Jumapili, 8 Novemba 2020

Hamjui yatakayokuwako kesho!

Mstari wa Msingi: Yakobo 4:13-15 “Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi.”


Utangulizi:

Mojawapo ya swali muhimu sana ambalo kila mwanadamu mwenye akili timamu huwa anajiuliza ni kuhusu kesho  “future”  kwamba itakuwaje kesho, nini kinafuata baada ya haya? Nini kinakuja, nini kitatokea wiki ijayo, mwezi ujao, mwaka ujao na wakati mwingine tunaona giza, na kujiuliza je tutakuwa na furaha au tutakuwa na dhuruba? Ni nani anaishikilia kesho yetu? Je napaswa kuwa na matumaini au kuogopa?


Itakuwaje mtihani unaokuja mbele yetu? Tutapata habari gani, itakuwaje matokeo ya uchaguzi wa, nani atashinda na itakuwaje akishinda fulani? Itakuwaje kazini, itakuwaje ndoa yangu, itakuwaje marafiki zangu, itakuwaje familia yangu? Itakuwaje afya yangu? Itakuwaje nikistaafu? Itakuwaje nikiachwa?


Watu wengi sana wanaogopa sana kuhusu maisha yajayo na kwa sababu hii ingawa wanajua umuhimu wa maswali hayo lakini kutokana na hofu au woga kisaikolojia watu wengi huwa wanapotezea swali hili Muhimu ili kupata unafuu na kutuliza maumivu yake, Mungu anajua kwamba swala kuhusu kesho ni swali tata sana kwa wanadamu na hataki tuogope wala kujisumbua hususani tunapokuwa na uhusiano mwema na yeye  Yesu Kristo anawatoa hofu kabisa waaumini wake akitaka jambo hili lisiwasumbue ona


Mathayo 6:31-34 “Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.”


Kwa kuwa Mungu anajua kuwa swala la kesho itakuwaje ni swala zito kwa wanadamu Maandiko yanawafundisha watu wa Mungu namna inavyowapasa kuenenda, watu wenye kiburi na watu wasiomjua Mungu huwa wana uhakika sana na maisha ya kesho kunakosababishwa na majivuno na kiburi.


Neno la Mungu linaonya kujisifu kuhusu kesho!


Watu wasiomjua Mungu huwa na tabia ya kujisifu na kujivuna kuhusu Kesho! Jambo ambalo neno la Mungu limeonya sana kwa njia nyingi na kwa mifano mingi wako watu ambao hujivunia kesho kana kwamba wanajua yatakayotukia kesho Biblia inaonya vikali sana kuhusu maisha yajayo au kuhusu kesho ona Mithali 27:1 “Usijisifu kwa ajili ya kesho; Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja.Wako watu hujivunia kuhusu kesho kana kwamba wana uhakika nayo na wanamuweka pembeni Mungu katika mipango yao na makusudi yake, Neema yake na wema wake  wako watu ambao walisahau kuwa kila kitu na kila jambo liko kwenye mikono ya Mungu, Mungu ana namna yake ya kuwanyoosha watu wenye kiburi


Ø Daniel 4:28-33 “Hayo yote yakampata mfalme Nebukadreza. Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli. Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu? Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako.Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng'ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote. Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng'ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.“

 

Ø Matendo 12:20-23 “Naye Herode alikuwa amewakasirikia sana watu wa Tiro na Sidoni; wakamwendea kwa nia moja, na wakiisha kufanya urafiki na Blasto, mwenye kukitunza chumba cha mfalme cha kulalia, wakataka amani; kwa maana nchi yao ilipata riziki kwa nchi ya mfalme. Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho.


Ø Luka 12: 15-21 “Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”  

 

Ø Mjezi wa Meli ya TITANIC  ambayo ilikuwa meli ya kifahari sana iliyokuwa na viwanja vya mpira, kumbi za starehe na mabwawa ya kuogelea alipoulizwa kuhusu uimara wa meli hiyo alijigamba na kusema hata Mungu hawezi kuizamisha, meli hii ilizama siku ya nne tu tangu ilipoanza safari kutoka Uingereza baada ya kugonga mwamba wa barafu katika bahari ta Atlantic  mnamo asubuhi ya tarehe 15/04.1912, Meli hii ilikuwa na abiria wapatao 2240 na kati yao zaidi ya 1500 walipoteza maisha, hatujui kesho yetu, kila aina ya kile tunachokifikia duniani hatuna budi kukumbuka kuwa ni kwa neema ya Mungu tu!


Mifano hii yote katika Biblia imeandikwa ili kutuonya sisi wanadamu ya kwamba hatuna kesho, kujilimbikizia mali na kuwa na choyo hakuongezei uzima wetu duniani, kila aina ya mafanikio tuliyionayo hayatokani na uwezo wetu ni neema ya Mungu  na wema wake ona Paulo mtume ndiye mtume aliyefanya kazi kubwa kuliko mitume wote lakini wakati wote alikumbuka kuwa alifanya chini ya neema ya Mungu na sio uwezo wake ona  1Wakoritho 15:10 “Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.Tunapaswa kuhakikisha kuwa tunaitegemea neema ya Mungu na kumtukuza yeye katika kila jambo na kumtanguliza yeye, kila mmoja anapaswa kuhakikisha anajilinda na kiburi kwa vile maisha hayako katika mikono yetu! Na Hatujui yatakayokuwako Kesho!


Hamjui yatakayokuwako kesho! 


Hakuna ajuaye kesho, Kesho iko katika mikono ya Mungu, Mungu anajua yote kuhusu kesho, Mungu anajua kila kitakachotokea anajua kitakachotokea kesho, wiki ijayo, mwezi ujao na miaka ijayo kwa hiyo kesho iko katika mikono ya Mungu Isaya 46:9-10 “kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.” Mungu anautangaza mwisho tangu mwanzo, Mungu anakujua na wewe nawe anajua unayoyahitaji anajua utakuwa nani anajua atakayeolewa na wewe anajua utakayemuoa anajua utakuwa na watoto wangapi anajua mwanzo na hata mwisho wa maisha yetu, alitambua mwisho wa Yusufu na kuutangaza kwa njozi kabla,  Mungu alikuwa anajua kuwa mavazi ya Yesu yatapigiwa kura miaka 1000 kabla ya Yesu Daudi alitabiri kitakachompata Yesu ona Zaburi 22:18 “Wanagawanya nguo zangu, Na vazi langu wanalipigia kura.” na Mathayo 27:35 “Walipokwisha kumsulibisha, waligawa mavazi yake, wakipiga kura; [ili litimie neno lililonenwa na nabii, Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura.]”  Mungu anaweza kutuambia hata leo akitaka kuhusu kesho yetu na hivyo kama tunamtegemea na kumuamini tunapaswa kuwa na unyenyekevu na kumtegemea yeye na kumtanguliza yeye na kumuomba yeye, Kesho yetu iko mikononi mwa Mungu hatupaswi kusahau hilo yeye amakuwepo tangu mwanzo na yuko hata milele, Yesu ni yeye yule jana leo na milele anajua kila kitu kitakachotokea  na anampango mwema kwa aajili ya kila mmoja anayemtanguliza na kumtegemea yeye Warumi 8:28-30 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.” 


Mkumbuke Mungu katika mipango yako yote. 


Ni muhimu kufahamu kuwa maandiko yanatufundisha kwamba tunapaswa kumtanguliza Mungu mbele katika kila jambo, katiia mipango yetu maono yetu ndote zetu na kazi zetu tunapaswa kumuomba Mungu na kumtanguliza yeye na hatupaswi kuzitegemea na kujivunia akili zetu wenyewe, Watu wenye kiburi hawa na choyo wadhalimu hujisifia tama zao na hawataki kumkumbuka wala kumtanguliza Mungu kwa namna yoyote ile Zaburi 10:2-3 “Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza. Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake, Na mwenye choyo humkana Bwana na kumdharau.” 


Na. Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima !

0718990796

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni