Alhamisi, 15 Oktoba 2020

LENGO KUU LENYE FAIDA KUU!

Wakati huu tulio nao ni wakati wa mwisho 1Yohana 2;18. “Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. “ Mwisho wa mambo yote umekaribia 1Petro 4;7. “Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala.” bado kitambo kidogo Yeye ajaye yaani Yesu Kristo anakuja, wala hatakawia Waebrania 10;37 “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia.” katika wakati huu wa mwisho ni muhimu kwa kila mmoja wetu kujifunza na kutafakari kwa makini somo letu la leo ‘Lengo kuu lenye faida kuu ”Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele sita vifuatavyo.:-

*      Malengo mbalimbali ya wanadamu katika maisha

*      Tatizo kubwa la malengo ya kawaida ya wanadamu

*      Lengo kuu lenye faida kuu

*      Mifano ya watu wenye Busara waliokuwa na lengo kuu lenye faida kuu maishani mwao

*      Mifano ya watu wapumbavu ambao hawakuzingatia lengo kuu lenye faida kuu

*      Yatupasayo Kufanya




Malengo mbalimbali ya wanadamu katika maisha

     Ukimuuliza mtu awaye yote maswali haya Je ni kitu gani unachotamani kuwa nacho maishani mwako? ukipata nini utakuwa na furaha isiyo na kikomo? wanadamu mbalimbali watakuwa na majibu Tofauti katika kujibu maswali haya au kwa Maneno mengine watakuwa na malengo mbalimbali. katika Biblia tunawaona watu waliokuwa na malengo mbalimbali katika maisha yao 


Luka 12;13 “Mtu mmoja katika mkutano akamwambia, Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu” 

tunaona juu ya mtu mmoja aliyelenga tu kupata urithi. Ina maana hata mzazi wake alipokuwa hai aliwaza moyoni kwamba siku ya kugawiwa urithi itafika lini, Lengo lake ilikuwa ni mali za baba yake mbaya sana 


Luka 12 16-19 “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.” tunaona mtu moja mkulima aliyekuwa tajiri sana yeye lengo lake lilikuwa kujenga ghala kubwa na kuweka nafaka zake na vitu vyake ili apumzike, kula kunywa na kufurahia. Maandiko yanatupa habari za mtu mwingine  aliyekuwa na cheo kikubwa sana huko Shamu huyu aliitwa Naaman yeye alikuwa jemedari wa jeshi la mfalme wa Shamu,alikuwa mtu mkubwa mwenye Kuheshimiwa wa pili kutoka kwa mfalme huyu Tofauti na waliotangulia alikuwa na lengo la kupona ukoma 


2Falme 5;1-3. Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani.  Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.” 


Wako watu vilevile hali kadhalika wanaweza kuja kwa Yesu Kristo lakini malengo yao yakiwa ni kupokea miujiza yao, kuponywa magonjwa yao ama wanaweza kumfuata Yesu kwa sababu kadhaa wa kadhaa Mwanamke Hana, pamoja na kupendwa sana na mumewe na kupata kila kitu lakini aliwaza moyoni mwake wakati wote kupata mtoto 


1Samuel 1;1-11 “Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu  naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja akiitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea Bwana wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa Bwana, walikuwako huko. Hata siku ile ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, waume kwa wake, sehemu zao; lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda Hana, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo.  Ila mwenzake humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo. Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa Bwana, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula. Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwani huli chakula? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi? Ndipo Hana akainuka, walipokwisha kula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la Bwana.  Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana.  Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.” watu wengine katika 


Yakobo 4;13 “Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida;” 


wao walikuwa na lengo kuu  la kufanikiwa kibiashara na kupata utajiri,hata hivi leo kama ilivyokuwa kwa watu hawa lengo lao kuu ni kupata mchumba, kuolewa au kuoa, kuwa na digrii tatu, kuwa na cheo cha rais n.k Mtu aliye na lengo kuu la kupona au kupata mtoto anaweza hayo tu wakati wote na kwake mengineyo hayana uzito mkubwa kwake, wengine watakuja Kanisani kama hapa lakini lengo lao ni kupona tu, kuolewa au kuwa na mtoto na wokovu au kumtumikia Mungu kwake havina uzito mkubwa kila mmoja hana budi kujiuliza lengo lake kuu alilonalo ni nini? Wengine watatamani kuwaombea maelfu ya watu na kuwaona wanapokea miujiza yao n.k.

Tatizo kubwa la malengo ya kawaida ya wanadamu

Tatizo lililopo ni kwamba hata kama malengo waliyo nayo wanadamu yanatimia bado hayawapi furaha isiyo na kikomo. Mtu akipona ugonjwa wake au mateso yake kwa miujiza mkubwa bado hatimaye atakufa tu Lazaro aliyefufuka katika 


Yohana 11;38-44 “Basi Yesu, hali akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango, na jiwe limewekwa juu yake.  Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne. Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu? Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma.  Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake”.          


hatimaye alikufa tena,na wengine wengi walioombewa na Yesu wakapata miujiza yao kama kipofu Bartimayo aliyepata kuona,hatimaye alikufa,mtu hata akipata utajiri na mali iwe ni mamilioni ya mapesa, magari mengi, nyumba na kadhalika akifa haondoki navyo anaviacha vyote Zaburi 49;16-19 “Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi. Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata. Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai, Na watu watakusifu ukijitendea mema, Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake Hawataona nuru hata milele”. katika yote haya na malengo mengineyo mengi  hakuna cha kudumu  yote haya ni ya kupita wafalme wengi waliokuwa maarufu na wengi waliokuwa maarufu hapa duniani wamepita wamekufa na imebaki historia tu. Wanasiasa wengi, wakubwa na maarufu duniani, waimbaji, wachezaji, wasanii, matajiri na wanasayansi na wenye umaarufu wa kila aina wote wamepita duniani na historia zao zimehifadhiwa hakuna cha kudumu, wahubiri maarufu waliotikisa dunia na kila mwenye mafanikio ya kila namna duniani wamepita hakuna jipya chini ya jua mambo yote ni ubatili tu kila kitu kina mwisho na hakuna cha kudumu kwa msingi huo malengo yetu duniani ni ya muda mfupi tu na sio ya kudumu wala hayana faida za kudumu!

Lengo kuu lenye faida kuu.

Lengo kuu lenye faida kuu ni kupata uzima wa milele au kuingia mbinguni mtu anapokuwa na lengo hili moyoni mwake wakati wote na kulipa uzito mkubwa kuliko malengo mengine yote mtu huyu anakuwa ameigundua siri, kukosa uzima wa milele kunaitwa kupotea katika Biblia 

Yohana 3;16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele       

Mtu Yeyote mwenye Busara atawaza kwanza juu ya uzima wa milele kuliko uzima huu wa Muda tu katika miili yetu wakati wote atawaza kama mtu mmoja aliyekwenda mbio akitafuta juu ya jambo hili wakati wa Yesu 

Marko 10;17 “Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? “ 


unaona swala kubwa sana na la msingi kuliko yote ni kuwa kuna maisha baada ya kufa, Je utakuwa wapi baada ya maisha yako duniani kuisha?  Iko jehamnamu ya moto milele na milele na uko uzima peponi milele na milele! Mtu anayekusudia kuupata uzima wa milele ndiye mtu mwenye akili kubwa kuliko wote, wako watu katika Biblia ambao licha ya Mungu kuwabariki kwa Baraka mbalimbali walikuwa na mawazo ya ufalme wa Mungu! Nahii ilikuwa ndio busara kubwa sana!

Mifano ya watu wenye Busara waliokuwa na lengo kuu lenye faida kuu maishani mwao.

Biblia inasema Ibrahamu alikuwa tajiri sana kwa mifugo,kwa Fedha na dhahabu Mwanzo 13;2, Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu.hata hivyo wakati wote lengo lake kuu lilikuwa kuingia mbinguni, aliacha kila kitu na kuwaza juu ya mbinguni  tunaelezwa katika 

Waebrania 11;8-10, kwamba “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako. Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.  Sara, Habili, Henoko na Nuhu na wengine wengi walitamani wakati wote kuingia mbinguni kuliko kupata mtoto,kupona n.k 

Waebrania 11;16  Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji.” Ayubu pamoja na utajiri wake yeye pia aliwaza juu ya kuingia mbinguni ukuu na utajiri kwake havikuwa na uzito mkubwa kuliko wokovu na kumuona Yesu 

Ayubu 1;1-3, Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. Kisha walizaliwa kwake wana saba, na binti watatu.  Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watu wa nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.          

Mtume Paulo hakuwaza tu kuifanya kazi ya Mungu au kufanya miujiza mikubwa mingi, lakini pamoja na kutumiwa sana na kupewa mafunuo makubwa Matendo 19;11-12, Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.” 2Petro 3;15-16  Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa;  vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe.” 


Paulo mtuma alikuwa ni mtume aliyafanya kazi kubwa kuliko mitume wote, aliyetumiwa na Mungu kwa miujiza ya kupita kawaida na kutumiwa kuandika Nyaraka na agano jipya karibu nusu na robo alihubiri njili na kuupoindua ulimwengu wa wakati wake hata hivyo hakusahau kuwa na lengo kuu  wakati wote lengo lake lilikuwa kwenda Mbinguni kuikaa na Kristo,Jambo hili alilitamani upeo ona  Wafilipi 1;23,” Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo maana ni vizuri zaidi sana;” hatuna budi kukumbuka kwamba tunaweza kufanya miujiza mingi lakini tukajikuta miongoni mwa watu wa kupoteza, ikiwa tutakuwa na maisha yaliyo jaa dhambi na tukajikuta kuwa sisi ni watu wa kukataliwa  


Mathayo 7;21-23 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.  Tunaweza tukawahubiri wengine na kuwafundisha lakini sisi tukashindwa kuingia mbinguni Paulo mtume alikataa kuwa mtu atakayewahudumia na kuwahubiri wengine kisha yeye kuwa mtu wa kukataliwa ona 

1Koritho 9;26-27, Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa; bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.”  Yusufu wa Armathaya, masatahiki yeye aliwaza mbinguni Marko 15;43. “akaenda Yusufu, mtu wa Arimathaya, mstahiki, mtu wa baraza ya mashauri, naye mwenyewe anautazamia ufalme wa Mungu; akafanya ujasiri, akaingia mbele ya Pilato akauomba mwili wake Yesu.”

Mifano ya watu wapumbavu ambao hawakuzingatia lengo kuu lenye faida kuu

Mtu yule mkulima tajiri aliyekuwa na lengo kuu la kujenga ghala kubwa la kuweka nafaka na vitu vyake ili apumzike ale kunywa na kufurahia badala ya kuwaza kwanza juu ya uzima wa milele anaitwa na Mungu “mpumbavu” 

Luka 12;16-21. “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”  Mtu mwingine tajiri Yeye aliwaza tu kula kwa anasa siku zote na kuvaa kwa anasa lakini hakuwaza juu ya uzima wa milele Tofauti na masikini lazaro matokeo yake alipokufa alikwenda kwenye mateso ya milele motoni 

Luka 16;19-30.” Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu. Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu.

Yatupasayo kufanya .

·         Kuwa na lengo hili kuu la kuingia mbinguni na kuliweka kuwa la kwanza ya yote mengine Mathayo 6;33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”

·         Kuhakikisha tumetubu dhambi zetu kwa kumaanisha kuziacha ili tupate rehema ya kuingia Mbinguni Mithali 28;13 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”

·         Kuangalia tusianguke dhambini tena 1Koritho 10; 12 ”Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.” na kuhakikisha lolote lile jingine mbali na lengo kuu lenye faida kuu yaani kuingia mbinguni halichukui nafasi ya kwanza, tunaweza tukaitenda kazi ya Bwana lakini tukasahau utakatifu kwanza kutenda kazi huko hakutatusaidia kuiona mbingu.

Preached by Bishop Zachary Kakobe 15 October 1995 my Spiritual Father

Composed by Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

0718990796

Ikamote@yahoo.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni