Jumapili, 17 Januari 2021

Wapandao kwa machozi watavuna kwa kelele za furaha!

Zaburi 126:1-6Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni, Tulikuwa kama waotao ndoto. Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko, Na ulimi wetu kelele za furaha. Ndipo waliposema katika mataifa, Bwana amewatendea mambo makuu.  Bwana alitutendea mambo makuu, Tulikuwa tukifurahi. Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa, Kama vijito vya Kusini. Wapandao kwa machozi Watavuna kwa kelele za furaha. Ingawa mtu anakwenda zake akilia, Azichukuapo mbegu za kupanda. Hakika atarudi kwa kelele za furaha, Aichukuapo miganda yake.”

Utangulizi:

Zaburi ya 126 ni mojawapo ya zaburi zilizoitwa zaburi za kupandia yaani ziliimbwa wakati watu wanapanda kwenda nyumbani mwa bwana Hekaluni aidha pia ni zaburi ya kihistoria inayoelezea maisha  ya wana wa Israel hususani Wayahudi waliorudi kutoka uhamishoni Babeli, Wayahudi hao walichukuliwa mateka wakati wa Mfalme Nebukadreza kwa kusudi la kuwatumikisha hivyo waliishi uhamishoni kama watumwa walifanyishwa kazi kwa faida ya taifa la wakaldayo, Hata hivyo baada ya miaka kadhaa kupita Mungu aliwajia tena watu wake na kuwaletea ukombozi, yaani walirejea katika nchi yao kwa amri ya mfalme Koreshi, makundi matatu ya wayahudi walirejea nyumbani kundi la Kwanza wakati wa Zerubabel na kundi la pili wakati wa Ezra na la tatu wakati wa Nehemia  hivyo inaaminika kuwa zaburi hii inaaminika iliimbwa na wana wa Asafu waliorejea kutoka uhamishoni wakati wa Ezra ona

Ezra 2:1-2, 41. “1. Basi hawa ndio wana wa wilaya, waliokwea kutoka katika ule uhamisho wa hao waliokuwa wamechukuliwa, ambao Nebukadneza, mfalme wa Babeli, aliwachukua mateka mpaka Babeli, nao wakarudi Yerusalemu na Yuda, kila mtu mjini kwake; 2. ndio hawa waliokuja pamoja na Zerubabeli, Yoshua, Nehemia, Seraya, Reelaya, Mordekai, Bilshani, Mispari, Bigwai, Rehumu, na Baana. Hii ndiyo hesabu ya wanaume wa watu wa Israeli; 41 Waimbaji; wana wa Asafu, mia moja ishirini na wanane.”


Wimbo huu ulijulikana kama wimbo wa kupandia yaani wayahudi walikuwa wakiuimba kila wakati walipokuwa wakipanda kwenda Yerusalemu kuabudu Hekaluni,  Kumbuka kuwa Nyumba ya Mungu yaani Hekalu lilijengwa juu yam lima yaani sayuni na hivyo mara kwa mara mtu alipoenda nyumbani kwa Bwana ilikuwa ni kama anapanda, Zaburi hii ilitungwa na wana wa Asafu wakati wa Ezara  na wimbo huu ulitumika katika maeneo makuu matatu kushukuru, kuomba na kutia moyo

1.       Kama njia ya kumshukuru Mungu kwa wale waliokuwa wamerejea kutoka utumwani  kwamba Mungu alikuwa amewatendea mambo makubwa sana amewakomboa amewapa uhuru, nyakati za ukoloni wa kizamani mataifa yenye nguvu walipowateka watu waliwachukua kuwa watumwa katika nchi zao, ni watu wa ulaya kama Wayunani na warumi ndio walioanzisha iana ya utumwa au utawala wa kumtawala mtu katika taifa lake lakini wakaldayo na mataifa ya kale waliua watu na wengine waliwahamisha  hivyo kurudi nyumbani hasa wayahudi  kurudi Israel kwao ni Muujiza mkubwa sana ni kurudi katyika uwepo wa Mungu ni jambo la kushangaza mataifa hivyo katika zaburi hii wanashukuru kurejea nyumbani

Zaburi 126:2-3
unaonyesha “Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko, Na ulimi wetu kelele za furaha. Ndipo waliposema katika mataifa, Bwana amewatendea mambo makuu. Bwana alitutendea mambo makuu, Tulikuwa tukifurahi.


2.   Aidha wimbo huu pia ulitumika kuwaombea dua na kuwatia moyo  na kuwataka wale ambao bado walikuwa wamesalia huko utumwani kuendelea kumuomba Mungu ili nao waweze kutoka katika utumwa  walikumbuka kuwa wako ndugu zao ambao bado hawajarejea hivyo walitoa wito na kumsihi Bwana awarejeza ndugu zao walioko kifungoni utumwani nchi ya mbali  ona   

       Zaburi126:4Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa, Kama vijito vya Kusini.”

3.  Na eneo la tatu lilitumika kuwatia moyo watu wote waliokuwa wanapitia shida za aina yoyote na changamoto za aina yoyote katika maisha kuwa maisha yao wanayoyapitia ya aina yoyote ile yanafananishwa na maisha ya mkulima na kuwa mtu awaye yote anapopitia taabu na machungu ya aina Fulani ni lazima aelewe kuwa wakati huo katika maandiko unafananishwa na wakati wa kupanda, kupanda kunajumuisha maandalizi ya shamba, kulima na kukatua ardhi  na ujuzi wa nyakati kwamba mvua zitaanza lini? huu ni wakati wa taabu na shida ambayo inahitaji uvumilivu  na kwa kweli wakati wa kuandaa shamba mpaka kupanda ndio wakati Mgumu sana kwa mkulima kuliko wakati wa kuvuna, wakati wa kuandaa shamba na kupanda wakulima wengi hawaonekani mjini wala nyumbani, wanaamka mapema sana kwenda shambani ili walime kabla jua halijawa kali, wakulima hupata taabu sana wanapojiandaa kupanda kwa huku wakijua kuwa uko wakati watafurahia mavuno hivyo kipindi hiki ni kipindi cha machozi.  Wana wa Asafu wanafananisha kipindi cha kupanda kama kipindi cha machozi na wakati wa kuvuna kama wakati wa furaha,  ona

Zaburi 126:5-6 Wapandao kwa machozi Watavuna kwa kelele za furaha.Ingawa mtu anakwenda zake akilia, Azichukuapo mbegu za kupanda. Hakika atarudi kwa kelele za furaha, Aichukuapo miganda yake.”

Ni muhimu kufahamu hili kuwa maisha ya mwanadamu yana nyakati tofauti tofauti na kila wakati una umuhimu wake na wakati mwingine wakati mmoja una maana sana kwaajili ya wakati mwingine na kila wakati ni muhimu mno  kwa msingi huo ni muhimu kufahamu majira na nyakati ili uweze kujipanda vema kujua kuwa wakatio huu ni wa kupanda au wa kuvuna ukichanganya nyakati utapata tabu sana !  huwezi kuishi maisha ya mavuno wakati wa kipindi cha kupanda ukifanya hivyo utapata hasara kubwa sana ona

Muhubiri 3:1-8 “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa; Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga; Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza; Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia; Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa; Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena; Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani.”

Maisha yetu yanapofananishwa na nyakati zozote za taabu katika Biblia wakati huo unafananishwa na wakati wa kupanda “it’s a labour time” ni wakati wa taabu ni wakati wa subira ni wakati wa uvumilivu, wakulima huwa wanajitoa muhanga sana wakati wa kupanda yaani kuandaa mashamba kukatua ardhi huku wakivizia wakati sahihi wa kufanya hivyo, sasa wanadamu wenye akili timamu wanapaswa kujua ni namna gani watacheza au wataenenda na mapigo ya huo wakati, huwezi kuishi wakati wa kupanda kama ndio wakati wa kuvuna ni lazima ujue nyakati kwani wakati mmoja hutengeneza wakati mwingine, mtu akiishi kwa anasa wakati wa kupanda atakuwa na msiba wakati wa mavuno, maana wenzake walivumilia wakajitoa kupanda hivyo wakati wa mavuno watafurahi, wakati wa kupanda ni wakati wa subira na uvumilivu wala sio wakati wa kupendeza, maandiko yanavyotuasa wakati wote tutapopitia changamoto zinazotuonyesha kuwa ni kama tuko katika wakati wa kulia, au tuko katika wakati wa kufanya kazi  ni wakati ambao unahitaji uvumilivu kwani hatimaye Mungu ataleta mvua na mazao yatakua na tutavuna kwa furaha kubwa on

Yakobo 5:7-8,,10 -11 “7. Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. 8. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia.10-11 “10. Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu.11. Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”

Kimsingi neno la Mungu linatujuza kuwa uko wakati Mungu atatutendea mema, jambo kubwa la msingi ni kujua nyakati ni kuwa na hekima na ujuzi kwamba wakati huu ni wakati wa  namna gani na ni jambo gani tunapaswa kulifanya  tusiishi kizemba kumbuka  katika Israel kulikuwa na Kabila moja waliojulikana kama wana wa Isakari hawa waliitwa watu wenye akili sana na kazi yao kubwa walikuwa ni watu wenye kujua nyakati sio tu kujua nyakati bali pia kujua jambo gani linapaswa kutendeka kwa wakati huo ona

1Nyakati 12:32 “Na wa wana wa Isakari, watu wenye akili za kujua nyakati, kuyajua yawapasayo Israeli wayatende; vichwa vyao walikuwa watu mia mbili na ndugu zao wote walikuwa chini ya amri yao
”. 

Kila mmoja wetu anapaswa kujua nyakati na kuwa na akili kama wana wa isakari kujua nini kinatupasa kutenda kwa wakati, mwezi januari mpaka machi ni miezi muhimu sana kwa wanafunzi na walimu kujipanga kufundisha kwa bidii na kujifunza kwa bidii  katika wakati huu wa mwanzo kama hatutajua yatupasayo kufanya tukajifanya tunacheka na kumbe ni wakati wa kulia  tunaweza kujikuta tunakosea, mkulima anapaswa kujua wakati huwezi kupanda wakati wa hari, kama mwanafunzi anataka kustarehe wakati anajua wazi ni wakati wa kujisomea kwa bidii wakati wake wa mavuno utakuwa wakati wa majuto matokeo yatakapotoka anaweza kulia badala ya kufurahi kwa vile hakufahamu ni wakati gani alipaswa kusoma kwa bidii, wote tunajua kuwa ni mbaya sana mwanafunzi kuja na simu shuleni, wazazi pia wanapaswa kufahamu, unampa mtoto simu aje nayo shuleni atasomaje? Hii ni sawa na kuutumia wakati vibaya au kutokujua wakai na jambo la kufanya kwa wakati huo, huwezi kuchanganya masomo na mapenzi, au uvutaji wa bangi na tabia za ajabu ajabu wakati ukiwa mwanafunzi au kutumia ulevi au kufanya biashara ni dhahiri kuwa huo sio wajati wa kufanya hayo kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa kuna wakati wa kupanda wakati huu huwa kama wakati mchungu lakini kuna wakati wa kuvuna huu ni wakati ambapo tutayafurahia matunda ya kazi zetu, tunapoanza shughuli za kila aina mwanzoni mwa mwaka huu basi na tufanye kazi kwa bidii sana kama tupandao,lipa ada ya shule kama uliila wakati wa disemba hukujua kuwa kuna januari hukutofautisha wakati wa kupanda na wakati wa kuvuna? Ahaa ulivuna kabla ya kupanda sisi tutakudai ada ya shule tu!  Wakati ukiwa shuleni mwanafunzi  tujisiomee kwa bidii, tuhudhurie kazini kwa bidii, tuombe na kufanya ibada na  kila lililowajibu wetu kwa bidii tukijua wazi kuwa wapandao kwa machozi watavuna kwa kelele za furaha  na Mungu atatupa wakati wa faraja hatatuacha tuumie tu atakuwa pamoja nasi na tutafurahia uwepo wake kwa nguvu na ushujaa mwingi ataleta mvua yaani neema atayakuza mapando yetu na atatupa wakati wa mavuno, wakati wa matokeo mazuri, wakati wa kuvuna kwa hiyo ni muhimu kwetu tunapoendelea na wiki hii ya kazi ndani ya mwaka huu 2021 tujitoe kwa ngubvu zetu zote tukijua ya kuwa wapandao kwa machozi watavuna kwa kelele za furaha !   .

Wimbo wa Marehemu Fanuel sedekia unatukumbusha umuhimu wa kujua Majira na nyakati na kuzitumia kwa utukufu wa Mungu:-

Nitaimba haleluya asubuhi, nitaimba haleluya Mchana, nitaimba haleluya jioni haleluya na hata usiku X2, Muhubiri anasema kila jambo na wakati wake; wa kupanda na kuvuna wa kulia na kucheka x2  Haleluya nina wimbo; wa kila  wakati na kila majira wimbo wa nyakati zote na marira yote;  wimbo huo ni Haleluya Nitaimba haleluya asubuhi, nitaimba haleluya Mchana, nitaimba haleluya jioni haleluya na hata usiku X2,  – Fanuel Sedekia

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima       

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni