Alhamisi, 11 Juni 2020

Mama yangu alinichukua Mimba hatiani!


Zaburi 51:5 “Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani



Utangulizi:


Ni muhimu kufahamu kwamba Mojawapo ya Maandiko ambayo yamekuwa na changamoto kubwa sana kwa wasomi wengi wa Biblia na kukutana na ugumu katika tafasiri zake ni Pamoja na andiko hili katika Zaburi 51:5 “Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatianiwote tunajua wazi kuwa zaburi hii imeandikwa na Daudi, na maneno yake ni sehemu ya toba aliyokuwa akiifanya baada ya kufanya dhambi, ya zinaa na mke wa Huria na kufanya njama ya mauaji dhidi ya Uria ili kuficha ushahidi, ni baada ya kukabiliwa na Nabii  Nathan na kuonywa kuhusu kosa lake Daudi alitubu na kusema maneno haya yaliyopo katika zaburi ya 51.  Kuna maneno mengi sana aliyasema katika zaburi hii kama sehemu ya toba yake lakini neno kuu na ambalo linazua mjadala mkubwa sana kwa wasomi wengi wa Biblia ni maneno haya “MAMA YANGU ALINICHUKUA MIMBA HATIANI!”  Swali kubwa likiwa ni kwanini Daudi anazungumza maneno haya? Anamaanisha nini, Daudi anazungumzia hali ya mwanadamu kuzaliwa akiwa na asili ya dhambi? Au anamaanisha kuwa mwanadamu anaanza kuwa mwenye dhambi tangu siku mimba inapotungwa? Lakini pia inaweza kumaanisha kuwa Daudi aliamini kuwa mama yake alimzaa katika hali ya dhambi?


Kumbuka maneno haya- “Hatiani” Kama ilivyoaminika katika jamii yake kuwa mama yake alimzaa mtoto huyo kutokana na zinaa. Maandiko haya yenye uzito mkubwa na majonzi makubwa yanatusaidia kuelewa kitu fulani na kingine cha ziada katika maisha na mapito ya Daudi ambacho kinaweza vilevile kuhuisha maisha yetu kwa upya, Kwa msingi huo leo tutachukua muda kuweza kufanya uchunguzi wa kina sana na wa ndani zaidi kuhusu utata wa andiko hili na maana zake kwa kadiri ya mawazo mbalimbali ya wasomi wa Biblia na kwa kadiri ya neema kwa msaada wa Roho Mtakatifu mwalimu mkuu;-


Nani mwandishi wa Zaburi hii?


Ili andiko hili liweze kutafasirika vema jambo la kwanza ni lazima tuwe na uhakika wa mwandishi wa Zaburi hii, Mfano kama Zaburi hii imeandikwa na Sulemani na Sulemani labda ndiye aliyekuwa anatubu hapa kwa sababu zaburi hii ni zaburi ya toba ni zaburi ya kuomba rehema kwa Mungu unaweza kuona inavyoanza katika mstari ule wa kwanza hivi;- 

Zaburi 51:1-2 “Ee Mungu, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu.” 

Ni wazi kuwa mstari wa tano ungeweza kufikiriwa kuwa labda Sulemani anakumbuka historia ya kuzaliwa kwake, kupitia makosa ya Daudi kwa mama wa Sulemani ambaye ni Bathsheba mke wa Uria, Lakini maandiko yako wazi kuwa Bathsheba siye aliyekosea yeye alikosewa na adhabu ya Mungu ilianguka kwa mtoto wa kwanza ambaye Daudi alizaa na Bathsheba na ambaye alifariki mapema kama njia ya kutiwa nidhamu na Mungu, 

2Samuel 12:14 “Lakini, kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za Bwana nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atakayezaliwa kwako hakika yake atakufa. 

na kwa vile Uria aliyekuwa mume wa Bathsheba alikuwa amekwisha kuawa, na maandiko yako wazi kuwa Daudi alikuwa amemchukua Bathsheba kama mke wake sasa basi Sulemani anazaliwa kama mtoto halali wa Daudi kwa Bathsheba akitambuliwa na maandiko namna hii 

Mathayo 1:6 “Yese akamzaa mfalme Daudi. Daudi akamzaa Sulemani kwa yule mke wa Uria;” 

kimsingi hapa kosa lilikuwa la Daudi kuliko Bathsheba (japo wote wlifanya dhambi) na kama Zaburi hii ingekuwa ya Sulemani basi Mstari wa tano ungepaswa kusomaeka “Baba yangu alinitungisha mimba Hatiani” tukinena kiwazimu! Kwa msingi huo kwa namna fulani hatuoni wazi kuwa toba hii ni ya Sulemani, Lakini wote tunakubaliana wazi kuwa uchunguzi wa kimaandiko unaonyesha wazi kuwa zaburi hii ni miongoni mwa zaburi za toba na ni wazi kuwa iliandikwa na Daudi kwa kusudi la kutubia dhambi yake aliyoifanya kwa kumuingilia Mke wa Uria na pia kula njama za kumuua Uria na toba hii ilifanyika baada ya kukabiliwa na nabii Nathan ili Daudi arejee katika uhusiano wake na Mungu, Na kama hivyo ndivyo basi swala la msingi linabaki pale pale kwamba zaburi hii ni ya Daudi na maneno hayo ni toba ya Daudi na sio Sulemani, Sasa basi maneno yale “Mama yangu alinichukua Mimba hatiani!”  yana maana gani? Kwanini Daudi anayasema maneno hayo je alikuwa amamaanisha nini Hapa ziko dhana mbalimbali kuhusu maneno hayo:-


Mama yangu alinichukua Mimba hatiani!


1.       Mtazamo wa wayahudi: Kwa mujibu wa masimulizi ya Marabi, na maandishi ya kihistoria ya kiyahudi na tamaduni zao inaaminika kuwa maneno haya yalikuwa yakimaanisha kuwa Daudi alizaliwa nje ya ndoa yaani mama yake Daudi aliyeitwa NIZBETH alifanya zinaa kumpata mtoto huyo, swala hili liliaminika hivyo miongoni mwa Familia ya Yese, akiwemo Yese mwenyewe na kaka zake Daudi. Kwa hivyo kulikuweko na imani kwamba Daudi ni mwana wa haramu na wala sio mwana wa halali wa mzee Yese ona Zaburi 69:7-8 “Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu, Fedheha imenifunika uso wangu. Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, Na msikwao kwa wana wa mama yangu.” Maneno haya nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, kwa kiingereza “Stranger” katika Lugha ya kiibrania yanasomeka “MUZAR” yaani kwa kiingereza “Bastard” yaani mtoto asiye safi, mwana haramu!,  na neno lingine “Msikwao” kwa kiingereza “Alien” asiyetambulika yaani mwana wa mashaka, mgeni au mkimbizi, Kimsingi zaburi ya 69 kwa mujibu wa wanazuoni wa kiyahudi ni zaburi ya Daudi aliyoandika wakati wa maisha yake ya mapema akiwa kijana ikionyesha kuwa kijana huyu alikuwa na maumivu makali moyoni yanayotokana na mateso na kukataliwa kabisa, na ndugu zake wakiamini kuwa ni mwana wa haramu, na alichukiwa sana akihesabika kama sababu ya kusambaratika kwa familia na kudharaulika kwa mama yao. Zaburi ya 69 inafunua aina ya maisha magumu sana aliyopitia Daudi ya kukataliwa na kunyanyapaliwa na kudharauliwa na kila mtu aliyemuona inasemekana kuwa wakati wa maisha yake ya utotoni hadi ukubwani hakuwa na rafiki hata mmoja wa kumtia moyo alikuwa mtu wa kulaumiwa, kuaibishwa na kufedheheshwa tu, 

   Zaburi 69:19-20 “Wewe umejua kulaumiwa kwangu, Na kuaibika na kufedheheka kwangu, Mbele zako Wewe wako watesi wangu wote. Laumu imenivunja moyo, Nami ninaugua sana. Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna; Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu”.Zaburi hii ya 69 ilikuwa ni sauti ya mtu aliyeteseka mno, akidhalilishwa na kuaibishwa, Daudi alikuwa amezungukwa na Maadui wa ndani na nje katika jamii yake na wengi wakiwaza kumuua na wakati mwingine kitu kilipopotea alisingiziwa yeye na alilipishwa kwa nguvu ona  habari zake Zaburi 69:4 “Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua.Hiki kilikuwa kipindi kigumu sana katika maisha ya Daudi Zaburi ya 69 ni sauti ya mtu aliyelemewa na mzigo mzito sana na ni maombi ya ukombozi dhidi ya maisha ya mateso na Daudi inasemekana anayazungumza haya katika kipindi cha miaka 20-28 hivi cha maisha yake yaliyojawa na utata mwingi na kugubikwa na huzuni na kukataliwa.


Je nini sababu kubwa ya mateso haya ya Daudi nyumbani kwao?


Daudi alizaliwa katika familia ya Mzee Yese, Wayahudi wenyewe wanamuita Yishai, Mzee huyu alikuwa miongozi mwa wazee sabini waliokuwa wafanya sheria na waamuzi wa sheria za kiyahudi “Sanhedrin” yaani mahakama kuu ya Wayahudi, na alikuwa ni mtu aliyejipatia umaarufu mkubwa sana katika kizazi chake na katika mji wao Bethelehemu, inasemekana kuwa alikuwa mtu wa haki kiasi ambacho TALMUD (Shabbat 55b) imenukuu kuwa “Yese alikuwa mtu mwenye haki kiasi ambacho hakustahili kifo isipokuwa kwa sababu ya tatizo la Nyoka tu” yaani alikufa kwa sababu ya tatizo la Bustani ya Eden tu na tamko la Mungu kwa  Adam na Eva  kuwa watakufa siku watakapokula matunda waliyokatazwa, inasemekana kuwa hakuna dhambi wala hatia iliyowahi kuonekana ndani ya Mzee Yese.


Hata hivyo kulikuwa na tatizo moja kubwa sana katika familia ya Yese na hili ndilo lilopelekea Daudi kusema yeye amekuwa kama Mgeni kwa ndugu zake, Daudi hakuruhusiwa kula pamoja na familia yake, yeye aliwekewa chakula chake pembeni sana, alipewa kazi ngumu ya kuchunga kondoo sehemu yenye wanyama wakali kama Simba na Dubu ili yamkini ikiwezekana afie huko, Kwa hiyo Maisha ya Daudi ya ujanani yalikuwa maisha magumu mno na ni mtu mmoja tu aliyekuwa akiumizwa na maisha ya Daudi ambaye ni mama yake tu ambaye kukataliwa kwa mwanaye kulimjumuisha na yeye hata hivyo naye hakuwa na nguvu ya kuzuia kile alichotendewa yeye na mwanaye!, Daudi alihesabika kama mdudu tu na hakuna mtu alimhesabu kuwa kitu, alilaumiwa na watu na kufanyiwa dhihaka, kufyonywa na kuchekwa ona Zaburi 22:6-7 “Lakini mimi ni mdudu wala si mtu, Laumu ya wanadamu na mzaha wa watu. Wote wanionao hunicheka sana, Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao;” ukweli ni kuwa Daudi na mama yake Nizbeth walikuwa wakimuomba na kumsubiria Mungu awasaidie tu katika hali waliyokuwa wakiipitia wakati huu bado ilionekana kana kwamba Mungu amewaacha walikuwa wakimsubiria Mungu awaokoe na ukatili wa kifamilia uliokuwa ukiwakabili Zaburi 22:1-5 “Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha? Mbona U mbali na wokovu wangu, Na maneno ya kuugua kwangu?  Ee Mungu wangu, nalia mchana lakini hujibu Na wakati wa usiku lakini sipati raha. Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli. Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa. Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike.Haya yalikuwa maisha ya Daudi


NIZBETH ni nani hasa? Mwanamke huyu ni moja ya wanawake muhimu sana katika historia ya wayahudi, japo hatajwi katika maandiko lakini waebrania wanamuita Nitzevet Adael, kwa mujibu wa kitabu cha masimulizi ya Kiyahudi TALMUD mwanamke huyu ndie mama wa Mfalme Daudi na alikuwa na watoto tisa na wote alizaa na mzee Yese, watoto hao ni Eliabu, Abinadab, Shama, Nethaneel, Raddai, Ozem, Daudi, Seruiah na Abigaili.


Kwa mujibu wa masimulizi hayo ya kiyahudi ni Kwamba Mzee Yese ambaye wayahudi wanamuita Yishai  alikuwa ni mjukuu wa Boaz na Ruthu, baada ya miaka mingi sana ya ndoa yake yeye na Nizbeth na baada ya kuzaa watoto wa kiume kadhaa kabla ya kuzaliwa Daudi Mzee Yese alianza kuwa na mashaka kuhusu uzao wake hasa kwa sababu ya historia ya babu yake Boazi na Bibi yake Ruthu, kwamba ingawa Ruthu alikuwa amemuamini Mungu wa Israel lakini Ruthu alikuwa mmoabu hivyo kulikuwa na mashaka kama watoto waliozaliwa na huyu mmoabu wana haki ya kumtumikia Mungu wa Israel kama wayahudi wa asili? Japo Yese alikuwa mtu mkubwa lakini tafasiri za Torati kati yake na wenzake ziliwapa mashaka makubwa sana kama wajukuu wa Boazi yeye na wanawe wanaweza kuwa wenye kufaa kwa utumishi wa Mungu na utawala au ufanya sheria, hii ni kwa sababu wakati wana wa Israel wanatoka Misri wamoabu walisimama kikatili kinyume na Israel ili wasipite katika nchi yao na hivyo torati ya Musa ilikataza kabisa wana wa Israel wasioane na wamoabu ona::-


Kumbukumbu la Torati 23:2-3 “Mwana wa haramu asiingie katika mkutano wa Bwana; hata kizazi cha kumi asiingie aliye wake katika mkutano wa Bwana. Mwamoni wala Mmoabi wasiingie katika mkutano wa Bwana; wala hata kizazi cha kumi mtu wao asiingie katika mkutano wa Bwana milele;


Biblia ya kiingereza NIV inasomeka vema zaidi katika mistari hii Deuteronomy 23:2-3 “No one born of a FORBIDDEN MARRIAGE nor any of his descendants may enter the assembly of the LORD, even down to the tenth generation, No Ammonite or Moabite or any of his descendants may enter the assembly of The LORD even down to the tenth generation.


Kwa mujibu wa masimulizi ya Kiyahudi Boazi alipomuoa Ruthu alikuwa ni mfanya sheria na alikuwa na ufahamu kuhusu Sheria hii na labda angepata muda wa kufafanua kwa jamii kwa nini alioa mwanamke mmoabu na torati ilikataza? Je mwanaume akimuoa mwanamke wa Moabu ambaye amemuamini Mungu wa Israel je wanawe wataweza kuwa halali kuingia katika mkutano wa Bwana? Bahati mbaya inasemekana kuwa Boazi baada ya kumuoa Ruthu alikufa mara moja akimuacha mja mzito na kumzaa Obedi, Obedi yeye alimtumikia Mungu kwa Heshima kubwa na jina lake Obedi maana yake ni Mtumishi wa Mungu aliishi maisha ya haki sana na kuwa na heshima kubwa katika jamii jambo lililofanya akubalike katika jamii bila kujali kuwa mama yake alikuwa mmoabu, Hali kadhalika mwanaye yaani Yese naye aliishi maisha ya haki sana kiasi cha kukubalika na jamii ya Israel kuwa ni mwenye kufaa na watoto wake pia, hata hivyo  wakati wa maisha ya Yese kuliibuka mijadala mikubwa sana kuhusu Sheria ya Musa kwamba Israel wasioane na wamoabu na kuwa wamoabu wasiingie katika mkutano wa Bwana milele jambo hili lilimpa wasiwasi mkubwa sana Yese, jamii yake iliona kuwa Yese mwenye Damu ya kimoabu toka kwa bibi yake Ruthu na hata watoto wake wasingeweza tena kwa namna yoyote kuwa wenye kufaa kwa vile walijulikana kuwa na damu ya kimoabu kwa hivyo wametokana na ndoa zilizokatazwa na Torati ya Musa unaweza kuona! ushahidi wa maisha ya Daudi wakati wa mapambano na Sauli unathibitisha kwamba Daudi aliwakimbiza wazazi wake kwa mfalme wa Moabu ona 1Samuel 22:3-4 “Basi Daudi akaondoka huko, akakimbilia pango la Adulamu; na ndugu zake na watu wote wa mbari ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko. Na kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne. Kutoka huko Daudi akaenda Mispa ya Moabu; akamwambia mfalme wa Moabu, Tafadhali ukubali baba yangu na mama yangu watoke huko waliko, wakakae kwenu, hata nitakapojua Mungu atakalotenda kwa ajili yangu.  Akawaleta mbele ya mfalme wa Moabu, nao wakakaa pamoja naye wakati wote Daudi alipokuwa ngomeni.Inasemekana moja ya sababu ya familia hii ya Yese kwenda kujificha huko Moabu ni kwa sababu ya uhusiano wa Bibi yao Ruthu aliyetokea katika nchi ya Moabu


Kutokana na kuweko kwa mkanganyiko huo kuwa wayahudi wenye damu ya kimoabu wanafaa kuoana na wayahudi halisi au la? Yese na wanawe ni Wayahudi wenye asili ya kimoabu kutokana na babu yao Boazi kumuoa Ruth  aliyekuwa mwongofu wa kiyahudi kutoka moabu na mke wa Yese, Nizbeth alikuwa myahudi halisi wakati huu akiwa na watoto saba wa kiume na wawili wa kike, Daudi akiwa hajazaliwa wazee wa mji walimuamuru Yese aachane na Nizbeth na wala wasigusane tena!  Na kusiweko uhusiano tena kati ya Yese na Nizbeth, Hivyo familia ilikubaliana kuwa Yese na Nizbeth kuwa waachane (na kwa vile haukuwa ugomvi) waliachana katika hali ya upendo tu kwamba Nizbeth ambaye ni myahudi halisi asitende dhambi na myahudi mwenye damu ya kimoabu kwa hivyo Yese aliahidi kuwa atamtuza Nizbeth na kumlisha isipokuwa tu hakutakuwa na uhusiano wa kindoa ili kutunza heshima zao katika jamii!, watoto wote wakubwa wa Yese walifahamu utengano huo na walikubaliana. Jambo hili lilikubalika na Wazee ambao waliitwa “WAKETIO LANGONI” waketio langoni walikuwa ni wazee wa mji wenye kuheshimika kwa kufanya maamuzi ya kimahakama ona mfano Ruthu 4:1-12 “Basi Boazi akakwea kwenda mpaka langoni, akaketi pale; na tazama, yule mtu wa jamaa aliyekuwa karibu, ambaye Boazi amemnena, akapita. Naye akamwita, Haya! Wewe, karibu, uketi hapa. Naye akaja akaketi. Kisha akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, Ninyi nanyi, ketini hapa. Wakaketi. Kisha akamwambia yule jamaa, Huyu Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi aliyokuwa nayo ndugu yetu, Elimeleki; nami ilikuwa nia yangu nikujulishe wewe, na kukuambia, Uinunue mbele ya hawa waliopo na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya, uikomboe; lakini kama hutaikomboa, uniambie ili nijue mimi; kwa kuwa hakuna mtu wa kuikomboa ila wewe, na baada yako ni mimi. Naye akasema, Nitaikomboa mimi.  Ndipo Boazi aliposema, Siku ile utakapolinunua shamba mkononi mwa Naomi, unamnunua Ruthu pia, huyu Mmoabi, mkewe marehemu, ili makusudi umwinulie marehemu jina katika urithi wake. Basi yule jamaa aliyekuwa wa karibu akasema, Mimi sitaweza kulikomboa kwa nafsi yangu, nisije nikauharibu urithi wangu mwenyewe; basi haki yangu ya kulikomboa ujichukulie wewe, maana mimi sitaweza kulikomboa. Basi hii ilikuwa desturi zamani za kale katika Israeli, kwa habari ya kukomboa na kubadiliana, ili kuyahakikisha yote; mtu huvua kiatu chake na kumpa mwenziwe; ndivyo walivyohakikisha neno katika Israeli. Basi yule jamaa akamwambia Boazi, Wewe ujinunulie mwenyewe. Akavua kiatu chake. Naye Boazi akawaambia wale wazee na watu wote, Leo hivi ninyi ni mashahidi ya kwamba mimi nimenunua yote yaliyokuwa ya Elimeleki, na yote yaliyokuwa ya Kilioni na Maloni, mkononi mwa Naomi. Tena, huyu Ruthu Mmoabi, mkewe Maloni, nimemnunua awe mke wangu, makusudi nipate kumwinulia marehemu jina katika urithi wake, jina lake marehemu lisikatike miongoni mwa ndugu zake, wala langoni pa mji wake; leo hivi ninyi ni mashahidi.  Na watu wote waliokuwapo langoni, na wale wazee, wakasema, Naam, sisi ni mashahidi. Bwana na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wawili walioijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrata, na kuwa mashuhuri katika Bethlehemu. Nyumba yako na ifanane na nyumba yake Peresi, ambaye kwamba Tamari alimzalia Yuda, kwa wazao atakaokupa Bwana katika mwanamke huyu.” Unaona waketio Langoni walikuwa ni wazee wenye ujuzi wa torati waamuzi na ndio waliokuwa wakifanya maamuzi, kwa hiyo Langoni ilikuwa ni kama mahakamani, Hapo walipitisha kuwa Boazi amnunue Ruthu na kuwa mkewe kama jamaa aliye karibu, lakini kumbuka baadaye wazee waliokuweko katika kizazi za Yese ndio walioamua Yese aachane na Nizbeth na ndio vilevile walikuwa miongoni mwa watu waliomuona Daudi kama mtoto asiyefaa nao walishiriki kumsema vibaya ona Zaburi 69:10-12 “Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga, Ikawa laumu juu yangu. Nilipofanya gunia kuwa nguo zangu, Nikawa mithali kwao. Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki.Mtazamo wa wazee hao ilikuwa Yese na wanawe ingawa ni wema lakini wamezaliwa katika ndoa zilizokatazwa na torati ya Musa!


Baada ya miaka kadhaa kupita Yese alitamani tena kuwa na mtoto ambaye hatakuwa na maswali kuhusu asili yake kwamba asiwe mwamoni wala mmoabu, hivyo aliazimia kuanzisha uhusiano na mjakazi wa Nizbeth ambaye alikuwa mkanaani, Yese alimwambia mjakazi huyo maneno haya  “Kama nitakubalika kama Myahudi halali basi wewe utafaa kuwa mke halali uliyemuamini Mungu wa Israel kwa hiyo utaweza kunizalia mtoto halali asiye na lawama kwa vile haikubaliki kwa mtu mwenye damu ya mmoabu au mwamoni kuzaa na myahudi hivyo utakuwa huru wala hutakuwa mtumwa tena” Mjakazi huyo wa Nizbeth alielewa mpango huu wa Yese na alimueleza Nizbeth kwa vile alikuwa mwaminifu sana kwa bibi yake, Nizbeth alikuwa anapitia uchungu mkubwa sana wa kukaa hivihivi akiwa ametengwa na mumewe hivyo walikubaliana na mjakazi wake  kwamba usiku ule Yese atakapotaka kuingia kwako tafadhali uniache niingie mie kama Leah alivyofanyiwa na Raheli na mjakazi alikubali ombi la Nizbeth huku Yese akiwa hajui mpango huo, Nizbeth aliingia na kulala na mumewe na kwa bahati njema alipata ujauzito alitoka asubuhi na mapema kama ilivyo desturi za wakati huo na Yese hakujua kuwa alilala na mkewe halali Nizbeth (Ilikuwa desturi zamani katika jamii ya kiyahudi mwanamke kumuendea mwanaume wakati wa usiku na kuondoka asubuhi baada ya kumhudumia kwa tendo la ndoa) ona Ruthu3:1-14 “Kisha Naomi akamwambia mkwewe, Je! Mwanangu, si vizuri nikutafutie raha, ili upate mema? Basi na huyu Boazi, je! Siye wa mbari yetu, ambaye ulikuwapo pamoja na wasichana wake? Tazama, usiku wa leo atakuwa akipepeta shayiri pale ugani. Basi wewe oga, ujipake mafuta ujivike mavazi yako, kisha uende kwenye uga; walakini usijionyeshe kwake mtu yule, ila atakapokwisha kula na kunywa. Nayo itakuwa wakati atakapolala, utapaangalia mahali alalapo, nawe uingie, uifunue miguu yake ujilaze hapo; na yeye atakuambia utakalofanya. Akamwambia, Hayo yote unenayo mimi nitayafanya. Basi akashuka mpaka ugani; akafanya yote kama vile mkwewe alivyomwagiza. Ikawa huyo Boazi alipokwisha kula na kunywa, na moyo wake umekunjuka, alikwenda kulala penye mwisho wa chungu ya nafaka; na huyo mwanamke akaja taratibu, akaifunua miguu yake, akajilaza papo hapo. Na ikawa usiku wa manane yule mtu akasituka, akajigeuza; na kumbe! Yupo mwanamke amelala miguuni pake. Akasema, Ama! Ni nani wewe? Akamjibu, Ni mimi, Ruthu, mjakazi wako; uitande nguo yako juu ya mjakazi wako; kwa kuwa ndiwe wa jamaa aliye karibu. Akamwambia, Mwanangu, ubarikiwe na Bwana; umezidi kuonyesha fadhili zako mwisho kuliko mwanzo, kwa vile usivyowafuata vijana, kama ni maskini kama ni matajiri. Basi, mwanangu, usiogope; mimi nitakufanyia yote uyanenayo; kwa maana mji wote pia wa watu wangu wanakujua ya kwamba u mwanamke mwema.  Tena ndiyo kweli ya kuwa mimi ni wa jamaa yako aliye karibu; lakini kuna mtu wa jamaa aliye karibu kuliko mimi. Wewe ungoje usiku huu; kisha, asubuhi, kama akikubali kukufanyia impasavyo jamaa, haya, na akufanyie; lakini ikiwa hataki yeye, basi mimi nitakufanyia impasavyo jamaa; Bwana aishivyo. Ulale wewe hata asubuhi. Hivyo huyo mwanamke akalala miguuni pake hata asubuhi; akaondoka mapema asijaweza mtu kumtambua mwenziwe; maana Boazi amesema, Isijulikane kabisa ya kuwa mwanamke alifika penye uga.” Unaona kwa mujibu wa mila hii, Nizbeth alikwenda kulala na mumewe  na kuondoka asubuhi bila Yese kujua.


Baada ya miezi kama mitatu hivi ilibainika kuwa Nizbeth ana mimba, boma zima lilifahamu na watoto wake wakubwa walijua na mzee Yese pia alitambua kuwa Nizbeth ana mimba boma zima walikusudia apigwe mawe afe kwa sababu huenda mimba hiyo ameipata kwa uzinzi, Nizbeth hakutaka kabisa kuelezea namna alivyopata mimba hiyo kwa sababu alijua Yese atafadhaika sana na hakutaka kumuudhi, Nizbeth aliamua atakaa kimya tu! Aliweka nadhiri ya kukaa kimya mpaka Mungu mwenyewe alete haki, Yese akiwa hajui kabisa kuwa mimba hiyo imetokea vipi aliwaamuru watoto wake wasimuue Nizbeth wamuache aishi, lakini mtoto atakayezaliwa na ahesabike kama mtumwa tu na mwana wa haramu! Na asiruhusiwe kuoa Myahudi.


Tangu wakati huu hiki ndio kikawa chanzo kikubwa zaidi cha chuki dhidi ya Nizbeth na mwanaye Daudi, walichukiwa na jamii na kuhesabika kama watu wasiofaa na walioleta aibu kubwa sana katika familia ya Yese! Kijana huyu alianza kupitia maisha magumu na ya kukataliwa na jamii akihesabika kama mwana wa zinaa na mtoto wa dhambi!  Na mtumwa.  Alipelekwa kuchunga kondoo na kutokuhesabika kama sehemu ya familia ya Yese, habari zilienea Bethelehemu yote, na kama kitu kuilipotea alisingiziwa yeye na hata kulipishwa! Watu walisema mambo yote mema ya Boazi yamejulikana kwa Mwanae Yese na watoto wake saba lakini mambo mabaya ya kuoa Mmoabu ya Ruthu yamejulikana kupitia mtoto huyu mlaaniwa! Na ndio maana Daudi alikuwa akikaripiwa na nduguze na kuhesabika kama motto mwenye kiburi na anayestahili kushinda porini tu akiwachunga kondoo ona 1Samuel 17:12-28 “Basi Daudi alikuwa mwana wa yule Mwefrathi, wa Bethlehemu ya Yuda, aliyeitwa jina lake Yese; naye huyo alikuwa na wana wanane; na yeye mwenyewe alikuwa mzee siku za Sauli, na mkongwe miongoni mwa watu. Nao wale wana watatu wa Yese waliokuwa wakubwa walikuwa wamefuatana na Sauli kwenda vitani, na majina ya hao wanawe watatu waliokwenda vitani ni haya, mzaliwa wa kwanza Eliabu, na wa pili wake Abinadabu, na wa tatu Shama. Naye huyo Daudi alikuwa mdogo wa wote; na hao watatu waliokuwa wakubwa wakafuatana na Sauli.Basi Daudi alikuwa akienda kwa Sauli na kurudi ili awalishe kondoo za baba yake huko Bethlehemu.Naye yule Mfilisti hukaribia asubuhi na jioni, akajitokeza siku arobaini. Ndipo Yese akamwambia Daudi mwanawe, Haya! Sasa uwachukulie ndugu zako efa ya bisi, na mikate hii kumi, ipeleke upesi kambini kwa ndugu zako; ukampelekee akida wa elfu yao jibini hizi kumi, ukawaangalie, wa hali gani, kisha uniletee jawabu yao. Basi Sauli, na watu wote wa Israeli, walikuwa katika bonde la Ela, wakipigana na Wafilisti. Daudi akaondoka asubuhi na mapema, akawaacha kondoo pamoja na mchungaji, akavitwaa vitu vile, akaenda, kama Yese alivyomwamuru; akafika penye magari, wakati lile jeshi walipokuwa wakitoka kwenda kupigana, wakipiga kelele za vita. Nao Waisraeli na Wafilisti wakajipanga, jeshi hili likikabili jeshi hili. Basi Daudi akaviacha vile vyombo vyake katika mkono wa mlinda vyombo, akalikimbilia jeshi, akafika, akawasalimu ndugu zake. Hata alipokuwa akisema nao, kumbe! Yule shujaa alitokea, yule Mfilisti wa Gathi, jina lake Goliathi, akitoka katika jeshi la Wafilisti, akasema maneno yale yale; naye Daudi akayasikia. Na watu wote wa Israeli walipomwona yule mtu wakakimbia, wakaogopa sana. Watu wa Israeli wakasema, Je! Mmemwona mtu huyu aliyepanda huko? Hakika ametokea ili awatukane Israeli; basi, itakuwa, mtu yule atakayemwua, mfalme atamtajirisha kwa utajiri mwingi, naye atamwoza binti yake, na kuifanya mbari ya baba yake kuwa huru katika Israeli. Daudi akaongea na watu waliosimama karibu, akisema, Je! Atafanyiwaje yeye atakayemwua Mfilisti huyo, na kuwaondolea Israeli aibu hii? Maana Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai? Nao watu wakamjibu vivyo hivyo, wakisema, Ndivyo atakavyofanyiwa mtu yule atakayemwua. Naye Eliabu, mkubwa wake, alisikia hapo alipoongea na watu; na hasira yake Eliabu ikawaka juu ya Daudi, akasema, Mbona wewe umeshuka hapa? Na kondoo wale wachache umemwachia nani kule nyikani? Mimi nakujua kiburi chako, na ubaya wa moyo wako; maana umeshuka ili upate kuvitazama vita.”Unaweza kuona moyo wa kaka mkubwa dhidi ya Mdogo wake akimkemea Daudi na kumuona kama kiburi na mwenye moyo mbaya! haya ndio yalikuwa aina ya maisha ya Daudi, kutokana na kuzaliwa kwake kwa utata ilihesabika kama aliyezaliwa kwa zinaa ama kwa vile Nizbeth alikuwa amekiuka makubaliano na Yese na wazee.


Kwaajili ya haya Maisha ya Daudi yalikuwa ya kudharauliwa, kukataliwa, na kuhesabika kama mtu asiyefaa kitu au aliyelaaniwa, alilaumiwa kama mtu aliyesababisha kusambaratika kwa familia, alifedheheshwa na kuonekana kama mgeni na asiyetambulika au mkimbizi, Zaburi 69:7-8 “Maana kwa ajili yako nimestahimili laumu, Fedheha imenifunika uso wangu. Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, Na msikwao kwa wana wa mama yangu.” Sio tu kwa ndugu zake lakini hata jamii iliamini maneno ya ndugu wa Daudi na kufuata mfano wa familia yake Zaburi 69:10-12 “Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga, Ikawa laumu juu yangu. Nilipofanya gunia kuwa nguo zangu, Nikawa mithali kwao. Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki.Daudi aliishi maisha ya uchungu akimlilia Mungu kutokana na fedheha alizokutana nazo wakati wote ndugu zake walihakikisha kuwa wanampa uchungu kama chakula alifunga na kuomba na bado kwake ikawa kama ni swala la dhihaka Zaburi 69:17-21 “Wala usinifiche uso wako, mimi mtumishi wako, Maana mimi nimo taabuni, unijibu upesi. Uikaribie nafsi yangu, uikomboe, Kwa sababu ya adui zangu unifidie. Wewe umejua kulaumiwa kwangu, Na kuaibika na kufedheheka kwangu, Mbele zako Wewe wako watesi wangu wote. Laumu imenivunja moyo, Nami ninaugua sana. Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna; Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu. Wakanipa uchungu kuwa chakula changu; Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki.Licha ya mapito ya aina hii Daudi hakuruhusiwa kuikaribia nyumba ya Bwana wala kujihusisha na maswala ya ibada, yeye na mama yake walikuwa wakisubiri siku moja kweli itadhihirika kuhusu shutuma dhidi yake na mwanaye.


Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la Pembeni!


Habari za Daudi zinabadilika sasa baada ya Nabii Samuel kuamuriwa na Mungu aende Bethelehemu kwa kusudi la kumtia mafuta moja ya watoto wa Yese ambaye yeye Mungu atamuonyesha nabii Samuel ona 1Samuel 16:1-5 “Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi Bwana akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea Bwana dhabihu. Ukamwite Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako. Samweli akafanya hayo aliyosema Bwana, akaenda Bethlehemu. Wakaja wazee wa mji kumlaki, wakitetemeka, nao wakasema, Je! Umekuja kwa amani? Naye akasema, Naam, kwa amani; nimekuja kumtolea Bwana dhabihu; jitakaseni; njoni pamoja nami kwenye dhabihu. Akawatakasa Yese na wanawe, akawaita kwenye dhabihu.”



Maandiko yanaonyesha kuwa Samuel alipofika Bethelehemu wazee wa mji walikwenda kumlaki na kumsalimu na huku wakitetemeka, wote waliogopa na hofu hii haikuwa ya kawaida walihisi ujio huu wa nabii sio ujio wa kawaida hivyo walimuuliza kama amekuja kwa amani kwa mujibu wa maelezo ya marabi ni kuwa waliogopa kuwa huenda Samuel amesikia au kujulishwa dhambi yao dhidi ya kijana Daudi na labda amekuja kuwakemea vikali tabia yao na ile hali ya kumtesa kijana aliyeachwa machungani, Samuel aliwahakikishia kuwa amekuja kwa amani, na aliwataka wazee na Yese na wanae wajiunge katika ibada ya kumtolea Mungu dhabihu, Kama mzee aliyeheshimika ilikuwa ni kawaida kwa Yese kualikwa, Lakini wanae walipoalikwa hili lilikuwa jambo la kushitua kidogo, waliogopa kuwa mm huenda wamekosea sana kuwatenga watoto wa Yese na walijua kuwa labda Samuel atawakemea hadharani na kumbe Samuel alikuwa amefunuliwa kuwa Mfalme mpya ajaye ni mwana wa Yese na mbaya zaidi alikuwa ni Yule aliyekataliwa  na tena wala hakuletwa katika ibada hii ikifikiriwa kuwa hakuwa mwenye kufaa!


Swali la Samuel lilikuwa la kinabii, Mungu sio tu alimtuma kuchagua mfalme ajaye bali pia kuponya Moyo wa Nizbeth na mwanaye aliyekataliwa na jamii yake lakini pia kuuweka sawa moyo wa Yese na wazee kuwa machoni pa Mungu Yule mtoto alikuwa ni halali kwa Yese na Nezbeth na kuwa watoto wote wa Yese na Yese mwenyewe walikubaliwa na Mungu. Na wanastahili kumtumikia Mungu na kukaribia mkutano wa watu wa Mungu kama ilivyo kwa wayahudi wengine.


Swali Baada ya wana wote wa Yese kupitishwa mbele ya Samuel, Samuel alimwambia Yese Bwana hakuwachagua hawa kisha akamuuliza “Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa?  hapa ndipo palikuwa mahali pagumu sana kwa Yese kwa taarifa yako kwa vile alikuwa anaamini kuwa hawa ndio watoto wake wote angejibu tu kuwa ndio wote wapo hapa lakini ona “Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo” Daudi alikuwa hakubaliki na baba yake Yese alidhani kuwa mawazo ya Mungu na Samuel yatakuwa kama yake na kuwa atakubali kijana huyo abaki huko huko porini tu Lakini Samuel aliagiza aletwe mara moja na kuwa hakuna kitakachoendelea mpaka aje, kwaajili ya kumuheshimu nabii walitumwa wajumbe akamlete kijana huyo!


Inawezekana kwamba kila mmoja alishangaa tukio lile na huenda hata Samuel hakuweza kuamini kama huyu anaweza kuwa mtiwa mafuta sauti ya Mungu ikamwambia Samuel “Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye.Baada ya Samuel kumtia mafuta Sauti ya Nizbeth iliisikika ikipiga kelele za furaha kumbuka ni yeye pekee aliyekuwa akimuunga mkono mwanaye na pekee ndiye aliyekuwa faraja miaka 28 ya kuteseka kwake na ukimya wake wakikabiliwa na lawama sasa unafikia mwisho kwa Mungu kuingilia kati na kuthibitisha kuwa mtoto alikuwa na haki na mama yake alikuwa na haki na alikuwa mtoto halisi wa Yese! Na huu ukawa ndio mwisho wa mateso ya Nizbeth na mwanaye Daudi wakifurahi Nizbeth na Daudi waliimba Zaburi ya 118 na Mstari wa 22-23 wanasema maneno mazito Zaburi 118:22-23 “Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni.Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu.” Ilishangaza kuwa kijana aliyekataliwa na mji mzima ndiye Masihi wa bwana ndiye mpakwa mafuta ndiye mfalme ajaye! Wao walikuwa wamemkataa Daudi na Bwana alikuwa amemchagua Daudi, uchaguzi wa Daudi ulitoka kwa Mungu na ukawa ajabu kubwa sana machoni pa kila mmoja!


Kuna maswala mengi sana kuhusiana na habari hizi za siri katika maisha ya Daudi na familia yake lakini kama taarifa hizo zina ukweli na Yese na familia yake waliamini hivyo ndio maana na Daudi anayasema hayo kama taarifa ambayo ilienea katika jamii Zaburi 51:5 “Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani Mstari huu umekuwa mgumu kutafasirika kwa sababu tu wayahudi hawakuwa na hawaamini katika dhambi ya asili na Daudi alipata ufunuo mdogo sana kuhusu asili ya dhambi na ndio maana tafasiri ya maandiko hayo katika mtazamo wa agano jipya ni rahisi kuliko mtazamo wa kiyahudi! hata hivyo kwa kuwa mama wa Daudi Nizbeth na mjakazi wake walikuwa na uelewa kuhusu jambo hili Daudi alifahamu pia kupitia wao kwa upande mwingine kwamba habari zile kwamba amezaliwa kwa zinaa sio za kweli, hivyo alionewa kwa sababu isiyo kweli ona  Zaburi 69:4 “Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua.” na zilikuwa ni shutuma tu katika jamii yake na Mungu alilimaliza swala lile kupitia nabii Samuel na kutiwa mafuta kwa Daudi kama mwana wa Yese!.


Mapito haya ya Daudi kinabii pia yanatoa picha ya kile kilichokuwa kinaendelea katika familia ya Yusufu na Mariam, Mambo mengi yaliyompata Daudi yalikuwa ni unabii, yanatabiri jinsi mwanae yaani Masihi atakayoyapitia, Biblia haijaeleza kila kitu lakini kuna ukweli kuwa Yesu hakukubalika na Ndugu zake, Hata ingawa Mungu aliweka wazi kwa Yusufu kuwa mkewe alipata Mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, ni wazi kuwa katika jamii jambo hilo halikuweza kukubalika kama unavyoweza kufikiri Biblia inaonyesha kuwa ndugu wa Yesu Kristo walikuja kumkubali baadaye kama iliyokuwa kwa Daudi,  wao hawakumuamini kama masihi na ni Mariamu pekee ndiye aliyekuwa na uelewa kuwa Yesu ni mtoto wa namna gani kama ambavyo Nezbeth alivyomuelewa Daudi Yohana 7:1-5 “Na baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Uyahudi, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitafuta kumwua. Na sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya Vibanda, ilikuwa karibu. Basi ndugu zake wakamwambia, Ondoka hapa, uende Uyahudi, wanafunzi wako nao wapate kuzitazama kazi zako unazozifanya. Kwa maana hakuna mtu afanyaye neno kwa siri, naye mwenyewe ataka kujulikana. Ukifanya mambo haya, basi jidhihirishe kwa ulimwengu. Maana hata nduguze hawakumwamini.” Aidha watu wengine pia hawakuamini kuwa Yesu alizaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na ili kumkatisha tamaa adui zake waliwahi kumjibu kuwa wao hawakuzaliwa kwa zinaa ona Yohana 8:41 “Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu. Ndipo walipomwambia, Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu.” Unaweza kuona kwa ufupi mapito aliyopitia Daudi kinabii yalimtokea Yesu Kristo! Daudi anaposema mama yangu alinichukua Mimba hatiani wakati huu hakukuwa na ufunuo wa mwanadamu kuwa na asili ya dhambi, kwa hivyo watafasiri wengi wa biblia wakiwemo marabi, walikuwa wanafikri kuwa Daudi alikuwa akiizungumzia hali ya maneno yaliyoenea katika jamii yaje kuwa mama yake alimchukua mimba hatiani, na kama yalikuwa ni mapatano na Yese kuwa wasikutane ni dhahiri kuwa Nizbeth alifanya makosa kuchukua mimba na Yese nje ya mapatano na amri ya wazee, lakini kama mke halali wa Yese mama huyu ni shujaa wa imani kwani kupitia tendo hili, alivishinda vita vya kishetani vya kupamaba na uzao wa Masihi.


Sasa basi Daudi alikuwa na maana gani kusema mama yangu alinichukua Mimba hatiani kama tunaona kuwa Daudi ni mwana halali wa Yese hapa kuna mawazo mbalimbali kuhusu tafasiri za mstari huu ukiacha masimulizi ya Kiyahudi:-


2.       Asili ya dhambi: Mstari huu pia unaweza kumaanisha kuwa watoto wachanga wanazaliwa wakiwa na dhambi ya asili, kwamba tendo la Daudi kufanya dhambi, licha ya kuwa ni mtu aliyeupendeza moyo wa Mungu na bado alikuwa analenga kumpendeza Mungu na kamwe hakwepi ule wajibu wa kuwa anawajibika kwa Mungu kwa dhambi aliyoitenda lakini anapata utambuzi kuwa ameumbwa katika hali hiyo na sio kwaajili ya Muumba mwenyewe lakini kwa kurithi, kwa damu, tangu alipokuwa akitungishwa mimba au tangu mama yake anapokea ujauzito kuhusu yeye tayari alikuwa na dhambi ya asili inayotokana na uwepo wa dhambi kwa baba yetu Adamu Ezekiel 16:4 . “Na katika habari za kuzaliwa kwako, siku ile uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa, wala hukuoshwa kwa maji usafishwe; hukutiwa chumvi hata kidogo, wala hukutiwa katika nguo kabisa.Ezekiel anazungumzia kitovu cha kiroho japo kila mtoto anapozaliwa anakatwa kitovu, lakini kuna kitovu cha rohoni kinachotuunga kurithi maswala kadhaa kutoka kwa baba zetu kwa hiyo sisi tumefanya dhambi tangu tukiwa viunoni mwa baba yetu Adamu kama vile maandiko yanavyotufundisha kuwa Lawi alitoa zaka wakati Abraham anatoa zaka kwa Melkizedeki kwa vile alikuwa katika viuno vyake ona Waebrania 7:9-10 “Tena yaweza kusemwa ya kuwa, kwa njia ya Ibrahimu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya kumi; kwa maana alikuwa katika viuno vya baba yake, hapo Melkizedeki alipokutana naye.Kwa hivyo watoto wanarithi hatia kutoka kwa wazazi wao, na wanashiriki mema kutoka kwa wazazi wao kitendo cha Abrahamu kutoa zaka kinahesabika kibiblia kuwa Lawi naye alitoa zaka hata kabla ya kuzaliwa kwa vile alikuwa viunoni mwa baba yake na ndio maana watoto vilevile hufa kwa sababu mshahara wa dhambi ni mauti ona Warumi 6:23 “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Urithi wa kifo umetokana na urithi wa dhambi  na vyote hivi tumevirithi kutoka kwa Adamu baba yetu kwa msingi huo wanadamu wote ni wenye dhambi isipokuwa Yesu Kristo pekee, sasa basi Daudi anapotubia kosa lake anaakisi asili yake ya dhambi kwa kusema Tazama mimi naliumbwa katika hali ya uovu, mama yangu alinichukua mimba hatiani, akimaanisha kuwa alikuwa mwenye dhambi tangu inatungishwa mimba, kama vile adui alivyopanda magugu kwenye ngano mapema kabla havijaanza kuota na hii ilikuwa moja ya dhana ya kiyahudi pia kwamba mwanadamu huzaliwa katika hali ya dhambi Yohana 9:34 “Wakajibu, wakamwambia, Ama! Wewe ulizaliwa katika dhambi tupu, nawe unatufundisha sisi? Wakamtoa nje.” Hii inaweza kuwa tafasiri nzuri ya andiko hilo kwa mtazamo wa kikristo, japo katika agano la kale mtazamo huu na kwa wayahudi ulikuwa haujafunuliwa wazi.


3.        Mwenye dhambi kwa kuzaliwa: Daudi hapa ni kama anatambua kuwa yeye sio mwenye dhambi tu kwa kuzitenda lakini pia ni mwenye dhambi kwa kuzaliwa au kwa asili, Paulo mtume aliliambia kanisa la warumi kwamba Warumi 5:12 “Lakini karama ile haikuwa kama lile kosa; kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi.” Wala Daudi hakumaanisha kuwa tendo la ndoa katika ndoa ni dhambi, au mimba iliyotungwa kwa wazazi wake halali ilikuwa kosa lakini alikuwa na wazo kuwa mwanadamu ana asili ya uharibifu tu, Kama jinsi ambavyo mwembe huzaa mwembe, Mwanadamu hufanya dhambi kwa sababu ni mwenye dhambi kwa asili Warumi 3:10-12, 23 ”kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja., kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;Kwa msingi huo kwa vile wanadamu wote ni wenye dhambi kwa asili na kwa kuzitenda, hatuwezi kuingia katika ufalme wa Mungu bila kupokea asili mpya kwa neema ya Yesu Kristo na ndio maana pamoja na dua yake Daudi alijiombea moyo safi na kuumbwa upya kwa roho yake ona Zaburi 51:10-11 ”Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.” Wakati huu kazi za Kristo na Roho Mtakatifu zilikuwa sio dhahiri sana Lakini Daudi alikuwa na hisia za kinabii za kutamani kuzaliwa mara ya pili ili asili yake ya dhambi iweze kudhoofishwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu na kufanywa upya Yohana 3; 4-7 “Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.Mungu anapoingilia kati na kudhoofisha asili ya dhambi ndipo tunapata neema ya kuwa washirika wa tabia ya uungu ndani yetu 2Petro 1:4 “Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa.” Bila neema ya Mungu na uwezo war oho Mtakatifu kuingilia kati na kudhoofisha nguvu ya asili ndani yetu hatuwezi kuchagua kutokuitenda dhambi, isipokuwa kwa msada wa Mungu.


4.       Dhana ya tangu ujana au utoto: Daudi alikuwa kwenye maombi binafsi na toba yake kwa Mungu alikuwa ameelewa kuwa amemkosea Mungu na wala hakuwa anatafuta kujitetea kwa Mungu wake wala kusingizia dhambi yake kwa wazazi wake wala kujihesabia haki, Ezekiel 18:20 “Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake.” Daudi alikuwa anataka kuikamilisha toba yake kwamba sio tu nimekutenda dhambi binafsi, lakini kwa asili mimi ni mwenye dhambi, Matendo ya maisha yangu yameathiriwa tangu namna ya kuumbwa kwangu na hata kuzaliwa kwangu, Mama yangu alinichukua mimba hatiani, hamaaniishi anataka kumshutumu mama yake yeye alikuwa akijianika kwa Mungu na kumueleza Mungu mtazamo wake kwamba anastahili kuwa chombo cha hasira ya Mungu,  lakini zaidi sana anahitaji rehema, zaidi ya dhambi aliyoifanya lakini hata na tangu kuzaliwa kwake na kuumbika kwake ndani ya tumbo la mama yake. Mzizi wake wa dhambi unatoka mbali. Daudi anakubali kuwajibika kwa dhambi yake wala hamtwishi awaye yote maovu yake, kuumbwa katika hali ya uovu kwake pia haimaanishi kuwa anamlaumu Mungu muumba bali yeye anakubali kuwa mwanadamu kwaasili ni muovu, wayahudi wakati mwingine walitumia neno ujana, wakimaanisha vievile hatua za ukuaji kutoka mwaka 0-28 miaka ya ujana kwa hiyo walikuwa na semi kama mwanadamu ameharibika tangu ujana wake wakiwa na maana tangu mtu anajua mema na mabaya ona kwa mfano au tangu anaanza maisha Mwanzo 8:21 “BWANA akasikia harufu ya kumridhisha; BWANA akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu UJANA wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya.” Ona pia Yeremia 3:25 “Na tulale kwa aibu yetu, haya yetu na itufunike; kwa maana tumemwasi Bwana, Mungu wetu, sisi na baba zetu, tangu UJANA wetu hata leo; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu.” Isaya 7:15 “Siagi na asali atakula, wakati ajuapo kuyakataa mabaya na kuyachagua mema.” Waebrania walikuwa na dhana kuwa mwanadamu huanza kuhesabiwa haki wakati wa ujana wake yaani wakati ajuapo kutenda mema au mabaya Lakini Daudi anaona kuwa tangu mimba inapotungwa tayari hali ya kutenda tusiyoyataka inampata mwanadamu.

5.       Lugha ya kimashairi


Wengine hudhani kuwa Zaburi 51:5 ni Lugha ya kishairi tu ya kukuza mambo “hyperbole” Daudi alikuwa anatubu dhambi na kuikiri dhambi aliyokuwa ameifanya mbele za Mungu na kati kati ya toba yake  anajutia na kujikuza kuwa yeye ni mwenye dhambi zaidi ya kawaida na kuwa amekuwa mwenye dhambi kwa asili tangu kutungishwa mimba, Kwa hiyo wataalamu wa kimaandiko hufikiri kuwa ni lugha tu ya kishairi kama vile mtu anavyoweza kusema analowesha kitanda chake kwa machozi Zaburi 6:6 “Nimechoka kwa kuugua kwangu; Kila usiku nakieleza kitanda changu; Nalilowesha godoro langu kwa machozi yangu au kama vile Paulo anavyodai kuwa Mungu alikuja kuwaokoa wenye dhambi na wa kwanza wao ni mimi 1Timotheo 1:15  Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi.”   

         
6.       Lugha tu!


Wakati mwingine Lugha tu inaweza kusababisha mstari uweze kuwa mgumu kutafasirika kwa msingi huo tunapoangalia lugha zilizotumika katika Biblia mbalimbalia utaweza kugundua kuwa lugha iliyotumika hapo imefanywa kuwa ngumu na baadhi ya tafasiri za biblia na baadhi zimeifanya kuwa rahisi kwa Mfano:-

NIV Psalm 51:5 “Surely I was sinful at Birth, sinful from time my mother conceived me “Kwa hakika nalikuwa mwenye dhambi tangu kuzaliwa, mwenye dhambi tangu mama yangu anatunga ujauzito”

KJV Psalm 51:5 “Behold I was shapen in iniquity, and in sin did my mother conceive me” Tazama nimeumbwa katika hali ya uovu, na katika hali ya dhambi mama yangu alinipokea”

ESV.Psalm 51:5 “Behold I was brought forth in iniquity, and in sin did my mother conceive me” Tazama naliletwa katika hali ya uovu na katika hali ya dhambi mama yangu alinipokea

NLT Psalm 51:5 “For I was born a sinner,Yes from the moment my mother conceived me” Kwa dhambi nalizaliwa ndio tangu wakati mama yangu ananipokea”

SUV Zaburi 51:5 ““Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatiani

Tunajifunza kwamba wakati mwingine ili andiko liweze kuekleweka vema tunaweza kupitia tafasiri mbalimbali za kimaandiko na tukapata maana iliyokusudiwa kwa njia rahisi, na kifungu au mstari ukawa ni mwepesi kueleweka.


7.       Tamaa ya mama

Kwa mujibu wa uchunguzi wa ndani zaidi wa kimaandiko wenye lengo la kuuangalia mstari huu bila kuwa na mtazamo wa Kikrito wa kuwa mwanadamu ni mwenye dhambi kwa asili, unapoangalia Lugha zilizotumika hapa ni wazi kuwa Daudi hamaanishi dhambi kutoka kwa Adamu, bali anamaanisha dhambi ya mama yake, yaani kuwa mama yangu alinichukua mimba hatiani, bila kuweka mtazamo wa Kikristo unapochunguza maneno yaliyotumiwa na Daudi katika Mstari huu kuhusu mama yake kumchukua mimba hatiani kwa kawaida kwa waebrania neno kushika mimba au kuchukua mimba linatumika neno “HARAH” ambalo linamaanisha kuwa mwanamke ameshika mimba, sasa katika kifungu hiki Daudi anatumia neno “YACHAN” ambalo neno hili ni baya sana kutumika kwa mwanadamu neno hili linamaanisha kushika mimba katika tama ya kinyama yaani kama vile kondoo au Mbuzi ama Ngombe anavyopandisha joto akiwa anataka kupata ujauzito ndio hali inayoitumia Daudi kwa mama yake kuwa mjamzito, kwa hiyo huenda Daudi anamaanisha ile tama ya mama yake ya kutaka kupokea ujauzito ilikuwa ni tama kama ya mnyama mwenye joto, kwa hiyo Daudi anapotumia neno YACHAN anatumia neno gumu sana kuonyesha kwamba alizaliwa akiwa na hali ya tama na mama yake alimchukua mimba katika hali ya tama ambayo ni tama kama ile ya mnyama kwa hiyo mimba ya daudi ilipatikana kama matokeo ya tama ya mama yake iliyokuwa kama ya mnyama na huenda kwa tamaa kama ile ya Nizbeth naye alifanya unyama kumkabili mke wa Uria, Hivyo basi kama Nizbeth hakufanya zinaa kumpata Daudi, alimpata kwa kuvunja patano alilowekewa, alimpata kama matokeo ya tama kali ya mama yake Zaburi 51:5 ““Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatianihuu unaweza kuwa Mtazamo sahihi wa andiko hili kama hatutaweka fundisho la mwanadamu kuzaliwa akiwa na asili ya dhambi, lakini bado tunaona urithi wa aina ileile ya asili ya dhambi kwamba kama kulikuwa na tamaa ya kinyama kwa Nizbeth, Mwanae naye aliipata kwa Nizbeth na kama hivyo ndiyo ni tama ileile ya Eva kutamani lile tunda katika bustani ya edeni 


Hitimisho!


Ni muhimu kukubali kuwa Mstari huu ni mstari wa Msingi sana na dhana zote zinazotolewa na wanatheolojia kuhusu Mstari huu ni za msingi sana, zote zinatusaidia kufikiri vema na kujifunza vema neno la Mungu, Nimefurahia mtazamo wa kiyahudi kuhusu mstari huu kwa sababu ziko kweli kadhaa kuwa kuna mambo tulikuwa hatuyafahamu kuhusu maisha ya Daudi, sasa tunaweza kuisoma zaburi katika mtazamo mpana mno na kuelewa maumivu aliyoyapitia kijana huyu, lakini vilevile kinabii tunapata picha ya wazi kuhusu kile alichokipitia Mariamu na Mwanaye Yesu Kristo, kwamba kinafanana kwa ukaribu na kile kilichompata Daudi na Nizbeth!


Lakini ninaporejea sasa katikamstari wa msingi wa Zaburi 51:5 Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; Mama yangu alinichukua mimba hatianinaweza kuhitimisha kwa kusema haya Daudi hamaanishi kuwa Tendo la ndoa katika ndoa halali ni dhambi, wala hamaanishi kwamba kutungishwa mimba kwa mama yake na baba yake ni dhambi, Daudi aliwaheshimu sana Wazazi wake na kuwatunza na amani iliporeja nyumbani kwao ni yeye ndiye aliyewapeleka na kuwatunza kwa mfalme wa Moabu ona 1Samuel 22:3-4. “Kutoka huko Daudi akaenda Mispa ya Moabu; akamwambia mfalme wa Moabu, Tafadhali ukubali BABA YANGU NA MAMA YANGU watoke huko waliko, wakakae kwenu, hata nitakapojua Mungu atakalotenda kwa ajili yangu. Akawaleta mbele ya mfalme wa Moabu, nao wakakaa pamoja naye wakati wote Daudi alipokuwa ngomeni.” Ni wazi kuwa kama kulikuwa na utata uliisha baada ya Samuel Nabii kumaliza tatizo, Kwa hiyo ni dhahiri Mungu alitambua kuwa Yese na Nezbeth walikuwa wazazi halali wa Daudi na mapito yalikuwa ya kinabii tu, Daudi aliwaheshimu baba yake na mama yake na aliwatunza na kuhakikisha wako salama, Daudi hamaanishi kuwa alizaliwa kwa zinaa, kama mama yake alikwenda kwa mumewe usiku na kupata ujauzito bado ilikuwa ni ndoa halali, na iliathiriwa tu na utafutaji wa kweli za uchambuzi wa torati, tendo la Ndoa ni takatifu na ni zawadi ya Mungu na Mungu ameamuru kuwa ndoa na ziheshimiwe Waebrania 13:4, Zaburi 51:5 ni wazi kabisa kuwa kwa mtazamo na ufunuo wa kiagano jipya unamaanisha kuwa kwa kuwa sisi ni watoto wa Adamu tunazaliwa na hali Fulani ndani yetu inayotusukuma kuasi hata wakati mwingine mioyo yetu ikiwa haipendi, kwa hiyo kwa bidii ya kibinadamu hatuwezi kamwe kuishinda dhambi bila msaada wa kiungu Warumi 7:21-24 “Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya. Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu.Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?  Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.” Kwa ufunuo Fulani Daudi aliishia kusema aliumbwa katika hali ya uovu na alichukuliwa mimba hatiani, lakini ni wazi alikuwa ni kama mtu anayejiuliza ilikuwaje hata akatenda uovu ule mkubwa mtu ambaye moyo wake siku zote ulikuwa unalenga kumpendeza Mungu, kwa hiyo Daudi ni kama alitaka kusema hili anachokisema Paulo Mtume kuwa iko sheria ndani yetu ambayo inapingana na lile jema unalotaka kulitenda  na ni kwa msaada wa Roho Mtakatifu tu na Kazi aliyoifanya Yesu msalabani tutaweza kuwa huru kutoka katika vita vyetu vya asili vinavyotupinga ndani kwa ndani kama nguvu ya “gravitation force” ama nia ya mwili Warumi 7:24-25 “Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.” Na Warumi 8:1-3 “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti. Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili;
               
Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima
0718990796

Maoni 9 :

  1. Mungu akubariki sana Mtumishi wa Jehovah. Kwa kweli huu mstari wa Zaburi 55:5 zaburi ya Daudi ulikuwa unanifikirisha sana, ila leo nimesoma na nimeelewa vizuri mno. Namtukuza sana Mungu kwa ajili yako jinsi alivyoweka shule hii kwenye ufahamu wako, hapa nilikuwa darasani na nimekupata vizuri. UBARIKIWE SANA NA YESU

    JibuFuta
  2. Mungu wa mbinguni akubariki

    JibuFuta
  3. Mungu wa mbinguni akubariki Sana
    Na kukuongeza viwango vya nguvu ya kiroho

    JibuFuta
  4. Amen Amen 🙏🙏🙏
    MUNGU akubariki sana Mtumishi wa BWANA.

    JibuFuta
  5. MUNGU AKUBARIKI SANA ZABURI YA55:5 ILIKUWA INANICHANGANYA SANA.

    JibuFuta
  6. Mungu akubariki kwa kazi nzuri

    JibuFuta
  7. Kazi nzuri inapendeza kusoma, napenda xana historia za bibilia

    JibuFuta
  8. Napenda xana

    JibuFuta
  9. Dah mm naxhukuru xana kwa kupata elimu hii pia na mungu akuweke xana na kukupa upeo zaidi ili tupate vingi kupitaia ww mtumixhi maana ni elimu kubwa xana hii na bila roho wa mungu huwez ijua

    JibuFuta