Mwanzo 3:16 “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako,
na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye
atakutawala.”
Utangulizi:
September 4-15 Mwaka 1995
Kulifanyika mkutano mkubwa wa nne wa dunia wa wanawake huko Beijing nchini
China. Mkutano huo ulipewa jina la
kiingereza “Action for Equality:
development and peace”, yaani kwa tafasiri ya Kiswahili changu naweza
kusema “Haki sawa kwa maendeleo na amani”
Kongamano hili la wanawake lilipewa jina hilo na umoja wa mataifa, Katika mkutano
huu mkubwa, serikali za dunia zilikusanyika zikiwakilishwa na wanawake maarufu
kutoka sehemu mbalimbali duniani zikiwa na wito wa kuitaka dunia kufikia
malengo ya usawa yaliyokubaliwa na jukwaa hilo la wanawake lililofanyika
Beijing likijulikana kama “The Beijing
Platform for Action”, Kutoka Tanzania mwakilishi mmojawapo maarufu alikuwa
mama Gertrude Mongella (Kushoto pichani hapo juu) ambaye wakati huo pia alikuwa
ni spika wa bunge la Africa kwa upande wa wanawake, pamoja na maswala mengine swala kubwa lilosisitizwa ni usawa katika
uwakilishi lakini kubwa zaidi ni haki za wanawake duniani. Mkutano huo wa
Beijing ulihitimishwa kwa kutoa tamko la Beijing yaani “Beijing Declaration.” Na lilikuwa ni tamko lenye maazimio yapatayo
38 na mengi yakiwa na mkazo kuhusu haki za wanawake.
Je unapata picha gani unaposoma
habari za mikutano mikubwa kama hii na maazimio makubwa ya wanawake? Hasa
yanayodai haki na haki hii ni usawa baina yao na wanaume, ni ukweli ulio wazi
na usiopingika kuwa katika jamii mwanamke amebaki nyuma kwa kiwango kikubwa na
sehemu kubwa sana uwezo wao haufanani na ule wa wanaume, tangu katika malezi na
hata ukuaji kumekuwa na kipaumbele zaidi kwa watoto wa kiume penginepo kuliko
watoto wa kike, maumbile na maswala mengine ya kijamii mila na tamaduni
zimemuacha mwanamke nyuma kwa kiwango kikubwa na kwa sababu hiyo kuna uwezekano
mkubwa kuwa labda umoja wa mataifa umeliona hilo na hivyo ukaandaa makongamano
kadhaa yenye maazimio ya kumuinua mwanamke, hatuna shaka kabisa kuwa uko ukweli ulio wazi
kuwa mwanamke akiendelea jamii inaeweza kuendelea na kupiga hatua kwa kiwango
kikubwa, Mwanafalsafa mmoja maarufu wa Afrika nchini Ghana James Aggrey alisema
ulimuelimisha mwanamke umeielimisha jamii, kwa hiyo wanawake wakiendelezwa na
kupewa fursa sina shaka kabisa watakuwa msaada mkubwa kwa jamii duniani.
Hata hivyo ni muhimu kufahamu na
kujiuliza kuwa kwa nini wanawake wamejikuta katika changamoto hizi na swala
kubwa zaidi kwanini wanapigania haki na usawa linapokuja swala la ulinganifu na
wanaume? Fahamu ya kuwa wanawake wanajaribu au wanataka kujikomboa, wanataka
kujikomboa kutoka katika kile ambacho maandiko yametamka kuwahusu, Liko tatizo
ambalo wala sio la mfumo dume, wala sio la mila na desturi wala sio la
kitamaduni ni tatizo la kiroho ni tatizo ambalo msingi wake na chanzo chake
kilisababishwa na wanawake wenyewe, na hii ni kwa mujibu wa maandiko
matakatifu, wakati mwingine wanawake wanapokuwa katika harakati zao huwa
wanatamka kirahisi tu kuwa hata tamaduni mila na kidini ziliwakandamiza! Lakini
leo nataka itambulike wazi kiini cha tatizo ili kwamba mwanamke aweze kuwa na
ukombozi sahihi anapaswa kujua haki zake za msingi kama zilivyotamkwa na
Maandiko matakatifu au na Mungu mwenyewe ili ajue mipaka yake ya haki na
ukombozi anaoupigania wakielewa hayo watakuwa na amani ya kweli na watapata
uhuru wa kweli.
Chanzo cha tatizo.
Neno la Mungu linaonyesha wazi kabisa
kuwa mwanamke na mwanaume waliumbwa wote wakiwa na haki sawa, wote wakiwa
wakamilifu na wote wakiwa wamepokea tamko la Baraka za Mungu katika kuutawala
ulimwengu ona Mwanzo 1:26-31 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura
yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi
yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu
kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba.
Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na
kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe
chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche
utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake
yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; na chakula cha kila mnyama wa nchi,
na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye
uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. Mungu akaona kila
kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku
ya sita.”
Unaona maandiko yako wazi kabisa kuwa Mungu amewapa
wanadamu namaanisha wanawake na wanaume kwa pamoja thamani kubwa sana wote
walitamkiwa baraka ya kuongezeka na kuijaza nchi na kuitiisha na kuitawala wote
walipewa mtaji sawa utawala sawa na uhuru sawa kwa msingi huo mwanamke na
mwanaume walikuwa ni watawala wenza wenye usawa unaofanana, lakini wote pia
walikuwa na jukumu la kumuabudu Mungu na kumtii kwa usawa na kwa pamoja, Hata
hivyo Mwanamke alipaswa sio kumsikiliza Mungu tu, lakini alipaswa kumsikiliza
na Mumewe sawasawa na kumsikiliza Mungu, agizo la kutokula matunda ya mti wa
ujuzi wa mema na mabaya kimsingi lilitolewa kwa Adamu pekee na huenda labda
mwanamke alisikia agizo hilo baadaye kutoka kwa mwanaume angalia
Mwanzo 2:15-17 “BWANA
Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.
BWANA Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza
kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku
utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika”.
Unaposoma maandiko
haya ya uchanganuzi wa uumbaji utaweza kuona kuwa agizo hili lilitolewa kwa
Adamu na kisha baadaye Eva aliumbwa kwa hiyo ni wazi katazo la ule mti wa ujuzi
wa mema na mabaya Eva alilisikia kutoka kwa mumewe, lakini haki ya utawala
iliwahusu wote, hii maana yake kwa kuwa mwanaume aliumbwa kwanza kisha mwanamke
baadaye na kwa kuwa mwanaume alipaswa kumfundisha mwanamke amri na maagizo ya Mungu, ni wazi na haki
utakubaliana nami kuwa Mwanaume, alikuwa na majukumu yenye ngazi ya juu zaidi
ya mwanamke kutokana na kuwa aliumbwa kwanza, Lakini vilevile alikuwa mwalimu
na amri ile alipewa yeye hivyo alikuwa ni msimamizi wa kazi ya uumbaji na maelekezo
aliyopewa na Muumba. Ni wazi basi kuwa swala la Kufundisha na kutawala lilikuwa
jukumu kuu la Mwanaume na swala la kusikiliza lilikuwa la mwanamke yaani Mungu
angetoa maelekezo kwa Adamu na Adamu angeleta ufafanuzi na maelekzo kwa
mwanamke naye pamoja na jamii wangetekeleza kile Mungu alichokusudia kwa hivyo
kwa itifaki, Mungu ni kichwa cha kila mwanaume na mwanaume ni kichwa cha
mwanamke hapo ndipo itifaki ya uumbaji na upokelewaji wa maagizo ya Mungu
ungepaswa kwenda kwa namna hiyo ona
1Wakoritho
11:3 “Lakini nataka mjue ya kuwa kichwa cha kila
mwanamume ni Kristo, na kichwa cha mwanamke ni mwanamume, na kichwa cha Kristo
ni Mungu.” Unaweza kuona kwa msingi huo ili Baraka za Mungu ziweze
kutiririka lazima itifaki ya kiungu izingatiwe, hili lisipoeleweka vema na wala
kuzingatiwa mambo mabaya sana yatatokea na uwepo wa Mungu utaondoka, Mungu ni
Mungu wa utaratibu wala sio Mungu wa machafuko!
Sasa basi jambo mojawapo kubwa na
la kusikitisha ni kuwa mwanamke alikuwa ni kiumbe mwenye udadisi mkubwa na akili
za kuhoji na kutafiti kile kilichosemwa na Mungu na mumewe Adamu na kutokana na
udadisi wake mwanamke akawa mwanadamu au kiumbe wa kwanza kuharibu utaratibu
huo uliokusudiwa na Mungu ona sasa Mwanzo
3:1-6 “Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama
wote wa mwitu aliowafanya BWANA Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo
alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? Mwanamke akamwambia
nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio
katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. Nyoka
akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku
mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu,
mkijua mema na mabaya. Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula,
wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika
matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.” Hiki ndio chanzo
cha tatizo, Mwanamke amekuwa mwanadamu wa kwanza kusababisha dhambi na mauti
kuingia ulimwenguni, ndio kiumbe wa kwanza kuharibu utaratibu, ndie kumbe wa
kwanza kutokutaka kumsikiliza Mungu wala mumewe na alichagua kumsikiliza
ibilisi na kusababisha kuharibika kwa utaratibu na mpango kamili wa Mungu
katika maisha ya wanadamu, Paulo mtume akimuasa Timotheo katika waraka wake
anamtaka Timotheo kukumbuka habari hizi na kuwaonya wanawake wawe katika
utulivu, akimkumbusha kile kilichotokea bustanini na namna ya kuhakikisha kuwa
utaratibu unafuatwa kanisani ona 1Timotheo
2:12-14 “Simpi
mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika
utulivu. Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye. Wala Adamu
hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.”
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
kifungu hiki Paulo mtume hakumaanisha kuwa wanawake hawawezi kusimama na
kufundisha katika kanisa, Nyakati za kanisa la kwanza wanawake walifanya kazi
ya kuhubiri injili na kufundisha neno la Mungu na mfano mzuri ni Prisilla na mumewe
Akila wanaotajwa katika Matendo ya Mitume
18:24-26 “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo,
mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika
maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa
ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua
ubatizo wa Yohana tu. Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila
na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi
zaidi.” Lakini vilevile
tunasoma habari za Fibi aliyekuwa na huduma katika kanisa huko Kenrea ona katika Warumi
16:1 “Namkabidhi kwenu Fibi, ndugu yetu, aliye
mhudumu wa kanisa lililoko Kenkrea;” Huenda muhudumu huyu alikuwa
mwanamke na alifundisha katika kanisa lakini kimsingi lugha inayotumika katika 1Timotheo 2:12-14 kwamba simpi mwanamke nafasi ya kufundisha sio
inayotokana na neno la Kiyunani “DIDASKEIN”
(Didasko) Ambalo maana yake ni kufundisha yaani kutoa maarifa na ujuzi na kuupeleka kwa wengine, Neno
linalotumika pale simpi mwanamke nafasi ya kufundisha ni neno la Kiyunani “AUTHENTEIN” (Authenteo) ambalo kwa
kiingereza lingeweza kusomeka kama “exercise
authority” au “Dominate” yaani
to have control over a place or person yaani wanawake wasishikishe adabu
wanaume au wasitiishe wanaume, wasiwaamuru kama wenye mamlaka hii ndio lugha
halisi ya kibiblia hapa wasiwatawale wasiwe na amri juu yao.
Hivyo basi tunapata picha kuwa ni
Eva aliyekuwa wakwanza kutamani na kujaribu kula matunda ya mti ule wa ujuzi wa
mema na mabaya ambao Mungu alikuwa amekataza, na ni yeye aliyeweza kutumia
ushawishi wake na mamlaka yake kuamuru na kumkosesha na Mumewe Adamu naye akala
ni sawa na kusema wazi kuwa dhambi iliingia ulimwenguni kupitia amri ya
mwanamke na matokeo yake na athari zake zikawa nyingi ikiwemo kuvurugika kwa
mpango kamili wa Mungu kwa mwanaume na mwanamke kama watawala wenza. Kwa hiyo
dhambi ya mwanamke ilikuwa ni kujiamulia, kula matunda ya mti wa ujuzi wa mema
na mabaya na kumuamuru mumewe naye ale. Na hivyo kuingiza mauti ulimwenguni.
Na tamaa yako itakuwa
kwa mumeo, naye atakutawala
Mungu ni Mtakatifu na ni lazima
aihukumu dhambi, imefanyika kwa kusudi au kwa bahati mbaya lazima
ataishughulikia tu, Mungu aliwahukumu wote na kuwaadhibu wote kutokana na kosa
walilolifanya lakini kila mmoja kwa namna yake, Adamu alimlaumu Eva kwa kosa
lake, na Eva alimlaumu nyoka kwa kosa lake na wote akiwemo nyoka waliadhibiwa
na Mungu kutokana na makosa yao, sisi nasi kila mmoja ataadhibiwa mbele za
Mungu kutokana na makosa yake, bila kujali ni mazingira gani yamepelekea
tukafanya dhambi lakini ni lazima tukae na kukumbuka kuwa mshahara wa dhambi ni
mauti na kila dhambi ni lazima iadhibiwe na kuhukumiwa na Mungu mwenyewe mwenye
haki!
1.
Kwa Nyoka.
Kwa kuwa Nyoka
ndiye aliyetumiwa na Ibilisi moja kwa moja Mungu alimlaani, ni jambo gumu sana
Mungu kutoa laana kwa kiumbe chake chochote, Lakini shetani alikuwa ana ujuzi
kuwa wao ni malaika na malaika kama viumbe vya kiroho hawafi, na hivyo
alistahili laana, kwani kupitia ushawishi wake amesababisha mwanadamu kuwa na
mauti katika mwili wake hivyo shetani kama mwanzilishi wa dhambi alilaaniwa,
Aidha nyoka ambaye alikuwa kiumbe wa kawaida aliyetumiwa na Shetani kuzungmza
na mwanamke yeye alilaaniwa kutembea kwa tumbo na kula mavumbi lakini pia kuwa
adui wa mwanadamu, Nyoka alitumiwa na shetani kuwashawishi wazazi wetu wa
kwanza kufanya dhambi, kwa kusudi na kwa nia ovu kabisa na hivyo alilaaniwa bila
mjadala na kupokea adhabu yake, adhabu ya nje ilimuhusu nyoka halisi na adhabu
ya ndani kiroho ilimuhusu shetani na majeshi yake. Ona
Mwanzo 3:14 “BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu
umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote
walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha
yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na
uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.”
2.
Kwa Mwanamke.
Eva alikuwa ni
kiumbe wa pili kutamkiwa adhabu japo wanadamu hawakulaaniwa, Eva alipokea
kifurushi cha adhabu chenye mafungu matatu, Ikiwa ni pamoja na kuzaa kwa
uchungu, Tamaa yake kuwa kwa mumewe, na mumewe kumtawala, huu haukuwa mpango wa
Mungu katika mahusiano, lakini ni mpango uliotokana na kuharibika kwa mwanadamu
kutokana na kuingia kwa dhambi ulimwenguni, wanawake wote waliowahi kuzaa
wanaujua au wameuonja uchungu huo, na uchungu huu unaendelea katika uhalisia wa
maisha ya wanadamu wote
Mwanzo 3:16. “Akamwambia
mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa
watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.”
Hata hivyo swala
la tamaa yako itakuwa kwa mumeo naye atakutawala ndio mahali panapochanganya
watu kwa miaka mingi na wasiweze kuelewa maana ya msemo huu, ili kuweza kuelewa
jambo hili hatuna budi kuliangalia kwa jicho linguine Biblia ya kiingereza ya
The New Living Translation ndio imetafasiri kwa namna iliyonyooka zaidi kwani
inasomeka hivi “you will desire to
control your husband, but he will rule over you” yaani kwa Kiswahili chake
tungeweza kusema namna hii “Utatamani
kumtawala mwanaume lakini yeye atakutawala wewe” unaweza kuona kumbuka kuwa
Mungu alikuwa anatamka adhabu kutokana na anguko la mwanadamu kwa kila mmoja
kulingana na kukosea kwake, kwa hiyo mwanamke hapa kutokana na kuwa wa kwanza
kwa hiyo kwa neno hili dhambi inaathiri uhusiano wa mwanamke na mwanaume katika
ndoa na laana moja wapo au adhabu mojawapo ya kudumu ambayo haiondoki hata kwa
wokovu, ni hii wanawake watatafuata wawe wanajua au hawajui watatafuta
kuwatawala wanaume na sio kuwatawala tu hata kuwaondoa au kuwaua, au kuwaondoa
kabisa wasiwepo hata kama wanaume watawapenda vipi wake zao, wao badala ya
kufurahia upendo na muungano huu ambao Mungu aliukusudia, Mungu hapa anatangaza
mgogoro utakaokuwepo kati ya mwanaume na mwanamke kutokana na madhara ya
dhambi, lakini pia anahitimisha kwa kuonyesha matokeo ya mgogoro huo, hiki ndio
wanawake watakuwa wanakitafuta siku zote za maisha yao hata kama watakuwa
wameokoka jaribu kubwa la wanawake litakuwa hilo na matokeo ya mgogoro huu ni
wao ndio watakaotawalika, Lugha inayotumika hapo na mumeo atakutawala katika
lugha ya kiibrania linatumika neno “Mashal”
linasomeka “Maw-shal” Maana yake ni KUTAWALIWA, kwa msingi huo sasa katika utaratibu mpya wa haki na
utawala Mwanamke anapaswa kujinyenyekeza chini ya utawala wa mumewe ili aweze
kuwa sawa na aweze kuwa na furaha na amani japo jambo hili halitawafurahishwa
kwa vile ni adhabu kutoka kwa Mungu unaona! Waefeso 5:22-25 “Enyi wake, watiini waume
zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo
naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa
limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi
waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa
ajili yake;” Kwa msingi huo ni muhimu kufahamu kuwa swala la
wanawake kujitiisha chini ya mwanaume ni adhabu na hivyo haliwezi kuleta furaha
kwao, wao ndio wa kwanza kuleta dhambi na mauti na kutumia uwezo wao wa
kushawishi na mwanaume akatii, adhabu yake ilikuwa awe mtii kwa mumewe japo
hawatakuwa na furaha kwa sababu watajiona kama wamekuwa duni lakini vilevile
heshima yao inapatikana kwa kuolewa na kupendwa, siri kubwa ya mafanikio ya
mwanamke na ili aweze kuishi kwa furaha ni kujinyenyekeza kwa Bwana zao yaani
waume zao, mwanamke hata awe na fedha kiasi gani, hata awe na mafanikio kwa
kiwango gani au awe na cheo kikubwa kiasi gani jambo pekee linaloweza kumjengea
heshima ni kuwa na mume na kujinyenyekeza kwa mumewe, endapo mwanamke atakataa
jambo hili heshima yake na furaha yake haiwezi kuwa kamili. Kama wanawake
hawatagundua siri hii watajikuta wanafanya mikutano mikubwa mingi na kupitisha
maazimio mengi sana lakini wanapaswa kukumbuka kuwa mwanaume kuwa juu na kuwa na mamlaka dhidi yao ni mgogoro
uliotangazwa na Mungu katika bustani ya Adeni na dawa yake ni kuukubali mgogoro
huo na kukubali kutawalika kinyume cha hapo watakuwa wanamuasi Mungu.
3.
Kwa
Wanaume.
Mwanzo 3:17-18 “Akamwambia
Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao
nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula
mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe
utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata
utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe,
nawe mavumbini utarudi.”
Kiumbe wa mwisho
kutamkiwa adhabu alikuwa Mwanadamu na kwa Mara ya kwanza Biblia inamtaja kwa
jina lake Adam yeye anahukumiwa kutokana na kosa la kumsikiliza mwanamke na
kukubali ushawishi wake Ushauri wa Mungu ni bora zaidi kuliko wa mwanamke Mithali 15:22-26 “Pasipo
mashauri makusudi hubatilika; Bali kwa wingi wa washauri huthibithika. Mtu
hulifurahia jibu la kinywa chake; Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema
kama nini! Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu; Ili atoke katika kuzimu
chini. Bwana ataing'oa nyumba ya mwenye kiburi; Bali atauthibitisha mpaka wa
mjane. Mashauri mabaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maneno yapendezayo ni safi”
Kuzungumza ukweli kuwa ni huyu mwanamke uliyenipa alinishawishi nikala hakukuwa
na msaada kwa Adamu alikuwa amesikiliza ujinga na hivyo alikuwa amefanya
machukizo kwa Mungu, hukumu yake itakuwa katika kujipatia riziki zake za kila
siku, yaani kazi za mikono yake zitampa shida Adamu, wakati mwanamke familia itamtesa
mwanaume atapatatabu kazini, atakula mkate kwa shida kazi ambazo zingempa raha
nafsini mwake zitampa taabusiku zote za maisha yake, adhabu ya Eva inahusisha
taabu za kifamilia na kuwa mtumwa wa mwanaume lakini adhabu ya Adamu inahusisha
kuwa mtumwa wa mazingira na kuishi kwa shida au kwa jasho yaani lazima afanye
kazi
Hitimisho.
Adhabu zilizotajwa hapo juu
haziondoki kwa wokovu wala kwa maombezi, njia ya kweli ya kufanikiwa ni kufanya
kazi kwa bidii, kila mwanaume anapaswa kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili
aweze kuwa mwenye furaha lazima ajaribu kwa kila njia kuyatawala mazingira,
ambayo ingekuwa rahisi kuyatawala kwa neema ya Mungu kabla ya anguko lakini
sasa atayatawala kwa jasho, wanawake nao hawawezi kuwa na uwezo wa kufikia
kilele cha mafanikio bila kuwa wanyenyekevu, Ndoa na kuheshimu mumeo hata kama
una kitu gani ndiko kutakakomfanya mwanamke awe na furaha ya kweli huu ndio
mpango wa Mungu uliokamili, hivyo wanawake wanapotafuta haki zao na usawa
miongoni mwa jamii wasome kwa bidii, wasaidie katika kufanya kazi na wafanikiwe
katika kila Nyanja lakini wakumbuke Mungu amemuweka mwanaume juu yao, wanawake
wanapookolewa hawana tofauti na wanaume wote wana haki sawa. Wanawake wote
hawajaamuliwa kuwanyenyekea wanaume, lakini ilivyo ni kuwa kila mwanamke
aliyeolewa anapaswa kumtii mumewe na sio kila mwanaume, kwa hiyo ili furaha
yako itimie mtii mumeo swala hili linatakiwa lifanyike kwa hiyari ili liweze
kuleta Baraka kwa nini kwa wanawake kuwatii waume zao kunafananishwa na kumtii
Kristo hivyo mwanamke anaweza kuyatenda mapenzi ya Mungu akiwa chini ya mumewe,
na kwa nini hili lifanyike kwa sababu Mungu amemuweka mwanaume katika nafasi ya
utawala, kwa hiyo yanapokuwepo makongamano ya haki sawa wanawaka wanapaswa
kupigania haki zao ili wainuke na kutatua changamoto zao lakini katika muktadha
wa kukumbuka kuheshimu utaratibu ambao Mungu ameuweka ili amani ya kweli
iwatawale na waweze kupendwa na waume zao.
Na. Rev. Innocent Kamote.
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima
Nimesoma na kupata maarifa. Ni maombi yangu Mungu aendelee kukupa maono na maarifa zaidi ya kuendelea kujenga na kueneza ufalme wake hapa duniani.Ahsante!.
JibuFuta