Isaya 52:7 “Jinsi ilivyo mizuri juu ya
milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari
njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu, Auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki!”
Utangulizi:
Ujumbe huu wa Nabii Isaya ulikuwa
ni ujumbe wa maono ya siku ya ukombozi wa Yerusalem ambao vilevile huitwa
sayuni, Ni ujumbe unaohusiana na Israel (Wayahudi) kuletewa ujumbe wa amani
kutoka kwa mfalme Koreshi ya kwamba Mungu amemtuma awatangazie uhuru wayahudi
waliokuwa utumwani huko Babel kwamba warejee kwao na kuujenga tena mji wao na
Hekalu la Mungu wao baada ya kuwa utumwani kwa miaka mingi, Nabii anaona maono
ya ukombozi anawaona wajumbe juu ya milima ya Yudea wakiiletea Yerusalem habari
za kufunguliwa kwake! Ona
Isaya 40:9-11 “Wewe
uuhubiriye Sayuni habari njema, Panda juu ya mlima mrefu; Wewe uuhubiriye
Yerusalemu habari njema, Paza sauti kwa nguvu; Paza sauti yako, usiogope;
Iambie miji ya Yuda, Tazameni, Mungu wenu. Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama
shujaa, Na mkono wake ndio utakaomtawalia; Tazameni, thawabu yake i pamoja
naye, Na ijara yake i mbele zake. Atalilisha kundi lake kama mchungaji,
Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake; Na kuwachukua kifuani mwake, Nao wanyonyeshao
atawaongoza polepole.”
Nabii Isaya hakupata nafasi ya
kuona kile kilichowapata wana wa Israel (Wayahudi) waliochukuliwa utumwani
wakati wa Mfalme Nebukadreza, lakini aliweza kuona na kutabiri katika ulimwengu
wa kiroho na kuwaona wayahudi wakipelekwa utumwani lakini vilevile wakirejea,
Unabii wake huu hasa unatoa matumaini kwa Wayahudi ambao wangechukuliwa
utumwani na kuwatia moyo ya Kwamba Mungu angewatokea tena na kuwarejeza.
Wayahudi walichukuliwa utumwani
na Mfalme aliyeitwa Nabukadreza kimsingi mfalme huyu wa wakaldayo, alikuwa ni
mwana wa Nabopolassar na alipata
utawala mwaka wa 604 Kabla ya Kristo
baada ya kuanguka kwa utawala wa waashuru, Jina lake kamili hasa linaandikwa na
kutamkwa kama Nebuchadrezzar ambalo
kwaasili ni “Nabu-Kudurri-usur”
ambalo maana yake ni Nebo linda mipaka
yangu (Nebo ni mungu wa wakaldayo) Mfalme huyu aliyekuwa katili sana na
aliyekuwa dikteta mkubwa mno ametajwa zaidi ya mara tisini katika agano la kale.
Wayahudi wanamkumbuka Mfalme huyu
kama moja ya wafalme katili sana ambaye wao wanamuhesabu kuwa aliwafanya
wayahudi kama moja ya wanyama, alipopata utawala alikuwa na kampeni ya kupanua
mipaka yake ya kuitawala Dunia mpaka Misri na kuhakikisha kuwa kila mfalme
anamtii yeye na akawa mfalme wa wafalme, Wayahudi pia walitawaliwa na mfalme
huyu, na Yehoyakimu mfalme wa wayahudi alitakiwa kujinyenyekesha chini yake na
alipoasi jamaa alimuharibu ona
2Wafalme
24:1-3 “Katika siku zake akakwea Nebukadreza,
mfalme wa Babeli na Yehoyakimu akawa mtumishi wake muda wa miaka mitatu;kisha, akageuka,akamwasi.Naye
Bwana akatuma juu yake vikosi vya Wakaldayo, na vikosi vya Washami, na vikosi
vya Wamoabi, na vikosi vya wana wa Amoni, akawatuma juu ya Yuda ili kuiharibu,
sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa mkono wa watumishi wake manabii.
Hakika kwa amri ya Bwana mambo hayo yalimpata Yuda, ili waondoshwe kutoka
machoni pake, kwa sababu ya dhambi zake Manase, kadiri ya yote aliyoyafanya;”
Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Nebukadreza vilevile aliliharibu Hekalu la
Yerusalem na kuchukua vyombo vitakatifu na kuvipeleka katika hekalu lake huko
Babeli wakati wa mfalme Yehoyakimu
2Nyakati
36:5-7 “Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka
ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala katika Yerusalemu miaka kumi
na mmoja; akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, Mungu wake. Juu yake akakwea
Nebukadreza, Nebukadreza akachukua baadhi ya vyombo vya nyumba ya Bwana mpaka
Babeli, akavitia katika hekalu lake huko Babeli.” Aidha alimuua
mfalme wa wayahudi na kuutupa mwili wake bila kuuzika sawa na alivyotabiri
nabii Yeremia ona
Yeremia 22:18-19 “Basi, Bwana asema hivi, katika habari ya Yehoyakimu,
mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; Hawatamwombolezea, wakisema, Aa! Ndugu yangu;
au, Aa! Dada yangu; wala hawatamlilia, wakisema, Aa! Bwana wangu; au, Aa!
Utukufu wake. Atazikwa maziko ya punda, akibururwa, na kutupwa nje ya malango
ya Yerusalemu.” Ona pia
Yeremia 36:30-32 “Basi,
Bwana aseme hivi, katika habari za Yehoyakimu, mfalme wa Yuda; Hatakuwa na mtu
wa kukaa katika kiti cha enzi cha Daudi; na mzoga wake utatupwa nje wakati wa
mchana upigwe kwa hari, na wakati wa usiku upigwe kwa baridi. Nami nitamwadhibu
yeye, na wazao wake, na watumishi wake, kwa sababu ya uovu wao, nami nitaleta
juu yao, na juu ya wenyeji wa Yerusalemu, na juu ya watu wa Yuda, mabaya yote
niliyoyatamka juu yao, lakini hawakukubali kusikiliza. Ndipo Yeremia akatwaa
gombo lingine, akampa Baruku, mwandishi, mwana wa Neria, naye akayaandika
maneno yote yaliyotoka katika kinywa cha Yeremia, ya kitabu kile
alichokiteketeza Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika moto; tena maneno mengi
zaidi kama yale yakatiwa ndani yake.” Licha ya kumuua mfalme wa
wayahudi na kumtupa bila kuzikwa, Nebukadreza pia alichukua utumwani kundi la
wayahudi wapatao 4,600 ona
Yeremiah 52:27-30 “Naye mfalme wa Babeli akawapiga na kuwaua huko Ribla katika nchi ya
Hamathi. Ndivyo Yuda alivyochukuliwa utumwani, akatolewa katika nchi yake. Watu
hawa ndio wale ambao Nebukadreza aliwachukua mateka; katika mwaka wa saba,
Wayahudi elfu tatu na ishirini na watatu; katika mwaka wa kumi na nane wa
Nebukadreza aliwachukua toka Yerusalemu watu mia nane na thelathini na
wawili;katika mwaka wa ishirini na tatu wa Nebukadreza, Nebuzaradani, amiri wa
askari walinzi, akawachukua mateka katika Wayahudi watu mia saba na arobaini na
watano; jumla ya watu hao wote ni watu elfu nne na mia sita.”
Mfalme huyu ambaye hakuwa na huruma
aliamuru mateka watembee moja kwa moja bila mapumziko mpaka Ukaldayo bila
kupumzika hata hatua moja, akiamini kuwa wayahudi wakipewa nafasi tu watapata
muda wa kusali na kuomba na kutubu kwa Mungu wao na wanaweza kupata rehema,
hivyo ili wakose pumzi ya kupata kanafasi ka toba na kusababisha Mungu wao
kubadili mawazo alihakikisha kuwa wanakula kibano sawia, alipofika ukaldayo
alifanya sherehe kubwa sana ya kufurahia ushindi wake na kuwalazimisha wayahudi
waimbe nyimbo za Sayuni kwa miungu yake huko
Zaburi 137:1-3 “Kando ya mito ya Babeli
ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati
yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka
tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni.”
Vijana wazuri wenye nguvu na hekima walihasiwa ili wawe watumishi wa mfalme
yaani walifanywa kuwa matowashi, akiwepo Daniel, Hanania, Mishael na Azaria,
walikuja kujulikana baadaye kama Shedrack, Meshak na Abednego ona Daniel 1:1-4 “Katika
mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, Nebukadreza mfalme
wa Babeli,alikwenda Yerusalemu akauhusuru. Bwana akamtia Yehoyakimu, mfalme wa
Yuda, katika mkono wake, pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu; naye
akavichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka nyumba ya mungu wake; akaviingiza vile
vyombo katika nyumba ya hazina ya mungu wake. Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu
wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa
uzao wa kiungwana; vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima,
werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama
katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na
lugha yao.”
Licha
ya mateso haya ya kiutu na kisaikolojia Mateka wengi waliachwa na njaa,
walipigwa na jua kali, walitembezwa wakiwa uchi mpaka wakawa weusi, njaa ilisumbua
watu wazima mpaka vitoto vichanga, ilifikia hatua hata wanawake waliokuwa na huruma walikula
watoto wao kwa zamu Maombolezo 4:8-10 “Nyuso zao ni nyeusi kuliko makaa; Hawajulikani katika
njia kuu; Ngozi yao yagandamana na mifupa yao Imekauka, imekuwa kama mti. Heri
wale waliouawa kwa upanga Kuliko wao waliouawa kwa njaa; Maana hao husinyaa,
wakichomwa Kwa kukosa matunda ya mashamba. Mikono ya wanawake wenye huruma
Imewatokosa watoto wao wenyewe; Walikuwa ndio chakula chao Katika uharibifu wa
binti ya watu wangu.” Kuna maswala mengi sana ya kikatili
yaliyofanywa na Mfalme huyu mkubwa sana na dikteta wa hali ya juu aliyekuwa
amejaa kiburi mpaka aliponyenyekeshwa na Mungu, ukweli ni kuwa hata wayahudi
walipofika utumwani hawakuwa na maisha salama waliendelea kutumikishwa katika
shughuli ngumu na kali na mateso. Aidha kiimani walilazimishwa kuabudu na
kuitumikia miungu migeni ya Ukaldayo kwa ujumla waliishi Maisha ya wasiwasi na
kutokuelewa kuwa kesho yao itakuwaje jambo hili liliwafanya waikumbuke Sayuni,
wakumbuke Yerusalem wawe na tamaa ya kurudi kwao, Kwa hiyo nabii Isaya licha ya kuona mateso haya kinabii vilevile
alitabiri kuwa anawaona malaika wa Bwana wanashuka juu ya milima ya uyahudi
wakitangaza habari njema, ni habari ya kuwekwa huru, ni habari ya kuamuriwa
kurudi Yerusalem, ni habari ya kurudi nyumbani, ni habari ya kwenda kuwa na
ushirika na Mungu wao ni habari ya kwenda sehemu ambako unabii wa kuja kwa
masihi ungetimizwa ni habari ya kurejeshewa kwa matumaini yao, ni habari ya
kuelezewa ya kuwa mambo yatakuwa mazuri, Nabii isaya anasema ni Mizuri kama
nini Miguu yao juu ya milima ya uyahudi waletao habari za amani, waenezao
habari njema wasemao habari za wokovu waambiao watu Mungu ndiye anayetawala
yaani ufalme wa Mungu u karibu hii
ilikuwa ni kauli ya furaha kwa watu waliokata tamaa, kila mmoja anaweza akawa
yuko katika hali ya mateso na hali isiyofurahisha wala kuridhisha kila mmoja
anahitaji ukombozi, anahitaji kusikia habari njema Baada ya kutimizwa kwa
unabii huu wa Isaya Mungu alimuinua mfalme mkuu Koreshi wa uajemi ambaye alitoa
habari njema kwa kuwaruhusu Wayahudi warejee Yerusalem ili kulijenga tena
hekalu na vilevile kukomesha utumwa wa wana wa Israel na mateso yao ona Isaya 44:28 “nimwambiaye
Koreshi, Mchungaji wangu, naye atayatenda mapenzi yangu; hata ataunena
Yerusalemu, Utajengwa; na hilo hekalu, Msingi wako utawekwa.” Isaya
45:1-5 “Haya ndiyo Bwana amwambiayo Koreshi, masihi
wake, ambaye nimemshika mkono wake wa kuume, ili kutiisha mataifa mbele yake,
nami nitalegeza viuno vya wafalme; ili kufungua milango mbele yake, hata
malango hayatafungwa. Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali
palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata
mapingo ya chuma; nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za
mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana, nikuitaye kwa jina lako,
naam, Mungu wa Israeli. Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi wangu, na Israeli, mteule
wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la sifa; ijapokuwa hukunijua.
Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu; nitakufunga
mshipi ijapokuwa hukunijua;” Unabii Isaya wa isaya ulitimizwa miaka
180 baadaye Isaya alikuwa na maono ya ajabu sana mpaka ya kutaja jina la Mfalme
huyo mabaye Mungu alimuita Mtumishi wake na mpakwa mafuta waka na Mchungaji
wake, hii ni wazi kuwa mtumishi awaye yote wa Mungu atakayetenda mapenzi halisi
ya Mungu ni yule mwenye miguu mizuri anayetangaza habari njema na za amani na
za wokovu na za kuwaweka watu huru, katika namna nyembamba kiongozi huyo ni
Koreshi bali katika namna pana Kiongozi huyo ni Yesu Kristo, lakini wale
wanaoihubiri habari njema yaani injili pia wanaitwa ni wenye miguu mizuri kwa
sababu wanafanya yale mapenzi ya Mungu kwa watu wake.
Paulo anaitumia kauli hii ya
Nabii Isaya katika Warumi 10:15b “Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni
mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema” Wahubiri katika
agano jipya wanapaswa kuwatangazia watu habari njema za matumaini ya Kwamba
Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai ndiye aliyekuwa anatabiriwa kutuletea
habari njema ya ukombozi ya kuwekwa huru sio tu kwa Israel bali na kwa mataifa
mengine, watu wameteseka vya kutosha chini ya utawala wa mfalme asiyekuwa katika
mikono ya Mungu, shetani ni mfalme wa wafalme aliye katili sana mwenye kuwatesa
watu na kutokuwapoa pumzi ya uhuru wala nafasi ya toba, Lakini Yesu ni Mfalme
wa wa falme mwenye rehema, Wahubiri katika agano jipya hawapaswi kuwatisha
watu, wala kuwabebesha watu mizigo, bali
wanapaswa kuwafungua watu kutoka katika vifungo vyao, watu wa Mungu wana
mahitaji ya aina mbalimbali na wanahitaji ukombozi wa kweli wala sio vitisho na
migandamizo kutoka kwa watu waovu wanajipa mamlaka kubwa na kusahau kuwa yuko
Mungu wa mbinguni na kuwa Mungu huyo ndiye anayetawala, Mungu anachokitaka kwa
watu wake ni kuwatangazia habari njema huu ndio mpango wake Israel wote
walikuwa wakiusubiri mpango huu ona Isaya
58:6 “ Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii?
Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa,
na kwamba mvunje kila nira? ”
Mungu anapenda watu wake wasamehewe,
walegezewe mizigo yao inayowaelemea, wajisikie huru kutika kila aina ya uonevu
na kila aina ya magereza inayowatesa hata kama ina nguvu kiasi gani nira yake
ivunjwe mtu anayefanya hayo ndiye mwenye kuleta habari njema ndiye ambaye miguu
yake ni mizuri kama nini, ndiye anayetangaza habari za kweli za wokovu, ni
ujumbe kama huu ndio tunayaita maneno ya neema na nitangazo la namna hii ndio
Yesu Kristo alikuja kulitimiza na kulifanya Luka 4;16-22 16. “Akaenda Nazareti, hapo
alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi
yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta
mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta
kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa
kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka
wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu
wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo
maandiko haya yametimia masikioni mwenu. Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia
maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu?
” unaona Masihi Yesu Kristo mwenyewe alipoianza kazi ya kuhubiri
injili yaani habari njema alitangaza kufunguliwa kwa watu na jamii ya watu wa
kwao WALISTAAJABIA MANENO YA NEEMA
YALIYOTOKA KINYWANI MWAKE. Huyu ndiye ambaye kila mtu alikuwa anamgoja
anayetangaza habari ya mema, habari za amani habari za kuwaweka huru
waliosetwa, habari za kuwafungua waliofungwa, habari za vipofu kuona habari ya
kutangaza jubilii yaani mwaka wa bwana wa neema, Mtu wa namna hii ndiye ambaye
tunasema ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari njema, kutana sasa na
wale wasiotangaza habari njema miguu yao ni mibaya utasikia Leo tunamtangaza
dada fulani au kaka fulani kuwa tumemkabidhi kwa shetani, leo natangaza kumtega
fulani, leo namfukuza fulani kutoka katika kanisa letu, leo tunaanza mfungo wa
siku miamoja, leo ni siku ya kumtolea Bwana Isaka wako, leo ameondoka katika
kanisa hili habari zake ndio kwishinei, leo nalaani wanaopingana nami, dhehebu
hili ndilo bora kuliko lile, muhubiri yule anahubiri mafundisho potofu na yasiyofaa,
yule ndio mzinzi namba moja, huyu jamaa si aliwahi kufumaniwa, yule hanizidi
mimi kwa maombi, sisi ndio waanzilishi
wa imani, sisi tunauzoefu, mimi sibabaishwi na hiki ama kile, mimi nimetembea
sana nimezunguka nchi nyingi sana duniani, mimi utaniambia nini, mimi nina
miaka mingi sana katika wokovu au nimekutangulia sana katikla huduma na
kadhalika nisikilize, watu hawahitaji kujua umezunguka nchi ngapi, hawahitaji
kujua umesoma kiasi gani watu wanahitaji kustaajabia maneno ya neema yanayotoka
kinywani mwako, watu wanahitaji kutangaziwa msamaha wa dhambi, wanahitaji wokovu, wanahitaji utawala na
ufalme wa Mungu, wanahitaji kufundishwa na kuwekwa huru kutoka katika vifungo
mbalimbali, wanahitaji kuelekezwa kwa masihi ili awaponye na kuwaweka huru,
watu wanaotangaza habari za namna hii ni adimu sana kuwapata siku hizi, watu
watamleta Isaka wao na hata Yakobo kama tu watahudumiwa vema na kutangaziwa
utawala na malamaka ya kiungu hawa ndio Isaya anawatabiri kuwa ni mizuri kama
nini miguu yao wahubirio habari njema, wanaoleta habari njema wanaotangaza
amani, wanaotangaza mambo mema, wanaotangaza wokovu na kuwaambia watu uko
ufalme wa Mungu na kuwaelekeza watu kwa Yesu!
Ni Mizuri kama nini
miguu yao, wahubirio habari ya mema!
Isaya 52:7 “Jinsi ilivyo mizuri juu ya
milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari
njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu, Auambiaye Sayuni, Mungu wako
anamiliki!”
Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hongera sana Mtumishi wa Mungu. Bwana aendelee kukubariki, nilikuwa naandaa somo kuhusu Efeso 6:15 na andiko lako limekuwa la msaada haswa katika mateso na udikteta wa nebukadreza in relation to mateso na udikteta wa shetani kwa watu wa Mungu.
JibuFuta