwa tayari kuomba radhi ikiwa umekosea,  au kukubali kukosoelewa na kupokea maoni ya jamii kuhusiana na ulichokitoa au kukisema na ikiwezekana kuwa tayari kushitakiwa mahakamani na hata kufungwa na au hata kuuawa na wale watakaochukizwa na habari ulizozitoa, kila habari unayoitoa ni muhimu kufahamu kuwa itakugharimu Yesu alisema kila neno lisilo na maana atakalolinena mwanadamu atatoa hesabu yake Mathayo 12:36-37Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwaYesu atakapokuja atawahukumu wazishi wote hapa aliwaonya watu waliokuwa wakitoa habari zisizo sahihi kuhusu utendaji wa Yesu Kristo, Yesu anatoa pepo kwa Roho wa Mungu wapotoshaji wakesema anatumia nguvu za mkuu wa pepo Baalzebub, lazima ieleweke wazi kuwa watioa habari watawajibika sio mbele za wanadamu tu na mbele za Mungu!


Hitimisho!

Biola shaka kuna kitu umejifunza hapo sisi kama wakristo ndio chumvi ya ulimwengu napenda kila mmoja wetu aelimike na kukubalia kujifunza kuwa katika wakati huu wa utandawazi wakati ambapo kila mwanadamu anauwezo wa kutoa taarifa, kupokea taarifa na kusambaza taarifa ni Muhuhimu kwetu tukaacha kujisahau na kukumbuka kuwa ziko kanuni za neno la Mungu ambazo zinatuongoza jinsi na namna ya kuitumia mitandao hii ya kijamii, ninapohitimisha nataka kukukumbusha mambo kadhaa ya msingi yafuatayo:-

a.       Tumia mitandao ya kijamii kuhudumu kwa neno la Mungu na kusambaza habri njema
b.      Kumbuka kujitenga kwa muda na mitandao ya kijamii na kwenda kuomba
c.       Kumbuka kuwakumbusha watu kutubu na kuishi maisha yanayompendeza Mungu
d.      Kumbuka kutia moyo mambo yaliyo mema kwa ku like na kuweka maoni yako na kukosoa vikali maovu na kuonyesha wazi jambo au kitu usichopendezwa nacho tumia neno la Mungu
e.      Tumia mitandao ya kijamii kudumisha uhusiano na kutafuta amani na watu wote na sio kuharibu
f.        Tumia mitandao ya kijamii kuonyesha semina, mikutano ya neno la Mungu na maswala muhimu ya kijamii onya karipia fundisha na jihadhari na matapeli
g.       Zingatia kanuni husika tulizojifunza na muombe Mungu ziwe kanuni muhimu katika maisha yako, asomaye na afahamu, ukiyajua hayo heri wewe ukiyatenda


Na. Mchungaji Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima
0718990796

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni