Jumanne, 16 Juni 2020

Hata nikamtwaa kuwa mke wangu?


Mwanzo 12:18-19 “Ndipo Farao akamwita Abramu, akasema, N'nini hili ulilonitendea? Mbona hukuniambia ya kuwa huyo ni mkeo? Mbona ulisema, Huyo ni umbu langu, hata nikamtwaa kuwa mke wangu? Basi sasa, huyo mke wako umchukue, uende zako





Utangulizi:


Mojawapo ya Habari za kibiblia ambazo zinazua maswali mengi kwa wanafunzi wa Biblia ni Pamoja na habari ya Abrahamu na Sara Kushuka Misri, kwaajili ya kujihami na njaa iliyotokea katika inchi ya kanaani, wote tunakubaliana kuwa tunaifahamu habari hii, lakini kama wanafunzi wa Biblia tunapoisoma habari hii kuna maswali kadhaa wa kadhaa yanayoibuka kutokana na kisa hiki, mengine yakiwa na majibu na mengine yakituacha katika hali ya utata, Ndio kuna maswali mengi tunaweza kujiuliza mfano, Sara aliyekuwa na miaka 65 wakati huu na bado anaonekana alikuwa mzuri sana kiasi cha kuhatarisha maisha ya Abrahamu?, hii inaweza kukustaajabisha, lakini sio hivyo tu  Abrahamu aliyekuwa baba wa Imani na mtu wa haki anawezaje kusema Uongo? Je alidanganya au alisema ukweli? Aliposema Sara ni dada yangu huku akiwa ni mke wake?, lakini sio hivyo tu anawezaje kumuachia mkewe kirahisi achukuliwe na mtu mwingine?, sio hivyo tu kwa nini swala hili lilijirudia kama mara tatu katika kitabu cha Mwanzo, na nini tunajifunza kutokana na habari ya Sara na Abrahamu kushuka Misri? Lakini swali kubwa na makini zaidi Je Farao alifanikiwa kumfanya Sara kama mke wake? Hili ndio swali zito zaidi kuliko mengine tunapotafakari kitu cha kujifunza!. Kwanza tupate habari kamili:-

Mwanzo 12:10-20 “Basi kulikuwa njaa katika nchi ile; Abramu akashuka Misri, akae huko kwa muda maana njaa ilikuwa nzito katika nchi. Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso; basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai. Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako. Basi ikawa Abramu alipofika Misri, Wamisri wakamwona huyo mwanamke ya kwamba yeye ni mzuri sana. Wakuu wa Farao wakamwona, nao wakamsifu kwa Farao; basi yule mwanamke akachukuliwa nyumbani mwa Farao. Naye akamtendea Abramu mema kwa ajili yake; naye alikuwa na kondoo na ng'ombe, na punda waume, na watumwa, na wajakazi, na punda wake, na ngamia.  Lakini BWANA akampiga Farao na nyumba yake mapigo makuu, kwa ajili ya Sarai, mkewe Abramu. Ndipo Farao akamwita Abramu, akasema, N'nini hili ulilonitendea? Mbona hukuniambia ya kuwa huyo ni mkeo? Mbona ulisema, Huyo ni umbu langu, hata nikamtwaa kuwa mke wangu? Basi sasa, huyo mke wako umchukue, uende zako. Farao akawaagiza watu kwa ajili yake, wakampeleka njiani, na mkewe, na kila alichokuwa nacho.”


Kushuka Misri kwa sababu ya Njaa.


Biblia iko wazi kuwa wakati huu sio kuwa Abrahamu alikuwa ameacha kumuamini Mungu hapana, Yeye alikuwa ameshuka Misri kwa sababu ya njaa kali iliyotokea katika nchi ya Kanaani Mwanzo 12:10 “Basi kulikuwa njaa katika nchi ile; Abramu akashuka Misri, akae huko kwa muda maana njaa ilikuwa nzito katika nchi.Ukame wa muda mrefu ulikuwa umeendelea katika mashariki ya kati nyakati za Abrahamu na kuathiri maeneo yote yanayotegema mvua, athari ziliwapata wakulima pamoja na wafugaji pia kwahiyo kwaajili ya mifugo na mahitaji ya chakula Abrahamu aliona vema kwenda Misri na maandiko yako wazi kuwa alikuwa akae kwa muda kwa sababu ya njaa, Lakini pia wote tunakubaliana kuwa Misri tangu miaka mingi walikuwa wanatumia kilimo cha umwagiliaji kutokana na kuwepo kwa bonde la Mto Nile hali kadhalika inawezekana jamii za wafugaji waliteremka pembezoni mwa mto huo kwaajili ya malisho ya wanyama na maji.
Tunajifunza kwamba tunapomtii Mungu haimaanishi kuwa hatutakutana na changamoto za kimaisha ni wazi kuwa Abrahamu alimtii Mungu na kufika katika inchi ile ambayo Mungu alimuonyesha, Abrahamu alikuwa na mke tasa,

Mwanzo 11:30 “Na Sarai alikuwa tasa, hakuwa na mtoto.”,
Lakini pia alikuwa amekwenda mbali sana na familia yake Mwanzo 12:1 “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha;” na sasa akiwa amemtii Mungu anakutana na janga la Njaa katika inchi ya kanaani, hatupaswi kuona kuwa ni jambo geni kukutana na changamoto za aina mbalimbali tuwapo duniani pamoja na kuwa tunamtii Mungu, tunaweza kukutana na upinzani mkubwa, mambo magumu na matatizo, Lazima tukubali kuwa tuko duniani na kuwa nayo ni njia ya Mungu ya kutufundisha maswala muhimu, lazima tusonge mbele katika kumtii  na kutimiza kusudi lake 1Petro 4:12-13 “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.” Unaweza kuwa umefuata taratibu zote katika kuoa kwako lakini ukashangaa ndoa yako ina changamoto lukuki kuliko ya wale walipita shotikati, Mungu anaweza kuwa amesema nawe ufungue huduma kwa sauti ya wazi na ukatii lakini ukakutana na changamoto za ajabu sana kana kwamba si yeye aliyekuita mahali hapo na maswala mengine kadha wa kadha, hayo yasituvunje moyo wala kututoa katika kulitimiza hivyo kusudi la Mungu.

Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu


Kama majaribu hayo hayatoshi akiwa Misri sasa Abrahamu anakutana na changamoto nyingine angalia Mwanzo 12:11-16 “Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso; basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai. Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako Basi ikawa Abramu alipofika Misri, Wamisri wakamwona huyo mwanamke ya kwamba yeye ni mzuri sana. Wakuu wa Farao wakamwona, nao wakamsifu kwa Farao; basi yule mwanamke akachukuliwa nyumbani mwa Farao. Naye akamtendea Abramu mema kwa ajili yake; naye alikuwa na kondoo na ng'ombe, na punda waume, na watumwa, na wajakazi, na punda wake, na ngamia.
Changamoto kubwa kwa Abrahamu sasa ni hofu, hofu ya kupoteza maisha kwaajili ya uzuri wa Sara mkewe, Abrahamu alitambua kuwa ana mke mzuri na kuwa hawezi kumkatalia Farao asimchukue bila kuuawa kwa hiyo alimweleza sara aseme kuwa yeye ni ndugu yake, na kwaajili ya hayo alifadhiliwa sana na Farao, na kupewa muzi, kondoo, punda na ngamia pamoja na watumwa na vijakazi utajiri wake ukaongezeka sana, na Ibrahimu alivipokea.

Watu wengi wanamlaumu sana Abrahamu kwa kosa hili, wanajiuliza kwanini Abrahamu alipokea mali hizi zote kana kwamba amemuuza Sara aidha kwa tendo hili inaonekana kana kwamba Abrahamu kama baba wa imani hapa alikosa kumuamini Mungu dhidi ya ulinzi wake kwake na mkewe, hivyo inaonekana kama Ibrahimu hapa amefanya swala la kipagani, vyovyote vile uonavyo ni lazima tukubali kuwa katika masiah haya kila mmoja wetu anaweza kukutana na changamoto ya aina Fulani na ukajikuta kuwa unapata ufumbuzi wa kibinadamu ambao kwa mtazamo wa wengine inaweza kuwa sio sahihi, chukulia mfano umeingiliwa na majambazi nyumbani na wanataka kumuua baba yako na mama yako, lakini wazazi wako wakawa wamejificha mahali na wewe unapajua lakini majambazi hawapajui na wanakuuliza wako wapi baba yako na mama yako tuwamalize tuwaue? Kwa sababu unajua kusema uongo ni dhambi je unaweza kuwaelekeza majambazi aliko baba yako na mama yako ili wawaue? Au mfano umekutana na mama amebeba mtoto na mtoto wake anaonekana ana sura mbaya sana lakini mama Yule na motto wake wanakuchekea kwa tabasamu zuri na unataka kumtia moyo mama yule je utamueleza kuwa mama hongera una mtoto ana uso mbaya kweli! Ni mara ngapi tu mewasifia watu kuwa wako vizuri na huku tunajua moyoni dhahiri kuwa hawako vizuri? Unaweza kuona sio kuwa tunajifunza uongo lakini tunajifunza kuwa yako mazingira ambayo kwa ubinadamu wetu hatuwezi kuchomoka kama unawekwa kwenye kona sawasawa, watu wengi wa Mungu makanisani ni wepesi sana kuhukumu na kuzogoma wanapoona makosa yaw engine na wakati mwingine wanakuwa na kimbelembele kushauri nini cha kufanya ilihali hawajui kuwa wewe unapitia mazingira ya namna gani, kwa bahati yako mazingira ambayo Mungu tu ndio anaweza kuelewa na kutujali, Tukio la Abrahamu hapa linaweza kuwa sio tukuio zuri wala lenye kuleta heshima au kuonyesha kujaa imani, ni tukio linaloonyesha mwanadamu akitafuta kujiokoa kwa njia zake lakini Mungu ndie hakimu wake na sio sisi! Kutokana na tukio hili Ibrahimu alimpoteza Sara na Sara alichukuliwa kuwa mke wa Farao.

Hata nikamtwaa kuwa mke wangu?


Hayoyote yalikuwa ni utangulizi tu kwangu, lakini hoja kubwa ambayo nilitaka wanafunzi wa Biblia tuweze kuidadavua kwa pamoja ni swala zima la kuchukuliwa kwa mke wa Ibrahimu Nyumbani kwa Farao ili kuwa mke wake swali kubwa hapa ni je farao alifanikiwa kumuingilia Sara kama mkewe? Kuna makundi makuu mawili ya mawazo ya wasomaji wa biblia kundi la kwanza wanaamini kuwa Sara alichukuliwa na Farao na huenda Farao alifanikiwa kumuingilia sara kama mke wake hii ni kutokna na uwazi wa biblia hapa na utofauti wa tukio kama hili kwa Abimeleki ona matukio haya

Mwanzo 12:18-20 “Ndipo Farao akamwita Abramu, akasema, N'nini hili ulilonitendea? Mbona hukuniambia ya kuwa huyo ni mkeo? Mbona ulisema, Huyo ni umbu langu, hata nikamtwaa kuwa mke wangu? Basi sasa, huyo mke wako umchukue, uende zako. Farao akawaagiza watu kwa ajili yake, wakampeleka njiani, na mkewe, na kila alichokuwa nacho.
 

      
Mwanzo 20:1-12 “Ibrahimu akaondoka huko kwenda nchi ya kusini, akakaa kati ya Kadeshi na Shuri, naye akatembea katika Gerari. Ibrahimu akamnena Sara mkewe, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akapeleka watu akamtwaa Sara. Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu. Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee BWANA, Je! Utaua hata taifa lenye haki? Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi. Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse.Basi sasa umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao. Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumwa wake wote, akawaambia maneno hayo yote masikioni mwao, nao watu hao wakaogopa sana. Kisha Abimeleki akamwita Ibrahimu, akamwambia, Umetutenda nini? Nimekukosa nini, hata ukaleta juu yangu na juu ya ufalme wangu dhambi kuu? Umenitenda matendo yasiyotendeka. Abimeleki akamwambia Ibrahimu, Umeona nini hata ukatenda jambo hili? Ibrahimu akasema, Kwa sababu naliona, Yakini hapana hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa ajili ya mke wangu. Naye kweli ni ndugu yangu, binti wa baba yangu ila siye mwana wa mama yangu, ndipo akawa mke wangu.”

Sara anachukuliwa na farao na kufanywa kuwa mke wake na maandiko yako kimya kama endapo Farao alifanikiwa kumuingilia Sara au hapana, wakati katika kifungu cha Pili kabla Abimeleki hajamgusa Sara Mungu aliingilia kati na kumuonya kwa njia ya ndoto kwa aajili ya hayo wako wanaoamini kuwa Sara aliingiliwa na Farao, lakini Sara hakuguswa na Abimeleki! Kwa sababu ya lugha ile “hata nikamtwaa kuwa mke wangu” wengi wanaamini kuwa farao alimwingilia Sara, hoja zinajengwa kwamba hiki ndio kilikuwa kipimo kingine cha kuthibitisha kuwa sara alikuwa tasa, akiwa na miaka 65 hapa badomanaonekana kuwa mwanamke mzuri sana na wa kuvutia kiasi cha kuhatarisha maisha ya mumewe, Kama Sara angeshika mimba ya Farao ni wazi kuwa Abrahamu ndiye ambaye angejulikana kuwa ana tatizo, kwa hivyo wenghi wanaotetea hoja kuwa Farao alimuingilia Sara wanajaribu kutofautisha Lugha iliyotumika kwa Farao na ile iliyotumika kwa Abimeleki ikionyesha nkuwa Kuwa kule kwa Abimeleki Mungu aliingilia kati lakini kwa Farao Mungu aliachia Ibrahimu avune matunda ya uongo wake !

Mungu alumuhukumu Farao!


Binafsi sikubaliani na kundi la watu wanaofikiri kuwa Sara aliingiliwa na Farao, japo sihukumu mawazo yao lakini nataka kujenga hoja za kibiblia ili tuweze kuwa na uelewa mwema zaidi, kwanza ni muhimu kufahamu kuwa lugha ile Hata nikamtwaa kuwa mke wangu  katika tafasiri ya Biblia ya kiebrania kwa kiingereza ingeweza kusomeka namna hii “and i took her to me to wife” yaani kwa tafasiri nyepesi nilimchukua kwa kusudi la kuwa mke wangu, Ni muhimu kufahamu kuwa kabla farao hajamgusa tayari yeye na watu wake wote walipigwa na mapigo makubwa sana na inawezekana kupitia waonaji wake farao alitafuta sababu ya mapigo hayo mazitio huenda kupitia waganga au manabii wake na waonaji na wakamjulisha kuwa mapigo hayo yametoka kwa Mungu na ni kasababu amemtwaa mke wa mtu, na huenda Sara alikiri wazi kuwa yeye ni mke wa Abrahamu na sio ndugu, Farao alielewa kuwa mwanamke yule alikuwa ni mke wa mtu na alimrejesha haraka na kumuondoa katika inchi yake, Kwa kawaida kulinga na mila na desturi za kale mwanamke alipochukuliwa awe mke wa mtu au mfalme hakuwa anapelekwa moja kwa moja siku hiyo hiyo bali aliwekwa kwenye Haremu yaani jumba la kifalme na kuanza kuandaliwa unaweza kuona Esta 2:12 “Basi ilipowadia zamu yake mwanamwali mmojawapo aingie kwa mfalme Ahasuero, hali akiisha kufanyiwa sawasawa na sheria ya wanawake miezi kumi na miwili; yaani, ndivyo zilivyotimia siku zao za utakaso, miezi sita kwa mafuta ya manemane, na miezi sita kwa manukato na vifaa vya utakaso wa wanawake;” unaona kwa hivyo kulikuwa na muda maalumu wa maandalizi kabla mwanamke huyo kupelekwa kwa mfalme kulikuwa na miezi ya uangalizi kama miezi 12 kabla ya mke maalumu hii ilikuwa ni kwa sababu mbalimbali za kiusalama, taratibu na kuwalinda wafalme na magonjwa na kadhalika kwa hiyo kwa Sara huenda pia alikuwa yuko katika maandalizi, kwa hivyo kumrejesha kwa mumewe lilikuwa tendo la haki lilolofanya na Farao.

Pamoja na hayo pia maandiko yanathibitisha wazi kuwa Mungu aliingilia kati biola kujali madhaifu yao ya kibinadamu lakini kwaajili ya agano lake aliwaadhibu wenye mamlaka ili wasiwaonee wapakwa mafuta wake ona Zaburi 105:14-15 “Hakumwacha mtu awaonee, Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao. Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu.Kwa hiyo kwa mujibu wa maandiko ni wazi kuwa Sara hakuguswa na mwisho wa siku Farao alimrejesha Sara kwa Abrahamu kama Abimeleki alivyofanya pia, farao alihakikisha kuwa Abrahamu anakuwa saklama ana anaondoka Misri mara moja, Licha ya kuwepo kwa udhaifu wa Abrahamu Mungu ni mwingi wa rehema alitimiza ahadi yake kwa Abrahamu na Abrahamu aliondoka akiwa na ulinzi na mali nyingi bika kukaa sana Misri

Tukio hili linaweza kuwa funzo kwetu kwamba wakati mwingine Mungu anaweza kuruhusu mabaya yakatupata au yakampata mtu katika mazingira Fulani kwa kusudi la kutokeza mema Faraoa lipigwa mapigo makubwa sana ambayo yalipelekea atende wema huku akigundua kuwa yuko Mungu aliye hai, kila jambo linalotutokea katika maisha yetu lina makusudi yake, katika maisha yetu Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”.  Mungu wakati wote anatuwazia mema ingawa Abrahamu alitegemea kuokolewa kwa akili zake na ujanja wake alikamatwa kwa uongo wake lakini Mungu alithibitisha nguvu zake na kuonyesha kuwa ni yeye pekee mwenye uwezo wa kuokoa, Mungu anakusudi kwa kila jambo hata mateso, Mapenzi yake yatatimizwa na jina lake litatukuzwa tu


Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!

0718990796/0784394550
ikamote@yahoo.com

Maoni 1 :

  1. Bwana Asifiwe mtumishi wa Mungu. Nimependa sana ufafanuzi huu, hili ni jambo lililokuwa linanitatiza sana. Ninaamini kila mwenye mke halali na mwenye mapenzi ya kweli, hii habari itamgusa!
    Barikiwa sana.

    JibuFuta