Jumatatu, 3 Mei 2021

Unapokutana na Mitihani!


Kumbukumbu La Torati 8:15-16 “aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako.”



Utangulizi:

Wakati mwingine ili Mungu aweze kutuimarisha na kutukomaza ili kutupeleka katika kusudi lake alilolikusidia basi hutupitisha katika majaribu ya aina mbalimbali kwaajili ya kutufundisha hali kama hii hututokea katika siku za maisha yetu tuwapo duniani na zaidi sana katika maisha ya shuleni, maisha ya uanafunzi huwa yanahitimishwa kwa mitihani, huwezi kumtenganisha mwanafunzi na mitihani hata kidogo, mtihani ndio unaoamua hatima ya mwanafunzi na kumpeleka katika kiwango kingine cha kusudi la utumishi wake duniani.

Ni msimu mwingine tena wa mitihani, kwa majuma kadhaa sasa wanafunzi wetu watakuwa wanakaa kwaajili ya mitihani yao, ambayo kimsingi vilevile itaamua hatima ya maisha yao ya baadaye, kwa hivyo wote tunakubaliana kuwa ni wakati muhimu sana, Mitihani ni sehemu ya kipimo cha yale tuliyojifunza na uwezo wetu wa kuelewa lakini sio hivyo tu ndiyo inayotupeleka juu kuelekea hatua nyingine ya kielimu katika maisha, kwa msingi huo kama wanafunzi tutakuwa tumewahi kukutana na mitihani ya aina mbalimbali kama hii tunayokutana nayo sasa, Pamoja na uzuri na umuhimu wa mitihani wakati wa mitihani ndio wakati ambao wanafunzi wengi hujikuta katika msongo mkubwa wa mawazo na kufikiri itakuwaje, Je tunawezaje kuikabili mitihani, Neno la Mungu linatupa kanuni za kutusaidia namna na jijnsi ya kushinda wakati wa mitihani Roho wa Mungu aliniambia nisema haya kwa wanafunzi wanofanya mitihani wakati huu.

1.       Hesabia kuwa ni wakati wa furaha  #

 

Yakobo 1:2 “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali;” Hapo Biblia inazungumzia kufurahi wakati tunapopitia katika majaribu ya aina mbalimbali, Biblia inazungumzia kihalisia habari ya changamoto kadhaa katika maisha ya ukristo na maisha ya duniani kwa ujumla, lakini kwa vile imesema majaribu mbalimbali mimi nataka kuweka majaribu kama mtihani, nataka kuitumia kanuni ileile ya jambo lile-lile ambalo huwa ni jaribu katika maisha huwa ni changamoto huwa linatuhuzunisha na kutuondolea furaha kuwataka wanafunzi wafahamu kuwa wakati wa mitihani japo wanatumia sana akili, na wanapaswa kuongeza umakini mkubwa, wanakesha bongo zinachoka lakini wafahamu vilevile kuwa sio wakati wa kuhuzuinika ni wakati wa kufurahi, ni wakati wa kujiachia katika neema ya Mungu na kuondoa hofu kabisa kila mmoja akijua kuwa mtihani una faida kubwa na kuwa utampeleka katika ngazi ya juu zaidi hivyo wakati kama huo sio wa kulia na kuumia bali ni wakati wa furaha relax.

 

2.       Fanya kwa utukufu wa Mungu.

 

Maandiko yanatufundisha kuwa lolote tulifanyalo kwa neno au kwa tendo, tulifanye kwa utukufu wa Mungu

1Wakoritho 10:31 “Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.”

Hatufanyi mtihani kwaajili ya mashindano, hatushindani na mtu, tunafanya lolote tulifanyalo kwaajili ya kumpa Mungu utukufu, kwa msingi huo hakikisha kuwa Mungu anakwenda kutukuzwa kwa kile unachokwenda kukifanya, acha mashindano, usishindane na mtu, wala shule yako isifanye mashindano na shule nyingine,usiogope pia unapoona mwenzako ameandika sana na kujaza kurasa haimaanishi kuwa ndio amejaza point, usiogope, mwenzako anapoongeza booklet ya kujibia usipasuke moyo na kudhani kuwa labda mambo ni mazuri kwake wala na wewe usiige kwa sababu balada ya kwenda kwenye point unaweza kujikuta unajaza blaablaa kwa sababu ya kutaka kuwa kama Fulani kumbuka kuwa unafanya mtihani kwa kusudi la kumpendeza Mungu, hivyo usijilinganishe na mwingine endapo wasimamizi wa mtihani wanaruhusu mtu kutoka haraka wewe usitoke kwa haraka unapoona kuna mtu kamaliza wewe fuata muda uliopangwa katika ratiba na mtihani wako ukikumbuka kuwa wewe uko pale kwa kusudi la kumpendeza Mungu na sio wanadamu

2Wakoritho2:9 “Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye.”

Vyovyote vile jitahidi kuufanya mtihani wako kwa kusudi la kumpendeza Mungu, Mungu anakuona, anajua hitaji lako, anajua wazazi wako wamewekeza kiasi gani anajua walimu wako wamejitahidi kiasi gani sasa wakati wa mtihani hakikisha kuwa unafanya mtihani kwa kusudi la kumpendeza yeye, na kusudi lako kubwa liwe kwamba Mungu atukuzwe kwa matokeo mema ya mtihani wako!

 

3.       Mwamini Mungu!

 

Sisi hatuingii katika chumba cha mtihani kama wapagani,au kama watu wasio na imani au matumaini tunaingia tukiwa na Mungu aliye hai, ni lazima tumtangulize Mungu mbele na ili tumpendeze yeye lazima tuwe na imani naye Maandiko yanasema pasipo imani haiwezekani kumpendeza,  kwa hiyo ingia katika chumba chako cha mtihani ukiamini na kujua wazi kuwa yuko Mungu na kuwa hatakuacha

Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.”

Mafanikio yetu na kuthibitika kwetu kutakuja tu endapo tutamuamini Mungu, na kwa kuwa sisi tunamtumaini yeye ni dhahiri kuwa tutafanikiwa

2Nyakati 20:20 “Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini Bwana, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.”
Hakuna mtu amemuamini Mungu kisha Mungu akamuacha hivihivi tu!

 

4.       Fanya mtihani kwa jina la Yesu

Mtu anaweza kujiuliza Je naweza kutumia jina la Yesu kufanya mtihani ndio Jina la Bwana ni ngome imara mwenye haki huikimbilia akawa salama ona

Mithali 18:10 “Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.”
Yesu mwenyewe alisisitiza kuwa tukiomba lolote kwa jina lake baba wa Mbinguni atalitenda ona

Yohana 14:13-14 “Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.”
Tunaweza kulitumia Jina la Yesu kila wakati katika taabu yoyote naye atatusaidia, hili ndio jila lenye kuleta msaada ndio jina linaloweza kutuokoa bila kujali historia zetu au wapi tumetokea Biblia inasema kila, nakazia tena KILA, yaani bila kujali wewe ni nani, ni wa kabila gani, ni wa ukoo gani, ni wa taifa gani, ni wa dini gani bila kujali haki yako unapoliitia jina hili litaleta wokovu ulio sawa na mahitaji yako ona

Matendo 2:21 “Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa.”
Wengine wanaweza wasikubaliane nami kwamba tunaweza kulitumia jina la Yesu katika mambo mazito sio kulichezea katika mitihani, nisikilize mitihani ndio inayoamua hatima ya maisha yetu, hivyo wakati wa mitihani sio wakati wa mchezo, tunamuhitaji Mungu na tunamuhitaji Bwana Yesu wakati wa mitihani yetu kwa msingi huo ni muhimu kwetu tukafanya mtihani huo kwa jina la Yesu, Biblia imesema lolote tufanyalo nakazia tena LOLOTE tufanyalo ukiwemo mtihani tulifanye kwa jina la Yesu ona

Wakolosai 3:17 “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.”
Unaona kumbe maandiko yanatutia Moyo kuwa tunaweza kufanya kila tunachokifanya kwa jina la Yesu, iwe kwa neno au kwa tendo, ikiwa watakatifu waliotutangulia katika agano la kale walifanya vita kwa jina la Bwana je kuna dhambi gani kufanya mtihani kwa jina la Bwana wa majeshi?

5.       Usiibe/. Wala usifanye udanganyifu!.

 

Kutoka 20:15-16 “Usiibe, Usimshuhudie jirani yako uongo.” Ni amri mbili ambazo zinafuatana katika maandiko, na katika amri Kumi, wote tunajua madhara ya udanganyifu, tunafahamu namna dunia ilivyoingia katika huzuni kubwa sana kwa sababu ya udanganyifu, shetani alipofanikiwa kumdanganya hawa alisababisha uharibifu mkubwa, wakati wa mitihani shetani hatakosa kuwajaribu watu walio dhaifu, usikubali kujaribiwa, usikubali kumpa shetani nafasi, Biblia inasema wala msimpe ibilisi nafasi, nafasi moja tu inaweza kusambaratisha na kuharibu maisha yako, hairuhusiwi kufanya udanganyifu wa aina yeyote wakati wa mtihani, Mungu anataka tuwe waaminifu tu, hivyo basi jitahidi kutumia akili zako na kumtegemea Mungu, hakuna msaada unaoweza kupewa na walimu wako wala mtu yeyote wala mzazi wako zaidi ya msaada ule waliokusaidia kukulipia ada na kukufundisha, hivyo uwe na bidii, ukaufanye mtihani ule kwa akili zako mwenyewe na kwa msaada wa Mungu aliye hai, wala usiibe wala usifanye udanganyifu ambao unaweza kuwa na madhara makubwa kwako, lakini vilevile kwa shule yako na kwa wenzako, na pia kusababisha hasara kwa taifa na kuitia dosari wilaya yako mkoa wako na kadhalika, hivyo tusijaribu kwa namna yoyote ile kufanya udanganyifu kwaajili ya utukufu wa Mungu!, Mungu atatukuzwa vipi kama tumeibia, Mungu atatukuzwa tu kama tulisoma kwa bidii, tukamuomba , tukamtegemea na kumuamini naye akatusaidia basi.

 

6.       Muombe Mungu!

 

Wako watu ambao wanadharau maombi, wanadhani kuwa hayana msaada wowote wala kitu chochote cha ziada hususani linapokuja swala la Mtihani, dhana hii ni ya kijinga, Hatupaswi kuzitumainia akili zetu wenyewe japokuwa kutumia akili sio dhambi, akili ni karama ya kwanza ambayo mwanadamu amepewa na Mungu, tuna haki ya kuitumia, lakini ni kosa kubwa sana kukataa masaada wa Mungu wakati wa jaribio lililoko mbele yetu, Neno la Mungu linasema tusijisumbue katika jambo lolote bali kwa kuomba ona

Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”  

Maombi ni silaha ya kipekee ambayo tunaweza kuitumia katika nyakati zote na kwa jambo lolote, hatuna budi kuliamini neno la Mungu na kuomba, Yesu mwenyewe alipokuwa anakabiliwa na Mtihani wa kufa msalabani aliomba na malaika wa Bwana wakaja kumtia nguvu, inawezekana mtihani wenyewe ukawa sio tatizo lakini hofu yetu, kukosa kwetu amani, kuogopa kukawa ndio tatizo kwa hiyo ni muhimu kuomba ili tuhifadhiwe mioyo yetu na nia yetu na amani ya Mungu ipitayo akili zote itatuhifadhi.

 

7.       Usiogope

 

Hofu ya mitihani ni moja ya maumivu na homa kubwa sana ya wanafunzi wakati wa mtihani, wakati wa mtihani watu wengi hujiuliza itakuwaje, mioyo inawadunda watu wanaogopa, namimi pia nimefanya mitihani katiika viwango mbalimbali vya msingi, sekondari, vyuoni na katika kozi nyinginezo, nimejiona na nimeona pia watu wengi wakiogopa mitihani, Hata wachungaji katika vyuo vya Biblia huogopa mitihani, woga sio mzuri, woga unaweza kuchelewesha kufikia kusudi la Mungu ndani yako, katika Kiwango “level” ya chuo nilipokuwa na chukua digrii ya ualimu, ilikuwa ni ruhusa kutokufanya mtihani kama unaona hauko tayari na maandalizi yako sio mazuri, lakini pia ilikuwa ruhusa kurudia mtihani ukifeli, sikupenda kurudia mtihani nilitamani kufaulu mara moja nitakapoufanya mtihani wangu, lakini mara kadhaa niliahirisha kufanya mtihani kwa kutokujiamini kuwa laba maandalizi yangu hayatoshi hivyo nilihairisha mara kwa mara,lakini mwisho nikaona mbona ninapoteza Muda, mbona ninajichelewesha kufikia kusudi la Mungu analotaka kunitumia kwalo? Nikamuamini Mungu nikaomba, Mungu aliponitia nguvu kufanya nilikasirika na kuamua kuifanya yote bila kujali nilifanikiwa kuimaliza kwa wepesi sana, hata hivyo nilikuja najishangaa kwa nini niliogopa sasa, niliogopa nini kumbe mbiona inawezekana, ni kwa sababu waliita chuo kikuu kwa hiyo nilidhani sio mahali pa mchezo na kuwa kila kitu ni kigumu kumbe inawezekana kama wengine walivyoweza. Kuogopa kunaweza kuchelewesha lile ambalo Mungu alikuwa amelikusudia kwetu, Hofu ni mbaya, wana wa Israel walipoogopa walishindwa kuirithi nchi ya kanaani kwa wakati iliokusudiwa na hivyo ikawagharimu miaka mingi,

Hesabu 14:1-9 “Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri. Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli. Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope.”

Wakati wote linapokuja swala lolote linalotupa changamoto Fulani hatupaswi kuogopa, tunapaswa kuona kama Kalebu na Yoshua kuwa kama Bwana yuko pamoja nasi hakuna linaloweza kusimama kinyume nasi, tunaliitia jina la Bwana katika shida zetu na tunaingia katika chumba cha mtihani tukiwa na imani kuwa yuko pamoja nasi

Zaburi 118:5-9 “Katika shida yangu nalimwita Bwana; Bwana akanijibu akaniweka panapo nafasi. Bwana yuko upande wangu, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Bwana yuko upande wangu, msaidizi wangu, Kwa hiyo nitawaona wanaonichukia wameshindwa. Ni heri kumkimbilia Bwana Kuliko kuwatumainia wanadamu. Ni heri kumkimbilia Bwana. Kuliko kuwatumainia wakuu.”

Unaona mwandishi wa zaburi ana ushujaa mwingi sana kwa sababu ana uhakika kuwa Bwana yuko upande wake sisi nasi Mungu yuko pamoja nasi kwa hiyo hatupaswi kuogopa na ushindi ni dhahiri kuwa utakuwa upande wetu ona

Warumi 8:31 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?”

 

8.       Fanya kwa bidii.

 

Kama jinsi ambavyo tumeiona kuwa mtihani ni nafasi, ni nafasi kwa sababu ndio unaoamua hatima ya maisha yetu, na kutupeleka kule kwenye utume ambao Mungu ametuitia kuufanya duniani kwa hiyo “it is an opportunity” ni fursa kwa msingi huo hatuna budi kuhakikisha kuwa tunaufanya vizuri sana

Muhibiri 9:10 “Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe.”

Unaona maandiko yanatutia moyo kufanya kila kitu kwa ufasaha, hakikisha unaandika vizuri, unapangilia vizuri, unaonyesha machakato wa namna na jinsi ulivyopata majibu, nenda kwenye pointi kama hakuna cha kuelezea usipige blaablaa nyingi, kumbuka huufanyi mtihani kwaajili ya kuwapendeza wanadamu bali kwaajili ya utukufu wa Mungu, hivyo mambo ya Mungu hayapaswi kufanywa kwa upuuzi, hivyo fanya kazi yako vema.

 

9.        Jipumzishe! (Relax)

 

Mwanzo 2:1-3 “Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.”

Kama tumemuomba Mungu na kuzingatia yote yale ambayo Mungu ametupa kuyafanya yaani tumejisomea sana, tulikesha sana, tulifunga na kuomba, tunamuamini Mungu hatuogopi tuna uhakika kuwa Mungu yuko upande wetu basi “Relax” usijisumbue pumzisha akili zako acha kuwa na msongo wa mawazo, uwe na utulivu, wala hata usijadili kitu na mtu utakapotoka nje hasa kwa mtihani ambao umekwisha kuumaliza, tafakari na utulie na upumzike hii nayo ni kanuni ya kiungu unapomaliza kufanya assignment ambayo Mungu amekupa unahitaji kupumzika “Relax”

Yona 4: 5-6 “Ndipo Yona akatoka mjini, akaketi upande wa mashariki wa mji, akajifanyia kibanda huko, akakaa chini yake uvulini, hata aone mji ule utakuwaje. Na Bwana Mungu aliweka tayari mtango, akaufanya ukue juu ya Yona, ili uwe kivuli juu ya kichwa chake, na kumponya katika hali yake mbaya. Basi Yona akafurahi sana kwa sababu ya ule mtango.”

 

10.   Chochea karama iliyoko ndani yako kwa kuwekewa Mikono

 

Nilitaka kumalizia mahubiri yangu na poit namba 9 tu lakini Roho wa Mungu akanitaka niweke hii ya kuwekewa Mikono, unapofika wakati wa Mtihani kama hivi ni muhimu kufahamu kuwa kila mtu, kila kijana kila mtoto, Mungu ameweka kitu ndani yake, lakini wakati mwingine hakiwezi kujitokeza bila kuwekewa Mikono, hii ni sihara ya maombezi yenye kuleta neema kubwa sana japo sio lazima, lakini ni kanuni bora ya kimaandiko, kama sio tatizo mchungaji na aweke mikono juu ya wale wanaokwenda kufanya mitihani yao, inahitajika neema, kuwekea mikono mtu hufanya hekima na maarifa ya kiungu yawe juu yake ona

Kumbukumbu la Torati 34:9 “Na Yoshua, mwana wa Nuni, alikuwa amejaa roho ya hekima; maana Musa alikuwa amemwekea mikono yake juu yake; wana wa Israeli wakamsikiliza, wakafanya kama Bwana alivyomwamuru Musa.”


Mmmh kumbe basi mtu anapowekewa Mikono karama zilizojificha ndani yake huibuka na kumpa neema ya kuwa na hekima na maarifa kama ilivyokuwa kwa Musa alimuwekea mikono Yoshua na Paulo mtume alimuwekea mikono Timotheo, mtu anapowekewa mikono aidha roho ya woga huondoka na amani ya Mungu humkalia hivyo uko umuhimu wa kuwawekea mikono watahiniwa endapo mazingira na muda unaruhusu kufanya hivyo kwa watumishi husika Kama Paulo alivyofanya kwa Timotheo. ona

2Timotheo 1:6-7 “Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.”

 

Uongezewe neema!

 

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni