Alhamisi, 29 Aprili 2021

Atakaye kupenda Maisha

1Petro 3:10-12Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana. Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu; kwamba ni vigumu sana kuyapenda maisha hususani nyakati ambazo tunapitia maswala magumu, watu wengi wanapopitia nyakati ngumu sana katika maisha yao huwa wanatamani kufa na au wanakata tamaa kabisa hata kufikia hatua ya kufikiri kuwa Mungu hawajali na kujishughulisha tena na maisha yao, Je umewahi kupitia maswala magumu sana katika maisha hata kufikia ngazi ya kukata tamaa na kutamani kufa  au kufikiria kuwa Mungu hakujali? watu wengi wamewahi kufikiri hivyo, hata mimi pia katiika vipindi Fulani mbalimbali,  maisha sio kitu rahisi lakini maisha ni ya muhimu sana, maisha yana changamoto nyingi sana lakini bado maisha yanabaki kuwa ni ya muhimu mno!.  Mtume Petro anawaandikia Wakrito ambao walikuwa wanapitia nyakati za Mateso na nyakati ngumu sana na anatoa ushauri unaokwenda sambamba na Zaburi  iliyoandikwa na Mfalme Daudi kuhusu Maisha:-


Zaburi 34:12-16 “Ni nani mtu yule apendezwaye na uzima, Apendaye siku nyingi apate kuona mema? Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila. Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.”


Petro anaunga mkono kile kilichosemwa na Daudi au anahubiri kitabu cha zaburi ya 34:12-16 akionyesha ni namna gani watu wa Mungu wanapopita katika magumu wanapaswa kuyatazama maisha, Petro pamoja na Daud mwandishi wa Zaburi wanatutia moyo kuwa na imani kwa ahadi za Mungu wakati wote hata wakati tunapopitia changamoto za aina mbalimbali katika maisha  na kuendelea kuyapenda maisha ili Mungu atukuzwe wakati wa Magumu yetu, tunaonyesha ukomavu na imani badala ya kuchukizwa nayo kama ilivyokuwa kwa Suleimani mwandishi wa kitabu cha Muhubiri ambaye aliyaiona maisha kuwa jambo lisilo na maana na hasa maisha ya mtu wa kawaida asiye na imani huyaona maisha kama kujilisha upepo, Maisha yana maana kubwa sana hata pamoja na magumu unayoyapitia! Hivyo hatuna budi kuyapenda:-


Petro anaona kuwa ziko kanuni ambazo angaweza kutushauri wote tunaoishi bila kujali kuwa tunaishi katika mazingira mazuri au mabaya kiasi gani lakini Maisha ni zawadi ni neema ambayo Mungu ametupa hivyo wakati wote tuwapo duniani, tunapaswa kumshukuru Mungu kwa imani sasa katika kanuni hizo Petro anatuasa kwanza


1.       Kuuzuia ulimi usinene mabaya !

 

Ni muhimu kufahamu kuwa ulimi ndio kiungo chepesi zaidi kutumika katika maisha ya mwanadamu,  mtu mwenye ukomavu na busara au mtu mkamilifu ni yule mwenye uwezo wa kujua namna na jinsi ya kuutunza Ulimi, na kuutumia Biblia inaonyesha ya kuwa kiungo hiki kinabeba mamlaka kubwa sana katika maisha yetu ikiwa ni pamoja na uzima na mauti ona Mithali 18:20-21 “Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.” Kwa haraka sana ni ulimi ndio unaoweza kutubadilishia hali ya ulimwengu wetu kuwa wa furaha au wa amani, kuyatawala mazingira ama kutawaliwa kutengeneza hali ya hewa au kuiharibu, kunung’unika au kushangilia mwenendo wetu mbele za Mungu na wanadamu unaweza kuathiriwa au kuwekwa sawa kwa ulimi! Maneno ni silaha yenye nguvu sana inayoweza kuinua watu au kuwaharibu watu! Patro ananyesha wazi kuwa tunaweza sana kujizuia maisha yetu na dhuruba za ulimwengu kama endapo tu tutaweza kuzuia ndimi zetu ona Mithali 21:23 “Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu.” Uwezo wa kuchagua nini cha kuzungumza na nini cha kutokuzungumza uko katika uchaguzi wetu, lakini wakati wote ni muhimu sana kukumbuka namna na jinsi tunavyoutumia ulimi, Ni vigumu sana kumsoma na kumjua kwa undani mtu asiyezungumza, mara tu unapozungumza ndipo watu wanapoweza kukujua wewe ni nani nani mtu wa namna gani, Maneno yetu yanafichua kile kilichoko ndani yetu  Moja ya hukumu watakayohukumiwa wanadamu mbele za Mungu ni pamoja na kile wanachokizungumza Mathayo 12:33-37 “Ufanyeni mti kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri; au ufanyeni mti kuwa mbaya na matunda yake mabaya, kwa maana kwa matunda yake mti hutambulikana. Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya. Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa.” Ni kutokana na hekina na ujuzi wake Petro kuhusu Maisha yeye anaona ni vema kutuasa kutikunena na hasa kunena mabaya, kila mtu mwenye hekima anapaswa kujua yampasayo kunena na ikiwezekana azungumze maneno ya kujenga sio mabaya au yenye hila ndani yake, Dhambi nyingi tunazozifanya na namna tunavyowazunguzia watu kwa wema au kwa ubaya kwa kujenga au kwa kuibomoa tunatumia ulimi, karibu kila iana ya dhambi ni lazima itauhusisha ulimi, kwa msingi huo Daudi na Patro wanatutaka sisi kuutumia ulimi kuleta uponyaji duniani na sio kuharibu Mithali 12:17-19 “ Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo hutamka hila. Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; Bali ulimi wa mwenye haki ni afya. Mdomo wa kweli utathibitishwa milele; Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.” Kama hakuna sababu ya kuzungumza ni vema kutokuzungumza kuliko kuzungumza maneno ya kubomoa, kuna thawabu kubwa sana Mbinguni kwa watu wa Mungu ambao watakuwa na ujuzi wa namna na jinsi ya kuutumia ulimi, na ni vema vile vile kwa pamoja tukiwa tunatafakari na kujadili mambo yaliyo mazuri, yaliyo ya staha, yenye kujenga , yenye wema, yenye kupendeza, yenye sifa nzuri hayo ndio maswala ya kuyajadili na ndivyo neno la Mungu linavyotutaka Wafilipi 4:8 “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.”        Tukitafakari mambo mema tutazungumza mambo mema na tutaufanya ulimwengu uwe mahali pema pa kuishi na vilevile katika maisha yajayo baada ya kufa tutakuwa na wakati mwema na Mungu, kwa msingi huo basi kanuni ya kwanza ya kutufanya tuishi maisha mazuri  na kuufurahia uumbaji wa Mungu na kuona siku njema ni kuzungumza mambo mazuri yaliyo mema kwa msingi huo basin i vema mno tukaangalia kile Daudi alikisema na kile ambacho Petro alikihubiri kwamba kama tunapenda maisha na kutaka kuwa na siku njema katika kipindi hiki kifupi sana ambacho Mungu ametupa kuwepo duniani basi ni vema tunayapokea maisha kwa shukurani, kwa tabia njema tukiwa tumejaa neema na kuhakikisha kuwa tunawajenga wengine kwa utukufu wa Mungu baba! Matumizi ya ulimi yanatujengea kanuni kubwa na njema na nzuri ya kuyafurahia maisha kwa hiyo kuna umuhimu wa kujilinda na kujihami tusinene mabaya, tusihukumu kwa haraka na kuhakikisha kuwa tunatenda mema, Neno la Mungu linatutaka kwamba hata kama tunaishi katika nyakati ambazo kila mtu anazungumza mabaya ni wakristo pekee na watu weme na wenye hekima wanaoweza kuufanya ulimwengu kuwa mahali pema kwa kuzungumza maneno mema na mazuri ya neema na tukatae kabisa kutumika kama chombo cha shetani kwa kuuujaza ulimwengu maneno mabaya hata kama tunapitia mambo magumu Wakolosai 4:5-6 “Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.” Tunapozungumza haya unaweza kujiuliza kwamba sasa nitafanyaje maana huenda mimi niko miongoni mwa watu wenye midomo michafu sana yaani katika watu ambao wana majibu mabaya mimi nimo, katika watu ambao wanajua kunya kwa mdomo, wanajua kutema vyondo na mimi nimo na sasa nimeyaharibu maisha yangu kwa kuzungumza yasiyopaswa nawezaje kuwa mwema tena? Usiogope kama uliutumia ulimi wako vibaya kabla hatujafika katika hatua nyingine yako mambo muhuimu ya kufanya :-

 

a.       Muombe Mungu akutakase Moyo wako, akili zako na maneno yako:

 

Ni vigumu kuishi maisha matakatifu na kumpendeza Mungu kama maneno yetu ni mabaya meneno yetu ni kipimo ya kile kilichoko moyoni mwetu, akilini kwetu na ndio huwa kinadhihirishwa kwa kusema kwetu ona Luka 6:45 “Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.”  Yesu anaonyesha wazi kuwa kile tunachokinena ni matokeo ya kile kilichoko moyoni, Kwa msingi huo basi hatuna budi kumuomba Mungu atusafishe na kututakasa, mioyo yetu, akili zetu na maneno yetu, Mungu akitusamehe na kutusafisha maneno yetu yatakuwa na nguvu ya kuumba mambo mema kwaajili ya Mungu Ona Isaya 6:1-7 “Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka. Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake. Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi. Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa.” Isaya ni nabii aliyetumiwa sana na Mungu, Lakini kabla ya kutumwa alijitakasa alitubia uovu wake na Mungu akamtakasa kinywa chake na ndipo akamtumia, hatuna budi kuhakikisha kuwa tunaomba na kujitakasa ili kwamba Mungu aweze kuyalinda mawazo yetu na kutulinda na uharibifu. Kumbuka kwamba tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mungu aliuumba ulimwengu huu kwa neno tu na mara kadhaaa laifanya miujiza kwa kutamkqa neno ona Mwanzo 18:10-14 “Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? BWANA akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume.” Unaweza kuona Mungu hapa anatamka neno na lile neno linakuwa kama vile alivyotamka, sisi nasi tumeumbwa kwa mfano wake Mungu akikitakasa kinywa chetu na kujifunza nidhamu ya kutunza kinywa tutakuwa na mamlaka katika matamshi yetu nan a kusababisha uumbaji, mimi ni Mwalimu pia wa chuo cha Biblia chuo cha Biblia kibiblia huitwa chuo cha manabii, hivyo nafundisha manabii pia ni Mwalimu wa manabii ili nabii aweze kuwa na mamlaka anapaswa kuwa na kinywa safi ili kinywqa cheke kiwe na mamlaka na ndio maana kabala Mungu hajamtumia nabii isaya alimtakasa kinywa cheke kisha akaweka neno lake hivyo isaya akatabiri mambo mengi kuhusu masihi na yakatimia, Manabii wengi walikuwa wakijitunza vinywa vyao na hivyo vinywa vyao vikawa na mamlaka kubwa sana ona, Nabii Elisha alitamka tu kama Mungu alivyomtamkia Sara na kile alichokinena kikatimia  2Wafalme 4:16-17 “Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa Mungu, usiniambie mimi mjakazi wako uongo. Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto mume wakati uo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia.”Elisha anatufundisha kuwa tunaweza kutamka kitu kama Mungu nqa kikawa vilevile kwaajili ya hayo tujnaina kuwa kuna umuhimu mkubwa sana wa kuomba kutakaswa ili kwamba vivywa vyetu viweze kuwa na mamlaka ona 1Wafalme 17:1 “Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.” “2 Wafalme 6:24-30 “Ikawa baada ya hayo, Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya majeshi yake yote, akakwea akauhusuru Samaria. Njaa ikawa kuu huko Samaria; na tazama, wakauhusuru, hata kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa vipande themanini vya fedha, na kibaba cha mavi ya njiwa kwa vipande vitano vya fedha. Ikawa mfalme wa Israeli alipokuwa akipita ukutani, mwanamke mmoja akamwita akisema, Unisaidie, bwana wangu, mfalme. Akasema, Bwana asipokusaidia, nikusaidieje mimi? Ya sakafuni, au ya shinikizoni? Mfalme akamwambia, Una nini? Akajibu, Mwanamke huyu aliniambia, Mtoe mtoto wako, tumle leo, na mtoto wangu tutamla kesho. Basi, tukamtokosa mtoto wangu, tukamla; nikamwambia siku ya pili, Mtoe mtoto wako, tumle; naye amemficha mtoto wake.  Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya huyo mwanamke, aliyararua mavazi yake; (naye alikuwa akipita juu ya ukuta;) na watu wakaona, na tazama, alikuwa amevaa magunia ndani mwilini mwake.Tatizo la Njaa hapa lilikuwa kubwa sana mpaka yakatokea hayo yaliyotokea lakini Elisha alitamka neno la matumaini ambalo ni vigumu kuamini kuwa linaweza kutokea katika mazingira kama yale lakini kwakuwa kinywa chake kilikuwa na mamlaka Mungu aliweza kutekeleza kile alichokisema ona 2 Wafalme 7:1-2 “Elisha akasema, Lisikieni neno la Bwana; Bwana asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria. Basi yule akida, ambaye mfalme alikuwa akitegemea mkono wake, akamjibu yule mtu wa Mungu, akasema, Tazama, kama Bwana angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akamwambia, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula.”  Hali kama hii hata sisi tunaoishi zamani za siku hizi zama za agano jipya tunaweza kabisa kutumia ndimi zetu kwa mamlaka makubwa endapo tutakubali Mungu atutakase ndimi zetu na kututuimia Matendo 3:6 “Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende.” Kwa msingi huo tunaona kuwa kuna faida kubwa sana kuwa na nidhamu kwa kutunza ndimi zetu na kutakaswa kwa ndimi zetu ili kwamba vinywa vyetu viweze kutumiwa na Mungu kwa mamlaka iliyokubwa zaidi, hata Pepo huwa wanatii watu wanaojua kutumia vinywa vyao vyema .

 

 

b.      Omba kwamba Mungu ailinde dhamiri yako:

 

Ni muhimu kuyapima maneno yetu kabla ya kuyazungumza, Ni muhimu kwetu kumuomba Mungu azilinde dhamiri zetu ili kwamba wakati wote tukusudie kuzungumza mambo mazuri wakati wote tunapokusudia kuzungumza na kama ni mazingira ambayo hatupaswi kusema lolote itakuwa vema basi tukanyamaza au kumuomba Mungu atulinde vinywa vyetu ona Zaburi 19:14 “Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.” Mara kwa mara wanadamu tunapenda, na kulalamika hususani mbele ya rafiki zetu, wanfanyakazi, wanafunzi, wageni na kaedhalika kwa kawaida hakuna mwanadamu anayefurahia kimsingi kusikia malalamiko yetu, malalamiko huinajisi mioyo, kwa msingi huo ni vema sana tukazuia vinywa vyetu lakini kwa kuwa hatuwezi basin a tumuombe Mungu kama mwandishi wa zaburi ili kwamba Mungu atusaidie kila tunalolizungumza lipate kibali mbele za Mungu!, Watu wengi sana wanafikiri kuwa Musa hakwenda kanaani kwa sababu aliupiga mwamba hapana Musa alizunguimza yasiyofaa Zaburi 106:32-33 “Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, Hasara ikampata Musa kwa ajili yao, Kwa sababu waliiasi roho yake, Akasema yasiyofaa kwa midomo yake.” Wana wa Israel kwa sababu ya kunungunika kwao mara kwa mara walimkosesha Musa na kumfanya Musa kutamka mambo yasiyofaa na kwa sababu hiyo, hakuruhusiwa kuingia Kanaani.


Ni muhimu kukumbuka kuwa maandiko yanatuambia katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu kwa msingi huo ni muhimu kumuomba Mungu atupe akili ya kijizuia Mithali 10:19 “Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.” Kama wewe ni mropokaji sana katika maneno ni muhimu sana kumuomba Mungu akuwekee walinzi katika kinywa chako maneno yasikuchomoke tu kama risasi katika bunduki iliyokwisha kutenguliwa kitufe Zaburi 141:1-3 “Ee Bwana, nimekuita, unijie hima, Uisikie sauti yangu nikuitapo.  Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba, Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.  Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.” Unaweza kuona mfano kwa watakatifu waliotutangulia walijua hatari ya kuropoka walitaka Mungu aweke mngojezi katika vinywa vyao, sisi nasi hatuna budi kumuomba Mungu aweke walinzi kwenye vinywa vyetu

 

c.       Tujifunze kuzungumza maneno ya kujenga:

 

Neno la Mungu linatufundisha ya kuwa tunaweza kutumia vinywa vyetu kujenga, na hilo ndilo kusudi kubwa la Mungu kutuweka Duniani, Biblia inaonya kuwa haifai kuzungumza maneno ya kubomoa, ulimi unafananishwa na chemichemi, hakuna chemichemi moja inayoweza kutoa aina mbili za maji yaani kama ni maji ya chumvi itakuwa ya chumvi na kama ni maji matamu itakuwa maji matamu ona Yakobo 3:10-11 “Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo. Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu?”  Yakobo anataka kama tunazungumza jambo basi tuzungumze kwa kusudi la kujenga, kwa msingi huo uko umuhimu wa kumuomba Mungu atuongoze na kutusaidia ili tuzungumze maneno ambayo yatamjengea heshima yeye  Waefeso 4:29 “ Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.”  Kumbe tunapaswa kuzungumza maneno mema yanayomfaa mwenye uhitaji kufaa mana yeke kujenga kutia ujasiri, kutia moyo, kuleta tumaini, kuwatoa watu kwenye maumivu, kuwaendeleza kuwahuisha na kuwainua,wakati wote tujihadhari na mambo ushirika au maneno yatakayoharibu 1Wakoritho 15:33 “Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.” Aidha biblia inatutaka tusiwe watu wa mizaha kupitiliza Mithali inaonya kuwa kuna hukumu ambazozimewekwa tayari kwa wenye mizaha Mithali 19:28-29 “Shahidi asiyefaa kitu hudhihaki hukumu, Na vinywa vya wasio haki humeza uovu. Hukumu zimewekwa tayari kwa wenye mzaha; Na mapigo kwa mgongo wa wapumbavu.”    Biblia inatufundisha kuwa wako vijana 42 ambao walipomuona nabii Elisha ambaye alikuwa na upaa walimchokoza kwa kumtania  na akachukizwa na jambo hilo kiasi ambacho nabii aliweza kuamuru Dubu ambaye aliwararua vijana wale ona 1Wafalme 2:23-24 “Akakwea kutoka huko mpaka Betheli; naye alipokuwa akienda njiani, wakatoka vijana katika mji, wakamfanyizia mzaha, wakamwambia, Paa wewe mwenye upaa! Paa wewe mwenye upaa! Akatazama nyuma akawaona, akawalaani kwa jina la Bwana. Wakatoka dubu wawili wa kike mwituni, wakawararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao.Kwa msingi huo tumeona kwa mujibu wa Petro kuwa ili mtu aweze kufurahia maisha na kuona siku njema anapaswa auzuie ulimi wake usinene mabaya au midomo yake isiseme hila na kwamba ni vema kutumia ulimi kwa kuijenga jamii hapo tutayafurahia maisha.

 

2.       Na midomo yake isiseme hila!

 

Mojawapo ya tabia ambazo zimeumiza watu wengi sana duniani ni pamoja na hila au kutenda hila au kusema hila Biblia ya kiingereza imetumia neno GUILE kuzungumzia hila ambalo tafasiri zake ni pamoja na Deceit, au cunning ambalo maana yake ni mbinu za kudanganya, au kwa lugha nyingine ni kufanyiwa utapeli, udanganyifu, ujanja wenye nia ya kudanganya Biblia ya Kiswahili inatumia neno hilo HILA, Mungu anapendezwa sana na mtu ambaye hana hila ona Zaburi 32:1-2 “Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake. Heri Bwana asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni mwake hamna hila.” Kristo Yesu alipokuwa akiwachagua wanafunzi wake alimuona mmoja wa wanafunzi wake akija na alimsifia kuwa ni Myahudi kwelikweli ambaye hakuna hila ndani yake ona Yohana 1:47-48 “Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake. Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona.” 


Sasa basi ili tuweze kuyafurahia maisha neno la Mungu linatuonya kuwa tujihadhari na hila katika maisha yetu, tuhakikishe kuwa rohoni mwetu hakuna hila ili tuweze kumpendeza Bwana, Yakobo ni mfano wa mtu aliyekuwa na hila, jina lake pia maana yake ni mwenye hila alitumia hila kumlaghai kaka yake Esau ili kupata haki ya uzaliwa wa kwanza ona Mwanzo 25:29-34 “Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana. Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu. Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.” Licha Yakobo kufanya hila kuupata haki ya mzaliwa wa kwanza pia alitumia hila kupata Baraka kutoka kwa baba yake, Mwanzo 27:19-20 “Yakobo akamwambia babaye, Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama ulivyoniambia. Ondoka, tafadhali, ukae kitako, ule mawindo yangu, ili roho yako inibariki. Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna hii, mwanangu? Akasema, Kwa sababu BWANA, Mungu wako, amenifanikisha.”  Hata hivyo Hila alizokuwa nazo zilimtokea puani katia maisha yake, aliishi maisha ya kudanganywa nay eye kwa miaika Mingi sana kazi kubwa ilifanyika ya kumbadilisha kutoka kuacha hila na kuwa Israel, ni kweli hila zinaweza kukufanikisha kwa kitambo na kutupa kile tunachofikiri itatupa Lakini Mungu kwa namna yoyote ile hawezi kukubali kuibariki hila na mwisho wa siku lazima tuvuine kile tulichokipanda Mwanzo 29:16-26 “Labani alikuwa na binti wawili, jina la mkubwa ni Lea, na jina la mdogo ni Raheli. Naye Lea macho yake yalikuwa dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri uso. Yakobo akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo. Labani akasema, Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa kwangu. Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile alivyompenda. Yakobo akamwambia Labani, Nipe mke wangu, maana siku zangu zimetimia; niingie kwake. Labani akakusanya watu wote wa mahali pale, akafanya karamu. Ikawa wakati wa jioni akamtwaa Lea, binti yake, akamletea Yakobo, naye akaingia kwake. Labani akampa Lea mjakazi wake Zilpa, awe mjakazi wake. Ikawa, kulipokuwa asubuhi, kumbe! Ni Lea. Akamwambia Labani, Nini hii uliyonitenda? Sikukutumikia kwa Raheli? Mbona umenidanganya? Labani akasema, Havitendeki hivi kwetu, kumtoa mdogo kabla ya mkubwa;” Hila sio njema na wakati wote inapotajwa katika Biblia haielezwi kama kitu kizuri hakuna uzuri wowote katika hila , Hila siku zote inahusishwa na kazi za ibilisi ona 2wakoritho 11:3 “Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.Mungu ni mwaminifu naye anapendezwa nasi tukiwa na tabia inayofanana na yeye hivyo anatoa wito kwetu kuwa watu wasio na hila, Yesu Kristo mwenyewe hakuwa na hila ona 1Petro 2:21-22 “Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake”. Hila ndio moja ya dhambo mbaya ya kuepukwa Pale Yesu alipomwambia Nathaniel kuwa hakuna hila ndani yake alikuwa amemaanisha kuwa ni mtu mwenye kiwango cha juu sana cha uadilifu, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa mbali na hila katika jina la Yesu amen

 

3.       Na aache mabaya:

 

Wito wa Mungu wakati wote kwa watu wake ni kuacha mabaya, ili mtu aweze kuwa na siku njema aweze kuufurahia uumbaji na utendaji wa Mungu ni lazima aacha mabaya, Neno kuacha mabaya katika lugha nyingine linatumika neno “Let him eschew evil” Lugha hii ina maana ya kujiepusha na maovu mfano imetumika pia katiika Ayubu 1:1 “Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu.”  Ingawa hatuwezi wakati wote kuepuka kukutana na changamoto mbalimbali lakini hatuna budi kuhakikisha kuwa wakati wote tunaendelea kuwa na huruma na upendo kwa jamii, na hakuna matu anayeweza kuishi maisha ya raha moja kwa moja tuwapo duniani lakini ili tuweze kuyafurahia maisha maisha ya uzima wa milele mbinguni basin i lazima tujiepushe au kuacha mabaya hii ndio njia itakayotupatia maisha mema, Kumbuka Petro alikuwa anawaandikia wakristo waliokuwa wanapoitia katika mateso, kwa hivyo kwao hazikuwa siku njema lakini alikuwa akizungumza kuwa uvumilivu wao utawaleta hatimaye katika kufurahia siku njema kwa hivyo aliwaasa wasiache njia “ekklineo” – wasiende nje ya njia njema, Zaburi 1:1-6 “Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa. Sivyo walivyo wasio haki; Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo. Kwa hiyo wasio haki hawatasimama hukumuni, Wala wakosaji katika kusanyiko la wenye haki. Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki, Bali njia ya wasio haki itapotea.Ni wito wa kiungu wakati wote kuwaita watu wageuke na kuacha njia zao mbaya ili aweze kuwaponya na kuwabariki Ezekiel 33:11 “Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, SIKUFURAHII kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia, yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli? ” ni ahadi ya Mungu kila wakati kuwabariki watu na kuwatendea mema iwapo wataacha njia mabaya 2Nyakati 7:14 “ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.” Biblia inatutia moyo kuwa rehema za Mungu ziko haijalishi kwamba umewahi kuwa muovu kwa kiwango gani lakini ukibadilisha njia yako leo Mungu yuko tayari kuyabariki maisha yako na kuanza nawe ukurasa mbaya maandiko yamesisitiza wakati wote kuacha njia mbaya, kuishi maisha ya toba kila wakati na kuendelea kumpendeza yeye Isaya 55:6-8 “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa. Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana.

 

4.       Atende mema!.

 

Petro anaonekana kuathiriwa sana na usomaji wa zaburi, kwani anarejea tena katika kile ambacho alinukuu kutoka katika Zaburi ya Daudi ambayo mara kadhaa imesisitiza kuwa sasa kwa kuwa tumeacha mabaya na tutende mema ona Zaburi 37:1-4 “Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya, Usiwahusudu wafanyao ubatili. Maana kama majani watakatika mara, Kama miche mibichi watanyauka. Umtumaini Bwana ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. Nawe utajifurahisha kwa Bwana, Naye atakupa haja za moyo wako.” Ona pia Zaburi 37: 27-28 “Jiepue na uovu, utende mema, Na kukaa hata milele.     Kwa kuwa Bwana hupenda haki, Wala hawaachi watauwa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa.” Mara kadhaa maandiko yameonyesha kile ambacho Mungu anakitaka kwetu na ambacho ni kutenda mema Mika 6:8 “Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!

 

5.       Atafute amani.

 

Mwisho Petro anataka tuitafute amani, kwa kweli neno la Mungu Biblia kwa mukhtasari ni kitabu cha amani, ili mtu awe kamili anapaswa kuwa na amani na Mungu na amani na wanadamu, hili ndio agizo la kibiblia, Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;Amani ina faida kubwa sana kwetu tunapotaka kustawisha uhusiano wetu kwa Mungu na wanadamu, hatuwezi kuwa sawa na Mungu kama hatuna amani na mtu fulani 1Yohana 4:20-21 “Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.” Mke na Mume wasipokaa kwa akili na kuhakikisha kuwa wana amani maombi yao yanaweza kuzuiwa 1Petro 3:7 “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.Watu wanapokosa amani kati yao na akama hawajatengeneza au kupatana jambo hilo husima a kama ukuta katika ain azote za ibada ikiwepo sadaka Mathayo 5:23-24 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.” Yesu alimaanisha wazi kuwa hatuwezi kupokea Baraka zozote zile kama tumevuruga amani, hivyo ni muhimu kupatana na mashitaki wako upesi ili asizuie Baraka zako katika ulimwengu wa Roho, Maagizo ya kibiblia yanatutaka tuitafute sana amani kwa sababu kuna gharama kubwa sana kuipata, amani inapaswa kutafutwa kwa bidii, Yakobo alikuwa amemuuzi kaka yake Esau kiasi ambacho Esau aliapa kuwa atamuua, jambo hili lilisabababisha akimbie mbali ujombani, lakini huko nako hakuwa na amani maisha yake yalikuwa taabuni kwa sababu Esaua angemuua na Esau aliposikia kuwa Yakobo anakuja alikuja na kikosi cha askari mia nne huu ulikuwa wakati mbaya sana katika maisha ya Yakobo na hapa ndipo alipoutafuta uso wa Mungu na vilevile alitafuta msamaha wa kweli kutoka kwa Esau ona Mwanzo 32: 1-8 “Yakobo akashika njia yake na malaika wa Mungu wakakutana naye. Naye Yakobo alipowaona, alisema, Hili ni jeshi la Mungu. Akapaita mahali pale, Mahanaimu. Basi, Yakobo akapeleka wajumbe mbele yake kwenda kwa Esau nduguye mpaka nchi ya Seiri katika nyika ya Edomu. Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini kwa Labani, na kukawia huko hata sasa, nami nina ng'ombe, na punda, na kondoo, na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari, nipate neema machoni pako. Wale wajumbe wakarudi kwa Yakobo wakisema, Tulifika kwa ndugu yako, Esau, naye anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye.Ndipo Yakobo akaogopa sana, na kufadhaika sana, akawagawanya watu waliopo pamoja naye, na kondoo, na ng'ombe, na ngamia, wawe matuo mawili. Akasema, Akija Esau kwa kundi la kwanza, akalipiga, kundi litakalosalia litaokoka.Ni wazi kuwa Esau angekuja kufanya vita na Yakobo na yakobo aliogopa na aliamua kumuomba Mungu usiku ule na Mungu alimuelekeza namna ya kupata amani ilimgharimu sana lakini alifabya bidii ili aweze kuwa na amani na ndugu yake, kila atakaye kupenda maisha yaani maisha haya nay ale yajayo hana budi kujikita katika kuitafuta amani kwa bidii, Yakobo aliiitafuta sana na Mungu akamfanikisha  Mwanzo 33:1-11 “Yakobo akainua macho yake, akaona, na tazama, Esau anakuja na watu mia nne pamoja naye. Akawagawanyia Lea, na Raheli, na wale vijakazi wawili, wana wao. Akawaweka hao vijakazi na wana wao mbele, na Lea na wanawe nyuma yao, na Raheli na Yusufu mwisho. Akapita mwenyewe mbele yao, akainama mpaka nchi mara saba, hata alipomkaribia ndugu yake. Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na kumwangukia shingoni, akambusu; nao wakalia. Akainua macho yake, akawaona wale wanawake na watoto, akauliza, Ni nani hawa walio pamoja nawe? Akasema, Ni watoto Mungu aliompa mtumwa wako kwa neema yake. Ndipo wale vijakazi, na wana wao, wakakaribia wakainama.Lea naye, na wanawe, wakakaribia wakainama. Baadaye Yusufu na Raheli wakakaribia, wakainama. Akasema, Kundi hili lote nililolikuta, maana yake ni nini? Akasema, Kunipatia kibali machoni pa bwana wangu.  Esau akasema, Ninayo tele, ndugu yangu, uliyo nayo na yawe yako. Yakobo akasema, Sivyo; kama nimekubalika machoni pako tafadhali upokee zawadi yangu mkononi mwangu, iwapo nimeona uso wako kama kuona uso wa Mungu, ukapendezwa nami. Pokea, tafadhali, mbaraka wangu, ulioletewa, kwa sababu Mungu amenineemesha, na kwa sababu ninavyo hivi vyote Akamshurutisha, naye akapokea.”

 

1Petro 3:10-12Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila. Na aache mabaya, atende mema; Atafute amani, aifuate sana. Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya.”

 

Na. Rev. Innocent Kamote.

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni