Jumapili, 13 Juni 2021

Hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena Milele !


Msatri wa Msingi: Kutoka 14:14-14Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.”




Utangulizi:


Siku moja Bwana Mungu aliviita viungo vyote katika mwili wa mwanadamu na akataka kuwauliza ili kujua wanafanyaje kazi? Kichwa kilielezea yote, Moyo, mikono miguu na kila kiuongo kwa jinsi yake, Lakini kiungo kimoja kilikuwa na malalamiko dhidi ya kiungo kingine, kiungo kilichokuwa na malalamiko kilikuwa ni *Ulimi* na mlalamikiwa alikuwa ni *Meno*, Kesi iliposikilizwa, ulimi ulisema kuwa mimi ni laini sana Mzee na umeniweka na Meno ambaye kwaasili yeye ni mgumu, tunapokuwa katika kazi ya kulainisha chakula mara kwa mara Meno huning’ata na kuniumiza na hivyo nachukua siku kadhaa kupona na kuendelea na kazi zangu, Mungu alimwambia ulimi usilalamike, ulaini wako haumaanishi kuwa wewe ni dhaifu kuliko meno, wewe ni mgumu sana, kuliko unavyojifikiri utaumizwa na utapona, na utaendelea kuwepo,  lakini sivyo ilivyo kwa meno ambaye anaonekana kuwa mgumulakini ukweli yeye ni dhaifu, baada ya miaka kadhaa utahesabia meno na utakubaliana nami kuwa mengine yataliwa na wadudu na hutayaona tena na yatang’olewa, lakini wewe ulimi utadumu hata mwisho wa dahari, ni kweli ulimi ulivumilia na kutoa muda kwa meno na wakati wa uzee, ni ulimi pekee aliyeonekana kudumu na kutokuchoka tena ukiwa na nguvu zake vilevile!


Lolote lile linalokusumbua katika maisha yako, na kukuumiza lipe muda tu, iko siku litang’oka, Wamisri waliwaonea wana wa Israel na kuwatumikisha kama watumwa kwa miaka mia nne na thelathini, Lakini siku moja wakati Israel wakiivuka bahari ya shamu, Musa alitabiri kuwa hawa wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele, unabii huu ulidumu kwa muda mfupi tu, kwani hata Musa aliusema akiwa kama kiongozi na mwenye kuwatia moyo watu wake kama mchungaji, lakini yeye mwenyewe alimlilia Mungu kwa hali aliyokuwa anaiona, Mkono wa Mungu ulikuwa mwema kwani aliwafutilia mbali Wamisri wale waliokuwa wakiwaandama wana wa Israel ili kuwaonea.


Leo nakutangazia kwa jina la Yesu, Magumu yote yanayokukabili na changamoto zote unazozipitia hautakuja uzione tena milele, Bwana atakupigania nawe hutanung’unika milele, Bwana atakustarehesha, Bwana atakupigania nawe utanyamaza kimya, kila changamoto unayokutana nayo katika maisha yako na inayoonekana kuwa ngumu au tishio kwako, hayo ni kama magego tu na wewe ni kama ulimi wewe ni imara zaidi kuliko wao na kuliko changamoto zako, Mungu anayejua kuwa uko katikati ya magumu atakutetea, Changamoto hizo kwa mamlaka niliyopewa kama mtumishi wake natangaza  leo ziwe mwisho na usizione tena katika jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai, Natangaza kuwa changamoto zinazokukabili hautaziona tena, sema amina

Na. Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!


Maoni 1 :

  1. Mungu akubariki kwa neno zuri limenisaidia

    JibuFuta