Jumanne, 4 Agosti 2020

Haki yenu isipozidi hiyo haki ya Waandishi na Mafarisayo



Mathayo 5:20 “*Maana nawaambia haki yenu isipozidi Hiyo haki ya waandishi na mafarisayo hamtaingia kamwe katika ufalme wa Mbinguni*



Utangulizi:

Waandishi na Mafarisayo ni akina nani ?

Ni muhimu kufahamu kuwa  nyakati za ulimwengu wa agano jipya yaani wakati wa Yesu Kristo katika Dini ya kiyahudi kulikuwa na Makundi (Madhehebu) mbalimbali ya watu mbalimbali wenye misimamo kadhaa ya kidini lakini makundi makubwa yaliyojulikana zaidi walikuwa Mafarisayo na Masadukayo, lakini kulikuwa na kundi lingine maarufu lililojulikana kama waandishi au wanasheria, na mengineyo yenye misimamo ya kisiasa na kidini lakini hapa nitawazungumzia Waandishi na mafarisayo tu kwa sababu ndio ambao wametajwa katika mstari wa Msingi kwamba “Haki yetu (Wakristo au wanafunzi wa Yesu) isipozidi hiyo haki ya Waandishi na mafarisayo Hatutaingia kamwe katika ufalme wa Mungu” kwanza tuwajue hao ni kina nani:-

Waandishi

Waandishi ni kundi la jamii katika dini ya kiyahudi waliokuwepo wakati wa Agano jipya ambao walikuwa ni walimu na watafasiri wa Sheria ya Musa Yesu alilitaja kundi hili kwa sababu walikuwa wasomi na watu waliobobea katika ujuzi wa torati, kazi yao kubwa pia ilikuwa kunakili sheria kutoka katika magombo ya chuo yanayochakaa au ya zamani na kuyanakili katika magombo mapya aidha watu hawa pia walijikita katika kusoma na kuielewa sheria ili kuwafundisha au kuwafafanulia watu.

                      Walijulikana pia kama wanasheria
                      Ni kundi la uamsho wa kimaandiko lililoanza wakati wa Ezra mwandishi baada ya watu kurejea kutoka uhamishoni Babeli
                      Waliitwa “SOFERIM” Kwa Kiebrania, maana yake watu wanaojua maandiko lakini pia waliitwa wenye hekima.

Ezara 7:10 “Kwa maana huyo Ezra alikuwa ameuelekeza moyo wake kuitafuta sheria ya Bwana, na kuitenda, na kufundisha maagizo na hukumu katika Israeli”.

Mafarisayo.

Kundi lingine la kidini katika dini ya kiyahudi waliokuwepo pia wakati wa agano jipya na wakati wa Yesu walijulikana kama Mafarisayo hawa walikuwa watu walijitahidi sana kuishi kwa haki na kuitii sheria ya Mungu kivitendo na kwa kujiamini na kujivunia Yesu alilitaja kundi hili kwa sababu lilikuwa na bidii katika utii wa torati lakini sio kwa moyo mweupe na hata wale waliokuwa na moyo mweupe waliishika sheria katika misingi ya kujipatia haki nje ya neema ya Mungu  Matendo 26:4-5Kwa maana Wayahudi wote wanajua maisha yangu tangu ujana, yaliyokuwa tangu mwanzo katika taifa langu huko Yerusalemu, wakinijua sana tangu mwanzo, kama wakipenda kushuhudia, ya kwamba nalikuwa Farisayo kwa kuifuata madhehebu ya dini yetu iliyo sahihi kabisa
               
                      Pamoja na Torati ya Musa pia waliamini maandiko mengine ya manabii na masimulizi ya kale ya kiyahudi kuwa ni neno kamili la Mungu
                      Walikazia sana maswala ya uadilifu kuliko Theolojia
                      Waliamini kuwa kuna maisha baada ya kufa, na pia wafu watafufuliwa
                      Wakliamini uwepo wa malaika, maono, na kuwepo kwa pepo wabaya

Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na mafarisayo!

Moja ya maandiko ambayo hutumiwa vibaya na wahubiri wengi wa injili ni na walimu wa Biblia  ni pamoja na andiko hili  *Mathayo 5;20* Maana nawaambia haki yenu isipozidi Hiyo haki ya waandishi na mafarisayo hamtaingia kamwe katika ufalme wa Mbinguni*” kimsingi kutokana na maandiko haya wakristo waliookoka na hata wale wasiookoka wametengenezewa makongwa mengi  na mazito sana  siku zote watafasiri wa neon la Mungu au maandiko wakikosea hata kidogo tu katika kuitafasiri maandiko wanaweza kusababisha tatizo kubwa sana sawa na Daktari kuzidisha dozi au kutoa dozi iliyo chini ya kiwango na ndivyo ilivyotokea kwa miaka mingi katika tafasiri ya mstari huu hebu sasa tuuangalie tena mstari huu kwa kina kwa kawaida mstari huo unasomeka hivi “*Maana nawaambia haki yenu isipozidi Hiyo haki ya waandishi na mafarisayo hamtaingia kamwe katika ufalme wa Mbinguni*” ndugu msomaji wakristo wengi  narudia tena wamefanywa kuwa watumwa na kubeba mizigo isiyowahusu kupitia andiko hili jinsi andiko hili lilivyo na kile kinachotafasiriwa au kukaziwa na wahubiri  na badhi ya walimu wa maandiko ni tofauti sana na hata na jinsi Kristo alivyokusudia  andiko hili kutumika.

Kwa ujumla kile ambacho wahubiri  na waalimu wengi wa neon la Mungu wengi wanakimaanisha katika maandiko haya ni kama maandiko haya yanasomeka hivi “*Maana nawaambia Matendo yenu yasipozidi Hayo Matendo ya waandishi na mafarisayo hamtaingia kamwe katika ufalme wa Mbinguni*” nimewahi kuwasikia wahubiri wakikazia wakristo kuwa na matendo yanayowazidi mafarisayo na waandishi yaani waalimu wa sheria tunapounganisha na swala zima la wokovu mafundisho ya aina hiyo sio injili sahihi tuliyoipokea toka kwa Bwana,

Wakati Fulani kwa sababu ya mafundisho ya aina hiyo nilikuwa nimejipangia kuwa ni lazima niamke kuomba Alfajiri kama vile waislam wafanyavyo na kwakuwa niliamini kuwa wao hawana Mungu wa kweli na aliye hai  kama niliye naye, Na kutokana na msisitizo wa mahubiri ya wachungaji wengi nilijifunza kuwa ninalazimika kuamka kabla ya Waislamu  hawajaamka na kumuomba Mungu ili matendo yangu yazidi hayo matendo ya mafarisayao na kwakuwa maisha yangu ya mwanzo kabla ya kumjua Mungu nilikuwa nikilala na kuamka kwa saa nilizotaka uamkaji wa Alfajiri lilikuwa jambo jipya katika maisha yangu na halikuwa jambo jepesi kusema ukweli. niliambiwa kuwa huko Korea ya kusini wakristo huamka alifajiri na kumuomba Mungu na wamepata mafaniko makubwa sana lakini sisi Afrika Mashariki wamishionari wetu  waliokuja mapema na kuleta Ukristo hawakuwa wametufunza kuamka alfajiri kwa  Msingi huo mwanzoni nilichapa usingizi lakini nilipomjua Mungu na kujifunza kuhusu kuamka alifajiri niligundua kuwa ninapaswa kuwawahi waislamu na siku kama ikitokea nimechelewa kuamka na wakanitangulia nilijihisi vibaya na kuonakama  kuwa siku hiyo ni chungu na sio siku nzuri  na labda imeharibika na nilihisi au niliiishi kwa maumivu ambayo sikuwa nayo kabla ya kuokoka kwa nini nilijifunza kuwa matendo yangu lazima yazidi yale ya Mafarisayo.

Kumbe nilikuja kugundua siri kutoka kwa Roho wa Mungu kuwa Mungu hakumaanisha kile nilichokifanya kimsingi Yesu alikuwa akizungumzia “*HAKI*” na sio “*MATENDO*” nililazimika kujifunza kuhusu haki kama mstari halisi unavyosema na niligundua kuwa kwanza hakuna mwanadamu mwenye haki hata mmoja *Warumi 3:10-12, Biblia inasema hivi “Kama ilivoandikwa ya kwamba hakuna mwenye haki hata mmoja hakuna afahamuye, Hakuna amtafutaye Mungu Wote wamepotoka wameoza wote pia hakuna mtenda mema la! Hata mmoja”* nilijiuliza kama hakuna mwenye haki hata mmoja inakuwaje Yesu aseme haki yetu isipozidi haki ya mafarisayo hatutauona ufalme wa Mbinguni?

Nikagundua kuwa kumbe Mafarisayo hawakuwa na haki hawakuwa na haki ya kweli haki waliyokuwa nayo ilikuwa haki ya nje tu, Yesu aliwataja waandishi kwa sababu walikuwa wasomi waliobobea katika maandiko na aliwataja mafarisayo kwa kuwa walikuwa na juhudi ya kutafuta haki kwa nguvu zao, Makundi haya yalikuwa na haki ya nje ya kidini tu na haikuwa haki yenye faida yoyote kwa ufalme wa Mungu haki yao iliwekwa katika misingi ya matendo ya nje yasiyotoka moyoni na yenye kubeba utukufu wa kibinadamu tu na zaidi sana waliwadharau watu wengine wakifikiri kuwa watu hao ni wenye dhambi na wasiofaa au ambao hawawezi kukubaliwa na Mungu kwa sababu ya kujifikiri kuwa waio ni bora zaidi  ona kwa mfano Luka 18:10-14  Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.” Unaweza kuona kwa hiyo kwa mtazamo wa nje na wa kibinadamu waandishi na Mafarisayo waliokuwa wenye haki iliyochanganyika na kiburi, wakijidhani kuwa wao ni watakatifu na wenye kibali kwa Mungu kuliko wengine walikuwa hawana ujuzi kuwa Mungu ndiye mwenye kutuhesabia haki na kuwa ni Mungu ndiye anayeujua moyo wa Binadamu.      

 “*Mathayo 23;25-28* “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote.Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi”.

Yesu anawaonya mafarisayo “*Ole wenu waandishi na Mafarisao wanafiki …..*” kumbe mafarisayo walikuwa wanafiki hawakuwa na haki ya kweli, Haki yao ilikuwa haki ya nje walifanya mambo ili waonekane na watu *Mathayo 23;5a* “*Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu*;” kumbe mafarisayo haki yao ilikuwa ni haki ya nje haki ya kujionyesha tu walionekana na watu kuwa ni wenye haki lakini kwa kweli hawakuwa na haki ya kweli na ndio maana na sio hivyo tu walikuwa na dhambi ya dharau au walikuwa na kiburi wakijifikiri kuwa waoa ni watakatifu au wana kibali kwa Mungu kuliko watu wengine waliowadhani kwa akili zao na mawazo yao kuwa ni wenye dhambi ona maneno haya Luka 18:9 “Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.   Ni kwaajili ya haya utaweza kuona kuwa Yesu alisisitiza kuwa ni lazima iwepo haki mbadala, haki ambayo ni tofauti na haki na ile ya  waandishi na mafarisayo  ambayo kimsingi ni haki ya nje.  Sasa ili mtu aweze kuingia katika ufalme wa mbinguni hawezi kuingia kwa haki kama ile ya waandihi na mafarisayo ambayo ilikuwa ya nje ni kweli walionekana wanashika sheria walionekana wanaomba, walisifu na kufunga walisoma neno la Mungu  na hata kuhudhuria ibada  hata hivyo walifanya hayo ili waonekane na watu wasifiwe waonekane kuwa wao ni wa kiroho na washika dini wakubwa huu haukuwa mtazamo sahii, haki mbadala ni haki ambayo haitokani na matendo ya sheria  ni haki kutoka moyoni ni haki itokanayo na imani  ni neema ya kukubali kazi aliyoifanya Yesu Kristo kwaajili yetu Msalabani ni haki itokanayo na Kristo *Warumi 3;21-26*Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti;  kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake,ili aonyeshe haki yake ,kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa.apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.*

Angalia pia Waefeso 2;1-9 *Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu

hii ndio haki mbadala aliyoizungumzia Bwana Yesu kwa hiyo Kristo hajatuita katika mashindano ya kuwazidi wale tunaowaita mafarisayo kwa matendo kama ukifanya hivyo wakikushinda unakuwa chini ya kongwa ambalo hata kabla ya kuokoka hukuwa nalo, Mtu anapomuamini Yesu mara moja Yesu anafanyika kuwa haki yetu ipatikanayo kwa neema na  wala sio kwa matendo  neema ya Kristo ndani yetu inatugeuza na kutufanya kuwa wema yenyewe na hivyo kutupelekea katika Tito 2:11-12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na HAKI, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;  Kwa hiyo Yesu hakumaanisha kuwa matendo mema ni mabaya la hasha matendo mema yanakubalika kwake ykihusisha imani na rehema kutoka kwake Yesu yeye ndiye anakuwa haki yetu ambayo ni zawadi kutoka kwake ni neema kutoka kwake  Biblia inasema hivi

1Wakoritho 1:30 -31 “Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na HAKI, na utakatifu, na ukombozi; kusudi, kama ilivyoandikwa, Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana.

2Wakoritho 5:21 “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa HAKI ya Mungu katika Yeye.”

Kumbe unaweza kuona haki halisi haitokani na nafsi zetu haki halisi ni ile tunayopewa kwa imani kwa kumuamini Yesu na kukubali kazi yake aliyoifanya pale msalabani, ni aina hii ya haki ndiyo ambayo Yesu alikuwa anaizungumzia na manabii walitabiri kwa kumuamini Mungu yeye sasa anafanyika kuwa haki yetu

Yeremia 23:5-6 “Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi. Katika siku zake Yuda ataokolewa, Na Israeli atakaa salama, Na jina lake atakaloitwa Ni hili, Bwana ni haki yetu.”   

Kujaribu kwa njia za kibinadamu kuishi maisha ya kujitafutia haki bila imani kwa Yesu Kristo kutatufabya tuishi katika Kongwa kubwa sana la matendo yatakayotufanya tuuone wokovu kuwa ni kitu kigumu sana na kumbe wokovu ni mwepesi na raha nafsini mwetu

Ukiyajua hayo heri wewe ukiyatenda

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!

Maoni 2 :

  1. Kazi Yako siyo Bure Mwalimu wangu .. Let the fire burning 🔥🔥

    JibuFuta
    Majibu
    1. Kazi Yako siyo Bure Mwalimu wangu.. 🔥🔥🔥 Mchungaji Joshua Mapamba

      Futa